TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 14890
Pakua: 2106


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 19 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14890 / Pakua: 2106
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

Mwandishi:
Swahili

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَىٰ تِسْعَ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ فَاسْأَلْ بَنِي إِسْرَائِيلَ إِذْ جَاءَهُمْ فَقَالَ لَهُ فِرْعَوْنُ إِنِّي لَأَظُنُّكَ يَا مُوسَىٰ مَسْحُورًا ﴿١٠١﴾

101. Hakika tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize wana wa Israil; alipowajia na firauni akamwambia: Hakika mimi nakuona wewe umerogwa.

قَالَ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ بَصَائِرَ وَإِنِّي لَأَظُنُّكَ يَا فِرْعَوْنُ مَثْبُورًا ﴿١٠٢﴾

102. Akasema: Hakika umekwishajua kuwa hakuziteremsha hizi isipokuwa Mola wa mbingu na Ardhi, kuwa ni dalili. Hakika mimi nakuona, ewe firauni, umeangamia.

فَأَرَادَ أَن يَسْتَفِزَّهُم مِّنَ الْأَرْضِ فَأَغْرَقْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ جَمِيعًا ﴿١٠٣﴾

103. Na akataka kuwahamisha katika ardhi, Tukamzamisha yeye na waliokuwa pamoja naye wote.

وَقُلْنَا مِن بَعْدِهِ لِبَنِي إِسْرَائِيلَ اسْكُنُوا الْأَرْضَ فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ الْآخِرَةِ جِئْنَا بِكُمْ لَفِيفًا ﴿١٠٤﴾

104. Na tukawaambia, baada yake, wana wa Israil: kaeni katika ardhi, Na itakapokuja ahadi ya Akhera tutawaleta nyote pamoja.

TULIMPA MUSA ISHARA TISA

Aya 101 – 104

MAANA

Hakika tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi.

Yamewishatangulia maelezo, katika Aya kadhaa, kuhusu Musa(a.s) na watu wake na miujiza yake na pia kuhusu Firauni na wakuu wake na utaghuti wake.

Inawezekana kuwa mnasaba wa kutajwa miujiza ya Musa hapa, ni kuwa Mwenyezi Mungu alipotaja mapendekezo ya washirikina kwa Muhammad(s.a.w.w) , alifuatishia kuonyesha mapendekzo ya Firauni kwa Musa na matokeo yake yakawa ni balaa kwake; kwamba itatokea hivyo hivyo, lau Mwenyezi Mungu atajibu mapendekezo ya washirikina kwa Muhammad(s.a.w.w) .

Kwa sababu wao watayakataa yatakapowajia; sawa na walivyofanya watu wa Firauni na wangeliangamia kama alivyoangamia Firauni. Kwa hiyo kukosa kujibiwa ni heri kwao na Mwenyezi Mungu anajua yanayowafaa waja na yale ya kuwaharibia.

Musa ana ishara na miujiza mingi, ikiwemo ile ya kuifanya risala yake iwe nyepesi; kama vile kuondoka mifundo ya ulimi wake, kuneemeshwa na kufadhilishwa wana wa Israil kwa kutolewa maji katika jiwe, kuteremshiwa manna na salwa au kuhofishwa kwa kufunikwa na mlima. Mingine ni ya kumpa fundishoFirauni na watu wake ili waweze kuamini au malipo ya inadi yao.

Hiyo ndiyo miujiza tisa iliyoashiriwa na Aya. Iliyo dhahiri zaidi ni kugeuka fimbo kuwa nyoka, mkono kuwa mweupe na kuangamizwa makafiri baharini. Ama sita iliyobakia, mitano yake imeashiriwa na Aya hii:

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُّفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿١٣٣﴾

“Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu” Juz; 9 (7:133)

Na wa sita ni kuangamizwa mali zao: “Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanawapoteza watu na njia yako.

Mola wetu! Ziangamize mali zao na zitie shida nyoyo zao, Na hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumiza. Akasema Mwenyezi Mungu, maombi yenu yamekubaliwa. Basi muwe na msimamo wala msifuate njia ya wale wasiojua.” Juz; 11 (10:88-89).

Waulize wana wa Israil

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) . Makusudio ya wana wa israili ni wale walioamini; kama vile Abdullah bin Salam na maswahiba zake. Lengo la swali hili na jawabu ni kuwadhihirishia mayahudi na wasiokuwa mayahudi ukweli wa Mtume mtukufu kwa kila alilowaletea kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Alipowajia na Firauni akamwambia: Hakika mimi nakuona wewe umerogwa.

Yaani umchawi, kwa maana ya kuwa umepewa elimu ya uchawi, kwa dalili ya Aya nyingine isemayo: “Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.” Juz; 9 (7:109). Walisema hivyo baada ya kushuhudia fimbo inageuka kuwa nyoka mkubwa na mkono rangi ya maji ya kunde kuwa mweupe bila ya ubaya.

Akasema; hakika umekwishajua kuwa hakuziteremsha hizi isipokuwa Mola wa mbingu na Ardhi, kuwa ni dalili. Hakika mimi nakuona, ewe firauni, umeangamia.

Makusudio ya ‘hizi’ ni ishara tisa.

Firauni alipomwambia Musa, mimi nakuona u mchawi, Musa alimjibu kuwa unajua kwa hakika ukweli wa ishara na niliyokuletea na kwamba hizo ni dalili wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu zinazokuonyesha wewe na watu wote kuwa mimi ni mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini wewe unafanya inadi na kiburi kwa ajili ya kupupia cheo chako.

Ikiwa wewe unaniona kuwa mimi ni mchawi basi mimi ninakuona wewe umeangamia; na hayo ni malipo ya kukadhibisha kwako haki na atakayekuwako ataona. Kila mwenye kuipinga haki na akaona uzito kuambiwa basi huyo ni mwanachama wa Firauni na mila yake.

Na akataka kuwahamisha katika ardhi.

Aliyetaka kuwatoa ni Firauni, na waliotakiwa kutolewa ni Musa na watu wake. Maana ni kuwa Firauni alitaka ardhi ya Misri isikaliwe na Wana wa israil kwa kuwaua, kuwachukua mateka na kuwafukuza. Lakini janga likamgeukia yeye, kama inavyokuwa kwa kila taghuti.

Tukamzamisha yeye na waliokuwa pamoja naye wote.

Mwenyezi Mungu aliwangamiza baada ya kuwapatia hoja na dalili wazi, lakini wakakataa isipokuwa ukafiri na kupetuka mipaka.

Na tukawaambia, baada yake, wana wa Israil: kaeni katika ardhi.

Ardhi iliwakunjukia wana wa Israil, baada ya kupata amani kwa kuangamia Firauni, Mwenyezi Mungu akawapa hiyari ya kukaaa popote katika nchi. Ilitakikana washukuru Mungu kwa neema hii, lakini wao wakapetuka mipaka na wakafanya uovu:

Wakaabudu ndama badala ya Mwenyezi Mungu, wakasema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumbwa na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu ni fukara na wao ni matajiri, wakawaua mitume, wakala haramu na riba, wakaipotoa Tawrat, wakajaribu kumuua Bwana Masih, na kumzulia mama yake uovu na mengineyo aliyoyasajili Mwenyezi Mungu katika Tawrat, Injili na Qur’an na watu wakayasajili katika vitabu vya historia na vya Hadith vya zamani na vya sasa. Uzayuni unatosha kuwa ni ushahidi wa hakika ya kikundi hiki kiovu na kwamba hicho ni shari na balaa kwa ubinadamu.

Na itakapokuja ahadi ya Akhera tutawaleta nyote pamoja.

Maneno hapa wanaambiwa wana wa Israil na akhera ni Siku ya Kiyama, kuletwa pamoja ni mkusanyiko wa wanaotofautiana. Makusudio ni kutoa hadhari na kiaga kwa wale watakokuja katika wana wa Israil kuleteta fitina na ufisadi katika nchi.

Hii ndio dhahiri ya tamko la Aya, Lau ingelikuwa inafaa kufasiri Qur’an kwa maoni yetu, basi tungelisema kuwa neno ‘kuletwa pamoja’ linaashiria kujumuika mayahudi na uzayuni, kutoka huko na huko, katika ardhi ya Palestina na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawasalitia uovu mkali na itakuwa ni ahadi itakayotimizwa. Usawa ni tuliyoyaelezea katika Aya ya 4 ya sura hii, rudia huko.

وَبِالْحَقِّ أَنزَلْنَاهُ وَبِالْحَقِّ نَزَلَ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿١٠٥﴾

105. Na kwa haki tumeiteremsha na kwa haki imeteremka. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.

وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلًا ﴿١٠٦﴾

106. Na Qur’an tumeigawanya ili uwasomee watu kwa kituo; na tumeiteremsha kidogo kidogo.

قُلْ آمِنُوا بِهِ أَوْ لَا تُؤْمِنُوا إِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ سُجَّدًا ﴿١٠٧﴾

107. Sema, iaminini au msiiamini. Hakika wale waliopewa ilimu kabla yake, wanaposomewa, huanguka kifudifudi wanasujudu.

وَيَقُولُونَ سُبْحَانَ رَبِّنَا إِن كَانَ وَعْدُ رَبِّنَا لَمَفْعُولًا ﴿١٠٨﴾

108. Na wanasema: Ametakasika Mola wetu, Hakika ahadi ya Mola wetu lazima itimizwe.

وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا ﴿١٠٩﴾

109. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidishia unyenyekevu.

قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ وَلَا تَجْهَرْ بِصَلَاتِكَ وَلَا تُخَافِتْ بِهَا وَابْتَغِ بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا ﴿١١٠﴾

110. Sema, mwiteni Mwenyezi Mungu (Allah) au mwiteni Mwingi wa rehema (Rahman), kwa jina lolote mtakalomwita, Yeye ana majina mazuri. Wala usiisome jahara Swala yako wala usiifiche, bali tafuta njia baina ya hizo.

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

111. Na sema, sifa njema zote ni za ambaye hakujifanyia mtoto wala hana mshirika katika ufalme, wala hana msaidizi kwa sababu ya udhaifu na mtukuze kwa matukuzo makubwa.

KWA HAKI TUMEITEREMSHA

Aya 105 – 111

MAANA

Na kwa haki tumeiteremsha na kwa haki imeteremka.

Wafasiri wana kauli nyingi katika jumla mbili hizi; Yenye nguvu zaidi ni ile aliyoisema Tabrasi na Razi. Kwa ufupi wa kauli yao ni kuwa makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Na kwa haki tumeitremsha’, ni kwamba Qur’an imedhamini haki na makusudio ya ‘Na kwa haki imeteremka’ ni kwamba Mwenyezi Mungu kwa kuiteremsha Qur’an alitaka watu waiamini na waitumie. Hilo lilipatikana kwa hakika; ambapo waislamu waliiamini na wakaitumia wale wenye ikhlasi.

Sisi tuko pamoja na Razi na Tabrasi katika kufasiri jumla ya kwanza. Ama jumla ya pili, tuonavyo sisi ni kuwa kila walilokuwa nalo watu kabla ya kuteremshwa Qur’an na watakalokuwa nalo baada ya kuetremshwa, basi Qur’an inalikubali ikiwa ni la haki, kheri na masilahi.

Kwa maneno mengine ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kusema katika jumla ya kwanza kuwa ameiteremsha Qur’an kwa haki kheri na masilahi, katika jumla ya pili anasema pia Qur’an inakubaliana na kila lililo haki lenye kheri na masilahi wakati wowote litakapokuwa, kabla au baad aya Qur’an.

Kuna Aya zilizo na maana ya tafsiri hii; kama vile:

وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ ﴿١٧﴾

“Ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi” Juz.13 (13:17)

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ ﴿١٨٥﴾

“Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi wala hawatakii yaliyo mazito” Juz;2 (2:185).

Imam Ja’far As-swadiq(a.s) naye amesema:“Kila lenye masilahi kwa watu kwa namna moja au nyingine, basi linajuzu.”

Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.

Umbashirie Pepo mtiifu na umonye na moto muasi. Baada ya hapo anayetaka aamini na anayetaka na akufuru.

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ مَن يَضِلُّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿١١٧﴾

“Hakika Mola wako anawajua vyema wanaopotea njia yake na anawajua sana wanaoongoka,” Juz;8 (6:117).

JE, QUR’ANI ILISHUKA KIDOGO KIDOGO?

Na Qur’an tumeigawanya ili uwasomee watu kwa kituo.

Qur’an haikuteremka kwa Muhammad kwa mpigo; bali iliteremka kidogo kidogo, ikifiuatana na mara nyingine ikichelewa kulingana na masilahi na matukio ambayo huzuka mara kwa mara. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu:

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾

“Hakika tumeitermsha Qur’an katika laylatul-qadr (usiku wa heshima),” (97:1).

Maana yake ni kuwa ilianza kuteremshwa usiku huo, kisha ikaendelea hadi kufa Mtume(s.a.w.w) na kuanzia mwanzo hadi mwisho wa kushuka kwake ilikuwa ni miaka ishirini na tatu.

Mwenyezi Mungu amebainisha lengo la kufanya hivyo kwa kusema: ‘ili uwasomee watu kwa kituo;’ yaani kutoa muda ili iwe rahisi kuifahamu na kuihifadhi.

Aya hii ni dalili wazi ya kumkosoa anayesema kuwa Qur’an imeshuka kwa mara moja yote na mtume akaifikisha kidogo kidogo. Mwenyezi Mungu amemrudi mwenye kusema hivi kwa kauli yake: “Na wakasema wale waliokufuru: kwa nini hakuteremshiwa Qur’an kwa jumla moja?” (25: 32) Yaani moyo wako uweze kuwa na nguvu kuweza kufahamu maana ya Qur’an na siri zake.

Zaidi ya hayo kuna Aya kadhaa zinazosimulia visa na matukio yaliyojitokeza upya au kubainisha hukumu yake; kama vile kisa cha Badr, Uhud, Ahzab na Hunayn. Pia kisa cha Wakiristo wa Najrani na mayahudi wa Madina. Vile vile tukio la wake wa Mtume, mwanamke aliyemjadili Mtume kuhusu mumewe na mengineyo.

Amesema Sheikh Mufid: “Qur’an imeshuka kwa sababu na matukio kwa hali baada ya hali. Hilo linafahmika kutokana na dhahiri ya Qur’an, Hadith mutawatr na kongamano la maulama.”

Na tumeitermsha kidogo kidogo.

Jumla hii ni tafsiri na ubainifu wa yaliyo kabla yake.

Sema: iaminini au msiamini. Hakika wale waliopewa ilimu kabla yake, wanaposomewa, huanguka kifudifudi wanasujudu. Na wanasema: Ametakasika Mola wetu, Hakika ahadi ya Mola wetu lazima itimizwe. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidishia unyenyekevu.

Kabla yake, ni kabla ya Qur’an. Wanaoambiwa ni washirikina ambao walimwekea masharti Muhammad(s.a.w.w) ya kumwamini; kama ilivyoelezwa katika Aya ya 9 ya Sura hii. Kuanguka kifudifudi ni kusujudu kwa uso. Kumetajwa kusujudu mara mbili, kwa sababu kwa kwanza ni kwa ajili ya kumwadhimisha Mwenyezi Mungu na kwa pili ni kwa kuathrika na Qur’an katika nafsi zao.

Wale ambao wamepewa elimu kabla ya Qur’an ni wale waloiangalia haki katika watu wa Kitabu ambao walimwamini Muhammad(s.a.w.w) na wenye maumbile safi, kama wale tutakaowadokeza katika kifungu kinachofuatia.

WANYOOFU

Mnyoofu ni yule aliyeacha batili na kufuata haki na njia yenye kunyooka. Wakati wa Jahiliya kulikuwa na watu waliopetuka mazingira yao, na kwa mamubile yao safi waliweza kutambua kwamba kuna muumba mmoja mwenye uwezo wa ulimwengu huu na kwamba baada ya mauti kuna ufu- fuo, hisabu, adhabu na thawabu.

Vile vile kwamba kuabudu masanamu ni ujinga na upotevu. Kuna baadhi ya shairi zao katika kitabu Al-aghani Juzuu ya 3 na Sirat ibn Hisham, Juzuu ya 1. Chapa ya mwak 1936:

• Je, ni Mungu mmoja au elfu miungu?

• Ni dini iliyokioja iliyogawanyika mafungu

• Lakini namuabudi Mola wangu Rahamani

• Anisamehe zangu dhambi Mola ghafuri manani

• Tawaona watu wema makazi yao Peponi

• Na makafiri madhalima kwenye sairi Motoni

Ibn Hisham anasema katika Juzuu ya 1 ya As-siratun-nabawiyya: “Walikusanyika makuraishi katika Idd yao ya masanamu waliyokuwa wakiyaadhimisha, wakajitoa watu wane ambao ni: Waraqa bin Nawfal, Abdallah bin Jahsh, Uthman bin Alhuwayrith na Zayd bin Amr. Wakaambiana: Wallah hawa watu wenu hawana chochote, wameikosea dini ya baba yao Ibrahim! Nini haya mawe tunayozungukia, hayasikii, hayaoni, hayadhuru wala hayanufaishi!

Zayd hakuingia kwenye uyahudi wala unaswara (ukiristo), Aliacha dini ya watu wake kwa kujiepusha na masanamu, mfu, damu na dhabihu zilizokuwa zikitolewa kwa masanamu. Akakataza kuwaua watoto wa kike na akawa anamwambia baba yake: “Usimuue mimi nitamgharimia malezi yake.”

Alikuwa akijasiri kuwaambia watu wake na kuwakosoa huku akiwaambia: “Mimi ninamwabudu Mola wa Ibrahim. Ewe Mola wangu! Lau ningejua namna inayopendeza zaidi ya kukuabudu ningeliifanya; lakini siiju, Kisha anasujudi kwenye kiganja chake.

Zayd aliendela kuwasafihi maquraishi na ibada yao. Walipoona ni hatari walimtaka ami yake Khattwab, baba wa Umar bin, Alkhattab amzuie na amkataze, naye akamkataza. Lakini Zayd bado aliendelea na mwito wake. Al-Khattab akawa anawatuma vijana wahuni wa Kikuraishi, akiwemo mtoto wake Umar, kumzuia asiingie Makka, Zaidi akawa anapenye Kisiri.

Walipofahamu walimwambia al-Khattab na wakawa wanamfukuza na kumwudhi kwa sababu ya kuogopa kwao asije akawavutia watu kwenye dini yake, Baadaye Zaid akatoka kutafuta dini ya Ibrahim(a.s) . Akawa anahangaika huku na huko katika nchi mbalimbali. Hata hivyo alipokanyaga nchi ya Lakhm, alishambuliwa na kuuawa. Rafiki yake Waraqa alimlilia na kumtungia mashairi haya:

• Hakika bin Amri meongozwa kwa wema

• Mejiepusha na tanuri ya moto unaochoma

• Me mwabudu adhimu Mola aso mithili

• Ukaiacha mizimu ya matwaghuti jahili

• Rehema za Mola wake kiumbe humfikia

• Hata chini ajizike bonde sabini kungia

Zaidi aliuawa kabla ya kutumwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) , lakini mtoto wake alimwamini Mtume(s.a.w.w) Yeye pamoja Umar bin al-Khattab, ambaye alikuwa ni binamu yake, walimwendea Mtume na kumwuliza: Tunaweza kumuomba Mwenyezi Mungu amsamehe Zaid bin Amr?” Mtume alijibu: “Ndiyo. Yeye atafufuliwa kama mwakilishi pekee wa jamaa zake.”

Abdallah bin Jahsh, alibakia mpaka ukaja Uislamu, akasilimu na akahama yeye na mkewe, Ummu Habiba bint Abi Sufyan, kwenda Habasha (Ethiopia), akafia huko baada ya kurtadi kwa kuingia kwenye dini ya unaswara (ukiristo) Baadae Mtume akamuo Ummu Habiba.

Uthman bin Huwayrith, alikwenda kwa Kaizari mfalme wa Roma na akawa Mnaswara, huko alipewa cheo kikubwa na akafa Sham. Waraqa aliingia dini ya unaswara (ukristo) na akasoma vitabu vitakatifu vya dini hiyo mpaka akavifahamu barabara. Aliishi Makka, kama mtawa, akiwakataza watu wake kuabudu masanamu.

Warqa alikuwa ni binamu wa Khadija, mke wa Mtume(s.a.w.w) . Uliposhuka wahyi kwa mtume alikwenda naye kwa binamu yake huyo. Akamuuliza, ewe mwana wa ndugu yangu, unaona nini? Mtume alipomwambia akasema: “Huyo ndiye Malaika Mkuu amabye aliwashukia Musa, Natamani ningekuwa kijana, natamani niwe hai wakati watu wako watakapokutoa. Mtume akasema: Hivi watanitoa? Akasema ndio! Hakuna mtu yeyote kabisa aliyekuja na mfano wa jambo lako ila hufanyiwa uadui. Kama nikiwahi siku hiyo nitakusaidia sana!

Waraqa alitamka kwa wahyi wa umbile lake safi, “Ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu” Kila mtu atakayerejea kwenye umbile lake hili atamwamini Muhammd(s.a.w.w) na atamsaidia kwa sababu “Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu, Hiyo ndiyo dini iliyo sawasawa, Lakini watu wengi hawajui.” (30:30).

Sema, mwiteni Mwenyezi Mungu (Allah) au mwiteni Mwingi wa rehe- ma (Rahman), kwa jina lolote mtakalomwita, Yeye ana majina mazuri.

Washirikina walikuwa na masanamu mbalimbali, wakiyaita kwa majina ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalii yoyote.

Katika majina hayo hakukuwa na jina la Rahman. Kwa hiyo Mtume alipowalingania kumwabudu Rahman ndio wakasema, ni nani huyo Rahman? “Na wanapoambiwa msujudieni mwingi wa rehema (Rahman) wao husema: Ni nani huyo mwingi wa rehma? Je,tumsujudie unayetuamrisha wewe?” (25:60) Yaani ni wasifu gani huu ambao hauna athari yoyote kwa waungu wetu?

Kauli yake Mwenyezi Mungu: Sema, mwiteni Mwenyezi Mungu (Allah) au mwiteni Mwingi wa rehema (Rahman) ni jawabu tosha la upinzani wao.

Kwa sababu maana yake ni kwamba majina na matamshi ni nyenzo tu ya ibara. La kuzingatia ni yule anayeitwa. Mwiteni mtakavyo katika majina yake, yote ni mazuri; Kwa sababu yanaleta ibara ya maana nzuri nayo yako sawasawa katika uzuri.

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ﴿١٨٠﴾

“Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri,” Juz; 9 (7:180).

Kwenye Juzuu hiyo ya 9, tumefafanua zaidi katika kifungu cha ‘Je, majina ya Mwenyezi Mungu ni hayo hayo au yana kiasi.’

Wala usiisome jahara Swala yako wala usiifiche, bali tafuta njia baina ya hizo.

Makusudio ya jahara kwenye Swala ni kusoma kwa sauti kubwa na kuficha ni kusoma kwa sauti ndogo. Imam Jafar Asswadiq(a.s) anasema katika kufasiri Aya hii: “Jahara ni kuinua sauti na kuficha ni kiasi ambacho masikio yako hayasikii. Na soma kisomo kilicho baina yake”

Na sema: sifa njema zote ni za ambaye hakujifanyia mtoto wala hana mshirika katika ufalme, wala hana msaidizi kwa sababu ya udhaifu, na mtukuze kwa matukuzo makubwa.

Tunamuhimidi Mwenyezi Mungu kwa utukufu wa hisani yake na ukuu wa buruhani yake. Tunamuepusha na kuwa na mtoto kwa vile anajitosha na kila kitu, si muhitaji; na kwa kuwa mtoto anafanana na baba yake na kumrithi na Yeye hana wa kufanana naye wala wa kumrithi.

Tunamwepusha na mshirika kwa vile hiyo ni dalili ya kushindwa:

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرًا ﴿٤٤﴾

“Hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushindwa na chochote mbinguni wala ardhini; Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye uweza.” (35:44).

Kila mwenye nguvu mbele yake ni dhaifu na kila mwenye utukufu kwake ni dhalili; ndio maana inakuwa Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi na Mwenye shani kiasi wasichoweza kusifu wanaosifu na kutekeleza haki yake wenye kushukuru.

MWISHO WA SURA YA KUMI NA SABA

12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

Sura Ya Kumi Na Nane: Surat Al-Kahf

Imeshuka Makka isipokuwa Aya moja tu; kama ilivyoelezwa katika Majmaul-bayan. Ina Aya 111

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu

لْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَنزَلَ عَلَىٰ عَبْدِهِ الْكِتَابَ وَلَمْ يَجْعَل لَّهُ عِوَجًا ﴿١﴾

1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye amemteremshia mja wake Kitabu wala hakukifanya kombo.

قَيِّمًا لِّيُنذِرَ بَأْسًا شَدِيدًا مِّن لَّدُنْهُ وَيُبَشِّرَ الْمُؤْمِنِينَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ أَجْرًا حَسَنًا ﴿٢﴾

2. Kimenyooka ili kitoe onyo kutoka kwake na kiwabashirie waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri.

مَّاكِثِينَ فِيهِ أَبَدًا ﴿٣﴾

3. Wakae humo milele.

وَيُنذِرَ الَّذِينَ قَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا ﴿٤﴾

4. Na kiwaonye wale wanaosema Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto.

مَّا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ وَلَا لِآبَائِهِمْ كَبُرَتْ كَلِمَةً تَخْرُجُ مِنْ أَفْوَاهِهِمْ إِن يَقُولُونَ إِلَّا كَذِبًا ﴿٥﴾

5. Hawana ujuzi wa hili wala baba zao. Ni neno kuu litakalo vinywani mwao, hawasemi ila uongo tu.

فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ عَلَىٰ آثَارِهِمْ إِن لَّمْ يُؤْمِنُوا بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَسَفًا ﴿٦﴾

6. Huenda utajiangamiza nafsi yako kwa kusikitikia hali yao ikiwa hawataamini mazungumzo haya.

إِنَّا جَعَلْنَا مَا عَلَى الْأَرْضِ زِينَةً لَّهَا لِنَبْلُوَهُمْ أَيُّهُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ﴿٧﴾

7. Hakika tumevifanya vilivyo katika ardhi kuwa ni pambo lake ili tumjaribu ni nani kati yao mwenye vitendo vizuri zaidi.

وَإِنَّا لَجَاعِلُونَ مَا عَلَيْهَا صَعِيدًا جُرُزًا ﴿٨﴾

8. Hakika sisi tutavifanya vilivyo juu yake kuwa nchi iliyo kame.

AMEMTEREMSHIA KITABU MJA WAKE

Aya 1 – 8

MAANA

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye amemteremshia mja wake -Muhammad-Kitabu wala hakukifanya kombo, kimenyooka ili kitoe onyo kutoka kwake – Yeye Mungu -na kiwabashirie waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri; wakae humo milele.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameiitaja Qur’an katika Aya zake kadhaa kwa sifa za haki uongozi na nuru. Hapa ameiita kwa sifa za msimamo na kutokuwa kombo na kwamba inambashiria mwema kupata thawabu na neema ya milele na kuwaonya wafisadi kupata adhabu na moto wa milele.

