Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UHALALI WA KUTAWASALI KWA WAFU 2

0 Voti 00.0 / 5

UHALI WA KUTAWASALI

Sehemu ya Pili

UFAFANUZI KUHUSU KUFAA KUTAWASAL KWA MAWALII WALIOKUFA.

AsKwa majina naitwa SAIDI karimu Omari nipo Morogoro , :

Na vp kuhus Tawassul : Ufafanuzi kuhus kufaa kutawassal kwa mawalii ingali wakiw si hai

            MAJIBU. 2

Ndiyo inafaa, inajuzu kwa mujibu wa Qur-ani Tukufu na Matukio haya yaliyofanywa na Maswahaba wa Mtukufu Mtume saww

Wala usidhani wale walio uliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wafu, bali wako hai wanaruzukiwa kwa Mola wao. 3:169

ولا تحسبن الذين قتلوا في سبيل الله أموتا بل احياء عند ربهم يرزقون ١٦٩ .

Wakifurahia kile walichokipewa kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, na wanawafurahikia (wakionyesha furaha zao hizo kwa) walio nyuma yao ambao hawajawafuata (ambao hawajafa), kwamba Hapana khofu juu yao wala wao hawatahuzunika.3:170

فرحين بما آتاهم الله من فضله ويستبشرون بالذين لم يلحقوا بهم من خلفهم لا خوف عليهم ولا هم يحزنون.

Tawasuli nyingine ambayo Mtukufu Mtume saww anatufundisha kutumia Wasila katika kufanikisha maombi yetu, ni ile hadithi ambayo imepokewa na Abi Said Al Khudry. Katika tawasuli hiyo wasila ni wazi kabisa na inahimizwa mtu kuisoma kila siku mara tano. Mtukufu Mtume saww amesema kuwa:

"Mtu yeyote atokaye nyumbani kwake kwenda kuswali na akasema; Ewe! Mola wangu nakuomba kwa haki ya wakuombao na kwa haki ya mwendo wangu huu.

Rejea: Ihyau ya Ibn Khuzaima Jz 1 UK 323.; Attarghiib Wattarhiib Jz 1 UK 179.

Katika hadithi hiyo Mtukufu Mtume saww ameomba kwa haki ya viumbe wale wamumbao." Na tawasuli hii haina shaka na karibu vitabu vyote vya mafunzo ya ibada imetajwa na kuhimizwa kila muislam aombaye kwayo.

Upo ushahidi mwingine unaothibitisha kwamba kutawasal kwa majina ya Mitume na Mawalii inafaa na ni mujarrabu ni kuwa Mitume wa Mwenyezi Mungu walifanya hayo. Tuangalie hadithi iliyopokewa na Imamu Hakim kwa mapokezi Sahihi.

Mtukufu Mtume saww alisema: Wakati Adam alipofanya  kosa alisema: Ewe Mola wangu ninakuomba kwa haki ya Muhammad unisamehe. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamuuliza; Ewe Adam unajuaje Muhammad hali sijamuumba? Adam akasema Mola wangu uliponiumba kwa mikono yako na ukanipulizia roho itokayo kwako nilinyanyua kichwa changu nikaona katika nguzo za Arshi imeandikwa; "Hapana Mungu mwingine isipokuwa Allah na Muhammad ni mjumbe wake."

Nikafahamu kuwa huliweki jina lako pamoja na la mwingine isipokuwa aliyempenzi wako katika viumbe wako. Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: umesema kweli Adam kwa hakika yeye (Muhammad) ni mpenzi wangu katika viumbe wote. Umeniomba kwa jina lake nimekusamehe na kama si yeye (Muhammad) nisingekuumba.

Rejea: Al Mawahibu Laduniya Hakim Jz 2 UK 651; Dalailun Nubuwat cha Bayhaqi Jz 2 UK 62;: Ashafaus Saqimi ya Imamu Sabki;  Majmauz Zawaidi ya Al Hafidhu na Twabarani Jz 8 UK 253; Al Wafaa ya Sheikh Bakalain na Ibn Jauz; Al bidayat ya Ibn Kathir Jz 1 UK 180; Al Fatawa ya Ibn Taymiyya Jz 2 UK 150.

Maimamu wote tuliowataja wameipokea hadithi hiyo kwa mategemeo (Isnadi) Sahihi. Hadithi hiyo ni tawasuli na Nabii Adam as aliomba kwa cheo cha Mtukufu Mtume Muhammad saww asamehewe makosa yake. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anamhakikishia Nabii Adam kuwa amepokea maombi yake kwa haki ya Mtume Muhammad saww.

Hadithi nyingine ni ile ya Mtukufu Mtume saww yeye mwenyewe kuomba Du'a na katika Du'a hiyo akajifanya kuwa yeye ni Wasila. Wakati alipofariki bi Fatimah Bint Asad mamake Amirul Muuminina Ally bin Abi Twalib, Mtume saww alimwita Usamah Bin Zaidi, Abu Ayubu na Umar Bin Khatabi akawaamuru kuchimba kaburi. Ilipofikia Sehemu ya mwandani Mtume saww alichimba mwandani kwa mikono yake mwenyewe na alipomaliza aliomba akisema:.

Mwenyezi Mungu ni ambaye huweka uhai na mwenye kufisha hali kuwa yeye hayamfiki mauti. Msamehe mama yangu Fatimah Bint Asad na umtamkishe hoja yake kwa haki ya Mtume wako (mimi) na Mitume wa kabla yangu, hakika wewe ni mbora wa wenye Kurehemu, kisha akamswalia swala ya jeneza kisha akamuweka mwandani akiwa yeye (Mtume saww) na Abbasi na Abu Bakr.

Rejea: Majmauz Zawaidi Jz 9 UK 257 kwa mapokezi ya Twabarani, Ibn Hibbani na Hakim

Hapana shaka kuwa kwa hadithi hiyo Mtukufu Mtume saww Yeye mwenyewe alijifanya Wasila na akawafanya Mitume wote kuwa Wasila kupokewa Du'a yake.

Hadithi nyingine ni iliyopokewa na kusimuliwa na Al Hafidhu Abu Bakr Al Bayhaqi na Imamu Maalik akisema: Wakati wa utawala wa Umar bin Khatabi ukame uliwapata watu, Bilali Bin Rabaaha akaja mpaka kwenye kaburi la Mtukufu Mtume saww akasema:

 Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu omba mvua kwa ajili ya Ummah wako kwani wao wanahiliki, Bilali Bin Rabaaha akaijiwa na Mtukufu Mtume saww katika usingizi na kumwambia: "mwendee Umar na umpe Salam kutoka kwangu na wape habari kuwa mvua itabyesha, na mwambie Umar (aache ubabe) atumie busara na upole.

Bilali Bin Rabaaha akamwendea Umar akampa habari hiyo na Umar aliposikia taarifa hizo alilia sana.

Rejea: Fat'hul Bari Bisharhil Bukhari Jz 2 UK 410.; Al Bidayat cha Al Hafidhu Ibn Kathir Jz 1 UK 91. Mafahiim cha Sayyid Muhammad Alawi Maliky, UK 67; Dalailun Nubuwat cha Bayhaqi Jz 7 UK 47; Al Istiab cha Ibn Abdil Bary Jz 2 UK 464; Irshad Sari Jz 1 UK 313-314 ; Iqtidhwau ya Ibn Taymiyya UK 373.

Khalifa Mansuri Abbasiy alipofanya ziyara ya kumzuru Mtume saww katika kaburi lake Madina alimuuliza Mufti wa Madina Imamu Maalik Bin Anas akisema: "Ewe baba Abdallah! Je! Niekekee Kibla na kuomba au nimuelekee Mtume saww (katika kaburi lake)?

Imamu Maalik Bin Anas akajibu: kwa nini uugeuze uso wako kwake hali ya kuwa Yeye ndiye Wasila wako na Wasila wa Baba yako Adam mpaka siku ya Kiyamah? Bali mwelekee Mtume saww na omba kwaye Mwenyezi Mungu atayapokea maombi yako (kwani) Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema kuwa:

Lau wao wanapojidhulumu nafsi zao wangekujia wewe Muhammad na wakamtaka msamaha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume naye akawaombea bila shaka wangemkuta Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwenye kupokea Msamaha mwenye Kurehemu."4:64.

Rejea: Wafaul Wafaa Jz 2 UK 1376; Aduraru Saniyya cha Sayyid Ahmed bin Zain Dahlan Mufti wa Makkah UK wa 10; Ashifau Saqimi cha Imamu Sabki"' ; Mawahibu Laduniya ya Allama Hakim Qastalani; Al Khulaswatul Wafaa ya Sayyid Samhudi; Al Jawahirul Akhbar cha Ibn Hajar.

Zipo hadithi nyingi sana zinazoonyesha kuwa Maswahaba wa Mtukufu Mtume saww walikuwa wakifika katika kaburi la Mtukufu Mtume saww na kuomba Du'a mbele yake.

Aisha mke wa Mtukufu Mtume saww alikuwa akiwaelekeza Maswahaba kwenda kwenye kaburi la Mtukufu Mtume saww kwa ajili ya kuomba haja zao hasa maombi ya mvua na mvua ikanyesha.

Rejea: Sunanu Daramy Jz 1 UK 43.

Umar bin Khatabi alikuwa kila anapofikwa na ukame akiomba mvua kwa (Baraka za) Abbasi bin Abdul Mutwalib na akiomba kwa kusema,; Ewe Mola wangu tulikuwa tunatawasal kwako kwa njia ya Mtume wako na unatuletea mvua, na hakika tunatawasal kwako kwa haki ya ndugu wa Baba yake Mtume wetu tukiomba utuletee mvua."

Rejea: Sahihi Bukhari Jz 2 UK 32 mlango wa swala ya kuomba mvua.

Kwa hali yoyote itakavyokuwa Mtume saww ni Wasila wetu kama ambavyo Imamu Maalik alimwambia khalifa Mansuri Abbasiy. Kila baada ya Adhana tunatakiwa kumuombea Du'a Mtume saww apewe daraja ya juu ya kuwa Wasila wa wanadamu wote, ikiwa ni pamoja na Mitume wote na watu wao.

Sehemu ya Du'a hiyo inasema:-

آت سييدنا محمداً الوسيلة.

Mpe Bwana wetu Muhammad Uwasila ( daraja ya juu ya kuwa muombezi wa wanadamu wote siku ya Kiyamah) Du'a na maombi yetu yanapita kwake na kukaguliwa kama vile Yeye mwenyewe Mtume saww asemavyo: "Uhai wangu ni bora kwenu na kufa kwangu ni bora kwenu (kwani) amali zenu hupitishwa kwangu.

Nikukuta mazuri humshukuru Mwenyezi Mungu, na nikikuta kinyume na kheri hukutakieni Msamaha.

Pia Mtukufu Mtume saww katika hadithi iliyopokewa na Utba bin Ghaz'wan, ametufundisha njia ya kupata msaada kutoka kwa viumbe wa Mwenyezi Mungu tusiowajua akisema: Mmoja wenu atakapopotelewa na kitu au akahitaji msaada naye akiwa katika ardhi ambayo hakuna mzungumzaji, basi aseme: Eee! Waja wa Mwenyezi Mungu nisaidieni, hakika Mwenyezi Mungu anao waja ambao sisi hatuwaoni.

Bedui mmoja alimwendea Mtume saww baada ya kupoteza nuru ya macho na kumtaka amuombee Du'a ili apate kuona. Mtukufu Mtume saww alimuamrisha kutawadha na kisha kuswali rakaa mbili na kisha aombe kwa kusema:-

Eee! Mwenyezi Mungu hakika mimi naelekea kwako (kupitia) kwa Mtume wako Muhammad, Nabii ambaye ni Rehema, Eee! Muhammad hakika mimi naelekea kwako hadi kwa Mola wangu katika kutatua tatizo langu, na useme haja yako."

Bedui yule baada ya kuomba kwa Du'a hiyo alianza kuona kama kawaida.

Rejea: Sunan Nisa'i na Sunanu Tarmidhy.

Fuatana nami kwenye makala zangu ujifunze zaidi inshaallah.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini