Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

USHAHIDI WA HADITHI NYINGINE JUU YA AHLUL BAYT (A.S)

0 Voti 00.0 / 5

USHAHIDI WA HADITHI NYINGINE JUU YA AHLUL BAYT (A.S)

Kuna hadithi nyingi sana za Mtume Muhammad (s.a.w.w) zinazoonyesha fadhail na uongozi wa Ahlul Bayt (a.s). Tutatoa hadithi chache hapa chini, kutoka katika vitabu vya Kisunni ili kuthibitisha nafasi ya Ahlul Bayt baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w):

1- Ibn Abbas amesimulia kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) kasema: "Nyota huwaongoza watu wa dunia ili wasiangamie. Hali kadhalika Ahlul Bayt wangu ni viongozi wa Ummah wangu watakao uepusha ummah wangu kutokana na utengano na kutofautiana (kukhitilafiana); na yeyote miongoni mwa makabila ya kiarabu atakayewapinga, atakuwa ni kutoka katika kundi la Iblis". Rejea (Mustadrak Sahihein, Juz .2, Uk. 343; Sawaiq Al-Muhriqah, Uk. 235).

Ingekuwa wakureishi walikubaliana juu ya Uimamu wa Ali bin Abitalib (a.s) na wangekuwa hawakumpinga Mtume (s.a.w.w) juu ya suala hili, Ummah wa Kiislamu ungekuwa umeepukana na Utengano na Khitilafu. Lakini kwa bahati mbaya ukhalifa wa Ali (a.s) ulifosiwa, na Ahlul Bayt walipingwa.

2- Jinsi ya Kumsalia Mtume (s.a.w.w), Mtume Muhammad (s.a.w.w) amewaelekeza waislamu kuwajumuisha Ahlul Bayt wake (Aali Muhammad) wakati wa kumsalia Mtume (s.a.w.w), na hairuhusiwi kuliondoa neno Aali Muhammad wakati wa kumsalia Mtume (s.a.w.w) . Kwenye Sahih Bukhari, imeelezwa kwamba, siku moja masahaba walimuuliza Mtume Muhammad (s.a.w.w): "Ewe Mtume wa Allah, tumeelewa jinsi ya kukusalim, lakini tufundishe jinsi ya kukusalia (kumsalia Mtume)". Naye alijibu: "Semeni Allaahumma salli alaa Muhammad wa alaa Aali Muhammad, kama sallayta Alaa Ibrahima wa alaa Aali Ibrahim, Innaka Hamidun Majid.
Rejea (Sahihi Bukhari, Juz.8, Uk. 245).
Swali hili liliulizwa na masahaba baada ya amri ya kumsalia Mtume (s.a.w.w) kuteremka katika Qur'an hku ikisema: "INNALLAHA WA MALAAIKATAHU YUSALLUNA ALAN NABII. YAA AYYUHAL LADHIINA AAMANU SWALLU ALAIHI WA SALLIMU TASLIIMA" - "Kwa hakika Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamtakia rehema Mtume. Enyi mlioamini! Mtakieni rehema Mtume na msalieni". (Ahzab 33:56).
Maulamaa wa Kisunni na wa Kishia wamekubaliana kuwa aya hii ilishuka kwa ajili ya fadhail za Mtume na Ahlul bayt wake. Rejea vitabu vifuatavyo vya Kisunni: 1- Asbabun Nuzul cha Wahidi,Uk. 271. 2- Al -Mustadrak cha Hakim, Juz. 3, Uk. 148.

3- Tafsiir Fakhruddin Raazi, Juz. 25, Uk. 226. 4- Riyadhu Swalihiin cha Nawawi, Uk. 4555. 5- Jamii' Li Ahkamil Qur'an cha Qurtubi, Juz.14, Uk. 233-34.
Imesimuliwa katika Sawaiq Al-Muhriqah cha IbnHajar (Uk. 144) kwamba: Mtume Muhammad (s.a.w.w) alisema: "Msiibutue sala pale mnaponisalia (laa tusalluu alaiyya salaaatul BATRAA)". Baada ya kuulizwa nini hiyo sala ya batraa (ubukuaji wa sala ya Mtume (s.a.w.w)), Mtume (s.a.w.w) alijibu: "Mnaposema : Allahuma swalli alaa Muhammad - na mkaishia hapa, hii ndio salaaatul BATRAA, na badala yake nisalieni hivi: Allahumma swalli alaa Muhammad wa Aali Muhammad."
Kwa bahati mbaya ndugu zetu wa Kisunni wanapomsalia Mtume (s.a.w.w), wanajiepusha kusema kuwasalia AALI MUHAMMAD, hivyo wanamsalia Mtume (s.a.w.w) sala isiyotimia na wanakwenda kinyume na maelekezo ya Mtume (s.a.w.w). Kwa mfano katika mawaidha au vikao, wasikilizaji wa Kisunni, kwa kawaida wanaposikia jina la Mtume humsalia sala isiyokamili kwa kusema ALLAHUMMA SWALLI WA SALLIM ALAIHI, bila kusema WA AALIHI. Hata maulamaa wa Kisunni wanapoandika jina la Mtume (s.a.w.w) wanaiandika sala isiyotimia ambayo ni SWALLALLAHU ALAIHI WASSALLIM; wanaondoa "WA AALIHI", Je ni ujinga au wivu, au kujiegemeza upande wao / kujipendelea hata kama sio sahihi au nini, nashangaa? Katika hadithi nyingine, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alisema: "Yeyote atakaye sali sala na ndani ya sala yake na asinisalie mimi na Ahlulbyt wangu, basi sala yake haitokubaliwa". (Tazama : Shifaa ya Qaadhi Ayadh Maghrabi Juz. 2, Uk. 55; vile vile Sawaiq Al-Muhriqa cha Ibn HajarUk. 139).
Mwanachuoni wa Kisunni Fakhrud Diin Raazi katika Tafsiri yake (Juz.7, Uk. 391) amesema Ahlubayt ni sawa na Mtume katika mambo matano: (1) katika kuwasalia (2) Salamu (3) Tahara yaani Ismah (wametoharia kuokana na madhambi) (4) Sadaka kwao ni haramu (5) Kuwapenda ni wajibu.
Imam Shafii amesema katika shairi lake maarufu kuwasifu Ahlulbayt: "Ahlulbayt wa Mtume, kukupendeni nyinyi ni wajibu kwa kila mwislamu kama ilivyofunuliwa kwenye Qur'an. Hii ni fadhaila kubwa sana kiasi ya kwamba kwa yeyote ambaye hatowasalia, basi sala yake inakuwa batili".

3 Aya ya Mawaddah - "QUL LAA AS'ALUKUM ALAIHI AJRAN ILLAL MAWADDATA FIL QURBAA". - "Sema sikuombeni ujira isipokuwa nakutakeni muwapende jamaa zangu wa karibu". (Shura 42:23). Tafsiri zote na vitabu vya hadithi kwa pamoja vinasema kuwa Ahlulbayt na Qurba hapa ni Ali, Fatima, Hassan na Hussein, na kuwapenda ni wajibu kwa kila mwislamu kwa sababu iliposhuka aya hii Mtume (s.a.w.w) aliulizwa: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani hao jamaa zako wa karibu (Qurbaa) ambao kuwapenda imekuwa ni wajibu kwa kila mwislamu? Mtume a(s.a.w.w)lijibu: "Ni Ali, Fatima na watoto wao wawili ambao ni Hassan na Hussein". Tazama : 1. Sahih Bukhari, Juz. 6, Uk. 129. 2. Tafsiir Tabara, Juz. 25, Uk. 14. 3. Tafsiir Al -Kasshaf, Juz. 3, Uk. 402. 4. Tafsiir Al -Waadhih , Juz. 25, Uk. 19.
Aya hii ya Mawaddah iliposhuka (42:23), baadhi ya watu walianza kuwaza akilini mwao kuwa Mtume (s.a.w.w) anataka tuwapende Ahlulbayt wake kwa matakwa yake mwenyewe. Hivyo Jibril alikuja na kumwambia Mtume. Baadhi ya watu wanakulaumu kua unafanya upendeleo. Hivyo aya hii ikashuka: "Je mnasema ameitunga Qur'an?" (Shura 42:24).
Alhamdulillah, sisi Shia Ithna Ashariyah tunawapenda Ahlulbayt, na tunawapa nafasi wanayostahili kupewa, tunawafanyia Maulid kila mmoja wao, tunafurahia furaha zao na hatuzifurahii huzuni zao, na tunaamini kuwa wao ni viongozi wetu baada ya Mtume (s.a.w.w.).
Tunawaita Waislamu wote kujiunga nasi katika kuwafuata Ahlulbayt baada wa Mtume (s.a.w.w). Qur'an inasema katika aya hiyo hiyo ya Mawaddah : "Na yeyote atakayechuma wema (kwa kuwapenda Ahlulbayt) tutamzidishia wema, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukurani .(Shura 42:23). Rejea (Tafsiir Baghawi na Tafsiir Tha'labiy).

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini