TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO22%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
  • Anza
  • Iliyopita
  • 19 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16828 / Pakua: 3980
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

Mwandishi:
Swahili

1

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَإِن كَادُوا لَيَفْتِنُونَكَ عَنِ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ لِتَفْتَرِيَ عَلَيْنَا غَيْرَهُ وَإِذًا لَّاتَّخَذُوكَ خَلِيلًا ﴿٧٣﴾

73. Na hakika walikaribia kukufitini uache tuliyokupa wahyi ili utuzulie mengine, Na hapo wangelikufanya rafiki.

وَلَوْلَا أَن ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدتَّ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلًا ﴿٧٤﴾

74. Lau sikukuweka imara ungelikurubia kuwaelekea kidogo.

إِذًا لَّأَذَقْنَاكَ ضِعْفَ الْحَيَاةِ وَضِعْفَ الْمَمَاتِ ثُمَّ لَا تَجِدُ لَكَ عَلَيْنَا نَصِيرًا ﴿٧٥﴾

75. Hapo basi, tungelikuonjesha maradufu ya uhai na maradufu ya mauti; kisha usingelipata wa kukunusuru nasi.

وَإِن كَادُوا لَيَسْتَفِزُّونَكَ مِنَ الْأَرْضِ لِيُخْرِجُوكَ مِنْهَا وَإِذًا لَّا يَلْبَثُونَ خِلَافَكَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٧٦﴾

76. Na kwa hakika walikaribia kukukera katika nchi ili wakutoe humo; na hapo wasingelibakia nyuma yako ila muda mchache.

سُنَّةَ مَن قَدْ أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ مِن رُّسُلِنَا وَلَا تَجِدُ لِسُنَّتِنَا تَحْوِيلًا ﴿٧٧﴾

77. Ndio desturi ya wale tuliowatuma kabla yako wala hutapata mabadiliko katika desturi yetu.

JE MTUME ANAHADAIKA NA DINI YAKE

Aya 73 -77

MAANA

Na hakika walikaribia kukufitini uache tuliyokupa wahyi ili utuzulie mengine, Na hapo wangelikufanya rafiki.

Waliokaribia ni washirikina. Walijaribu washirikiane na Mtume(s.a.w.w) kwa kumtaka awakubalie matakwa yao na wamfanye kuwa ni kiongozi na rafiki. Miongoni mwa hayo ni kuigusa miungu yao au angalau aache kuikashifu, lakini Mtume hakuwakubalia matakwa yao washirikina, kwa sababu yeye ni maasum na maasum hawezi kuchangia dini yake na risala yake na mambo mengine.

Unaweza kuuliza : Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘walikaribia kukufitini’ inafahamisha kuwa yeye Mtume alikaribia kuwakubalia matakwa yao?

Jibu : Aya hii inafungamana moja kwa moja na Aya inayofuatia.

Lau sikukuweka imara ungelikurubia kuwaelekea kidogo.

Kwa hiyo maana ni kuwa, hakika wewe Muhammad lau si ulinzi wetu kwako kwa kukupa isma (kuhifadhika) ya dhambi, basi ungelikaribia kuwaelekea washirikina na kuwatikia maombi yao, Isma ndiyo iliyokuzuia kuwakubalia. Ni sawa na kusema: ‘Lau si fulani ungeliangamia’ Umetangulia mfano wake katika Juz; 12 (12: 24).

Zaidi ya hayo, kufikiria kufanya kitu ni jambo jingine na kukifanya ni jambo jingine. Kuna Hadith mutawatir kutoka kwa Mtume kwamba yeye amesema: “Umeondolewa umma wangu yale yanayozungumzwa na nafsi zao madamu hawakufanya au kuzungumza,” yaani kujizungumzia mtu mwenyewe nafsini mwake, hakuna athari, Kuna mapokezi yanayosema, kuwa washirikina walipomwambia Mtume alinyamaza, hakuwajibu.

Hapo basi, tungelikuonjesha maradufu ya uhai na maradufu ya mauti.

Maana ni kuwa, ewe Muhammad! Lau ungeliwaelekea washirikina tungelikuadhibu mara mbili zaidi ya mwengine, duniani na Akhera. Kwa sababu adhabu ya wakuuu inakua kulingana na ukuu wao na cheo chao. Hii ni kiasi cha kukadiria tu, na ‘kukadiria muhali sio muhali.’

Kisha usingelipata wa kukunusuru nasi, kukukinga na adhabu.

Katika Nahju-lbalagha imeelezwa: “Siku ya Kiyama ataletwa kiongozi mkandamizaji, akiwa hana wa kumsaidi wala wa kumtolea udhuru, atatupwa katika Jahannam, azunguke humo kama pia, kisha afungwe kwenye shimo lake.”

Na kwa hakika walikaribia kukukera katika nchi ili wakutoe humo; na hapo wasingelibakia nyuma yako ila muda mchache.

Waliposhindwa washirikina na Mtume walijaribu kumkera kwa kila njia ili atoke Makka, Lau wangelimtoa, basi Mwenyezi Mungu angeliwangamiza muda kidogo baada ya kutoka kwake.

Unaweza kuuliza kuwa : si walifanya hivyo washirikina pale walipoafikiana kumuua Mtume, mpaka akalazimika kutoka kwenda Makka kwa kuhofia, kama ilivyoelezwa katika Juz. 9 (8:30).

Jibu : makusudio ni kuwa lau washirikina wangelimtoa wao kwa nguvu na kua ni mkimbizi aliyefukuzwa asiyejua pa kwenda, basi Mwenyezi Mungu angeliwangamiza haraka sana. Lakini Mtume alitoka Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwenda kwa watu ambao walijitolea kwake kwa hali na mali na familia.

Ndio desturi ya wale tuliowatuma kabla yako wala hutapata mabadiliko katika desturi yetu.

Yametangulia maelezo kuhusu hukumu ya Mwenyezi Mungu na kadha yake, kwamba kaumu yoyote itakayomtoa Mtume wao kwa nguvu, Mwenyezi Mungu anaiangamiza haraka. Na hii ndio desturi katika viumbe vyake, haibadiliki wala haigeuki, inaendela wakati wote na mahali kote.

أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨﴾

78. Simamisha Swala linapopinduka jua mpaka giza la usiku, na Qur'an ya alfajiri; hakika Qur'an ya alfajiri imekuwa ni yenye kushuhudiwa.

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ﴿٧٩﴾

79. Na katika usiku amka kwayo ni ziada kwa ajili yako; huenda Mola wako akakuinua cheo kinachosifika.

وَقُل رَّبِّ أَدْخِلْنِي مُدْخَلَ صِدْقٍ وَأَخْرِجْنِي مُخْرَجَ صِدْقٍ وَاجْعَل لِّي مِن لَّدُنكَ سُلْطَانًا نَّصِيرًا ﴿٨٠﴾

80. Na sema: Mola wangu! Niingize muuingizo mwema na nitoe kutoka kwema, na unipe madaraka kutoka kwako ya ushindi.

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا ﴿٨١﴾

81. Na sema, haki imefika na batili imetoweka. Hakika batili ni yenye kutoweka.

SIMAMISHA SWALA LINAPOPINDUKA JUA

Aya 78-81

MAANA

Aya ya kwanza na ya pili ni miongoni mwa Aya za hukumu, zilizoshuka kwa ajili ya kubainisha nyakati za Swala. Wana-Fiqh wana kauli kadhaa, kama zifuatavyo:

1.Simamisha Swala linpopinduka jua mpaka giza la usiku.

Wametofautiana katika makusudio ya kupinduka jua, Imesemekana ni wakati wa kutua jua na ikasemkena ni kupinduka nusu ya mzingo wa mbingu (meridian), na hiyo ndiyo kauli ya wengi.

Imepokewa kutoka kwa Imam Ja’far As-swadiq(a.s) kwamba giza la usiku ni nusu ya usiku.

Katika tafsiri za kisunni na kishia imeelezwa kuwa Aya hii imekusanya nyakati zote za Swala tano: Adhuhuri na Alasiri zinaingia katika kupinduka jua. Magharibi na Isha zinaingia katika giza la usiku na Asubuhi katika Qur’an ya alfajiri.

Katika Shia amesema Tabrasi kwenye Majmau-bayan: “Aya hii imeku- sanya Swala tano: Swala ya adhuhuri na alasiri zinaingia katika kupinduka jua, swala ya magharibi na isha zinaingia katika giza la usiku na makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni swala ya alfajiri; Hizi ndizo Swala tano.”

Katika sunni amesema Razi: “Simamisha Swala, yaani idumishe kuanzia wakati wa kupinduka jua mpaka giza la usiku, inaingia swala ya adhuhuri, alasiri magharibi na isha” Kisha akaendela kusema: “wamekongamana kuwa makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni Swala ya asubuhi.”

Ilivyo ni kwamba mafaqihi, katika vitabu vyao, wanaanza maneno kwa Swala ya adhuhuri kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘linapopinduka jua’ ambapo ameanzia Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa kutaja wakati wake.

Kuongezea mapokezi ya Hadith zinazoelezea kuwa adhuhuri ndiyo ya kwanza kufaradhishwa, kisha zikafuatia nyingine kwa utaratibu ulivyo. Hilo lilikuwa Makka usiku wa Israi, mwaka mmoja kabla ya Hijra (kuhamia Madina).

Madhehebu za kiislamu zimeafikiana kuwa haifai Swala kabla ya kuingia wakati wake na kwamba jua likipinduka ndio umeingia wakati wa Adhuhri, lakini wametofautiana kwenye kiwango cha muda huu, unaisha wakati gani?

Shia Imamiya wamesema kuwa mara tu bada ya kupinduka jua unahusika wakati wa Swala ya adhuhuri kwa kiasi cha kuswaliwa kwake na kiasi cha kuweza kuswaliwa swala ya alsiri mwisho wa mchana kinahusika na Swala ya alasiri. Baina ya wakati wa kwanza na wa mwisho ni wa ushirikano wa Swala mbili; yaani inaweza kuswalia adhuhuri na alasiri.

Dhahiri ya Aya iko pamoja nao: ‘linpopinduka jua mpaka giza la usiku’ wala Mwenyezi Mungu hakutenganisha; kama ilivyo kwenye madhehebu nyingine.

Wengineo wamesema kuwa wakati wa adhuhuri unaanza linapopinduka jua mpaka kuwa kivuli cha kila kitu mfano wake, ikizidi hapo wakati wa adhuhuri utakuwa umekwisha na utakuwa wakati wa alasiri umeingia. Ufafanuzi uko katika kitabu chetu: Al-fiqh ala madhahib al-khamsa (Fiqh kwenye madhehebu matano).

2.Na Qur’an ya alfajiri. Hakika Qur’an ya alfajiri imekuwa ni yenye kushuhudiwa.

Wameafikiana kwamba makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni ile inayosomwa katika Swala ya alfajiri, yaani ya asubuhi. Vil vile wameafikiana kwamba wakati wake unaanzia kutokeza alfajiri ya kweli mpaka kutoka jua (mawiyo); isipokuwa Maliki anasema kuwa asubuhi ina nyakati mbili: Ya hiyari, inaanzia alfajiri hadi kujuana nyuso. Na wakati wa dharura unaoanzia kujuana nyuso hadi kutoka jua. Kauli ya kushangaza ni ile ya masufi wanaosema kuwa makusudio ya alfajiri ni kupasuka moyo.

Wamekongamana mafaqihi, kwa ushahidi wa Tabrasi na Razi, kwamba makusudio ya yenye kushuhudiwa, ni kwamba Malaika wa usiku na mchana wanakusanyika ili washuhudie Swala. Wametegemea riwaya aliyoipokea Bukhari kutoka kwa Abu Hurayra, katika Sahih Bukhari Juzuu ya 6 mlango wa sura Bani Israil, Sisi tunaishuku riwaya hii. Na tunafasiri yenye kushuhudiwa, kuwa ni kuhudhuria hisiya. Kwa sababu mtu wakati wa asubuhi hisia zake zinakuwa zipo baada ya kupumzika na usingizi. Ndio maana ikasemwa ‘usingizi unabeba maazimio ya siku’

3.Na katika usiku amka kwayo ni ziada kwa ajili yako.

Kwayo ni hiyo Qur’an. Kwa ajili yako ni kumuhusisha yeye tu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amekufaradhishia wewe Muhammad swala nyingine, zaidi ya zile tano ambazo ni zako na wengine, uiswali usiku. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ ﴿١﴾ قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٢﴾

“Ewe mwenye kujifunika nguo! Simama usiku isipokuwa kidogo” (73:1-2)

وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا ﴿٢٦﴾

“ Na usiku umsujudie Yeye na umtakase usiku mrefu.” (76:26).

Swala hii inaitwa Swala ya usiku (swalatu-llayl); wakati wake ni kuanzia nusu ya usiku hadi alfajiri. Ni wajibu kwa Mtume(s.a.w.w) , kama tulivyoeleza mwanzo na ni sunna kwa mwenginewe.

Huenda Mola wako akakuinua cheo kinachosifika.

Huenda ni neno la kutarajia ikiwa linatoka kwa kiumbe na ni la mkato ikiwa linatoka kwa muumbaji, Hapa anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) .

Hakuna kitu zaidi ya Muhammad wala cheo zaidi ya Muhammad na kizazi zaidi ya kizazi cha Muhammad; isipokuwa yule ambaye hakuna mfano wake kitu chochote. Kuna Hadithi isemayo kuwa Mtume(s.a.w.w) alifasiri cheo chenye kusifika katika Aya hii kuwa ni cheo atakachowaombea umma wake kesho.

Na sema: Mola wangu! Niingize muuingizo mwema na nitoe kutoka kwema.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu kuomba dua hii. Kuingia kwema na kutoka kwema ni fumbo la haki na ikhlsi katika itikadi, makusudio, vitendo, harakati zote na kupumzika. Hakuna shaka kuwa mwenye kuwa na silaha ya haki na akamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake, basi atamuimarisha kwa kauli thabiti, atampa hoja imara na umakini wa moyo ulio mwema na safi.

Na unipe madaraka kutoka kwako ya ushindi.

Kuna ushindi na madaraka yanayozidi kutajwa Mtume mtukufu pamoja na jina la Mwenyezi Mungu mara tano kwa siku, katika adhana na katika swala za wajibu na sunna? Kuna nguvu gani na heshima adhimu kuliko ile aliyompa Muhammad, aliposema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ﴿٧﴾

“Anachowapa Mtume kichukueni na anachowakataza kiacheni,” (59:7).

Na sema haki imefika na batili imetoweka. Hakika batili ni yenye kutoweka.

Haki ni risala ya Muhammad, itikadi na sharia. Vinginevyo ni batili, kiuhalisi na mbele ya Mwenyezi Mungu; hata kama vitaaminiwa na watu wa ardhini wote. Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya batili hapa ni ushirikina na kwamba Mtume(s.a.w.w) alipoikomboa Makka aliingia Al- ka’ba na mlikuwa na masanamu 360, akawa anazisukuma huku akisema: “Haki imefika na batili imetoweka, Hakika batili ni yenye kutoweka.”

NGUVU YA HAKI NA NGUVU YA BATILI

Unaweza kuuliza : Mara nyingi tunaona na kushuhudia watu wa batili wakishinda na watu wa haki wakishindwa. Hii si inapingana na kauli ya Mwenyezi Mungu ‘Hakika batili ni yenye kutoweka’?

Jibu : Hakika haki ina nguvu za dhati zisizoepukana nazo kwa hali yoyote; nazo zinatenda kazi na kuathiri kwenye nyoyo safi zilizo takatifu. Mara nyingi athari hii inafikia kiwango ambacho hakuna nguvu yote yote inayoweza kuisimamisha; si mapanga ya wachinjaji wala unyongaji wa mataghuti.

Historia inatusimilia jinsi mashahidi wa itikadi walivyojitolea kuwa mashahidi kwa nyuso za kutabasamu na nafsi zilizo radhi; bali hayo yametokea wakati wetu huu huko Vietnam, Korea, Palestina na kwengineko.

Ndio! Ni kweli hawa ni wachache; kama ilivyo kawaida ya kila jambo tukufu lenye thamani. Lakini wangelikuwa wengi kwa idadi au wengi kwa viwango vya asilimia, basi dunia ingelijaa uadilifu, na dhulma na jeuri isengelikuwa na athari yoyote. Sisi hatuna shaka ubinadamu utakwenda na njia hii; hata kama muda utakuwa mrefu.

Ama batili, haina nguvu wala urefu, isipokuwa kuweko kwake kunategema rushwa, dhulma, ukandamizaji, kuwafukuza watu njama n.k.

Haya yote yataondoka kadiri siku zinavyokwenda na hali kubadilika. Ama nguvu ya haki huwa inakwenda na wakati, inabakia hivyo hivyo tu wakati wote. Kwa sababu inategema hiyo haki yenyewe, kama ilivyo. Kwa ajili hii ndio tunasema tena: Sisi tuna imani isiyokuwa na shaka kwamba mwisho ni wa haki na neno la juu litakuwa la haki peke yake.

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾

82. Na tunateremsha katika Qur’an ambayo ni ponyo na rehema; Wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa hasara.

وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ كَانَ يَئُوسًا ﴿٨٣﴾

83. Na tunapomneemesha mtu hugeuka na kujitenga kando na inapomgusa shari hukata tamaa.

قُلْ كُلٌّ يَعْمَلُ عَلَىٰ شَاكِلَتِهِ فَرَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَنْ هُوَ أَهْدَىٰ سَبِيلًا ﴿٨٤﴾

84. Sema: kila mmoja anafanya kwa namna yake, Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia.

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾

85. Wanakuuliza kuhusu roho, Sema: roho inatokana na amri ya Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.

QUR’ANI NI PONYO

Aya 82-85

MAANA

Na tunateremsha katika Qur’an ambayo ni ponyo na rehema.

Qur’an ni rehema kwa yule anayeitakia nafsi yake rehema na ni ponyo la ukafiri, ulahidi, ujinga, ufisadi na kila uchafu, kwa yule mwenye kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na haki.

Imam Ali(a.s) katika kuisifu Qur’an ansema:“Hakika hiyo ni kamba imara, nuru inayobainisha, ni dawa yenye kuleta nafuu, ni kichujio cha takataka, ni hifadhi kwa mwenye kushikamana nayo na ni uokovu kwa mwenye kufungamana nayo.” Mwenye kuhalifu hukumu miongoni mwa hukumu za Qur’an atakuwa miongoni mwa madhalimu na waliohasirika.

Wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa hasara.

Qur’an ni rehema kwa waumini na nakama kwa madhalimu na wafisadi, kwa sababu kila wanapoasi hukumu miongoni mwa hukumu zake, wanazidi dhambi na adhabu.

Na tunapomneemesha mtu hugeuka na kujitenga kando na inapomgusa shari hukata tamaa.

Maana ya Aya hii yanafupilizwa na kauli ya Imam Ali(a.s) katika wasifu wa mtu: “Akijitosheleza huchangamka na kushawishika na anapofukarika hukata tamaa na kubweteka. Umepita mfano wake katika Juz; 11 (10:12) na Juz. 12 (11: 9).

Sema: kila mmoja anafanya kwa namna yake, Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia.

Wafasiri wamesema: “Namna, ni njia. Na maana ya Aya ni kuwa kila mmoja kati ya mumin na kafiri anafanya kwa njia yake na maumbile yake” lakini sisi tutaifafanua, kama tulivyoifahamu, katika hali zifuatazo:

1. Neno kila mmoja linafahamisha kuenea kwa mtu mmoja mmoja; kwa mfano ukisema: kila mtu analifahamu hili, ni kama umesema: Zayd analifahamu na Bakari, Hindu n.k. (yaani kila mmoja ana namna yake ya kulifahamu) Lakini ukisema: watu wote wanalifahamu, itakuwa kadhia ni moja na hukumu itakuwa imewaenea kwa ujumla sio kwa mtu mmoja mmoja. Kwa hiyo maana ya Aya ni kuwa kila mmoja katika watu ana namna yake inayomuhusu yeye peke yake; kama vile alama za vidole, kila mmoja ana zake.

2. Imepokewa Hadith kutoka kwa Ja’far As-swadiq(a.s) kwamba yeye amefasiri namna kwa maana ya nia. Usahihi wa tafsiri hii unafahamika kutoka na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia’ iliyokuja moja kwa moja bila ya kuweko kiunganishi kingine.” Yaani Mwenyezi Mungu anamjua anayetaka kuongoka na kufu- ata njia yake bila ya makusudio mengine yoyote isipokuwa dhati yake Aliye Mtukufu.

Kwa hiyo maana ya Aya yatakuwa: Kila mtu anafanya kulingana na nia yake na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atapambana naye kulingana na nia yake; ikiwa kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi itakuwa ni shari.

Mwenye kudhihirisha kheri mbele ya watu ili awahadae watu na kumbe ana malengo ya shari, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni mshari. Na mwenye kuiba mkate ili ajisitiri njaa baada ya kukosa budi, akiwa hana njia nyingine, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu hastahiki adhabu.

ROHO INATOKANA NA AMRI YA MOLA WANGU

Wanakuuliza kuhusu roho, Sema: roho inatokana na amri ya Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.

Roho ina maana nyingi. Makusudio yake hapa ni uhai. Mtume(s.a.w.w) aliulizwa kuhusu roho, Mwenyezi Mungu akamwamrisha amwambie muulizaji kuwa roho ni katika vitu vinavyopatikana kwa amri ya Mungu ambayo ni kusema ‘Kuwa na ikawa.’

Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa vitu viko aina mbili: Aina ya kwanza, Mwenyezi Mungu anavileta kupitia sababu za kimaumbile kutokana na maada; kama mwili wa binadamu.

Aina ya pili ni ile inayopatikana kwa kiasi cha amri tu; ambayo ni neno ‘kuwa’ Na roho ni katika aina hiyo. Aya imeliweka wazi hilo, Kwa sababu neno: ‘roho inatokana na amri ya Mola wangu,’ ni ishara ya neno ‘amri’ lilioko katika kauli yake nyingine Mwenyezi Mungu:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾

“Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia kuwa! Na kikawa,” (36:82).

Majaribio yamethibitisha hakika hii na wakaiamini wale waliobobea na kumaliza miaka mingi kwenye utafiti wa asili ya uhai. Waliamni hakika hii baada ya kubainika kwamba sababu ya moja kwa moja ya uhai haina muungano wowote wa kuishia kwenye maada. Lau ingelikuwa inaishia kwenye maada, wangeliweza kumtengeneza binadamu kwenye viwanda vyao na maabara yao.

Wamejaribu wakashindwa: “Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” Yaani kadiri viwanda vyenu vinavyotengeneza vitu vya ajabu, lakini si chochote kulingana na chembe hai za nzi, sikwambii nzi mwenyewe: “Enyi watu! Umepigwa mfano, basi usikilizeni, Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawataumba hata nzi, wajapojumuika kwa hilo, Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kutoka kwake.

ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ ﴿٧٣﴾

Amedhoofika huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa,”(22:73)

Umepita mfano wake katika Juz; 9 ( 6:95).

MWENYEZI MUNGU NA ELIMU YA CHEMBE HAI

Imetokea sadfa, wakati nikifasiri Aya hii, nikasoma makala katika gazeti Ruzil Yusuf la Misri[9] toleo la April 1969 likiwa na maelzo haya:

“Mwili wa mtu una mamilioni ya chembe hai ambazo haziwezi kuonekana isipokuwa kwa darubini. Katika miaka ya karibuni ilikuwa ni vigumu kuweka elimu ya chembe kwa sababu wataalamu walikuwa hawawezi kuz- ifungua hizo chembe au kuzidunga sindano. Kwa vile kazi ilikuwa inahi- taji chombo kidogo kuliko milimita elfu moja, basi sindano nayo ingelihi- tajika iwe na ncha ndogo kuliko milimita milioni moja.

Hatimae walifanikiwa wataalamu kuzifungua chembe hizo kupitia mwanga, sawa na tunavyowasha sigara kutokana na mwanga wa jua kupitia kioo. Ni njia pekee iliyowawezesha wataalamu kuzifungua chembe hai na kugundua kuwa ni mkusanyiko uliosheheni makumi ya viumbe mbalimbali, kila kimoja kikiwa na sifa yake maalum na kazi yake na mfungamano ulionacho pamoja na wakazi wengine wa chembe hizo.

Kuweza kufahamu kazi hizo na mifungamano hiyo, kutahitajia miaka ya utafiti kama sio vizazi. Ndio ikaanza elimu ya chembe hai na tukawa sasa tunajua kwamba chembe hai zina mwili na viungo, utando, nyuzi na mengineyo ya kushangaza akili.

Imedhihirika kwamba chembe hai za damu ni mkusanyiko wa chembe zinazoelea. Idadi yake ni mara kumi zaidi ya watu wote. Mkusanyiko huo unatengeneza chembe nyingine kila baada ya miezi mine na kuhifadhi idadi ya chembe nyingine, kiasi ambacho zile zinazokuja hazipungui wala kuzidi zile zilizoondoka. Wala hazina matatizo ya makazi kwa sababu ya wingi, kama ilivyo kwa watu.

Hapa ndio kuna maajabu! Ubongo wa mifupa uzalishe mikondo ya damu ya aina na iliyo na kazi tofauti tofauti yenye chembe nyekundu na nyeupe zinazoua na zinazokinga, Vipi basi jinsi moja ilete jinsi nyingi tofauti tofauti? Kwani ngamia anaweza kuzaa ndovu, tena azae mamba, kisha azae kicheche? Lakini kwenye damu linapatikana hilo. Haya ni maajabu kweli! Kwa ufupi kabisa ni kwamba chembe hai hivi sasa zimekuwa ndio gumzo kubwa la utafiti wa kisayansi na njia yake mpya; pengine ni njia pekee ya kufahamu siri za uhai.”

Umeona maajabu haya! Kiumbe kidogo ambacho hakiwezi kuonekana isipokuwa kwa kukuzwa mara elfu, tena hakiwezi kupasuliwa ila kwa mwangaza, unywele kwake ni kama ndovu aliye kwenye chungu chungu.

Pamoja na yote haya, kiumbe hiki kina viungo, mishipa, utando na mengineyo; kama mwanadamu. Kisha viumbe hivi, vya ajabu, vinafanya maskani yake ndani ya mwili wa mtu, vikiwa ni mamilioni, kwa kiasi cha miezi mine kisha vinakuja vingine kwa idadi ile ile ya vile vilivyoondoka bila ya kuzidi wala kupungua; kisha vingine na vingine na kuendelea.

Je, hii yote ni sadfa? Je, sadfa inaweza kukaririka mara bilioni. Je, viungo vyote hivyo, utando na nyuzi zilizofumwa kwa nidhamu na mpangilio ni sadfa?

Je sadfa inaweza kuzalisha vitu vya aina mbali mbali kutoka katika aina moja? Maswali yote haya na mengineyo yanataka jawabu.

Hapana! Tena hapana kabisa! Hakuna tafsiri ila kuweko Mjuzi mwenye uweza wa kuumba ulimwengu na uhai kwa neno ‘Kuwa’ na ikawa.

Baada ya hayo, kila sayansi inavyozidi kupiga hatua, ndio dalili na ushahi- di wa kuweko Muumba mwenye amri, unazidi. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu, aliyesema: “Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu”.

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَلَئِن شِئْنَا لَنَذْهَبَنَّ بِالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ ثُمَّ لَا تَجِدُ لَكَ بِهِ عَلَيْنَا وَكِيلًا ﴿٨٦﴾

86. Na tungelipenda, tungeliyaondoa tuliyokupa wahyi; kisha usingelipata wakili wa haya juu yetu.

إِلَّا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ إِنَّ فَضْلَهُ كَانَ عَلَيْكَ كَبِيرًا ﴿٨٧﴾

87. Isipokuwa rehema itokayo kwa Mola wako. Hakika fadhila yake kwako ni kubwa.

قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا ﴿٨٨﴾

88. Sema: Lau wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’an, basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ فَأَبَىٰ أَكْثَرُ النَّاسِ إِلَّا كُفُورًا ﴿٨٩﴾

89. Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur’an kwa kila mfano, lakini watu wengi wamekataa isipokuwa kukanusha tu.

TUNGELIPENDA TUNGELIONDOA

Aya 86- 89

MAANA

Na tungelipenda, tungeliyaondoa tuliyokupa wahyi.

Razi anasema, katika kufasiri Aya hii, kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kubainisha, katika Aya iliyotangulia, kuwa yeye amewapa elimu kidogo tu, hapa anabainisha kwamba yeye lau angelitaka kuwaondolea hiki kidogo, angeliweza, Na hilo ni kwa kufuta kuhifadhika kwake moyoni na maandishi yake ya vitabuni.

Kisha usingelipata wakili wa haya juu yetu, utakayemtegemea akutetee kukurudishia tulichokichukua kwako.Isipokuwa rehema itokayo kwa Mola wako ; Hiyo pekee ndiyo inayoweza kukurudishia ambacho tungekichukua kwako.

Hakika fadhila yake kwako ni kubwa kutokana na elimu aliyokupa na ubwana juu ya watu wote.

Sema: lau wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’an, basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.

Umepita mfano wake katika Juz 1 (2: 23).

Hakika tumewaeleza watu katika hii Qur’an kwa kila mfano, katika yanayohusiana na itikadi, sharia na maadili. Na tukaweka hoja mkataa na dalili wazi, lakini watu wengi wamekataa isipokuwa kukanusha tu, na kuwa mbali na haki. Kwa sababu iko chungu na ni nzito, hawawezi kuivumilia isipokuwa wenye takua.

وَقَالُوا لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ تَفْجُرَ لَنَا مِنَ الْأَرْضِ يَنبُوعًا ﴿٩٠﴾

90. Na walisema: hatutakuamini mpaka utuchimbulie katika ardhi hii chemchemi.

أَوْ تَكُونَ لَكَ جَنَّةٌ مِّن نَّخِيلٍ وَعِنَبٍ فَتُفَجِّرَ الْأَنْهَارَ خِلَالَهَا تَفْجِيرًا ﴿٩١﴾

91. Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu na utupitishie mito kati yake ikimiminika.

أَوْ تُسْقِطَ السَّمَاءَ كَمَا زَعَمْتَ عَلَيْنَا كِسَفًا أَوْ تَأْتِيَ بِاللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ قَبِيلًا ﴿٩٢﴾

92. Au utuangushie mbingu vipande vipande, kama ulivyodai, au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika ana kwa ana.

أَوْ يَكُونَ لَكَ بَيْتٌ مِّن زُخْرُفٍ أَوْ تَرْقَىٰ فِي السَّمَاءِ وَلَن نُّؤْمِنَ لِرُقِيِّكَ حَتَّىٰ تُنَزِّلَ عَلَيْنَا كِتَابًا نَّقْرَؤُهُ قُلْ سُبْحَانَ رَبِّي هَلْ كُنتُ إِلَّا بَشَرًا رَّسُولًا ﴿٩٣﴾

93. Au uwe na nyumba ya dhahabu au upae mbinguni, Na hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie Kitabu tukisome. Sema: ametakasika Mola wangu! Kwani mimi ni nani, isipokuwa ni mwanadamu Mtume?

وَمَا مَنَعَ النَّاسَ أَن يُؤْمِنُوا إِذْ جَاءَهُمُ الْهُدَىٰ إِلَّا أَن قَالُوا أَبَعَثَ اللَّـهُ بَشَرًا رَّسُولًا ﴿٩٤﴾

94. Na nini kilichowazuia watu kuamini ulipowajia utume, isipokuwa walisema: je, Mwenyezi Mungu hupeleka mwanadamu kuwa Mtume?

قُل لَّوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَّسُولًا ﴿٩٥﴾

95. Sema: Lau ingelikuwa duniani kuna Malaika wanaotembea kwa utulivu, basi bila ya shaka tungeliwateremshia Malaika kuwa Mtume wao.

قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿٩٦﴾

96. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.

KUFIKIRIA MALI

Aya 90-96

KUJIPENDA

Kila mmoja wetu anajipenda; awe mwana mume au mwanamke, mzee au mtoto, mwenye takua au muovu n.k. Ni binadamu gani asiyekuwa na shauku na maisha yake na kutetea heshima yake na uhalisi wake? Lau si hivyo uhai usingeendelea kuwako wala tusingeendelea, Hakuna tofauti katika kujipenda huko baina ya watu; isipokuwa tofauti iko katika aina zifutazo:-

Kuna yule anayekuwa kwenye msingi wa maumbile na akili. Hili linafa- hamika kutokana na jinsi mtu anavyoheshimu haki za wengine, kutosheka na alichoandikiwa kilichotokana na jasho lake na kusaidiana na kila mwenye kutumai kheri na manufaa ya watu kwa namna moja au nyingine; bali hata kujitolea juu ya hilo.

Kwani mwenye kutoa na kujitolea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, atakuwa amejipenda, atake asitake, kwa sababu Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa mwenye kufanya wema, vile vile jamii inamsifu na kumtukuza yule mwenye kujitolea kwa ajili ya hiyo jamii.

Na kuna yule anayejipenda kwa kutumia yale yanayopituka akili, dini na uhalisi. Hili linafahamika kutokana na tamaa ya mtu ambaye haioni umuhimu wala manufaa ya mwingine isipokuwa wake.

Hili halikubaliki na mantiki yoyote; hata ya yahisia na ya kuonekana; sawa na alivyosema Mwenyezi Mungu: “Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi, Hao ndio walioghafilika.” Juz; 9 (7: 179). Hawa wako kila mahali na kila wakati; miongoni mwao ni wale aliowaashira Mwenyezi Mungu kwa kuli zake zifuatazo:-

1. Na walisema: hatutakuamini mpaka utuchimbulie katika ardhi hii chemchem.

wapenda raha katika washirikina walitoa pendekezo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa awachimbulie chemchem au mto, wao sio watu wengine, kwa ajili ya chumo na faida. Kuna mapokezi yanayosema kuwa vijoho na wapenda anasa walisema: Ewe Muhammad! Hii ardhi ya Makka ni finyu, basi yaondoe majabali yake na utuchimbulie chemchem ili tunufaike na ardhi.

2.Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu na utupitishie mito kati yake ikimiminika.

Yaani kama hutatuchimbulia chemchem, basi angalu jichimbulie wewe, ili uwe unafanana na hadhi ya juu, Lakini ukiwa huna kitu basi wewe unatakikana uwasikilize walio nacho. Kwamba mali peke yake ndiyo itakayomfanya aliye nayo awe anafaa kuwa kiongozi na bwana mkubwa. Hawakujua kuwa risala ya Muhammad(s.a.w.w) ni utajiri mkubwa wa mtu, uhai wake, na kwamba Muhammad ni rehema kwa watu wa ardhini itakayowaokoa na ufukara, ujinga, dhulma na utaghuti. Wapi na wapi wanaoabudu mali na kupigana vikumbo na tamaa waweze kujua rehema na kheri?

3.Au utuangushie mbingu vipande vipande, kama ulivyodai, au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika ana kwa ana.

Walitaka wachimbuliwe chemchem yao au yake; kam sio hivyo au vile, basi awalete adhabu kutoka mbinguni au Mwenyezi Mungu mwenyewe aje na malaika kushuhudia kuwa Yeye ni Mtume.

Hii vile vile inatokana na fikra yao kwamba anayestahiki uongozi ni tajiri, sio fukara. Dalili ya hilo ni kule kuweka sharti la kumwamini Muhammad na jambo wanaloliona kuwa haliwezekani. Ni wazi kuwa kulazimisha jambo lisilowezekana maana yake ni kung’ang’ania matakwa yao ya kuchimbuliwa chemchem ardhini; sawa na kusema: Sifanyi hivi mpaka ngamia apite kwenye tundu ya sindano.

4.Au uwe na nyumba ya dhahabu.

Yaani iliyojengwa kwa dhahabu au iliyopambwa nayo. Hii vile vile inatokana na fikra ya mali.

Au upae mbinguni.

Nalo hili linafungamana na jambo lisilowezekana. Maana yake ni kung’ang’ania kuwa mali ndio kitu pekee cha kumweka mtu kwenye cheo.

Na hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie Kitabu tukisome.

Baadhi ya wafasiri wapya wanasema: “Unadhihiri utoto wa kuhafamu na kufikria; kama unavyodhihiri ukaidi wa kipumbavu.” Lakini hapana huo si utoto wala si upumbavu; isipokuwa hilo linatokana na ufisadi, kujibagua, uporaji, unyang’anyi na kuabudu mali. Kitu kinachofahamisha hilo zaidi ni kule kupendekeza na kuweka sharti la kumfuata Mtume awe na nyumba ya dhahabu kuwa ndio muabudiwa wao wa kwanza na ndio mfano wao mkuu.

Sema: Ametakasika Mola wangu! Kwani mimi ni nani, isipokuwa ni mwanadamu Mtume?

Anayefuata amri ya yule aliyemtuma na kukatazika kwa makatazo yake:

وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ﴿٣٨﴾

“Haiwi kwa Mtume kuleta muujiza isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.” Juz; 13 (13:38).

Na nini kilichowazuia watu kuamini ulipowajia utume, isipokuwa walisema: je, Mwenyezi Mungu hupeleka mwanadamu kuwa Mtume?

Wafasiri, akiwemo Tabrasi na Razi, wameiangalia Aya hii kuwa haiungani na Aya zilizotangulia na wakasema katika kuifasiri: Hakika washirikina wa Makka hawakumwamini Muhammad(s.a.w.w) kwa sababu wao walikuwa wakiitakidi kuwa mjumbe ni lazima awe ni katika jinsia ya malaika, si katika jinsia ya watu. Lakini tafsiri hiyo iko mbali sana kutokana na njia zifuatazo:-

Washirikina wa kikuraishi walikuwa wakiamini utume wa Ibrahim na kwamba wao wanatokana na kizazi chake.

Kauli ya washirikina: ‘Hatutakuamini mpaka utuchimbulie,’ inafahamisha kuwa wanaamini risala ya binadamu; isipokuwa walitoa sharti la kuwa Mtume awe tajiri: “Na walisema: kwanini hii Qur’an haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii” (43:31) Makusudio ya mtu mkubwa ni Walidi bin Mughira, katika viongozi wa Makka au Urwa bin Masud katika viongozi wa Taif.

Lau ingelikuwa tafsiri kama wanavyosema, basi washirikina wangelikuwa na udhuru katika kupinga kwao utume wa Muhammad (s.a.w.), kwa sababu watakuwa wanafanya lile wanaloliitakidi, na Mwenyezi Mungu amewasifu kwenye Aya nyingi kuwa wanadhihirisha yale waliyoyaficha:

بَلْ بَدَا لَهُم مَّا كَانُوا يُخْفُونَ مِن قَبْلُ ﴿٢٨﴾

“Bali yamewadhihirikia waliyokuwa wakiyaficha zamani,” Juz, 7 (6:28)

“Na wakazikataa kwa dhulma na kujitia uluwa na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo.” (27:19).

Kwa ufupi ni kuwa maana sahihi ya Aya ni kwamba washirikina wali- poshindwa na hoja ya utume wa Muhammad, walikimbilia ubabaishaji na kujaribu kuwapoteza wajinga wasiokuwa na akili.

Ndio wakasema kama mbinu tu za kuhadaa, kuwa Mwenyezi Mungu hamtumi Mtume binadamu, isipokuwa Malaika tu. Walisema haya wakiwa wanajua kwamba wao ni waongo. Ndio maana Mwenyezi Mungu akasema ‘Ispokuwa walisema’ na wala hakusema walidhani n.k. Hii inafahamisha kuwa kupinga kwao ni kiasi cha inadi tu ya kauli si ya itikadi.

Sema: Lau ingelikuwa duniani kuna Malaika wanaotembea kwa utulivu, Yaani wanaotembea kama wanadamubasi bila ya shaka tun- geliwateremshia Malaika kuwa Mtume wao.

Hekima ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) inataka apeleke Mtume kwa viumbe wake kutokana na jinsi yao. Wakiwa ni watu basi mtume wao atatokana na wao na wakiwa ni Malaika basi watakuwa hivyo hivyo. Kwa sababu jinsia inapendelea zaidi kwenye jinsia yake:

لَقَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْ أَنفُسِهِمْ ﴿١٦٤﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumini kwa kuwaletea Mtume miongoni mwao” Juz. 4 (3:164).

Washirikina wanajua hilo, lakini wanafanya vitimbi na hadaa. Umetangulia mfano wake katika Juz.7 (6:9).

Unaweza kuuliza: Jibril ni Malaika naye alikuwa mjumbe wa Mungu kwa Muhammad ambaye ni mtu, imekuwaje? Jibu: baina ya hawa wawili kuna aina fulani ya kukurubiana katika jinsi; kwamba kila mmoja wao ni mjumbe kutoka kwa Mungu.

Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.

Mwenyezi Mungu ni shahidi wa Muhammad kwa miujiza aliyoidhihirisha mikononi mwake, historia inashuhudia heri ya utu iliyopatikana kutokana naye na risala yake inashuhudia kwamba yeye ni rehema kwa viumbe na lolote katika sera ya Muhammad ni hoja tosha ya ukweli wake na utukufu wake.

وَمَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِ وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُمْ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِهِ وَنَحْشُرُهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ عُمْيًا وَبُكْمًا وَصُمًّا مَّأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ كُلَّمَا خَبَتْ زِدْنَاهُمْ سَعِيرًا ﴿٩٧﴾

97. Na anayeongozwa na Mwenyezi Mungu ndiye aliyeongoka na anayempotoa, basi, hutawapatia walinzi wasiokuwa Yeye. Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali ya kukokotwa juu ya nyuso zao wakiwa ni vipofu na mabubu na viziwi. Makazi yao ni Jahannam. Kila moto ukifanya kuzimika tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu.

ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُم بِأَنَّهُمْ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا وَقَالُوا أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا وَرُفَاتًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ خَلْقًا جَدِيدًا ﴿٩٨﴾

98. Hayo ni malipo yao kwamba wao walizikataa ishara zetu na wakasema: je, tutakapokuwa mifupa na mapande yaliyosagika, je tutafufuliwa kuwa viumbe wapya?

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ قَادِرٌ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُمْ وَجَعَلَ لَهُمْ أَجَلًا لَّا رَيْبَ فِيهِ فَأَبَى الظَّالِمُونَ إِلَّا كُفُورًا ﴿٩٩﴾

99. Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mbingu mfano wao? Na yeye amewawekea muda usio na shaka yoyote, lakini madhalimu hawataki isipokuwa ukafiri.

قُل لَّوْ أَنتُمْ تَمْلِكُونَ خَزَائِنَ رَحْمَةِ رَبِّي إِذًا لَّأَمْسَكْتُمْ خَشْيَةَ الْإِنفَاقِ وَكَانَ الْإِنسَانُ قَتُورًا ﴿١٠٠﴾

100. Sema, lau mngelikuwa mnamiliki hazina ya rehema ya Mola wangu, basi mngeliizuia kwa kuchelea kuisha. Na mtu ni mchoyo sana.

ALIYEONGOZWA NA MUNGU

Aya 97-100

MAANA

Na anayeongozwa na Mwenyezi Mungu ndiye aliyeongoka na anayem- potoa, basi, hutawapatia walinzi wasiokuwa Yeye.

Hii ni kumwelezea aliye mwema; yaani anayekuwa hivyo mbele ya Mwenyezi Mungu; na wala sio yule watu wanayesema kuwa ni mwema. Kuna Hadith isemayo: “Dhahiri ni ya watu na batini ni ya Mungu.” Katika Nahjulbalagha imeelezwa: ”Utajiri na ufukara ni baada ya kuonekana kwa Mungu.”

Wafisadi na wapotevu hawana wa kuwanusuru wala kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7: 178). Ama adhabu ya wapotevu wanaopoteza, ameiashiria Mwenyezi Mungu kwa kusema:

Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali ya kukokotwa juu ya nyuso zao wakiwa ni vipofu na mabubu na viziwi. Makazi yao ni Jahannam. Kila moto ukifanya kuzimika tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu.

Hili ni fumbo la uchungu wa adhabu na ukali wake kwa yule Mwenye kupinga hisabu na adhabu yake mpaka ajue aliyoyapinga:

كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا أُعِيدُوا فِيهَا وَقِيلَ لَهُمْ ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ ﴿٢٠﴾

“Na wataambiwa: onjeni adhabu ya moto ambayo mlikuwa mkiikadhibisha” (32:20).

Na hayo ni malipo yao kwamba wao walizikataa ishara zetu pamoja na ufafanuzi wa kutokea ufufuo. Walikanusha na wakapinga si kwa chochote ila ni kwa kuona ni mbali hilo.

Na wakasema: je, tutakapokuwa mifupa na mapande yaliyosagika, je tutafufuliwa kuwa viumbe wapya?

Imekwishatangulia Aya hii neno kwa neno katika Aya ya 49 ya Sura hii.

Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mbingu mfano wao? Na yeye amewawekea muda usio na shaka yoyote, lakini makafiri hawataki isipokuwa ukafiri.

Makusudio ya muda hapa ni muda wa ufufuo na kwamba huo utakuwa tu. Wameukana na hali wanaona kuumbwa kwa mbingu na ardhi huku wakikubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziumba na akazipangilia vizuri kwa uweza wake, lakini wakasema kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kuwarudisha tena baada ya kutoweka, kwa vile hilo ni jambo zito.

Ndio Mwenyezi Mungu akawaambia kuwa mwenye kuweza kukifanya kitu bila ya kitu basi ana uweza zaidi kukikusanya kitu hicho baada ya kutawanyika.

Maana ya Aya hii yamekwisha tangulia kwenye Aya nyingi, Angalia Juz.13 (13:5).

Hebu tusome kwa pamoja hoja hizi za kufunga mdomo wa mpinzani wa ufufuo, kwa mfumo usiokuwa na ushabiki; kisha useme: Ole wao wenye kukadhibisha:

“Walisema: Je, tutakapokufa na tukawa mchanga na mifupa ndio tutafu- fuliwa? Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni ngano za watu wa kale.”

“Sema: Ni ya nani ardhi na mbingu na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?”

“Watasema ni ya Mwenyezi Mungu.”

“Sema: Basi je, hamkumbuki?”

“Sema ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa Arshi kuu?”

“Watasema ni Mwenyezi Mungu.”

“Sema: Basi Je, hamuogopi?”

“Sema: ni nani ambaye ufalme wa kila kitu umo mikononi mwake, naye ndiye alindaye na halindwi, ikiwa mnajua?”

“Watasema ni vya Mwenyezi Mungu”

“Sema: basi vipi mnadanganywa?” 23: (82 – 89).

Huu ni ushahidi wazi kwamba itikadi ya kiislamu iko kwenye misingi ya elimu na uhuru wa akili na rai, Tazama: Juz; 7 (6:4) “Kifungu hakuna udikteta katika ardhi wala mbingu.”

Sema lau mngelikuwa mnamiliki hazina ya rehema ya Mola wangu, basi mngeliizuia kwa kuchelea kuisha.

Rehema ya Mwenyezi Mungu inaenea kwenye kila jambo, kama vile afya, ufahamu, mali na neema nyinginezo, lakini makusudio yake hapa ni kuhusu mali, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t): “Kuhofia kuisha” na ile Aya ya 90 ya Sura hii.

Ubainifu wake ni kuwa Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake awaambie wapenda anasa kuwa nyinyi mlitaka Mwenyezi Mungu awazidishie mali zenu na utajiri wenu kwa kuchimbua mito ardhini, huku akiwa anajua kwamba nyinyi lau mtamiliki hazina ya mbingu na ardhi ambayo haishi, basi mngeendelea na ubahili wenu na uchoyo kwa kuhofia kuisha. Hili linatilia mkazo tuliyosema kwamba wapenda anasa hawafikirii isipokuwa mali.

Na mtu ni mchoyo sana

Katika Juz. 12 (11: 9) tumesema kuwa Qur’an, haikusudii, kwa wasifu huu, kumueleza binadamu alivyo; isipokuwa ni kutafsiri tabia ya binadamu katika badhi ya hali zake. kwa maelezo zaidi rudia huko.

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَلَا تُبَذِّرْ تَبْذِيرًا ﴿٢٦﴾

26. Na mpe jamaa wa karibu haki yake na maskini na mwana njia, wala usifanye ubadhirifu.

إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾

27. Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashetani, na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake.

وَإِمَّا تُعْرِضَنَّ عَنْهُمُ ابْتِغَاءَ رَحْمَةٍ مِّن رَّبِّكَ تَرْجُوهَا فَقُل لَّهُمْ قَوْلًا مَّيْسُورًا ﴿٢٨﴾

28. Na ikiwa unajipurukusha nao kwa kutaraji rehema ya Mola wako, basi sema nao maneno laini.

وَلَا تَجْعَلْ يَدَكَ مَغْلُولَةً إِلَىٰ عُنُقِكَ وَلَا تَبْسُطْهَا كُلَّ الْبَسْطِ فَتَقْعُدَ مَلُومًا مَّحْسُورًا ﴿٢٩﴾

29. Wala usiufanye mkono wako umefungwa shingoni mwako, wala usiunyooshe wote kabisa, utabaki mwenye kulaumiwa, mwenye kuishiwa.

إِنَّ رَبَّكَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿٣٠﴾

30. Hakika Mola wako humkunjulia riziki amtakaye na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni mwenye habari, aonaye.

وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلَاقٍ نَّحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا ﴿٣١﴾

31. Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao Hakika kuwaua ni hatia kubwa.

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

32. Wala msiikurubie zinaa; Hakika hiyo ni uchafu na njia mbaya.

وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَمَن قُتِلَ مَظْلُومًا فَقَدْ جَعَلْنَا لِوَلِيِّهِ سُلْطَانًا فَلَا يُسْرِف فِّي الْقَتْلِ إِنَّهُ كَانَ مَنصُورًا ﴿٣٣﴾

33. Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua), ila kwa haki. Na aliyeuliwa kwa kudhulumiwa, basi tumempa madaraka walii wake, lakini asipetuke mpaka katika kuua, kwani hakika yeye anasaidiwa.

وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا ﴿٣٤﴾

34. Wala msiikurubie mali ya yatima isipokuwa kwa njia bora zaidi, mpaka afikie kukomaa kwake; Na tekelezeni ahadi. Hakika ahadi itasailiwa.

وَأَوْفُوا الْكَيْلَ إِذَا كِلْتُمْ وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٣٥﴾

35. Na timizeni kipimo mnapopima, na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni kheri kweni na hatima njema.

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

36. Wala usifuatilie ambalo huna ujuzi nalo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitasailiwa.

وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولًا ﴿٣٧﴾

37. Wala usitembee katika Ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.

كُلُّ ذَٰلِكَ كَانَ سَيِّئُهُ عِندَ رَبِّكَ مَكْرُوهًا ﴿٣٨﴾

38. Hayo yote ubaya wake ni wenye kuchukiza mbele ya Mola wako.

ذَٰلِكَ مِمَّا أَوْحَىٰ إِلَيْكَ رَبُّكَ مِنَ الْحِكْمَةِ وَلَا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتُلْقَىٰ فِي جَهَنَّمَ مَلُومًا مَّدْحُورًا ﴿٣٩﴾

39. Hayo ni katika hekima alizokupa wahyi Mola wako. Usimfanye mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukalaumiwa, uliyetupwa.

WASIA 10

Aya 26 – 39

MAANA

1.Na mpe jamaa wa karibu haki yake na maskini na mwana njia wala usifanye ubadhirifu.

Amenukuu Tabrasi katika Majmaul-bayan kutoka kwa Assadiy, ambaye ni miongoni mwa wafasiri wakubwa, kwamba makusudio ya jamaa wa karibu ni jamaa wa Mtume(s.a.w.w) .

Abu Hayan Al-andalusi amenukuu kutoka kwa Imam Ali bin Husein(a.s) kwamba yeye amesema: “Hao ni jamaa wa Mtume(s.a.w.w) , Mwenyezi Mungu ameamrisha kuwapa haki yao kutoka katika hazina.

Amesema Abu Bakar Al-mua’firi Al-maliki katika Ahkamul-qur’an: “Anaingia katika jamaa wa karibu jamaa wa Mtume kuingia kwa kutangulia na kwa njia ya aula tu. Lakini hakika Aya ni ya ndugu wa mtu walio karibu zaidi. Ama jamaa wa karibu wa Mtume Mwenyezi Mungu amebainisha kuwahusu wao na akaeleza kwamba kuwapenda ndio ujira wa Mtume kwa yale aliyotuongoza.”

Imesemekana kuwa makusudio ya jamaa wa karibu ni yule ambaye ana haki ya kumtunza na kurithi, masikini ni muhitajia na mwananjia ni msafiri aliyekatikiwa njiani asiyekuwa na uwezo wa gharama za kurudi kwao. Hawa wawili wana haki ya zaka; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٦٠﴾

“Hakika sadaka ni ya (hawa) tu: Mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao na kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na mwana njia.” Juz.10 (9:60).

Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashetani, na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya wabadhirifu kuwa ni ndugu wa shetani, kwa sababu ubadhirifu ni jambo linalochukiwa na Mwenyezi Mungu na kila linalochukiwa na Mwenyezi Mungu linapendeza kwa shetani.

Hakuna anayetofautiana na wenzake kuwa maana ya ubadhirifu ni kutoa mali kwenye njia isiyokuwa yake na kuiweka mahali pasipokuwa pake, iwe kwa uchache au kwa wingi. Kwa ibara ya watu wa mantiki ni kwamba ubadhirifu ni katika aina si katika idadi.

Unaweza kuuliza kuwa : kauli ya isiyokuwa njia yake na pasipokuwa mahali pake inafanana na maneno yenye kutatiza ambayo yanahitaji ufafanuzi na maelezo; basi ni ipi hiyo njia yake na mahali pake?

Jibu : kila mwenye kutumia mali yake katika mambo yanayomletea madhara au yasiyokuwa na manufaa yoyote, basi huyo ni mwenye israfu, mbadhirifu na safihi, kikawaida na kisharia; isipokuwa mali anayoitoa kwa ajili ya kuvuta sigara. Tumedokeza kuhusu matumizi mabaya na kuzuiliwa kutumia matumizi ya kimali kwa mwenye kufanya hivyo, katika Juz. 4 (4:5).

WAKO WAPI WAADILIFU?

Swali la pili linaweza kuja hivi: Mtu ametumia mali yake kwa kunywa pombe, kula nyama ya nguruwe na mengineyo katika yaliyoharamishwa ambayo yanamletea manufaa ya sasa na madhara ya muda ujao. Mtu huyu watu wengi hawamuoni kuwa ni mbadhirifu wala safihi; sasa je, sharia ya kiislamu inawajibisha kuzuiliwa matumizi ya kimali, kwa vile yeye ni safihi mwenye kufanya israfu?

Jibu : Mtu mwenye akili anayo ruhusa ya kutumia mali yake bila ya kuiingiliwa; awe mumin au kafiri, fasiki au mwadilifu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Mkiwaona wana uwekevu, basi wapeni mali zao” Juz. 4 (4:6) na wala hakusema mkiwaona wana uwekevu wa dini au uadilifu. Imepokewa Hadith Mutawatur kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kwamba yeye amesema: “Watu wamesalitiwa na mali zao,” na wala hakusema waumini au waadilifu.

Kwa hiyo sharti pekee la kusihi matumizi haya ni uwekevu katika mali si katika dini. Lau ingelikuwa uadilifu na uongofu ni sharti la kusihi matumizi ya mtu katika mali yake, basi nidhamu ingeliharibika na maisha yangesimama, kwa sababu watu wa duniani wako kama tunavyowajua, tutawatoa wapi watu wa dini na waadilifu?

Hanafi, Malik na Hambali wako katika rai yetu hii. Ama Shafii, wamesema kuwa uongofu ndio unaofaa katika dini na mali, kama ilivyoelezwa katika kitab Al-mughni cha Ibn Abi quddama.

Na ikiwa unajipurukusha nao kwa kutaraji rehema ya Moa wako, basi sema nao maneno laini.

Wakusema nao hapa ni jamaa wa karibu, masikini na msafiri aliyeishiwa njiani. Maana ni kuwa, akikuuliza kitu katika mali na wala usipate cha kumpa na ukamuomba Mwenyezi Mungu amtosheleze yeye na akutosheleze wewe kutokana na fadhila yake na rehema yake, basi sema naye kwa kauli laini kwa kumpa maneno mazuri yatakyompa matumaini na matarajio katika moyo wake. Kuna Hadith isemayo: “ Ikiwa hamna wasaa wa kuwapa watu mali zenu basi mnao wasaa wa kuwapa maadili yenu” Mshairi naye anasema: Kutamka kuwe kwema ikiwa hali si njema.

UISLAMU NA NADHARIA YA MAADILI

2.Wala usiufanye mkono wako umefungwa shingoni mwako, wala usiunyooshe wote kabisa, utabaki mwenye kulaumiwa, mwenye kuishiwa.

Kipimo na uwiano ndio msingi wa kila kitu katika Uislam kiitikadi, kisharia na kimaadili; sio ki ulahidi na kiidadi ya waungu. Na si kwa kuondoa milki ya mtu wala kuweka milki ya utaghuti na wala sio udikteta wa kikundi cha watu au wa mtu mmoja wala si utawala wa kila anayetaka, sio utawa wala sio kuzama kwenye matamanio. Kila kitu kinakuwa na uhalali na uharamu:

وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾

“Na kila kitu kwake, ni kwa kipimo” Juz; 13 (13:8).

Kusema kwake ni kwa kipimo ni kuwa na nidhamu inayoafikiana na hekima na masilahi, hakuna kupetuka mpaka wala kupetusha mipaka; wala hivi hivi au kombokombo. Kila kitu kina mpaka wake mbele ya Mwenyezi Mungu ambayo ni wajibu kwa kila mtu asimame kwenye mipaka hiyo bila ya kuikeuka. Kwa mfano mipaka ya hukumu na utawala ni uadilifu; mipaka ya kumiliki ni kutomdhuru mtu au watu; mipaka ya matumizi ni kutofanya uchoyo wala kufanya ubadhirifu na matendo mengineyo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameuletea ibara uchoyo kwa kufunga mkono shingoni, kwa sababu mchoyo anazuia mkono wake kutoa. Na kauli yake: ‘wala usiunyooshe wote kabisa’ anakusudia mkono ambao hauzuii kitu. Mwisho wa wote hawa wawili ni mmoja – kuishiwa na lawama.

Mwenye israfu atauma mkono wa kuishiwa, kujuta na kulaumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu, watu na yeye mwenyewe, pale atakapokuwa mikono mitupu; wakati ambapo bakhili analaumiwa na kila mtu, na kuishiwa kwake kesho ni zaidi kuliko mbadhirifu. Jambo bora zaidi ni wastani.

Unaweza kuuliza : Je, hii ina maana Uislamu unakubaliana na nadharia ya Socrates inayosema: Kila ubora ni kati ya mabaya mawili. Kwa hiyo ushujaa ni wastani baina ya kujitutumua na woga, ukarimu ni baina ya israfu na uchoyo, unyenyekvu ni baina ya kutahayari na kukosa haya nk?

Jibu : Hapana! Kwani Uislam unapanga ubora na kuweka sharia ya hukumu kwa misingi ya masilahi ya mtu mmoja mmoja hadi watu wengi. Kila jambo ambalo linaendeleza maisha basi ni wajibu wa lazima kwa kiongozi na wajibu wa kutosheana (kifaya) kwa raia.

Na kila lenye manufaa kwa upande fulani basi ni bora; bali ni ibada ya wajibu kwa kila mwenye uweza au suna kulingana na kiwango cha manufaa. Mwenyezi Mungu anasema:

وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ﴿١٧﴾

“Ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi” Juz; 13 (13:17).

Mtume(s.a.w.w) amesema: “Bora ya watu ni yule wanayenufaika naye.” Dalili wazi zaidi ya hakika hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili ambaye anawaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.” Juz.9 (7:157).

Msingi huu wa Qur’an – masilahi - unaweza kulingana na nadharia ya wastani kwenye vitu vyenye wastani; kama vile ukarimu kuwa baina ya uchoyo na israfu. Lakini unatofautiana katika vitu visivyo na wastani; kama vile uaminifu ni dhidi ya hiyana, wala hakuna jingine la kuleta wastani kuwa ni baina ya uaminifu na hiyana; Tumezungumzia kuhusu maadili katika Juz. 6 (5:79).

Hakika Mola wako humkunjulia riziki amtakaye na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni mwenye habari aonaye.

Makusudio ya kumpimia ni kuifanya finyu. Kila kitu kiko mikononi mwake, riziki na zisizokuwa riziki. Kwa sababu Yeye ni mmliki wa milki zote, lakini hekima yake imetaka na kupitisha kutomruzuku yeyote isipokuwa kwa sababu za kiulimwengu ambazo ameziumba na kuziwekea njia za kuchuma mali n.k. Angalia Juz. 6(5: 66) na Juz; 13 (13: 26).

3.Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao pia. Hakika kuwaua ni hatia kubwa.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6: 151).

4.Wala msiikurubie zinaa. Hakika hiyo ni uchafu na njia mbaya.

Imekuwa ni uchafu kwa vile mwishilio wake ni kuvurugika na kuchanganyika nasaba. Inatosha zina kuwa ni uovu kwa vile ni katika sifa mbaya za kushutumiwa.

5.Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua), ila kwa haki.

Umetangulia mfano wake katika katika Juz. 8 (6: 151).

Na aliyeuliwa kwa kudhulumiwa, basi tumempa madaraka walii wake, lakini asipetuke mpaka katika kuua, kwani hakika yeye anasaidiwa.

Kila aliyeuawa bila ya kufanya kosa linalowajibisha kuuliwa basi ameuawa kwa dhulma. Walii wa aliyeuawa ni ndugu zake kwa upande wa baba. Ikiwa hawako basi ni hakimu wa sharia. Kupetuka mpaka katika kuua ni kuua wawili kwa mmoja; kama walivyokuwa wakifanya wakati wa jahilia.

Maana ni kuwa ndugu wa aliyeuawa kwa dhulma wana haki ya kuua aliyeua au kuchukua fidiya; kama ilivyoelezwa katika Hadith tukufu: “Mwenye kuua basi watu wa aliyeuawa wana hiyari mbili: wakipenda wataua na wakipenda watachukua fidiya.”

Kwa vile ndugu wa aliyeuawa wana haki hiyo, basi ni wajibu wa hakimu na kila mwislamu kusaidia kutimizwa haki hii; Yametangulia maelezo kuhusu haya katika Juz. 2 (2:178).

6.Wala msiikurubie mali ya yatima isipokuwa kwa njia bora zaidi, mpaka afikie kukomaa kwake.

Imekwishapita Aya kama hii kwa herufi zake katika Juz. 8 (6: 152).

7.Na tekelezi ahadi; Hakika ahadi itasailiwa.

Kila aliloliamrisha Mwenyezi Mungu na kulikataza ni wajibu kutekelezwa; ikiwa ni pamoja na mapatano ya bei, ajira n.k. Kwa maelezo zaidi angalia Juz. 6 (5:1).

Na timizeni kipimo mnapopima na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni kheri kwenu na hatima njema.

Kukamilisha kipimo ni wajibu wa kisharia na kidesturi; wala hauhusiki na dini kuliko dini nyingine au desturi kuliko desturi nyingine. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehimiza kukamilisha kipimo kwa mifumo mbalimbali; kama vile: pimeni kwa mizani zilizo sawa, timizeni kipimo na mizani, wala msipunguze na wala msipetuke mipaka. Siri ya hilo ni kwamba ustawi wa jamii hauwezi kuwa bila ya usawa wa vipimo.

KUSEMA BILA YA UJUZI

9.Wala usifuatilie ambalo huna ujuzi nalo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitasailiwa.

Neno kufuatilia limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu Qafwa lenye maana ya kufatilia athari ya jambo. Miongoni mwa majina ya Mtume(s.a.w.w) ni Almuqfi (mfuatiliaji) kwa vile yeye ni mtume wa mwisho.

Kusema jambo bila ya ujuzi ni vibaya hata kwa yule asiyemwamini Mungu na siku ya mwisho. Mwenyezi Mungu ametaja masikio, macho na moyo akikusudia mwenye vitu hivyo vitatu.

Na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu ataviuliza na kuviadhibu ikiwa vitawekewa vitu visivyovijua; kama vile lau mtu atasema nimesikia naye hakusikia, nimeona naye hakuona au ni ninaitakidi na kuazimia naye hana itikadi wala maazimio yoyote.

Hakuna tofauti baina ya anayekusudia uongo na anayekurupuka kusema jambo bila ya kulithibitisha. Kwani kusema kwa dhana na shubha ni kusema bila ya ujuzi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

إِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا ﴿٣٦﴾

“Hakika dhana haifai kitu mbele yake haki” Juz; 11 (10:36)

إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ ﴿١١٦﴾

“Hawafuati ila dhana na hawakuwa ila wenye kuzua tu.” Juz; 8 (6: 116)

Mwenyezi Mungu amelinganisha dhana na kuzua.

Kutokana na Aya hii yanajitokeza mambo yafuatayo:

(i) Kubatilika na uharamu wa Taqlid (kufuata) kwa yule mwenye uwezo wa kuchambua hukumu kutoka kwenye rejea zake. Kwa sababu ameacha elimu yake na akaumia elimu ya mwingine. Hii ni rai ya Shia Imamia. Zaydiya, Muu’tazila, Ibin Hazm, Sheikh Muhammad Abduh, Sheikh Shaltut na wengineo. Tumezungumza kwa ufafanuzi kuhusu taqlid katika Juz. 8 (2:259).

(ii) Uharamu wa kutoa hukumu kwa kutumia qiyas (kukisia) na istihsan (kuchukulia kuwa ni vizuri).

Qiyas ni kulinganisha jambo ambalo halikutajwa katika hukumu na jigine lililotajwa kutokana na kuwa na sababu moja.

Kwa mfano sharia kusema kuwa nyanya wa upande wa mama anarithi na ikanyamazia nyanya wa upande wa baba. Tukasema kuwa huyu pia atarithi kwa kukisia kuwa yeye pia ni nyanya.

Istihsan ilivyosimuliwa kutokana na Abu Hanifa ni kutoa hukumu kwa atavyoonelea mujtahidi kuwa ni vizuri bila ya kuweko dalili yoyote isipokuwa anavyoonelea yeye tu.

Rejea Kitabu Allami’ fi usulilfiqh cha Abu Is-haq, Ibrahim bin Ali bin Yusuf Fayruz Abadiy, uk; 65 chapa ya 1939. Mwenya kitabu hicho ametoa mfano wa mwenye kusema:

‘Nikifanya jambo fulani basi mimi ni Myahudi’ akifanya jambo hilo itabidi atoe kafara kwa kuchukulia kuwa ni kama aliyeapa kwa kusema: ‘Wallahi nikifanya jambo fulani basi mimi ni Myahudi.’

Kila mwenye kujasiri kutoa fatwa na kubainisha halali na haramu na yeye si kufu wa kufanya hivyo, basi atakuwa amesema uongo na kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake na atakuwa ni katika wale waliokusudiwa na ile Aya isemayo:

تَاللَّـهِ لَتُسْأَلُنَّ عَمَّا كُنتُمْ تَفْتَرُونَ ﴿٥٦﴾

“Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua” Juz; 14 (16:56)

Na kauli ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w) : “Mwenye kunisemea uongo kwa makusudi basi na ajichagulie makazi yake motoni” Kumsemea uongo Mwenyezi Mungu na Mtume ni kutoa riwaya kutokana nao au kunasibisha halali na haramu kwao.

Siku hizi mamufti wazushi wamekuwa wengi walioifanya dini kuwa ni njia ya kutafutia riziki na pazia ya kuwa wahaini na vibaraka. Wengine wameanzisha vyama vya kutumikia uzayuni na ukoloni, lakini vina majina ya kiislamu na waislamu ili kuwahadaa na kuwapoteza watu.

Sheikh mmoja aliniuliza kuhusu wake wa Habil na Qabil kuwa je, hao ni katika hurilaini wa peponi au sio? Nikamjibu kuwa masuala haya yanaju- likana kwa kunakili sio kwa kiakili, na nukuu yake haitumiwi isipokuwa ikiwa ni ya Qur’an au Hadith mutawatir wala hakuna nukuu yoyote ya hilo. Kwa hiyo inatupasa tunyamaze yale aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu.

Akasema: Itakuwaje? Je, tuseme tumeshindwa tutakapoulizwa? Nikamwambia: Je, tunatakikana tujue kila kitu kwa vile sisi tuna vilemba vya ushekhe?

Wala usitembee katika Ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.

Mjinga anaweza kuwa na kiburi na kujifanya mkubwa anapomiliki ghururi za dunia; kama vile jaha na mali. Lakini likimtokea jambo la ghafla katika mambo yaliyojificha, basi anakuwa mnyonge na kudangana hana la kufanya. Mwenye akili ni yule anayejijua, akafikiri na kuzingatia.

Kauli yake Mwenyezi Mungu‘Wala usitembee katika Ardhi kwa maringo’ ni kukataza kiburi na kuamrisha kunyenyekea. Kauli yake:‘Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima’ ni fumbo la kushindwa mtu na kwamba yeye ni mdhaifu wa kufikia anayoyataka; kama alivyo mdhaifu wa mwili wake kuweza kufikilia jabali kwa urefu na kuweza kuipasua ardhi kwa wayo wake.

Hayo yote ubaya wake ni wenye kuchukiza mbele ya Mola wako.

Hayo ni kuishiria yaliyotangulia kutajwa katika yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu na kuyakataza. Makusudio ya ubaya wake ni yale aliyoyakataza hasa. Maana ni kuwa vitu vyote hivi ambavyo amevikataza Mwenyezi Mungu anavichukia, na mwenye kuvifanya ni mwenye kughadhibikiwa na Mwenyezi Mungu na mwenye kustahili adhabu.

Hayo ni katika hekima alizokupa wahyi Mola wako.

Hayo ni ishara ya maamrisho na makatazo yaliyotanglia kutajwa. Hekima ni kukiweka kitu mahali pake; Hakuna mwenye shaka kwamba hukumu zake zote Mwenyezi Mungu ziko mahali pake. Na kwamba mwenye kuichukua atakuwa ameichukua kwa haki, heri na uadilifu.

Usimfanye mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukalaumiwa uliyetupwa.

Imetangulia Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Sura hii Aya 22. Mwenyezi Mungu ameanzia na kukataza shirki na akamalizia nako, kwa sababu tawhid ndio kianzio na lengo la Uislamu, dini ya Mwenyezi Mungu iliyo ya haki. Kwa kuwa hukumu zote zinatoka kwake, basi hakuna halali ila aliyoiamrisha wala haramu ila aliyoiharamisha.

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

أَفَأَصْفَاكُمْ رَبُّكُم بِالْبَنِينَ وَاتَّخَذَ مِنَ الْمَلَائِكَةِ إِنَاثًا إِنَّكُمْ لَتَقُولُونَ قَوْلًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾

40. Je, mola wenu amewachagulia waototo wa kiume na yeye akajichukulia watoto wa kike katika Malaika? Hakika nyinyi mnasema kauli kubwa.

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ لِيَذَّكَّرُوا وَمَا يَزِيدُهُمْ إِلَّا نُفُورًا ﴿٤١﴾

41. Hakika tumekwishabainisha katika Qur’an ili wapate kukumbuka, lakini haiwazidishii isipokuwa kuwa mbali.

قُل لَّوْ كَانَ مَعَهُ آلِهَةٌ كَمَا يَقُولُونَ إِذًا لَّابْتَغَوْا إِلَىٰ ذِي الْعَرْشِ سَبِيلًا ﴿٤٢﴾

42. Sema lau kama wangelikuwa pamoja naye miungu mingine, kama wasemavyo, basi wangelitafuta njia ya kumfikia Mwenye Arshi.

سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يَقُولُونَ عُلُوًّا كَبِيرًا ﴿٤٣﴾

43. Ametakasika na ametukuka juu kabisa na hayo wanayoyasema.

تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤٤﴾

44. Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na hapana kila kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake, lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye maghufira.

JE, MOLA WENU AMEWACHAGULIA WAVULANA?

Aya 40 – 44

MAANA

Je, mola wenu amewachagulia waototo wa kiume na yeye akajichukulia watoto wa kike katika Malaika?

Qur’an inazingatiwa kuwa ni hoja isiyokuwa na ubishi, katika yote iliyoyasema na kuyasajili; Aya hii inaelezea vile washirikina walivyokuwa wakiitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ana mabinti katika aina ya malaika. Vile vile walikuwa wakiitakidi kwamba mtoto wa kiume ni bora kuliko wa kike; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: “Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.” Juz; 14 (16:58).

Kwa hiyo basi wao walijinasibishia ubora na uduni wakamnasibishia Mungu. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawatahayariza na ujinga huu, akawaambia:

Hakika nyinyi mnasema kauli kubwa , kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu hana mshirika wala aliyeshabihiana naye. Lau angelikuwa na mtoto angelikuwa huyo mtoto wake atamrithi na kushabihiana naye, lau angelikuwa na mzazi angelikuwa mzazi wake ni mshirika wake kwenye utukufu na enzi, bali huyo mzazi angelikuwa ni mtukufu zaidi yake, kwa sababu yeye ndiyo sababu ya kupatikana kwake.

Pengine mantiki ya wajahili ni kwamba siri iliyowafanya wamnasibishie Mungu mabinti na wao watoto wa kiume, ni kuwa Mwenyezi Mungu hahofii ufukara kwa sababu ya kuwa na watoto wengi wala aibu ya kuwa na mabinti.

Hakika tumekwishabainisha katika Qur’an ili wapate kukumbuka, lakini haiwazidishii isipokuwa kuwa mbali.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameweka dalili na hoja za kupatikana kwake na umoja wake na akazifafanua kwa kupiga mifano na mifumo mbalimbali ili wafahamu na waelewe, lakini wao wameng’ang’ania njozi na kuiga. Wakazidi inadi na kuwa mbali.

Razi anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu amekithirisha kutaja dalili katika Qur’an; kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka washirikina wazifahamu na kuziamini; Hii inafahamisha kwamba Yeye, aliyetukuka, anafanya vitendo vyake kwa hekima na inafahamisha kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka imani kwa kila mmoja ni sawa aamini au asiamini.”

Kauli hii ya Razi inapingana na aliyoyaelezea mara kwa mara kwamba vitendo vya Mwenyezi Mungu havina sababu ya malengo, na kwamba Yeye ndiye aliyetaka kafiri awe kafiri; kama ilivyo kwa madhehebu ya Ashaira. Lakini Mwenyezi Mungu anataka kuinusuru haki na kuidhihirisha hata kwenye ulimi wa yule anayeipinga bila ya kujitambua.

Sema lau kama wangelikuwa pamoja naye miungu mingine, kama wasemavyo, basi wangelitafuta njia ya kumfikia Mwenye Arshi.

Watu wa tafsiri wametaja maana mbili za Aya hizi:

Kwanza: Ikisemwa kuwa kuna miungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu basi msiwahesabu hao waungu kuwa ni nyota, binadadamu, mawe au vitu vingine. Kwa sababu hivi vyote vimeumbwa na Mwenyezi Mungu, vinamwabudu na kujikurubisha kwake.

Basi mambo yakiwa hivi ni juu yenu enyi washirikiakina kumwabudu Mwenyezi Mungu; kama ambavyo vile manvyoviabudu vinamwabudu Yeye tu.

Maana au tafsiri ya pili ambayo ina nguvu zaidi ni: Lau kungelikuwa na waungu wengine, basi wangelipingana na Mwenyezi Mungu na wangelitafuta nji ya kufikia kwenye madaraka. Hakuna mwenye shaka kwamba kupingana na kuzozana viongozi kunaleta vurugu na ghasia; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّـهُ لَفَسَدَتَا فَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٢٢﴾

“Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu, bila shaka hizo mbingu na ardhi zingelifisidika,” (21:22).

Tumefafanua hayo katika kufasiri, Juz; 5 (5:48).

Ametakasika na ametukuka juu kabisa na hayo wanayoyasema.

Amejivua Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kauli ya madhalimu na washiriki- na kwamba Yeye ana washirika na watoto.

KILA KITU KINAMTAKASA (KINAMSABBIH)

Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na hapana kila kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake.

Ndio! Kila kitu kinamtaksa na kumsifu Mwenyezi Mungu Mtukufu, hilo halina shaka. Tasbih au utakasho wa kitu unatofautiana na kitu kingine kulingana na kilivyo hicho kitu.

Mwenye akili anamtakasa na kumsifu Mwenyezi Mungu kwa ulimi wake, vitu vingine vinamtakasa kwa lugha ya hali. Kwa maneno mengine vinamtakasa na kumsifu kwa jinsi vilivyopatikana umbile lake na mpangilio wake, kuwa yuko mpangiliaji mzuri aliyevifanya viwe hivyo vilivyo; sawa na unavyojulisha mchoro mzuri kuwa mchoraji ni hodari aliye bingwa.

Lugha ya hali ina nguvu na ni fasaha zaidi kuliko lugha ya maneno. Kwa sababu ya maneno inahitajia dalili, lakini ya hali hiyo yenyewe ni dalili inayopeleka kwenye elimu na yakini; Yamekwisha tangulia maelezo ya hayo katika kufasiri Juz; 13 (13:15).

Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake; Hakika Yeye ni Mpole Mwenye maghufira.

Hawawezi kufahamu walahidi na washirikina tasbihi zao, kwa sababu ya kujiweka mbali kwao na utukufu wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake au kwa sababu ya kuzembea kuchunguza na kutambua siri na maajabu ya ulimwengu.

Anasema Ibn Arabi katika kitabu Alfutuhatil-makkiyya Juz; 4: “Mwenyezi Mungu ana ishara aina kwa aina: Kuna zile zinazotambulika kwa kutumia akili, zinazotambulika kwa usikizi na zile zinazotambulika kwa kuona. Kwa hiyo ni juu ya kila mtu kutumia vyombo hivi kuweza kujua ishara za Mwenyezi Mungu ambazo amezitaja katika kitabu chake. Akishajua na kuamini kwazo na akatenda kwa mujibu wake basi atakuwa ni miongoni mwa watu wa Qur’an na watu mahususi wa Mwenyezi Mungu.”

