Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA PILI)

0 Voti 00.0 / 5

ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA PILI)
NAFASI YA ADHANA NDANI YA SHERIA YA KIISILAMU.
HAKUNA MWANADAMU YEYOTE ALIYEHUSIKA KATIKA KULETA SHERIA YA DHANA
Hakika adhana na iqama ni kati ya mambo yaliyothibiti ndani ya dini na ni alama ya dini. Mwenyezi Mungu aliyateremsha ndani ya moyo wa mbora wa mitume, na bila shaka Mwenyezi Mungu aliyefaradhisha Sala na ndiye aliyefaradhisha adhana na iqama, na hakika chanzo cha vyote ni kimoja.
Na wala hakuna mwanadamu yeyote aliyehusika katika kuleta sheria hiyo, si katika hali ya macho wala ya usingizi. Na hii ndio hali ya ibada zote ambazo mwanadamu hufanya kumwabudu muumba wake. Wala ndani ya sheria ya Uislamu hatujaona ibada ya kisheria ambayo imewekwa na mwanadamu kisha Mwenyezi Mungu akaipitisha na kuiunga mkono isipokuwa katika mambo maalumu ambayo yamewekwa na Mtume mtakasifu. Jambo linalodhihirisha hilo ni kuwa vipengele vyote kuanzia takbira mpaka tahlili vina mvuto wa kimungu na maana ya hali ya juu na ya ndani zaidi, ambayo huamsha hisia za mwanadamu na kumpeleka katika maana ya juu na nzuri zaidi ya ile iliyomo akilini mwa watu.
Hivyo laiti adhana na iqama vingetokana na chanzo kisichokuwa ufunuo wa Mwenyezi Mungu basi visingekuwa na mvuto huu wa kimungu. Hivyo Mwislamu hana njia isipokuwa ni kukubali mambo mawili:
1: Hakika sheria ya adhana na iqama inatokana na Mwenyezi Mungu, na yeye ndiye aliyemfunulia mja wake adhana na iqama, wala mwanadamu hakuhusika na lolote katika jambo hilo.
2. Kama ilivyokuwa asili ya adhana ni ufunuo wa Allah aliouteremsha katika moyo wa Mtume (s.a.w.w.) basi hivyo hivyo kila kipengele kati ya vipengele vya adhana ni ufunuo alioteremshiwa Mtume (s.a.w.w.) hivyo mwanadamu yeyote hana haki ya kupunguza au kuongeza kipengele chochote katika adhana.
HISTORIA YA KULETWA SHERIA YAADHANA NDANI YA HADITHI ZAAHLUL-BAYT
Maimam wote wa Ahlul-Bayt wamekubaliana kuwa adhana ni miongoni mwa mambo ya ibada, hivyo ina hadhi kama vile ibada nyingine, na aliyeileta ikiwa ni sheria ni Mwenyezi Mungu. Imam aliteremka na adhana kisha akamfunza Mtume na Mtume akamfunza Bilal, wala hakuna yeyote aliyeshiriki katika kuleta sheria ya adhana. Jambo hili ni kati ya mambo waliyokubaliana maimam wa Ahlul-Bait. Na kuna riwaya na maneno yao mengi yanayothibitisha hilo, na sisi hapa tutatoa machache tu kwani: Katika cheni nzima inakutosha sehemu ya shingo .1
Amepolea Kulayni kwa njia sahihi toka kwa Zararat na Al-Fadhil, toka kwa Aba Jafari Al-Baqir kuwa alisema: Mtume alipopelekwa mbinguni alifika sehemu iitwayo Nyumba inayozuriwa (Baytul-Maamur), wakati wa Sala ukaingia hapo, Imam akaadhini na kukimu hapo Mtume akatangulia kisha malaika na mitume wengine wakapanga safu nyuma yake Muhammad ( s.a.w.w.)..
2. Pia kapokea Kulayni kwa njia sahihi toka kwa Imam Sadiq amesema: Pindi Imam alipoteremka na adhana kwa Mtume wa Allah kichwa cha Mtume kilikuwa mapajani mwa Ali (a.s.) hivyo Imam aliadhini na kukimu. Baada ya Mtume kuzinduka alisema: Ewe Ali umesikia? Akajibu: Ndiyo.. 2Akasema: Umehifadhi? Akajibu: Ndiyo. Akasema: Mwite Bilal. Hapo Ali akamwita Bilal kisha akamfundisha.3
3. Pia amepokea kwa njia sahihi toka kwa Umar bin Udheynat toka kwa Sadiq (a.s.) alisema: Kundi hili limepokea nini? Nikasema niko chini yako, ni kuhusu nini? Akasema: Kuhusu adhana. Nikasema, wao husema kuwa Ubayy bin Kaab aliiona ndotoni. Akasema: Wamesema uongo, hakika dini ya Allah ni tukufu zaidi ya kuonekana ndotoni. Akasema: Sudayri Al-Swayrify akamwambia: Niko chini yako, hebu tusimulie habari za jambo hilo. Akasema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu sana hivyo pindi alipompeleka nabii wake Miraji na kumfikisha mbingu ya saba. Akaendelea mpaka mwisho wa hadithi ya kwanza. 4
4. Muhammad bin Makkiy Al-Shahidu amepokea katika kitabu Ad-Dhikra toka kwa mwanachuoni wa kishia mwanzoni mwa karne ya nne - Nikimaanisha Ibnu Abi Aqiil Al-Aammaniy, kuwa alipokea toka kwa Imam Jafar Sadiq kuwa: Imam aliwalaani watu wanaodai kuwa eti nabii alichukua adhana toka kwa Abdallah ibnu Zaid, 5 Imam akasema: Ufunuo unateremka kwa nabii wenu kisha ninyi mnadai eti alichukua adhana toka kwa Abdallah bin Zaid?6
Si Shia peke yao ndiyo waliyopokea riwaya hizi toka kwa Maimam wa Ahlul-Bait. Hivyo Al-Hakimu na wengine nao wamepokea riwaya kama hizi toka kwa maimam. Zifuatazo ni baadhi ya riwaya zilizopokewa kwa njia ya masunni kuhusu suala hili
5. Al-Hakim amepokea toka kwa Sufiani bin Alayli kuwa: Yalipotokea yale yaliyotokea kati ya Hasan bin Ali na Muawiya bin Abu Sufian nilikwenda Madina nikamkuta amekaa, akasema:
Basi tukazungumzia adhana mbele yake, hapo baadhi yetu wakasema: Hakika chanzo cha adhana ni ndoto aliyoiona Abdallah bin Zaid. Hapo Hasan bin Ali akawaambia: Hakika hadhi ya adhana ni kubwa zaidi ya hilo, Jibril aliadhini mbinguni mara mbili mbili kisha akamfunza Mtume wa Allah. Akakimu mara moja moja 7 kisha akamfunza Mtume wa Allah.. 8
6. Al-Muttaqi Al-Hindi amepokea toka kwa Ashahidu Zaid bin Imam Ali bin Al-Husain toka kwa babu zake toka kwa Ali (a.s.) kuwa: Mtume alifunzwa adhana na kufaradhishiwa Sala usiku wa miraji9.
7. Al-Halabiy amepokea toka kwa Abi Al-Alaiy kuwa: Nilimwambia Muhammad bin Al-Hanafia kuwa: Sisi husimulia kuwa chanzo cha adhana hii ni ndoto aliyoiona mtu kati ya Answari alipokuwa usingizini. Akasema: Akashtuka sana Muhammad Al-Hanafia kwa hilo na kusema: Mmelizushia uongo jambo ambalo lina asili ndani ya sheria ya Uislamu na mafunzo ya dini yenu, hivyo mkadai eti lilitokana na ndoto aliyoiona mtu kati ya Answari usingizini mwake. Ndoto ambayo huenda ikawa ni uongo au kweli, na huenda ikawa si chochote. Akasema: Nikamwambia: Hadithi hii imeenea kwa watu. Akajibu: Naapa kwa Allah hili ni batili.10
8. Al-Mutaqiy Al-Hindiy amepokea toka kwenye Musnadi ya Rafiu bin Khudeyji kuwa: Alipopelekwa Mtume mbinguni alifunuliwa adhana, Hivyo Jibril akateremka na adhana na kumfunza Mtume. (Tabarani na yeye kapokea katika kitabu Al-Awsatwu toka kwa Mwana wa Omar).11
9. Inaonekana kuwa adhana ilitokana na ufunuo wa Allah hiyo ni kwa mujibu wa riwaya aliyopokea Abdul-Razaq toka kwa Atwai.12
10. Al-Halabii amesema: Zimepokewa hadithi zinazoonyesha kuwa sheria ya adhana iliteremshwa kipindi cha Makka kabla ya kuhama. Kati ya hadithi hizo ni Ile iliyomo ndani ya kitabu cha Tabraniy toka kwa Ibnu Omar. Na hapa akanukuu riwaya ya nane.13 Hii ndio historia ya adhana na kwa njia hii ndivyo sheria hii ya adhana ilivyoletwa, huku Shia wakiichukua toka chemchemu safi toka kwa watu ambao wao ndio wasiri wa Sunna ya Mtume, watu ambao mkweli hupokea toka kwa mkweli mpaka mwisho hukomea kwa Mtume . Pia riwaya nyingine zimeunga mkono jambo hili kama ulivyoona.
JINSI ILIVYOLETWA SHERIA YA ADHANA
KWA MUJIBU WA RIWAYA ZA AHLU-SUNNA
Kuna mambo yaliyomo ndani ya riwaya za Kisunni kuhusu jinsi ilivyoletwa sheria ya adhana. Mambo hayo hayasihi kabisa kunasibishwa na Mtume. Matokeo ya riwaya hizo ni kuwa: Mtume alikuwa akihimiza Sala ya jamaa lakini alikuwa hajui ni kwa njia gani angeweza kuwakusanya watu kwa ajili ya Sala kutokana na umbali uliopo kati ya nyumba moja hadi nyingine pia mtawanyiko uliopo kwa muhajirina na answari katika mitaa ya madina. Hivyo katika kutatua hili Mtume akaomba ushauri; ndipo aliposhauriwa mambo yafuatayo:
1. Atumie kuweka bendera pindi watu wakiiona watatangaziana wao kwa wao, lakini Mtume hakupendezwa na rai hiyo.
2. Wakamshauri atumie tarumbeta, lakini Mtume hakupendezwa na hilo.
3. Atumie kengele kama wanavyofanya wakristo. Mwanzo Mtume hakupendezwa na hilo lakini baadae akaamrisha itumike hivyo, ikatengenezwa kengele ya mbao ili iwe inapigwa ili watu wakusanyike kwa ajili ya Sala.
4. Mtume alikuwa katika hali kama hiyo ndipo alipokuja Abdallah bin Zaid na kumwambia Mtume kuwa, yeye alikuwa katika usingizi mwepesi ndipo alipokuja mtu na kumuotesha adhana.
Akasema Umar bin Al- Khattab kuwa alikuwa tayari keshaiona adhana hiyo kabla ya siku ishirini lakini alificha.
Akasema: Kisha Umar akamsimulia Mtume. Hapo Mtume akamuuliza: Ni kitu gani kilichokuzuia usinieleze?
Akajibu: Abdallah bin Zaidi kanitangulia hivyo nikaona haya. Hapo Mtume akasema: Ewe Bilal, simama na ufanye atakachokuamrisha Abdallah bin Zaid. Hapo Abdallah akamfunza Bilal na Bilal akajifunza adhana na akaadhini. Huu ni muhtasari wa yale yaliyopokewa na watu wa hadithi kuhusu jinsi sheria ya adhana ilivyoteremka, hivyo wajibu wetu sasa ni kuchambua maneno na upokezi wa riwaya. Na ufuatao ni uchambuzi wake.
RIWAYA KUHUSU JINSI SHERIA YAADHANA ILIVYOLETWA NDANI YA VITABU TEGEMEZI VYA HADITHI ( SUNAN )
1-Amepokea Abu Daudi (202 . 275) kuwa: Ametusimulia Abadu bin Musa Al-Khataly na Ziad bin Ayyub (Na hadithi ya Abadi ndiyo timilifu) wao wawili wamesema: Ametusimulia Hashimu toka kwa Abi Bashiri toka kwa Abi Amiri bin Anasi toka kwa ami zake wa ki-Answari. Amesema: Mtume alitilia umuhimu sana Sala hivyo akawa akitafuta namna ya kuwakusanya watu kwa ajili ya Sala hapo akaambiwa: Wakati wa Sala ukiingia weka bendera, pindi watakapoiona bendera hiyo watatangaziana wao kwa wao. Lakini akupendezwa na hilo.
Akasema: Akatajiwa tarumbeta. Ziad anasema: Yaani tarumbeta la Mayahudi. Lakini hakupendezwa na hilo huku akisema: Hilo ni jambo la Mayahudi..
Akasema: Akatajiwa kengele. Akasema: Hilo ni jambo la Wakristo. Ndipo alipoondoka Abdallah bin Zaid huku akifikiria jambo linalomshughulisha Mtume. Ndipo alipooteshwa adhana usingizini. Akasema: Asubuhi mapema akaamkia kwa Mtume na kumwambia: Ewe Mtume, mimi nilikuwa katika usingizi mwepesi ndipo aliponiijia mtu na kunionyesha adhana ..
Akasema: Umar bin Al-Khattabi alikuwa tayari kesha iona adhana hiyo kabla ya siku ishirini lakini akaificha14 Akasema: Kisha Umar akamsimulia Mtume. Hapo Mtume akamuuliza: Ni kitu gani kilichokuzuia usinieleze? Akajibu: Abdallah bin Zaidi kanitangulia hivyo nikaona aibu. Hapo Mtume akasema: Ewe Bilal simama na ufanye atakachokuamrisha Abdallah bin Zaid. Akasema: Hapo Bilal akaadhini. Abu Bashiri akasema: Hapo Abu Umairi akaniambia: Answari wanadai kuwa laiti si Abdallah bin Zaidi kuwa mgonjwa siku hiyo basi Mtume angamfanya kuwa muadhini.
2- Ametusimulia Muhammad bin Mansur At-Tusi, Ametusimulia Yaqubu, Ametusimulia baba yangu toka kwa Muhammad bin Ishaq. Ametusimulia Muhammad bin Ibrahim bin Al-Harith At-Taymy toka kwa Muhammad bin Abdallah bin Zaid bin Abdallah amesema: Ametusimulia baba yangu Abdallah bin Zaid amesema kuwa: Pindi Mtume alipoamrishwa itengenezwe kengele ili ipigwe kwa ajili ya kuwakusanya watu kwa ajili ya Sala, basi nikiwa usingizini alinizunguka mtu huku akiwa amabeba kengele nami nikamwambia: Ewe mja wa Mwenyezi Mungu, je unauza kengele? Akanijibu: Unataka ufanyie nini kengele hii? Nikamjibu: Tuwaitie watu waje kwenye Sala. Akasema: Je hutaki nikufundishe njia bora kuliko hiyo?. Nikasema: Nataka. Anasema: Akasema: Uwe ukisema:
الله اكبر الله اكبر لااله الا الله لااله الا الله
(Allah mkubwa Allah mkubwa. Allah mkubwa Allah mkubwa. Nashuhudia kuwa hapana mola wa haki isipokuwa Allah. Nashuhudia kuwa hapana mola wa haki isipokuwa Allah. Nashuhudia kuwa hakika Muhammad ni Mtume wa Allah. Nashuhudia kuwa hakika Muhammad ni Mtume wa Allah. Njooni kwenye Sala. Njooni kwenye Sala. Njooni kwenye ushindi. Njooni kwenye ushindi. Allah mkubwa Allah mkubwa. Hapana mola wa haki isipokuwa Allah).
Akasema: Kisha akarudi nyuma kidogo na kusema: Wakati wa kukimu Sala sema:
الله اكبر الله اكبر لااله الا الله لااله الا الله
(Allah mkubwa Allah mkubwa. Nashuhudia kuwa hapana mola wa haki isipokuwa Allah. Nashuhudia kuwa hakika Muhammad ni Mtume wa Allah. Njooni kwenye Sala. Njooni kwenye ushindi. Imesimama Sala imesimama Sala. Allah mkubwa Allah mkubwa. Hapana mola wa haki isipokuwa Allah).
Nilipoamka asubuhi nilikwenda kwa Mtume na kumpa habari ya yale niliyoyaona. Mtume akasema: Inshaallah hiyo ni ndoto ya kweli, simama umfundishe Bilal uliyoyaona ili aadhini kwa namna hiyo, hakika yeye ana sauti nzuri kuliko wewe.. Nikasimama na Bilal nikawa nikimfundisha na yeye akiadhini.
Akasema: Omar bin Al-Khatabu akasikia, wakati huo alikuwa nyumbani kwake hivyo akatoka huku akiburuza joho lake na kusema: Naapa kwa yule aliyekupa unabii kwa haki ewe Mtume wa Allah, hakika mimi niliona mfano wa hili aliloliona..
Mtume akajibu: Basi kila sifa njema ni ya Allah15
Ibnu Majah ( 207 . 275) amepokea kwa njia mbili zifuatazo:
3. Ametusimulia Abu Ubaydi: Muhammad bin Maymun Al-Madaniy. Ametusimulia Muhammad Salmat Al-Haraniy. Ametusimulia Muhammad Is.haqa. Ametusimulia Muhammad Ibrahim Al-Tamimiy, toka kwa Muhammad Abdallah Zaid, toka kwa baba yake amesema: Mtume alichukizwa na tarumbeta akaamrisha ichongwe kengele ndipo alipooteshwa Abdallah bin Zaid adhana usingizini..
4. Ametusimulia Muhammad bin Khalid bin Abdallah Al-Wasatwiy. Ametusimulia baba yangu toka kwa Abdul-Rahmani Is.haqa, toka kwa Al-Zahriy toka kwa Salim, toka kwa baba yake kuwa: Mtume alitaka ushauri wa watu kuhusu namna ya kuwakusanya kwa ajili ya Sala. Wakamtajia tarumbeta lakini hakupendezwa nalo kwa sababu ya mayahudi. Kisha akatajiwa kengele nayo ikamchukiza kwa sababu ya wakiristo. Ndipo usiku huo mtu mmoja kati ya Answari akaoteshwa wito, na mtu huyo anaitwa: Abdallah bin Zaid na Umar bin Al-Khattab. Al-Zahriy akasema: Bilal akaongeza katika wito wa asubuhi :
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi). Mtume akaridhia16
Tirmidhi kapokea kwa njia ifuatayo:
5- Ametusimulia Said bin Yahya bin Said Al-Amawiy, ametusimulia Muhammad bin Is.haqa toka kwa Muhammad Ibrahim Al-Harith Al- Tamimiy, toka kwa Muhammad Abdallah bin Zaid, toka kwa baba yake. Amesema: .Tulipoamka asubuhi nilikwenda kwa Mtume na nikamsimulia ndoto yote.... mpaka mwisho.
6-Tirmidhi amesema: Hadthi hii kaipokea Ibrahim bin Saadi kwa utimilifu sana na urefu zaidi toka kwa Muhammad Is.haqa. Kisha Tirmidhiy akaongeza: Na Abdallah bin Zaid ndiye Ibnu Abdurabah. Na sisi hatujui chochote kilicho sahihi alichopokea toka kwa Mtume isipokuwa ni hadithi hii ya mpokezi moja inayohusu adhana. 17
Haya ndiyo yaliyopokewa na watu wa Sunna toka kwenye Sahihi Sita au vitabu sita huku vikiwa vina umuhimu mkubwa zaidi ya vitabu vingine vya Sunna, kama vile: Sunanil-Daramy au Ad-Darqutniy au yaliyopokewa na Ibnu Saad katika kitabu chake Twabaqat na Bayhaqiy katika kitabu chake Sunan. Kutokana na nafasi maalumu ya vitabu hivyo sita ndiyo maana tumebainisha yale yaliyomo ndani ya vitabu hivyo maarufu vya Sunna na kuacha yale yaliyomo ndani ya vitabu vingine. Hebu sasa tusome riwaya hizi kuanzia ibara (matnu) na sanadi (njia za upokezi) ili tupambanukiwe na ukweli kisha tutataja maelezo mengine yaliyomo ndani ya vitabu vingine.
REJEA:
•    1. Riwaya mbili hazipingani kwani ni mara ngapi Imam ameshuka na ufunuo wa aya moja mara mbili, na atakayefuatilia ataona wazi kuwa lengo la adhana katika riwaya ya mwanzo si lile lililopo kwenye riwaya ya pili.
•    2. Ali tangu udogo alikuwa akisikia maneno ya malaika: Angalia Sahih Bukhari: 4 / 200, na sherehe yake: Irshadil-Sari: 6 /99 na nyingine. Mlango: Watu wanasemeshwa na malaika bila ya kuwa manabii. Amepokea Abu Huraira toka
kwa Mtume kuwa alisema: .Lilikuwa likifanyika hata kwa waliyokuwa kabla yenu kwa Bani Israili..
•    3. Al-Kulayniy: Al-Kafy: 3/302 mlango: Chanzo cha adhana hadithi ya 1 na 2
•    4. Al-Kafy: 3/482 Juz. 1. Mlango wa mambo nadra. Tutakuletea huko kuwa karibuni
watu kumi na nne walidai eti wameiota adhana.
•    5. Itakufikia riwaya toka ndani ya vitabu sita (As-Sunan)
•    6. Wasailul-Shiat: Juzuu ya 4/612 Mlango wa kwanza kati ya milango ya adhana
na iqama. Hadithi 3
•    7. Kilichopokewa toka kwao (a.s.) ni kuwa iqama ni mara mbilimbili isipokua kifungu cha mwisho ndio mara moja
•    8. Al-Hakimu: Al-Mustadarak: 3/181, Kitabu: Kuwajua Maswahaba
•    9. Al-Mutaqiy Al-Hindiy: Kanzul-Amali: 12/350 namba 35354
•    10. Burhanul-dini Al-Halabiy: As-Sirat Al-Halabiyat: 2/300-301.
•    11. Kanzul-Ummal:8/329 namba 231338, kipengele cha adhana
•    12. Abdurazaqi bin Hamam Al-Swinaiy (126-211 ) mtunzi: 1/456 namba 1775
•    13. As-Sirat Al-Halabiyat : 2/296 mlango: Kuanza sheria ya adhana
•    14. Hivi inasihi kiakili mtu afiche ndoto hiyo siku ishirini ndoto ambayo ina raha kwa Mtume na maswahaba zake, kisha baada ya kuisikia kwa Ibnu Zaidi atoe udhuru kuwa aliona aibu, ilihali hata mimi siwezi kuwa na akili kama hizi za khalifa. Zaidi ya hapo inagongana na hadithi ya pili.
•    15. Abu Daud: As-Sunan: 1/134/135 namba 498-499 Utafiti wa Muhammad Muhyi-dini. Hadithi hii inazungumzia kitendo cha Omar kujua adhana baada ya adhana ya Bilal, kinyume na hadithi iliyotangulia.
•    16. Ibnu Majah : As-Sunan: 1/232-233 mlango: kuanza kwa adhana namba 706- 707.
•    17. Al-Tirmidhi : As-Sunan: 1/358-361, mlango: yanayohusu mwanzo wa adhana namba 189.

ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini