TOFAUTI KUU ZA SHERIA 6

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

TOFAUTI KUU ZA SHERIA (6)

USIMAMIZI NA MUUNDO WA SHERIA.

Tofauti nyengine inahusiana na usimamizi na namna zinavyoundwa hizo sheria.

Kawaida, jamii fulani inaunda sheria zake kwa ajili ya kutawala jamii husika na kuilinda. Mfano Hitler alipoingia madarakani alipitisha sheria ya kuuawa kwa Mayahudi wote ilimradi tu kulinda maslahi ya wajerumani walio wengi ndani ya Ujerumani. Alipoondoka madarakani sheria hii ikafa. Ama kwa Sheria ya Kiislamu, sio ya jamii fulani pekee. Inagusa ulimwengu mzima hata kwa wasio Waislamu. Kwa mfano kuna sheria baina ya taifa la Kiislamu linavyoishi na wasio Waislamu (Dhimmi). Muislamu hatakiwi kuimwaga damu ya binaadamu hata awe Dhimmi bila ya sababu. Ni dhambi kubwa kuimwaga damu ya Muislamu bila ya sababu yoyote. Maingiliano baina ya Waislamu na wasio Waislamu, uchumi wa Kiislamu na siasa za Kiislamu ni vipengele vilivyokuwa huru kutumiwa na walimwengu wote kwani kuna faida kubwa. Ikiwa ni Muislamu au sio Muislamu. Sheria ya Kiislamu ni ya ulimwengu mzima na watu wake wote. Tofauti na sheria za binaadamu ambazo haziwezi kwenda pamoja na maendeleo anayofanya mwanaadamu duniani. Ni lazima zitabadilika tu.

Dhumuni kuu ya Sheria ya Kiislamu haikufungwa kuzunguka jamii pekee. Bali kumpa haki kila mmoja, kuunda jamii yenye tabia nzuri, taifa imara na mwisho kuifanya dunia sehemu inayofaa kuishi kwa mazingira yake mwenyewe binaadamu.

ADHABU (PUNISHMENT)

Adhabu za Sheria ya Kiislamu pia ni tofauti na sheria za mwanaadamu. Hakika haitakuwa sheria ikikosa adhabu, na kama sheria itakosa adhabu ni sawa na msumeno usokuwa na meno (makali) au kisu butu. Ingawa zote zinawaadhibu wanaokiuka hiyo sheria, lakini bado tofauti ipo.

Kabla ya kuendelea mbele, lazima tuelewe kuwa Uislamu umeletwa kwa wanaadamu wote. Hivyo kukataa kufuata Uislamu hapa duniani na kuabudia asiyekuwa Allah (Subhanahu Wataala) basi hilo pia ni kosa.

Sheria ambazo atakiuka Muislamu ataadhibiwa Qiyama na mara nyengine sheria inaruhusu kuadhibiwa duniani na Qiyama pia. Kwa mfano shirk, khadaa ya kujifanya umefunga, kibri, riyaa na dhambi nyenginezo ambazo haziwezi kuonekana ila kwa Allah (Subhanahu Wataala) zitaenda kuadhibiwa Qiyama, hii ni kwa sababu zinafanywa kupitia ndani ya nafsi ya mwanaadamu. Ni Yeye Allah (Subhanahu Wataala) pekee mwenye uwezo wa kuona kinachopita ndani ya nafsi. Kwa nini tuseme hivi?

Chukua mfano wa Marekani akirusha roketi kwenye mwezi, hakika haitoachiwa kwenda tu yenyewe, bali itakuwa inarikodi na kuangaliwa huku duniani kila hatua inayokwenda na namna mashine yake inavyofanya kazi. Pia “black box” kwa upande wa ndege “aeroplane” inarikodi hata mazungumzo ya pilot, na ndio maana ndege inapopata ajali kwanza hutafutwa hiyo “black box”. Hivyo kila mtengenezaji hukijua vizuri mwenendo wa anachotengeneza, na hamna mwengine wa kujuwa nafsi ya mwanaadamu ila Muumba Subhaana.

Na kwa mfano wa adhabu zinazoweza kuthibitika duniani ni zina, wizi, ulevi na mengineo ambayo mkosaji anaweza kutiwa hatiani tofauti na yale makosa yalokuwa yanapita ndani ya nafsi.

Pia Uislamu utamuadhibu mtenda dhambi aliyekuwa hajatiwa hatiani hapa duniani. Mfano wanaokiuka kutoa Zakaah, ingawa anaweza kufoji karatasi na kusema uongo ili tu kukwepa kutoa Zakaah hapa duniani lakini ataenda kuilipa huko Qiyama. Hamna kukimbia kosa ndani ya Uislamu, limetendwa basi litahesabiwa tu mbele ya Muumba. Mfano mwengine ni makafiri walokataa kufuata Uislamu. Pia nao wana hukmu zao siku ya Haki.

Tofauti na sheria za mwanaadamu ambazo zinamuadhibu mkosaji duniani pekee. Na ikiwa mwanaadamu atakwepa mkono wa sheria hadi kufa hatahisabiwa katu kuwa ni mkosaji. Uislamu unamkamata mkosaji duniani na kama hatakamatwa basi adhabu ipo siku ya Qiyama. Sheria ya Kiislamu inawafanya Waislamu kuwa makini muda wote kutokiuka sheria za dini.

MALIPO MEMA KWA ANAYEJIEPUSHA KUVUNJA SHERIA

Juu ya hayo, Uislamu unatoa malipo kwa mtiifu na adhabu kwa mtenda dhambi. Hivyo, Sheria za Kiislamu zinawakamata wote ikiwa ni mtiifu au ni mtenda makosa. Sheria za Kiislamu zinalinda kanuni zake na zinawalazimisha binaadamu kujisalimisha nazo sio kwa kuweka adhabu tu bali hata kwa kutoa malipo mazuri kwa mwenye kuzifuata. Ambapo sheria za mwanaadamu zinamuadhibu mkosaji na wala hazitoi zawadi kwa anayezifata. Jee tumepata kusikia Raisi/Hakimu akitoa zawadi kwa mwananchi aliyejiepusha kuiba hadi uzee umemfikia? Hapa sio mzee aliyeiba lakini hakukamatwa, tunazungumzia mzee aliyekuwa mswaafi wa matendo tokea kuzaliwa kwake.

Kwa mfano dhambi ya kuua mtoto, Allah (Subhanahu Wataala) anasema na tutajaribu kuitafsiri kama ifuatavyo:

{“Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi ndio Tunaowaruzuku wao na nyinyi (pia). Kwa yakini kuwaua ni khatia kubwa.”} [Suratu Bani Israil:31]

Hivyo binaadamu anayeacha kumuuwa mtoto wake anaahidiwa kuruzukiwa yeye na mtoto wake.

Ni Rehma Zake Allah (Subhanahu Wataala) kuweka malipo hata kwa jambo la kutosheleza shahawa za binaadamu kwa njia ya halali. Hili sio tendo jengine ila ni tendo la ndoa baina ya mume na mke nalo pia lina ajira ndani yake.

Imepokewa na Muslim kutoka kwa Abi Dharr Al-Ghaffarriy (Radhiya Allahu Anhu) kutokana na Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) amesema ((Hakika ya tasbiha ni sadaka, na kila takbira ni sadaka, na kila shukrani ni sadaka, na kila tahliyl ni sadaka, na kuamrisha mema ni sadaka, na kukatazana maovu ni sadaka, na kumuingilia mmoja wenu ni sadaka)) Wakasema Maswahaba (Radhiya Allahu Anhum), Je kumuendea mmoja wetu kwa kuondoa shahawa, pia ndani yake kuna malipo? Akasema Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam): ((Je, anaonaje kama ataendea tendo hilo katika haramu, halitakuwa dhambi?….Na hivyo basi, likiendewa kwa uhalali, lina malipo))

Allah (Subhanahu Wataala) pia Anatoa malipo kwa wacha Mungu. Allah (Subhanahu Wataala) Anasema na tutajaribu kuitafsiri kama ifuatavyo: [Suratun Nabaa:31-36]

{“31-Bila shaka wanaomcha Mwenyezi Mungu wamewekewa (mambo ya kuonyesha) kwao.

32 - Mabustani na mizabibu

33 – Na wanawake vijana walio hirimu (na waume zao)

34 – Na gilasi zilizojaa (vinywaji vizuri vizuri).

35 – Hawatasikia humo (maneno ya) upuuzi wala ya kukadhibishana.

36 – Watalipwa kutoka kwa Mola wako atia yenye kutosha.”}

Sheria za Kiislamu zinagusa nyanja zote muhimu za maisha, roho, usalama, amani na heshima. Kwa vile kuna malipo mazuri kwa mwenye kushikamana nazo, basi hakika ni kivutio kwa mwenye kushikamana nazo. Vitu hivi vyote vinakosekana kutoka sheria za mwanaadamu. Kwa sababu kushikamana kwa Sheria za Kiislamu ni kitendo cha utiifu na kujitoa mhanga kwa ajili ya Muumba, utiifu ambao unamweka karibu na Muumba wake.

Ikiwa kanuni zimeegemea kwa dini na kujilinda nazo, mwanaadamu yoyote atahofia adhabu zake hata kama sheria za mwanaadamu hazitamtia hatiani. Mfano, Uislamu unaamrisha kuwa msafi na kuweka mazingira safi. Hivyo kiimani tunajuwa kuwa Allah (Subhanahu Wataala) anatuona, hivyo hata ukiwa pwani hutokaa ukatupa uchafu ndani ya bahari (kwani kutaathiri viumbe baharini) seuze kwa kutupa uchafu duniani. Hii ni kwa sababu ya “mkono wa sheria” chini ya Utakaso Wake Allah (Subhanahu Wataala) ambao hautegemei kukamatwa mtuhumiwa wala kushitakiwa kabla ya Mahkama za sheria. Hakuna njia ya kukimbia mtenda dhambi asotubia ila atahukumiwa tu.

Kwa kumalizia makala hii, majumuisho yafuatayo yanatolewa kwa tofauti kuu mbili baina ya sheria hizi:

KWANZA, kiini cha Sheria ya Kiislamu ni kutoka kwa Allah (Subhanahu Wataala). Kwa upande wa sheria za mwanaadamu zinatokana na akili za binaadamu. Sheria na adhabu zake ndani ya Uislamu zinapatikana kwenye viini vikuu: Qur-aan na Sunnah. Fiqhi hutumika kutoa ufumbuzi wa jambo kutoka Qur-aan na Sunnah. Utawala wa Taifa la Kiislamu hauruhusiki kuharamisha halali iliyobainishwa chini ya Muumba wala kinyume chake. Halali, haraam na adhabu zake ni vitu vinavyozuiwa kwa hali zote.

PILI, maadili ndani ya sheria za Kiislamu yana nafasi muhimu. Wakati sheria za mwanaadamu inakataa kabisa maadili na haijishughulishi nayo. Uislamu unachukua maadili ni asili ya dini, hakuna mtengano wowote.

Kwa mfano, muislamu anawajibu wa kuwatumikia vizuri wazee wake bila ya hata kusema “AH!” na wazazi wakifika uzee basi ukae nao kwa wema. Sheria ya mwanaadamu haina kanuni kama hiyo. Au kwa mfano mwengine ni mwanamke anayevaa hijaabu vizuri, sio kwamba ndio amemaliza sheria zote za dini. Na haimlazimu mwanamke huyu kuswali, hataaa. Hapa Uislamu unagusa maadili (kuvaa hijabu) na kuswali, (sheria) zote zafuatwa bila ya kuacha nyengine.

Fikra ya kuwa sheria ni upande mmoja na maadili upande mwengine ni kosa. Mtengano huu hauna nafasi ndani ya Uislamu kwani unaweza kusababisha kutokea kwa watu wa aina mbili ambao wote hawataweza kukubalika. Kwa mfano:

Wa mwanzo ni mtu mwenye maadili mabaya lakini ni mzuri wa kufuata sheria. Mfano kutowatumikia vizuri wazee lakini hana chembe ya uzinifu.

Wa pili ni mfuataji mbaya wa sheria lakini anajionesha kwa watu kutenda mema.  Mtu huyu hana tofauti na Mnafiki. Hivyo huwa anachanganya mambo tu, huku yupo na kule yule. Allah (Subhanahu wa Taala) amemwita mtu kama huyu kwa jina la Mudhabdhabiyna. Mfano anatoa hukumu ya waliodhulumiana hali ya kuwa yeye mwenyewe ni mdhulumu mkuu.

Mifano hii inadhihirisha ya kuwa upande wa sheria za mwanaadamu huangukia baina ya pande hizo mbili. Binaadamu anajizuia kuiba kwa sababu tu ni kosa mbele ya sheria lakini hatoi kipato chake kuwasaidia masikini kwa sababu sheria haijashurutisha hivyo. Na kwa upande wa pili unamkuta mtu ameamua kuvunja sheria na kuanza kuiba lakini anatoa mali yake kuwasaidia masikini.

Pia tunaona sheria za mwanaadamu zinazuia wari/wajane kupata mimba lakini haiwazuii kufanya tendo la ndoa (Sheria ya Kuwalinda Wari na Wajane Namba 4 ya mwaka 1985 kifungu cha 3 – Zanzibar). Kwa sababu kujamiiana ni tendo linalogusa maadili na sheria za mwanaadamu hazijishughulishi na vitu vya maadili kama kujamiiana wasokuwa wanandoa, kutembea utupu wanawake, kuchanganya mavazi baina ya mwanaume na mwanamke na mengineyo.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhanahau wa Taala Atuhifadhi na makosa, Atupe malipo kwa amali zetu njema. Atuepushe na elimu isiyokuwa na manufaa. Tunamuomba Atuthibitishe katika itikadi hii na Atuonjeshe matunda Yake na Atuongezee katika fadhila Zake na Asizipoteze nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na Atumiminie Rehma kutoka Kwake kwani Yeye ndiye Mpaji.

Shukrani zote ni Zake Yeye Mola wa ulimwengu, na viumbe vyote vya dhahir na siri. Mola wetu Msalie na Mpe Amani Mtume wako Muhammad (SwallaAllahu Alayhi wa Salam) pamoja na Masahaba wake na Aali zake wema, na kila atakayewafuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Kiama. Kwake Yeye Allah twajitakasa na Kwake twaomba Atutakabalie dua zetu.

MWISHO