Kisha akaendelea kusema Ibn Arabi: “Chukua kupatikana kote kuwa ni Kitabu kinachotamka haki” Hii ni kama kauli ya mmoja wa wataalamu wa elimu ya Mwenyezi Mungu: “Hakika Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: kimoja kinatamka kwa lugha ya makala, hicho ni Qur’an na kingine kinatamka kwa lugha ya hali nacho ni ulimwengu.”

وَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ جَعَلْنَا بَيْنَكَ وَبَيْنَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ حِجَابًا مَّسْتُورًا ﴿٤٥﴾

45. Na unaposoma Qur’an tunaweka baina yako na ya wale wasioamini Akhera pazia linalowafunika.

وَجَعَلْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ أَكِنَّةً أَن يَفْقَهُوهُ وَفِي آذَانِهِمْ وَقْرًا وَإِذَا ذَكَرْتَ رَبَّكَ فِي الْقُرْآنِ وَحْدَهُ وَلَّوْا عَلَىٰ أَدْبَارِهِمْ نُفُورًا ﴿٤٦﴾

46. Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu na tunaweka kwenye masikio yao uziwi, Na unapomtaja Mola wako peke yake katika Qur’an, basi wao hugeuka nyuma wakaenda zao.

نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَسْتَمِعُونَ بِهِ إِذْ يَسْتَمِعُونَ إِلَيْكَ وَإِذْ هُمْ نَجْوَىٰ إِذْ يَقُولُ الظَّالِمُونَ إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا رَجُلًا مَّسْحُورًا ﴿٤٧﴾

47. Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayosikilizia wanapokusikiliza, na wanaponon’gona, wanaposema hao madhalimu: nyinyi hamfuati isipokuwa mtu aliyerogwa.

انظُرْ كَيْفَ ضَرَبُوا لَكَ الْأَمْثَالَ فَضَلُّوا فَلَا يَسْتَطِيعُونَ سَبِيلًا ﴿٤٨﴾

48. Tazama vipi wanavyokupigia mfano, Basi wamepotea, kwa hiyo hawawezi kuipata njia.

UNAPOSOMA QUR’AN

Aya 45 – 48

MAANA

Na unaposoma Qur’an tunaweka baina yako na ya wale wasioamini Akhera pazia linalowafunika.

Kuna kauli nyingi katika kufasir Aya hii; Yenye nguvu zaidi ni ile isemayo kuwa jamaa katika washirikina walikuwa – Muhammad anaposoma Qur’an – wanajaribu kumzuia kwa kumuudhi, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia endelea kusoma Qur’an na kutoa mwito wa Mwenyezi Mungu wala usichoke.

Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu na tunaweka kwenye masikio yao uziwi.

Hili ni fumbo la inadi ya washirikina. Ama kunasibisha vifuniko na uziwi kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), tumekuzungumzia kwa ufafanuzi katika kufasiri Juz; 7 (6:25). Hiyo ni mfano wa Aya hii kinukuu na kimaana.

Na unapomtaja Mola wako peke yake katika Qur’an, basi wao hugeuka nyuma wakaenda zao.

Walikuwa washirikina, inaposomwa Qur’an, wanapomsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Lailaha illallah (hapana Mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu) basi wanaachana naye na kwenda zao huku wakisema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ ﴿٥﴾ وَانطَلَقَ الْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ امْشُوا وَاصْبِرُوا عَلَىٰ آلِهَتِكُمْ ﴿٦﴾

“Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu. Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nenedeni zenu na dumuni na miungu yenu.” (38: 5-6).

Sio siri kuwa upinzani huu ni kwa vile tu tamko la tawhid linakusanya msingi wa kusema: “Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu ni yule mwenye takua zaidi” (49: 13). Sio utabaka na ubaguzi.

Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayosikilizia wanapokusikiliza, na wanaponon’gona, wanaposema hao madhalimu: Nyinyi hamfuati isipokuwa mtu aliyerogwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema: ‘na tunaweka kwenye masikio yao uziwi’ sasa anasema: Sisi tunajua vizuri kwamba wewe wakati unaposoma Qur’an washirikina hawakusikilizi kwa moyo safi, bali wanakusikiliza kwa kwa roho ya chuki, inadi na kiburi, kisha wanaambiana na pia kuwaambia wengine, kuwa Muhammad ni mchawi ameingiwa na jini linalozungumza hekima na ufasaha huu kwenye ulimi wake; itakuwaje azungumze hivi naye hajui kusoma wala kuandika, tena hana hazina ya dhahabu au fedha wala hana shamba la mitende na mizabibu.

Hii ndio fikra yao ya kitabaka, kwamba mwenye mali tu ndio anayeweza kuwa na cheo kitukufu kiwe cha dini au cha kawaida: “Na walisema: kwa nini hii Qur’an haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii” (43:31) Ama akili, ukweli na uaminfu kwao hauna maana.

Tazama vipi wanavyokupigia mfano.

Walizidi mno kwa Muhammad(s.a.w.w) kwa vile kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kutamka maneno ya Mwenyezi Mungu; mara wakamwita mwendawazimu, mara mchawi, mara kuhani na mara nyingine wakamwita mshairi.

Muhammad ambaye ametumwa kukamilisha tabia njema, amekuwa mchawi na mwendawazimu? Kwa nini amekuwa hivyo? Kwa vile yeye anatamka haki na kuitolea mwito na wala hakukubaliana na matamanio ya wabatilifu na wafisadi. Zaidi ya hayo hana farasi wala mali.

Kwa ufupi ni kwamba watu wa matamanio na matakwa, hisia zao ziko upande mmoja tu, matamanio na masilahi yao binafsi. Hawasikii wala hawaoni isipokuwa kwayo tu; kiasi cha kuhalalisha yote kwenye hawa zao na matamanio. Kwa hali hii ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na juu ya macho yao pana kifuniko” Juz, 1 (2:7) na tafsiri ya kila Aya iliyo na maana haya katika maneno ya Mtukufu Aliyetukuka.

Basi wamepotea, kwa hiyo hawawezi kuipata njia, ya kuwakadhibisha wenye haki, isipokuwa uzushi, upotevu, ulaghaii, uadui, njama na rushwa.

وَقَالُوا أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا وَرُفَاتًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ خَلْقًا جَدِيدًا ﴿٤٩﴾

49. Na wakasema: je, tutakapokuwa mifupa na mapande yaliyosagika, je tutafufuliwa kuwa viumbe wapya?

قُلْ كُونُوا حِجَارَةً أَوْ حَدِيدًا ﴿٥٠﴾

50. Sema: kuweni hata mawe au chuma.

أَوْ خَلْقًا مِّمَّا يَكْبُرُ فِي صُدُورِكُمْ فَسَيَقُولُونَ مَن يُعِيدُنَا قُلِ الَّذِي فَطَرَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ فَسَيُنْغِضُونَ إِلَيْكَ رُءُوسَهُمْ وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هُوَ قُلْ عَسَىٰ أَن يَكُونَ قَرِيبًا ﴿٥١﴾

51. Au umbo lolote mnaloliona kubwa katika vifua vyenu, Watasema: Ni nani atakayeturudisha tena? Sema: Ni huyo aliyewaumba mara ya kwanza. Watakutikisia vichwa vyao Na watasema: lini hayo? Sema: asaa yakawa karibu.

يَوْمَ يَدْعُوكُمْ فَتَسْتَجِيبُونَ بِحَمْدِهِ وَتَظُنُّونَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٥٢﴾

52. Siku atakayowaita nanyi mkamwitikia kwa kumsifu. Na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mchache tu.

TUTAKAPOKUWA MIFUPA NA MAPANDE YALIYOSAGIKA

Aya 49 – 52

MAANA

Na wakasema: je, tutakapokuwa mifupa na mapande yaliyosagika, je tutafufuliwa kuwa viumbe wapya?

Hii ndio hoja ya mwenye kutilia shaka ufufuo, tangu zamani hadi sasa, kuwa itakuwaje mtu arudi kuwa hai baada ya kuwa vumbi linalotifuka?

Jibu : Yule aliyeweza kuumba kitu na kukifanya kiwepo baada ya kuwa hakipo, basi ni wazi kuwa anaweza kukikusanya baada ya kutawanyika. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameitaja shaka hii na jawabu lake kwenye Aya kadhaa; miongoni mwazo ni ile iliyo katika sura Yasin:

وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ ﴿٧٨﴾ قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ ﴿٧٩﴾

“Akasema: ni nani huyo atakayeihuisha mifupa nayo imekwisha mung’unyika? Sema: atahiuisha huyohuyo aliyeiumba mara ya kwanza na Yeye ni mjuzi wa kila kuumba” (36: 78 – 79).

Tumelifafanua suala hili katika Juz; 13 (13:5).

Sema: kuweni hata mawe na chuma au umbo lolote mnaloliona kubwa katika vifua vyenu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia wale wanaokanusha ufufuo kuwa hata kama mtakuwa mawe au chuma au kitu kikubwa zaidi ya hivyo tutawaumba tu kuwa watu hai.

Anayeweza kuumba kutokana na chuma au jiwe au kitu kigumu zaidi ya hivyo, basi ni muweza zaidi wa kumrudishia uhai yule aliyempa uhai mwanzo. Kwa sababu kuvikusanya vitu baada ya kutawanyika ni rahisi zaidi kuliko kuvianzisha upya.

Kwa ufupi ni kuwa kumfufua mtu baada ya kufa ni wepesi zaidi kuliko kukifanya chuma kuwa mtu, Anayeweza hivi basi hashindwi kufanya vile.

Watasema: Ni nani atakayeturudisha tena kwenye uhaai baada ya kuwa mavumbi yanayopeperuka. Jibu la swali hili ni:

Sema: Ni huyo aliyewaumba mara ya kwanza.

Mwenye kurudisha ndiye yule aliyeanza; Kuanza na kurudisha ni kumoja tu; bali kurudisha ni wepesi zaidi, kwa sababu ni kurudisha ilivyokuwa. Tunasema hivi, kama mfano tu, tukijua kuwa Mwenyezi Mungu anaumba vichache na vingi na pia vidogo na vikubwa kwa neno.

كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾

“Kuwa! Na kikawa” (36:82).

Watakutikisia vichwa vyao kwa stihzai na kukadhibishaNa watasema: lini hayo? Makusudio ya swali hili ni kuona kuwa haiwezekani.

Sema: asaa yakawa karibu. Makusudio ya karibu hapa ni kuhakikika na kutokea, kwani ‘Kila lijalo liko karibu.’

Siku atakyowaita nanyi mkamwitikia kwa kumsifu.

Makusudio ya Siku ni siku ya Ufufuo, kuitwa ni kupuziwa parapanda, kuitikia ni fumbo la kutoka kwao makaburini na kumsifu ni kutii na kufuata:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ ﴿٥١﴾

“Na itapulizwa parapanda mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao” (36:51).

Na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mchache tu.

Watu watakapotoka makaburini watadhani kuwa wao hawakukaa duniani isipokuwa siku moja au sehemu ya siku:

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الْأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ ﴿١١٢﴾ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلِ الْعَادِّينَ ﴿١١٣﴾

“Atasema: mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka? Watasema tulikaa siku moja au sehemu ya siku,” (23:112- 113).


4

5

6

7

8

9