TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU Juzuu 13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 12874
Pakua: 2100


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 17 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12874 / Pakua: 2100
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU Juzuu 13

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَيْهِ قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ مَسَّنَا وَأَهْلَنَا الضُّرُّ وَجِئْنَا بِبِضَاعَةٍ مُّزْجَاةٍ فَأَوْفِ لَنَا الْكَيْلَ وَتَصَدَّقْ عَلَيْنَا إِنَّ اللَّـهَ يَجْزِي الْمُتَصَدِّقِينَ ﴿٨٨﴾

88. Basi walipoingia kwa Yusuf walisema: “Ewe mheshimiwa! Imetupata shida sisi na watu wetu na tumeleta mali kidogo, basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka; hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka.”

قَالَ هَلْ عَلِمْتُم مَّا فَعَلْتُم بِيُوسُفَ وَأَخِيهِ إِذْ أَنتُمْ جَاهِلُونَ ﴿٨٩﴾

89. Akasema: “Je, mnajua mlivyomfanyia Yusuf na ndugu yake mlipokuwa wajinga?”

قَالُوا أَإِنَّكَ لَأَنتَ يُوسُفُ قَالَ أَنَا يُوسُفُ وَهَـٰذَا أَخِي قَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا إِنَّهُ مَن يَتَّقِ وَيَصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٩٠﴾

90. Wakasema: “Je, wewe ni Yusuf?” Akasema: “Mimi ni Yusuf na huyu ni ndugu yangu! Mwenyezi Mungu ametuneemesha, Hakika mwenye takua na akasubiri basi Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wafanyao mema.

قَالُوا تَاللَّـهِ لَقَدْ آثَرَكَ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَإِن كُنَّا لَخَاطِئِينَ ﴿٩١﴾

91. Wakasema: “Wallah! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha kuliko sisi na hakika sisi tumekuwa ni wenye hatia.

قَالَ لَا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ يَغْفِرُ اللَّـهُ لَكُمْ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٩٢﴾

92. Leo hapana lawama juu yenu, Mwenyezi Mungu atawasamehe naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wenye kurehemu.”

اذْهَبُوا بِقَمِيصِي هَـٰذَا فَأَلْقُوهُ عَلَىٰ وَجْهِ أَبِي يَأْتِ بَصِيرًا وَأْتُونِي بِأَهْلِكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٣﴾

93. Nendeni na kanzu yangu hii na muirushe usoni mwa baba yangu atakuwa ni mwenye kuona, na mje nao watu wenu wote wa nyumbani.

MIMI NI YUSUF

Aya 88 – 93

MAANA

Basi walipoingia kwa Yusuf walisema: Ewe mheshimiwa! Imetupata shida sisi na watu wetu na tumeleta mali kidogo, basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka, Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka.

Yaa’qub aliwausia wanawe warudi Misr, wakakubali na wakarudi mara ya tatu, wakaingia kwa mheshimiwa wakiwa hoi, wakiomba wahurumiwe na wakaanza kulalamika njaa: tumepatwa na shida pamoja na watu wetu, tupe sadaka, mali yetu ni kidogo, Mungu anawapenda wanaotoa sadaka, Zama huwa zinageuka. Walisema haya wakiwa ni wajukuu wa Ibrahim(a.s) lakini shida imewazidia mambo yakawa kwa namna ambayo hawakutegemea.

Akasema: Je, mnajua mlivyomfanyia Yusuf na ndugu yake mlipokuwa wajinga?

Baada ya Yusuf kusikia malalamiko ya ndugu zake na kusikia shida ya watu wake alishikwa na huruma za udugu, akawaambia kuwalaumu au kuwapa mawaidha kuwa mnakumbuka mlipomwitikia shetani mkamtupa ndugu yenu Yusuf kisimani. Baadae mkamsumbua sana mdogo wake Bin-yamin. Juzijuzi tu mlisema kuwa kama ameiba basi nduguye pia aliiba huko nyuma? Je, mjinga anaweza kufanya zaidi ya mlivyofanya?

Wakasema: Je, wewe ni Yusuf?

Wafasiri hapa wana maneno yasiyoafikiana na Aya, lakini yanaafikiana na maudhui na yanasaidia kuzingatia. Kwa ufupi ni haya: Nduguze Yusuf waliposikia maneno ya Yusuf, walianza kukumbuka umbile la Yusuf, uso wake, sauti yake na ishara za mikono yake.

Kwa vyovyote iwavyo wao au baadhi yao walianza kufikiria kuwa huyo ni Yusuf ndipo wakaanza kusema Je, wewe ni Yusuf? Walisema hivi wakiwa wanangoja jawabu, Basi likawa jawabu ambalo hawakulitegemea:

Akasema: Mimi ni Yusuf na huyu ni ndugu yangu, Mwenyezi Mungu ametuneemesha.

Namtaka msomaji asimame hapa kidogo alinganishe walikuwaje walipoambiwa hayo kulinganisha na walivyokuwa siku walipomtupa kisi- mani wakiwa hawana dini wala huruma ya udugu?!

Hakika mwenye takua na akasubiri basi Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wafanyao mema duniani na Akhera.

Makusudio ya wafanyao mema ni wale waliofanya na wakavumilia na kuwa na subira kwenye misukosuko waliyoipata na wakawa mara kwa mara wanazidiwa na waovu, lakini mwisho ni wa wacha Mungu. Ushahidi wa hilo hauanzii kwenye zama za Namrud na kuishia kwa Hitlar tu.

Binadamu leo anakabiliwa na mitihani ya Uzayuni na ukoloni wa Amerika ambao ndio washari wakuu na wafisadi. Hatuna shaka kwamba mwisho wa wote hao utakuwa kama mwisho wa mataghuti waliotangulia.

Hatusemi hivi kwa ushabiki, isipokuwa hiyo ni hali halisi ya kihistoria. Haki ina wenyewe wanaoitafuta na kujitolea mhanga na kwamba heri ina nguvu inayoisaidia, na iko siku itashinda dhidi ya dhulma na utaghuti.

Wakasema: Wallah! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha kuliko sisi na hakika sisi tumekuwa wenye hatia.

Walikiri kuwa Mwenyezi Mungu amemfadhilisha kuliko wao kimali, elimu, akili, uzuri na hatimae kwa cheo na heshima. Wakakiri makosa na kuomba msamaha. Yusuf mkarimu na mwana wa mkarimu alisema:

Leo hapana lawama juu yenu, Mwenyezi Mungu atawasamehe

Yusuf alisamehe yaliyopita bila ya nguvu wala lawama na akawaombea Mungu awasamehe waliyoyakosea naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wenye kurehemu, kwa yule anayetubia na akarudi nyuma. Katika Nahjul balagha imesemwa:“Hasira hazimfanyi kuacha huruma wala huruma hamufanyi kuacha kuadhibu”.

Kuna hadith Mutawatir kutoka kwa Mtume kwamba alipopata ushindi wa kuiteka Makka aliwaambia makuraish: “Je, mnadhani nitawafanya nini?” Wakasema: “Sisi tunadhania heri tu, ndugu mkarimu na mwana wa ndugu mkarimu.” Akasema: “Basi nendeni zenu nimewaachia huru, leo hapana lawama juu yenu; kama alivyosema ndugu yangu Yusuf.”

Nendeni na kanzu yangu hii na muirushe usoni mwa baba yangu atakuwa ni mwenye kuona na mje nao watu wenu wote wa nyumbani.

Hebu turudi nyuma kwenye Aya 18 ya Sura hii iliyoko Juz, 12, ili tulinganishe kati ya kanzu ya kwanza na hii ya pili: Ya kwanza ilimletea Ya’qub balaa na ugonjwa. Ya pili ikamletea raha na dawa. Vile vile tulinganishe baina ya hali ya wanawe walipoleta ya kwanza walijiomboleza na walipoleta ya pili walikuwa na furaha.

Kama mtu atauliza: iweje kanzu irushwe usoni na kuponyesha? Tutajibu kuwa hatupati tafsiri nyingine isipokuwa muujiza; sawa na moto wa Ibrahim, fimbo ya Musa na kuzungumza kwa Isa akiwa mchanga.

وَلَمَّا فَصَلَتِ الْعِيرُ قَالَ أَبُوهُمْ إِنِّي لَأَجِدُ رِيحَ يُوسُفَ لَوْلَا أَن تُفَنِّدُونِ ﴿٩٤﴾

94. Na ulipoondoka msafara, baba yao alisema: “Hakika mimi ninasikia harufu ya Yusuf, lau kama hamtanipuuza.”

قَالُوا تَاللَّـهِ إِنَّكَ لَفِي ضَلَالِكَ الْقَدِيمِ ﴿٩٥﴾

95. Wakasema: Wallah hakika wewe bado uko katika upotevu wako wa zamani.

فَلَمَّا أَن جَاءَ الْبَشِيرُ أَلْقَاهُ عَلَىٰ وَجْهِهِ فَارْتَدَّ بَصِيرًا قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ إِنِّي أَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٩٦﴾

96. Alipomfikia mbashiri aliirusha kanzu usoni pake akarejea kuona, Akasema: Je, sikuwaambia kuwa mimi ninajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua?

قَالُوا يَا أَبَانَا اسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا إِنَّا كُنَّا خَاطِئِينَ ﴿٩٧﴾

97. Wakasema: “Ewe baba yetu! Tuombee maghufira kwa dhambi zetu, hakika sisi tulikuwa ni wenye hatia.

قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّي إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٩٨﴾

98. Akasema: Nitawaombea msamaha kwa Mola wangu. Hakika yeye ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.

NASIKIA HARUFU YA YUSUFU

Aya 94-98

MAANA

Na ulipoondoka msafara, baba yao alisema: Hakika mimi ninasikia harufu ya Yusuf, lau kama hamtanipuuza.

Kuondoka msafara ni kuondoka pale ulipokuwa, ambapo ni Misr na kuelekea nchi ya Kanani alipokuwa akikaa Ya’qub. Kupuuza ni kumtuhumu na upotofu.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Ya’qub alinusa harufu ya kanzu ya Yusuf kwa mbali mara tu msafara ulipoanza kuondoka, kabla ya kumaliza nchi ya Misr; ingawaje masafa yalikuwa marefu.

Aliyechukua kanzu ya Yusuf alikuwa masafa ya mwendo wa siku nane, na imesemekana ni siku kumi. Wafasiri wamelibakisha neno na dhahiri yake, wakasema kuwa Ya’qub alipata harufu ya Yusuf hasa pamoja na umbali wa masafa na wakazingatia huo ni muujiza aliomuhusisha nao Mwenyezi Mungu Ya’qub.

Sio mbali kuwa harufu ya Yusuf ni fumbo la makisio ya kutokata tamaa amabayo, huwapata baadhi ya watu; hasa wale wenye nyoyo safi. Na kwamba moyo wa Ya’qub ulihisi kukurubiana kukutana na Yusuf, kwa hiyo akalifasiri hilo kwa harufu.

Maana hayo yanatiwa nguvu na kwama Ya’qub hakukata tamaa ya kukutana na Yusuf hata mara moja. Hilo linatolewa ushahidi na kauli zake katika Sura hii; kama ifuatavyo:

Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye wala msikate tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu, Aya 87 Huenda Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Aya 83 Ewe mwanangu! Usiwasimulie ndugu zako ndoto yako wasije wakakufanyia vitimbi, Aya 5, Juz.12 “Na kadhalika Mola wako atakuteua na atakufundisha tafsiri ya mambo na atatimiza neema yake juu yako, Aya 6, Juz.12 “Mimi ninajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua Aya 96.

Wakasema: Wallah hakika wewe bado uko katika upotevu wako wa zamani.

Waliosema ni wale waliokuwepo alipokaa Ya’qub aliposema nasikia harufu ya Ya’qub. Maana ni kuwa waliokuwepo walimwambia Ya’qub kuwa wewe unakosea katika kung’ang’ania kwako kumngoja Yusuf ambaye amekwishakwenda, kama walivyokwenda wengine waliokufa.

Alipomfikia mbashiri aliitupa kanzu usoni pake akarejea kuona.

Ya’qub hakukosea katika hisia zake, Mbashiri (Mwenye kuleta habari njema) alimjia akiwa amechukua kanzu ya Yusuf; mara tu, ile kanzu ilipogusa uso wa Ya’qub, neema ya kuona ikarudi na furaha ya maisha. Inasemekana kuwa aliyechukua kanzu ya Yusuf ni yule yule aliyechukua kanzu iliyotapakazwa damu ya uwongo, miaka arubaini iliyopita, ili afute uovu kwa wema. Vile vile inasemekana kuwa hakuna ajabu ya Ya’qub kurudiwa na macho kwa furaha, kwani mara nyingi raha na furaha huponyesha magonjwa. Majaribio ya tiba yanathibitisha hilo.

Akasema: Je, sikuwaambia kuwa mimi ninajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua?

Hii inaashiria kauli yake katika Aya 86 ya Sura hii: “Akasema: Majonzi yangu na huzuni yangu ninamshtakia Mwenyezi Mungu Na ninajua kwa Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua”

Wakasema: “Ewe baba yetu tuombee maghufira kwa dhambi zetu, hakika sisi tulikuwa wenye hatia.”

Ndugu zake Yusuf walijuta kwa kitendo chao, wakatubia makosa yao, na wakamuomba baba yao awaombee kwa Mwenyezi Mungu kuwatakabalia toba yao na awaghufurie dhambi zao na wakajiwekea sharti la kutorudia maasi.

Akasema: Nitawaombea msamaha kwa Mola wangu. Hakika yeye ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.

Mmojawapo wa wafasiri wa kisasa anasema: “neno ‘nita’ haliepuki kuwa kwenye moyo wa mtu aliyejeruhiwa” anamaanisha kuwa moyo wa Ya’qub bado una kitu kwa watoto wake, pamoja na toba yao na kuomba kwao masamaha.

Lakini huku ni kutatizika na kufanya makisio kwa nyoyo za mitume na za watu wengine. Ilivyo hasa ni kuwa Ya’qub, aliahirisha kuwaombea dua mpaka awe faragha katika mkesha wenye giza aweze kumwomba Mola wake awatakabalie toba. Kwa sababu hilo linapelekea kukubaliwa dua. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ ﴿١٨﴾

Na wanaomba msamaha nyakati za kabla ya Alfajiri (51:18)

وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ ﴿١٧﴾

Na wanaoomba maghufira kabla ya Alfajiri Juz.3 (3:17)

فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَبَوَيْهِ وَقَالَ ادْخُلُوا مِصْرَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ ﴿٩٩﴾

99. Na walipoingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema: Ingieni Misr, Inshallah, mko katika amani.

وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ وَخَرُّوا لَهُ سُجَّدًا وَقَالَ يَا أَبَتِ هَـٰذَا تَأْوِيلُ رُؤْيَايَ مِن قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّي حَقًّا وَقَدْ أَحْسَنَ بِي إِذْ أَخْرَجَنِي مِنَ السِّجْنِ وَجَاءَ بِكُم مِّنَ الْبَدْوِ مِن بَعْدِ أَن نَّزَغَ الشَّيْطَانُ بَيْنِي وَبَيْنَ إِخْوَتِي إِنَّ رَبِّي لَطِيفٌ لِّمَا يَشَاءُ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿١٠٠﴾

100. Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi na wakapomoka kumsujudia Na akasema: “Ewe baba yangu! Hii ndio tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani, Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe ya kweli, Na Mwenyezi Mungu alinifanyia wema kunitoa gerezani na kuwaleta nyinyi kutoka jangwani baada ya shetani kuchochea kati yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni Mpole kwa alitakalo. Hakika yeye ni Mjuzi, Mwenye hekima.

رَبِّ قَدْ آتَيْتَنِي مِنَ الْمُلْكِ وَعَلَّمْتَنِي مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَنتَ وَلِيِّي فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿١٠١﴾

101. Ewe Mola Wangu! Hakika umenipa utawala na umenifunza tafsiri ya matukio. Ewe mvumbuzi wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye walii wangu katika dunia na akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Mwislamu na unikutanishe na watu wema.”

ذَٰلِكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ أَجْمَعُوا أَمْرَهُمْ وَهُمْ يَمْكُرُونَ ﴿١٠٢﴾

Hayo ni katika habari za ghaibu tulizokupa wahyi. Na hukuwa pamoja nao walipoazimia shauri lao wakipanga njama.

KUKUTANA YUSUF NA YA’QUB

Aya 99–102

MAANA

Na walipoingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema: “Ingieni Misr, Inshallah, mko katika amani.”

Ya’qub alihuzunika sana kwa kumkosa Yusuf, alilia sana huku akijua kuwa kilio hakitafanya kitu, lakini alikuwa akipunguza joto la kufarikiana. Huzuni yake iliendelea kwa muda mrefu sana. Kwa sababu Yusuf alikaa miaka kadha katika nyumba aliyonunuliwa, miaka gerezani, miaka ya kuwa mtumishi wa serikali, ikafuata miaka saba ya mavuno ndipo ikaja miaka ya ukame.

Kila muda ulivyokuwa ukizidi kuendelea ndipo huzuni ya Ya’qub ilivyoendelea; kama inavyoashiria kauli ya waliomwambia: “Wallah hakika wewe bado uko katika upotevu wako wa zamani.”

Tukijua kiwango cha huzuni aliyokuwa nayo Ya’qub kwa kumkosa mwanawe, ndipo tutakapojua kiwango cha furaha aliyokuwa nayo kwa kukutana na Yusuf. Kwa sababu furaha ya kupona ugonjwa inakuja kwa kiwango cha maumivu yalivyokuwa au kuzidi furaha.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa makusudio ya wazazi wake ni baba yake na mama yake mdogo (khalat), kwa sababu mama yake alikuwa ameshakufa. Wengine wakaenda mbali, kwamba mama yake alifufuliwa kaburini, ili aone utukufu wa mwanawe na aweze kumsujudia. Wala hakuna haja ya uhakiki huu na mfano wake; isipokuwa ni kurefusha maneno tu.

Unaweza kuuliza : kuwa kifua cha Aya hakiafikiani na mgongo wake, kwa sababu kifua kinasema, Walipoingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake, na inajulikana kuwa Yusuf alikuwa Misr. Mgongo nao unasema: Ingieni Misr, wakati wao tayari wako Misr kwa Yusuf?

Jibu : Imesemekana katika jawabu kuwa Yusuf, aliwajengea hema wazazi wake karibu na mpakani huko ndiko walikoingia na akawakumbatia, na walipoanza mwendo wa kutoka kwenye hema wakielekea Misr ndipo alipowaambia ingieni Misr, Jawabu hili linachukua tamko la Aya zaidi ya inavyochukulika. Sio mbali kuwa makusudio ya ingieni Misri ni kaeni humo kwa amani; kama ilivyotokea. Ambapo mfalme aliwakatia ardhi yenye rutuba na kizazi cha Ya’qub kikandelea hapo kwa muda mrefu.

Imelezwa katika Majmaul-bayan “Aliwaambia mko katika amani, kwa sababu wao hapo mwanzo walikuwa wakimuhofia mfalme wa Misr, wala hawawezi kuingia ila kwa Pasipoti yake – yaani pasi za safari kama hivi sasa – Amesema Wahab: kwamba watu wa Ya’qub waliingia Misr wakiwa ni watu 73 na wakatoka pamoja na Musa wakiwa ni watu 600570” Vilevile imeelezwa katika Majmaul-bayan kuwa baina ya Yusuf na Musa kuna miaka 400.

Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi.

Aliwakalisha kwenye kiti ambacho alikuwa akikaa yeye akiwa anaendesha mambo ya serikali, kwa ajili ya kuwaadhimisha.

Na wakapomoka kumsujudia.

Waliopomoka ni wazazi pamoja na ndugu zake na aliyesujudiwa ni Yusuf, yaani wazazi wake pamoja na ndugu zake walimsujudia Yusuf. Makusudio ya kusujudi hapa ni kiasi cha kuinama kwa kumuadhimisha na kumtukuza. Na ilikuwa kuinama ndio maamkuzi ya heshima wakati huo, kama ilivyoelezwa katika baadhi ya tafsir.

Imesekana kuwa waliyemsujudia ni inamrudia Mungu na kwamba sijda ilikuwa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa sababu ya neema hii kubwa. Lakini kauli hii inapingana na dhahiri ya Aya wala haifikiani na kauli ya Yusuf katika Aya ya 4. “nimeota zikinisujudia, Yaani kumsujidia yeye sio mwengine.

Na akasema: “Ewe baba yangu! Hii ndio tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe ya kweli.

Anaishiria kauli yake katika mwanzo wa Sura hii, Juz. 12 : “Ewe baba yangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja na jua na mwezi nimeo- ta zikinisujudia.” Maelezo yake na ufafanuzi uko huko.

Katika tafsir ya Razi, imeelezwa: “Wametofautiana katika kiwango cha muda baina ya kuota ndoto na kukutana. Ikasemekana ni miaka 80, wengine miaka 70 na ikasemwa ni miaka 40, na hiyo ndio kauli ya wengi; na kwamba umri wake aliishi miaka 120”

Sisi hatujui kwa yakini umri wake ulikuwa miaka mingapi alipotiwa kisimani wala muda aliokaa katika nyumba aliyonunuliwa au muda wake gerezani na kutumikia serikali.

Kwa sababu hatukupata kauli yoyote ya kutegemea kutuongoza kwenye hilo na kauli za wafasiri zimegongana, lakini wengi wamesema kuwa aliishi miaka 120.

Na Mwenyezi Mungu alinifanyia wema kunitoa gerezani na kuwaleta nyinyi kutoka jangwani.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) humjaribu mtu kwa raha, kama anavyomjaribu kwa shida. “Akasema: Haya ni katika fadhila za Mola wangu, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru?” (27: 40). Imam Ali(a.s) anasema:“Hazikuadhimishwa neema za Mwenyezi Mungu na yoyote ila huzidi haki ya Mwenyezi Mungu juu yake kwa cheo”

Yusuf alipata majaribu ya tabu akavumilia, na ya raha akashukuru. Ndio hapa anazizungumza neema za Mwenyezi Mungu juu yake na kuzihesabu hisani alizofanyiwa: amenitoa gerezani, akanitukuza kwenye cheo na akawaleta watu wangu wa nyumbani, ambapo walikuwa jangwani wakifuga ngamia na mbuzi na kondoo ambao pia nao walimalizwa na ukame wakawa kwenye ardhi tupu isiyo na chochote, wakimwambia mheshimiwa: “Fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka”

Wala hakutaka kutaja kutolewa kwake kisimani kwa kuchunga hisia za ndugu zake. Vile vile uadui wao aliuelekeza kwa shetani bila ya kuuelekeza kwao moja kwa moja kwakusema:

Baada ya shetani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni mpole kwa alitakalo.

Anawafanyia upole wema na kuwafikisha anapotaka kwenye enzi na utukufu.

Hakika yeye ni Mjuzi Mwenye hekima.

Tofauti baina ya ujuzi wake na hekima yake ni kwamba vitendo vyake vyote na hukumu zake zinakuja kulingana na hekima, “Ewe Mola wetu hukuviumba hivi bure” Juz.4 (3:919).

Ama elimu yake, haiepukani na kinachojulikana. Kwa maneno mengine ni kuwa elimu yake ni kukiambia kitu kuwa kikawa.

Ewe Mola Wangu! Hakika umenipa utawala na umenifunza tafsiri ya matukio. Ewe mvumbuzi wa mbingu na ardhi! Wewe ndiwe mtawala wangu katika dunia na akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Mwislamu na unikutanishe na watu wema.

Maana ya mvumbuzi ni kuwa ameziumba bila ya mfano mwingine uliotangulia. Ametaja mbingu kwa tamko la wingi na ardhi kwa tamko la umoja kwa vile mtu huona kwa macho yake mbingu nyingi, lakini haoni isipokuwa ardhi moja.

Maana ya wewe ni mtawala wangu ni kuwa wewe ndiye unayosimamia mambo yangu yote ya dunia na akhera. Baada ya Yusuf kutaja, neema za Mwenyezi Mungu kwake, alimwelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kumshukuru kwa utawala aliompa na kumuhusisha na utume, akiwa amewakilisha kwake mambo yake yote huku akimwomba afe kwenye utifu na radhi zake Mwenyezi Mungu na pia amjumuishe na watu wema waliopita miongoni mwa wazazi wake na amjalie ni kizazi chema kilichobakia baada ya wazazi wake.

Hayo ni katika habari za ghaibuu tulizokupa wahyi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kisa cha Yusuf, alimwelekea Mtume wake mtukufu Muhammad(s.a.w.w) kwa Aya hii. Lengo ni kutoa hoja kwa anayekanusha utume wake.

Ufupisho wake ni kuwa hayo tuliyoyasimulia kuhusu Yusuf, kwa ufafanuzi huu, hakuyashuhudia Muhammad(s.a.w.w) wala kuyasoma katika kitabu au kusikia kutoka kwa mtu yeyote, isipokuwa ni Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaojulisha ukweli wake na utume wake.

Na hakuwa pamoja nao walipoazimia shauri lao wakipanga njama.

Walioazimia ni ndugu wa Yusuf. Anayeambiwa ni Muhammad(s.a.w.w) . Watu wote wanajua kuwa Muhammad(s.a.w.w) hakuwako wakati walipofanya shauri la kumtupa Yusuf shimoni na pia walipofanya njama kwa baba yake kusema kuwa ameliwa na mbwa mwitu.

Vilevile watu wanajua kuwa Muhammad(s.a.w.w) hakusoma kitabu wala kuwa mwanafunzi wa ustadh yeyote. Kwa hiyo basi hakuna njia iliyobaki ya kuyajua hayo isipokuwa wahyi wa mbinguni.

Mfano wa Aya hii ni ile isemayo: “Hizo ni habari za ghaibuu tunazokupa wahyi, Hukuwa ukizijua wewe wala watu wako kabla ya hii. Basi subiri! Hakika mwisho ni wa wacha Mungu.” Juz.12 (11:49)

JE, KISA CHA YUSUF NI CHA MAPENZI?

Kwa mtazamo wa juu juu, inaweza kudhaniwa kuwa sura ya Yusuf inafanana na kisa ambacho mhusika mkuu ni mwanamke aliyetawaliwa na tabia ya kike iliyompa ashiki kwa kijana mtanashati ambaye hajapatapo kumuwaza mwingine mfano wake kwa uzuri, na kwamba kijana huyo alijizuia kwa uchaji Mungu wake na kuhofia hisabu na malipo ya Mungu, sawa na kisa cha Sallam Mughniya pamoja na Abdurrahman Al-Qass[1] .

Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa ingelikuwa vizuri kama kisa hiki kisingetajwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, Baadhi ya waumini wanasema kuwa Mwenyezi Mungu ana hekima ya ndani katika Sura hii ambayo hatuijui.

Hawa wakawa wamejichunga sana; kama walivyokosea Khawarij Maymuniya walipoikana sura ya Yusuf kwa vile ni kisa cha mapenzi jambo ambalo liliwatoa nje ya madhehebu ya Kiislamu.

Hakika tuliyoishilia nayo, wakati tukifasiri Sura hii ni kwamba mwenye kuisoma kwa kuitilia manani na kuzingatia maana yake (Tadabbur) na akagundua siri zake na malengo yake ataamini kabisa kwamba Sura hii inaeleza mfano ulio wazi zaidi kuwa mara nyingi kushikamana na msimao wa kiroho ni nyenzo ya kufaulu katika maisha haya yaliyojaa ufisadi.

Mwenye kuisoma kijujuu atasema kama walivyosema Maymuniya kuwa ni kisa cha mapenzi au walivyosema baadhi ya waumini kuwa Mungu ana hekima isiyojulikana katika kisa hiki. Ni kweli hawezi kuijua isipokuwa yule mwenye kuyazingatia vizuri (kuyafanyia tadabbur) maneno ya Mwenyezi Mungu na Aya zake.

Tutaonyesha baadhi ya uhakika ulioko kwenye sura hii unaojitokeza kwa kila mwenye kuutafuta, kama ifutatavyo:-

1. Mvutano baina ya haki na batili unaendelea daima katika maisha haya, wala haitapatikana suluhu baina yake. Natija ya kimaumbile ya hilo ni kwamba mwenye kufuata njia ya batili atapata upinzani kutoka kwa wenye haki, lakini kwa njia ya uadilifu na ukweli, sio kwa uwongo na hadaa. Kwa sababu wao hawaitaki silaha isiyokubaliwa na haki na uadilifu.

Vile vile naye mwenye kufuata njia ya haki atapigwa vita na wabatilifu, lakini kwa uzushi na kila aina ya vitimbi. Kwa sababu mwenye kung’ang’ania ubatilifu, hana silaha isipokuwa kupotoa na kuzulia. Ndio maana haki ikawa ni ghali na yenye takilifa nyingi kwa anayeifuata na kushikamana nayo.

Mwenyezi Mungu amepigia mfano wa hakika hii kwa Sura ya Yusuf. Mke wa mheshima alimtaka Yusuf, lakini akakafaa na akajihifadhi kwa sababu ya kumcha Mungu (takua).

Akamtishia kifungo kama hatafanya lakini akajizuia na wala asifanye huku akisema: “Ewe Mola wangu! Gereza linapendeza zaidi kwangu kuliko haya wanayoniitia”; Kwa hiyo akajitolea kwa thamni ghali kuliko nafsi yake kwa sababu dini ina thamani na ni ghali zaidi.

Hata hivyo wale wanaoipinga haki mwisho wanaangusha silaha chini kwa wenye haki, kama ilivyotokea kwa nduguze Yusuf na mke wa mheshimiwa.

2. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Kama asingeona dalili ya Mola wake,” inatupa udhibiti wa kiujumla na makisio sahihi ya mapambano baina ya mumin na asiyekuwa mumin. Mwenye kuitikia buruhani hii wakati wa mtihani, kama alivyofanya Yusuf, basi huyo ni katika wale ambao imani na yakini imetulizana katika nyoyo zao kwa haki na uadilifu. Na mwenye kusukumwa na matamanio na shahawa zake na akajitia hamnazo akaacha buruhani ya mola wake, basi huyo hana dini kitu.

3. Yanapotokea matatizo watu wema wanajulikana na kuwa ni tegemeo la watu, kama alivyo tegemea mfalme wa Misr kwa Yusuf akiwa yuko gerezani, ili aweze kuikinga nchi na balaa la miaka ya ukame. Hali ya ufisadi inawainua waovu na kuwaweka chini wema, lakini shida na matatizo yanadhihirisha hakika ya mambo.

4. Kuizowesha nafsi kutegemea njia ya haki kutaleta natija nzuri na bora. Yusuf alivumilia kisimani, gerezani, kuuzwa kama mtumwa na kutuhumiwa, lakini natija ikawa yeye ndiye bwana mkubwa mheshimiwa, anaambiwa na mfalme “Hakika wewe leo kwetu ni mwenye heshima mwenye kuaminika.” Na nduguze Yusuf wanasimama wakiwa wamehemewa wakitaka kuhurumiwa huku wakisema: “basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka; hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wanaotoa sadaka” Na mwisho wanakuja kumsujudia. “mvumilivu hula mbivu”.

Huu ndio mtazamo wa haraka haraka wa baadhi ya mazingatio na mafundisho ya sura hii tukufu. Mwenye kutaka ufafanuzi na aisome kwa ukamilifu pamoja na tafsiri yake.

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

103. Na watu wengi si wenye kuamini ujapopupia.

وَمَا تَسْأَلُهُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٤﴾

14. Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Haikuwa hii ila ni mawaidha kwa wal- imwengu

وَكَأَيِّن مِّنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ ﴿١٠٥﴾

105. Ni ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazozipitia na hali ya kuwa wanazipuuza.

وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ ﴿١٠٦﴾

106. Na wengi wao hawamwamini Mwenyezi Mungu pasi na kuwa ni washirikina.

أَفَأَمِنُوا أَن تَأْتِيَهُمْ غَاشِيَةٌ مِّنْ عَذَابِ اللَّـهِ أَوْ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١٠٧﴾

107. Je wanaaminisha kuwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ya kuwagubika au kuwafikia saa (Kiyama) kwa ghafla na hali hawatambui?

NA WATU WENGI SI WENYE KUAMINI AYA

Aya 103-107

MAANA

Na watu wengi si wenye kuamini ujapopupia.

Muhammad(s.a.w.w) ana ishara na miujiza inayojulisha juu ya utume wake, zikiwemo sharia na sera zake. Nyingine ni Qur’an na ufasaha wake, mafunzo yake, uhakika wake na kutolea habari mambo ya ghaibuu. Miongoni mwa ghaibuu hizo ni kisa cha Yusuf kwa ufafunuzi wake, kama tulivyotaja katika Aya 102 ya Sura hii.

Mtume Muhammad(s.a.w.w) alikuwa akipupia sana watu waamini na waongoke, hasa kaumu yake ya kiquraish, lakini wengi wao hawakuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu ya masilahi yao binafsi; kama vile viongozi na wenye nguvu, au kwa sababu ya ujahili na kuiga; kama vile wanyonge na wafuasi.

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwambia mtume wake mtukufu kuwa wewe huwezi kumwongoza umpendaye pamoja na ikhlasi yako na miujiza yako na wewe huna haja nao wala imani yao.

Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Haikuwa hii ila ni mawaidha kwa walimwengu.

Neno ‘hii’ ni Qur’an ambayo inaongoza kwenye usawa ikizielekeza akili kwenye ishara za Mwenyezi Mungu na dalili za uadilifu na umoja wake. Inaongoza na kuelekeza kupitia mdomoni mwa Mtume Mtukufu Muhammad(s.a.w.w)

Ni ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazozipitia na hali ya kuwa wanazipuuza.

Kana kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake, wewe tulia moyo wako wasipokuamini wewe na dalili za utume wako, kwani wao wamenikufuru mimi nikiwa muumba wao na mwenye kuwaruzuku. Nimeujaza ulimwengu dalili za utukufu wangu na uwezo wangu, lakini bado wakazipinga. Basi hakuna ajabu wakikupinga wewe pamoja na miujiza iliyodhihiri mikononi mwako.

Na wengi wao hawamwamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni washirikina.

Hili ni jawabu la swali linalokadirika kutokana na Aya iliyotangulia, “Na watu wengi siwenye kuamini ujapopupia. Swali lenyewe linakuja hivi: Vipi Mwenyezi Mungu aseme watu wengi hawaamini na inajulikana kuwa waarabu na watu wa Kitabu wanakiri kuweko muumba na wao ndio waliokuwa watu wengi wakati huo? Bali Qur’an yenyewe inakubali hilo wazi wazi pale iliposema: “Na ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema ni Mungu” (29:16).

Kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajibu swali hili la kukadiriwa kwa kusema wengi wao kuamini kwao hakuachani na ushirikina, yaani wanamshiriksha Mungu, Wanakubali kuwa mumba yuko, lakini wengi wao wana mfanyia washirika.

Kwa mfano Mayahudi au kikundi katika wao wanasema Mungu ana mtoto anayeitwa Uzayr, Manaswara (wakirsto) nao wanasema mtoto wa Mungu ni Masih. Waarabu wanayashirikisha masanamu katika ibada wanamwambia Mwenyezi Mungu: labeka huna unayeshirikiana naye isipokuwa anayeshirikiana nawe. Kwa hiyo hakuna tofauti baina ya anayekanusha na anayeshirikisha.

Je wanaaminisha kuwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ya kuwagubika au kuwafikia saa (kiyama) kwa ghafla na hali hawatambui?

Katika aya 103 Mweyezi Mungu(s.w.t.) alimwambia mtume wake kuwa wao hawakuamini katika 105 alimwambia wao wamenikufuru mimi hali ya kuwa ni muumba na katika 106 akasema hata wale wanaonikubali wananifanyia washirika. Ikawa ni mazoweya ya kuyafuatishia haya kwa makemeo na kiaga cha adhabu kali.

Unaweza kuuliza : Kutaja ghafla hakuhitajii tena kutaja hawatambui, je, kuna lengo gani la kukaririka?

Jibu : Neno ghafla linaashiria kutokea adhabu wakiwa macho, lakini kutotambua inawezekana kuwa katika hali ya kuwa macho au kulala, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t):

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُهُ بَيَاتًا أَوْ نَهَارًا ﴿٥٠﴾

Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu yake usiku au mchana” Juz.11 (10:50)

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٨﴾

108. Sema: Hii ndiyo njia yangu ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa busara mimi na wanaonifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِم مِّنْ أَهْلِ الْقُرَىٰ أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ اتَّقَوْا أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٠٩﴾

109. Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipokuwa ni wanaume tuliowapa wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa wenye takua, Basi hamtii akili?

حَتَّىٰ إِذَا اسْتَيْأَسَ الرُّسُلُ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ قَدْ كُذِبُوا جَاءَهُمْ نَصْرُنَا فَنُجِّيَ مَن نَّشَاءُ وَلَا يُرَدُّ بَأْسُنَا عَنِ الْقَوْمِ الْمُجْرِمِينَ ﴿١١٠﴾

110. Hata mitume walipokata tamaa na wakadhani kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusra yetu, wakaokolewa tuwatakao, na adhabu yetu haiondolewi kwa kaumu ya wakosefu.

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١١١﴾

111. Kwa hakika katika simulizi zao mna mazingatio kwa wenye akili. Si hadithi za kuzuliwa, lakini ni kusadikisha yaliyo kabla yake na ufafanuzi wa kila kitu na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.

SEMA HII NI NJIA YANGU

Aya 108 -111

MAANA

Sema: Hii ndiyo njia yangu ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa busara mimi na wanaonifuata.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Muhammad awaambie washirikina kuwa hii ndiyo njia yangu na desturi yangu, hakika yake iko dhahiri na ni halisi, ni mwito wa Mwenyezi Mungu kutokana na elimu, hoja na mantiki.

Hakuna mwenye shaka kuwa mitume wote na wafuasi wao wenye ikhlasi wanalingania kwenye imani ya Mungu na siku ya mwisho, kusimamisha haki na uadilifu, kuwa wanafanya hayo kwa hekima na mawaidha mazuri, na kukabiliana na hoja kwa hoja na fikra kwa fikra, kwenye mantiki yaliyosalimika ambayo yanategemea risala ya mitume na mwito wa viongozi wema.

Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.

Huu ni ubainifu na tafsiri ya mwito wa Muhammad(s.a.w.w) kwamba umetakasika na kila aina ya shirki.

Na hatukuwatuma mitume kabla yako isipokuwa ni wanaume tuliowapa wahyi miongoni mwa watu wa mijini.

Makusudio ya miji ni yoyote ile iwe mikubwa au midogo sio mashambani. Wafasiri wamesema:

Inafahamisha aya kuwa Mwenyezi Mungu hakutuma mtume mwanamke kabisa wala mwanamume kutoka mashambani, kwa sababu wao ni wazito wasiokuwa na maana.

Wafasiri wamewataja watu wa mashambani kuwa hawana maana na wakasahau kuwa wao ndio wakweli zaidi wa lahaja wenye maumbile safi ya tabia kuliko watu wa mijini, na pia wamesahau wanawake wa mjini wanavyojishughulisha kupaka rangi za mdomo na kujikwatua nyuso.

Hali yoyote iwayo ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi pa kuweka ujumbe wake.

Ama lengo la Aya ni kutoa hoja kwa yule anayepinga risala ya Muhammad(s.a.w.w) kwamba yeye hakuwa peke yake katika ujumbe wake. Walikuweko watu wa kawaida mfano wake kabla yake, wakila chakula wakitembea masokoni mijini na mwito wao ulikuwa sawa na wake.

Sasa mnaona ajabu gani, enyi washirikina, kwenye risala ya Muhammad, na msione ajabu ya kutumwa mwenginewe?

Aya hii inafaa kuwa jawabu la wale aliowaashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya:

وَإِذَا رَأَوْكَ إِن يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَـٰذَا الَّذِي بَعَثَ اللَّـهُ رَسُولًا ﴿٤١﴾

Na wanapokuona hawakufanyii ila kejeli tu: je, huyo ndiye Mwenyezi Mungu amemtuma kuwa mtume? ( 25:41)

Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha?

Umetangulia mfano wake katika Juz 4 (3:137).

Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa wenye takua, Basi hamtii akili?

Kusema kwake “kwa wenye takua” ni dalili wazi kuwa njia ya wema wa mtu katika akhera ni amali njema hapa duniani na amali bora zaidi humu duniani ni ile inayolenga heri ya mtu na kuongoka kwake, kuchunga haki yake na uhuru wake usichezewe na dhulma.

Hata mitume walipokata tamaa na wakadhani kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusra yetu, wakaokolewa tuwatakao, na adhabu yetu haiondolewi kwa kaumu ya wakosefu.

Makusudio ya wakadhani, hapa ni kuwa na yakini, yaani wakaona. Mitume waliwalingania umma kwa Mungu na hawakuitikiwa, wakawaonya na adhabu kali ya dunia kabla ya akhera, lakini wakadharau

na kufanya maskhara. Mitume wakangoja adhabu iwashukie wenye dharau, lakini muda ukawa mrefu kiasi cha kukata tamaa na kudhani kuwa adhabu haitakuja na kiaga hakitakamilika. Lakini hatimaye adhabu ikwashukia wakosefu na wenye takua wakaokoka bila ya kuguswa na dhara yoyote au kuhuzunika.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu “walikata tamaa na wakadhani” ni fumbo tu la machungu ya kungoja sana. Mifano ya mfumo huu wa mafumbo ni mingi na imezoeleka katika lugha ya kiarabu na fasihi yake.

Hata hivyo wafasiri hapa wana kauli na rai zilizo mbali kabisa na ufahamisho wa matamko na mfumo mzima wa maneno, mbali ya kuwa unamzidisha msomaji kuduwaa na kupotea.

Kwa hakika katika simulizi zao mna mazingatio kwa wenye akili.

Neno akili hapa limefasiriwa kutoka na neno lub lenye maana ya kokwa au kiini. Akili imeitwa hivyo kwa vile ndio kitu muhimu kwa binadamu. Maana ya simulizi zao ni masimulizi ya Yusuf na nduguze pamoja na mke wa mheshimiwa na mfalme.

Tumekwisha bainisha kuwa katika kisa cha Yusuf kuna mafunzo aina kwa aina, yaliyomuhimu zaidi ni kuwa mwenye kuachana na watu na akamtegemea Mungu peke yake lazima mwisho wake utakuwa mwema.

Si hadithi za kuzuliwa, lakini ni kusadikisha yaliyo kabla yake na ufafanuzi wa kila kitu na ni uwogofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.

Kila kilichokuja katika Qur’ani ni haki na ukweli, kikiwemo kisa cha Yusuf. Na kimekuja kama alivyokieleza Mwenyezi Mungu kwa Mitume wake waliotangulia katika vitabu vya mbinguni. Na inajulikana kuwa Muhammad hakukisoma yeye mwenyewe wala kukisikia kwa mwinginewe.

Zaidi ya hayo ni kuwa katika Qur’an kuna ubainifu wa itikadi na sharia, na kwamba hiyo ni uwongofu kwa anayetaka uwongofu kwa njia yake na rehema kwa yule atakayetumia hukumu zake na kuwaidhika na mawaidha yake. Hakuna shaka kwamba wanaowaidhika na uwongofu wa Mwenyezi Mungu ni wale.

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾

“Ambao wameamini na hawa kuchanganya imani yao na dhullma, Hao ndio watakaopata amani na ndio waliongoka” Juz 7 (6:82).

MWISHO WA SURA YA KUMI NA MBILI