IMAMU WA KUMI NA MBILI


IMAMU WA KUMI NA MBILI

Kwa hakika, Imam Muhammad Bin Hassan Al-Askari ni mtoto wa Imam Hassan Al-Askari, Imamu wa 11 wa Shia, na alizaliwa mwaka 255 Hijri, kuzaliwa kwake kumeshuhudiwa na Maulamaa na wanahistoria wa Madhehebu zote za Kiislamu. Kichekesho kikubwa ni huko kwa ndugu zetu wa Kisuni wanaosema wamesoma dini kuamini kuwepo kwa Maimamu 11 hawa wanaokubaliwa na Shia kuwa walikuwepo na walikuwa niwatu wema, lakini wakati huo huo kuamini kuwa Imam Hassan Al-Askari ambaye ni imamunwa 11 hakuwa na mtoto ili wapate kusema kuwa Imamu wa 12 ni Imamu wa Kubuniwa kama mlivyosikia maneno haya hivi karibuni.

Kichekesho kingine ni huko kwa watu kama wao kuamini kuwa Imamu huyo aitwaye "Al-mahdi" bado hajazaliwalakini atazaliwa na atakuwa ni katika kizazi cha Mtume Muhammad (s) sawa na itikadi ya Shia inayosema kuwa Imamu huyo wa 12 atakuwa ni katika kizazi cha Mtume Muhammad (s). Hivyo, iwapo amezaliwa au hajazaliwa Imamu huyo ni LAZIMA ATAKUWA NI KATIKA KIZAZI CHA MTUME MUHAMMAD (s), jambo hili pia kama wangeweza kulikataa wangelikataa na kutwambia kuwa Imamu huyo atakuwa katika kizazi cha Abu Sufiyan lakini wameshindwa kusema hayo!

Hivyo, itikadi ya Kishia juu ya Imamu huyo ni hivyo, hivyo, kama amezaliwa au hajazaliwa Imamu huyo ni Imamu wa kumi na mbili na damu yake ni hiyo hiyo, na kwamba anatokana na Ahlul Bayt (a.s) na jina lake ni hilo hilo "Muhammad". Wanaopinga kuwa AlMahdi si "Muhammad Bin Hassan Al-Askari (a.s) wanasema alMahdi atakuwa ni "Muhammad Bin Abdullah", lakini hii ni habari iliyotoka katika Riwaya na Hadithi zilizotabiri kuja kwa Al-Mahdi, mara nyingi, "riwaya na hadithi" huzungumzia mambo kwa lughaya mafumbo na maneno ya kuazima (Istiara) na maneno ya kugauzwa yenye kumaanisha dhati ya mtu huyo huyo, kama huko kutajwa kwa jina la "Ahmad" katika Injili ya Nabii Issa (a.s) na Kur'ani kumaanisha mtume Muhammad (s), au huko kutajwa tu katika Kur'ani kwa neno "abdana" (mja wetu) kuamansiha "Nabii Khidhir a.s" kwa hivyo jina "Abdullah" lenye kumaanisha jina la baba la huyo Mahdi ndilo hasa lililokuwa kun'ya na laqab la Imam wa kumi na moja ambaye ndiye huyo huyo Imam Hassan Al-Askari, hivyo hakuna makosa ya kutabiri katika jina la Muhammad Bin Hassan Al-Askari kwa kuwa huyo Imam Hassan Al-Askari alikuwa pia akijulikanwa kwa laqab hiyo ya "Abdullah" (mja wa Allah).

Hivyo, usahihi wa itikadi wa Shia unathibitishwa na huko kwa Sunni kutokuwatambuwa hao Maimamu 12 waliotajwa katika Hadithi ya Jabir bin Samrah iliyoko katika Sihaah Sittah isemayo:
(i) "Amesimlia Jabir ibn Samura: Nimemsikia Mtume wa Allah akisema, 'Kutakuwa na Makhalifa kumi na wawili kisha akasema maneno ambayo sikuyasikia vyema, lakini baba yangu amesema, wote watatokana na kizazi cha Quraishj" [Sahih al-Bukhari (English), juzuu ya 9 Hadithi namba:.329, Kitabul Ahkam; Sahih al-Bukhari, (Arabic), juzuu ya 4, Hadithi namba: 165, Kitabul Ahkam]
(ii) Mtume amesema, " Dini hii ya Kiislamu itabakia katika kheri mpaka siku ya Kiama na itakuwa na Makhalifa waongofu kumi na mbili kwenu, na wote watatokana na Ukoo wa Quraishi" [Sahih Muslim, (English), Chapter DCCLIV, juzuu ya 3, ukurasa wa 1010, Hadithi namba: 4483; Sahih Muslim (Arabic), Kitab al-Imaara, 1980 Saudi Arabian Edition, juzuu ya 3, ukurasa wa 1453, Hadithi namba: 10]

Imam Al-Juwayni amewataja Maimamu na Makhalifa hao katika Hadithi aliyoitaja kwa kusema kuwa MtukufuMtume amesema "Mimi na Ali na Hassan na Hussein na tisa katika kzazi cha Hussein ndio waliotakaswa (kwa ajili ya uongozi huo)" Tazama:
[Al-Juwayni, Fara'id al-Simtayn, Mu'assassat al-Mahmudi li-Taba'ah, Beirut 1978, uk. Wa 160.] Maulamaa wa Kiislamu na Imam wa kumi na mbili aitwaye Muhammad Al-MahdiBin Hassan Al-Askari

1. Imam Muhammad b. Talha Shafi'i ameandika hivi: "Abu al-Qasim Muhammad b. Hasan alizaliwa mwaka 258 AH/873 CE katika Samarra. Jina la Baba yake lilikuwa ni Hasan. Miongoni mwa lakab zake ni Hujjat, Khalaf Salih na Muntazar (anayengojewa)." Baada ya maneno haya Imam Ibnu Talha amemalizia kwa kusema ' Hadithi hizina ripoti zinathibitisha kuwa Imam Hasan Al-Askari alikuwa na mtoto aliyejitenga na watu naye atatokea siku za mbele' [1]

2. Imam Muhammad b. Yusuf, yeye alipoandika juu ya kifo cha Imam Hasan 'Askari, ameeleza pia kuwa Imam Hassan Al-Askari hakuwa na motto yo yote isipokuwa huyo Muhammad Al-Mahdi. Kisha akasema 'inasemekana kuwa yeye ndiye huyo anayengojewa"[2]

(3) Imam Ibn Sabbagh al-Maliki ameandika kwenye 'mlango wa 12 wa maisha ya huyu Imamu wa mwisho wa Shia ambaye ni Abu al-Qasim Muhammad, Hujjat, Khalaf Salih, mtoto wa Imam Abu Muhammad Hasan Al-Askari kuwa 'yeye ndiye Imamu wa kumi na mbili wa Shia kisha ameripoti baadhi ya hadithi juu ya Mahdi na kudhihiri kwake"[3]

(4) Imam Yusuf b. Qazughli, baada ya kupima na kujadili sana juu ya maisha ya Imamu Hasan 'Askari, ameandika hivi 'mtoto wake alikuwa anaitwa Muhammad, na lakab yake ni Abu 'Abd Allah na Abu al-Qasim.. Uimamu umefikia mwisho kwa kudhihiri kwake, kisha akaleta baadhi ya Hadithi juu ya Al-Mahdi..[4]

(5) Imam Shablanji al-shafi'I kwenye Kitabu chake kiitwacho Nur al-absar, ameandika hivi; 'Imam Muhammad ni mtoto wa Imam Hasan 'Askari. Mama yake alikuwa ni suria aliyeitwa Narjis au Sayqal au Sawsan. Laqab yake ni Abu al-Qasim. Shia wao wanamjuwa kama ndiye Hujjat, Mahdi, Khalaf Salih, Qa'im, Muntazar, na Imamu wa zama"[5]

(6) Imam Ibn Hajar Al-Askalani, yeye katika Kitabu chake kiitwacho 'al-Sawa'iq al-muharriqa, kwenye biography ya Imam Hasan 'Askari ameandika hivi; 'Imau huyu hakuacha mtoto isipokuwa huyo Abu al-Qasim, ambaye ni huyo Muhammad alHujjat. Mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka mitano (5) pale baba yake alipokufa"[6]

(7) Imam Muhammad Amin al-Baghdadi katika Kitabu chake kiitwacho Saba'ik al-dhahab amesema hivi 'Muhammad, ambaye pia anatambuliwa kama ni Mahdi, alikuwa na umri wa miaka mitano (5) pale baba yake alipokufa"[7]

(8) Imam Ibn Khallikan ameandika kwenye Kitabu chake mashuhuri kiitwacho "Wafayat al-a'yan": kuwa "Abu al-Qasim Muhammad b. al-Hasan al-'Askari ni Imamu wa kumi na mbili wa Shia, Shia wanaamini kuwa huyu ndiye anayengojewa na ndiye al-Mahdi"[8]

(9) Imam Sha'rani kwenye kitabu chake maarufu kiitwacho "al-Yawaqit wa al-jawahir" anasema kuwa "Mahdi ni mtoto wa Imam Hasan 'Askari. Alizaliwa usiku wa tarehe 15 shaaban, mwaka 255 AH. Yupo hai na atabakia hivyo mpaka pale atakapodhihiri pamojana Nabii Issa (a.s). Hivi sasa, ni 957 AH, kwa hivyo atakuwa na umri wa miaka 703.[9]

(10) Huyo huyo Imam Sha'rani, amemnukuu Sheikh Muhyiddin al'Arabi kwenye Kitabu chake maarufu kiitwacho "Al-Futuhat al makiyya, sehemu ya:366, na kusema kuwa "Pale Dunia itakapotawaliwa na Madhalimu na kujaa dhulma, al-Mahdi atadhihiri, naye ataleta uadilifu katika Ulimwengu huu na usawa na haki. Al-Mahdi atatokana na kizazi cha Mtukufu Mtume kutoka katika tumbo la Fatima. Babu yake atakuwa ni Husayn, na baba yake atakuwa ni Imam Hasan 'Askari, ambaye ni mtoto wa Imam 'Ali Naqi, ambaye naye ni mtoto wa Imam Muhammad Taqi, ambaye naye ni mtoto wa Imam 'Ali Rida, ambaye ni mtoto wa Imam Musa Kazim, ambaye ni mtoto wa Imam Ja'far Sadiq, ambaye ni mtoto wa Imam Muhammad Baqir, ambaye ni mtoto wa Imam Zayn al-'Abidin, ambaye ni mtoto wa Imam Husayn b. 'Ali b. Abi Talib."[10]

(11) Imam Abu al-Falah Hanbali kwenye kitabu chake maarufu "Shadharat al-dhahab" na Imam ad-Dhahabi kwenye kitabu chake "al-'Ibar fi khabar min ghabar" wameandika hivi 'Muhammad al-Mahdi alikuwa ni mtoto wa Hasan 'Askari, ambaye alikuwa naye ni mtoto wa 'Ali Hadi, mtoto wa Jawad, mtoto wa 'Ali Rida, mtoto wa Musa Kazim, mtoto wa Ja'far Sadiq,… na kun'nya yake ilikuwa ni Abu al-Qasim na Shia wanamjuwa kama ndiye Khalaf Salih, Hujjat, Mahdi, Muntazar na ndiye kwao ni Imamu wa zama(Sahib al-zaman)."[11]

(12) Imam Muhammad b. 'Ali al-Hamawi amesema: "Abu al-Qasim Muhammad Muntazar alizaliwa mwaka 259 AH/874 CE huko Samarra ya Iraq."[12] Tazama marejeo ya habari hizo katika:

1. Matalib al-su'al (1287 AH edition), uk wa 89.
2. Kifayat al-talib, uk. wa 312.
3. Fusul al-muhimma (Second edition), uk. wa 273 na 286.
4. Tadhkirat khawass al-umma, uk. wa 363.
5. Nur al-absar (Cairo edition), uk. wa 342.
6. al-Sawa'iq al-muharriqa, uk. wa 206.
7. Saba'ik al-dhahab, uk. wa 78.
8. Wafayat al-a'yan (1284 AH edition), juzuu ya 2, uk. Wa 24.
9. al-Yawaqit wa al-jawahir (1351 AH edition), juzuu ya 2, uk. Wa 143.
10. al-Yawaqiit wa al jawahir uk. Wa 143.
11. Shadharat al-dhahab (Beirut edition), juzuu ya 2, uk. Wa 141; al-'Ibar
fi khabar min ghabar (Kuwait edition), juzuu ya 2, uk. Wa 31.
12. Ta'rikh mansuri, microfilm copy of the Moscow manuscript, folio namba: 114.

Mwisho:
1. Mtume amesema, "baada yangu kutakuwa na Maimamu kumi na mbili, na wotewatatoka katika ukoo wa Kikuraishi" Basi tufahamisheni hawa Maimamu kumi na mbili ni Maimamu gain? Kwa makala hii namuomba huyu jamaa anayesema kuwa Mahdi wa Shia ni Imamu wa kutungwa, atuambiye pia hawa Maimamu kumi na mbili ni nani na atutajie majina yao tafadhali.
2. Kama nilivyosema kabla ya kuwa, Seif Bin Omar At-Tamimi Mzandiki wa Iraq amewadanganya waisilamu kwa kuwatungia Abdullah Bin Sabaa, leo hii uongo wake unasambazwa katika mitandao yetu na hao wanafunzi wake ambao mpaka sasa licha ya kujifakharisha ya kujuwa elimu za tariikh na Hadiith wameshindwa kutambuwa kuwa kisa cha Andallah Bin Sabaa "ni kisa cha kutungwa na kubuniwa" na huyo Seif Bin Omar. Basi mko wapi nyinyi mnaojidai kuwa mnajuwa Hadithi na methodology zake? Tafadhali tuambieni Imam Dhehabi na Maimamu wengine wa Hadithi wamesema nini juu ya huyu Seif Bin Omar Tamimi ambaey leo mnafaidika na uongo wake dhidi ya Shia?

UMRI WA IMAM AL-MAHDI
Hivi punde amejitokeza jamaa mwengine mwenye jina jengine lakini analeta mawdhui zile zile zilizoletwa na watu waliomtangulia, mimi sinahaja ya kutafuta jina lake sahihi wala kutia shaka juu ya jina lake, lakini nahusika na makala aliyoiandika tu. Inabidi kufahamu kuwa mtoto na mwanadamu hukuwa kimwili, kiakili, kitabia, kiroho na hakuwi kama kitunguu kwa kutuna umbo lake tu.. Basi huko kukuwa kwa ajabu kwa Imamu wa kumi na mbili kunaitwa kwa lugha ya kidaktari kuwa ni "proportional balance growth" kwa kuwa watoto wengi huwa hawapati aina hiyo ya kukuwa katika maisha yao. Pia kuishi miaka mingi si ajabu katika ulimwengu huu, Allah amewapa waja wake neema nyingi sana, katika neema alizowapa waja wake wengine ni huko kuishi miaka mingi kama alivyoishi Nabii Nuwh (a.s).

Mimi pia huushangaa umri huo wa ajabu wa Imamu wa kumi na mbili, lakini ningekuomba utuambie kutokana na elimu yako, hawa Yaajuj na Maajuuj wana umri gain sasa? Na hasa tukitilia maanani kuwa wado wapo hai kwenye ukuta wao waliojengewa na Dhul-Karnayn? Pia naomba uniambie Nabii Khidhri (a.s) kwa sasa anaingia umriwa miaka mingapi? Hasa tukitilia maanani kuwa yeye amezaliwa na kusihi miaka mingi zaidi kabla ya huyu Imamu wa kumi na mbili wa Shia?

Tafadhali husika na mijadala ya kielimu na kuleta fikra zitakazoleta matumaini ya upendo, upanuzi wa elimu, maelewano na sio kuleta kejeli na kukufurishana. Mimi nimefaidika sana na Jadweli yako inayoeleza umri wa Maimamu hao, basi nakuomba pia utufahamishe masuala hayo niliyokuuliza kwa faida ya wote. Kwa barua hii pia nakuomba upitie hizo rai za Maulamaa na maneno yao juu ya kuwepo kwa Imamu wa kumi na mbili na kuzaliwa kwake, kisha utuambie maoni yako khasa juu ya kutaja kwao kwa Imamu huyo.

NASAHA
La maana ni HUKO KUTAMBUWA KUWA KILA MTU ANA HAKI YA KUFATA RAI AU FIKRA ANAYOITAKA, HAKUNA HAJA YA KULETA KEJELI IWAPO HUKUBALIANI NA MWENZAKO JUU YA ITIKADI YAKE, LENGO NI KUFAHAMISHANA NA KAMA HUKURIDHIKA PASIWE NA HAJA YA KUKUFURISHANA AU KULETA MASHINDANO YA MABARAZANI, MIMI SINA HAKI YA KUKULAZIMISHA KUAMINI YALE USIYOTAKA AU KUYAFAHAMU HALKADHALIKA NA WEWE USIWE HIVYO, HIVI NDOVYO WASTAARABU WANAVYOISHI...

Kur'ani inasema " Sema, mimi au nyinyi mmoja wetu yuko katika upotevu uliodhahiri" (Kur'ani)

HII NDIO MANTIKI YA KUR'ANI, KIASI AMBACHO BWANA MTUME ANAAMBIWA ATANGAZE HAYO KWA WALE ASIOKUBALIANA NAO KIITIKADI WALA FIKRA KIASI AMBACHO YEYE MWENYEWE AMEJIKUBALISHA KUJITOLEA KWA KUSEMA IBARA HIZO" Haya Maa Salaam.

MWISHO