12%

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ ﴿١١٣﴾

113. Haimfalii Mtume na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina ijapokuwa ni jamaa. Baada ya kuwabainikia kuwa wao ni watu wa motoni.

وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ ﴿١١٤﴾

114. Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila ni kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye, lakini ilipom pambanukia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye. Hakika Ibrahim alikuwa Mpole sana wa moyo mvumilivu.

ABU TWALIB NA KUWATAKIA MSAMAHA WASHIRIKINA

Aya 113 – 114

KUSHUKA AYA

Watu wamesema mengi kuhusu Uislamu wa Abu Twalib, ami yake Mtume(s.a.w.w) . Kauli zimetofautiana na viko vitabu vya zamani na karibuni kuhusu suala hilo. Vile vile maudhui haya yaliwahi kutolewa katika kurasa za gazeti la Majallatul-Arabi Na 108 na 110.

Wanaosema kuwa alisilimu, wametoa dalili kwa yale aliyopambana nayo kutoka kwa vigogo vya maquraish na kauli zake katika kumsifu Mtume kishairi n.k. Ama wale waliosema kuwa alikuwa mshirikina, walitoa dalili kwa riwaya inayosema kuwa Aya mbili hizi zilishuka kuhusiana na Abu Twalib.

Nilipofika hapa kufasiri, nilifuatilia riwaya na kauli katika vitabu vya zamani na vya sasa kuhusu sababu za kushuka Aya mbili hizi, nikatoka na natija kuwa wapokezi na wafasiri wametofautiana kwenye kauli tatu kuhusu sababu za kushuka Aya hizi.

KAULI YA KWANZA

Kuwa jamaa katika Waumini walisema, tuwatakie msamaha wafu wetu washirikina; kama alivyomtakia msamaha Ibrahim baba yake, ndipo zikashuka Aya mbili hizi.

Haya yametajwa na Tabari, Razi na Abu Hayan Al-andalusi. Vile vile mwenye Tafsiri Al-manar na wengineo.

Kauli hii ina nguvu kuliko kauli nyingine, kwa sababu katika Aya hizo kuna matamko yanayofahamisha hivyo; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu “…na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina ijapokuwa jamaa …”

Kwa hiyo kukatazwa waumini kuwatakia msamaha jamaa zao, washirikina, kunatambulisha kuwa wao walikuwa wakiwatakia msamah au walijaribu kufanya hivyo.

Vile vile kauli isemayo:“Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake …”

Hilo ni jawabu la kauli ya waumini waliposema: Kama alivyomtakia msamaha Ibrahim baba yake.

KAULI YA PILI

Kwamba Mtume(s.a.w.w) alikwenda kwenye kaburi la mama yake akalia, na kumtaka idhini Mola wake amwombee msamaha, ndipo zikashuka Aya mbili hizo. Kauli hii wameitaja wale tuliowanukuu kwenye kauli ya kwanza.

Kauli hii inaizidi ile isemayo kuwa zilishuka wakati wa kufa Ami yake Abu Twalib. Kwa sababu Abu Twalib alikufa Makka katika mwaka wa huzuni miaka mitatu kabla ya Hijra, na Sura ya Tawba yenye Aya hizo mbili ilishu- ka Madina mwaka wa 9 Hijra – miaka 12 tangu kufa AbuTwalib.

KAULI YA TATU

Kwamba Aya mbili hizi zilishuka kwa Abu Twalib kwa madai ya kwamba Mtume alimwambia Ami yake, AbuTwalib akiwa karibu ya kukata roho: “Ewe Ami sema: “Lailaha illa llah” lakini hakusema, Mtume akasema: “Nitakuombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu maadamu sijakatazwa”

Kauli hii imejibiwa na kundi la maulama kwa kauli mbili:

Kwanza : kuwa Aya mbili, kama tulivyodokeza, zilishuka baada ya kufa Abu Twalib.

Pili : kwamba Abu Twalib alikufa baada ya kusilimu na kuufanyia ikhlasi Uislamu wake, Tazama kitabu Al-Ghadiri cha Aminiy J7 Uk 369 chapa ya mwaka 1967.

HALI HALISI

Kama tukiachana na kauli za wafasiri na wapokezi, tukaiweka itikadi ya Abu Twalib kutegemea alivyokuwa, kulingana na mambo yalivyo, basi natija itakuwa kwamba Abu Twalib alikuwa akiamini utume wa Muhammad(s.a.w.w) katika kauli zake zote na vitendo vyake, Na huo ndio Uislamu hasa.

Mtume aliinukia akiwa ni yatima wa baba na mama – Baba yake alikufa akiwa yuko tumboni na inasemekana kuwa alikuwa mtoto mchanga. Mama yake akafa akiwa na miaka sita, Akabaki katika malezi ya babu yake, Abdul Muttwalib, kiasi cha miaka minane.

Babu yake alipofikiwa na mauti alimkabidhi kwa Abu Twalib. Abu Twalib hakuwa ndiye mtoto mkubwa wa Abdul Mutwalib, wala hakuwa na mali nyingi isipokuwa alikuwa ndiye mwenye heshima, mwenye hulka nzuri na mkarimu sana kuliko ndugu zake wote.

Kwa hiyo Abu Twalib akamlea vizuri; akampenda sana kuliko watoto wake; alitunga kasida ndefu na fupi kumsifu; alikuwa akitabaruku naye na akimtegemea wakati wa balaa kutokana na karama zilizodhihiri kwake.

Imepokewa kutoka kwa Ibn Asakir, kwamba watu wa Makka walipatwa na kahati; akatoka Abu Twalib na Muhammad akiwa ni kijana akaomba mvua kwa uso wake. Ikabubujika mvua na ardhi ikarutubika.

Ismail Haqqi anasema katika Rawhilbayaan katika kufasiri (12:45): “Abu Twalib alimlea na kumhami Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na kumtetea katika uhai wake”.

Ilivyo ni kwamba yeye ni miongoni mwa waliokuwa na imani kama ilivyotangulia kuelezwa.

JE, KUNA SIRI GANI?

Ikiwa Abu Twalib anampenda Muhammad, anajitolea kwa nafsi yake na kuwa tayari kufa ili amsaidie, kutegemea ukweli wake na msimamo wake, naye aliona aliyoyaona katika karama zake, kabla ya utume na baada ya utume, kwa nini basi asiamini utume wake?

Ikiwa ni kweli madai ya kuwa Abu Twalib si Mwislamu basi itabidi kuweko na siri iiyomzuia kuwa Mwislamuu Je, ni siri gani hiyo? Je, Abu Twalib, aliyekuwa akimjua kiuhakika Muhammad, alimwona na mambo yanayopingana na Utume? Hapana! Mwenye kudai hivyo si Mwislamu kabisa!

Kisha itakuwaje Muhammad(s.a.w.w) aweze kuwakinaisha wachunga ngamia na wale waliokuwa hawajui chochote zamani, lakini ashindwe kumkinaisha ami yake, Abu Twalib ambaye alikuwa akimjua chimbuko lake?

Je, Abu Twalib alikuwa na akili ndogo kuliko Bedui wa jangwani, au alikuw ana tamaa iliyomzuia kusilimu, kama walivyozuilika wenye tamaa? Matamanio ambayo yangeweza kumzuia Abu Twalib kuingia Uislamu ni moja kati ya mambo mawili: Ama kuhofia mali yake na utajiri wake, na ilivyo ni kwamba Abu Twalib aliishi maisha ya kifukara na alikufa fukara. Au itakuwa ni kuhofia kuondokewa na uongozi katika nyumba ya Hashim nk, na ni kinyume cha hivyo.

Ikiwa sababu hizo mbili hazipo, na tukiunganisha kukosekana sababu na mambo yanayoelekeza Uislamu wake, ambayo ni kumpenda kwake Muhammad na kujua uhakika wake, basi natija ni kwamba Abu Twalib sio tu kuwa alisilimu bali ni katika waislamu wa mwanzo.

Vile vile ikiwa itabatilika kauli kuwa Aya mbili zilimshukia Abu Twalib na haikuthibitika riwaya sahihi kwamba zilishuka kwa sababu ya mama wa Mtume, basi itabakia kauli ya kwanza, kwamba ziliwashukiwa watu waliokuwa au waliojaribu kuwaombea msamaha watu wao; na dhahiri ya Aya mbili inaliweka wazi hilo.

MAANA

Haimfalii Mtume na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina ijapokuwa ni jamaa.

Imeelezwa katika Tafsir Tabari haya yafuatayo; ninanukuu: “Watu katika maswahaba wa Mtume(s.a.w.w) walisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Katika mababa zetu wako waliokuwa na ujirani mwema, wakiunga udugu, wakisadia na kutekeleza madeni; je, tuwatakie msamaha? Akasema: Kwa nini isiwe hivyo, nami nitamtakia msamaha baba yangu, kama Ibrahim alivyomtakia msamaha baba yake, Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hiyo.”

Utauliza : kuwa itakuwaje Mtume(s.a.w.w) atoe idhini kwa masahaba zake kuwatakia maghufira baba zao washirki na ikiwa ni haramu?

Jibu : Kila kitu ni halali mpaka kikatazwe; na wakati Mtume alipotoa idhini kuombea msamaha hakukuwa kumekatazwa; baada ya kukatazwa, aliwakataza.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) anabainisha sababu za kukataza kwa kusema:

Baada ya kuwabainikia kuwa wao ni watu wa motoni.

Aya hii inatufahamisha kuwa mtu anahukumia ukafiri wake na imani yake kutokana na dhahiri ya hali yake, na kwamba ambaye dhahiri yake ni ukafiri basi haifai kumtakia msamaha wala kumrehemu.

Utauliza : Ikiwa kuwaombea msamaha washirikina ni haramu, kwanini Mtume aliwaombea msamaha watu wake walipomvunja meno na wakamchana uso wake? Imethibitika kwamba yeye alisema: “Ewe Mola Wangu! Wasamehe watu wangu, kwani wao hawajui.”

Wafasiri wengi wamelijibu swali hii kwamba Aya imekataza kutakiwa msamaha washirikina waliokufa, sio waliohai wanaotarajiwa imani yao.

Jibu : tunaloliona ni kwamba kutaka msamaha kwa Mtume(s.a.w.w) kulikuwa ni kusamehe haki yake ya kibinadamu, sio kusamehe haki ya Mwenyezi Mungu na maghufira kwa ushirikina.

Na, hakuna mwenye shaka kwamba inafaa kwa mtu kusamehe haki yake, inayomhusu yeye tu, kwa mwislamu na kafiri.

Swali la pili : Ibrahim alikuwa akimlingania baba yake kwenye imani na kumhimiza na kumwahidi kumtakia msamaha; kama asemavyo Mwenyezi Mungu:

إِلَّا قَوْلَ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ لَأَسْتَغْفِرَنَّ لَكَ وَمَا أَمْلِكُ لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ ﴿٤﴾

“… Ila kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika nitakuombea msamaha, wala similiki chochote kwa ajili yako mbele za Mwenyezi Mungu…”(60:4)

Naye alitekeleza ahadi yake hii na akamwombea msamaha kwa kusema:

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾

“Ewe Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wawili na waumini, siku ya kusimama hisabu.” (14:41)

Sasa vipi Ibrahim(a.s) alimtakia msamaha baba yake, ambapo kumtakia msama mshirikina hakufai? Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejibu swali hilo kwa kusema:

Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila ni kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye, lakini ilipompambanukia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye.

Yaani Ibrahim(a.s) alimtakia msamaha baba yake kwa vile tu, alimwahidi kuwa atamwamini Mungu. Alipovunja ahadi na kumbainikia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu alijiepusha naye.

Sio mbali kuwa dua ya Ibrahim(a.s) kwa baba yake, ni sawa na dua ya Muhammad(s.a.w.w) kwa watu wake washirikina; yaani kusamehe haki yake ya kibinadamu, sio haki ya Mwenyezi Mungu na kutakia msamaha ushirikina.

Hilo linatambulika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu.

Hakika Ibrahim alikuwa Mpole sana wa moyo mvumilivu.

Mpole wa moyo ni yule mnyenyekevu na mvumilivu ni yale anayesamehe akiwa na uwezo. Na, Ibrahim alisamehe kauli ya baba yake:

لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾

“Usipokoma nitakupiga mawe, na niondokelee mbali kwa muda mhache” (19:46)

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِلَّ قَوْمًا بَعْدَ إِذْ هَدَاهُمْ حَتَّىٰ يُبَيِّنَ لَهُم مَّا يَتَّقُونَ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١١٥﴾

115. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwapoteza watu baada ya kuwaongoza; mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo Hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu.

إِنَّ اللَّـهَ لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿١١٦﴾

116. Hakika Mwenyezi Mungu ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, huhuisha na hufisha; nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

MWENYEZI MUNGU HAWAPOTEZI WATU

Aya 115 –116

MAANA

Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwapoteza watu baada ya kuwaongoza.

Makusudio ya kuwapoteza ni kuwahisabu na kuwachukulia kuwa wamepotea. Na makusudio ya watu ni waumini tu; kwa dalili ya kauli yake, ‘baada ya kuwaongoza.’

Maana ni kuwa waumini wakifanya kitu chochote wasichokijua kuwa ni halali au haramu; kama vile kuwaombea msamaha au kuwarehemu washirikina kwa kutojua uharamu, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatawaadhibu, mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo kwa ubainifu ulio wazi wa kiasi. Baada ya ubainifu, wakifanya uasi,hapo watastahiki adhabu.

Tafsiri bora ya Aya hii ni kauli ya Mtume mtukufu(s.a.w.w) : “Mtu yoyote aliyefanya jambo kwa kutojua hana neno.” Na kauli ya Imam Ja’far Asswadiq(a.s) : “Kila kitu ni halali mpaka kikatazwe.”

Hakika Mwenyezi Mungu ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, huhuisha na hufisha, nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Aya ikowazi na mfano wake umekwishapita mara nyingi na utaendelea kuja. Lengo ni kuwa binadamu daima awe pamoja na Mungu na kuukumbuka ukuu wake; na kwamba yeye peke yake ndiye bwana wake, ili asiweze kupetuka mpaka wowote katika mipaka yake.

لَّقَد تَّابَ اللَّـهُ عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٧﴾

117. Hakika Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Mtume na wahajiri na Answar waliomfuata saa ya dhiki. Baada ya nyoyo za baadhi yao kukurubia kugeuka, Kisha akawakubalia toba. Hakika yeye kwao ni Mpole Mwenye kurehemu.

وَعَلَى الثَّلَاثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُوا حَتَّىٰ إِذَا ضَاقَتْ عَلَيْهِمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ وَضَاقَتْ عَلَيْهِمْ أَنفُسُهُمْ وَظَنُّوا أَن لَّا مَلْجَأَ مِنَ اللَّـهِ إِلَّا إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ لِيَتُوبُوا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١١٨﴾

118. Na pia wale watatu walioachwa nyuma, mpaka ardhi ikawa finyu juu yao pamoja na wasaa wake; na nafsi zao zikadhikika juu yao, na wakayakinisha kuwa hakuna kwa kumkimbia Mwenyezi Mungu isipokuwa kwake. Kisha akawakubalia toba ili wapate kutubu. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwingi wa kukubali toba Mwenye kurehemu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ ﴿١١٩﴾

119. Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wa kweli.

MWENYEZI MUNGU AMEMKUBALIA TOBA MTUME

Aya 117 – 119

MAANA

Bado maelezo ni ya vita vya Tabuk na matukio yake, Vita hivi vina mambo yake mahsusi yasiyokuwa katika vita vingine.

Miongoni mwa mambo hayo au yaliyo muhimu ni kuwa jeshi lilikuwa katika joto, njaa, kiu na uchache wa vipando, Ndio maana jeshi hili likaitwa ‘Jeshi gumu.’

Wapokezi wanasema kuwa kikundi fulani cha jeshi la Waislamu walikuwa wakipokezeana kupanda ngamia mmoja; chakula chao kilikuwa ni shayiri yenye wadudu na tende yenye mabuu, Mmoja wao alikuwa anaweza kufyonza tende akipata ladha yake, humpa mwenzake. Kuhusu maji walikuwa wanapochinja ngamia wanakamua mavi yaliyo katika utumbo wake na kurambisha ndimi zao.

Wanafiki walirudi nyuma kwenye vita hivi, Yamekishatangulia maelezo kuwahusu wao, Ama Waumini, ambao walimfuata Mtume(s.a.w.w) katika vita vya Tabuk, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewashiria kwa kusema:

Hakika Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Mtume na wahajiri na Answar waliomfuata saa ya dhiki.

Ikisemwa kuwa fulani ametubia basi hufahamika kuwa alikuwa na dhambi, kisha akatubia, na ikisemwa kuwa Mwenyezi Mungu amepokea toba hufahamika kuwa amemkubalia toba yake. Lakini vile vile ina maana ya kuelekezwa rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi yake kulingana na jumla ilivyo.

Maana ya kukubaliwa toba ndiyo yaliokusudiwa kwa wale watatu. Na maana ya rehema na radhi ndiyo yaliyokusudiwa kwa Mtume na swahaba waliomfuata katika saa ya dhiki. Hii inatokana na hali halisi ilivyo ya isma ya Mtume(s.a.w.w) na utiifu wa waliomfuata katika saa ya dhiki.

Baada ya nyoyo za baadhi yao kukurubia kugeuka.

Waliorudi nyuma walirudi nyuma, na Waumini katika wahajiri na Answari wakamfuata, lakini kikundi katika hawa walipozidiwa na shida na ugumu wa safari walilegea na kukusudia kuachana na Mtume, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwapa uthabiti na kuwalinda. Hivyo wakavumilia na kujitolea.

Kisha akawakubalia toba kutokana na vile walivyoazimia kumwacha Mtume.

Makusudio ya kuwakubalia toba hapa ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwachukulia kuwa hawakudhamiria dhambi, Kwa sababu mwenye kud- hamiria dhambi kisha asilitende, haandikiwi kitu.

Hakika yeye kwao ni Mpole, Mwenye kurehemu.

Kwa vile yeye alijua kwao ukweli katika imani yao na ikhlasi katika nia yao na kwamba dhamira yao ilikuwa ni jambo lililozuka tu na kuondoka bila ya kuacha athari yoyote.

Na pia wale watatu walioachwa nyuma, mpaka ardhi ikawa finyu juu yao pamoja na wasaa wake; na nafsi zao zikadhikika juu yao, na wakayakinisha kuwa hakuna kwa kumkimbia Mwenyezi Mungu isipokuwa kwake.

Wameafikiana wafasiri na wapokezi kwamba watatu hao ni katika waumini wa Kianswari, waliobaki nyuma katika vita vya Tabuk kwa uvivu na kupuuza, sio kwa unafiki na inadi. Hao ni Kaab bin Malik, Mar’wan bin Rabii na Hilal bin Umayya Al-waqif.

Masimulizi ya hao tunamwamchia Twaha Hussein aliyeleta Muhtasari wa yale waliyoyoafikiana wote na yanayofahamika katika Aya, Anasema katika Kitab mir-atul-islam:

“Watatu hawa walikuwa na imani kubwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wenye mapenzi ya ukweli kwake yaliyowafanya wasiongezee kosa la uwongo baada ya lile la kubaki nyuma. Kwa sababu ya ukweli na kuhofia Mwenyezi Mungu kuwafedhehesha waongo, walikiri makosa yao; na Mtume akawasikia na kutangaza kuwa wao ni wakweli, lakini pamoja na hayo hakuwasamehe; akaamrisha waumini wasiwasemeshe. wakawa wametengwa wakiwa mbali kabisa na watu; wakawa katika hali ambayo, jela ilikuwa bora kuliko hali hiyo.

Siku moja Mtume akatuma ujumbe wa kuwaaamuru watengane na wake zao. Hilo sio ajabu, kwa sababu wake zao ni waumini; na amri imetoka kuwa waumini wote watengane nao.

Baada ya kupita siku hamsini wakiwa wamejuta sana, Mwenyezi Mungu aliteremsha Aya kuwatakabalia toba yao. Waumini wote wakalifurahi hilo wakawa wanawapongeza hawa watatu kwa kutakabaliwa toba. Kaab, alifurahi sana; akadhamiria kutoa sadaka mali yake yote, lakini Mtume akamwamuru atoe sehemu tu, Kaab akaahidi kutosema uwongo mpaka kufa.

Kisha akawakubalia toba ili wapate kutubu. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwingi wa kukubali toba Mwenye kurehemu.

Utauliza : kuwa dhahiri ya kukubaliwa toba ni kuwa walitubu na wakakubaliwa toba; na dhahiri ya ili wapate kutubu ni kuwa hawajatubia bado; sasa je, kuna wajihi gani?

Swali hilo limejibiwa kwa majibu mengi . Lenye nguvu zaidi ni lile lise- malo kuwa makusudio ya kukukabaliwa toba ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwakubalia toba ili watubu na wasiendelee na dhambi na waseme lau Mwenyezi Mungu atatukubalia toba yetu, basi tutatubu kabisa. Hiyo inafanana na mtu unayempenda akikufanyia uovu nawe unataka kumsamehe, ukamfundisha msamaha ili aombe, nawe umsamehe.

Tumeweka mlango maalum wa toba katika Juz.4 (4: 17).

Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wa kweli.

Wakweli ni Mitume na wale ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na kuwatakasa kabisa kabisa. Kwa maneno mengine, makusudio ya ukweli hapa sio kutosema uwongo tu katika mazungumzo, kwa sababu wako watu wasiosema uwongo lakini haifai kuwafuata katika kila jambo; isipokuwa makusudio ni ukweli katika kauli vitendo na elimu ambavyo vitamwandaa mwenye navyo kuweza kufuatwa.