Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 17

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN A S

SIKU YA ASHURA.

BWANA WA MASHAHIDI 2.

Sehemu ya Thelathini na moja

JIHADI YA IMAMU HUSSEINI AS.28

MUHAMMAD BIN ABI SAIDI

Haaniy bin Thabit al Hadharamiy amesema :. Mimi nilikuwa nimesimama siku ya Ashuraa alipouliwa Hussein a.s. Ndipo nilipomwona kijana katika watu wa Hussein a.s amevaa shati na kikoi, na katika masikio yake kuna hereni mbili na mkononi mwake ana nguzo, alikuwa akitoka katika Mahema hayo na hali ni mwenye hofu, anageuka kulia na kushoto. Mwanaume mmoja akamwendea kwa kukimbia hadi alipomkaribia, akainama kwenye Farasi wake akamkata yule kijana kwa upanga wake, alipozidiwa akajitambulisha mwenyewe. Na kijana huyo ni Muhammad bin Abu Saidi bin Aqiil bin Abi Twalib as, wakati huo mama yake alikuwa anamtazama kwa mshangao.

ABDULLAH BIN HASSANI

Kisha walikaa kidogo wakamrejea Hussein a.s wakamzunguka akiwa amekaa ardhini hawezi kuamka, Abdullah bin Hassan ambaye alikuwa na miaka kumi na moja, akamtazama Mjukuu wa Mtume na ammi yake, huku watu wakiwa wamemzunguka, ndipo Akatoka kuelekea kwa ammi yake, Zainabu akataka kumzuia lakini akaponyoka na kumuendea ammi yake, ndipo Bahri bin Ka'ab akatupa upanga ili ampige Hussein a.s, kijana akapiga kelele :. Ewe mtoto wa Muovu unataka kumpiga ammi yangu? Akampiga nao lakini mtoto akauzuia kwa mkono wake, nao ukamkata hadi kwenye mwili, akabaki akiwa ameelea, kijana akapiga kelele :. Ewe ammi yangu! Na akaangukia kwenye miguu ya Hussein a.s, akamkumbatia na akasema :. Ewe mtoto wa ndugu yangu, kuwa mvumilivu kwa yaliyokupata na yahesabie hayo kuwa ni katika Kheir, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu atakukutanisha na baba zako wema.

Kisha akanyanyua mikono yake kwa kusema :. Ewe Mwenyezi Mungu wafurahishe kwa muda mchache na uwatawanye kabisa, na wajaalie njia za mfarakano wala usiridhie utawala kutoka kwao kamwe, hakika wao wametuita ili watunusuru kisha wakatugeuka wakawa wanatuuwa. Hurmalah bin Kahil l.a akampiga mshale akamchinja kijana yule akiwa katika miguu ya ammi yake.

Hussein a.s akabaki ameanguka hajiwezi, na lau wangetaka kumuuwa wangemuuwa lakini kila kabila lilikuwa linaliachia kabila jingine na linachukia kutangulia. Shimr bin Dhilijawshen I.a akapiga kelele :. Ni nini kusimama kwenu? Na mnangoja nini kwa mwanaume aliyekwisha choshwa na mishale na mikuki, mshambulieni. Za'rat bin Sharik akampiga juu ya bega lake la kushoto, Al Hasiyn akampiga mbele kwenye koo lake na mwingine akampiga kwenye bega lake. Sanan bin Annas akakichoma kifua chake.

Hilal bin Nafi'u amesema :. Nilikuwa nimesimama kando ya Hussein a.s, naye akiwa anagaragara, Wallahi katu sikuona maiti iliyotapakaa damu yenye uso mzuri na wenye nuru zaidi kuliko yeye, nuru ya uso wake ilinishughulisha katika kufikiria kumuuwa, katika hali hii aliomba maji wakamnyima, mwanaume akamwambia :. Hautoyaonja maji hadi uingie motoni ukanywe katika maji yake.

Hussein a.s akasema :. Mimi Nitakwenda motoni? Bali Nitakwenda kwa babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu na nitaishi naye katika nyumba yake ndani ya makazi ya kweli kwa Mfalme Muweza, na nitamshitakia Maovu mliyonitendea na mliyonifanyia. Wote wakakasirika kana kwamba Mwenyezi Mungu hakujaalia huruma katika moyo wa mmoja wao.

MAOMBI

Hussein a.s alipozidiwa alinyanyua kichwa chake na kusema :. Eee Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye Mamlaka, mkali wa kuadhibu na asiyehitajia viumbe, mkuu wa viumbe, Muweza wa anachokitaka, mwingi wa huruma, mkweli wa ahadi, Mwenye kuneemesha, Mwenye kuleta mtihani, aliye karibu mno akiombwa, Mmiliki wa vilivyoumbwa, Mwenye kukubali toba kwa Mwenye kumtaka msamaha, Muweza kwa niliyoyaomba, Mwenye Shukurani anaposhukuriwa, Mwenye kukumbuka anapokumbukwa na kuombwa kwa kuhitajia, nakuomba nikiwa fakiri, nakuomba hali ya kuwa na hofu, nalia hali ya kuwa na shida, nataka msaada kwako hali ya kuwa dhaifu, nakutegemea hali ya kuwa ni mwenye kutosheka.

Ewe Mwenyezi Mungu hukumu baina yetu na watu wetu, hakika wao wametudanganya, wametudhalilisha, wametuhadaa, na wametuuwa, na sisi ni kizazi cha Nabii wako, watoto wa kipenzi chako Muhammad s.a.w.w. ambaye umemtuma kwa ujumbe wako na ukamwamini kwa wahyi, basi tujaalie faraja na Njia katika jambo letu.

Ewe mwingi wa rehema tunaisubiri hukumu yako, eee Mola na hakuna Mungu isipokuwa wewe, ewe msaada wa wenye kutaka msaada, sina Mola isipokuwa wewe wala sina mwenye kuabudiwa isipokuwa wewe, nasubiri katika hukumu yako, ewe msaada kwa asiyekuwa na msaada, ewe mwenye kudumu asiyeisha, ewe mwenye kufufua wafu, ewe Msimamizi wa kila nafsi kwa kila ilichokichuma, hukumu baina yangu na baina yao, na wewe ni mbora wa kuhukumu.

Fuatana nami sehemu ya Thelathini na mbili ya historia ya Imamu Hussein Bin Ally as, mapambano ya Bwana wa Mashahidi 3

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini