Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UUMBAJIi WA DUNIA KATIKA QUR'ANI TUKUFU NA HADITHI

5 Voti 02.4 / 5


Uumbaji wa dunia katika Qur'ani Tukufu na hadithi

Tangu zamani wasomi wamekuwa wakifuatilia kutaka kujua chanzo cha kuumbwa mwezi, nyota na sayari ya dunia. Suala muhimu lililokuwa likiwashughulisha ni kujaribu kugundua vitu vilivyotumika katika uundwaji wa dunia. Wasomi hao walikuwa wakiamini kuwa, kwa kugawa mada asilia zilizotumika katika ujenzi wa kitu, wangeweza hatimaye kufahamu kitu au vitu vya awali vilivyotumika katika uundwaji wa kitu hicho. Kwa kuzingatia suala hilo tunaona kwamba baadhi ya wasomi wa zamani, walitaja maji, hewa, moto na udongo kuwa elemeti na vitu vya asili vilivyotumika katika uumbaji wa dunia, huku wengine wakizungumzia elementi moja isiyojulikana na kuitaja kuwa chimbuko la uumbwaji dunia. Kwa hakika elementi hiyo inayotajwa na wasomi hao, inaweza kuwa ni atomi ambayo ilikuja kuvumbuliwa na wasomi katika tafiti zao mbalimbali za kielimu. Atomi ni chembechembe yenye vipengele vinavyoweza kuzidisha chembechembe ya awali.

Qur’ani Tukufu ni Kitabu cha mbinguni ambacho kimewataka wanadamu kutafakari kuhusiana na uumbaji wa kuvutia wa dunia. Aya tofauti za Qur’ani zimeashiria nukta kadhaa za kuvutia kama vile; ni vipi ulimwengu uliumbwa na ni hatua gani zilizotumika katika uumbaji huo. Baadhi ya aya hizo takatifu zinautaja moshi (yaani gesi) na zingine kuyataja maji kuwa chanzo cha uumbaji wa mbingu na ardhi. Kuhusiana na suala hilo, Abdul-Ghani Khatib anaandika katika kitabu kiitwacho “Qur’an na elimu ya leo” kuwa: “Mwenyezi Mungu kwanza alianza kuumba maji kisha akaumba pamoja nayo vitu vingine. Wakati huo maji yakatoa joto kali ambalo nalo lilitoa mvuke. Mvuke huo ndio moshi ambao ulikuwa mzito na mweusi. Baada ya hapo Mwenyezi Mungu akaufanya kuwa mzito uliopandana na kuufanya kuwa wa aina tofauti tofauti.” Imam Baqir (as) anazungumzia maudhui hiyo kwa kusema kama ninavyomnukuu: “Kila kitu kilikuwa maji, na arshi ya Mwenyezi Mungu ilikuwa juu yake. Kisha Mwenyezi Mungu akaibua mripuko ndani ya maji hayo kisha akazima miale yake na wakati huo kukatokea gesi ambayo ilitumika katika uumbaji wa mbingu.” Mwisho wa kunukuu. Tazama Tafsir Nur al-Thaqalayni Juzu ya 4 uk 540.

Aya ya 11 ya Surat Fuswilat inasema kuwa uumbaji wa mbingu umetokana na gesi kwa kusema: “Kisha akaielekea mbingu na hali i moshi, ndipo alipoiambia (mbingu) na ardhi: Njooni mkipenda au msipende, vyote viwili vikasema: Tumekuja hali ya kuwa wenye kutii.” Kuhusiana na aya hiyo Ayatullahil-Udhmaa Makarim Shirazi, ambaye ni mfasiri wa Qur’ani anaandika kama ninavyomnukuu: “Sentesi ya (hali i moshi) inaonyesha kuwa, kitu cha awali kuumbwa ni mbingu na kwamba uumbaji huo ulitokana na gesi pana na kubwa. Na mtazamo huo unaenda sambamba kabisa na utafiti wa hivi karibuni kuhusiana na uumbaji. Hadi sasa nyota nyingi za mbinguni zinaonekana kwa sura ya mrundikano wa gesi na moshi.” Mwisho wa kunukuu. (Tafsiri Nemuneh juzu ya 20 uk 228). Baadhi ya wafasiri wanaamini kuwa uumbaji wa mbingu ulikuwa kabla ya uumbaji wa sayari ya dunia huku wakisema kuwa uumbaji wa maji, mimea na milima ulikuja baada ya uumbaji wa sayari hiyo. Na utaratibu huo unaenda sambamba na elimu ya leo. Wasomi hao wanategemea nadharia ya aya za 27 na 32 za Surat Naziat zinazosema: “Je, nyinyi ni wenye umbo gumu zaidi, au mbingu alizozijenga? Akainua kimo chake na akaitengeneza vizuri. Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana. Na ardhi baada ya hayo akaitandaza. Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake. Na milima akaiimarisha.”

Kuhusiana na suala hilo George Gamow mtaalamu wa elimu ya fizikia mwenye asili ya Urusi anaandika kuwa, elementi ya kwanza iliyotumika katika uumbaji wa nyota, ilitokana na gesi na anasema kama ninavyomnukuu: “Elimu ya nyota inatufikisha kwenye ukweli huu kwamba, nyota zina mwanzo na zote kwa pamoja ziliumbwa kutokana na gesi iliyokuwa na joto kali.” Mwisho wa kunukuu. Kile kinachodhihiri kutoka katika aya takatifu za Qur’ani ni kwamba, kabla ya hatua ya moshi ziliyopitia mbingu na ardhi, kulikuwa na hatua nyingine ambayo mara nyingi hatua hiyo inatajwa kuwa ni maji ambayo yalikuwa na taathira muhimu katika uumbaji huo. Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani Tukufu wanalitaja neno “Maau-yaani maji” lililotumiwa katika uumbaji wa ulimwengu kuwa ni maji, huku wengine wakilitaja kuwa ni maji yaliyochemshwa na kuwa ya  moto ambayo ndani yake hutoka gesi iliyorundikana na nzito. Baada ya gesi ile kubinyana na kisha kugandana na kuwa mithili ya tufe, ndipo kukatokea nyota na sayari nyingine. Suala hilo linashabihiana kwa kiasi kikubwa na nadharia ya “Mripuko mkubwa-Big Bang”. Hata hivyo kutokana na kukithiri nadharia za kielimu kuhusiana na uumbwaji wa ulimwengu, huku kukiwa bado hakuna nadharia yenye uthibitisho wa moja kwa moja kuhusiana na suala hilo, hatuwezi kunasibisha moja ya nadharia hizo na Qur’ani Tukufu.

Nadharia ya mripuko mkubwa au kwa ibara nyingine“Big Bang”inasema kuwa,  mripuko huo ulitokea yapata miaka bilioni 14 iliyopita na katika kipindi maalumu, mahali padogo palipokuwa na bonge na nishati kubwa duniani. Kwa hakika kiini chote kilichopo duniani ikiwemo nyota nyingi vilikuwa vimegandana kwa pamoja na ghafla ndipo kukatokea mripuko mkubwa usiotazamiwa na uliokuja kutambuliwa kwa jina hilo. Wataalamu wa elimu ya fizikia wanaamini kuwa, mripuko huo ulikuwa wenye nguvu na joto kali. Ni kwa kupitia mripuko huo, ndipo kukatokea chembechembe zilizorundikana mithili ya rundo kubwa la gesi. Kwa mara nyingine kila rundo kubwa la gesi liligawika na kupelekea kutokea nyota. Hivi sasa nadharia ya Big Bang ndiyo inayoonekana kukubalika kwa kiasi kikubwa kuhusiana na uumbwaji dunia. Hata hivyo ikiwa tutarudi nyuma zaidi kabla ya mripuko huo mkubwa, unataraji tutakuta nini? Tutasema nini? Ni nguvu gani iliyoibua mripuko huo? Hii ni katika hali ambayo aya nyingi za Qur’ani si tu kwamba zimeashiria kiini cha maisha na uumbaji wa ulimwengu, bali pia zimebainisha ni namna gani ulimwengu ulivyoumbwa na kwa muda wa siku ngapi. Aya za 9 hadi 12 za Surat Fuswilat zinasema: “Sema: Je, kwa hakika mnamkataa aliyeumba ardhi katika nyakati mbili, na mnampa washirika? Huyo ndiye Mola wa walimwengu. Na akaweka humo milima juu yake na akabarikia humo na akapima humo chakula chake katika nyakati nne, ni sawa kwa waulizao. Kisha akaielekea mbingu na hali i moshi, ndipo alipoiambia (mbingu) na ardhi: Njooni mkipenda au msipende, vyote viwili vikasema: Tumekuja hali ya kuwa wenye kutii. Basi akazifanya mbingu saba katika nyakati mbili, na kila mbingu akaifunulia kazi yake, na tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa na kuilinda, hicho ndicho kipimo cha Mwenye nguvu, Mwenye kujua.” Katika aya hizi Qur’ani Tukufu inaashiria nyakati sita za uumbaji wa ulimwengu. Nyakati mbili zilikuwa kwa ajili ya uumbaji wa mbingu, nyakati mbili kwa ajili ya uumbaji wa ardhi na nyakati mbili nyingine kwa ajili ya uumbaji wa vile vilivyomo mbinguni na ardhini.

Ayatullahil-udhmaa Makarim Shiraz, mfasiri mkubwa wa Qur’ani Tukufu anazungumzia suala hilo la nyakati katika uumbaji kwa kuandika: "Nyakati ya kwanza ni wakati ambao ulimwengu ulikuwa katika hali ya mrundikano wa gesi. Nyakati ya pili ni kipindi ambacho mrundikano huo mkubwa wa gesi ulipogawanyika. Nyakati ya tatu ilikuwa ni kuanzisha mfumo wa jua na sayari zake “The Solar System”. Nyakati ya nne ilikuwa kuipoza ardhi na kuiandaa kwa ajili ya maisha ya wanadamu. Nyakati ya tano ilikuwa ni ya kuweka mimea na miti ardhini. Na nyakati ya sita na ya mwisho, ilikuwa ni kuumba wanyama na mwanadamu kwenye ardhi hiyo. (Tafsir Nemuneh juzu ya 6 ukurasa 202.)

Ni matumaini yangu kuwa mmenufaika vya kutosha na kuweza kufahamu jinsi dunia ilivyoumbwa.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini