TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 8972
Pakua: 2090


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 8972 / Pakua: 2090
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE Juzuu 14

Mwandishi:
Swahili

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَا يَبْعَثُ اللَّـهُ مَن يَمُوتُ بَلَىٰ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٨﴾

38. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu (kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu. Ndio! Ni ahadi iliyo lazima kwake, lakini watu wengi hawajui

لِيُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي يَخْتَلِفُونَ فِيهِ وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّهُمْ كَانُوا كَاذِبِينَ ﴿٣٩﴾

39. Ili awabainishie yale walioyokhitalifiana na ili wajue waliokufuru kwamba wao walikuwa waongo.

إِنَّمَا قَوْلُنَا لِشَيْءٍ إِذَا أَرَدْنَاهُ أَن نَّقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٤٠﴾

40. Kauli yetu kwa kitu tunachokitaka kiwe, ni kukiambia: Kuwa tu! Basi kinakuwa.

وَالَّذِينَ هَاجَرُوا فِي اللَّـهِ مِن بَعْدِ مَا ظُلِمُوا لَنُبَوِّئَنَّهُمْ فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَلَأَجْرُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾

41. Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, hakika tutawaweka katika dunia kwa wema. Na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi, lau wangelikuwa wanajua.

الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٤٢﴾

42. Wale wanosubiri na wakamtegemea Mola wao.

WANAAPA KWA MWENYEZI MUNGU

Aya 38 – 42

MAANA

Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu.

Katika Aya ya 20 ya Sura hii, Mwenyezi Mungu aliwaambia washirikina kuwa nyinyi mnaabudu aliyeumbwa badala ya kumwabudu muumbaji, Katika Aya ya 24, amewasimulia kuwa wameibandaka jina Qur’an kuwa ni ngano za watu wa kale. Katika Aya ya 35 ametaja Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa wao wanategemeza shirki yao na shirki ya mababa zao kwa Mwenyezi Mungu.

Katika Aya hii tuliyonayo Mwenyezi Mungu anasema kuwa wao wanapinga ufufuo, wakiapa viapo vya nguvu na kufanya juhudi kueleza kuwa mwenye kufa yake yamekwisha, kwa sababu kitu kikitawanyika hakiwezi kujirudia mara ya pili.

Hayo tumeyazungumzia katika Juz, 13 (13:5).

(Kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu, Ndio! Ni ahadi iliyo lazima kwake, lakini watu wengi hawajui.

Washirikina walikuwa wakiaamini kuweko Mwenyezi Mungu na kuweko washirika wake na walikuwa wakipinga ufufuo. Kwa vile wao wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu, ndio likaja jibu kuwa ufufuo uko tu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu wanayemwamini kuwa yuko, ndiye aliyetoa ahadi ya ufufuo na ahadi yake ni kweli. Ama kuvikusanya viungo baada ya kutawanyika kwake, hilo ni jepesi zaidi kuliko kuviumba. Kwa sababu ambaye amefanya kitu kilichokuwa hakipo basi ni rahisi zaidi kwake kuki kusanya baada ya kutawanyika.

Ili awabainishie yale walioyokhitalifiana na ili wajue waliokufuru kwamba wao walikuwa waongo.

Ufufuo una hekima nyingi sana; mingoni mwazo ni hizi zifuatazo:- Kujulikana mzuri na mbaya, mwema na muovu na malipo wanayostahiki. Hekima nyingine ni Mwenyezi Mungu kuwabainishia viumbe haki waliyokuwa wakihitalifiana; kama vile Tawhid, utume, halali na haramu.

Wale walioapa kuwa hakuna ufufuo wajue na wahakikishe kuwa wao walikuwa waongo katika viapo vyao.

Kauli yetu kwa kitu tunachokitaka kiwe, ni kukukiambia: Kuwa tu! Basi kinakuwa.

Mwenyezi Mungu alianza kuumba kwa neno ‘kuwa’ na atarudisha kwa neno hilohilo, “Na hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi na Yeye ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhu- lumiwa, hakika tutawaweka katika dunia kwa wema.

Aya hii inawahusu moja kwa moja waliohama (wahajiri) katika maswahaba wa mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ambao walipata mtihani mwema kwa kumsaidia Mtume; wakacha dunia, watu wao na mali zao kwa kukimbia na dini yao na kumfuata Mtume wao kwa ajili ya kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ama wema ambao Mwenyezi Mungu amewapa duniani kabla ya Akhera ni majumba yao na milki zao mpya hapo Madina, kwani zilikuwa ni bora kuliko zile za Makka.

Na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi kuliko dunia na vilivyomo lau wangelikuwa wanajua!

Maneno hapa, wanaambiwa washirikina ambao walipinga ufufuo, Ama waumini, hasa maswahaba, wao wanajua kwa yakini kuwa thawabu za Akhera ni kubwa na adhimu zaidi. Tumezungumzia kuhusu Hijra na wahajiri katika Juz. 5 (4: 97 – 100) na kuhusu Wahajiri na Answari katika Juz. 10 (72 – 75).

Wale wanosubiri na wakamtegemea Mola wao.

Hakika Mumini wa kweli ana sifa na alama. Zilizo muhimu zaidi ni hizi zifuatazo:-Kuacha ubinafsi, kujitoa mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuvumilia maudhi na mashaka kwa ajili ya kuihakikisha haki na kuibatilisha batili na kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake, sio mali wala cheo au ukoo; sawa na walivyokuwa maswahaba wa Mtume mtukufu(s.a.w.w) .

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِمْ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٤٣﴾

43. Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi, Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.

بِالْبَيِّنَاتِ وَالزُّبُرِ وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٤٤﴾

44. Kwa hoja zilizo wazi na kwa Vitabu. Na tumekuteremshia ukumbusho ili uwabainishie watu yale waliyoteremshiwa wapate kufikiri.

أَفَأَمِنَ الَّذِينَ مَكَرُوا السَّيِّئَاتِ أَن يَخْسِفَ اللَّـهُ بِهِمُ الْأَرْضَ أَوْ يَأْتِيَهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٤٥﴾

45. Je, wameaminisha waliofanya vitimbi vya uovu kwamba Mwenyezi Mungu awadidimize katika ardhi au iwafikie adhabu kutoka wasipopajua?

أَوْ يَأْخُذَهُمْ فِي تَقَلُّبِهِمْ فَمَا هُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٤٦﴾

46. Au Awakamate katika nyendo zao na wasiweze kuponyoka?

أَوْ يَأْخُذَهُمْ عَلَىٰ تَخَوُّفٍ فَإِنَّ رَبَّكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٤٧﴾

47. Au awakamate kidogo kidogo? Kwani hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma.

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ يَتَفَيَّأُ ظِلَالُهُ عَنِ الْيَمِينِ وَالشَّمَائِلِ سُجَّدًا لِّلَّـهِ وَهُمْ دَاخِرُونَ ﴿٤٨﴾

48. Je hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu vivuli vyao vinaelekea kuliani na kushotoni vikimsujudia Mwenyezi Mungu na vikimnyenyekea?

وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مِن دَابَّةٍ وَالْمَلَائِكَةُ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ﴿٤٩﴾

49. Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika, nao hawatakabari.

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ﴿٥٠﴾

50. Wanamhofia Mola wao aliye juu yao na wanafanya wanayoamriwa.

WAULIZENI WENYE UKUMBUSHO

Aya 43 – 50

MAANA

Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi.

Washirikina waliukana utume wa Muhammad na wakasema kuwa Mwenyezi Mungu hakutuma mtu kuwa mjumbe. Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao kwamba mitume na Manabii wote waliotangulia walikuwa ni watu wanaume wakiletewa wahyi; kama vile: Nuh, Ismail, Musa na wengineo. Kwa sababu lengo la kutumwa Mtume haliwezi kutimia ila ikiwa aliyetumwa ni jinsi ya wale waliotumiwa:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ﴿٤﴾

“Na hatukumtumma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia.” Juz. 13 (14:4)

قُل لَّوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَّسُولًا ﴿٩٥﴾

“Sema: Ingelikuwa katika Ardhi kuna malaika wanotembea katika ardhi kwa utulivu, basi hakika tungeliwateremshia Malaika kuwa ni mitume wao” (17:95).

Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.

Makusudio ya wenye ukumbusho hapa ni wenye elimu wanaochunga haki; ni sawa wawe ni katika Watu wa kitab au wengineo. Maana ni kuwa enyi washirikina! Mkiwa na shaka na maneno yetu, basi waulizeni wajuzi wawambie kuwa mitume wote walikuwa ni watu.

Kwa hoja zilizo wazi na kwa Vitabu.

Yaani Mwenyezi Mungu aliwatuma Mitume wakiwa na hoja zilizowazi ambazo ni dalili na ishara. Na kwa vitabu ambavyo vina ubainifu wa dini, itikadi na sharia.

Na tumekuteremshia ukumbusho ili uwabainishie watu yale waliyoteremshiwa wapate kufikiri.

Maneno anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) , Makusudio ya ukumbusho hapa ni Qur’an. Ilivyo hasa ni kuwa lengo la kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu ni kuwaongoza watu kwenye haki na uadilifu na maisha ya amani na raha.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wapate kufikiri’ ni kuwa wapate kuizingatia vizuri Qur’an na kugundua siri zake na malengo yake wapate kujua kuwa imeteremshwa kwa maslahi yao.

Je, wameaminisha waliofanya vitimbi vya uovu.

Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya waliofanya vitimbi hapa ni washirikina wa kiquraish, kwa vile wao ndio waliomfanyia uovu Mtume(s.a.w.w) na wakamfanyia njama. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewahofisha na aina nne za adhabu:

1.Kwamba Mwenyezi Mungu awadidimize katika ardhi; kama alivyomfanyia Qarun:

فَخَسَفْنَا بِهِ وَبِدَارِهِ الْأَرْضَ فَمَا كَانَ لَهُ مِن فِئَةٍ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُنتَصِرِينَ ﴿٨١﴾

“Na tukamadidimiza yeye na nyumba yake, wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia zaidi ya Mwenyezi Mungu” (28:81)

2.Au iwafikie adhabu kutoka wasipopajua , awaangamize ghafla, kama alivyofanya kwa watu wa Lut.

3.Au awakamate katika nyendo zao na wasiweze kuponyoka , Yaani awaangamize wakiwa wanashughulika kutafuta riziki.

4.Au awakamate kidogo kidogo.

Neno kidogo kidogo, limefasiriwa kutokana na neno takhawwuf; kama walivyosema wafasiri wengi wakiongozwa na Tabrasi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatawaangamiza mara moja bali atawapa balaa ya kupungukiwa na watu na mali kidogo kidogo mpaka wa mwisho wao.

Kwani hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma.

Miongoni mwa huruma zake ni kutowaharakishia adhabu wanayostahiki waasi, kwa kutumai kuwa watatubia na kuongoka.

Je hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu vivuli vyao vinaelekea kuliani na kushotoni vikimsujudia Mwenyezi Mungu na vikimnyenyekea.

Wanaoambiwa hapa ni wale waliofanya vitimbi vya uovu, waliotajwa katika Aya iliyotangulia na pia inawezekana wanaambiwa watu wote. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema kwa kuwatahayariza wapinzani wenye inadi.

Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Vivuli vinaelekea’ ni kuwa kila kitu kina kivuli; kama vile milima, miti, wanyama, majengo n.k. Na kauli yake: ‘kuliani na kushotoni’ ni ishara ya upande wa kitu kilicho na kivuli. Kwa sababu kivuli cha kitu kinakuwa upande mmoja kuanzia mawiyo hadi Adhuhuri na kinageuka upande wa pili kuanzia adhuhri hadi machweo.

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaleta ibara ya kulia kwa upande mmoja na ibara ya kushoto kwa upande wa pili. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu: “ Na vivuli vyao asubuhi na jioni” Juz. 13 (13: 15) Ama kauli yake vikimsujudia Mwenyezi Mungu ni fumbo la utiifu. Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu alipotaja kulia ametaja kwa tamko la umoja na alipotaja kushoto akatumia tamko la wingi (yamin wa shamail)[4] ?

Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu ambayo la karibu zaidi ni kuwa mfumo wa fasihi ya kiarabu wakitaja vitu viwili vyenye maana mbili tofauti kimoja kinatajwa kwa umoja na kingine kwa wingi; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu: “Amejaalia viza na mwanga.”

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kuwahadharisha washirikina na wenye inadi, anasema katika Aya hii, kwamba kila kilicho ulimwenguni – isipokuwa washirikina na wenye inadi – vinamnyenyekea na kufuata amri yake.

Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika nao hawatakabari.

Viumbe vyote vya juu na chini vinafahamisha waziwazi kuweko aliyevifanya na kufahamisha uweza wake, elimu yake na hekima yake na dalili hii ndio tasbihi, tahmid, sujudi na rukui kwa muumbaji.

Pia haya ndio makusudio ya kusujudi kwa viumbe visivyo na akili; kama ambavyo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na hakuna kitu chochote ila kinamtakasa kwa sifa zake” (17: 44). Lengo la kutaja wanyama na Malaika, baada ya kutaja vilivyo katika mbingu na ardhi, ni ubainifu wa kuchanganya aina zote za viumbe, Yametangulia maelezo yake katika Juz, 13 (13:13-25).

Wanamhofia Mola wao aliye juu yao na wanafanya wanayoamriwa.

Aya hii inafahamisha waziwazi kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu humhofia na hutii amri yake na makatazo yake, na inafahamisha katika madhumuni yake kwamba mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu kisha akadai kuwa anamwamini na anamhofia, basi huyo ni mwongo katika madai yake.

وَقَالَ اللَّـهُ لَا تَتَّخِذُوا إِلَـٰهَيْنِ اثْنَيْنِ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ ﴿٥١﴾

51. Na amesema Mwenyezi Mungu: Msiabudu miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu. Basi niogopeni mimi tu.

وَلَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَهُ الدِّينُ وَاصِبًا أَفَغَيْرَ اللَّـهِ تَتَّقُونَ ﴿٥٢﴾

52. Ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, na dini ni yake Yeye daima, Je, mtamcha mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu?

وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ ﴿٥٣﴾

53. Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu, Kisha ikiwagusa dhara mnamlilia yeye.

ثُمَّ إِذَا كَشَفَ الضُّرَّ عَنكُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنكُم بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ ﴿٥٤﴾

54. Kisha anapowaondolea dhara, kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao.

لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ فَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٥٥﴾

55. Ili wakufuru tuliyowapa, Basi stareheni mtakujajua.

HAKIKA YEYE NI MUNGU MMOJA TU

Aya 51 – 55

MAANA

Na amesema Mwenyezi Mungu: Msiabudu miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu. Basi niogopeni mimi tu.

Kuna desturi maarufu kwa wanafiqhi isemayo: Hakika dharura hupimwa kwa kiasi chake na kwamba kinachozidi haja na dharura basi ni upuzi.

Desturi hii tunaweza kuitumia kwa yule anayemshirikisha Muumba, kwamba kuchukulia kuwa kuna Muumba mwenye kupanga vizuri mambo na mwenye hekima ni jambo la lazima halikimbiliki katika mtazamo wa kiakili, ambapo haiwezekani kuufasiri ulimwengu na vilivyomo ndani yake kuanzia nidhamu na mfumo isipokuwa lazima awepo mpangaji wa hayo Mwenye hekima.

Kwa hiyo baada ya kuchukulia huku haiwezekani kubakia madai yoyote ya kuchukulia kuwa kuna Mungu mwingine, katika mtazamo wa kiakili; bali akili inalikataa hilo, Angalia katika Juz. 5 (4:48-50) kifungu ‘Dalili ya umoja na utatu’.

Kisha umoja wa Mwenyezi Mungu una athari na mambo yanayolazimiana nao, ameyadokeza Mwenyezi Mungu kwa kauli yake kama yafuatavyo:-

1.Ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini.

Hilo halina upinzani wala ubishi, kwa sababu yeye ndiye aliyeiumba mbin- gu na ardhi na viliyvomo ndani yake.

2.Na dini ni yake Yeye daima.

Makusudio ya dini hapa ni kufuatwa na utiifu. Ikiwa Mwenyezi Mungu ni muumba na mmiliki wa kila kitu basi imethibitika kuendelea kutiiwa Yeye tu si mwenginewe.

3.Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu,

Kwa sababu Yeye ni Muumba wa kila kitu moja kwa moja kwa neno ‘kuwa na kikawa’ au kupitia kitu kingine.

Kisha ikiwagusa dhara mnamlilia Yeye; kisha anapowaondolea dhara, kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao.

Muumin wa kweli anamtegemea Mwenyezi Mungu katika hali zote, lakini mfanyabiashara humkimbilia Mwenyezi Mungu wakati wa dhiki na anajipurukusha naye wakati wa raha. Umepita mfano wa Aya hii katika Juz, 11 (10: 12).

Ili wakufuru tuliyowapa.

Makusudio ya kukufuru hapa ni kukufuru neema; zikiwemo kuondolewa madhara. Maana ya ‘ili’ ni natija; kama kusema amejitia kwenye hatari ili afe.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaneemesha lakini natija ya neema yake ikawa ni kukufuriwa neema zake.

Basi stareheni mtakujajua mwisho wenu mbaya na mtajuta, ambapo hakutafaa chochote kujuta kwenu.

وَيَجْعَلُونَ لِمَا لَا يَعْلَمُونَ نَصِيبًا مِّمَّا رَزَقْنَاهُمْ تَاللَّـهِ لَتُسْأَلُنَّ عَمَّا كُنتُمْ تَفْتَرُونَ ﴿٥٦﴾

56. Na ambao hawajui wanawawekea sehemu ya tunavyowaruzuku. Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua.

وَيَجْعَلُونَ لِلَّـهِ الْبَنَاتِ سُبْحَانَهُ وَلَهُم مَّا يَشْتَهُونَ ﴿٥٧﴾

57. Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu mabinti. Ametakata na hayo! Na hali wao hupata wanavyovitamani.

وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِالْأُنثَىٰ ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٥٨﴾

58. Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.

يَتَوَارَىٰ مِنَ الْقَوْمِ مِن سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ أَيُمْسِكُهُ عَلَىٰ هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُ فِي التُّرَابِ أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ﴿٥٩﴾

59. Anajificha na watu kwa ubaya wa aliyobashiriwa. Je, akae naye juu ya fedheha au amfukie mchangani, Ehe! Yamekuwa maovu wanayoyahukumu.

لِلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ مَثَلُ السَّوْءِ وَلِلَّـهِ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٦٠﴾

60. Sifa ya wale wasioamini Akhera ni uovu na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu na Yeye ni Mwenye nguvu Mwenye hekima.

WANAMFANYIA MWENYEZI MUNGU MABINTI

Aya 56 – 60

MAANA

Na ambao hawajui wanawawekea sehemu ya tunavyowaruzuku, Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua.

Wanaoweka ni washirikina na wanaowawekea ni masanamu. Imesemwa ‘hawajui’ kwa masanamu badala ya ‘hayajui’ kwa vile wao wameyaweka daraja ya wenye akili; kama vile ilivyosemwa katika Aya ya 20 ya Sura hii: “Na wale ambao wanawaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.” Kwa hiyo Qur’an imelitumia neno hilo kulingana na itikadi ya washirikina.

Maana ni kuwa washirikina waliyawekea, fungu katika mali zao, masana- mu ambayo yameganda hayana chochote yajualo wala hisia zozote.

Inawezekana kuwa ‘ambao hawajui’ ni washirikina. Kwa maana ya kuwa washirikina waliyawekea fungu masanamu wakiwa hawajui kuwa masanamu hayana fungu lolote katika mali zao wala katika zisizokuwa mali zao. Lakini kufasiri kwa maana haya kunakalifisha kukadiria maneno yasiyokuwepo. Umepita mfano wake katika Juz. 8 (6: 136).

Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu mabinti, Ametakata na hayo! Na hali wao hupata wanavyovitamani

Waliposikia kuwa Mwenyezi Mungu ana Malaika wakafikiria ni wanawake tena ati ni mabinti wa Mungu. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanayomsifu. Wakamabandikiza yale wanayoyachukia wao, huku wenyewe wakiwa na wavulana wanaowapenda. Mwenyezi Mungu anasema: “Je, Mola wenu amewachagulia wavulana na Yeye akawafanya Malaika ni wanawake? Kwa hakika nyinyi mnasema kauli kubwa (17: 40).

Baadhi ya tafsiri zinasema kuwa walioitakidi hivi ni Bani Khuza’a na Kinana.

Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.

Qur’an hutumia neno ‘bishara’ kwa habari njema na mbaya; kwa mfano:

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ﴿٢٥﴾

“Na wabashirie walioamini na wakafanya vitendo vizuri, kwamba watapata mabustani”

Juz,1 (2:25).

وَبَشِّرِ الَّذِينَ كَفَرُوا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣﴾

Na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo, Juz, 10 (9:3).

Kusawijika uso ni fumbo la kuhuzunika sana. Waarabu hulitumia neno hilo kwa mtu aliyepatwa na mambo ya kuchukiza.

Ingawaje hii ni desturi ya kijahili na Qur’an ikaikemia na kuwasafihi watu wake, lakini kuna Waislamu wengi wanachukia kupata watoto wasichana, na wanasawijika nyuso wakipewa habari za kuzaliwa msichana.

Anajificha na watu kwa ubaya wa aliyobashiriwa.

Wakati wa jahiliya, mtu akiwa mkewe anaanza uchungu wa kuzaa anajificha mpaka ajuea atakayezaliwa, akiwa ni mwanamume anajitokeza na kufurahi na akiwa ni mwanamke huhuzunika na kufikiria afanye nini.

Je, akae naye juu ya fedheha abakie na udhaliliau amfukie mchangani akiwa hai? Imesimuliwa kuwa baadhi ya waarabu walikuwa wakiwazika hai watoto wao wa kike, wengine wakiwatupa, wengine wakiwachinja na hata wengine walikuwa wakiwatosa.

Walikuwa wakifanya hivyo ama kwa hasira au kwa kuogopa ukata; kama alivyodokeza Mwenyezi Mungu kwa kusema: “Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao.” Juz. 8 (6:151).

Imesimuliwa kuwa mtu mmoja alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: mimi sina raha tangu nisilimu. Kwani nilikuwa na binti wakati wa ujahili, nikamwaamrisha mke wangu ampambe kisha nikatoka naye hadi kwenye bonde lenye kina nikamtupa huko, akaniambia: ‘Baba yangu unaniua! Kila ninapokumbuka kauli yake hiyo sioni kitu chochote kinachonifaa.

Inaweza kudhania kuwa ukatili huu unatokana na ujinga na kutoendela, lakini sisi hivi sasa tuko kwenye zama za kutembea angani, bado wakoloni na wazayuni wanatupa makombora kwa vikongwe, wanawake na watoto huko Vietnam na Palestina.

Wanayatupa sio kwa hasira za kijinga wala kuhofia ukata; isipokuwa ni kwa sababu ya kuzidisha faida na kurundika utajiri. Sasa ni nani kati ya makundi mawili haya ndio walio waovu zaidi. Je, watu wa jahilia au ni wakoloni na wazayuni walio katika wakati wa elimu na mwanga?

Ehe! Yamekuwa maovu wanayoyahukumu na wanayoyazua na kuyafanya, Sisi tuna hakika kabisa kuwa kila mwenye kuzama kwenye uovu mwisho utamrudia mwenyewe.

Sifa ya wale wasioamini Akhera ni uovu na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Mataghuti wana sifa mbaya ambayo ni dhulma, unyang’anyi, ufisadi na kuua watoto na wasio na hatia. Na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu ambazo ni umoja, uadilifu, utukufu na sifa zote nzuri za ukamilifu.

Ilivyo ni kuwa lengo la kutaja sifa za Mwenyezi Mungu pamoja na kuwataja wao ni kujibu kauli yao kuwa Mungu ana wasichana na wao wana wavulana.

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِظُلْمِهِم مَّا تَرَكَ عَلَيْهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ ﴿٦١﴾

61. Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa dhulma yao asingeliacha juu yake hata mnyama mmoja, lakini anawaakhirisha mpaka muda uliowekwa, Utakapofika muda wao hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia.

وَيَجْعَلُونَ لِلَّـهِ مَا يَكْرَهُونَ وَتَصِفُ أَلْسِنَتُهُمُ الْكَذِبَ أَنَّ لَهُمُ الْحُسْنَىٰ لَا جَرَمَ أَنَّ لَهُمُ النَّارَ وَأَنَّهُم مُّفْرَطُونَ ﴿٦٢﴾

62. Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu yale wanayoyachukia, Na ndimi zao zitasifia uwongo kwamba wao watapata mema, Hapana shaka hakika wamewekewa moto nao watatangulizwa.

تَاللَّـهِ لَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ أُمَمٍ مِّن قَبْلِكَ فَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَهُوَ وَلِيُّهُمُ الْيَوْمَ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

63. Wallahi! Tulituma kwa umma zilizokuwa kabla yako, Lakini shetani aliwapambia vitendo vyao. Kwa hiyo leo huyo ndiye msimamizi wao na wana wao adhabu chungu.

وَمَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ إِلَّا لِتُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي اخْتَلَفُوا فِيهِ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٦٤﴾

64. Na hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitalifiana na kiwe ni uongofu na rehema kwa watu wanaoamini.

MWENYE KUHOFIA MAUTI HUHARAKISHWA

Aya 61 -64

MAANA

Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa dhulma yao asingeliacha juu yake hata mnyama mmoja, lakini anawakhirisha mpaka muda uliowekwa

Juu yake hapa ni juu ya Ardhi, kutokana, mfumo wa maneno ulivyo na pia neno mnyama linafahamisha hivyo. Mtu amemdhulumu Muumba wake kwa kumkana, kumfanyia washirika na kuwa ana mtoto. Vile vile mtu mwenye nguvu amemdhulumu ndugu yake mdhaifu, akamafanya mtumwa na akampora nguvu yake na nyenzo za maisha yake.

Pia mwenye kiburi amejidhulumu kwa kupetuka mipaka na ghururi. Lakini pamoja na yote hayo Mungu hakumharakishia adhabu; Kwani ana haraka ya nini? Anaogopa wakati usimpite au anahofia waasi wasitubie; na yeye ndiye aliyewahimiza kufanya hivyo?

Imesemekana kuwa anawacheleweshea ili waweze kurejea kwenye toba. Hilo haliko mbali kutokana na upole, huruma na ukarimu wake.

Aya hii inafanana na ile isemayo: “Na Mola wako ni mwenye maghufira, mwenye rehema. Lau angeliwachukulia kwa yale waliyoyachuma angeliwaharakishia adhabu, lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya kuepukana nayo” (18: 58).

Utakapofika muda wao hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia.

Imetangulia tafsiri yake katika Juz; 4 (3: 144 -148) kifungu cha ‘Ajali haina kinga’ Pia imetajwa neno kwa neno katika Juz; 8 (7:34).

Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu yale wanayoyachukia wao ya kuwa na mabinti na kushirikiana uongozi.

Na ndimi zao zitasifia uwongo kwa kusema kwaokwamba wao watapata mema; yaani Pepo.

Wamemzulia Mwenyezi Mungu kwamba Yeye ana washirika na ana mabinti; kisha wakasema uwongo kwamba wao watapata Pepo; ndio Mwenyezi Mungu akawakadhibisha kwa kusema:Hapana shaka hakika wamewekewa moto nao watatangulizwa; yaani wataharakishwa.

Wallahi! Tulituma – Mitume –kwa umma zilizokuwa kabla yako ewe Muhammad, lakini hawakuwaitikia mitume wao, bali waliachana nao na wakawaudhi; kama walivyokufanyia wewe washrikina wa kiqurayishi, basi poa moyo wala usihuzunike.

Lakini shetani aliwapambia vitendo vyao ambavyo ni kufru, upotevu, ukiukaji mipaka na ufisadi.

Kwa hiyo leo huyo ndiye msimamizi wao leo na wana wao adhabu chungu.

Shetani alitawala mambo ya mataghuti katika maisha ya dunia baada ya kumpa hatamu za uongozi, kwa hiyo akawaongoza kwenye madhambi na maangamizi. Basi malipo yake na yao kwa Mwenyezi Mungu ni Jahannam, ni mahali pabaya kabisa.

Imam Aliy anasema: “Ajali ya mtu imefichwa, tamaa yake imemhadaa, na shetani ni wakala wake, anampambia maasi ili ayafanye, na anamdhoofisha na toba ili aipe muda. Mpaka ukifika muda anaghafilika na aliyokuwa nayo” yaani anakufa kwenye upotevu na maasi, nayo ni mauti mabaya.

Na hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitalifiana na kiwe ni uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini

Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) na Kitabu ni Qur’an nayo ni uwongofu na rehema kwa mwenye kutaka. Pia ndiyo hukumu inayofafanua kila itikadi na kila sharia na ni kauli na vitendo, “Ewe Mola utujaalie ni wenye kushikamana na kamba yake na kuongoka na uongozi wake”.

وَاللَّـهُ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ ﴿٦٥﴾

65. Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaosikia.

وَإِنَّ لَكُمْ فِي الْأَنْعَامِ لَعِبْرَةً نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهِ مِن بَيْنِ فَرْثٍ وَدَمٍ لَّبَنًا خَالِصًا سَائِغًا لِّلشَّارِبِينَ ﴿٦٦﴾

66. Na katika wanyama mna mazingatio. Tunawanywesha katika vile vilivyomo matumboni mwao, vikatoka, baina ya kinyesi na damu, maziwa safi, mazuri kwa wanywao.

وَمِن ثَمَرَاتِ النَّخِيلِ وَالْأَعْنَابِ تَتَّخِذُونَ مِنْهُ سَكَرًا وَرِزْقًا حَسَنًا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾

67. Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza kileo na riziki nzuri. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaotumia akili.

وَأَوْحَىٰ رَبُّكَ إِلَى النَّحْلِ أَنِ اتَّخِذِي مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا وَمِنَ الشَّجَرِ وَمِمَّا يَعْرِشُونَ ﴿٦٨﴾

68. Na Mola wako akampa wahyi nyuki kwamba, tengeneza nyumba katika milima, na katika miti, na katika wanaoyajenga.

ثُمَّ كُلِي مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ فَاسْلُكِي سُبُلَ رَبِّكِ ذُلُلًا يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاءٌ لِّلنَّاسِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٦٩﴾

69. Kisha kula katika kila matunda na ufuate njia za Mola wako zilizo dhalili. Na katika matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbalimbali, ndani yake kina matibabu kwa watu. Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaofikiri.

MWENYEZI MUNGU AMETERMSHA MAJI KUTOKA MBINGUNI

Aya 65 – 69

NAHAW (SARUFI)

Katika Juz. 7 (6: 134) Mwenyezi Mungu amerudisha dhamir ya wanyama kwa muannath ( ya kike) na hapa ameirudisha kwa dhamir ya mudhakkar (ya kiume). Wamejibu kwamba dhamir hapa inarudia kwenye baadhi; yaani baadhi ya wanyama ambao ni wakike, na kule inarudia kwa wanyama wote.

MAANA

Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaosikia kwa kuzingatio na kutilia manani maji na faida zake.

Aya hii na inayofuatia ni katika Aya za mambo ya ulimwengu ambazo Qur’an inazikariri kwa lengo la kuleta uzinduzi kwenye dalili za Tawhid na ufufuo, Aya hii imekwishapita katika Juz.1 (2:22, 164), Juz. 7: (6:99), Juz. 13 (13: 17), (14: 32) na sura hii tunayoifasiri Aya ya 6.

Na katika wanyama mna mazingatio, Tunawanywesha katika vile vilivyomo matumboni mwao, vikatoka, baina ya kinyesi na damu, maziwa safi, mazuri kwa wanywao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja baadhi ya faida za wanyama katika Juz; 8 (6:142) aliposema: “Na katika wanyama wale wabebao na wa kutoa matandiko.”

Katika sura hii tuliyo nayo, mbele, kwenye Aya 80, amesema: “Na akawafanyia kutokana na ngozi za wanyama wenu nyumba mnazoziona nyepesi siku ya kusafiri kwenu na siku ya kutulia kwenu.

Na katika sufu zao na manyoya yao na nywele zao mnatengeneza vyombo na vifaa vya kutumia kwa muda.” Mwanzoni mwa sura hii amekusanya faida za wanyama kwa kuhusisha maziwa akasema kuwa yanatoka katika matumbo ya baadhi ya wanyama; yaani wa kike, Angalia kifungu cha Nahw.

Wataalamu wanasema kuwa wanyama wanakula mimea, baada ya kutafuna matumbo yanatoa nje kinyesi chenye madhara na kufyonza majimaji yenye manufaa ambayo yanageuka damu inayotembea kwenye mishipa. Baadhi ya damu hii inapofika kwenye viwele inageuka na kuwa maziwa safi ya kunywa.

Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza kileo na riziki nzuri. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaotumia akili

Dhahiri ya neno kileo hapa ni kinywaji chochote kinacholevya, kiwe ni pombe au kitu kingine. Lakini Aya haidokezi hukumu ya ulevi kwa umbali wala karibu; kwamba wakati huo iliposhuka ulevi ulikuwa halali au haramu; isipokuwa inaelezea desturi ya watu kwamba wao wanatengeneza kinywaji na ulevi kutokana na matunda ya mitende na mizabibu. Ama riziki nzuri makusudio yake ni tende mbichi na za kuiva, zabibu mbichi na kavu, siki, jamu n.k.

Yamekuja maelezo kutoka baadhi ya mapokezi kwamba makusudio ya kileo katika Aya, ni kilicho haramu na riziki nzuri ni kilicho halali.

Tumefafanua dalili za uharamu wa pombe katika Juz. 2 (2: 219) na pia katika kitabu Fiqhul-imam Ja’far asswadiq Mlango wa Al-at’ima wa wal Ashriba (Vyakula na vinywaji)

Na Mola wako akampa wahyi nyuki.

Makusudio ya wahyi hapa ni maumbile ya akili ambayo Mwenyezi Mungu alimpa nyuki.

Kwamba tengeneza nyumba katika milima na katika miti na katika wanaoyajenga.

Yaani wanayoyajenga watu.

Razi anasema: “Kuna aina mbili za nyuki: Ile inayokaa milimani na kwenye misitu, hawashughulikiwi na mtu yoyote. Ndio makusudio ya kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Kwamba tengeneza nyumba katika milima na katika miti’ na aina nyingine inakaa katika majumba ya watu na wanashughulikiwa na watu. Ndio makusudio ya kauli yake: ‘katika wanaoyajenga’.

Kisha kula katika kila matunda maua na mimea unayoipenda,Na ufuate njia za Mola wako zilizo dhalili. Yaani ni dhalili kwa kwa ajili yako wewe nyuki ili upate wepesi wa kupita

Na katika matumbo yao kinatoka kinywaji amabacho ni asali wanayoitema kama mate.Chenye rangi mbali mbali nyeupe, nyekundu na yanjano, kulingana na mimea waliyokula.

Ndani yake kina matibabu kwa watu; kama vile ukosefu wa damu, kutosagika vizuri chakula tumboni, vidonda vya mdomoni, matatizo ya mapafu na kibofu cha mkojo. Pia maradhi ya figo na mengineyo waliyoyataja watabibu.

Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaofikiri katika alivyoviumba Mwenyezi Mungu na maajabu yake yanayofahamisha kuweko mpangiliaji hodari Mwenye hekima.

Wataalamu wameandika mengi kuhusu mipangilio ya hali ya juu ya nyuki, nidhamu yake na jinsi wanavyosaidiana katika maisha yao, kujenga nyumba na usalam, Huko nyuma tumeashiria kwamba hatimae imegunduliwa kuwa linapozidi joto nyuki huanza kazi ya kuchukua maji kwenye visiku vyao.

Wengine wanayanyunyiza ndani ya masega na wengine wanatingisha mbawa zao ili wafanye tiyara ya hewa. Kwa hiyo maji yananyunyizika kwa haraka jambo ambalo linafanya joto lipungue.

Mfano huu pekee unatosheleza yote yaliyoandikwa kuhusiana na mpangilio wa nyuki.

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ ثُمَّ يَتَوَفَّاكُمْ وَمِنكُم مَّن يُرَدُّ إِلَىٰ أَرْذَلِ الْعُمُرِ لِكَيْ لَا يَعْلَمَ بَعْدَ عِلْمٍ شَيْئًا إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ قَدِيرٌ ﴿٧٠﴾

70. Na Mwenyezi Mungu amewaumba kisha anawafisha, na miongoni mwenu wapo wanaorudishwa kwenye umri dhaifu kabisa ili asijue kitu baada ya kujua. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye uweza.

وَاللَّـهُ فَضَّلَ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الرِّزْقِ فَمَا الَّذِينَ فُضِّلُوا بِرَادِّي رِزْقِهِمْ عَلَىٰ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَهُمْ فِيهِ سَوَاءٌ أَفَبِنِعْمَةِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ ﴿٧١﴾

71. Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki, Na wale waliofadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ambao imewamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo, Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَتِ اللَّـهِ هُمْ يَكْفُرُونَ ﴿٧٢﴾

72. Na Mwenyezi Mungu amewafanyia wake kutokana na nyinyi wenyewe. Na amewafanyia kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu na akawaruzuku vitu vizuri. Basi je, wanaamini upotofu na wanazikufuru neema za Mwenyezi Mungu?

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَهُمْ رِزْقًا مِّنَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ شَيْئًا وَلَا يَسْتَطِيعُونَ ﴿٧٣﴾

73. Na badala ya Mwenyezi Mungu wanaabudu wasiowamilikia riziki yoyote kutoka mbinguni na ardhini wala hawana uwezo.

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧٤﴾

74. Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Hakika Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.

MUNGU AMEFADHILISHA BAADHI YENU KATIKA RIZKI

Aya 70 – 74

MAANA

Na Mwenyezi Mungu amewaumba kisha anawafisha na miongoni mwenu wapo wanaorudishwa kwenye umri dhaifu kabisa ili asijue kitu baada ya kujua. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye uweza.

Mtu anapitia hatua nyingi, kuanzia utoto hadi ubarobaro na ujana. Na kuanzia ujana hadi uzee na ukongwe. Kila hatua ina sababu zake za kimaumbile. Zinategemezwa kwake Mwenyezi Mungu kwa vile Yeye ndiye aliyeyaumba maumbile.

Umri dhaifu ni ukongwe ambapo mwili, akili, kumbukumbu na hisia nyingine za ndani na nje zote zinaadhoofika. Na zikishadhoofika hivyo basi hapo ndio mwisho wake, hazitarajiwi kurudia hali yake ya kwanza; bali zinazidi kudhoofika kila siku zinaavyozidi kupita; hasa kumbukumbu, ndio zinaakosekana kabisa na kurudia hali ya utoto; kama kwamba hakuwahi kujifundisha chochote wala kufanya majaribio yoyote.

Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki, Na wale waliofadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ambao imewamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo, Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?

Baadhi wamefikiri dhahiri ya Aya hii inafahamisha kuwa riziki ni kwa qadha na qadari ya Mungu. Kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyemfanya huyu kuwa tajiri na yule kuwa fukara.

Lakini Aya iko mbali tena mbali, sana na maana haya, kwa sababu imeku- ja kuwarudi washirikina. Ufafanuzi wa hilo ni kwamba washirikina walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika, Mwenyezi Mungu akawarudi kwa kuwambia kuwa nyinyi washirikina hamridhii watumwa wenu washirikiane nanyi kwenye mali zenu na kuwa wao ni sawa na nyinyi katika riziki zenu na milki zenu.

Ikiwa nyinyi hamkubali hivyo, imekuwaje fahamu zenu zione kuwa ni sawa watumwa wa Mwenyezi Mungu wawe washirika wake katika kuumba kwake?

Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa hoja ya mantiki yao na makisio yao kwa kuwaambia: Nyinyi mnajifanya ni mabwana na mna watumwa wasiokuwa na chochote, basi ni kwa mantiki gani mkasema kuwa masanamu au wengineo katika watumwa wa Mungu wasiokuwa na chochote wawe wana chochote?

Unaweza kuuliza : Kauli ya Mwenyezi Mungu ‘Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki’ si inafahamisha kuwa kuzidiana riziki ni kwa qadha ya Mwenyezi Mungu na qadari yake?

Jibu : Tumekariri mara kwa mara kuwa kuitegemeza riziki kwa Mungu ni kwa upande wa kutegemeza kitu kwenye sababu yake ya kwanza na kwa kuizindua akili kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa ulimwengu na vilivyomo. Tumezungumzia kwa ufafanuzi suala hilo kwa anuani ya ‘Riziki na ufisadi’ kwenye Juz. 6 (5: 64-66) na kwa anuani ya ‘Je, riziki ni bahati au majaliwa?’ katika Juz, 7 (7:100), Pia ‘Mtu na riziki’ katika Juz, 13 (13: 26).

Na Mwenyezi Mungu amewafanyia wake kutokana na nyinyi wenyewe.

Yaani katika jinsi yenu, sio duni wala ya hali ya juu, ili ukamailike utu kwa pande mbili, zisadiane na zishirikiane katika maisha kwa pande zote.

Tafsiri iliyo wazi zaidi ya jumla hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ﴿٢١﴾

Na katika ishara zake ni kuwa amewaumbia wake zenu kutokana na nyinyi wenyewe ili mpate utulivu kwao na amejalia baina yenu mapenzi na huruma”(30:21).

Na amewafanyia kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja neema ya wake, sasa anataja neema ya watoto nao ni kipambo cha dunia kama mali.

Na akawaruzuku vitu vizuri : vyakula, vinywaji, kivazi, maskani na vipando kuongezea wake na watoto, Baada ya neema zote hiziBasi je, wanaamini upotofu?

Makusudio ya upotofu hapa ni wale wanaowashirikisha na Mungu kwa kuamini kuwa ndio wanaowapa neema wao au kwa kushirikiana na Mwenyezi Mungu.

Na wanazikufuru neema za Mwenyezi Mungu? kwa kula riziki yake na kumwabudu mwingine

Na badala ya Mwenyezi Mungu wanaabudu wasiowamilikia riziki yoyote kutoka mbinguni na ardhini wala hawana uwezo.

Riziki ya mbinguni ni mvua na riziki ya ardhini ni mimea na madini. Wasiowamilikia riziki ni masanamu. Maana ya kuwa hawana uwezo ni kuwa masanamu hayana uwezo kabisa wala kuweza kumiliki.

Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano kwa kumfanya kuwa ana wanoshabihiana naye: “Hapana kitu kama mfano wake, Na Yeye ni mwenye kusikia Mwenye kuona” (42:11).

Hakika Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.

Kutokana na elimu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na ujinga wenu, basi ni wajibu kwenu kutofanya au kusema jambo lolote isipokuwa yale aliyowafundisha Mwenyezi Mungu kupitia kwa manabii na mitume yake.