Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 15

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN A S

Sehemu ya kumi na sita

Jihadi ya Imamu Hussein Bin Ally as 13

JESHI LA YAZID LASOGEA TAYARI KWA VITA

Umar bin Saad aliondoka usiku wa Alihamisi baada ya kupita siku tisa za Muharram, na akatangaza katika kambi yake kuondoka kuelekea upande wa Hussein as, Hussein as alikuwa amekaa mbele ya hema lake ameinamia panga lake anasinzia, mara akamuona Mtume wa Mwenyezi Mungu saww akisema: "Hakika wewe utakuja kwetu hivi karibuni." Zainabu akasikia sauti za wanaume akamwambia ndugu yake: "Maadui wamekaribia kwetu." Ndipo Hussein as akamwambia ndugu yake Abbas as panda farasi mwenyewe ili ukutane nao na uwaulize kipi kinawaleta na wanataka nini?

Abbas as akaondoka na wapanda farasi ishirini miongoni mwao akiwemo Zuheiri na Habib Bin Mudhwahir (mzee mwenye miaka 90), na akawauliza juu ya hilo. Wakasema: "Imekuja amri ya Amir kwamba tuwaambie muwe chini ya hukumu yake au tuwapige vita." Abbas as akamjulisha ndugu yake Abu Abdillah as waliyokuja nayo kaumu, akasema: "Rudi kwao na uwaambie watupe muda usiku huu mpaka kesho huenda tutaswali kwa Mola wetu usiku tumuombe na tumtake maghufira, kwani yeye anajua kwamba napenda swala kwa ajili yake, kusoma kitabu chake, kuomba dua kwa wingi na kutaka maghufira."

Abbas as akarejea na akawaambia wampe muda wa usiku, Ibn Saad akasimama na akawauliza watu, Amru bin Al Hajjaj akasema: "Subhanallah wangekuwa wanatoka ad Daylam na wakakuomba hili lingekupasa uwakubalie." Qays bin Al Ash'ath akasema: "Wakubalie haya waliyokuomba, kwani utawapiga vita asubuhi." Ibn Saad akasema: "Wallaahi lau ningejua kuwa atafanya hivyo basi nisingemwachia usiku huu."

Kisha akatuma ujumbe kwa Hussein as: "Hakika tumewaacha mpaka kesho, kama mtajisalimisha tutawapeleka kwa Amir Ibn Ziyad, na kama mtakataa basi hatutawaacha."           Hussein as akakusanya watu wake karibu na jioni kabla ya kuuliwa kwake kwa usiku mmoja, akasema:

"Namshukuru Mwenyezi Mungu shukrani njema kabisa, na namshukuru kwa neema na shida, Ewe Mwenyezi Mungu nashukuru kwa kutukirimu Unabii, umetufundisha Qur'an, umetufundisha dini na umetujaalia masikio, macho na nyoyo, na hukutujaalia kuwa miongoni mwa mushirikina. Ama baad: Hakika mimi sijui wafuasi waaminifu na bora kuliko wafuasi wangu, Wala Ahlubaiti wema na wenye kuunga udugu kuliko Ahlubaiti wangu, Mwenyezi Mungu awalipe kheri nyote kwa ajili yangu.

Babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu saww ameshanipa habari kwamba mimi nitapelekwa Iraq na nitateremkia katika ardhi inayoitwa Amuur au Karbala na humo nitakufa Shahidi na wakati umewadia, Eee, hakika mimi nadhani siku yetu kwa hawa maadui ni kesho, na mimi nimeshawaruhusu basi nendeni wote mko huru, hamna dhima yeyote kwangu, na huu usiku umeshawafunika basi uchukulieni kuwa ni hifadhi, na kila mwanaume kati yenu amshike mkono mwanaume katika Ahlubaiti wangu, Mwenyezi Mungu awalipe kheri nyote, na tawanyikeni katika usiku wenu na Sehemu zenu kwani watu wananitaka mimi, na kama watanipata basi hawatamtaka asiye kuwa mimi."

Ndugu, watoto wake na watoto wa Abdillah Bin Ja'afar as wakamwambia: "Hatufanyi hivyo! Mwenyezi Mungu hatatuonyesha hilo kamwe." Aliwatangulia kwa kauli hiyo Abbas Bin Ally as, akafuatiwa na Bani Hashim. Hussein as akawageukia watoto wa Aqili na akasema: "Imewatosha kuuliwa kwa Muslim, nendeni nimewaruhusu." Wakasema: "Watu watasemaje na tutawaambia nini? Sisi tumemwacha mzee wetu, bwana wetu na watoto wa Ami zetu walio bora, na wala hatujapigana pamoja nao kwa kutupa mishale, mikuki, wala kwa kupiga mapanga na wala hatujui walichokifanya. Hapana Wallaahi hatufanyi hivyo, lakini tutakufidia kwa nafsi zetu, mali zetu na ahali zetu, tutapigana pamoja na wewe mpaka tupitie mapito yako, kwa kweli Mwenyezi Mungu ayafanye maisha yawe mabaya baada yako."

Muslim bin Awsajah akasema: "Sisi tukuache, je, tutakuwa na udhuru gani kwa Mwenyezi Mungu katika kutekeleza haki yako? Lakini Wallaahi sitakuacha mpaka nipige mkuki katika vifua vyao na nimpige kwa mkono wangu na kwa upanga wangu yule aliyesimama miongoni mwa wapiganaji wao, na kama nisingekuwa na silaha nitakayowapiga nayo basi ningewapiga kwa mawe mpaka nife pamoja na wewe."

Said bin Abdillah Al Hanafiy akasema: "Wallaahi hatukuachi mpaka Mwenyezi Mungu ajue kuwa tumehifadhi haiba ya Mtume wake kwako. Wallaahi kama ningejua kuwa nitauliwa kisha nitafufuliwa kisha nitachomwa moto kisha niwe majivu, nifanywe hivyo mara sabini, basi nisingekuacha mpaka nife kwa kukutetea. Na vipi nisifamye hivyo hali ya kuwa ni kifo kimoja tu kisha ni utukufu ambao haumaliziki milele."

Zuheiri Bin Al Qayni akasema: "Wallaahi natamani niuliwe kisha nifufuliwe mpaka niuliwe mara elfu, na kwamba Mwenyezi Mungu alinde kwa kifo hicho nafsi yako na nafsi ya hawa watoto miongoni mwa Ahlubaiti wako."

Na wafuasi waliobaki walizungumza maneno yanayofanana na ya baadhi yao, na Hussein as akawashukuru.

Hussein as alipojua kutoka kwao uaminifu na ikhilasi katika kujitolea kwa ajili yake, akawaeleza wazi akisema: "Hakika mimi nitauliwa kesho na nyote mtauliwa, na habaki yeyote miongoni mwenu hata Qasim na Abdillah mtoto mchanga isipokuwa mtoto wangu Ally Zainul Abidiina, Mwenyezi Mungu hajakata kizazi changu kwake, naye ni baba wa Makhalifa (Maimamu) nane."

Wote wakasema: "Tunamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametukirimu kwa nusura yako na kututukuza kwa Kupigana pamoja na wewe, je, huridhii tuwe pamoja na wewe katika daraja yako ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Basi akawaombea kheri akawaondolea pazia kwenye macho yao wakaona aliyowaandalia Mwenyezi Mungu miongoni mwa neema za peponi na akawafahamisha  na kuwaonesha makazi yao humo.

Fuatana nami katika Sehemu ya kumi na saba historia ya Imamu Hussein Bin Ally as

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini