TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 14900
Pakua: 2111


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 19 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14900 / Pakua: 2111
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ وَيُبَشِّرُ الْمُؤْمِنِينَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ أَجْرًا كَبِيرًا ﴿٩﴾

9. Hakika hii Qur’an inaongoza kwenye yaliyonyooka kabisa na inawabashiria waumini ambao wanatenda mema kwamba watapata malipo makubwa.

وَأَنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٠﴾

10. Na kwamba wale wasioamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu.

وَيَدْعُ الْإِنسَانُ بِالشَّرِّ دُعَاءَهُ بِالْخَيْرِ وَكَانَ الْإِنسَانُ عَجُولًا ﴿١١﴾

11. Na mtu huomba shari kama vile aombavyo kheri. Na mtu amekuwa ni mwenye pupa.

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ آيَتَيْنِ فَمَحَوْنَا آيَةَ اللَّيْلِ وَجَعَلْنَا آيَةَ النَّهَارِ مُبْصِرَةً لِّتَبْتَغُوا فَضْلًا مِّن رَّبِّكُمْ وَلِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ وَكُلَّ شَيْءٍ فَصَّلْنَاهُ تَفْصِيلًا ﴿١٢﴾

12. Na tumeufanya usiku na mchana kuwa ni ishara mbili, Tena tukaifuta ishara ya usiku. Na tukaifanya ishara ya mchana ni ya kuangazia ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu, Na kila kitu tumekifafanua wazi wazi.

QUR’ANI INAONGOZA KWENYE YALIYONYOOKA

Aya 9 -12

MAANA

Hakik hii Qur’an inaongoza kwenye yaliyonyooka kabisa na inawabashiria waumini ambao wanatenda mema kwamba watapata malipo makubwa.

Yaliyonyooka kabisa ni mila au njia ambayo imenyooka. Neno hili lina maana ya kuenea masilahi zaidi kwenye kila kitu, wakati wowote, mahali popote na kwa mtu yeyote.

Aya hii ni madai yaliowazi yaliyosajiliwa na Qur’an anayoyaamini kila Mwislamu - kwamba Uislamu ndio dini bora zaidi ya dini zote. Dalili ya usahihi wa madai haya na ukweli wake ni Qur’an kutokana na itikadi yake, sharia yake na mafunzo yake mengine kuongezea sera ya mwenye ujumbe huo, Muhammad Bin Abdillah(s.a.w.w) ambaye ameijaza ardhi elimu, imani, wema na uadilifu baada ya kuwa na ujahili, kufuru na ufisadi.

Maulama wamethibitisha hakika hii na wakatunga mamia ya vitabu katika kufasiri maneno ya Mwenyezi Mungu na hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu na sera yake, itikadi sharia na maadili ya kiislamu ambayo yamethibitika katika nyanja mbalimbali, Tumetaja baadhi katika juzuu zilizotangulia za tafsiri hii. Tutaonyesha baadhi ya mifano ya misingi hiyo kama ifuatavyo:

1. Uislamu Ni Dini Ya Maumbile

Kila msingi katika misingi ya Uislamu, kila tawi katika sharia yake na kila hukumu katika hukumu zake, imejikita kwenye umbile safi: “Ndilo umbile alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu, Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.”

Aya inaonyesha wazi kwamba Uislamu unaitikia matakwa ya maumbile ya binadamu na kunyoosha mikono yake kwa kila jipya lenye faida; ni sawa liwe limekuja kutoka mashariki au magharibi. Amesema Imam Ali(a.s) : “Hekima ni adimu kwa Mumin. Chukua hekima hata kama ni kutoka kwa wanafiki.” Akasema tena: “Angalia kauli usiangalie aliyesema” Kuna hadith nyingi zenye maana haya.

2. Imani Ya Uislamu Kwenye Elimu

Uislamu unaamini elimu na kusimamia kwake maisha katika pande zote. Mwenyezi Mungu anasema katika sura hii tuliyo nayo Aya 36: “Wala usifuatilie ambalo huna ujuzi nalo.” Amesema tena:

قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١١١﴾

Sema: Leteni dalili zenu kama nyinyi ni wasema kweli.” Juz.1 (2:111)

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٤٣﴾

“Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui” Juz,14(16:43).

Mtume(s.a.w.w) amesema: “Wino wa mulama utapimwa na damu ya mashahidi siku ya kiyama.” Imam Ali naye amesema: “Elimu ni dini, inafuatwa dini kwayo.”

Maana ya kuamini elimu ni kuamini maendeleo na kufanya mambo kwa ajili ya maisha yaliyo bora na ya ukamilifu.

3. Kuiachia Huru Akili

Uislamu unatoa mwito wa kufikiri, kutaamali na kuchunguza maumbile haya kwa kutafiti kuweza kujua siri zake, faida zake na manufaa yake. Vilevile kujua mafungamano ya mtu na muumba wake. Pia Uislamu unatoa mwito kwa dini, elimu na falsafa, kutilia umuhimu mambo yanayoonekana na maarifa ya hisia; jambo ambalo wamekuwa nalo waislamu tangu mwanzo, kisha likaenda kwa wazungu. Ikawa msingi wa elimu ya majaribio uko kwao:

أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ ﴿١٨٥﴾

Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu. Juz. (7:185).

4. Uhuru Wa Kufikiri

Uislamu unatoa uhuru wa kusema na kufikiri, kiasi ambacho Mwenyezi Mungu aliwaruhusu watumishi wake, Malaika, wamuhoji huku wakisema:

قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ ﴿٣٠﴾

Utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu? Juz; 1 (2:30).

Pia aliruhusu Ibrahim(a.s) amjadili kuhusu watu wa Lut:

فَلَمَّا ذَهَبَ عَنْ إِبْرَاهِيمَ الرَّوْعُ وَجَاءَتْهُ الْبُشْرَىٰ يُجَادِلُنَا فِي قَوْمِ لُوطٍ ﴿٧٤﴾

“Basi hofu ilipomwondokea Ibrahim na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya watu wa Lut.” Juz; 12 (11:74).

Bali alimruhusu hata Iblis kutoa hoja mbele yake:

قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾

“Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo” Juz, 8 (7:12).

5. Wigo Mpana

Mafunzo yote ya kiislam yanaenea kwa wote; hayahusiki na mtu wala kikundi wala hayabagui:

إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ﴿١٣﴾

“Hakika mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye takua zaidi” (49:13)

Hadith inasema: “Nyote mmetokana na Adam, na Adama ametokana na mchanga”.

6. Jihadi

Uislamu umelazimisha jihadi ya hali na mali dhidi ya dhulma na ufisadi kwa kila mwenye uwezo. Mwenyezi Mungu anasema:

“Nendeni mkiwa wepesi na wazito, na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, Hilo ni kheri kwenu mkiwa mnamjua.” Juz; 10 (9:41).

Imam Ali(a.s) anasema:“Wallah! Lau si Mwenyezi Mungu kuchukua ahadi kwa Maulama kwamba wasiafiki kuvimbiwa kwa dhalim wala kufa njaa kwa aliyedhulumiwa, ningelitupilia mbali kamba yake na ningelim- nywesha wa mwisho wake kwa glasi ya wa mwanzo wake na dunia yenu hii kwangu ingelikuwa ya upuzi kuliko kamasi za mbuzi.”

Ustadh Muhammad Sa’d Jalal, katika Jarida la Al-katib la Misr anasema, ninamnukuu: “Makusudio ya Imam (Ali) ni kuwa lau si ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa maulama kutokubali tofauti mbaya baina ya watu katika kula; ambapo wengine wanavimbiwa kwa kula ili wengine wawe na njaa, basi asingeli- fanya juhudi ya kuitaka haki yake ya ukhalifa ambayo ndiyo nyenzo ya kuthibitika uadilifu wa kuzuia tofauti iliyotajwa. Kwa hiyo jihadi yake haikuwa kwa ajili ya kutamani utawala na manufaa ya nafsi yake; isipokuwa ilikuwa ni kwa ajili ya kutekeleza hukumu ya uadilifu wa kijamii katika kugawa utuajiri kwa waislamu wote kwa namna ambayo hatakuweko mwenye kuvimbiwa kwa kula wala mwenye utapia mlo.”

7. Mali Ni Ya Mwenyezi Mungu

Vyote vilivyomo ulimwenguni ni mali ya Mwenyezi Mungu na binadamu ni wakala wa vile vilivyomo mikononi mwake. Kwa hiyo ni juu yake kutotumia ila kwa idhini na amri ya yule mwenyewe anayemuwakilisha: “Ni vyake vilivomo mbinguni na vilivyo katika ardhi na viliomo baina yao na viliyomo chini ya ardhi” (20:6) (57:7) Angalia Juz; 4 (180).

8. Uislamu Na Maisha

Uislamu unalenga binadamu aishi katika uwiano unaokwenda sambamba na nidhamu ya ulimwengu na mahitaji ya maisha:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ﴿٢٤﴾

Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita kwenye lile litakalowapa uhai, juz.9 (8:24).

Angalia maelezo yake huko, Hivi karibuni kimetoka kitabu kipya cha mwandishi Wilfred Smith, Anasema katika kitabu hicho: “Waislamu wana uwezo, kulingana na dini yao, wa kuleta maendeleo pamoja na mahitaji ya sayansi na kuchangia katika kutengeneza jamii itakayoongozwa na maendeleo ya kijamii kwa uadilifu na heshima.”

Na kwamba wale wasioamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu.

Hakuna tofauti baina ya anayemkufuru Mwenyezi Mungu na anayekufuru siku ya mwisho. Kwa sababu kukataa kurudishwa viumbe baada ya kufa, maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu hawezi hilo; na hivyo hasa ni kufuru.

Imam Ali(a.s) anasema:“Namstaajabu yule anayemtilia shaka Mwenyezi Mungu naye anaona umbile lake; na namstaajabu yule anayekanusha ufufuo wa Akhera naye anaona ufufuo wa kwanza.”

Na mtu huomba shari kama vile aombavyo kheri.

Katika maisha haya kuna huzuni na furaha, tamu na chungu, Hakuna kimo- jawapo kinachodumu. Ni kuanzia hapa ndio ikasemwa: ‘siku ni mbili: kuna siku yako na siku ya kwako.’ Lakini baadhi ya watu wanapopatwa na jambo baya lolote wanalalamika na mishipa kuwasimama, wakidhani kuwa wako kwenye matatizo makubwa yasiyotatulika. Kwa hiyo wanajiombea shari, kama wanavyojiombea heri. Na hii ni aina ya ujinga na upumbavu. Lau wangelingojea siku kidogo tu, matatizo yangeliondoka pamoja na siku zinavyokwenda

Na mtu amekuwa ni mwenye pupa katika kujiombea shari bila ya kuwa na subira na uvumilivu.

Makusudio ya mtu hapa ni baadhi sio watu wote. Kwenye Nahjul-balagha kuna msemo huu: “Msilifanyie haraka lile linalokuwa kwa kungojewa, Wala msione kuchelewa litakalokuja kesho, Ni mangapi yaliyopatikana yakidhaniwa hayatapatikana?”

Na tumeufanya usiku na mchana kuwa ni ishara mbili.

Ni dalili mbili za kuweko Mwenyezi Mungu; Kwa sababu zinafuatana kulingana na kanuni thabiti na nidhamu ya kudumu kwenye maelfu ya miaka; hakuna hata mwaka mmoja uliotufautiana na mwingine. Yote hayo, na mengine mfano wake, ni dalili mkataa ya kuweko mpangiliaji mzuri na mhandisi mwenye ujuzi wa hali ya juu sana.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawapa mwito wataalamu na wenye fikra kumwamini Yeye kupitia kufikiria vizuri na kuzingatia maumbile ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, jinsi vilivyopangiliwa kwa utaalamu wa hali ya juu; kama vile kufuatana usiku na mchana na mengineyo yanayoonekana ulimwenguni.

Ama wale watu wa kawaida anawalingania kwa kukumbuka neema zake:

فَلْيَعْبُدُوا رَبَّ هَـٰذَا الْبَيْتِ ﴿٣﴾ الَّذِي أَطْعَمَهُم مِّن جُوعٍ وَآمَنَهُم مِّنْ خَوْفٍ ﴿٤﴾

Basi na wamwabudu Mola wa nyumba hii, ambaye amewaliwasha kutokana na njaa na akawasalimisha na hofu (106: 3-4).

Tunasema hivi huku tukijua kuwa miito yote miwili (kufikiria maumbile na neema) inaweza kuwa pamoja.

Tena tukaifuta ishara ya usiku.

Kusema ishara ya usiku ni kubainisha; maana yake ni hiyo hiyo ishara ambayo ni usiku.

Unaweza kuuliza kuwa : dhahiri ya neno kufuta ni kuondoka kabisa na inajulikana usiku upo kwa hisia na kuona?

Makusudio ya kufuta hapa ni kuondoka athari ya kiutendaji. Kwa sababu watu wanatulia kinyume na mchana ambapo watu wanafanya kazi na kuhangaika huku na huko. Kwa hiyo linalofutwa hapa ni ule utulivu. Mwenyezi Mungu anasema:

وَجَعَلَ اللَّيْلَ سَكَنًا ﴿٩٦﴾

Ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, Juz. 6 (6:96)

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا ﴿١٠﴾ وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ﴿١١﴾

Na tukaufanya usiku kuwa ni sitara na mchana kuwa ni wakati wa maisha (78:10–11).

Na tukaifanya ishara ya mchana ni ya kuangazia kila kitu kionekane ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu.

Usiku ni wa utulivu na kupumzika na mchana ni wa kutafuta riziki kwa mkono na kutoka jasho, sio kwa kughushi, hila, hiyana na kuwa kibaraka ili mtafute fadhila kutoka kwa ofisi za mabalozi na za upelelezi. Fadhila ya Mwenyezi Mungu inatolewa kwa kila mwenye kuitaka; nayo ni bora na ni yenye kubaki, tena ni safi na twahara.

“Ewe Mola tujaalie tutosheke na halali yako tusiwe na haja na haramu yako na tutosheke na twa yako tusiwe na haja na maasi yako na fadhila yako tusiwe na haja ya kumuomba asiyekuwa Wewe”

Na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu.

Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz; 10 (9:36).

Na kila kitu tumekifafanua waziwazi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametubainishia halali na haramu, akatuwekea hoja, dalili na mawaidha. Mwema ni yule aliyejikomboa na matamanio na akajikwamua na hawa ya nafsi yake.

وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا ﴿١٣﴾

13. Na kila mtu tumemfungia ndege wake shingoni mwake, Na siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa.

اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا ﴿١٤﴾

14. Soma kitabu chako! Nafsi yako leo inakutosha kukuhisabu.

مَّنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾

15. Anayeongoka hakika anaongoka kwa faida ya nafsi yake tu, na anayepotea anapotea kwa hasara ya nafsi yake tu. Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine, Wala sisi hatuadhibu mpaka tupeleke Mtume.

NDEGE SHINGONI

Aya 13 – 15

LUGHA

Makusudio ya ndege hapa ni matendo ya mtu ya kheri na shari. Waarabu walikuwa wakiona ni bahati njema ndege anayekuja upande wa kuume kwa sababu mtu anaweza kumpiga na wakiona ni kisirani ndege akitokea upande wa kushoto, kwa sababu hawezi kumpiga.

Ndio likaazimwa neno ndege kwa matendo ya heri na shari [6] .1 Shingoni mwake ni fumbo la kuwa nayo; kama vile amefunga koja au mkufu.

MAANA

Aya hizi tatu zinatofautiana kimatamshi, lakini zinashabihiana kimaana, Kauli yake Mwenyezi Mungu: Na kila mtu tumemfungia ndege wake shingoni mwake ni fumbo la kuwa mtu peke yake ndiye mwenye jukumu la matendo yake. Na kauli yake:

Na siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa.

Maana yake ni kuwa mtu kesho hataweza kuficha kitu chochote katika mambo aliyoyatenda:

يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُّحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِن سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا ﴿٣٠﴾

“Siku ambayo kila nafsi itakuta kheri iliyoitenda imehudhurishwa Na iliyoyatenda katika uovu, itapenda lau kungekuwa na masafa marefu baina ya uovu huo na yeye.” Juz. 3(3:30)

Kwa maelezo zaidi angalia huko.

Pia kauli yake Mwenyezi Mungu: Soma kitabu chako! Nafsi yako leo inakutosha kukuhisabu.

Hakuna haja ya shahidi wala mhasibu kesho; Kwa sababu mtu mwenyewe atajishuhudia na atajihisabu. Twabrasi anasema: “Atakuwa anajihisabu mwenyewe kwa sababu Siku ya Kiyama atakapoyaona matendo yake yote yameandikwa na kuona malipo yake pia yameandikwa kwa uadilifu, hayakupunguwa wala kuzidishiwa adhabu hata kidogo, atakiri na kukubali yeye mwenyewe, wala hatakuwa na hoja wala upinzani, Itawadhihirikia watakaofufuliwa kuwa hakuna dhulma.

Anasema Hasan:“Ewe mwanadamu! Amekufanyia insafu yule aliyekufanya ujihisabu mwenyewe.”

Anayeongoka hakika anaongoka kwa faida ya nafsi yake tu, na anayepotea anapotea kwa hasara ya nafsi yake tu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6: 104) na Juz. 11 (10: 108).

Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:164), Wala sisi hatuadhibu mpaka tupeleke Mtume.

Angalia Juz. 2 (2:159) kifungu cha ‘Ubaya wa adhabu bila ya ubainifu’.

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَإِذَا أَرَدْنَا أَن نُّهْلِكَ قَرْيَةً أَمَرْنَا مُتْرَفِيهَا فَفَسَقُوا فِيهَا فَحَقَّ عَلَيْهَا الْقَوْلُ فَدَمَّرْنَاهَا تَدْمِيرًا ﴿١٦﴾

16. Tunapotaka kuangamiza mji, huwaamrisha wapenda anasa wake, lakini hufanya maovu humo; basi hapo kauli huhakikika katika mji huo na tukauangamiza maangamizo makubwa.

وَكَمْ أَهْلَكْنَا مِنَ الْقُرُونِ مِن بَعْدِ نُوحٍ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿١٧﴾

17. Na karne ngapi tumeziangamiza baada ya Nuh? Na Mola wako anatosha kuwa ni mwenye habari na mwenye kuona dhambi za waja wake.

مَّن كَانَ يُرِيدُ الْعَاجِلَةَ عَجَّلْنَا لَهُ فِيهَا مَا نَشَاءُ لِمَن نُّرِيدُ ثُمَّ جَعَلْنَا لَهُ جَهَنَّمَ يَصْلَاهَا مَذْمُومًا مَّدْحُورًا ﴿١٨﴾

18. Anayetaka ya upesi upesi (dunia) tutamharakishia humo tunayoyataka kwa tunayemtaka; kisha tunamwekea Jahannam; ataiingia hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa mwenye kufurushwa.

وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾

19. Na mwenye kutaka ya mwisho (Akhera) na akayahangaikia kwa mahangaikio yake huku akiwa ni mumin, basi hao mahangaikio yao yatakuwa ni yenye kushukuriwa.

كُلًّا نُّمِدُّ هَـٰؤُلَاءِ وَهَـٰؤُلَاءِ مِنْ عَطَاءِ رَبِّكَ وَمَا كَانَ عَطَاءُ رَبِّكَ مَحْظُورًا ﴿٢٠﴾

20. Wote hao tunawasaidia, hawa na hao, katika atia za Mola wako; na atia za Mola wako hazizuiliki.

انظُرْ كَيْفَ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَلَلْآخِرَةُ أَكْبَرُ دَرَجَاتٍ وَأَكْبَرُ تَفْضِيلًا ﴿٢١﴾

21. Angalia jinsi tulivyowafad- hilisha baadhi yao kuliko wengine. Na Akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.

TUNAWAAMRISHA WAPENDA ANASA WAKE

Aya 16 -21

LUGHA

Neno ‘mutraf,’ambalo tumelifasiri kwa neno wapenda anasa, lina maana ya wale ambao wanastarehe watakavyo.

MAANA

Nilipofikia kufasiri Aya hii (tunawaamrisha watanasi wake), nilikumbuka swali nililoulizwa na mmoja wa mahatibu wa Iraq akisema: Kwa nini unawatukana wapenda anasa kwenye vitabu vyako? Nami nikamuuliza: Kwanini wewe unawatetea? Je, wewe ni mmoja wao? Au ni kwa vile wao ni mawalii wa neema zako? Basi akarudi nyuma na swali lake na akaomba msamaha. Hili limenifanya niieleze Aya hii kwa mfumo ufuatao:

1. Mbali ya neno ‘utajiri,’ neno ‘wapenda anasa’ pamoja na mnyumbuliko wake limekuja mara nane katika Qur’an; kama ilivyoelezwa katika Murshid, Katika Nahjulbalagha neno hili limeelezwa mara nyingi. Halikutajwa neno wapenda anasa ila pamoja na shutuma.

2. Watu wa Lugha wamesema: Neno Taraf katika mnyumbuliko wake linatumika hivi: Amejitanaasi mtu, kwa maana ya kujineemesha. Ameitanasi mali, kwa maana ya kuifuja. Pia neno hilo linakuwa kwa maana ya uovu na kiburi, Haya ndio maelezo yake kilugha. Ama sifa yake iliyotajwa katika Qur’an na kwengineko ni: Kughafilika na Mwenyezi Mungu, kuwafanyia uovu waja wa Mwenyezi Mungu, kuifanyia kiburi amri ya Mwenyezi Mungu na kuwapiga vita mawalii wa Mwenyezi Mungu. Vile vile kujifaharisha kwa wingi, kujiona, unyanyapaa na mengine mengi ya shutuma; isipokuwa yule aliyehurumiwa na Mungu na akajihurumia mwenyewe.

3.Tunapotaka kuangamiza mji, huwaamrisha wapenda anasa wake, lakini hufanya maovu humo; basi hapo kauli huakikika katika mji huo na tukauangamiza maangamizo makubwa.

Linaoamriwa ni uadilifu na twaa; yaani tunawamrisha uadilifu na utiifu. Wafasiri wametaja njia nne katika maana ya Aya hii. Yenye nguvu zaidi ni ile inayosema kuwa Mwenyezi Mungu amelitumia neno wapenda anasa kwa watu wote wa mji, katika mtindo wa kutumia sehemu kwa maana ya yote.

Mfano huu katika maneno ya waarabu unatumika sana, ikiwa hiyo sehemu ni muhimu zaidi; kama jicho katika mwili, wamelitumia kwa mstari wa mbele katika jeshi; kwa sababu jicho ni kiungo muhimu katika mwili [7] 1

Kwa kuwa wapenda raha ni wepesi zaidi na wajasiri wa kufanya maasi kuliko wengine, ndio ikafaa kulitumia neno hilo kwa watu wote wa mji; kama linavyotumika jicho kwa mtu.

Kwa hiyo basi maana ya Aya yanakuwa kwamba Mwenyezi Mungu hawaangamizi watu wa mji ila wakistahili hilo baada ya kuwekewa hoja kwa kutumwa mtume awaamrishe kheri, kuwakataza uovu, kuwahadharisha na uhalifu na maasi. Wakifanya uovu na kutoka kwenye utiifu, basi linahakika neno la adhabu juu yao na Mwenyezi Mungu huwateremshia maangamizi.

Ni kweli maana haya yanawafikiana na matamshi ya Aya, wala hayakataliwi na akili, lakini sisi tutaifasiri kwa njia njingine; kama ifuatavyo: Jamii yoyote iliyo na wapenda anasa, kwa maana tuliyoyataja, basi ni jamii inayoishi kwenye nidhmu ya ufisadi na dhulma. Kwani kuweko kwao ni sawa kabisa na kuweko saratani katika mwili.

Wa kulaumiwa kwanza kabisa kwa kupatikana wafisadi ni jamii yenyewe; kwa vile haikusimama kidete kuwapinga au angalu kutowaunga mkono; bali wanawabatiza majina ya waheshimiwa, kuwatukuza, kuwapa kura na kuwapa uongozi.

Hapa ndio inakuwa jamii yenyewe ni mshiriki kamili wa wapenda anasa na wafisadi katika makosa na madhambi yao yote na wanastahiki maangamivu; sawa na wapenda anasa.

Kuna Hadith isemayo:“Mwenye kuridhia dhulma ni kama mwenye kuifanya” “Mwenye kuinyamazia haki ni kama shetani bubu” Ikiwa mambo ni hayo itakuwaje kwa yule mwenye kuiridhia batili?

Anasema Seyyid Afghani: “Ewe mkulima unayechimba ardhi kwa jembe lako kwa nini usilitumie jembe hilo kuuchimba moyo wa anayekufanya mtumwa?” Tazama Juz; 13 (13:11).

Kwa hakika maangamizi yako aina nyingi; Yanaweza kuwa tufani tetemeko la ardhi, vimondo n.k. Vile vile yanaweza kuwa kwa udhalili na kusalitiwa shari.

Aina hii ni mbaya na ya kufedhesha zaidi. Wameadhibiwa nayo umma wa Muhammad(s.a.w.w) pale walipoacha jihadi, wakawafumbia jicho wafisadi na washari na wakaukubali udhalili na unyonge.

Imam Ali(a.s) anasema:“Hakika kwenye utawala wa kiislamu kuna hifadhi ya mambo yenu, basi upeni utiifu wenu…; Wallahi ni lazima mfanye hivyo au Mwenyezi Mungu atauondoa kwenu utawala wa kiislamu kisha usirudi kwenu kabisa mpaka mambo yarudie kwa wengine wasiokuwa nyinyi.”

Yaani tukiutii Uislamu tutaishi kwenye ngome imara tukiwa na hadhi na heshima; vinginevyo utawala utahama kwenda kwa maadui zetu, kisha usirudi kwetu; Kila ninaposoma onyo hili basi hujisikia natetema.

Na karne ngapi tumeziangamiza baada ya Nuh?

Makusudio ya karne hapa ni watu. Hii ni hadhari na ahadi kwa wale wanaomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w ) kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni muweza wa kuwafanya kama alivyowafanya wale waliowakadhibisha Mitume waliokuwa kwenye karne zilizopita; kama vile Ad na Thamud:

أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّـهِ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٩٩﴾

“Je, wamejiaminisha na hila ya Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.” Juz; 9 (7:99).

Imam Ali(a.s) amesema:“Hakika radhi ya Mwenyezi Mungu kwa waliobaki ni moja na uchukivu wa Mwenyezi Mungu kwa waliobaki ni mmoja. Jueni kuwa Yeye hataridhia chochote alichokichukia kwa waliokuwa kabla yenu wala hatachukia chochote alichowaridhia waliokuwa kabla yenu”

Na Mola wako anatosha kuwa ni mwenye habari na mwenye kuona dhambi za waja wake.

Kwa hiyo atamwadhibu anavyostahiki, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema kumwambia Abu dharr:“Hakika mumin anaziona dhambi ni jiwe kubwa analohofia kumwangukia na kwamba kafiri anaona dhambi zake ni kama nzi tu anayepita puani mwake.”

Anayetaka ya upesi upesi (dunia) tutamharakishia humo tunayoyataka kwa tunayemtaka.

Sio kuwa kila alitakalo mtu anapewa na Mungu, Kwani sisi huwa tunataka mambo mengi na hayawi. Ispokuwa makusudio ya Aya ni kuwa mwenye kufanya kwa ajili ya dunia tu, bila ya kuamini chochote isipokuwa manufaa yake, basi atapata matunda ya kazi yake na juhudi yake kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, kwani mja hawezi kufikia jambo lolote kama Mungu akikataa, hata kama atafanya kazi usiku na mchana. Hakika Mwenyezi Mungu hatupi tunayoyataka ila kwa kutaka kwake. Hayo ndio makusudio ya ‘tunayoyataka kwa tunayemtaka’

Kisha tunamwekea Jahannam; ataiingia hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa mwenye kufurushwa.

Kwa vile yeye anaamini masilahi yake tu na haoni umuhimu wowote isipokuwa nafsi yake, wala hafanyi lolote isipokuwa kwa ajili yake.

Na mwenye kutaka ya mwisho (Akhera) na akayahangaikia kwa mahangaikio yake huku akiwa ni mumin, basi hao mahangaikio yao yatakuwa ni yenye kushukuriwa.

Makusidio ya kuyahangaikia kwa mahangaikio yake ni kutaka kheri na kuifanya na kuiamini si kwa chochote isipokuwa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na kheri. Anayefanya hivi ndiye anayestahiki daraja na cheo mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya watu.

Ama anayefanya kwa ajili ya faida na biashara basi yake ni Jahannam. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasemama: “Ambaye Hijra yake (kuhama kwake) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi Hijra yake ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na ambaye hijra yake ni kwa ajili ya kuipata dunia au mwanamke amuoe, basi Hijra yake ni kwa lile alilololi- hajiria.

Muhtasari wa yote haya ni kuwa Uislamu ni njia inayomuelekeza mtu kufanya kheri na kuiacha shari hiyo yenyewe. Kwa hiyo itakuwa ni lazima kusema ukweli kwa kuwa ni lazima kufanya hivyo na ni lazima kujiepusha na uongo kwa kuwa ni lazima kujiepusha. Mtume(s.a.w.w) ameutolea ibara mwelekeo huu kwa kusema:“Hakika nimetumwa kutimiza tabia njema.” Ilivyo hasa ni kuwa tabia njema haiwi ila ikiwa imetakata na kila uchafu.

Wote hao tunawasaidia, hawa na hao,

Hiyo ni ishara ya makundi yote mawili: wale wanaotenda kwa ajili ya dunia na wale wanaotenda kwa ajili ya akhera.

Katika atia za Mola wako; na atia za Mola wako hazizuiliki.

Atia (vipawa) za Mwenyezi Mungu kwa mtu zinaanzia tangu kuumbwa kwake na kuweko kwake ambako hakupatikani ila kwake tu; kisha sababu za kubakia kwake na kukua kwake. Atia hizi zinamhusu mwema na muovu. Ama atia zake katika akhera zitawahusu wema wanaomcha Mungu tu.

Angalia jinsi tulivyowafadhilisha baadhi yao kuliko wengine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawagawanyi watu kwenye tabaka, wala kuto- fautiana katika haki za kibinadamu kwa mtu binafsi au makundi. Vipi iwe hivyo na hali yeye ndiye aliyesema:

إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ﴿١٣﴾

“Hakika mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye takua zaidi katika nyinyi” (49:13).

Kwa hiyo basi kuzidiana watu katika dunia, katika isiyokuwa haki ya kibinadamu, inafaa; kama vile afya, umri, riziki kupitia kufanya kazi, kurithi au njia nyingine yoyote aliyoihalalisha Mungu. Lakini utajiri unaokuja kwa ulanguzi, hila na uporaji unatokana na shetani, wala haifai kuunasibisha na Mwenyezi Mungu.

Na akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa watu wanatofautiana katika dunia, sasa anasema kuwa huko Akhera pia itakuwako tofauti, lakini huko tofauti ni kubwa sana. Kwani sifa zinazowatofautisha hapa ni utajiri na ufukara, elimu na ujinga, maradhi na siha na umri mrefu na mfupi; kisha wote wanaishia kwenye mauti kwa usawa, hata wema na waovu. Ama sifa watakazotofautiana huko Akhera, ni kuungua katika moto na kuwa kwenye neema na furaha. Wapi na wapi tofauti hii na ile.

لَّا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَّخْذُولًا ﴿٢٢﴾

22. Usimfanye mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukabaki ni mwenye kukalaumiwa uliyetupwa.

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾

23. Na Mola wako amepitisha kuwa msimwabudu yoyote ila Yeye tu na kuwatendea wema wazazi wawili. Mmoja wao akifikia uzee naye yuko kwako au wote wawili, basi usiwaambie Ah! Wala usiwakemee, Na sema nao kwa msemo wa heshima.

وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾

24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma na useme: Mola wangu! Warehemu kama walivyonilea utotoni.

رَّبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا فِي نُفُوسِكُمْ إِن تَكُونُوا صَالِحِينَ فَإِنَّهُ كَانَ لِلْأَوَّابِينَ غَفُورًا ﴿٢٥﴾

25. Mola wenu ni Mjuzi zaidi wa yaliyo katika nafsi zenu, ikiwa nyinyi mtakuwa wema. Hakika Yeye ni Mwenye kughufiria wanaorejea kwake.

USIWAMBIE AH!

Aya 22 – 25

MAANA

Usimfanye mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukabaki ni mwenye kulaumiwa uliyetupwa.

Maneno haya anaambiwa kila mtu, sio Mtume(s.a.w.w) kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘mmoja wao akifikia uzee naye yuko kwako au wote wawili; Na inajulikana kuwa Mtume alikuwa yatima.

Na Mola wako amepitisha kuwa msimwabudu yoyote ila Yeye tu na kuwatendea wema wazazi wawili. Mmoja wao akifikia uzee naye yuko kwako au wote wawili, basi usiwaambie Ah! Wala usiwakemee, Na sema nao kwa msemo wa heshima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma na useme: Mola wangu! Warehemu kama walivyonilea utotoni.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekutanisha shukrani ya wazazi wawili na shukrani yake na akawajibisha kuwatendea wema. Kuna Hadith isemayo: “Kuna mtu mmoja alikwenda kwa Mtume(s.a.w.w) akimtaka idhini ya kupigana jihadi pamoja naye. Akamuuliza: je, Wazazi wako wako hai? Akasema: Ndio. Akasema mtume: basi fanya jihad kwao.

Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘kama walivyonilea utotoni,’ ni ishara ya kuwa wao walijitolea nafsi zao kwa ajili yake, wakakesha usiku ili yeye alale, wakawa na njaa ili ashibe yeye na wakawa uchi ili yeye avae. Na hili ni deni shingoni mwake, ni wajibu alilipe atakapokuwa na nguvu na wao kuwa dhaifu, na kuwachukulia kwenye uzee wao sawa na wao walivyomchukulia alipokuwa mdogo, na wao wamemzidi kwa kumtangulia.

Imam Zaynul-abidin(a.s) anasema akiwaombea Mungu wazazi wake: “Ewe Mola wangu! Ni wapi na wapi urefu wa shughuli yao ya kunilea mimi? Ni wapi na wapi shida ya tabu yao ya kunilinda mimi? Ni wapi na wapi kujinyima kwao kwa jili ya kunifurahisha mimi? Ni mbali kwa mbali kabisa na jinsi walivyotekeleza haki yao kwangu; ni mbali kwambali yote hayo na jinsi ninavyowafanyia! Wala mimi sijatekeleza wadhifa wa kuwahudumia.”

Kila mmoja kati ya baba na mama anajitolea kwa nafsi yake na pumzi zake zote kwa ajili ya mtoto, kisha hataki malipo wala shukrani yoyote. Analotamani ni kuwa mtoto wake awe ni mtu mwenye kutajika. Nimepata mtihani wa kuwa baba, lakini wazazi wangu hawakuupata mtihani huo, kwa sababu nilikuwa yatima wa baba na mama.

Ninasema nimepatwa na mtihani huo, kwa sababu mimi sioni raha yoyote katika maisha haya isipokuwa raha ya mwanangu wa kike na kiume. Tabasamu moja tu ya mmoja wao kwangu ni sawa na dunia na vilivyomo ndani yake na hasononeki yoyote kati yao ila huwa ninahisi kuna mkono unatoa roho yangu iliyo mbavuni mwangu.

Mola wenu ni Mjuzi zaidi wa yaliyo katika nafsi zenu, ikiwa nyinyi mtakuwa wema. Hakika Yeye ni Mwenye kughufiria wanaorejea kwake.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua maazimio, kama anavyojua kauli na vitendo na kumlipa kila mmoja kulingana na nia yake. Mwenye kufanya uovu kisha akatubia sawasawa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.

Hiii ni tahadhari kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa yule mwenye kuwaudhi wazazi wake na akawa anawaona ni mzigo kwake, kama ambavyo pia ni hadhari ya kuacha ikhlasi katika kauli na vitendo.