Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KIFO CHA MTUME MUHAMMADI (S.A.W.W) SEHEMU YA KWANZA

0 Voti 00.0 / 5

KIFO CHA MUHAMMAD (s.a.w.w) MTUME WA ALLAH (s.w.t)

Malengo Ya Maisha Ya Muhammad Mustafa (s.a.w.w), Kama Mtume Wa Mwisho Wa Allah (s.w.t) Katika Dunia Hii Yalikuwa:

• Kuangamiza ibada ya masanamu na ushirikina;

• Kutangaza rasmi Tauhidi ya Muumba;

• Kufikisha Ujumbe wa Muumba kwa wanadamu;

• Kukamilisha mfumo wa dini na sheria;

• Kutakasa nafsi za wanaume na wanawake;

• Kukomesha dhulma, uovu na ujinga;

• Kuanzisha mfumo wa amani pamoja na haki;

• Kuunda chombo katika namna ya hali ya kisiasa kwa ajili ya utambuzi wa malengo hayo yote

yaliyopita, na chombo ambacho kitadumisha mwendo wa kazi yake.

Ndani ya ile miaka 23 ya kazi yake kama Mtume wa Allah, Muhammad (s.a.w.) alikuwa amefanikisha malengo yote Haya, na kisha ilianza kuonekana kama ilivyo kwa wanadamu wengine wote, yeye pia ilimbidui aondoke kwenye dunia hii. Kama ilivyoelezwa hapo kabla, alipokea taarifa hii kwa mara ya kwanza pale Suratun-Nasr (msaada), Sura ya 110 ya Qur’an Tukufu, iliyonukuliwa mapema katika kitabu hiki, iliposhushwa kwake.

Muhammad Mustafa alitumia maisha yake yote katika Swala na ucha-mungu lakini baada ya kuteremshwa kwa Nasr kuzama kwake katika kumuabudu Muumba wake kukawa kukubwa zaidi kuliko hapo kabla, katika kujiandaa kukutana Naye.

Mtume (s.a.w.w) mwenyewe alidokeza, angalau katika matukio haya mawili kwamba kifo chake hakikuwa mbali sana naye:

1. Katika hotuba yake ya Hija ya Muago pale Arafat siku ya Ijumaa, mwezi 9 Dhil-Hajj, mwaka wa 10 H.A., alisema: “Labda, hii ndio Hija yangu ya mwisho.” Katika kumalizia hotuba yake, aliuliza swali kwa mahujaji, yaani, “Mtakapoulizwa na Mola wenu kuhusu kazi yangu, majibu yenu yatakuwa yapi?” Mahujaji wakajibu kwa sauti moja: “Ulifikisha ujumbe wa Allah (s.w.t.) kwetu, na ulitimiza wajibu wako.” Alipolisikia jibu hili, alitazama kuelekea Mbinguni, na akasema: “Ewe Allah! kuwa shahidi kwamba nimetekeleza wajibu wangu.”

2. Wakati wa “kutawazwa” kwa Ali ibn Abi Talib pale Ghadir-Khumm, mnamo mwezi 18 Dhil-Hajj, 10 H.A., Muhammad (s.a.w.w), Mtume wa Allah (s.a.w.w) alizungumzia tena kifo chake kilichokuwa kinakaribia kwa kusema: “Mimi pia ni mwanadamu, na ninaweza kuitwa mbele ya Mola wangu wakati wowote.”

Makumi ya maelfu ya Waislamu waliyasikia matangazo haya ya Mtume wao (s.a.w.w), na wote walijua kwamba hatakuwa nao kwa muda mrefu zaidi. Yeye mwenyewe alijua kwam- ba alikuwa amekamilisha kazi yake ambayo Mola wake alimkabidhi, na alikuwa, kwa hiyo, na shauku ya kukutana Naye.

Mtume (s.a.w.w) alitumia nyakati zake za kila usiku pamoja na wake zake mbalimbali kwa zamu. Mnamo mwezi 19 Safar ya mwaka wa 11 H.A., ilikuwa ni zamu yake kulala kwenye chumba cha Aisha. Usiku, alitembelea viwanja vya makaburi vya Baqii akiwa pamoja na mtumishi wake, Abu Muwayhiba, ambaye baadae alisimulia kwamba:

 “Mtume (s.a.w.w) alisimama katikati ya makaburi na akayahutubia kwa maneno yafuatayo: ‘Amani iwe juu yenu ninyi mlioko kwenye makaburi haya. Mumebarikiwa katika hali yenu ya sasa ambamo mmejitokeza kutokea kwenye hali ambamo watu wanaishi katika dunia. Mashambulizi ya kuangamiza yanashuka moja baada ya jingine kama mawimbi ya giza, kila moja baya zaidi ya yale yaliyotangulia.’”

Muhammad Husein Haykal anasema kwamba yale maradhi “makali” ya Mtume (s.a.w.w) yalianza asubuhi iliyofuatia ule usiku ambao alitembelea uwanja wa makaburi, yaani, mnamo mwezi 20 Safar. Yeye anaendelea kusema:

Ilikuwa ni hapo kwamba watu waliingiwa na wasiwasi na lile jeshi la Usamah halikuondoka. Kweli, ile Hadith ya Abu Muwayhibah inatiliwa shaka na wanahistoria wengi ambao wanaamini kwamba maradhi ya Muhammad (s.a.w.w) yasingeweza kuwa ndio sababu pekee ambayo ilizuia hilo jeshi kutoondoka kwenda al-Sham, kwamba sababu nyingine ilikuwa ni kule kutoridhika kwa wengi, pamoja na idadi ya Muhajirina wakubwa na Ansari, kuhusiana na uongozi wa jeshi hilo. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935).

Itaendelea katika makala ijayo.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini