Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

SIKU YA MUBAHALA

0 Voti 00.0 / 5

SIKU YA MUBAHALA

MAANA YA MUBAHALA

Mubahala Ni: Kuapizana

Ujumbe wa Kikristo kutoka Najran ulifika kwa Mtume kujadili suala la Nabii Isa (a.s). Mtume aliwajulisha kuwa:

إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ  خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٥٩﴾

"Hakika mfano wa Isa (a.s) mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam, aliumbwa kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa naye akawa." 3:59.

Kwakuwa Nabii Isa alizaliwa bila baba, Wakristo wamedhani kuwa baba yake ni Mwenyezi Mungu.

Aya hii inaondoa dhana hiyo ambayo inapingana na utukufu wa Mwenyezi Mungu, na inawapigia mfano wa ajabu zaidi katika kuumbwa Adam bila ya baba wala mama. Aliumbwa kwa udongo kisha akaambiwa: kuwa naye akawa, na kwa neno hilo hilo Nabii Isa (a.s) ndivyo alivyoumbwa.

Ujumbe huo ulipokuwa haukukubaliana na hoja hii, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya:

"Na atakayehojiana nawe (Muhammad) katika hili baada ya ujuzi uliokufikia, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafis zenu, kisha tuombe kwa kunyenyekea tuijaalie laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie wenye kusema uongo." 3:61

Hili ilikuwa tarehe ishirini na nne mfungo tatu mwaka wa kumi, Mtume akawaita ili waanze kuapizana. Wakajibu: "Ngojea tujadiliane." Walipokwenda faragha, wakamuuliza Askofu Abdul Masih; ana Maoni gani katika suala hili? Akajibu:

Enyi Wakristo: Wallahi nyinyi mnajua kuwa Muhammad ni Nabii aliyeletwa na amekuja na ushahidi ulio wazi juu ya jambo la huyu ( Isa a.s). Wallahi hakuna watu walioapizana na Nabii wakasalimika, ikiwa mtaapizana naye mtaangamia."

Askofu yeye aliwaambia: "Enyi Wakristo: Mimi naziona nyuso hizi (kundi la Mtume) kama zitamuomba Mwenyezi Mungu auondoe mlima kutoka mahala pake, Wallahi atauondoa. Msiapizane naye mtaangamia, na hatabaki Mkristo ye yote hapa duniani mpaka siku ya Kiama."

Alipoulizwa Ahtam, akawaambia: Niacheni nikamuulize Muhammad, alipomkabili Mtume akamuuliza, "Ewe Abulqasim! Unatoka na kina nani kwa ajili ya maapizano haya?" Mtume (s.a.w.w) akamjibu: "Ninaapizana nanyi nikiwa na watu bora hapa duniani na watukufu mno mbele ya Mwenyezi Mungu, nao ni hawa (akawaonyesha) Ali, Fatima, Hasan na Husein."

Wakaogopa kuapizana na Mtume, na badala yake wakaomba sulhu kwa Mtume (s.a.w.w) kwa kutoa dirham arobaini elfu.

Katika Ayatul Mubahala, iliposema: "Tuwaite watoto wetu" Mtume (s.a.w.w) alimwita: Hasan na Husein. Iliposema: "Na wanawake wetu" Mtume (s.a.w.w) alimwita: "Fatima bint Muhammad." Iliposema: "Na nafsi zetu" mtume akamwita: "Ali".

Kwa hivyo Ali bin Abi Talib ni nafsi ya Mtume Muhamad (s.a.w.w).

Mwisho wa Makala

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini