TOFAUTI KUU ZA SHERIA 1

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

TOFAUTI KUU ZA SHERIA 1

ALLAH (Subhanahu Wataala) NA

SHERIA AZITUNGAZO MWANAADAMU.
"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha
(humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma na Mwenye Kurehemu, Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo. Sala na salamu ziwe juu ya kipenzi wa viumbe vyote duniani, mbora wa viumbe, Mtume wetu (Swalla Allahu Alayhi Wasalam). Shukrani ni zake Allah (Subhanahu Wataala) na Kwake tunajitakasa na Kwake tunaomba msaada, muongozo sahihi na msamaha wa makosa yetu. Tunaomba hifadhi Kwake Yeye Allah (Subhanahu Wataala) kutokana na vitimbi vya sheytan na hifadhi ya makosa ambayo tumeyatenda.

UTANGULIZI.

Hamna shaka yoyote kuwa kuna tofauti kubwa baina ya Sheria za Kiislamu na zile atungazo mwanaadamu. Sababu hii ndiyo inayowafanya maadui wa Uislamu kuzitaka Sheria za Kiislamu ziwe ni kama za kwao. Masikio na macho yetu hayajaacha kushuhudia ni namna gani Sheria za Kiislamu zinavyopingwa mbele ya wale Makafiri na hata Waislamu poa. Kwa Muislamu wa kweli anaelewa fika kuwa ni sheria za Allah (Subhanahu Wataala) ndizo zitampa mafanikio hapa duniani na Akhera. Nimejitahidi kutoa maneno yalokuwa magumu na kutumia zaidi maneno ya Kiswahili ili makala hii iweze kusomeka na Waislamu wote. Yapo baadhi ya maneno ambayo nimeyawekea kwenye mabano kwa ueleo mzuri. Hali kadhalika nimeonelea kuonesha mifano michache kwa kutumia sheria za nchi ili kuweka wazi hoja.
Makala hii nimeigawa na kuelezea kwenye vipengele vifuatavyo:
1. Asili ya Sheria za Kiislamu.

2. Sheria za Kiislamu hazina tofauti ya mwanaadamu.

3. Sheria za Kiislamu zinaenda na wakati.

4. Sheria za Kiislamu na Muumba.

5. Sheria na mahusiano ya wanaadamu.

6. Usimamizi na muundo wa sheria.

7. Adhabu (Punishment)

8. Malipo mema kwa anayejiepusha kuvunja sheria.
Baada ya kusoma makala hii, utakuwa na nafasi nzuri ya kuelewa ni namna gani sheria za Kiislamu zinamfaa binaadamu. Tofauti kuu baina ya Sheria za Kiislamu na zile zitungwazo na binaadamu utapata kuzielewa na kujiweka katika ufahamu mzuri wa dini ya Kiislamu. Mwisho utakuwa na uwezo mzuri wa kuzitetea sheria hizi mbele ya wale wasiozifahamu au wale wanaozikejeli.
I - ASILI YA SHERIA ZA KIISLAMU
Kwa dunia ya sasa na maisha yaliyotuzunguka, hapana shaka kuwa Sheria nyingi zinazotugusa ni kutoka kwa binaadamu ambazo zinaamrisha mwenendo wa binaadamu na mahusiano yake na Serikali ilokuwa madarakani. Qur-aan na mafundisho ya Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) ndio chanzo na msingi wa Sheria za Kiislamu.
Tunaposema sheria za Uingereza, Marekani n.k ni mifano ya sheria za binaadamu. Takriban mataifa mengi, yakiwemo Tanzania, Uganda na Kenya. Ukiachilia nchi za Kiislamu, nchi nyingi zina sheria za Muingereza (Common Law). Tofauti na sheria za Kiislamu ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja kwa Allah (Subhanahu Wataala). Sheria za duniani zinatoka kwa binaadamu ambaye ameumbwa na Allah (Subhanahu Wataala). Hivyo, sheria za binaadamu ni zenye kubadilika, wakati Sheria za Kiislamu hazibadiliki kwa sababu zimewekwa na Allah (Subhanahu Wataala). Tokea mwanzo wa kuumbwa mwanaadamu, ni jambo lisilopingika kuwa mwanaadamu hana ukamilifu kwenye maisha yake, ni mnyonge, asiyejitosheleza kwa nafsi yake moja. Matokeo yake ni sawa sawa na sheria zake, hazina ukamilifu wowote. Dunia inazunguka na kuendelea ndivyo sheria zake zinavyobadilika na kuhitaji mabadiliko ili ziendane na wakati. Kwa maneno mengine sheria za mwanaadamu hazina ukamilifu kwenye sehemu yoyote wala haziwezi kuwa kamili mpaka binaadamu aondokane na kasoro zote. Sheria za Kiislamu zinagusa sehemu zote za maisha ikiwa ni katika uchumi, jamii, siasa au imani.

MWISHO