Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 5

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN (A.S)

Sehemu ya Tano

JIHADI YA IMAMU HUSSEIN AS, 2

IMAM HUSSEINI (a.s) AENDA KUONGEA NA BABU YAKE

Katika usiku huu Hussein (a.s) alizuru kaburi la babu yake Mtume (s.a.w.w), nuru ikamwangazia kutoka kaburini, akasema: "Amani iwe juu yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni Hussein bin Fatimah, mtoto wako na mtoto wa bint yako na Mjukuu ambaye umemuacha katika ummah wako, washuhudie ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu, hakika wao Wamenidhalilisha na wala hawakunihifadhi.

Na haya ni malalamiko yangu kwako mpaka nitakapokutana nawe. Hakuacha kuwa ni mwenye kurukuu na kusujudu hadi asubuhi. Walid alituma mtu ambaye atamjulisha habari za Hussein (a.s) ambapo mjumbe hakumkuta nyumbani kwake, hivyo akadhani kwamba yuko nje ya Madina, mjumbe akamshuru Mwenyezi Mungu kwa kutopata mtihani wake.

Asubuhi Marwan alikutana na Abu Abdillahil Hussein (a.s) akampa nasaha ambayo alikuwa amewaandalia walio mfano wake, nayo ni kumpa kiapo cha utii kwa Yazeed l.a, kwani humo kuna Kheir ya dini na dunia, Hussain akasema :. Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika kwake tutarejea. Kisha akasema :.

Uislamu umekwisha kama ummah utapata balaa ya kiongozi mfano wa Yazeed, na niliishamsikia babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akisema :. Ukhalifa umeharamishwa kwa watu wa Abu Sufiyan, mtakapomuona Muawiyyah juu ya mimbari yangu pasueni tumbo lake. Na watu wa Madina walishamuona juu ya mimbari yake na hawakulipasua tumbo lake, hivyo Mwenyezi Mungu akawapa balaa la Yazeed fasiqi.

Mazungumzo yakawa marefu hadi Marwan akaondoka kwa hasira.

Katika usiku wa pili Hussein (a.s) alikwenda katika kaburi la babu yake Mtume (s.a.w.w) na akasali rakaa kadhaa kisha akasema :. Ewe Mwenyezi Mungu hakika hili ni kaburi la Nabii wako Muhammad (s.a.w.w), na mimi ni mtoto wa bint wa Nabii wako, na yamenifikia mambo ambayo umeshayajua.

Eee Mwenyezi Mungu hakika mimi napenda mema na nachukia Maovu, na nakuomba ewe Mwenye utukufu na ukarimu, kwa haki ya kaburi na aliye humo isipokuwa utanichagulia ambayo kuna Ridhaa yako na Ridhaa ya Mtume wako. "Imamu Hussein (a.s) akalia sana.

Ilipokaribia asubuhi akaweka kichwa chake juu ya kaburi akapata usingizi, akamuona Mtukufu Mtume (s.a.w.w) katika kundi la Malaika kuliani mwake, kushoto kwake na mbele yake, akamkumbatia Hussein (a.s) kifuani mwake na akambusu baina ya macho yake akasema :.

"Kipenzi changu ewe Hussein kana kwamba nitakuona hivi punde umetapakaa damu yako, umechinjwa katika ardhi ya Karbala baina ya waovu katika ummah wangu na wewe pamoja na hayo una kiu ya maji na hunyweshwi, una kiu na hupewi maji, wao baada ya hayo wanataraji shufaa yangu, Mwenyezi Mungu hatowapa shufaa yangu siku ya kiyama.

Kipenzi changu ewe Hussein, hakika baba yako, Mama Yako na kaka yako wamenijia na wao wanashauku nawe. "Hussein (a.s) akalia akamwambia babu yake amchukue pamoja naye na amuingize katika kaburi lake, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akasema:

Lazima upate shahada, upambane hadi wakuuwe ili yatimie yale aliyokuandikia Mwenyezi Mungu humo miongoni mwa thawabu kubwa, hakika wewe, baba yako na ami wa baba yako mtafufuliwa siku ya kiyama katika kundi moja na mwingizwe peponi.

Hussein (a.s) akazinduka na akasimulia ndoto yake kwa Ahlal Bayt Yake, huzuni yao ikazidi na vilio vyao vikawa vingi, na wakajua umekaribia wakati ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akiusema. Na kwa kuipupia kwao nuru ya Utume isije ikazuiwa kwao na wala wasije wakakosa haiba hiyo ya alawiya wakamkusanyikia na baadhi yao wakamtaka aondoke katika mji huo.

Fuatana nami sehemu ya Sita Hisoria ya Maasum Hussein bin Aliy (a.s).

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini