11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا زَحْفًا فَلَا تُوَلُّوهُمُ الْأَدْبَارَ ﴿١٥﴾
15. Enyi mlioamini! Mnapokutana vitani na wale waliokufuru, basi msiwageuzie migongo.
وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلَّا مُتَحَرِّفًا لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزًا إِلَىٰ فِئَةٍ فَقَدْ بَاءَ بِغَضَبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿١٦﴾
16. Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo – isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - hakika amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu; na makazi yake ni Jahannam, napo ni mwishilio muovu.
فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ قَتَلَهُمْ وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ رَمَىٰ وَلِيُبْلِيَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْهُ بَلَاءً حَسَنًا إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿١٧﴾
17. Hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua, Na hukutupa wewe ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa, Ili awajaribu waumini majaribu mazuri, Hakika Mweyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
ذَٰلِكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ ﴿١٨﴾
18. Ndiyo hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye adhoofishaye vitimbi vyamakafiri.
إِن تَسْتَفْتِحُوا فَقَدْ جَاءَكُمُ الْفَتْحُ وَإِن تَنتَهُوا فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَإِن تَعُودُوا نَعُدْ وَلَن تُغْنِيَ عَنكُمْ فِئَتُكُمْ شَيْئًا وَلَوْ كَثُرَتْ وَأَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٩﴾
19. Kama mnataka ushindi, basi ushindi umekwishawajia, na kama mkiacha, basi itakuwa kheri kwenu; na kama mtarudia sisi pia tutarudia; na jeshi lenu halitawafaa chochote hata likiwa kubwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waumini.
Aya 15 – 19
Enyi mlioamini! Mnapokutana vitani na wale waliokufuru, basi msi- wageuzie migongo.
Yametangulia maelezo kuwa washirikina walitoka Makka kuja kupambana na waislamu. Aya hii ni katika mafunzo ya vita, Inamaanisha waislamu wawe imara kumkabili adui wala wasikimbie wanapokutana vitani. Kwa sababu kukimbia ni unyonge katika dini na udhalili kwa waislamu.
Na atayewageuzia mgongo wake siku hiyo - isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - hakika amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu; na kimbilio lake ni Jahannam, napo ni mwisho muovu.
Mbinu za vita, ni kama kuacha mahali pake na kwenda mahali pazuri zaidi. Na kuungana na kikosi, ni kuungana na kikosi kingine kinachomhitajia au anachokihitajia.
Maana ni kuwa: Enyi waislamu! Mjizatiti na adui yenu katika vita wala msimkimbie ila ikiwa ni kuchagua sehemu nzuri au kupanga mpango mzuri kwa kuungana; na kwamba mwenye kukimbia adui bila ya sababu za msingi basi amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na marejeo yake ni Jahannam.
Mafakihi wametoa fatwa kuwa ni haramu kukimbia vita ila ikiwa idadi ya jeshi la adui ni kubwa kuliko jeshi la waislamu.
Tuanavyo sisi ni kuwa mafakihi hawawezi kuwa na fatwa hapa ya wajibu wa kubaki au kujuzu kukimbia; isipokuwa amri katika hilo ni lazima aachiwe kamanda mwaminifu mwenye majukumu ya vita na wala sio mafakihi. Kwa hiyo ni wajibu yeye aachiwe kupanga wajibu wa kubaki au kukimbia.
Anaweza akaonelea kuwa wabakie licha ya kuzidi idadi ya adui mara tatu zaidi, na anaweza akaona lazima wakimbie na kujiondoa vitani hata kama idadi ya waislamu ni maradufu ya maradufu. Kwa sababu kubaki ni tendo la kujiua. Na, katika hali zote ni wajibu kuchukua kauli yake sio kauli ya mafakihi wanayofutu wenyewe wakiwa wamelalia mito.
Zaidi ya hayo ni kwamba kauli ya mafakihi imepitwa na wakati, ambapo nguvu zilikuwa zikipimwa na idadi sio kwa aina, na kwa idadi ya jeshi sio kwa maandalizi yake ya silaha za kisasa.
Hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua.
Waislamu waliwashinda washirikina Badr; wakawauwa na kuwateka. Sababu ya ushindi huu ni uimara wa waislamu na uvumilivu. Ama sababu ya uimara huu na uvumilivu ni ile iliyoashiriwa na Aya iliyotangulia kuwa Mwenyezi Mungu alizikazanisha nyoyo za waislamu, akaimarisha nyayo zao, akawasaidia kwa Malaika na akaondoa hofu katika nyoyo zao na kuitia katika nyoyo za washirikina.
Kwa hali hiyo inafaa kunasibisha kwa waislamu kuuwa washirikina, kwa sababu ilikuwa ni kwa mikono yao na ni kwa sababu ya uimara na subira yao. Vilevile itafaa kunasibisha kwa Mwenyezi Mungu mtukufu kwa sababu yeye ndiye aliyewaandalia uimara na subira hiyo, Zaidi ya hayo yeye ndiye sababu ya sababu zote.
Imesimuliwa kwamba baadhi ya waislamu walisema siku ya Badr: “Mimi nimemuuwa fulani”, mwengine naye akasema, Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha kauli yake hiyo.
Na hukutupa wewe ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa.
Ndio Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa, lakini yeye alichagua kiganja cha kutupa cha Nabii Muhammad(s.a.w.w) ambaye amemfadhilisha juu ya viumbe vyote; akamhusisha na ujumbe wake ambao rehma yake imewaenea walimwengu wote.
Imepokewa kuwa Mtume alichukua gao la changarawe au mchanga, akawatupia washirikina, akasema: “Na zihizike nyuso”, hilo likafuatiwa na kushindwa kwao. Sio mbali kuwa riwaya hii ni sahih. Vilevile sio mbali kuwa makusudio ya kutupa ni kupanga mambo.
Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba matakwa ya Mwenyezi Mungu ndiyo sababu ya sababu. Kwani sababu yoyote ya tukio lolote iwe ya moja kwa moja au si ya moja kwa moja, basi itaishia kwenye nguvu kuu iliyopatikana bila ya mpatishaji. Vinginevyo basi neno kupatikana lisingekuwa na maana.
Ili awajaribu waumini majaribu mazuri.
Majaribu (mtihani) yanaweza kuwa ya neema ili kudhihirisha shukrani na yanaweza kuwa ni misukosuko ili kudhihirisha uvumilivu. Pia maana yake yanakuwa ni kupewa, Hayo ndio maana yaliyokusudiwa katika Aya hii.
Ama makusudio ya mazur ni ushindi na ngawira; yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaamrisha waislamu kuwa imara, wavumilivu na kuacha kukimbia vita; na akawaandalia wao njia ya hilo, ili awatimizie neema yake ya ushindi na ngawira.
Hakika Mweyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
Amesikia maombi ya msaada na akawaitikia, kwa vile alijua usafi wao wa nia na usahihi wa azma.
Ndiyo hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye adhoofishaye hila za Makafiri.
Hakuna neema kubwa na adhimu kuliko kudhoofishwa adui na kubatilishwa hila zake.
Kama mnataka ushindi, basi ushindi umekwishawajia, na kama mkiacha, basi itakuwa kheri kwenu; na kama mtarudia sisi pia tutarudia; na jeshi lenu halitawafa chochote hata likiwa kubwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waumini.
Maneno yote wanaambiwa washirikina kwa kuangalia mfumo wa maneno na kutimia maana.
Imepokewa kuwa Washirikina walipotoka Makka kuelekea Badr waliishika nguo inayofunika Al-Kaaba, wakamtaka nusura ya ushindi Mwenyezi Mungu, wakasema: “Ewe Mwenyezi Mungu lipe ushindi jeshi lililo juu na lililo tukufu kati ya majeshi mawili.”
Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu: Kama mnataka ushindi; yaani mkitaka ushindi kwa jeshi lililo juu na lililo na uongofu basi amekwisha lipa ushindi. Na kama mkiacha kupigana na waislamu na kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume, basi itakuwa ni bora kwenu baada ya kuonja kipigo cha kuuawa na kutekwa. Na kama mkirudia vita yatawafika tena yale yaliyowafika mwanzo.
Ama wingi ambao mnajitukuza nao, mmeuona haufai kitu, hauwazuilii kuuliwa, kutekwa na kushindwa. Kwani Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kutoa ushindi, naye yuko pamoja na waumini.
Ikiwa mnataka ushindi wa kweli basi acheni shirk na mumuami Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَوَلَّوْا عَنْهُ وَأَنتُمْ تَسْمَعُونَ ﴿٢٠﴾
20. Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye hali mnasikia.
وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ قَالُوا سَمِعْنَا وَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ ﴿٢١﴾
21. Wala msiwe kama wale wanaosema: Tumesikia; na kumbe hawasikii.
إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الصُّمُّ الْبُكْمُ الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ ﴿٢٢﴾
22. Hakika wanyama waovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni viziwi, mabubu ambao hawatumii akili.
وَلَوْ عَلِمَ اللَّـهُ فِيهِمْ خَيْرًا لَّأَسْمَعَهُمْ وَلَوْ أَسْمَعَهُمْ لَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٢٣﴾
23. Na kama Mwenyezi Mungu angelijua wema wowote kwao angeliwasikilizisha;na kama angeliwasikilizisha, wangeligeuka wakipuuza.
Aya 20 – 23
Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msi- jiepushe naye hali mnasikia.
Mwito huu umekuja baada ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waumin.” Lengo lake ni kumuelezea Mumini ambaye atapewa ushindi na Mwenyezi Mungu na atakayekuwa naye Mwenyezi Mungu popote alipo.
Huyo ni yule ambaye anamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika wanayomwamrisha na wanayomkataza na kwamba mwenye kumhalifu na kuasi; basi amestahiki adhabu na hizaya kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Wala msiwe kama wale wanaosema: Tumesikia; na kumbe hawasikii.
Mara nyingi kusikia kutumiwa kwa maana ya kukubali; kama vile mtu kusema: Mimi sikuzikilizi; yaani sikukubalii. Au kama vile kusema: Wenye kusikia sana uwongo; yaani wenye kuukubali
Haya ndiyo maana yaliyokusudiwa katika Aya hii, Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakataza waumini kuwa kama wanafiki wakidhihirisha kumkubalia Mtume na kutii amri yake na huku wakificha uhalifu na uasi.
Hakika wanyama waovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni viziwi, mabubu ambao hawatumii akili.
Kiziwi hasikii na bubu hasemi. Wanyama wana masikio ya kusikia, lakini hawafahamu maneno wanayoyasikia na wana ndimi lakini hawasemi, Kwa hiyo hawafahamu wala hawafahamiwi.
Mwenye kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume kisha asiongoke kwayo, basi mfano wake ni kama mfano wa mnyama kiziwi aliye bubu, husikia maneno, lakini hanufaiki nayo.
MWENYE KUTAFUTA HAKI NA MWENYE KUTAFUTA WINDO
Na kama Mwenyezi Mungu angelijua wema wowote kwao angeliwasikilizisha; na kama angeliwasikilizisha wangeligeuka wakipuuza.
Watu ni aina mbili:
1. Ni yule mwenye kuitafuta akiwa hana lengo lolote. Huyu hawezi kuamini msingi wala kuona rai yoyote ila baada ya utafiti na kutilia manani dalili kisha hujenga rai yake juu ya dalili hizo.
2. Ni mwenye kutafuta windo fulani. Haamini isipokuwa dhati yake na maslahi yake. Hukaribisha yale yanayoafikiana na maslahi yake, hata kama ni batili na hukataa yale yanayopingana nayo, hata kama ni haki.
Mwenyezi Mungu huwasikilizisha mwito wa haki wote wawili kwa njia ya sawa sawa, kuweka hoja. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾
Na hatukuwa ni wenye kuadhibu mpaka tumpeleke Mtume. (17:15).
Baada ya ubainifu unaotumiza hoja kwa wote, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anazidisha nasaha na mwongozo kwa wale wanaoitikia na kunufaika nao
وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ ﴿١٧﴾
“Na wale wanaokubali kuongoka huwazidishia uongofu.” (47:17).
Ama wale ambao hawaitikii isipokuwa manufaa yao ya kidhati, basi Mwenyezi Mungu huachana nao, maadamu nasiha haziwafai chochote. Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kama angejua wema wowote angeliwasikilizisha.”
Hilo linafahamika kutokana na kauli yake moja kwa moja bila ya kuingia kati kitu kingine: “Na kama angewasikilizisha wangeligeuka wakipuuza.” Yaani lau angeliwasikilizisha haki, wangeliachana nayo, kwani haikubaliani na hawaa zao.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٢٤﴾
24. Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita kwenye lile litakalowapa uhai. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba mtakusanywa kwake.
Aya 24
Mwenye kuujua vilivyo Uislamu atakuta kila asili ya itikadi yake na kila tawi la sharia yake inasimamia kwa uwazi au kuwa na madhumuni ya kufanya kazi kwa ajili ya uhai (maisha).
Kumwamini Mungu ni imani iliyo na mwito wa kujikomboa na utumwa, isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu mmoja peke yake, na kwamba hakuna utawala kwa sababu ya mali wala jaha au jinsi au kitu chochote kile isipokuwa kwa haki na uadilifu.
Kimsingi ni kwamba maisha mema yenye nguvu hayapatikani na ni muhali kupatikana ila kwa kushikamana na msingi huu na kuufuatilia.
Ama kuamini Utume wa Muhammad(s.a.w.w) kwenyewe ni kuamini sharia ya udugu na usawa, uhuru wa mtu na himaya yake na kila msingi ambao unampa binadamu kheri njema. Hilo ni kwa vile utume wa Muhammad unalenga kwenye uongofu wa mtu na wema wake na kueneza uadilifu baina ya watu.
Kuamini siku ya mwisho ni kuamini kuwa mtu hataachwa bure na kwamba yeye ataulizwa kila dogo na kubwa katika amali zake. Atahisabiwa na kulipwa; ikiwa ni kheri basi atalipwa kheri, na ikiwa ni shari basi atalipwa shari. Imani hii, kama unavyoona, inafanana na serikali kuu, au mhimizaji wa matendo yanayowajibisha kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume.
Hayo ni katika yale yanayohusiana na misingi ya itikadi. Ama matawi ya dini, yaani yale yanayofaa kufanywa na yasiyofaa katika sharia ya kiislamu, huwa yanasimamia misingi ya binadamu, iliyoashiriwa na kauli yake Imam Jafar As-Sadiq(a.s) :“Kila lililo na masilahi kwa watu kwa upande fulani basi linajuzu, na kila lililo na ufisadi kwa upande fulani basi halijuzu.
Huu ndio mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume ulioelezwa na Qur’an waziwazi:
Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita kwenye lile litakalowapa uhai.
Tukiinganisha Aya hii na ile isemayo:
قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ ﴿٣٢﴾
“Sema mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na kama wakikata, basi hakika Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri” Juz.3 (3:32),
Tutapata picha hii ya makisio ya kimantiki kuwa: Mungu na Mtume wametoa mwito kwa ajili ya maisha na akahukumu ukafiri wa kila anayepinga mwito huu. Kwa hiyo natija ni kuwa asiyetenda kwa ajili ya maisha basi ni kafiri[2] .
Kwa hali hiyo basi inatubainikia kuwa Uislamu unakwenda sambamba na maisha, na kwamba kila ambalo liko mbali na maisha basi si Uislamu chochote.
Kila mtu, vyovyote awavyo, akilingania kwenye maisha yasiyokuwa na unyanyasaji, dhulma au matatizo, basi mwito wake huo unakutana na mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume, apende asipende.
Na yule anayeikingamia njia ya maisha na maendeleo yake, basi huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume, hata akiswali usiku na kufunga mchana.
Ama vikundi vilivyojitokeza siku hizi ambavyo vimeiuza dini yake kwa uzayuni na ukoloni, huku vikijificha kwa jina la dini, tumevielezea kaatika Juz. 4 (3:142).
Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake na kwamba mtakusanywa kwake.
Moyo ndio mahali pa imani, ukafiri, ikhlas na unafiki. Pia ni mahali pa pendo na chuki. Kwenye moyo hutokea matendo mema na mbaya, Lau si moyo mtu asingekuwa mtu.
Inatosha kuwa moyo ni kitu kikubwa, kauli yake Mwenyezi Mungu katika Hadith Qudsi: “Haikunipanua ardhi yangu wala mbingu yangu, lakini umenipanua moyo wa mja wangu muu’min.” Hakuna mwenye shaka kwamba kinachompanua aliyeshindwa kupanuliwa na mbingu na ardhi, kuwa ni kikubwa zaidi ya ardhi na mbingu.
Utauliza : vipi kiungo hiki kidogo kiweze kupanua aliyeshindikana na ardhi na mbingu? Tena, kwa nini Mwenyezi Mungu mtukufu amehusisha moyo wa Mumini na wala sio wa kafiri?
Jibu : Makusudio ya upana katika Hadith Qudsi hii, sio upana wa mahali. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hana mahali isipokuwa makusudio ni kumfahamu Mwenyezi Mungu, na kwamba moyo wa mumini unamfahamu Mwenyezi Mungu mtukufu kwa namna isiyoweza mbingu na ardhi kufahamu.
Vilevile moyo wa kafiri, haufahamu chochote kuhusu Mwenyezi Mungu, kwa vile uko katika kifuniko cha upotevu na ufisadi. Mwenyezi Mungu mtukufu, anasema:
وَقَالُوا قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ وَمِن بَيْنِنَا وَبَيْنِكَ حِجَابٌ ﴿٥﴾
“Na wakasema: Nyoyo zetu ziko katika vifuniko kwa yale unayotulingania, na katika masikio yetu mna uzito, na baina yetu na baina yako kuna pazia” (41:5).
Kwa hivyo basi inatubainikia kuwa makusudio ya mtu ambaye Mwenyezi Mungu huingia kati yake na moyo wake, ni yule ambaye amepofushwa na hawaa zake na upotevu. Hivyo Aya hii inakuwa na maana ya Aya isemayo: “Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na juu ya macho yao pana kifuniko,”
Yaani hawanufaiki kwa nyoyo zao kwa sababu ya kutu za upotevu zilizo juu yake, mpaka ikawa kama kwamba Mwenyezi Mungu amepiga sili au amekaa kati yake na mwenye moyo huo.
Hivyo anakuwa kunasibisha muhuri na kuzuia kwake Mwenyezi Mungu mtukufu ni kimajazi sio kihakika.
Kundi la wafasirii wamesema kuwa maana ya kuingia kati ya mtu na moyo wake ni kwamba moyo unashikwa na Mwenyezi Mungu akiugeuza vile anavyotaka, hubadilisha ukumbusho ukawa usahaulivu na usahaulivu ukawa ukumbusho, hofu kuwa amani na amani kuwa hofu. Lakini tafsiri zote hizo ni za kudhania tu.