TOFAUTI KUU ZA SHERIA 5

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

TOFAUTI KUU ZA SHERIA (5)
SHERIA NA MAHUSIANO YA WANAADAMU.
Wamejiwekea wanaadamu sheria zinazoeleza mahusiano baina ya watu “tort.” Sheria hizi hazina uhusiano wa maadili, msingi mkuu wa sheria hizi (tort) ni kutoka kwa aliyevunjiwa hizo sheria na wala sio Serikali.
Kwa upande wa Uislamu, kiini kikuu cha mahusiano ya wanaadamu ni kutoka kwenye Qur-aan ambayo inakataza dhana mbaya, kupeleleza na kusengenya. Allah (Subhanahu Wataala) anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:
{Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na (kuwadhani watu) dhana (mbaya) kwani (kuwadhani watu) dhana (mbaya) ni dhambi. Wala msipeleleze (habari za watu). Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine. Je! Mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa? La, Hampendi; (Basi na haya msiyapende). Na Mcheni Mwenyezi Mungu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba (na) Mwingi wa kurehemu.} [Suratul Al-Hujurat: 149]
Hivyo, sio tu sheria ya Kiislamu inakataza mahusiano mabaya baina ya wanaadamu bali inaeleza kwanini asifanye hivyo na kutolea mfano ni namna gani lilivyo hilo kosa kuwa ni kubwa. Hapa tumeoneshwa kusengenya ni mfano wa kula nyama ya ndugu yako tena aliye maiti. Subhanallah!
Baadhi tu ya kasoro juu ya sheria hizi ni kama ifuatavyo:
Hazielezi (tort) ni kwa nini mwananchi asikiuke hizo sheria. Bali zinamzuia na kumlazimisha tu kufuata hiyo sheria. Kwa mfano asiwashe redio sauti kubwa hadi kumuudhi jirani. Akiwa hayupo jirani? Ni ruhusa kuwasha? Je wapita njia? Ndege warukao? Haki za majini na malaika zipo hapa? Majibu yote utayapata kuwa sheria za mwanaadamu hazina mazingatio kwa viumbe vyote. Zinagusa sehemu chache tu ya vitu.
Kasoro nyengine ni kuwa hazifikishwi Mahakamani kuvunjwa kwake ila mpaka aliyekosewa afunguwe kesi kwa gharama zake mwenyewe. Serikali haina mkono wake kwenye kesi hizi. Hii ni kwa sababu sheria za mwanaadamu hazitaki kujiingiza kwenye mahusiano haya wala hazigusi maadili. Tofauti na Uislamu, umegusa kila nyanja ya maisha ya mwanaadamu. Katu Taifa la Kiislamu haliruhusiwi kukimbia majukumu kwani sheria zote zinatoka kwa Mkuu wa Serikali zote duniani, naye ni Allah (Subhanahu Wataala).

MWISHO