Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 7

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN (A.S)

Sehemu ya saba.

Jihadi ya Imamu Hussen bin Aliy (a.s). 4

WASIA WA IMAMU HUSSEIN (A.S)

Imamu Hussein (a.s) aliandika Wasia kabla ya kutoka Madina kwa ndugu yake Muhammad bin Hanafiyyah: Hakika Hussein (a.s) anashuhudia kwamba hakuna Mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu na wala hana mshirika, na kwamba Muhammad ni mja wake na Mtume wake, alikuja kwa haki kutoka kwake. Na kwamba pepo  ipo kweli na ni kweli moto upo na kiyama kitakuja, na hakuna shaka kwa hilo na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.

Hakika mimi sikutoka kwa kutaka shari, Ujeuri ufisadi na wala kwa kutaka Udhalimu. Bali nimetoka kwa kutaka kutengeneza ummah wa babu yangu Mtume Muhammad (s.a.w.w), nataka kuamrisha mema na Kukataza Maovu, na ninapita katika mwendo wa babu yangu na baba yangu Ally bin Abi Twalib as.

إني لم أخرج أشرا ولا بطرا ولا مفسدا ولا ظالما إنما خجت لإصلاح دين جدي و أبي علي بن أبي طالب عليه السلام أن آمر بالمعروف وانهي عن المنكر.....

Atakaye nikubali kwa kuikubali haki basi Mwenyezi Mungu ni mbora wa haki, na atakayenikatalia hili basi nitasubiri mpaka ahukumu Mwenyezi Mungu baina yangu na kaumu yangu, naye ni mbora wa wanao hukumu.

Na huu ni Wasia wangu ewe ndugu yangu, na hakuna tawfiiq isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwake nimetegemea na kwake nitarejea. Kisha akakunja barua akaipiga muhuri na akampa ndugu yake Muhammad.

Hussein (a.s) alitoka Madina kuelekea upande wa Makkah usiku wa kuamkia Juma pili, siku mbili kabla ya kumalizika mwezi wa Rajab, akiwa pamoja na watoto wake, ndugu zake, watoto wa kaka yake Hassan (a.s), na Ahlul Bayt Yake Tukufu, alitoka huku akisoma :. Akatoka humo hali ana khofu akajifichaficha akisema :. Ewe Mwenyezi Mungu niokoe kutokana na watu madhalimu.... Alqasas 28:21.

فخرج منها خآئفا يترقب قال رب نجني من القوم الظالمين.

Akafuata njia kuu, akaambiwa lau ungeacha njia kama alivyofanya Ibn Zuber, ili asikukute anayekutafuta, akasema :. Hapana Wallahi siiachi mpaka ahukumu Mwenyezi Mungu atakavyohukumu.

Aliingia Makkah siku ya ijumaa baada ya kupita siku tatu katika mwezi wa Sha'ban huku akiwa anasoma :. Na alipoelekea upande wa Madiyana akasema :. Huenda Mola wangu ataniongoza njia ya sawa.. Alqasas 28:22.

ولما توجه تلقآء مدين قال عسى ربي أن يهديني سوآء السبيل

Alifikia katika nyumba ya Abbas bin Abdul Mutwalibi, watu wa Makkah wakasongamana kwake ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya Umra na watu wanaotoka mbali. Ibn Zuber alikuwa ameng'ang'ania kwenye kona ya Alkaaba na alikuwa akimwendea Hussein (a.s) pamoja na waliokuwa wakimwendea.

Na kitendo cha Hussein (a.s) kuingia Makkah kilikuwa pigo kwake, kwani yeye Hussein (a.s) ni Mtukufu kuliko yeye Ibn Zuber, na Hussein (a.s) anatiiwa zaidi na watu, hivyo Ibn Zuber hatapewa kiapo cha utii maadamu Hussein (a.s) yuko humo. Imamu Hussein (a.s) alitoka katika baadhi ya siku kwenda kuzuru kaburi la Bibi yake Khadija (a.s) akaswali huko na akamuomba Mwenyezi Mungu sana.

IMAMU HUSSEIN (A.S) KATIKA MJI WA MAKKAH.

 Na katika mji wa Makkah Hussein (a.s) aliandika nakala moja ya barua kwa Viongozi watano wa Basra, nao ni Malik bin Musma'a, Amru, Qays bin al Haytham, na Amru bin Ubaidah bin Mu'amar, na alizituma kupitia aliyekuwa Mtumwa wake aliyekuwa Anaitwa Sulaiman, na humo kulikuwa na haya :.

        Ama baada :. Hakika Mwenyezi Mungu amemteua Muhammad (s.a.w.w) kwa viumbe vyake na akamkirimu kwa Unabii wake na akamchagua kwa ujumbe wake, kisha akamfisha. Na alikuwa tayari ameshawanasihi waja wake na kufikisha aliyotumwa, na sisi tulikuwa ni watu wake, Mawalii wake, Mawasii wake, Warithi wake, na watu wenye haki zaidi kwa nafsi yake kuliko watu wengine.

Kaumu yetu ikatupokonya hilo, tuliridhia na tukachukia mgawanyiko na tukapenda afya "amani" na sisi tunajua kwamba tuna haki kwa hilo, haki ambayo inatustahiki kuliko hao walioichukua (Abu Bakr bin Abi Quhafa na Umar bin khatabi na Uthmani bin Afan, na Muawiyyah).

Nami nimetuma mjumbe wangu kwenu na barua hii, na mimi nawalingania katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah za Nabii wake, hakika Sunnah zimeuliwa na Bid'aa zimehuishwa, (watu wameng'ang'ania Bid'aa zilizo anzishawa ni Banu Umayyah, wakaacha Sunnah za Mtukufu Mtume (s.a.w.w)), kama mtasikia kauli yangu nitawaongoza katika njia ya uongofu.

BARUA ZA WATU WA KUFAH

Katika mji wa Makkah zilimfikia barua za watu wa Kufah kutoka kwa mtu mmoja mmoja, wawili wawili, watatu watatu, na wanne wanne, wote wakiomba Hussein (a.s) aende kwao kwa sababu hawana kiongozi na hawakusanyiki kwa Nu'man bin Bashir, si katika ijumaa wala katika jamaa. Barua zilizidi kuwasili kwake hadi imepokewa kuwa, kwa siku moja zilimfikia barua mia Sita, na zikakusanyika kwake kutoka pande mbali mbali barua kumi na mbili elfu, na barua zote hizo zinasisitiza kumuomba, lakini hakuwajibu,.

Na barua za mwisho kuwasili kwake ni kutoka kwa Sha'bathi bin Rabiy, Al Hajjaj bin Abujar, Yazidi bin Utarid bin al Harithi, Usirah bin Qays, Amru bin Rabiy, Muhammad bin Umair bin Utarid, na humo kulikuwa na :. Hakika watu wanakungojea, hawana rai isipokuwa wewe njoo upesi ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwani mimea imeshastawi, matunda yameiva, ardhi imetoa majani na miti imechanua, ukitaka njoo kwani utakuja katika jeshi lililoandaliwa kwa ajili yako.

Fuatana nami sehemu ya nane historia ya Maasum Hussein bin Aliy (a.s).

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini