TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Juzuu 12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 813
Pakua: 157


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 813 / Pakua: 157
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Juzuu 12

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea.

Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho : Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

Mwendelezo Wa Sura Ya Kumi na Moja: Surat Hud

وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦﴾

6. Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Na anajua makao yake na mapitio yake yote yamo katika Kitabu kinachobainisha.

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا وَلَئِن قُلْتَ إِنَّكُم مَّبْعُوثُونَ مِن بَعْدِ الْمَوْتِ لَيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿٧﴾

7. Naye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita. Ili awajaribu ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo? Na kama ukisema, hakika nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa, bila shaka waliokufuru watasema, hayakuwa haya ila ni uchawi ulio wazi.

وَلَئِنْ أَخَّرْنَا عَنْهُمُ الْعَذَابَ إِلَىٰ أُمَّةٍ مَّعْدُودَةٍ لَّيَقُولُنَّ مَا يَحْبِسُهُ أَلَا يَوْمَ يَأْتِيهِمْ لَيْسَ مَصْرُوفًا عَنْهُمْ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٨﴾

8. Na kama tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda uliohisabiwa bila shaka watasema, nini kinachozuia hiyo adhabu? Sikilizeni! Siku itakapowajia basi haitaondolewa kwao. Na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

HAKUNA MNYAMA YOYOTE KATIKA ARDHI

Aya 6 – 8

MAANA

Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu.

Neno Daabbah, kilugha lina maana ya kila anayetembea ardhini. Na kidesturi lina maana ya mnyama anayepandwa kama vile punda, farasi n.k.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ardhi na akampa kila anayetembea ardhini mahitaji yake yote, kuanzia mdudu, mbu, ndovu, binadamu n.k. Na akampa kila mmoja uwezo wa kuhangaikia riziki yake.

Kwa hiyo maana ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu amejaalia kwa kila kiumbe hai riziki yake iliyowekwa ardhini. Na wala sio kuwa Mwenyezi Mungu amekadiria riziki mahsus kwa kila kiumbe hai, ambayo haizidi kwa kuihangaikia wala kupungua kwa kuacha kuitafuta, kama wasemavyo wengine! La, Sio hivyo! Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: “Baadhi ya watu na washairi wanadai kuwa kuchumma na kuacha kuchumma ni sawa, kama wanavyosema baaadhi ya wajinga wasiojali:

Mekwishapita kalamu bure sijihangaishe

Kuhangaikia riziki ni sawa na kujikalia

Sijitie na wazimu wala sijishughilishe

Alo tumboni mwa mama riziki hujipatia

Mshairi huyu ndiye anayestahiki kuitwa mwenda wazimu wala sio yule anayeihangaikia riziki yake.

Kwa maelezo zaidi unaweza kurudia Juz.6 (5:64) kifungu cha ‘riziki na ufisadi,’ Juz.7 (5:100) kifingu cha ‘je riziki ni bahati au majaaliwa?’ Juz.8 (7: 56) kifungu cha ‘Mwenyezi mungu ameitengeneza vizuri ardhi na binadamu akaiharibu’

Na anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha.

Makusudio ya mapitio hapa ni alipokuwa kabla ya kuwa katika tumbo la uzazi na kabla ya kutembea ardhini. Na Kitabu kinachobainisha ni fumbo la kwamba Mwenyezi Mungu anajua vizuri kila kitu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayesababisha sababu za kuishi na uhai wa kila mnyama, vyovyote alivyo na atakavyokuwa; Kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu ni muweza na Mjuzi wa kila kitu.

Naye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:54)

Na arshi yake ilikuwa juu ya maji.

Makusudio ya arshi (kiti cha enzi) ni utawala na ufalme. Aya inafahamisha kuwa maji yalikuwa kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi. Ama yalitoka wapi au yalikuwa vipi, hakuna nukuu ya Aya wala Hadith mutawatir juu ya hilo. Akili peke yake haina ujuzi wa hilo.

Hatuna tafsiri yoyote kuhusu mada ya kwanza iliyoumbiwa ulimwengu, isipokuwa neno lake Mwenyezi Mungu. ‘kuwa ukawa’ atakayekanusha haya tutamsomeya:

لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ﴿٦﴾

“Mna dini yenu na mimi nina dini yangu.” (109:6)

Ili awajaribu ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo?

Yaani Mwenyezi Mungu ametuleta sisi katika ardhi na akatupatia nishati zilizomo ndani yake, ili awapambanue wale wanaoishi kwa jasho lao na wanaoishi kwa jasho la wenzao. Atawaadhibu hawa kwa kuasi kwao na kuwapa thawabu wale kwa utiifu wao.

Na kama ukisema, hakika nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa, bila shaka waliokufuru watasema hayakuwa haya ila ni uchawi ulio wazi.

Aya hii ni kama Aya nyingine miongoni mwa Aya nyingi zinazowaelezea wanaokadhibisha ufufuo; isipokuwa ina tofauti moja tu, kwamba hapa kumeelezwa kukadhibisha kwao kwa kufafanisha ufufuo na uchawi, kuwa ni kuwahadaa watu ili wavutike kumfuata Mtume Muhamad(s.a.w.w) .

Na kama tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda uliohisabiwa bila shaka watasema: Nini kinachozuia hiyo adhabu?

Yaani watasema ni kitu gani kinachozuia adhabu isitufikia ikiwa ni kweli?

Sikilizeni! Siku itakapowajia basi haitaondolewa kwao.

Kwa sababu adhabu yake Mwenyezi Mungu haiwezi kuzuiwa na watu wenye makosa.

Na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

Yaani adhabu itawashukia, kuwa ni malipo ya dharau zao na kutohofia kwao ghadhabu za Mwenyezi Mungu.“Dhambi kubwa ni ile aliyoipuuza mwenye dhambi hiyo” kama asemavyo Imam Ali(a.s) .

Na miongoni mwa kauli zake nyingine ni: “Mtu mwenye dhana nzuri zaidi ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemhofia zaidi Mwenyezi Mungu.”

وَلَئِنْ أَذَقْنَا الْإِنسَانَ مِنَّا رَحْمَةً ثُمَّ نَزَعْنَاهَا مِنْهُ إِنَّهُ لَيَئُوسٌ كَفُورٌ ﴿٩﴾

9. Na kama tukimwonjesha mtu rehma inayotoka kwetu, kisha tukamwondolea, hakika yeye hukata tamaa akakufuru.

وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ نَعْمَاءَ بَعْدَ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ ذَهَبَ السَّيِّئَاتُ عَنِّي إِنَّهُ لَفَرِحٌ فَخُورٌ ﴿١٠﴾

10. Na kama tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyompata, bila shaka husema: taabu zimeniondokea. Hakika yeye ndiye mwenye kufurahi sana akijitapa.

إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿١١﴾

11. Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema, hao watapata msamaha na ujira mkubwa.

KUHUSU MTU

Aya 9 – 11

MAANA

Na kama tukimwonjesha mtu rehma inayotoka kwetu, kisha tukamwondolea, hakika yeye hukata tamaa akakufuru.

Makusudio ya kuonjeshwa hapa ni kupewa. Mtu anaporuzukiwa afya njema, mali inayomtosha na familia nzuri, kisha akapatwa na jambo lolote baya, basi hukata tamaa na kuanza kukufuru na kutokuwa na shukrani hata na neema iliyobakia.

Na kama tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyompata, bila shaka husema, taabu zimeniondokea. Hakika yeye ndiye mwenye kufurahi sana akijitapa.

Akitoka kwenye uzito kwenda kwenye wepesi na kutoka kwenye hofu hadi amani, basi huanza kujisahau.

Tumekwishaeleza mara nyingi kwamba Mwenyezi Mungu anategemezewa yeye matukio yote kwa kuwa yeye ndiye sababu ya kwanza ya mambo, kwamba ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Hapana budi kudokeza kwamba Qur’ani inamwangalia mtu kulingana na itikadi yake na tabia yake. Anaamini nini na anafanya nini? Mtazamo huu unalazimiana na tabia ya Qur’ani, kama Kitabu cha dini na mwongozo. Ni kwa msingi huu ndipo anapohukumiwa mtu kuwa ni mwema au mwovu.

Na inajulikana kuwa itikadi ambayo Qur’ani inalingania ni kumwamini Mwenyezi Mungu na Mitume yake na siku ya mwisho, na matendo iliyoamrisha ni yale yaliyomo mema.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ ﴿٧﴾

“Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe.” (98:7).

Kwa maneno mengine ni kuwa Uislamu unamwelekeza mtu kwenye malengo ambayo anapaswa kushikamana nayo. Kama akiyawacha malengo hayo, basi Qur’ani inamwita mtu huyo kwa majina mabaya; kama vile dhalimu, mwenye hasara, kafiri, mjinga, mwenye kupetuka mipaka, mwenye inadi n.k. Kwa hakika sifa hizi hazielezei tabia ya mtu na umbile lake, isipokuwa ni tafsiri ya tabia yake katika baadhi ya misimamo yake.

Qur’ani inatufahamisha kuwa kila sifa iliyotajwa inaambatana na tukio fulani. Imemsifu mtu kuwa ni mwenye kukata tamaa pale anapopatwa na majanga, mwenye furaha akiwa amejitosheleza na mwenye fazaa akipatwa na madhara. n.k.

Watu wengi, hawaijui hakika hii. Wanadhani kuwa sifa hizi zimekuja katika Qur’ani kuelezea umbile la mtu alivyo, na wakawa wanamsifu nazo mtu kinyume na kinavyoeleza Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kama ingelikuwa kweli dhana yao hii, basi isingelifaa Mwenyezi Mungu kumwaadhibu kafiri na aliyepetuka mipaka, kwa sababu ni umbile lake kufanya hivyo. Pia kauli yake:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ ﴿٧٠﴾

“Na hakika tumewatukuza binadamu.” (17:70),

ingelikuwa ni kuutukuza ukafiri na dhulma. Mwenyezi Mungu ametakata na hayo kabisa.

Kwa hiyo basi makusudio ya mtu katika kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kama tukimwonjesha mtu”, ni yule asiyemwamini Mwenyezi Mungu au anayemwamini kinadharia tu, sio kimatendo. Kwa sababu anayemwamini kikweli kweli, humtegemea yeye tu, katika hali zote na anamshukuru wakati wa faraja na wa dhiki. Anamwogopa na kumnyenyekea akiwa tajiri na kuwa na subira akiwa fukara. Kwa sababu imani ni nusu mbili: nusu ya hofu na nusu ya kutarajia.

Linalosisitiza kuwa lengo la mtu hapa ni yule tuliyemtaja, ni kauli yake Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila kuweko na maneno mengine:

Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema, hao watapata msamaha na ujira mkubwa.

Waliofanya subira katika masaibu na madhara kwa kumwamini Mwenyezi Mungu kutumai kupata thawabu na radhi yake na wakatenda mema katika shida na raha. Hiyo ndiyo nembo ya wenye itikadi na msimamo. Kwa sababu itikadi ikituwa kwenye moyo wa mtu, inakuwa kama roho, haimbanduki mpaka kufa.

فَلَعَلَّكَ تَارِكٌ بَعْضَ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ وَضَائِقٌ بِهِ صَدْرُكَ أَن يَقُولُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ أَوْ جَاءَ مَعَهُ مَلَكٌ إِنَّمَا أَنتَ نَذِيرٌ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ ﴿١٢﴾

12. Basi pengine utaacha baadhi ya yale uliyopewa wahyi. Na kifua chako kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema, mbona hakuteremshiwa hazina? au wakaja naye Malaika? Hakika wewe ni muonyaji tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ قُلْ فَأْتُوا بِعَشْرِ سُوَرٍ مِّثْلِهِ مُفْتَرَيَاتٍ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٣﴾

13. Au wanasema ameizua? Sema, basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wa hii na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.

فَإِلَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّمَا أُنزِلَ بِعِلْمِ اللَّـهِ وَأَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَهَلْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٤﴾

14. Na wasipowaitikia, basi jueni ya kwamba imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana Mola isipokuwa Yeye, basi je, nyinyi ni Waislamu?

MBONA HAKUTEREMSHIWA HAZINA

Aya 12 – 14

MAANA

Basi pengine utaacha baadhi ya yale uliyopewa wahyi.

Mtume Muhammad(s.a.w.w) alikuwa akiwasomea washirikina Aya za Qur’anii kwa kuwalingania kwenye imani ya umoja na ufufuo. Mara nyingine wakimkejeli na mara nyingine wakitaka aina ya miujiza kwa kukaidi sio kutaka kuongoka. Hali hiyo ilikuwa ikimuuma Mtume Muhammad(s.a.w.w) na kumhuzunisha, ndipo Mola Mtukufu akamwambia, ili kumwondokea huzuni hiyo.

Endelea na mwito wako wala usijali wayasemayo na wayatakayo. Utawafanya nini hao! Je, uwaache wahyi na ufute kwenye Qur’anii yale yasiyowapendeza? Hapana! Wewe huwezi kufanya hivyo. Kwa hiyo basi kwa nini unahuzunika na kujitia jaka moyo?

Haya ndiyo maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu. ‘Basi pengine uache baadhi ya yale tuliyokupa wahyi.’ Kwa sababu Mtume ni maasum hawezi na haiwezekani kuacha kitu katika wahyi. Aya inafuatana na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu.

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ لَا يَحْزُنكَ الَّذِينَ يُسَارِعُونَ فِي الْكُفْرِ ﴿٤١﴾

“Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wanaofanya haraka kukufuru.” Juz.6 (5:41).

Na kifua chako kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema, mbona hakuteremshiwa hazina au wakaja naye Malaika?

Miongoni mwa mambo waliyoyataka washirikina, kwa Mtume Muhamamad(s.a.w.w) , ni kunyesha mvua ya dhahabu au amjie Malaika ashuhudie utume wake.

Hivi ndivyo wanavyofikiria wenye mali na utajiri tangu zamani na sasa. Wanaamini kwamba cheo ni lazima kiwe kwa wenye mali. Ama mafukara, wao ni wakufuata tu.

Majigambo yao haya yalimsababishia Mtume(s.a.w.w) huzuni, ndipo Mola akamwambia:

Hakika wewe ni muonyaji tu.

Lako ni kufikisha wahyi tu. Usifazahike na upumbavu wa wapumbavu na ujinga wa wajinga.

Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.

Kauli kwake ni yenye kuhifadhiwa na siri inafichika na kila nafsi ni rahani wa ilichokichumma. Aya hii inaambatana na tuliyo yataja Juz. 8 (6:111) kifungu cha ‘aina ya watu’.

Au wanasema ameizuia? Sema, basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wa hii na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.1 (2:23).

Na wasipowaitikia, basi jueni ya kwamba imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana Mola isipokuwa Yeye, basi je, nyinyi ni waislamu?

Wasipowaitikia ni wale wanaoikadhibisha Qur’ani na wasioitikiwa ni Mtume Muhammad(s.a.w.w) na kila mwenye kuulingania Uislam na ‘jueni’ anaambiwa kila mwenye kuikadhibisha Qur’ani wakati wowote na mahali popote alipo.

Maana ni kuwa wajue wanaokadhibisha ambao wameshindwa kuipinga Qur’ani, kwamba hiyo imeteremshwa kwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola isipokuwa yeye.

Hakuna lililobaki isipokuwa musilimu, kwani upinzani umewashinda. Inatosha kusema kuwa Qur’ani ni muujiza kule kuwa imebakia na thamani yake na utukufu wake pamoja na kuwa umepita muda mrefu.

Na itabakia hivyo ikimvutia kila mwenye kuisoma na mawenye kuisikiliza, mpaka siku ya mwisho. Na hilo ni kwa vile hakika yake ni ya kiutu inayokubaklika kwa kila mwenye akili, vyovyote alivyo.

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ ﴿١٥﴾

15. Wanaotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ وَحَبِطَ مَا صَنَعُوا فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٦﴾

16. Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu ispokuwa moto. Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.

أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّهِ وَيَتْلُوهُ شَاهِدٌ مِّنْهُ وَمِن قَبْلِهِ كِتَابُ مُوسَىٰ إِمَامًا وَرَحْمَةً أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ مِنَ الْأَحْزَابِ فَالنَّارُ مَوْعِدُهُ فَلَا تَكُ فِي مِرْيَةٍ مِّنْهُ إِنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٧﴾

17. Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake na anaifuata na shahidi atokaye kwake na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?) Hao wanamwamini yeye. Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake. Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako. Lakini watu wengi hawaamini.

WANAOTAKA MAPAMBO YA DUNIA

YA 15-17

MAANA

Wanotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.

Atakayepanda atavuna, mwenye kufanya biashara vizuri, atapata faida, mwenye kusoma kwa bidii, atafaulu, mwenye kujenga viwanda, kuchimba visima vya mafuta na madini bila shaka hazina yake itajaa mali na kila mwenye kulifanyia bidii jambo lolote, atapata matunda yake, awe mumin au kafiri.

Riziki huja ikiwa ni natija ya kazi; haipunguzwi na ulafi wala kuzidishwa na imani. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.” Hata hivyo ufisadi nao una athari zake; kama tulivyoieleza katika Juz. 6 (5:64).

Neema za maisha ya Akhera zinashikiliwa na kazi ya hapa duniani; sawa na mapambo katika maisha haya. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu na hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾

“Je, mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu haja wajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?” Juz.4 (3:142).

Amesema tena Mwenyezi Mnungu:

وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾

“Na anayeitaka Akhera na akaihangaikia inavyotakikana, naye ni mumin, basi hao mahangaiko yao yatakuwa ni yenye kushukuriwa” (17:19)

Mwenye kuhangaikia riziki yake nzuri ya halali, basi atakuwa amehangaikia dunia na Akhera.

Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu isipokuwa moto.

Hao ni ishara ya wale waliozama katika dunia wakawa hawajishughulishi na lolote isipokuwa dunia tu. Hawatakuwa na malipo yoyote isipokuwa adhabu.

Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.

Humo ni duniani. Maana ni kuwa matendo yao si kitu mbele ya Mwenyezi Mungu; hata kama watu watanufaika nayo, maadamu lengo halikuwa la heri ya kiutu. Kwa ufupi, mwenye kutafuta heri yoyote itamfikisha pale anapopataka; mwenye akili hujichagulia njia ya uokovu bila ya kudanganyika na chochote.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumtaja yule anayejishighulisha na dunia tu, amemtaja anayetenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kumlin- gania yeye tu, akiwa na dalili itokayo kwa Mola wake. Ufafanuzi ni kama ufuatao:

Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake.

Makusudio ya aliye na dalili wazi ni Muhammad(s.a.w.w) na dalili wazi ni Qur’ani.

Na anaifuata na shahidi atokaye kwake.

Tabari, Razi, Abu Hayan Alaandalusi na wengineo katika wafasiri, wamesema kuwa kuna kutofautiana kuhusu shahidi huyu anayemshuhudia Muhammad na utume wake. Wengine wamesema ni Jibril, wengine ni ulimi wa Muhammad na wengine wakasema ni Ali bin Abutwalib.

Waliosema kuwa ni Ali wametoa dalili kwa Hadith aliyoipokea Bukhari katika Sahih yake, inayosema: “Alisema Mtume(s.a.w.w) kumwambia Ali:Wewe ni katika mimi na mimi ni katika wewe.” Na Umar akasema: Mtume(s.a.w.w) alikufa akiwa yuko radhi naye (Ali).

Na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?).

Tawrat ilimbashiria Muhammad na utume wake kabla ya kushuhudiwa na Qur’ani. Tawrat ni Kitab cha Mwenyezi Mungu alichomteremshia Musa na ni kiongozi kinachofuatwa katika mambo ya kidini na rehema kwa anayekitumia kabla ya kupotolewa.

Hao wanamwamini yeye.

Yaani yeye Muhammad(s.a.w.w) na hao ni wale wanaofuata dalili za haki na ubainifu wake; kama vile Qur’ani na Kitabu cha Musa jinsi kilivyoteremshwa. Na hao, wanaoashiriwa, hawakutajwa katika Qur’ani, isipokuwa wametajwa kwa sifa zao.

Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake.

Makusudio ya makundi ni yaliyompiga vita Mtume(s.a.w. w ) . Mwenye Tafsir Al-manar na sheikh Al-maraghi, wamesema: “Amesema Muqatil: Hao ni ni ukoo wa Ummayya, ukoo wa Mughira bin Abdallah Al-makhzumi na jamii ya Twalha bin Abdallah na mfano wao katika Mayahudi na manaswara”

Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako.

Dhamir katika usiwe na shaka naye na hakika yeye, inaweza kuwa ni ya Muhammad au ya Qur’ani na msemo wa usiwe, unaelekezwa kwa kila aliyesikia ujumbe wa Muhammad. Maana ni kuwa haitakikani kwa mwenye akili kutia shaka kuwa Muhammad ni mtume na kwamba Qur’ani ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, baada ya kuweko na dalili zilizowazi juu ya hilo.

Ikiwa mtu anaweza kutia shaka kuwa Tawrat na Injil zimetoa bishara ya utume wa Muhammad, je anaweza kutia shaka kwamba Muhammad amewapatia watu njia za maisha na kwamba yeye ameleta ambayo hakuwahi kuwaletea nabii au kiongozi yeyote.

Lakini watu wengi hawaamini haki, kwa sababu hiyo ni adui wa dhulma yao na ufisadi wao katika nchi au kwa kuwa wao hawatilii umuhimu dini ya haki au batil madamu maisha yao hayategemei dini. Sisi tutaachana nao hawa na yale waliyojichagulia; na wao wawaache wengine na yale waliyojichagulia na wasiingilie dini wasiyoijua isipokuwa jina tu.

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أُولَـٰئِكَ يُعْرَضُونَ عَلَىٰ رَبِّهِمْ وَيَقُولُ الْأَشْهَادُ هَـٰؤُلَاءِ الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَىٰ رَبِّهِمْ أَلَا لَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الظَّالِمِينَ ﴿١٨﴾

18. Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo. Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao. Na watasema mashahidi: Hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.

الَّذِينَ يَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَيَبْغُونَهَا عِوَجًا وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ ﴿١٩﴾

19. Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.

أُولَـٰئِكَ لَمْ يَكُونُوا مُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كَانَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ يُضَاعَفُ لَهُمُ الْعَذَابُ مَا كَانُوا يَسْتَطِيعُونَ السَّمْعَ وَمَا كَانُوا يُبْصِرُونَ ﴿٢٠﴾

20. Hao hawataweza kuponyoka katika nchi na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu maradufu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٢١﴾

21. Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao. Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.

لَا جَرَمَ أَنَّهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْأَخْسَرُونَ ﴿٢٢﴾

22. Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَأَخْبَتُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٣﴾

23. Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kunyenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.

مَثَلُ الْفَرِيقَيْنِ كَالْأَعْمَىٰ وَالْأَصَمِّ وَالْبَصِيرِ وَالسَّمِيعِ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٢٤﴾

24. Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia. Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Je, hamfikiri?

WATAHUDHURISHWA MBELE YA MOLA WAO

Aya 18-24

MAANA

Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo.

Ikiwa kumzulia uongo kiumbe ni kauli mbaya, itakuwaje kwa muumba? Kumzulia uongo Mwenyezi Mungu kuko aina nyingi; kama vile kumfanyia washirika, kuhalalisha na kuharamisha bila ya hoja kutoka Qur’ani au Hadith, wizi na unyang’anyi kwa kisingizio cha demokrasia n.k.

Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao.

Hao ni ishara ya wale wazushi, na kwamba wao kesho watasimama kuhisabiwa; kaulizao na vitendo vyao vitahudhurishwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na watasema mashahidi: hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hahitajii mashahidi, kwa sababu yeye anajua na ni muweza wa kila kitu; anahukumu kwa ujuzi wake na uadilifu wake na kutekeleza kwa neno ‘kuwa.’

Ama ushuhuda wa Malaika na mitume na ushuhuda wa ndimi za waongo waliopotea na mikono yao na miguu yao, lengo lake ni kuzidisha majuto na kwamba wawe na yakini kuwa hawana hoja wala udhuru watakaoukimbilia; hakuna kuepuka laana ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.

Aya hii ni ubainifu na tafsiri ya madhalimu ambao Mwenyezi Mungu amewalaani; kwamba wao wanawazuia watu na tawhid na imani ya ufufuo. Vile vile wanawadanganya kwa shirki na kuikataa siku ya mwisho.

Hao hawataweza kuponyoka katika nchi.

Vipi waweze kufanya hivyo na hali lau Mwenyezi Mungu angelitaka asingeliacha yeyote kwenye ardhi

Na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu.

Hata masanamu waliyokuwa wakiyafanya mungu na kuyaabudu na pia watawa na wakuu wao waliowafanya waungu hawawezi kufaa kitu.

Watazidishiwa adhabu maradufu.

Hili ni jawabu la swali la kukadiriwa; kama kwamba muulizaji ameuliza wale waliozulia Mwenyezi Mungu uwongo wana hukumu gani? Basi Mwenyezi Mungu akajibu, watazidishiwa adhabu mara mbili.

Kuwa maradufu adhabu hapa ni fumbo la ukali wa adhabu. Wengine wamesema maana yake ni kuwa kila kosa lina adhabu yake: Watadhibiwa kwa uzushi na watadhibiwa kwa kuzuia njia na kupinga ufufuo.

Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.

Hii ni sababu ya kufanyiwa adhabu maradufu kwamba Mwenyezi Mungu akiwapa adhabu hii kwa vile walikuwa hawawezi kuisikiliza haki wala kuichunguza, kwa sababu ya kuzama kwao kwenye kufru na inadi.

Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao.

Mwenye hasara zaidi katia watu ni yule aliyejihasiri mwenyewe na adhabu isiyokwisha wala kupunguzwa.

Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.

Ambayo ni kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika na watetezi, kuhalalisha na kuharamisha kwa uwongo na uzushi.

Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa wao wamezitia hasara nafsi zao, amesisitiza kuwa hasara hii itatokea tu, haina kizuizi wala kuikimbia.

Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kun- yenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.

Baada ya Mwenyezi Mungu(s.w.t) kuwataja makafiri, amefuatilia kwa kuwataja wauminii na malipo yao; kama ilivyo desturi ya Qur’ani – kutaja vitu na vinyume vyake.

Neno kunyenyekea hapa limetumika kutokana na neno ‘khibt’ lenye maana ya kunyenyekea na utulivu. Tabrasi anasema: Asili ya neno khibt ni usawa wenye kuenea yaani ardhi iliyo sambamba.

Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia.

Makundi mawili ni makafiri na waumini. Moja halinufaiki na hisia zake, ambapo kipofu hanufaiki na macho yake na kiziwi hanufaiki na masikio yake; na jingine linanufaika na hisia hizo mbili. Imama Ali (a.s.) anasema: “Mwenye kuzingatia huwa na busara na mwenye busara hufahamu na mwenye kufahamu huwa na elimu.” Ni hivyo hivyo mwenye kusikia.

Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Kwa sifa na hali.Je, hamfikiri? Hiyo tofauti?

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ إِنِّي لَكُمْ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٢٥﴾

25. Hakika tulimpeleka Nuh kwa watu wake. Hakika: mimi kwenu ni muonyaji abainishaye.

أَن لَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ أَلِيمٍ ﴿٢٦﴾

26. Ya kwamba msiabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nawahofia na adhabu ya siku iumizayo.

UJUMBE WA NUH

Aya 25-26

MAANA

Aya mbili hizi zinaelezea kwa ufupi kwamba watu wa Nuh walikuwa wakiabudu masanamu. Inasemekana wao ndio wa kwanza kufanya shirki na kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawapelekea mtume awape bishara na maonyo.

Basi Nabii Nuh(a.s) akatekeleza risala yake kwa maneno haya mafupi: Mwabuduni Mwenyezi Mungu peke yake wala msimshirikishe na kitu.

Akadhihirisha hurumma yake kwao kwa kuwahofia kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama wataendelea na shirk. Huu ndio msingi wa kwanza wa risala ya mitume wote.

فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا نَرَاكَ إِلَّا بَشَرًا مِّثْلَنَا وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ وَمَا نَرَىٰ لَكُمْ عَلَيْنَا مِن فَضْلٍ بَلْ نَظُنُّكُمْ كَاذِبِينَ ﴿٢٧﴾

27. Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake: Hatukuoni ila ni mtu sawa na sisi. Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu; bali tunawaona kuwa mu waongo.

قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَآتَانِي رَحْمَةً مِّنْ عِندِهِ فَعُمِّيَتْ عَلَيْكُمْ أَنُلْزِمُكُمُوهَا وَأَنتُمْ لَهَا كَارِهُونَ ﴿٢٨﴾

28. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake, ikafichikana kwenu, Je, tuwalazimishe na hali nyinyi mnaichukia?

وَيَا قَوْمِ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مَالًا إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّهُم مُّلَاقُو رَبِّهِمْ وَلَـٰكِنِّي أَرَاكُمْ قَوْمًا تَجْهَلُونَ ﴿٢٩﴾

29. Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakika wao watakutana na Mola wao. Lakini mimi nawaona nyinyi ni watu wajinga.

وَيَا قَوْمِ مَن يَنصُرُنِي مِنَ اللَّـهِ إِن طَرَدتُّهُمْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٣٠﴾

30. Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza? Basi je, hamfikiri?

وَلَا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ إِنِّي مَلَكٌ وَلَا أَقُولُ لِلَّذِينَ تَزْدَرِي أَعْيُنُكُمْ لَن يُؤْتِيَهُمُ اللَّـهُ خَيْرًا اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا فِي أَنفُسِهِمْ إِنِّي إِذًا لَّمِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٣١﴾

31. Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa mimi ni Malaika. Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao. Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.

NUH NA WATU WAKE

Aya 27-31

MAANA

Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake, hatukuoni ilia ni mtu sawa na sisi.

Nuh alipowalingania watu wake kwenye tawhid walikataa mwito wake, kabla ya kuchunguza uhakika wake. Wakaleta sababu mbili: Ya kwanza, kwamba vipi watamfuata na hali yeye ni mmoja wao? Wao waliangalia msemaji, hawakuangalia yanayosemwa; wakapima haki na watu badala ya kuwapima watu na haki.

Unaweza kuuliza : Hili halihusiki na watu wa Nuh tu, tumewaona watu wengi wamewatukuza wageni kuliko wenyeji; na kuna usemi mashuhuri usemao: ‘msichana wa nyumbani ana sura mbaya,’ sasa kuna ubaya gani?

Jibu : ni kweli kwamba hayo hayahusiki na watu wa Nuh tu na wala Aya haipingi hilo; isipokuwa inawashutumu kwa jambo hilo na hii haiwabakishi watu wengine, wote wanashutumiwa.

Sababu ya pili waliyoisema wapinzaini ni:

Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu.

Yaani walimwambia Nuh na waumini kuwa vipi tuwafuate na nyinyi hamtuzidi na chochote kihali na kimali; sawa na walivyosema washirikina wa kiqurayash kumwambia Muhammad(s.a.w.w) :

لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ ﴿١٢﴾

“Mbona hakuteremshiwa hazina” (11:12).

Na wakasema tena:

لَوْلَا نُزِّلَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ ﴿٣١﴾

“Mbona hii Qur’ani haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili.” (43:31)

Bali tunawaona kuwa mu waongo , kwa vile nyinyi ni mafukara mlio maskini. Haya ndiyo matamshi ya wenye utajiri kung’ang’nia mali tu, lakini maneno ya kheri na matendo mema kwao ni maneno matupu yasiyokuwa na faida.

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake.

Hili ni jawabu la kauli yao, kuwa vipi tukuamini na wewe ni kama sisi. Maana ya jawabu ni kuwa nifanye nini ikiwa Mwenyezi Mungu amenichagua kutekeleza ujumbe wake na amenihusu mimi na rehema yake? Tena akanipa ubainifu kutoka kwake wa risla hii.

Je, nikatae; nimwambie Mwenyezi Mungu sitaki kutumwa na wewe wala sitafikisha ujumbe wako kwa waja wako. Je, yote hayo niyakatae?

Kwa vile nyinyi hamna akili ndioikafichikana kwenu risala na mmeshindwa kuifahamu.

Je, tuwalazimishe? Yaani tuwalazimishe na ujumbe wangu,na hali nyinyi mnaichukia?

Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili la kuwaonya.

Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu mwenye kuzungumzia jina la Mwenyezi Mungu, akiwa ni mkweli katika maneno yake, basi hataki malipo kutoka kwa mwenginewe. Na wanaotafuta riziki kwa jina la dini ndio waombao watu mali na sadaka; na ndio wengi siku hizi.

Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakiaka wao watakutana na Mola wao.

Kwa nini niwafukuze? Kwani ufukara ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu anajua imani yao kwa vile wao wanamwelekea yeye.

Lakini mimi nawaona ni watu wajinga . Na watu ni maadui wa wasichokijua.

Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza?

Je, mnaweza nyinyi au wengine kunikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Basi je, hamfikiri? Vipi atafikiri ambaye haogopi mwisho?

Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa ni Malaika.

Kauli hii ni ya Nuh(a.s) ikiwa ni ufafanuzi na tafsiri ya kauli yake: “Hakika mimi kwenu ni muonyaji abainishaye” Si lazima muonyaji amiliki mali, ili fukara aonekane mwongo; wala si lazima ajue ghaibu, ili aonekane mwongo yule asiyejua ghaibu; wala pia si lazima awe Malaika ili asiyekuwa Malaika ambiwe wewe si lolote isipokuwa ni mtu.

Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao.

Kuna mazoweya ya wenye mali kuona utajiri ndio kipimo cha haki na heri; bali hata wajinga na wapumbavu huona hivyo. Ama mbele ya Mwenyezi Mungu na watu wa Mwenyezi Mungu kipimo ni takua na amali njema na Nuh(a.s) anapima kwa vipimo vya Mwenyezi Mungu. Vipi awaambie waumini kuwa hamtapata heri ya Mwenyezi Mungu; kama walivyoambiwa na mataghut? Ila ikiwa yeye naye ni taghuti kama wao.

Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.

Kama wale waliomshirikisha Mwenyezi Mungu, wakavikataa vitabu vyake na mitume yake.