TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU Juzuu 13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 12981
Pakua: 2190


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 17 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12981 / Pakua: 2190
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU Juzuu 13

Mwandishi:
Swahili

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

اللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنثَىٰ وَمَا تَغِيضُ الْأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾

8. Mwenyezi Mungu anajua mimba aibebayo kila mwanamke na kinachopungua na kuzidi matumboni. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.

عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾

9. Ni mjuzi wa ghaibu na yanayoshuhudiwa, mkubwa aliyetukuka.

سَوَاءٌ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ ﴿١٠﴾

10. Ni sawa anayeficha kauli kati yenu na anayeidhihirisha na anayejibanza usiku na anayetembea mchana.

لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ ﴿١١﴾

11. Ana yanayomfuatilia mbele yake na nyuma yake yanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao, Mwenyezi Mungu akiwatakia watu uovu hakuna cha kumzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.

MWENYEZI MUNGU ALIJUA

Aya 8-11

MAANA

Mwenyezi Mungu anajua mimba aibebayo kila mwanamke na kinachopungua na kuzidi matumboni.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya iliyotangulia ametaja kuwa washirikina walimtaka Muhammad(s.a.w.w) muujiza zaidi unao fahamisha kuhusu utume wake.

Katika Aya hii anasema kuwa Yeye anajua kilicho katika matumbo ya uzazi awe ni mtoto wa kiume au wa kike mmoja au zaidi upungufu au ukamilifu. Basi mwenye kujua yote hayo, anajua kwamba kutaka muujiza zaidi ni inadi na kiburi tu, si kutaka kuongoka.

Wameafikiana Waislamu wote kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua viumbe vyote vikubwa kwa vidogo; Kwa sababu kila kiumbe kinajulikana mbele yake. Kwa ibara ya Muhyiddin bin Al-arabi:

“Hakika hakuna chochote kilichopo ulimwenguni ila kina wajihi maalum kwa yule aliyekifanya kiweko”

Kisha wanafalsafa wakatofautiana na ulamaa wa elimu ya Mwenyezi Mungu ambao wanasema kuwa Mwenyezi Mungu anajua mafungu yote; kama vile aina ya wanyama, mimea na vitu vingine kwa ujuzi wa moja kwa moja bila ya kuweko kitu chochote kati yake. Wanafalsafa nao wanasema anajua kupitia sababu zake na kinachozalikana nacho.

Sisi hatuoni faida yoyote ya tofauti hii; Kwa sababu ni juu ya Mwislamu kuamini kuwa elimu ya Mwenyezi Mungu imeenea kwenye kila kitu, kiujumla na kimafungu; hata mapigo ya moyo na pepesi za akilini. Ama kuamini elimu yake kwa namna hii au ile si chochote katika dini.

Kuna hadithi zinazokataa kuifikiria dhati ya Mwenyezi Mungu na kuamuru kufikiria kuumba kwake na utengenezaji wake.

Na kila kitu kwake ni kwa kipimo haumbi kimchezomchezo na bila ya misingi; bali kila kitu kina kiwango chake na nidhamu yake katika kipimo cha mafungu, mihimili athari na mahusiano yake. Vile vile kinamna kitakavyokuwa na sura, mahali, wakati, sababu na desturi yake. Yote hayo ni kulingana hekima na masilaha.

Analoweza binadamu ni kuona, kuchunguza, kupima na kukisia; Kwa hivyo anaweza akapatia au kukosea. Kwa sababu elimu ya mtu inatokana na kutafuta, kwa hiyo inahitaji msababishaji.

Mara nyingi sana kuna yanayodhaniwa kuwa ni sababu ya jambo fulani, kumbe sivyo kabisa. Ama elimu Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ya kidhati na hali halisi.

Ni mjuzi wa ghaibu na yanayoshuhudiwa, Mkubwa aliyetukuka.

Makusudio ya ukubwa sio ukubwa wa umbo na utukufu sio mahali panapohisiwa, bali hayo ni mafumbo ya utukufu wa dhati Yake na sifa Zake. Mjuzi wa ghaibuu ni kujua yale tusiyoyajua, yaliyo ughaibuuni kutokana na elimu yetu na yanayoshuhudiwa ni yale tunayoyaona na kuyashuhudia.

Hakika ulimwengu umejaa viumbe jinsi na aina mbali mbali za hali ya juu na za chini. Kuanzia vidudu hadi binadamu na Malaika, madini hadi mimea na wanyama, mpaka kufikia maji na hewa na mengineyo yasiyokuwa na ukomo.

Mtume anaweza kujua upande moja tu wa baadhi ya vitu vya ulimwengu lakini ujuzi wake, kadiri utakavyokuwa si chochote kulinganisha na asiyoyajua, Mengi yanayofichuka yanaficha siri nyingi.

Wala hajui yaliyoko ulimwenguni isipokuwa muumba wa ulimwengu huo tu. Yeye peke yake ndiye ambaye, kwake, siri na dhahiri ni sawa tu.

وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾

“Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” (17:85)

Ni sawa anayeficha kauli kati yenu na anayeidhihirisha na anayejibanza usiku na anayetembea mchana.

Umepita mfano wake katika Juz. 7(6:3) na Juz.10 (9:78).

Ana yanayomfuatilia mbele yake na nyuma yake yanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Anayefuatiliwa ni binadamu na yanayomfuatilia ni fumbo la hisia na silika zake ambazo zina athari katika kuwa kwake na kuhifadhi utu wake. Hayo yametokana na riwaya iliyopokewa kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq (a.s.).

Wafasiri wamesema kuwa makusudio yayanayomfuatilia ni Malaika, na tafsiri nyingine zinasema kuwa Mwenyezi Mungu hupeleka Malaika kumi mchana kumlinda binadamu na jua linapozama wanaondoka hao na kuja wengine kumi wa zamu ya usiku; na kwamba kila mtu anakuwa hivyo. Iblisi naye zamu yake ya kuwapoteza watu ni mchana na usiku ni zamu ya watoto wake.

Mbali ya kuwa maelezo hayo yako mbali na tamko linavyofahamisha, lakini akili pia inayakataa. Tuonavyo sisi ni kuwa makusudio ya yanayofuatilia ni hisia zinazomhifadhi mtu; kama tulivyotangulia kueleza. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuumba mtu, akampa masikio, macho, utambuzi na mengineyo, ili yamlinde na kumchunga.

Maana haya, ingawaje yako mbali na tamko la Aya, lakini yanaafikiana na hali halisi wala hayapingani na mfumo wa Aya. Ni kwa utambuzi, mtu ana mapambano kati ya manufaa na madhara, ni kwa macho anaweza kufuata njia iliyosalama na ni kwa kupenda dhati ndio atajihifadhi na maangamizi.

HABADILISHI MPAKA WAJIBADILISHE

Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao.

Wafasiri wamesema: Aya hii inafahamisha kuwa watu wanaoishi katika neema ya mali, amani na jaha, Mwenyezi Mungu hawezi kuwaondolea madamu wanaswali na kutoa Zaka, lakini wakiasi basi anawaondolea neema hii.

Ama sisi tutafasiri Aya hii katika mwelekeo wa mafunzo ya kiislamu na maana yanayochukuliwa na tamko la Aya.

Katika mafunzo ya Uislamu, yaliyo muhimu ni wajibu wa jihadi ya nafsi ikiwa inapondokea kwenye haramu na maangamizi au kuridhia udhalili na ufukara. Vile vile jihadi ya nafsi na mali katika njia ya uadilifu na kujikomboa kutokana na dhulma na utumwa.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kupinga udhalili, akapuuza uhai na kukataa kila kitu isipokuwa heshima yake au mauti, basi Mwenyezi Mungu atamshika mkono kumpeleka kwenye matakwa na malengo anayoyakusudia.

Na mwenye kubweteka kwenye raha na uvivu, vyovyote itakavyokuwa Mwenyezi Mungu atamdhalilisha na kumwachia udhaifu wake wala hatamwangalia au kumsikiliza; hata kama ataijaza dunia kwa unyenyekevu, vilio, na dua.

Kwa hivyo basi inatufunukia kuwa maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “ Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyo katika nafsi zao,” ni kuwa Yeye ambaye imetukuka heshima yake, atambakisha mtu kwenye udhalili ikiwa amekaa tu bila ya kujikwamua na kuipinga batili.

Ndio! Mwenyezi Mungu hawezi kutuondolea ufukara mpaka tuamini kuwa ufukara umetoka ardhini sio mbinguni, na mpaka tupigane jihadi dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji na mpaka tujenge viwanda na tulime mashamba.

Mwenyezi Mungu hatubadilishii ujinga mpaka tujenge mashule na vyuo vikuu, Mwenyezi Mungu hatubadilishii utumwa mpaka tulete mapinduzi dhidi ya dhulma. Na Mwenyezi Mungu hatatubadilishia matatizo mbalimbali mpaka tuzisafishe nyoyo zetu na tuondoe pingamizi na vikwazo vilivyo baina yetu.

Mwenyezi Mungu akiwatakia watu uovu hakuna cha kumzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.

Makusudio ya uovu hapa ni adhabu. Wakati wowote Mwenyezi Mungu anapomtakia mtu au kundi jambo lolote, basi hakuna wa kuzuwiya, na Yeye ni mwadilifu, hamtakii isipokuwa analostahiki. Ulinzi ni katika sifa za Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye analinda mambo na huyasimamia kwa mipangilio iliyo kamili.

هُوَ الَّذِي يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنشِئُ السَّحَابَ الثِّقَالَ ﴿١٢﴾

12. Yeye ndiye anayewaonyesha umeme kwa hofu na tamaa, na huyaleta mawingu mazito.

وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلَائِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ وَيُرْسِلُ الصَّوَاعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَن يَشَاءُ وَهُمْ يُجَادِلُونَ فِي اللَّـهِ وَهُوَ شَدِيدُ الْمِحَالِ ﴿١٣﴾

13. Na radi inamtakasa kwa kumsifu na Malaika pia kwa kumhofia. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye, Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu; na yeye ni mkali wa hila.

لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَيْءٍ إِلَّا كَبَاسِطِ كَفَّيْهِ إِلَى الْمَاءِ لِيَبْلُغَ فَاهُ وَمَا هُوَ بِبَالِغِهِ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ ﴿١٤﴾

14. Kwake ndio maombi ya haki, Na hao wanaoomba badala yake hawajibiwi chochote isipokuwa kama yule anyooshaye viganja vyake kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotevu.

وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ﴿١٥﴾

15. Na vilivyomo mbinguni na ardhini vinamsujudia Mwenyezi Mungu vitake visitake na vivuli vyao asubuhi na jioni.

ANAYEWAONYESHA UMEME

Aya 12-15

MAANA

Yeye ndiye anayewaonyesha umeme kwa hofu na tamaa na huyaleta mawingu mazito.

Umeme unaokusudiwa hapa ni ule wa radi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ulimengu; ulimwengu nao una mambo yake na desturi zenye athari; ukiwemo umeme radi mawingu, vimondo na mengineyo anayoweza kuyashuhudia mtaalamu na mtu wa kawaida na pia muumin na mlahidi. Wala hajui hakika yake na umbile lake isipokuwa wataalamu wahusika.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyategemeza kwake moja kwa moja, wala hakuyategemeza kwenye sababu za ulimwengu, kwa upande wa kutegemeza kitu kwenye sababu yake ya kwanza.

Lengo ni kukumbusha kwamba Yeye ndiye sababu ya sababu zote, na kwake Yeye pekee yanarejea mambo yote.

Kauli yake kwa hofu na tamaa ni kuashiria umeme, mara nyingine unakua ni kutoa onyo la kupiga radi ya kimondo na mara nyingine ni dalili njema ya mvua. Kwa hiyo mtu anapata hofu na furaha kwenye kitu hicho hicho kimoja.

Na radi inamtakasa kwa kumsifu na Malaika pia kwa kumhofia.

Makusudio ya kumtakasa (tasbih) ya radi ni kufahamisha uweza na cheo chake Mwenyezi Mungu; sawa na maandishi yanavyomfahamisha mwandishi na jengo na mjengaji wake.

Hapa ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ ﴿٤٤﴾

Na hapana kitu chochote ila kinamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumsifu” (17:44).

Yaani kinamfahamisha, Kwa maneno mengine kila kitendo kizuri kilichofanywa kwa mpangilio mzuri kinamfahamisha aliyekifanya jinsi alivyo na kumsifia, kwa lugha ya hali.

Hakuna mwenye shaka kwamba kila kilichomo ulimwenguni kimefanywa kwa mpangilio mzuri usio na kikomo. Kwa hivyo kinafahamisha jinsi alivyo muumba wake na kumsifia.

Kauli ya kushangaza ni ile ya baadhi ya masufi wanaosema kuwa radi ni kukoroma kwa Malaika na umeme ni mapigo ya nyoyo zao.

Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye.

Unaweza kuuliza : mapigo ya radi mitetemeko ni mambo ya kidhahiri ya kimaumbile na desturi yake. Ni wazi kwamba maumbile ni pofu hayachagui baina ya mwema na muovu, shari yake na heri yake inawaenea wote bila kutofautisha, lakini kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ‘yakampata amtakaye’ inatambulisha kutofautisha?

Jibu : Makusudio ya mapigo ya radi hapa ni adhabu ya radi aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa wale waliong’ang’ania shirki wakawafanyia inadi Mitume wao; kama vile kaumu ya A’d na Thamud, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِّثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ ﴿١٣﴾

“Kama wakikataa waambie nawahadharisha na pigo la radi mfano wa pigo la radi la A’d na Thamud.” (41:13).

فَقَالُوا أَرِنَا اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ بِظُلْمِهِمْ ﴿١٥٣﴾

“Walisema: ‘Tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi.’Wakapigwa na radi kwa sababu ya dhulma yao.” Juz.6 (4:153).

Imetangulia mara nyingi kuelezwa kwamba Qur’an inajitamkia yenyewe kwa yenyewe na baadhi yake ina shuhudia baadhi nyingine.

Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu.

Wanaobishana ni washirikina. Maana ni kuwa hawa wanabishana katika uweza wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake, Mtume Muhammad(s.a.w.w) na Utume wake na pia ufufuo na uwezekano wake, pamoja na kudhihiri dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, Muujiza wazi wa Utume wa Muhammad(s.a.w.w) na kushuka adhabu kwa wapinzani wa ufufuo na hisabu.

Na yeye ni mkali wa hila.

Yaani ni mwenye nguvu sana za kuwakamata maadui zake na maadui wa mawalii wake. Kwa ufupi ni kuwa washirikina wanabishana kwa maneno na Mwenyezi Mungu anakamata kwa vitendo.

إِنَّ بَطْشَ رَبِّكَ لَشَدِيدٌ ﴿١٢﴾

“Hakika mashiko ya Mola wako ni makali.” (85:12).

Kwake ndio maombi ya haki, Na hao wanaoomba badala yake hawajibiwi chochote isipokuwa kama yule anyooshaye viganja vyake kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotevu.

Mwenyezi Mungu ndiye haki, Mwenye kutenda kwa ajili yake na akamtegemea yeye, basi atamlipa thawabu na mwenye kuasi na akafanya jeuri atastahiki adhabu; mwenye kuomba mwenginewe, kama masanamu ,atakuwa ameomba batili isiyodhuru wala kunufaisha.

Na maombi ya makafiri hayako ila kwenye upotovu.

Sawa na mwenye kiu akidhani moshi ni mawingu na mangati kuwa ni maji. Ananyoosha viganja vyake ili avijaze maji na anafungua kinywa chake ili aburudike, mara hamna kitu.

Na vilivyomo mbingu ni na ardhini vinamsujudia Mwenyezi Mungu vitake visitake.

Umepita mfano wake katika Juz.3(3:83).

Na vivuli vyao asubuhi na jioni.

Kivuli ni akisi ya mwili ambao unakuwa nacho, ukitingishika nacho hutingishika; sawa na sura ya kitu kwenye kioo. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja asubuhi na jioni, kwa sababu kivuli kinarefuka katika nyakati mbili hizi.

Maana ni kuwa vilivyomo mbinguni na ardhini na pia vivuli vyao vinamsujudia. Unaweza kuuliza: Kivuli si chochote isipokuwa kinafuata na kinapigiwa mfano wa kutokuwepo kitu. Vipi Mwenyezi Mungu amejaalia ni kitu na akaunganisha na mwenye kivuli hicho?

Sufi wamejibu kuwa vilivyomo mbinguni na ardhini ni viwiliwili na vivuli ni roho.

Tunavyofahamu ni kuwa kivuli ni fumbo la kuenea kwenye kila kitu na kwamba kila kilichoko ulimwenguni kinamsujudia Mwenyezi Mungu; yaani kinakubali kuweko kwake, hata kivuli kingelimsujudia kama kingelikuwa ni kitu.

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿١٦﴾

16. Sema: Ni nani Mola wa mbingu na ardhi? Sema, ni Mwenyezi Mungu. Sema: Je, mnawafanya wengine badala yake kuwa ni walinzi na hawajifai wenyewe kwa nafuu wala dhara? Sema: Je, anaweza kuwa sawa kipofu na aonaye? Au je, huwa sawa giza na nuru? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika, walioumba kama kuumba kwake kwa hiyo kuumba kukashabihiana kwao? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu na yeye ni mmoja, Mwenye kushinda.

KIPOFU NA MWENYE KUONA

Aya 16

MAANA

Sema: Ni nani Mola wa mbingu na ardhi?

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa kila kilichomo ulimwenguni kinanyenyekea uweza wake, anawarudia washirikina na kuwauliza kupitia mdomoni mwa Mtume wake Mtukufu, kuwa ni nani aliyeumba ulimwengu ikiwemo ardhi yake na mbingu yake?

Kwa kuwa swali liko pamoja na jawabu lake; na wala aliyeulizwa hawezi kupinga, alimwamrisha Mtume wake awajibu:Sema: ni Mwenyezi Mungu.

Sema: Je, mnawafanya wengine badala yake kuwa ni walinzi na hawajifai wenyewe kwa nafuu wala dhara?

Mara nyingine, tena kwa kusisitiza hoja, Mwenyezi Mungu anamwamrisha Muhammad awaambie washirikina kuwa nyinyi mnaabudu mawe ambayo yenyewe hayajiwezi kujikinga na madhara wala kuleta manufaaa, je yataweza kumfaa mwingine?

Aya hii si majibu ya washirikina pekee, bali pia ni majibu ya wale wasemao kuwa akili za watu zinajitosha, hazihitajii kupelekewa mitume na kuteremshwa vitabu kutoka mbinguni. Waabudu mawe walikuwa na wanaendelea kuwa wanajiona ni wenye akili na pia watu wangine wanawaona hivyo.

Sema: Je, anaweza kuwa sawa kipofu na aonaye?

Makusudio ya kipofu ni kafiri. Kwa sababu hakuweza kutofautisha baina ya yule asiyejiweza, na mwenye kumiliki dhara na manufaa? Makusudio ya mwenye kuona ni mumin ambaye anatofautisha kati ya wawili hao (asiyejiweza na mwenye uwezo).

Au je, huwa sawa giza na nuru?

Giza ni fumbo la kufuru na nuru ni fumbo la imani. Mwenyezi Mungu anasema:

الر كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ﴿١﴾

“Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu gizani uwapeleke kwenye nuru” (14:1).

Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika, walioumba kama kuumba kwake kwa hiyo kuumba kukashabihiana kwao?

Hii ni kuwarudi washirikina. Ufupisho wake ni kuwa mawe ambayo wanayaabudu hayaumbi chochote; kama aumbavyo Mwenyezi Mungu. Sasa wamethubutu vipi kusema kuwa Mungu anaumba na masanamu yanaumba.

Ikiwa Mwenyezi Mungu anastahiki Uumbaji, basi vile vile atastahiki Uungu na ibada. Ufafanuzi ni kama ifuatavyo:

AKILI ZA WATU HAZIWATOSHELEZI

Maarifa ya mtu yanagawanyika kwenye mafungu mawili: Maarifa ya kiumbile ya kidhati na maarifa ya kinadharia ya kutafuta. Ya kimaumbile hayahitaji bidii wala juhudi, bali yanapatikana kiasi cha kuleta picha tu kichwani; kama kujua kwamba nuru sio giza, kuona si upofu, urefu sio ufupi, jiwe limeumbwa na haliwezi kuumba. Katika maarifa haya anashiri kimjuzi na asiyekuwa mjuzi, na mwenye kukosea hana udhuru wowote [2] .

Ama maarifa ya kinadharia ya kutafuta hayapatikani kwa kuleta picha, bali inahitajika kuyafanyia kazi, juhudi na bidii; kama vile kujua kuwa maji yameshikana au yameachana? Na kujua mardhi haya yanaambukiza au la.

Kadhia hii huitwa ‘nadharia’ ambayo inatofautiana kulingana na maarifa na vipawa vya wenye nadharia hizo. kukosea katika nadharia kunasame- hewa kukiwa kumetokea baada ya bidii na juhudi. Kwa sababu kupatia katika kila kitu ni jambo zito.

Masanamu waliyoyaabudu washirikina hayana mshabaha wowote na uungu kwa njia yoyote ile ya mbali au ya karibu, kuweza kumfanya mtu aingie shaka au aone uwezekano wa kuwa ni mshirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake.

Itakuwaje yakiwa hayo yenyewe yanakojolewa na mbwa na vicheche? Kuyaabudu ni upumbavu zaidi kuliko kusema kuwa giza ni nuru au kipofu anaona.

Unaweza kuuliza : Ni kweli kwamba kuna aina ya maarifa ambayo ni maumbile na kwamba kuukana uungu wa mawe ni mambo ya kimsingi yaliyo wazi yasiyohitaji nadharia, lakini washirikina pamoja na akili yao ya kimaumbile wameweza kuyaabudu, wakiwa ni wenye akili timamu. Je, ni kwa nini?

Jibu : Baadhi yao waliabudu kijujuu tu kwa sababu ya chumo na masilahi fulani, wengine waliabudu kwa kuiga na kurithi. Ilivyo ni kuwa akili inadhoofika na kurudi nyuma katika kuigiza au mazoweya, hasa muda ukiwa mrefu na kurithiwa na vizazi baada ya vizazi vingine.

Ndio maana ikawa dini iliyo salimika ni dharura na lazima kwa binadamu kadiri atakavyokuwa na akili na elimu. Kuna wengi sana waliozowea mifu- mo ya elimu na njia zake za undani, hivi sasa, wanaamini mambo mengi ya upotevu. Gustave Labon, anasema katika kitabu Al-arau wal-mutaqada (Rai na itikadi).

“Hakika wataalamu wanatokewa na mambo ya kijinga sawa na wanavyotokewa wasiojua chochote. Ni mara chache sana mtaalamu kusalimika na ujinga katika mambo yasiyokuwa fani yake.

Kwa maelezo haya ndio tunapata sababu ya wataalamu bora zaidi kuaamini mambo ya kipumbavu sana!! Kisha akatoa mifano mingi sana ya hilo; miongoni mwa mifano hiyo ni: kulikuwa na mtaalamu mmoja mkubwa katika zama zake alikuwa hawezi kutoka nyumbani kwake mpaka afunge kamba shingoni ya kumkinga na dege na uchawi.

Sema: Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu na yeye ni mmoja, Mwenye kushinda.

Ni mmoja katika dhati yake, sifa zake, na kuumba kwake. Mwenye kumshinda kila mwenye inadi na mwenye kuasi hukumu miongoni mwa hukumu zake.

Katika Juz.5 (4:48) Tumetaja dalili za umoja wa muumba. Hapa tutaunganisha na maelezo yaliyo katika Kitab Difau anil- Islam (kuutetea uislam) kilichoandikwa na Laura Fisheva Gallery na kutarjumiwa na Ustadh Munir Baalbaki.

Anasema: Mtume mwarabu alitoa mwito wa itikadi ya umoja wa Mungu (Tawhid) akapata upinzani wa wasio na mtazamo ambao ulimuongoza mtu kwenye shirk. Muhammad alitoa mwito wa kusoma kitabu cha maisha na kufikiria kwenye ulimwengu na desturi yake akiwa anaamini kuwa kila mwenye akili hana budi mwisho kuamini Mungu mmoja.

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TATU

أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا فَاحْتَمَلَ السَّيْلُ زَبَدًا رَّابِيًا وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِي النَّارِ ابْتِغَاءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَاعٍ زَبَدٌ مِّثْلُهُ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْحَقَّ وَالْبَاطِلَ فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ ﴿١٧﴾

17. Ameteremsha maji kutoka mbinguni na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake na mvo ukachukua mapovu yaliyokusanyika juu yake. Na katika vile wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo vingine hutokea povu mfano wake. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mfano wa haki na batili, Ama povu linakwenda bure; ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi, Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mifano.

لِلَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمُ الْحُسْنَىٰ وَالَّذِينَ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُ لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ سُوءُ الْحِسَابِ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿١٨﴾

18. Waliomwitikia Mola wao watapata wema na wasiomwitikia, hata wange-likuwa na vilivyomo ardhini vyote na mfano wake, hakika wangelivitoa kujikombolea. Hao wana hisabu mbaya kabisa na makao yao ni Jahannam, na hapo ni mahali pabaya mno.

POVU HALIDUMU

Aya 17-18

MAANA

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amefananisha baina ya mumin na kafir, akapiga mifano miwili: Kwanza, baina ya kipofu na mwenye kuona - kumfananisha kafiri na upofu na mumin na kuona. Pili, baina ya giza na nuru - kumfananisha kafiri na giza na mumin na nuru.

Katika Aya tuliyo nayo hivi sasa, amefananisha haki na batili akaleta mifano miwili vile vile: Kwanza, baina ya maji yanayokaa ardhini na kuwapatia watu heri na uhai. Pili, mapovu ambayo yanashuka kwenye maji kisha yanachukuliwa na mumbu na kwenda na upepo. Amefananisha haki na maji yenye kunufaisha, na batili akifananisha na mapovu yasiyokaa. Haya ndiyo aliyoyakusudia Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliposema:

Ameteremsha maji kutoka mbinguni na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake na mvo ukachukua mapovu yaliyokusanyika juu yake.

Makusudio ya kadiri yake ni kwamba kila bonde linachukua maji ya mvua kwa kiasi chake cha upana na kina yanayozidi yanaminika kwengine.

Ama mfano mwingine wa haki na batili alioufananisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni madini yanayoyeyushwa motoni ili yatengenezwe vipambo kama dhahabu na fedha au vifaa kama chuma risasi na shaba na povu linazimika kwenye madini yaliyoyeshwa ambayo yanapotea; kama yanavy- opotea mapovu yanayochukuliwa na mvo. Kwa hiyo haki ni kama myeyuko wa madini ulio na manufaa na batili ni povu linalotokana na myeyuko ambalo halina manufaa. Hiyo ndiyo maana ya kauli yake:

Na katika vile wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo vingine hutokea povu mfano wake.

Yaani kwenye madini pia hutokea povu lisilokuwa na manufaa sawa na povu la mvo.

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mfano wa haki na batili.

Yaani Mwenyezi Mungu analeta mfano na picha ya haki kwa ubainifu kati- ka picha ya maji na madini ambayo hupatiwa manufaa na batili katika picha ya povu lisilokuwa na manufaa.

Ama povu ambalo linachukuliwa na mvo au kuzimika kwenye madini yanapoyeyeshwalinakwenda bure bila ya manufaa.

Ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi nayo ni maji na madini hukaa ardhini kwa ajili ya heri na uhai

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mifano ya haki na batili na mingineyo.

Mara nyingi maana yanakuwa magumu kufahamika na watu wengi. Mifano ni nyenzo nzuri ya kufafanua na kuweka wazi, mbali ya kuwa mfano unaongezea uzuri wa ubainifu.

Mwenyezi Mungu amepiga mifano mingi katika Aya nyingi za ubainifu; kama vile ukafiri na imani kuupigia mfano wa giza na nuru au upofu na uoni. Vile vile mfano wa haki, katika Aya hii, kwa maji na madini, na wa batili kuwa povu.

Aya hii inaleta picha halisi ya Uislamu, Au kwa ufasaha zaidi, inaleta picha ya Mwislamu wa kweli, kuwa ni yule ambye watu wananufaika naye kwa manufaa yenye kudumu; sawa na yule aliyeihuisha ardhi baada ya kufa; na kama madini magumu yanayojengewa viwanda na viwanda vinazalisha zana na vifaa mbali mbali na kuleta maendeleo, vya mbali vikaletwa karibu. Kukawa na majeshi, wakatembea angani, ardhi ikalimwa na dunia ikajaa heri, amani na raha.

Natija ya hayo ni kwamba kila mwenye kunufaisha, akaleta utengeneo na katenda kwa ajili ya maisha ya binadamu mwenzake awe na uhuru, amani na raha, hakika mtu huyo atakuwa kwenye malengo ya Uislam, hata kama si Mwislamu. Kwa sababu yeye ni sawa na madini aliyoyatolea mfano wa haki Mwenyezi Mungu. Na kwamba kila mwenye kutenda kwa ajili ya uovu wa mtu. Yeye hana uislamu kitu, hata kama atafunga maisha na kuunganisha swala za usiku na alfajiri.

Waliomwitikia Mola wao watapata wema.

Yaani watapata wema kwa sababu ya kumwitikia Mola wao kwenye mwito wa kutenda kwa ajili ya manufaa ya watu na kwa ajili ya maisha bora. Ama makusudio ya wema ni ujira na thawabu na kwamba watu wa haki watanufaisha, kama maji yanavyonufaisha ardhi.

Na wasiomwitikia - nao ni wale wasiokuwa na maana, kama mapovu-hata wangelikuwa na vilivyomo ardhini vyote na mfano wake, hakika wangelivitoa kujikombolea. Hao wana hisabu mbaya kabisa na makao yao ni Jahannam, na hapo ni mahali pabaya mno.

Umetangulia mfano wake katika Juz.3 (3:91) na Juz,11(10:54).

أَفَمَن يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٩﴾

19. Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola wako ni haki, ni sawa na aliye kipofu? Wanaozingatia ni wenye akili tu.

الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَلَا يَنقُضُونَ الْمِيثَاقَ ﴿٢٠﴾

20. Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu wala hawavunji maagano.

وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ ﴿٢١﴾

21. Na wale ambao huyaunga aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe na humwogopa Mola wao na huihofu hisabu mbaya.

وَالَّذِينَ صَبَرُوا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٢﴾

22. Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao na wakasimamisha Swala na wakatoa kwa siri na kwa uwazi katika vile tulivyowaruzuku na wakayaondoa maovu kwa wema, Hao ndio watakaopata malipo ya nyumba.

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ ﴿٢٣﴾

23. Nayo ni Bustani (Pepo) za Milele wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao wake zao na vizazi vyao, Na Malaika wanawaingilia kila mlango.

سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٤﴾

24. (wakisema): Assalaam alaykum kwa sababu ya mlivyosubiri. Basi ni mema mno malipo ya nyumba.

وَالَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ ﴿٢٥﴾

25. Na wale wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuifunga na wanakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe na wanafanya ufisadi katika nchi. Hao ndio walio na laana na wana nyumba mbaya.

YALIYOTEREMSHWA KUTOKA KWA MOLA WAKO NI HAKI

Aya 19-25

MAANA

Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola wako ni haki, ni sawa na aliye kipofu? wanaozingatia ni wenye akili tu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kufananisha ukafiri na upofu, tena akafananisha haki kwa maji na batili kwa povu, sasa anafananisha mwenye kumwamini Muhammad na kuona na mwenye kumkana kwa upofu.

Mwenyezi Mungu ameeleza uhakika huu kwa njia ya swali ili kumsuta na kumtahayariza.

Wanaozingatia ni wenye akili tu wanasikiliza sauti kwa akili na yule asiyetia akilini isipokuwa yanayoafiki hawaa yake, ni sawa na asiye na akili.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja sifa za wenye akili ambazo zinafahamisha makusudio ya wenye akili kuwa ni waumini wenye takua; kama ifuatavyo:

1.Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu.

Kila lililo na dalili basi hilo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu na ni juu ya binadamu kutekeleza, lakini maibilisi wanapotosha uhakika kwa mapenzi yao kisha wananasibisha hawa zao hizi za kishetani kwa Mwenyezi Mungu na haki. Mwenyezi Mungu ametakata na yale wanayomzushia.

Wala hawavunji maagano, Hii ni kutilia mkazo kauli yake ‘wanatimiza’ ambapo wanalazimiana na utekelezaji ahadi bila ya kuvunja.

2.Na wale ambao huyaunga aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe.

Wafasiri wametaja kauli kadhaa katika kufasiri aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, Kauli iliyo karibu zaidi ya roho ya Uislamu na misingi yake, ni ile ya yule aliyesema: Makusudio ya aliyoamrisha yaungwe, ni msaada wa mtu kwa nduguye mtu, kusaidiana naye kuondoa madhara na kuleta manufaa kwa karibu au mbali.

3.Na humwogopa Mola wao na huihofu hisabu mbaya kimatendo sio kinadharia na kimaneno. Imam Ali anasema: “Mambo mema yanafahami- ka kwa imani na imani inafahamika kwa mambo mema.”

4.Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao. Wanapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanavumilia majeraha na maumivu; hawataki malipo wala shukrani isipokuwa radhi ya Mwenyezi Mungu peke yake.

5.Na wakasimamisha Swala ambayo mwanzo wake ni Takbira ihram: Mungu ni mkubwa zaidi (Allahu akbar) hakuna mkubwa zaidi yake vyovyote atakavyo kuwa. Na Mwisho wake swala ni Tahlil na Salaam: Hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu (lailalaha illallah) Hakuna anayeabudiwa isipokuwa Yeye; hakuna mali wala jaha au hisabu zinazoweza kuabudiwa wala hakuna nguvu inayonyenyekewa isipokuwa nguvu yake Mwenyezi Mungu pekee yake bila ya kuwa na mshirika.

6.Na wakatoa kwa siri na kwa uwazi katika vile tulivyowaruzuku, Mali ndiyo ugomvi. Angalia tulivyoielezea katika mwanzo wa Juz.4 (3:92).

7.Na wakayaondoa maovu kwa wema, Hao ndio watakaopata malipo ya nyumba.

Makusudio ya wema hapa ni msamaha na uovu ni haki maalum inayokuwa baina ya wawili; kama kisasi. Mwenyezi Mungu anasema: “Mmeandikiwa kisasi katika waliouawa; muungwana kwa muungwana na mtumwa kwa mtumwa na mwanamke kwa mwanamke, Na anayesamehewa na ndugu yake chochote, basi ni kufuatana kwa wema na kulipa kwa ihsani.” Juz.2 (2:178)

Ama haki ya Mwenyezi Haina kusameheana,

وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ﴿٢﴾

“Wala isiwashike kwa ajili yao huruma katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.” (24:2).

Nayo ni Bustani (Pepo) za Milele wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao wake zao na vizazi vyao.

Wema wote wataingia peponi, Iwapo duniani walikuwa na udugu na upenzi basi furaha itazidi kwa kuunganishwa tena na kukumbuka enzi zao walipokuwa duniani. Iwapo matendo yao yatatofautiana, basi udugu na urafiki utakatika siku hiyo:

فَرِيقٌ فِي الْجَنَّةِ وَفَرِيقٌ فِي السَّعِيرِ ﴿٧﴾

Kundi moja litakuwa Peponi na kundi jingine litakuwa Motoni. (42:7).

Na Malaika wanawaingilia kila mlango (wakisema): Assalaam alaykum kwa sababu ya mlivyosubiri. Basi ni mema mno malipo ya nyumba.

Maana ya Assalaamu alykum! Ni: Amani iwe juu yenu. Kauli yake Mwenyezi Mungu kwa sababu ya mlivyosubiri, inaashiria kwamba Pepo ni haramu isipokuwa kwa mwenye kufanya jihadi akasubiri, akavumilia tabu na mashaka ya jihadi, Imam Ali(a.s) anasema:“Pepo imezungukwa na machukivu na moto umezungukwa na matamanio. Na jueni kuwa hakuna yeyote anayemtii Mwenyezi Mungu ila hujiwa na machukivu,Na hakuna yeyote aliyemwasi Mwenyezi mungu ila hujiwa na matamanio.”

Na wale wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuifunga.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja wema na sifa zao na malipo mema aliyowaandalia, sasa anawataja wafisadi. Kwa ibara ya kuunganisha ni kuwa baada ya kutaja wanamapinduzi dhidi ya ufisadi anataja wapinzani wao.

Ni kawaida makundi mawili hayo kupingana, Watenda mema hutekeleza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wakatenda kulingana na akili na dhamiri na kila linalofahamishwa na dalili. Wafisadi wanavunja ahadi yake Mwenyezi Mungu na hutenda kulingana na mawazo ya kishetani wakiichanganya haki na batili na wakiificha haki na hali wanajua

Na wanakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe.

Wanawatawalisha mataghuti wakosaji na kuwasaidia kuwakandamiza watu wema kinyume na aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na kuyakataza.

Na wanafanya ufisadi katika nchi kwa kuidhihirisha dhulma na kuleta fitina vurugu, kuwapoteza wasio na hatia, kuleta utengano, kuleta maangamizi na kila aina ya ufisadi na upotevu.

Hao ndio walio na laana na wana nyumba mbaya.

Ikiwa matendo yao ni kinyume cha watendao mema, basi vile vile ni kawaida malipo yao yawe tofauti. Wema watapata pepo na nyumba yenye neema na waovu watapata Jahannam na mahali pabaya.

اللَّـهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ وَفَرِحُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا مَتَاعٌ ﴿٢٦﴾

26. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia. Wamefurahia maisha ya dunia na maisha ya dunia kwa kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe.

وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ قُلْ إِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَنْ أَنَابَ ﴿٢٧﴾

27. Na husema wale ambao wamekufuru: “Kwa nini hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake?” Sema: Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humuongoza anayeelekea kwake.

الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾

28. Wale ambao wameamini na zikatua nyoyo zao kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Ehe! Kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu nyoyo zinatua.

الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَآبٍ ﴿٢٩﴾

29. Wale ambao wameamini na wakafanya matendo mema, raha ni yao na marejeo mazuri.

HUKUNJUA RIZIKI

Aya 26-29

MTU NA RIZIKI

Katika Juz.6 (5:66) Tumelielezea suala hili. Pia katika Juz, 7 (5:100), tumefafanua zaidi katika kifungu ‘Je riziki ni bahati au majaliwa’ Hivi sasa tunarudia maudhui haya kwa mfumo mwingine kwa kuangalia umuhimu wake.

Mtu ana sifa nyingi, zikiwemo za kidhati na ulazima anazokuwa nazo bila ya kubanduka; kwa mfano kuwa mrefu au mfupi kuwa ni mtoto wa tajiri au fukara. Nyingine, sio za dhati ni za kutafuta; mfano kuwa mkulima, mfanyabiashara, tabibu au mwajiriwa n.k.

Utajiri nao una sababu zake; zikiwemo nasabu; yaani urithi, Huo unatambuliwa na kukubaliwa na dini, hata kama haukupatikana kwa jasho. Sababu nyingine ni ulanguzi na unyang’anyi; kama vile riba, ghushi, wizi, biashara ya haramu n.k. Huu ni haramu, hilo halina shaka. Sababu nyingine ya utajiri ni jasho la mtu na bidii; kama vile ukulima, viwanda n.k. Sababu hii ndio bora zaidi kiakili na kisharia.

Kwa hiyo basi, inatubainikia kuwa ufukara na utajiri unatokana na sanaa ya ardhini sio ya mbinguni. Lakini wako wanaotoka nje ya hayo na kuziita sababu za hayo kuwa ni tawfiki ya Mungu, wengine wakaita bahati, lakini hakuna hata mmoja wao anayethubutu kusema kuwa kadhaa na kadari inaingilia juhudi za mtu na kazi yake na kwamba inawaunga mkono wengine kwa kuwasaidia na kuwaacha wengine. Hakuna anayeweza kuthibitisha hilo. Vinginevyo ingelikuwa sababu zote ni bure tu, na kufanya kazi kungelikuwa ni maneno tu yasiyokuwa na maana.

Unaweza kuuliza : Kauli yako hii si inapingana na kauli ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia.

Jibu : Maisha ya watu yako makundi mawili: kuna wale walio na riziki pana na wale walio na riziki finyu. Kila moja kati ya utajiri na ufukara unatokana na sababu zake maalum ambazo tumekwisha zidokeza. Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia’ ni wasifu na kuelezea hali halisi ya watu; kana kwamba anasema watu ni makundi mawili mafukara na matajiri. Mwenyezi Mungu ameutegemeza ufukara na utajiri kwake ili kutanabahisha kuwa Yeye mtukufu ndiye muumba wa ulimwengu ambao una tabu na raha.

Ikiwa mtu atasema kwa nini basi Mwenyezi Mungu asingeumba ulimwengu usiokuwa na dhiki?

Majibu yake yako kwenye Juz, 5 (4:78), ‘Kifungu cha Haiwezekani kuongeza zaidi ya ilivyo’

Wamefurahia maisha ya dunia na maisha ya dunia kwa kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe.

Mfano wa Aya hii umekwishapita mara nyingi, ikiwemo ile ya Juz.4 (3:185). Kuongezea na tuliyoyazungumza huko, ni kwamba kuna aina ya watu wanafurahia mali kwa sababu inasitiri aibu yao na uovu wao. Wengi katika wao hawaoni kitu isipokuwa kwenye mali na utajiri. Ni maarufu kwa wamarekani kwamba wao hawaangalii kitu chochote ila kupitia dola (pesa). Hicho ndicho kipimo cha hadhi ya mtu, hata wataalamu na wenye vipaji, thamani yao ni vile vilivyo katika mifuko yao sio vilivyo vichwani mwao.

Na husema wale ambao wamekufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake?.

Umepita mfano wake katika Juz,1 (2: 118), Juz. 7 (6:37), Juz,11 (10:20) na kwa herufi zake hizihizi katika Juzu na sura hii tunayoendela nayo Aya 7.

Sema: Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humuongoa anayeelekea kwake.

Angalia kifungu cha ‘Uongofu na upotevu’ kwenye Juz,1 (2: 26) na kifungu ‘Upotevu’ katika Juz.5 (4:88).

Wale ambao wameamini na zikatua nyoyo zao kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Ehe! Kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu nyoyo zinatua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipotaja watu wa mali na furaha yao inayotokana na kutulizana kwao kwenye maisha yao, anawataja waumini kwamba ni wale wanaotulizana kwa dhikri ya Mwenyezi Mungu. Kutua au kutulizana moyo maana yake ni kuzidi asili ya imani; yaani uthabiti wa imani na utulivu wake. Kuna Aya inayosema:

قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ﴿٢٦٠﴾

“(Mwenyezi Mungu) akasema: Huamini? Akasema: Kwa nini! (naami-ni) Lakini upate kutulia moyo wangu.” Juz. 3 (2:260)

وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ ﴿١٠٦﴾

Na hali ya kuwa moyo wake umetulia juu ya imani (16:106).

Makusudio ya Dhikr sio kutamka maneno tu; isipokuwa ni dhikri ambayo inamzidisha yakini ya Mwenyezi Mungu yule mwenye kudhukuru na akawa ana mategemeo ya ahadi na miadi yake Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo dhikri ya matamshi tu na tasbihi sio dhikr ya kiuhakika. Dhikri inayozidisha yakini ni ile aliyoisema Mwenyezi Mungu:

فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ ﴿١٥٢﴾

Basi nidhukuruni nitawadhukuru Juz 2 (2:152).

Wale ambao wameamini na wakafanya matendo mema, raha ni yao na marejeo mazuri.

Makusudio ya raha ni Pepo. Aya hii inaoana na ile isemayo:

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ﴿٢٥﴾

Wabashirie wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, kwamba watapata mabustani yapitayo mito chini yake Juz.1 (2:25).