Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 13

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN A S

Sehemu ya kumi na tatu

Jihadi ya Imamu Hussein Bin Ally a.s 10

HUSSEIN a.s ATOA HABARI ZA KIFO CHAKE

Ulipofika mwisho wa usiku akawaamuru vijana wake watafute maji na kuondoka katika kasri ya Bani Muqatil, na walipokuwa wakienda walimsikia Hussein as anasema; " Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika kwake yeye tutarejea.

إنا لله و انا اليه راجعون

Kila sifa njema ni ya Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe wote." Na akakatiri mara ya pili, ndipo Ally Akbar akamuuliza juu ya kusema kwake hivyo, akasema: "Hakika mimi nilisinzia nikamuona mpanda farasi naye anasema: 'Watu wanakwenda na Mauti yanawaendea.' nikajua kuwa ni sisi tunaoelezwa." Ally Akbar akasema: "Mwenyezi Mungu asikuonyeshe ubaya, je hatuko katika haki?" Akasema: "Tuko kwenye haki, naapa kwa yule ambaye ni marejeo ya waja. " Ally Akbar akasema: "Ewe baba yangu basi hatutajali kufa katika haki." Hussein as akasema: "Mwenyezi Mungu akulipe, ni wema ulioje mtoto kumlipa kheri mzazi wake."

Hussein as akamgeukia Hurr na akasema: "Twende tutembee kidogo." Wote wakatembea mpaka wakawasili katika ardhi ya Karbala, Hurr akasimama na wafuasi wake mbele ya Hussein as na akamzuia kutembea na wakamwambia; "Hakika sehemu hii iko karibu na mto Furati."

Na inasemekana walipokuwa wanatembea farasi wa Hussein as alisimama na hakutembea kama alivyomsimamisha Mwenyezi Mungu Ngamia wa Nabii s.a.w.w pale Hudaibiya, hapo Hussein as akauliza kuhusu ardhi hiyo, Zuheiri akamwambia: "Kuwa mwongofu na wala usiulize juu ya kitu (chochote) mpaka Mwenyezi Mungu alete faraja, kwani ardhi hii inaitwa Twafu."

Hussein as akasema,: "Je, ina jina jingine?" Zuheiri akasema: "Inaitwa Karbala." Machozi yakadondoka na akasema: "Ewe Mwenyezi Mungu najikinga kwako kutokana na shida na balaa, كرب وبلا hapa ndiyo mwisho wa vipando vyetu, mahala pa kumwaga damu zetu na sehemu ya makaburi yetu, haya amenisimulia babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu saww."

Na kuwasili kwake Karbala ilikuwa katika mwezi wa Muharram 2 mwaka 61 hijiria. Alikusanya watoto wake, ndugu zake na Ahlubaiti wake, aliwatazama na kulia kisha akasema: "Ewe Mwenyezi Mungu kizazi cha Nabii wako Muhammad saww tumetolewa, tumefukuzwa natumefanyiwa fujo katika haram ya babu yetu, na Bani Umayyah wametufanyia uadui. Ewe Mwenyezi Mungu tuchukulie haki yetu na utunusuru kutokana na watu madhalimu."

Akawaelekea wafuasi wake akasema: "Watu ni watumwa wa dunia na dini ni muonjo katika ndimi zao, wanaihifadhi maadamu tu maisha yao yanakwenda vizuri, lakini wanapopata mtihani wenye kushikamana na dini wanakuwa wachache mno." Kisha akamshukuru Mwenyezi Mungu na akamtukuza, akamtakia rehema Muhammad na Ahali zake na akasema: "Ama baad, limetufika jambo kama mnavyoona, dunia imeshageuka imekuwa mbaya kabisa na imeacha mema yake, na hakujabaki humo isipokuwa unyevunyevu kama vile unyevunyevu wa chombo, ni maisha duni kama vile mfano wa chakula kibaya. Je, hamuoni kwamba haki haitendwi na batili haikatazwi, basi Muumini apende kukutana na Mola wake, hakika mimi sioni Mauti isipokuwa ni utukufu na maisha pamoja na madhalimu isipokuwa ni udhalili.

Zuheiri akasimama na akasema: "Tumesikia maneno yako ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi, Mwenyezi Mungu ametujaalia sisi Kupigana pamoja na wewe, viungo vyetu vitakatwa kwa kukutetea, kisha babu yako atakuwa muombezi wetu siku ya kiyamah."

Naafi'u Bin Hilali akasema: "wewe unajua kuwa babu yako ni Mtume wa Mwenyezi Mungu saww, hakuweza kuwanywesha mapenzi yake wala kuwarejesha katika jambo lake analolipenda, miongoni mwao kulikuwa na Wanafiki wanamwahidi kumnusuru na wanadhamiria kumfanyia hiyana, wanamkabili kwa maneno matamu kuliko asali na wanamfichia yaliyo machungu kuliko shubiri, mpaka Mwenyezi Mungu akamchukua.

Na baba yako Ally alikuwa katika mfano wa hayo, watu walikusanyika katika kumnusuru wakawapiga pamoja naye waovu, waasi na wakaidi, mpaka yakamjia Mauti yake akaenda katika rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi zake. Na wewe leo kwetu uko katika hali hiyo hiyo, atakayetengua ahadi yake na kuvua kiapo cha utii wake hatodhuru isipokuwa nafsi yake, na Mwenyezi Mungu atamtosheleza. Twende tuongoze, tuelekeze Mashariki au Magharibi ukitaka, Wallaahi hatuogopi makadara ya Mwenyezi Mungu wala hatuchukii kukutana na Mola wetu, na hakika sisi tuko katika nia zetu na akili zetu, tutampenda anayekutawalisha na tutamfanyia uadui anayekufanyia uadui."

Fuatana nami katika Sehemu ya kumi na nne ya historia ya Imamu Hussein Bin Ally as

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini