TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Juzuu 12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 11161
Pakua: 2131


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 11161 / Pakua: 2131
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Juzuu 12

Mwandishi:
Swahili

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَاخْتُلِفَ فِيهِ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ وَإِنَّهُمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ ﴿١١٠﴾

110. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, zikazuka khitilafu ndani yake. Na lau kama si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka ingelihukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka inayowahangaisha.

وَإِنَّ كُلًّا لَّمَّا لَيُوَفِّيَنَّهُمْ رَبُّكَ أَعْمَالَهُمْ إِنَّهُ بِمَا يَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١١١﴾

111. Na hakika Mola wako atawatimizia malipo ya vitendo vyao. Hakika yeye ana khabari za wanayoyatenda.

فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ وَلَا تَطْغَوْا إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿١١٢﴾

112. Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe na yule anayeelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe wala msipetuke mipaka. Hakika yeye anayaona mnayoyafanya.

وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ ﴿١١٣﴾

113. Wala msiwategemee madhalimu, usije ukawagusa moto. Na hamna walinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hamtasaidiwa.

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ ﴿١١٤﴾

114. Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Hiyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.

وَاصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿١١٥﴾

115. Na subiri, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanaofanya wema.

NENO LILILOKWISHATANGULIA

Aya 110- 115

MAANA

Na hakika tulimpa Musa Kitabu, zikazuka khitilafu ndani yake.

Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat. Kaumu ya Musa ilikhitalifiana kuhusiana na Tawrat, wengine waliiamini na wengine wakaikataa. Ndio ilivyo kwa umma wowote, wa zamani na wa sasa, hauafikiani kuhusu mtume wake au kiongozi wake aliyemwaminifu.

Bali wana wa israil waliwaua mitume wao. Hata wale waliomwamini Musa waliigeuza Tawrat baada yake, wakazusha mambo ya upotevu. Kwa hiyo siajabu kwako ewe Muhammad wakikuamini baadhi na wengine wakikukana.

Na lau kama si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka ingelihukumiwa baina yao.

Makusudio ya neno ni kupitisha kuakhirisha adhabu. Baina yao ni wale waliokhitalifiana katika Tawrat. Hekima yake ilitaka wasipate adhabu hapa duniani.

Na hakika wao wamo katika shaka inayowahangaisha.

Bado maneno yako kwa Musa(a.s ) , kaumu na Kitabu chake. Amekuwa mbali yule anayesema kuwa hapa maneno yametoka kwa wana wa Israil hadi kwa Muhammad(s.a.w.w) na Maquraishi.

Kwa ujumla ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameakhirisha adhabu ya waliokadhibisha Tawrat katika kaumu ya Musa, na waliokadhibisha Qur’ani katika kaumu ya Muhammad.

Na hakika Mola wako atawatimizia malipo ya vitendo vyao. Hakika Yeye ana khabari za wanayoyatenda.

Yaani kila muongo na mkweli atapata malipo ya matendo yake kesho yakiwa kamili. Ikiwa ni kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.

MSIMAMO

Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe na yule anayeelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe wala msipetuke mipaka. Hakika yeye anayaona mnayoyafanya.

Maana ya kusimama sawa sawa (msimamo) inatofautiana kulingana na inavyonasibiana. Kwa hiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٦﴾

“Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka” (11:56), ni kuwa Yeye anaongoza kwenye njia hiyo na kuamuru ifuatwe na kwenye msingi wake analipa thawabu na adhabu na kwamba vitendo vyake vyote vinaenda na hekima na maslahi.

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا ﴿١١٥﴾

“ Je, mlidhani kwamba tuliwaumba bure bure…?” (23:115)

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ﴿٢٧﴾

“Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake bure; hiyo ni dhana ya wale waliokufuru.” (38:27).

Na kama ukisifu kusimama sawa kwenye kitu na ukasema kitu hiki kiko sawasawa maana yake umekiweka mahali panapolingana nacho. Ama mtu aliye sawasawa (msimamo) maelezo yake mazuri ni yale aliyoyasema Mwenyezi Mungu:

الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّـهُ وَأُولَـٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٨﴾

“Ambao husikiliza kauli wakafuata zilizo nzuri zaidi. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza na hao ndio wenye akili” (39:18).

Kauli nzuri zaidi kwa Mungu na mwenye kumwamini ni hii Qur’ani:

اللَّـهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُّتَشَابِهًا ﴿٢٣﴾

“Mwenyezi Mungu ameteremsha hadith nzuri kabisa, Kitabu chenye maneno yenye kufanana.” (39:23).

Na kauli nzuri zaidi kwa Mungu na kwa watu wote ni ile inayozipa raha nyoyo za walimwengu sio wezi na wamwaga damu.

Kuna Hadith ya Mtume(s.a.w.w) inayosema: “Sura ya Hud imenizeesha” Inasemekana kuwa alikusudia Aya hii ya Sura ya Hud. Kwa sababu umma wake umeamrishwa kusimama sawa (msimamo) naye hana mategemeo kama watauitikia.

Na sisi tunaona sio mbali kuwa makusudio ya umma ni viongozi wake kwa sababu hao ndio asili ya ugonjwa na chimbuko la balaa. Tumezungumza msimamo katika maelezo ya Bismillah kwenye Juzuu ya kwanza. Itikadi ya Uislamu, sharia yake na maadili yake inakuwa katika neno moja ‘Unyoofu’ (msimamo).

MAJUKUMU YA MSHIKAMANO DHIDI YA DHULMA

Wala msiwategemee madhalimu, usije ukawagusa moto. Na hamna walinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hamtasaidiwa.

Dhulma haihusiki na wanaowafanyia uadui watu na uhuru wao tu, Imeelezwa katika Hadith na Nahju-lbalagha “Dhulma ni tatu: Dhulma isiyosamehewa, dhulma isiyoachwa na dhulma inayosamehewa.

Dhlma isiyosamehewa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu (ushirikina), Dhulma inayosamehewa ni kujidhulumu mja yeye mwenyewe kwa kufanya madhambi madogo; na dhulma isiyoachwa ni ya kudhulumiana waja wenyewe kwa wenyewe.”

Makusudio ya kutegemea madhalimu ni pamoja na kuwanyamazia kwa sababu ni wajibu kukataza maovu. Kuna Hadith isemayo: “Watu wakiona maovu na wasiyakanye, basi wanakurubia nao kuchanganywa kwenye adhabu. Imam Ja’far As-swadiq(a.s ) anasema: “Muumin kumsaidia mumin mwengine ni faradhi ya wajib.” Katika Kitabu Wasail katika mlango Aljihadi anil-ma’sum Imeelezwa: “Mwislamu anapigana kwa ajili ya Uislam au kuhofia miji ya waislamu.”

Kwa kutegemea Hadith hizo na nyenginezo, mafaqih wamegawanya jihadi kwenye aina mbili:

1. Jihadi ya kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuueneza Uislam.

2. Kuulinda Uislamu na miji ya Waislamu, bali ni kuitetea haki yoyote ni sawa iwe yake au ya mtu mwengine.

Mwenye Al-Jawahir amesema: “Akishambulia adui, anayehofiwa, himaya ya waislamu au kafiri akitaka kuteka miji ya waislamu, kuwachukua mateka na kupora mali zao, ikitokea hivyo, basi ni wajibu kuutetea kwa kila mtu: muungwana, mtumwa, mwanamume, mwanamke, mwenye afya, mgonjwa, kipofu, kilema na wengineo wakihitajika. Na wajibu wenyewe haungoje kuwepo Imam au idhini yake. Vile vile wajibu huo hahusiki na walioshambuliwa na kulengwa tu, bali ni wajibu kwa kila atakayejua hata kama siye aliyelengwa, ikiwa hajui kuwa walioshambuliwa wanamuweza adui yao. Na wajibu unasisitizwa kwa aliyekaribu na aliye karibu zaidi.”

Kisha akaendelea kusema mwenye A-Jjawahir “Kujitetea mtu ni wajib hata kama hadhanii usalama wake, kwa sababu tayari yuko hatarini kwa namna yoyote. Ama kupigania heshima yake na mali yake ni wajibu ikiwa anaona hakuna hatari ya nafsi yake, kwa kuhofia isiende nafsi, mali na heshima pamoja. Vile vile kutetea maisha ya mtu mwingine, mali yake au heshima yake.”

Mafaqihi wametoa fat-wa ya wajibu wa kumwokoa mwenye kuangamia na kuzima moto ikiwa unaangamiza mali ya mtu mwingine. Na kwamba ni wajibu kwa mwenye kuswali kukata swala yake ili kuzuia hatari ya nafsi yoyote muhimu au mali ambayo ana wajib kwake kuihifadhi; iwe ni yake au ya mtu mwingine. Na atakayemuona mtoto jangwani ni wajib kumwokota na kumuhifadhi ikiwa hawezi kujilinda.

Imepokewa riwaya kwamba watuhumiwa watatu, waliomuua mtu, waliletwa kwa Imam Ali(a.s) . Mmoja alimshika yule aliyeuliwa, wapili akaua na watatu akaangalia bila ya kufanya lolote. Yule aliyeua akamhukumu kuuliwa na aliyeshika, afungwe maisha na aliyeangalia, ang’olewe macho. Mafakihi wameitumia riwaya hii.

Mwenye kufuatilia utafiti wa vitabu vingi vya Fiqh ataona aina hii ya maelezo; nayo ni dalili mkataa kwamba mtu kumsaidia na kumwokoa mtu mwingine ni wajibu wa kisharia ikiwa ni umuhimu kufanya hivyo.

Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana.

Ncha ya kwanza ya mchana ni wakati wa swala ya asubuhi, ncha ya pili ni adhuhuri na alasiri, na usiku uliokaribu na mchana ni maghribi na isha. Aya nyingine inasema:

أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨﴾

“Simamisha swala jua linapopinduka mpaka giza la usiku na Qur’ani ya alfajiri. Hakika Qur’ani ya alfajiri ni yenye kushuhudiwa.” (17:78).

Kupinduka jua ni wakati wa swala ya adhuhuri na alasiri na giza la usiku ni wakati wa swala ya maghrib na isha na Qur’ani ya alfajiri ni swala ya asubuhi ambayo watu wanaishuhudia. Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqh, ikiwemo Juzuu ya kwanza ya Fiqhul-Imam Jaffer As-swadiq.

Hakika mema huondoa maovu.

Mwenye Majmaulbayan, akiwanukuu wafasiri wengi, anasema kuwa makusudio ya mema hapa ni swala tano na kwamba hizo zinafuta madhambi yaliyo baina yao. Wengine wakasema ni kule kusema tu: “Subhanallah walhamdulillah walailahaillaha illallah wallahu akbar”

Tafsiri zote zinakataliwa na akili. Kwani hakuna mahusiano yoyote baina yake si ya kihukumu wala sharia au akili. Vile vile si kikanuni wala kidesturi. Hukumu yoyote ya wajibu au haramu haiifungi hukumu nyingine. Ama hadith inayosema: “Kila anaposwali hufutiwa madhambi yaliyo baina ya swala mbili ni fumbo la kwamba swala ina mema mengi.

Ikiwa mwenye kuswali ana maovu huwekwa kwenye kiganja na yale mengine kwenye kiganja, hapo mazuri huondoa mabaya. Kwa sharti yasiwe makubwa wala yasiwe ni haki miongoni mwa haki za watu. Maelezo ya maudhui haya yamekwishatangulia katika Juz. 2 (2:217).

Hiyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.

Hiyo ni ishara ya amri ya kusimama sawa sawa (msimamo), kusimamisha swala na kukatazwa kuwategemea madhalimu. Makusudio ya wenye kukumbuka ni wenye kuwaidhika.

Na subiri, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanaofanya wema.

Hapo kuna ishara kwamba mwenye kufuata njia ya sawa sawa atapambana na wapotevu wenye kupotoka na kwamba subra (uvumilivu) katika jihadi yao ndio twaa bora na wema mkuu.

فَلَوْلَا كَانَ مِنَ الْقُرُونِ مِن قَبْلِكُمْ أُولُو بَقِيَّةٍ يَنْهَوْنَ عَنِ الْفَسَادِ فِي الْأَرْضِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّنْ أَنجَيْنَا مِنْهُمْ وَاتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا مَا أُتْرِفُوا فِيهِ وَكَانُوا مُجْرِمِينَ ﴿١١٦﴾

116. Basi mbona hawakuwamo katika watu wa karne ya kabla yenu wenye akili wakakataza ufisadi katika nchi? Na wakafuata wale waliodhulumu waliyostareheshewa na wakawa ni wakosefu.

وَمَا كَانَ رَبُّكَ لِيُهْلِكَ الْقُرَىٰ بِظُلْمٍ وَأَهْلُهَا مُصْلِحُونَ ﴿١١٧﴾

117. Na hakuwa Mola wako wa kuiangamiza miji kwa dhulma na hali watu wake ni watenda mema.

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَا يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ ﴿١١٨﴾

118. Na lau Mola wako angelitaka angeliwafanya watu wote kuwa umma mmoja. Na hawaachi kukhitalifiana.

إِلَّا مَن رَّحِمَ رَبُّكَ وَلِذَٰلِكَ خَلَقَهُمْ وَتَمَّتْ كَلِمَةُ رَبِّكَ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴿١١٩﴾

119. Ispokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu. Na kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako: kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa majini na watu kwa pamoja.

WATU WA KARNE ZILIZOTANGULIA

Aya 116-119

MAANA

Basi mbona hawakuwamo katika watu wa karne ya kabla yenu wenye akili wakakataza ufisadi katika nchi?

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja maangamizi yaliyowapitia kaumu ya Nuh, ya A’d, ya Thamud na wengineo kwa sababu ya jeuri na ufisadi wao, anasema hivi hawakupatikana watu na viongozi wema kuweza kuzuia dhulama na ufisadi.

Kwa sababu ya dhulma hiyo na ufisadi na wengine wakayanyamazia, basi walistahiki adhabu na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu wote;

Isipokuwa wachache tu, tuliowaokoa miongoni mwao.

Ambao ni mitume na wale walioamini pamoja nao. Yaani kikundi kidogo alichokiokoa Mwenyezi Mungu kilikuwa kikiamrisha mema na kukataza maovu, lakini hakuna amri kwa asiyetiiwa.

Na wale waliodhulumu waliyostareheshewa na wakawa ni wakosefu wakafuata.

Makusudio ya waliyostreheshewa ni mali zao. Wale wachache waliwakataza wengine ufisadi na dhulma, lakini kwa sababu ya mali zao hawakujali kabisa. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٣٤﴾ وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴿٣٥﴾

“Na hatukutumma mwonyaji yoyote kwenye mji, ila husema wenyeji wake waliostareheshwa: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo. Na wakasema sisi tuna mali nyingi zaidi na watoto, wala sisi hatutadhibiwa.” (34:34-35)

Na hakuwa Mola wako wa kuiangamiza miji kwa dhulma na hali watu wake ni watenda mema.

Vinginevyo angelikuwa sawa kwake, mwema na muovu na mzuri na mbaya. Haiwi hivyo kwa Mwnyezi Mungu:

مَّا يَفْعَلُ اللَّـهُ بِعَذَابِكُمْ إِن شَكَرْتُمْ وَآمَنتُمْ وَكَانَ اللَّـهُ شَاكِرًا عَلِيمًا ﴿١٤٧﴾

“Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye (kupokea) shukrani Mjuzi. Juz. 5 (4:147).

Na lau Mola wako angelitaka angeliwafanya watu wote kuwa umma mmoja.

Tangu iliposhuka Aya hii mpaka leo,watu wengi wanasema : Kwanini hakutaka Mwenyezi Mungu. Laiti Mwenyezi Mungu angelifanya hivyo miji ikawa na raha na kuepukana na balaa hili la kubaguana.

Jibu linafafanuka kwa namna ifuatayo:

1. Kabla ya kitu chochote inatakikana tuwe na yakini kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hataki waja wake wachukiane, wabughudhiane au wachinjane. Kwanini isiwe hivyo na hali yeye ndiye mwenye kusema:

وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا ﴿٤٦﴾

“Wala msizozane, msije mkafunjika moyo.” (8:46).

Haina maana kuwa kwa vile hakuwalazimisha mshikamano na maafikiano, basi anawataka wazozane na wapigane. Kwa mfano ukisema: Sitaki wanangu wawe na rai moja katika siasa. Haina maana kwamba unataka wapigane na wauane.

2. Kulazimisha kwenye dini kuna njia mbili: Kwanza, ni kutumia nguvu. Pili, ni kuumba Mwenyezi Mungu imani katika moyo wa mtu, kama alivyomba ulimi katika mdomo.

Njia ya kwanza inapingana na misingi ya dini na ya mantiki pia. Kwa sababu nguvu haitengenezi imani; bali ni kinyume. Kwa vile njia ya imani ya haki ni dalili. Ndio maana Qur’ani ikazionyesha dalili hizi kwa mifumo mbalimbali. Na ikamuhimiza mtu kuzichunguza, kuziangalia vizuri na kuzizingatia. Ni hiyari yake sasa kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Ama amri ya kupigana ni kwa ajili yakuitetea sharia ya haki na uadilifu na kuchunga usalama na amani kwa jamii.

Na njia ya pili, ya kuumba imani moyoni, itamatoa mtu kwenye utu wake, awe sawa na matunda yaliyo mtini, hana matakwa wala fikra juu ya muumbaji na hatastahiki kusifiwa wala kulaumiwa au kuwa na thawabu au adhabu. Yametangulia maelezo katika kufasiri Juz. 7 (6:35).

Kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutaka kwa namna yoyote ile kuwatumilia watu nguvu katika imani. Kwa sababu lau angelifanya hivyo angaliwaondolea sifa ya ubinadamu; wangelikuwa kama wanyama na wadudu, hawana majukumu yoyote wala hawahisabiwi chochote. Lakini Mwenyezi Mungu alitaka amtofautishe binadamu na viumbe vyote na afikie hali ambayo hakutakua na chochote juu yake isipokuwa Muumbaji tu.

Itakuwa Muhali kufikia cheo hiki bila ya juhudi na khiyari. Ndio maana Mwenyezi Mungu, amempa uwezo, utambuzi wa mambo, mhemuko na kumwonyesha njia mbili, kisha akamwachia uhuru wa hiyari, ili abebe mwenyewe lile atakalojichagulia.

Na hilo litamkamilishia ubinadamu wake kamili. Matokeo ya hayo sasa ni kutofautiana watu rai zao na itikadi zao. Angalia Juz. 2 (2:213) na Juz. 5 (4:78).

Na hawaachi kukhitalifiana.

Yaani watu waliopita walikhitalifiana na wataeendelea kukhitalifiana milele. Kwa vile hiyo ni natija ya kumfanya binadamu awe ni mwenye khiyari akielekea popote apendapo.

Ispokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu.

Makusudio ya waliorehemiwa ni wale walioshikamana kiuhakika na kiikhlasi, hawavurugani. Ikitokea kutofautiana basi ni katika rai na mitazamo. “Kutofautiana rai hakuharibu mapenzi.” Na kuweko mitazamo tofauti kunaleta faida. Kwa sababu kauli yenye nguvu ni ile ambayo inakuwa na nguvu hata kama kuna kauli nyinginezo.

Na kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaumba.

Yaani Mwenyezi Mungu amewaumba kwa hiyo rehema na kwa kuhurumiana wao kwa wao. Itawapa rehema yake Mwenyezi Mungu mtukufu, ikiwa wataitafuta haki na kuitumia.

Abu Bakr almua’firiy Al-andalusi (Mhispania) anasema katika Kitabu Ahkamul Qur’ani: “Hakika Mwenyezi Mungu amewaumba watu ili watofautiane sio wahurumiane.”

Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu anataka shari, kufru na maasi. Ikiwa Mwenyezi Mungu anataka shari basi kuna tofauti gani na Iblis aliyesema “Nitawapoteza wote”? Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu Juz. 7 (6:100).

Na litatimia neno la Mola wako: kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa majini na watu kwa pamoja.

Yaani Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ataijaza Jahannam waasi wafuasi wa shetani miongoni mwa majini na watu. Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema:

قَالَ فَالْحَقُّ وَالْحَقَّ أَقُولُ ﴿٨٤﴾ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكَ وَمِمَّن تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٨٥﴾

“Akasema: Haki na haki ninaisema. Hakika nitaijaza Jahannam kwa wewe na kwa wale wote wenye kukufuata miongoni mwao.” (38:84-85).

وَكُلًّا نَّقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَاءِ الرُّسُلِ مَا نُثَبِّتُ بِهِ فُؤَادَكَ وَجَاءَكَ فِي هَـٰذِهِ الْحَقُّ وَمَوْعِظَةٌ وَذِكْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿١٢٠﴾

120. Na yote tunayokusimulia katika habari za mitume ni ya kuufanya thabiti moyo wako. Na katika hii imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa wenye kuamini.

وَقُل لِّلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنَّا عَامِلُونَ ﴿١٢١﴾

121. Na waambie wale wasioamini: Fanyeni muwezavyo, nasi (pia) tunafanya.

وَانتَظِرُوا إِنَّا مُنتَظِرُونَ ﴿١٢٢﴾

122. Na ngojeni, hakika sisi tunangoja.

وَلِلَّـهِ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَيْهِ يُرْجَعُ الْأَمْرُ كُلُّهُ فَاعْبُدْهُ وَتَوَكَّلْ عَلَيْهِ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿١٢٣﴾

123. Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyofichikana katika ardhi na mbingu. Na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu yeye na umtegemee yeye Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.

TUNAYOKUSIMULIA

Aya 120-123

MAANA

Na yote tunayokusimulia katika habari za mitume ni ya kuufanya thabiti moyo wako. Na katika hii imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa wenye kuamini.

Hii ni ishara ya sura, ukumbusho ni mazingatio na makusudio ya kuufanya thabiti moyo wa Mtume(s.a.w.w) ni subra na uvumilivu wa maudhi katika njia ya ujumbe wake na kuufikisha. Maana ni kuwa habari za mitume na watu wao tulizokusimulia ni haki hazina shaka na kwamba lengo lake ni kukupunguzia adha inayokupata.

Kwani anayeona masaibu ya mwingine, yake huyaona madogo. Vile vile katika visa hivi kuna mawaidha na mazingatio kwa mwenye kuwaidhika na kuzingatia.

Kwa hakika wanahistoria wa zamani walikuwa wakitilia umuhimu matukio ya siasa na dola na wapya wakatilia umuhimu uchumi, sayansi, sanaa, fasihi na mengineyo katika harakati za binadamu.

Lakini Qur’ani inaleta matukio kuwa ni mazingatio na mawaidha yatakayomwongoza binadamu kwenye njia iliyo sawa. Kauli yake Mwenyezi MunguMtukufu: “N mawaidha na ukumbusho” inaeleza hivyo. Aya nyingine inasema:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِّمَن يَخْشَىٰ ﴿٢٦﴾

“Hakika katika hayo mna mazingatio kwa anayemcha (Mwenyezi Mungu)” (79:26).

Na waambie wale wasioamini: Fanyeni muwezavyo, nasi (pia) tunafanya.

Umepita mfano wake katika Juz. 8 (6:135).

Na ngojeni, hakika sisi tunangoja.

Vile vile mfano wake umepita katika (6: 158).

Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyofichikana katika ardhi na mbingu.

Kila siri kwake iko wazi na kila lililofichikana linaonekana. Katika mfano wa hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye; anajua kilichomo nchi kavu na kilichomo baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitabu kinachobainisha.” Juz.7 (6:59).

Na mambo yote yatarejeshwa kwake.

Wala hakuna kitu kinachokimbia ufalme wake.

Basi muabudu yeye na umtegemee yeye.

Yaani ikiwa Mwenyezi Mungu yuko hivi, basi yeye ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa na kutegemewa si mwengine. Amri ya kurukui na kusu- judi ni nyepesi, lakini kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuachana na wengine, asiyekuwa Yeye ni jambo zito, isipokuwa kwa wanaomcha Mwenyezi Mungu.

Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.

Atawalipa wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyafanya na atawalipa mema wale waliofanya mema. Imesemwa kwenye Nahjul balagha: “Usighafilike kwani wewe hujasahauliwa… Ee! Kuangamia kwa mwenye kughafilika kuwa umri wake ni hoja juu yake.” Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuhifadhi na yale yanayoleta majuto na majonzi.

MWISHO WA SURA YA KUMI NA MOJA: SURAT HUD