Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W) 6

0 Voti 00.0 / 5

BAADA YA KARAMU YA HARUSI KUFANYIKA SIKU TATU ILIYO ANDALIWA NA JABALI LA IMAN ABU TWALIB AS KWA AJILI YA MTUKUFU MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W)

BIBI KHADIJA NAYE AANDAA TAFRIJA KUBWA YA CHAKULA SIKU TATU MUTAWALIA NA KUWEKA HISTORIA KATIKA MAKKAH TUKUFU

Ilifuata zamu ya Khadija Kuonyesha ukarimu na wema wake. Ukarimu na wema yalikuwa mazoea yake makubwa. Na hafla gani ambayo ingefaa zaidi au kupendeza kama si kwenye Sherehe ya harusi yake kutosheleza hulka yake? Kwa hiyo, Khadija, alimwagiza mkuu wake wa Itifaki kutayarisha mipango kwa kuandaa Karamu/tafrija kubwa kabisa ya chakula na kuweka historia katika Makkah.

Hiyo ilikuwa Karamu ya kukumbukwa kweli. Hata ombaomba wa Makkah na makabila ya watu wanaohama hapa na pale na wanawake, walikuwa kwenye kundi la waalikwa. Watu walikula vyakula ambavyo kamwe hawajapata kuviona. Wale Waarabu wa jangwani ambao kamwe walikuwa hawajawahi kuonja kitu chochote isipokuwa maji ya chumvichumvi au yanayonuka katika maisha yao siku hiyo walikunywa maji ya waridi wakiwa wageni wa Khadija.

Kwa muda wa siku nyingi wageni waalikwa matajiri na fukara, mashuhuri na wenye daraja la chini, mamwinyi na wanyonge, vijana na wazee walikula nyumbani kwa Khadija. Khadija aliwapa wageni waalikwa walio masikini, vipande vya dhahabu na fedha na nguo, na alijaza nyumba za wajane wengi na watoto yatima mahitaji mengi ya muhimu ambayo hawakuwa nayo.

Khadija alikaa miaka mingi ya maisha yake akingojea mwanamume anayefaa kumuoa. Alipata mafanikio baada ya kungoja kwa muda mrefu alipojitokeza Muhammad, na wakaunganishwa katika ndoa takatifu.

Ndoa ya Muhammad na Khadija ilikuwa ya kwanza na ya mwisho kwa aina yake hapa duniani. Ilikuwa ni ndoa hiyi tu duniani pote ambayo ilipata neema za Akhera na mali za hapa duniani. Ilikuwa ndoa ambayo ilipata rehema nyingi zisizo na kipimo na hesabu za peponi na hapa duniani.

Inawezekana kabisa kwamba katika Bara Arabu lote, hakuna mwanamke yeyote ambaye alipata kwenda nyumbani kwa mumewe na mahari nyingi kiasi hicho kama alivyofanya Khadija. Ilijumuisha watumwa, wasichana, mbuzi na kondoo, na nguo zake binafsi za bei ghali, vitu vya ziada, vitu vya urithi visivyoweza kukadiriwa bei, mapambo, vitu vya thamani vya chuma, vito vya thamani na dhahabu nyingi na vipande vya fedha.

Mahari hii, ambayo haikutazamiwa kuwa hivyo kwa ubora na wingi wake, haikuwa zawadi aliyopewa Khadija, Bibi harusi na ami zake au kutoka kwa kaka zake. Haya yalikuwa ni matokeo ya jitihada zake mwenyewe. Alizalisha mali hiyo kwa uangalifu wake, bidii yake, busara zake na uwezo wa kuona mbali kifikira.

Lakini huu haukuwa ndiyo tu utajiri aliokuja nao Khadija. Khadija pia alikuja na utajiri wa moyo na akili, na hivi vilikuwa havina kipimo na visivyokwisha. Katika miaka iliyofuata, Khadija aliyatajirisha pasipo kipimo maisha ya mumewe kwa kutumia vipaji hivyo.

Mara tu Khadija alipoolewa, alionekana kupoteza upendeleo wake kwenye biashara na milki yake ya biashara. Maisha ya ndoa yalibadilisha tabia yake, kujitolea kwake, na wajibu wake. Alimpata Muhammad Mustafa, hazina kubwa kuliko zote hapa duniani. Mara Khadija alipompata Muhammad, dhahabu, fedha na almasi zilipoteza thamani; kwake Muhammad Mustafa Mjumbe mtarajiwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume mtarajiwa wa Uislamu, akawa ndiyo tu, kitu cha kuelekeza mapenzi yake, uangalifu wake na bidii yake.

Mambo kama yalivyokuwa, hakupoteza uwezo wake mkubwa wa kupanga mambo, lakini badala ya kutumia uwezo huo katika biashara zake, aliutumia kwa kumtumikia mumewe. Aliyapanga maisha yake yote upya na kumfanya Muhammad Mustafa kuwa ndiyo mhimili wake wa maisha.

Khadija hakusitisha biashara zake nyingi mara moja. Alizisimamisha kwa awamu. Kwa hiyo, kwa viwango alimsimamisha biashara ya kuingiza mali ndani ya nchi na kutoa nje ya nchi ambayo baba yake aliianzisha.

Miaka iliyofuata baada ya ndoa yake, Muhammad alianza kusafiri tena na misafara ya Khadija kwenda Syria. M. Shibli, mtaalamu wa historia kutoka India,  anasema kwamba pia alikwenda Yemen. Popote alipokwenda, alipata faida kubwa. Khadija pia aliajiri Mameneja wengine ambao waliuza bidhaa zake, au walinunua bidhaa kwa ajili ya mauzo yake, na wao pia walipata faida. Lakini, msisitizo ulibadilishwa, badala ya kupanua biashara yake kama alivyokuwa anafanya kabla ya kuolewa, Khadija alianza kupunguza bidhaa pole pole hadi hapo ambapo bidhaa zote ziliuzwa, na alikusanya fedha zote kutoka kwenye miradi.

Wakati Malkia wa Makkah alipoingia nyumbani kwa mumewe Muhammad Mustafa, awamu ya maisha yake ya furaha kubwa ilianza. Awamu hii ilidumu miaka Ishirini na tano hadi Kifo chake. Mara moja Khadija alibadili maisha yake na kuafikiana na mazingira mapya. Tangu siku ya kwanza alianza usimamizi wa kazi yake ambayo ilikuwa kufanya maisha ya mume wake kuwa ya furaha na mazuri. Katika kufanya kazi hii alifuzu vizuri sana kama historia ya siku zilizofuata ilivyosadikisha kwa ufasaha kabisa.

Maisha ya ndoa yalifungua ukurasa mpya wa maisha ya Muhammad na Khadija. Jambo la msingi la "ukurasa" huu mpya ilikuwa furaha, furaha isiyo na dosari. Pamoja na kwamba ndoa yao ilipewa baraka za furaha, pia ilipata neema ya watoto. Mtoto wao wa kwanza, alikuwa wa kiume aliyeitwa Qasim. Ilikuwa baada ya kuzaliwa Qasim, baba yake Muhammad Mustafa alipewa jina la Abu l Qasim (baba wa Qasim) kufuatana na mila za Kiarabu.

Pia mtoto wa pili wa kiume. Jina lake lilikuwa Abdullah. Alipewa majina ya lakabu ya Twahir na Twayyib. Watoto wote wawili bahati mbaya hawakuishi muda mrefu, walikufa wakiwa bado wachanga.

Mtoto wa tatu na wa mwisho aliyezaliwa mwaka wa 5 biitha na ndiyo huyo tu aliyeishi muda mrefu miongoni mwa watoto wa Muhammad na Khadija alikuwa binti yao Fatimah Zahraa, mtoto wa kike. Ingawa Mwenyezi Mungu aliwatunuku zawadi nyingi, hakukuwepo na chochote kile kingine walicho kithamini zaidi ya bint yao. Fatimah alikuwa "mwanga (nuru) wa macho" ya baba yake, na alikuwa " starehe ya moyo wa babake". Alikuwa pia "Kiongozi wa wanawake wa peponi. Na Malkia wa wanawake wa Ulimwengu wa mwanzoni na wa mwishoni.

 سييدة النسآء في الجنه، وسيدة النسآء العالمين.

Baba na mama walimpenda sana, na alileta pamoja naye matumaini na furaha na baraka na huruma zake Mwenyezi Mungu ndani ya nyumba yao.

Fuatana nami Sehemu ifuatayo historia ya Ma'asum Mtukufu Mtume Muhammad saww alipofikia umri wa miaka 30 alizaliwa kijana aliyekuja kuwa ni mlinzi wa maisha yake na maisha ya ujumbe wake.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini