11%

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَوَاعَدْنَا مُوسَىٰ ثَلَاثِينَ لَيْلَةً وَأَتْمَمْنَاهَا بِعَشْرٍ فَتَمَّ مِيقَاتُ رَبِّهِ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً وَقَالَ مُوسَىٰ لِأَخِيهِ هَارُونَ اخْلُفْنِي فِي قَوْمِي وَأَصْلِحْ وَلَا تَتَّبِعْ سَبِيلَ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٤٢﴾

142. Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini. Na Nabii Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifu- ate njia ya waharibifu.

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٤٣﴾

143. Na alipofika Musa kwenye miadi yetu Na Mola wake akamsemeza, alisema: Mola wangu nionyeshe nikutazame. Akasema: Hutaniona, lakini tazama jabali, kama litakaa pahali pake ndipo utaniona. Basi Mola wake alipojionyesha kwa jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika, na Musa akaanguka hali amezimia. Alipozinduka alisema: kutakasika ni kwako! Natubu kwako na mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

قَالَ يَا مُوسَىٰ إِنِّي اصْطَفَيْتُكَ عَلَى النَّاسِ بِرِسَالَاتِي وَبِكَلَامِي فَخُذْ مَا آتَيْتُكَ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

144. Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.

وَكَتَبْنَا لَهُ فِي الْأَلْوَاحِ مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْعِظَةً وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ فَخُذْهَا بِقُوَّةٍ وَأْمُرْ قَوْمَكَ يَأْخُذُوا بِأَحْسَنِهَا سَأُرِيكُمْ دَارَ الْفَاسِقِينَ ﴿١٤٥﴾

145. Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidha na ufafanuzi wa kila jambo. Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi, Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Aya 142 – 145

MAANA

Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini.

Nabii Musa(a.s) alimtaka Mola wake amteremshie Kitab atakachowaongozea watu kwenye yale wanayoyahitajia katika mambo ya dini yao. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwahidi kuteremshia Kitab baada ya siku thalathini, na utaendelea ushukaji wake kwa siku kumi. Kwa ujumla itakuwa muda wa miadi na wa kushuka ni siku arubaini.

Hapa tumefafanua baada ya kueleza kwa ujumla kwenye Juz. 1 (2:51).

Na Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu.

Nabii Musa alipoondoka alimwachia mahali pake ndugu yake Harun kwa Wana wa Israel; akampa nasaha kusimamia mambo yao na kuyatengeneza. Akamhadharisha na tabia zao zinazopondokea zaidi kwenye ufisadi. Ni jana tu walipokodolea macho ibada ya masanamu mpaka Nabii Musa akawaambia kuwa ni watu wajinga.

Harun akakubali nasaha kwa moyo mkunjufu, kama anavyokubali nasaha kaimu kiongozi mwenye ikhlasi kutoka kwa kiongozi wake mwaminifu.

Na alipofika Nabii Musa kwenye miadi yetu ambayo aliiweka Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumpa Tawrat,

Na Mola wake akamsemeza bila ya kumwona kwa sababu:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا ﴿٥١﴾

“Haikuwa kwa mtu aseme na Mwenyezi Mungu ila kwa wahyi au kwa nyuma ya pazia au kumtuma mjumbe” (42:51)

Nabii Musa alisema:Mola wangu nionyeshe nikutazame.

Baadhi ya maulamaa wanasema kuwa Nabii Musa hakumwomba Mola wake kumwona kwa ajili yake isipokuwa ni kwa ajili ya watu wake. Lakini hii inapingwa na kauli yake Nabii Musa pale aliposema:

Kutakasika ni kwako, na natubu kwako.

Vyovyote iwavyo ni kwamba Nabii Musa alitaka kuona, ni sawa iwe ni kwa ajili yake au kwa ajili ya wengine, sisi hatuoni ubaya wowote katika ombi hili, kwa sababu nafsi ya mtu ina hamu ya kutaka kujua yanayokuwa na yasiyokuwa hasa kuona kile ambacho kitazidisha utulivu wa nafsi.

Ibrahim(a.s) alitaka mfano wa hayo. Angalia Juz.3 (2:260).

Akasema: Hutaniona.

Kwa sababu kumwona Mwenyezi Mungu ni muhali. Tumeyazungumza hayo kwa ufafanuzi katika kufasiri Juz. 1(2:51).

Lakini tazama jabali, kama litakaa mahali pake utaniona.

Nabii Musa aligeuka kwenye jabali ili amwone Mwenyezi Mungu, mara akaanguka chini na hakuona chochote. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alifanya hivi ili kumfahamisha Nabii Musa(a.s) kwamba kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani kwake wala kwa mwingine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliuwekea sharti uwezekano wa kuonekana kwake kwa kutulia mahali jabali na jabali halikutulia, Kwa hiyo kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani.

Mfumo huu alioutumia Mwenyezi Mungu hapa ni kama ule wa kusema: Nitafanya hivi kunguru akiota mvi, Au akipita ngamia kwenye tundu ya sindano.

Basi Mola wake alipojionyesha kwenye jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika.

Yaani ilipodhihiri amri ya Mola wake; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا ﴿٢٢﴾

“Akaja Mola wako na Malaika (wamejipanga) safu kwa safu.” (89:22).

Yaani ikaja amri ya Mola wako.

Na Musa akaanguka chini amezimia.

Akawa hana fahamu kwa kishindo cha ghafla, Mwenyezi Mungu akamhurumia akazinduka.

Alipozinduka alisema: Kutakasika ni kwako! Natubu kwako. Kwa kukuomba kukuonana mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

Kwa sababu wewe ni mtukufu zaidi ya kuonekana kwa jicho.

Makusudio ya wa mwanzo sio kulingana na hisabu ya wakati; isipokuwa makusudio yake ni uthabiti na kutilia mkazo.

Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.”

Baada ya Nabii Musa kunyenyekea kwa muumba wake, Mwenyezi Mungu alimkumbusha neema yake, kubwa zaidi ni Utume na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Makusudio ya watu ni watu wa zama zake, kwa dalili ya kauli yake: Kwa ujumbe wangu. Kwani Mwenyezi Mungu aliwachagua Mitume wengi kabla ya Nabii Musa na baada yake.

Ama kuhusika kwake na kuzungumza naye hakuna dalili ya ubora zaidi. Ikiwa kunafahamisha ubora wowote basi kupelekewa roho mwaminifu kwa mwisho wa Mitume na bwana wa Mitume ndio daraja ya juu na bora zaidi.

Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidaha na ufafanuzi wa kila jambo.

Makusudio ya mbao ni Tawrat kwa sababu ndiyo aliyoteremshiwa Nabii Musa, ndani yake mna mawaidha na upambanuzi wa hukumu.

“Kila jambo ni neno la kiujumla, lakini limekusudia mahsusi; yaani kila linalofungamana na maudhui ya risala miongoni mwa mawaidha, hukumu, misingi ya itikadi, kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu, Mitume yake na siku ya mwisho, na hukumu za sharia, kama halali na haramu. Kwa hiyo kauli yake: Mawaidha na maelezo ni ubainifu wa tafsiri ya kauli yake kila jambo. Kwa sababu makusudio ya maelezo ni kubainisha hukumu za kisharia.

Basi yashike kwa imara.

Yaani ichunge Tawrat na uitumie kwa ukweli wa nia.

Na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi.

Kila aliloliteremsha Mwenyezi Mungu ni zuri, lakini kuna yaliyo mazuri zaidi. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: “Na fanyeni wema, Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”

Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Yaani fasiki na dhalimu atafikwa na majanga. Haya ndiyo niliyoyafahamu kutokana na jumla hii kabla ya kupitia tafsir, Baada ya kuzipita nikakuta kauli kadhaa. Miongoni mwazo ni kwamba Mwenyezi Mungu atawaonyesha makao ya Firauni na watu wake baada ya kuangamizwa kwao. Nyingine inasema kuwa atawaonyesha ardhi ya Sham iliyokuwa mikononi mwa waabudu mizimu wakati huo.

سَأَصْرِفُ عَنْ آيَاتِيَ الَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٤٦﴾

146. Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki. Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَلِقَاءِ الْآخِرَةِ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٤٧﴾

147. Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zime- poromoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

وَاتَّخَذَ قَوْمُ مُوسَىٰ مِن بَعْدِهِ مِنْ حُلِيِّهِمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا اتَّخَذُوهُ وَكَانُوا ظَالِمِينَ ﴿١٤٨﴾

148. Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti, Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

وَلَمَّا سُقِطَ فِي أَيْدِيهِمْ وَرَأَوْا أَنَّهُمْ قَدْ ضَلُّوا قَالُوا لَئِن لَّمْ يَرْحَمْنَا رَبُّنَا وَيَغْفِرْ لَنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿١٤٩﴾

149. Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

NITAWAEPUSHIA AYA ZANGU

Aya 146 – 149

MAANA

Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki.

Wenye kufanya kiburi katika ardhi ni wale wanaopinga haki na wasiotaka kutawaliwa nayo. Kusema kwake bila ya haki ni kwa ufafanuzi, sio kwa kuvua; sawa na kusema: “Na wakiwaua mitume bila ya haki.”

Neno Aya katika Qur’an mara nyingine hutumia kuwa ni Aya zenye misingi ya itikadi na hukumu ya sharia na mfano wake. Mara nyingine hutumi- ka kuwa ishara yaani hoja na dalili zenye kuthibitisha uungu na utume.

Ikiwa makusudio ni maana ya kwanza katika Aya hii tunayoifasiri, basi maana yatakuwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazihifadhi Aya na kuzilinda zisipotolewe; sawa na kauli yake: “Hakika sisi ndio tuliouteremsha ukumbusho huu na hakika ndio tutakaoulinda”

Na ikiwa makusudio ni maana ya pili, yaani ishara kwa maana ya dalili na hoja, basi maana ni kwamba baada ya wapinzani kujiepusha nazo na kuacha kuzisikiliza, basi Mwenyezi Mungu ataachana nao, wala hatawategemeza kwenye imani. Tumekwisha elezea hilo mara kadhaa; kama vile katika kufasiri Juz.5 (4:88).

Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

Huu ni ubainifu wa hakika ya wenye kiburi na sababu inayowajibisha kiburi chao vilevile. Ama hakika yao ni kuwa wao hawajizuilii na uovu wala hawapondokei kwenye uongofu.

Sababu inayowajibisha hilo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaletea hoja na dalili; akawataka wazichunguze, wazizingatie na wazitumie vile inavyotakikana, wakakataa na wakaendelea kuzipinga tena bila ya kuzichunguza. Lau kwamba wao wangeliziitikia na kuzichunguza dalili hizo kungeliwapelekea kuamini na kuikubali haki; wala wasingelikua na kiburi na kufanya ufisadi katika nchi.

Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zimeporomoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

Kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na kukutana na Mola wake, basi yeye ni katika wale watakaoangamia kesho na yote yale aliyokuwa akijifaharisha nayo yatakuwa si lolote. Hayo ni malipo ya ukafiri wake na inadi yake.

Yamenipendeza yale aliyoyasema mfasiri mmoja Mwenyezi Mungu amughufirie na amrehemu, namnukuu: “Kuporomoka amali kunachukuliwa kama wanavyosema: ‘Ameporomokaa ngamia.’ ikiwa amekula mmea wenye sumu na tumbo lake likafura kisha akafa.

Hiyo ndiyo sifa ilivyo kwa batili inayowatokea wenye kukadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana na akhera, Mwongo hufura mpaka watu wanamdhania kuwa ni mkubwa mwenye nguvu, kisha huporomoka, kama alivyoporomoka yule ngamia, aliyekula mmea wa sumu.”

Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti.

Imetangulia kuelezwa katika Aya 142 kuwa Nabii Musa(a.s) alikwenda kwa miadi ya Mola wake, na kwamba yeye alimpa ukaimu nduguye Harun kwa watu wake. Vilevile imeelezwa katika Aya 138 kwamba Wana wa Israel baada ya kupita bahari walimtaka Nabii Musa awafanyie sanamu watakayoiabudu; si kwa lolote isipokuwa tu wameona ni vizuri waabudu masanamu.

Kwa hivyo mara tu Nabii Musa alipokuwa mbali nao waliitumia nafasi hiyo; Msamaria (Samiri): akakusanya mapambo ya wanawake akaten- geneza ndama; akatengeneza katika umbo ambalo liliweza kutoa sauti ya ndama.

Akawaambia huyu ni Mola wenu na Mola wa Musa; wakaingilia kumwabudu. Harun aliwakataza, lakini hakuweza kuwazuia, na hawakum- sikiliza isipokuwa wachache, Yametangulia kudokezwa hayo katika kufasiri Juz, 1 (2: 51), Pia yatakuja tena maelezo.

Aya hii tuliyo nayo, inatilia nguvu yale tuliyoyakariri katika Juzuu ya kwanza na ya pili, kuwa Israeli haithibiti ila kwenye misingi ya matamanio na hawaa; ikiwa ni kweli kuwa matamanio ni misingi.

Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

Haya ndiyo mantiki ya kimaumbile na akili ambayo inakataa mtu amwabudu Mungu aliyemtengeneza kwa mkono wake, lakini waisraili hawana akili wala maumbile au dini.

Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotoea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

Hii ndiyo sifa nzuri pekee na ndiyo ya kwanza na ya mwisho, iliyosajiliwa na Qur’an kwa waisrael kwa ujumla, bila ya kuangalia uchache wa wachache waliomwamini Nabii Musa hadi mwisho.

Baadhi ya Wafasiri wamechukulia dhahiri toba ya Bani Israel kwamba wakati huo ilikuwa ni masalia ya maandalizi ya wema, kisha masalia hayo yakaenda; wala haikubaki athari yoyote kwao ya kuonyesha kujiandaa kwa kheri. Kuchukulia huku hakuko mbali na ukweli na kunaashiriwa na Aya isemayo:

ثُمَّ قَسَتْ قُلُوبُكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَهِيَ كَالْحِجَارَةِ أَوْ أَشَدُّ قَسْوَةً ﴿٧٤﴾

“Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, zikawa kama mawe au ngumu zaidi” Juz.1(2: 74)

Aya hii ni baada ya kisa cha ng’ombe ambacho kilitokea baada ya kuabudu ndama.