BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE 8
- Imesambazwa tarehe
-
- Mwandishi:
- Sheikh Muhammad Ibrahim El-Qazwiniy
- Chanzo:
- Al-Islam.org
BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE
Sehemu ya Saba
B
KUTOKUVAA HIJABU NA UHARIBIFU WA NDOA
Hapana shaka, hayo ni matokeo ya wanawake kuuwacha utamaduni wao wa Kiislamu katika suala la mavazi, pia mienendo ya Waislamu imebadilika na wameshawishika na utamaduni mbaya wa kimagharibi. Kutokana na kupotea kwa Waislamu na kuacha mwelekeo na utamaduni wao, sasa hivi imekuwa kazi ngumu kuyaepuka maovu na balaa hizi isipokuwa njia pekee ni kurudia utamaduni wetu kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w.w).
Ewe msomaji mpendwa, hebu kaa tayari nikusimulie hicho kisa ili ujionee mwenyewe umuhimu wa Hijabu kwa maana yake kamili na pia ubaya wa kuacha Hijabu: "Naam, wanamichezo wa nchi fulani walitoa mwaliko wa kimichezo kwa mmoja wa wanamichezo mashuhuri wa nchi fulani. Kwa bahati nzuri mwanamichezo mualikwa aliukubali mualiko huo na kufanya safari kuelekea huko akifuatana na mkewe ambaye hakuwa amevaa Hijabu, na kwa sura binti huyo alikuwa kaumbika.
Walipofika uwanja wa ndege wa nchi aliyoalikwa mwanamichezo huyu na mkewe, kwa pamoja walilakiwa na wenyeji wao ambao nao ni wanamichezo. Mwanamichezo huyu mgeni alisalimiana na wenyeji wake kisha akamtambulisha mkewe kwa wenyeji hao nao wakampa mikono mkewe huyu, kitendo ambacho Uislamu umekiharamisha. Wanamichezo hawa wenyeji walionyesha furaha kubwa sana na tabasamu kwa mke wa rafiki yao kiasi kwamba mmoja wao alimtamani mke wa mgeni wao na akafikiria lau angemuoa yeye. Isitoshe alifikiria pia njia za kumuwezesha kutimiza azma yake hiyo. Mwisho wa yote alitumia kila ujanja na mbinu za kishetani za kumhadaa bibi yule na akapata fursa ya kukaa naye faragha. Hapo alimuuliza thamani ya mahari aliyopewa alipoolewa na mumewe, na bila kusita mwanamke yule alitaja thamani ile, k.m. dinari alfu moja. Bwana yule aliendelea kusema: 'Mimi nitakupa dinari elfu tatu kwa sababu uzuri wako unastahiki hivyo, siyo thamani aliyokupa mumeo ni ndogo mno na kwa kweli amekudhulumu.' Kisha akamuuliza mumeo ana kazi gani afanyayo zaidi ya michezo? Yule mama akajibu: 'Mume wangu ni karani katika wizara fulani.' Bwana yule aligutuka na kusema 'Aah!!! Hii ni dhuluma kubwa uliyofanyiwa, hivi kweli pamoja na uzuri wote ulionao unakuwa mke wa karani? Haiwezekani kabisa, wewe thamani yako ni kubwa mno. Napenda kukufahamisha kwamba, mimi ni mhandisi na ninayo shahada ya udaktari na nimemaliza Chuo Kikuu, nataka kukuoa lakini kwanza mumeo huyu akuache.' Na mwisho yule bwana alimuhadaa mke wa rafiki yao na wakaafikiana afanye kila hila adai talaka toka kwa mumewe naye atamuowa. Yote haya wakati yanafanyika masikini mume yule hana habari anandelea na michezo.
Ziyara hiyo ilipokwisha bwana yule na mkewe wakarudi nyumbani kwao. Baada ya safari yao bwana huyu akaanza kuona mabadiliko ya tabia ndani ya nyumba yake. Tabia ya mkewe ikawa si nzuri tena, wakati hapo zamani alikuwa akiliona tabasamu la mkewe ambalo lilikuwa likimsahaulisha taabu ya kutwa nzima kazini, leo ni kinyume chake. Baadaye alimuuliza mkewe sababu ya mabadiliko haya. Mke akajibu, 'Wewe umenidanganya.' Mume akasema, 'Nimekudanganya nini?' Mke akasema, 'Umenioa kwa mahari ndogo ambayo mimi sikustahiki, yuko mtu ambaye anaweza kunioa kwa mahari inayonistahiki na sasa nipe talaka yangu.' Mume huyu akili zilimruka baada ya kusikia majibu ya mkewe. Alipigwa na butwaa la majonzi ambalo yeye ndiye aliyeliandaa siku aliposafiri na mkewe asiye na sitara na kumtambulisha kwa watu wasio maharimu wake. Hata hivyo bwana huyu alijaribu kumpa rai mkewe abadili uamuzi wake, lakini jitihada zake zilishindikana na baadaye akamwacha mkewe kwa uchungu mkubwa hali akiwa bado anampenda. Na yule bibi baada tu ya kuachwa, alisafiri hadi kwa yule bwana aliyemuhadaa akiwa na ushahidi wa talaka mkononi ili akatimize lengo lake la kuolewa upya."
Fikiria ewe msomaji, hili ni tukio katika matukio mengi yanayoharibu ndoa za watu. Hebu tafuta sababu yake, hutapata isipokuwa ni kwa sababu bibi yule alikuwa hakusitiriwa Kiislamu, na lau angekuwa kavaa Hijabu inayositiri maungo yake na uzuri wake, je bibi huyu angetumbukia katika mtego huu? Je, mume huyu naye angeingia katika machungu ya kumwacha mkewe hali ya kuwa bado anampenda kutokana tu uovu aliouandaa mwenyewe kwa kumwacha mkewe bila ya kuwa na sitara ya Kiislamu? Lakini taabu hii na machungu haya aliyataka mwenyewe kwa kutomlea mkewe ndani ya malezi ya Kiislamu. Na haya ndiyo malipo ya mtu anayekwenda kinyume na kanuni za Kiislamu na hukmu za Qur-an.
Wakati huo huo tunajiuliza, hivi kweli mke huyu baada ya kuachwa na yule mume wa kwanza, je ndoa ile kwa huyu mume wa pili ilidumu?
Jawabu la swali hili linasema kuwa: "Mara nyingi ndoa za aina hi huwa hazidumu isipokuwa chache tu miongoni mwa hizo, kwa sababu mume wa aina hii huwa hamuowi mwanamke kwa lengo la kujenga maisha ya ndoa kwa maana ya mke na mume, bali huwa anaowa ili tu atosheleze matamanio yake ya kijinsiya na kuyashibisha matamanio yake ya kinyama. Matokeo yake ni kwamba bibi yule aliachwa na kurudi kwenye mji wao hali ya kuwa ni mwenye huzuni na majonzi tele. Alipata hasara ya kumpoteza mumewe wa kwanza ambaye alikuwa akiishi naye kwa kila aina ya mapenzi na huruma.
Ewe msomaji mpendwa, hili ni tukio moja tu kati ya maelfu ya matukio ya hiyana za ndoa za watu. Lakini hebu fanya uchunguzi juu ya sababu zinazosababisha hali hii. Huwezi kupata sababu isipokuwa ni ile tabia ya wanawake kujidhihirisha na kuyaacha wazi maungo yao. Lau mwanamke yule angelikuwa na Hijabu, akausitiri uzuri wake ipasavyo, hivi kweli angenaswa katika mtego huu? Na je, lau yule mume angejikuta ameanguka ndani ya machungu yale ambayo kwa hakika yeye mwenyewe ndiye aliyeyaandaa? Hapana shaka kwamba haya ndiyo malipo ya mtu yeyote anayekwenda kinyume na kanuni za Uislamu na hukmu za Qur'an.