Lengo la yote hayo ni kubainisha kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amiteremsha Qur’an ili twende na mwongozo wake, sio tuhifadhi Aya zake na matamko yake na kusoma tajwid nzuri na tafsiri tu; kama tulivyo.

Mtume(s.a.w.w) alisemana sisi ndio tulikuwa tunaambiwa - “Utakuja wakati kwa watu, dini haitabakia isipokuwa maandishi yake, wala Qur’an isipokuwa darasa yake” Ninaapa kuwa kila ninaposoma makemeo haya kutoka Mtume wa rehema, huwa manywele yananisismka.

Ni makemeo gani yanayotisha kuliko kua miongoni mwa waliokusudiwa na wasifu huu? Sisi hatuna imani isipokuwa jina, wala uislamu isipokuwa maandishi pia hatuna Qur’an isipokuwa kuisoma tu.

Walitia ila Qur’an walioitia na wakaipinga walioipinga tangu mwanzo. Sisi tukaimaini, lakini tunahalifu hukumu zake na mafundisho yake waziwazi. Tofauti yetu sisi na wanaoipinga ni kama ile tofauti baina ya anayesema: Mimi sioni hii kuwa ni haki, lau ningeliijua ni haki basi ningeliifuata na yule asemaye: Bila shaka mimi ninakubali kuwa hii ni haki, lakini sina ulazima nayo wala siiheshimu.

Na kiwaonye wale wanaosema Mwenyezi Mungu amejifanyia motto; Hawana ujuzi wa hili wala baba zao.

Maneno haya yanaungana na ya mwanzo: ‘ili kitoe onyo’ onyo la kwanza ni kwa kila mwenye kuasi na kustahiki adhabu na onyo la pili linahusu aliyemnasibisha Mungu kuwa ana mtoto. Ametakata Mwenyezi Mungu na hayo kabisa.

Mara nyingi maungano ya mahsusi kwenye ujumla yanafahamisha kuzidi huyo aliye mahasusi; Mfano kuunganisha Jibril na Malaika au kuanganisha waasi na wale wanaosema Mwenyezi Mungu ana mtoto. Kwa sababu kuse- ma kuwa Mwenyezi Mungu ana mtoto ni uasi zaidi.

Razi anasema kuwa waliosema Mungu ana mtoto ni makundi matatu: “Kundi la kwanza ni makafiri wa kiarabu waliosema kuwa Malaika ni mabinti wa Mungu. Kundi la pili ni manaswara (wakiristo) waliosema kuwa Masih ni mwana wa Mungu. Kundi la tatu ni mayahudi waliosema kuwa Uzayr ni mtoto wa Mungu.”

Makusudio ya kusema: ‘Hawana ujuzi wa hili’ ni wao hawategemei dalili yoyote ya hili; bali dalili iko kinyume. Ama kusema wala baba zao ni kusisitiza shutuma tu; kama kusema: Ni mshenzi mtoto wa mshenzi au ni maluuni mtoto wa maluuni.

Ni neno kuu litakalo vinywani mwao, hawasemi ila uongo tu.

Hakuna kitu kikubwa kuliko uongo, Uwongo mkubwa zaidi ni uongo juu ya Mwenyezi Mungu na kunasibisha uhalali na uharamu kwake bila ya dalili. Na mkubwa kuliko yote ni kumnasibishia mtoto.

Huenda utajiangamiza nafsi yako kwa kusikitikia hali yao ikiwa hawataamini mazungumzo haya.

Makusudio ya mazungumzo hapa ni Qur’an, kwa mafikiano ya wote. Kuisifu Qur’an kuwa ni mazungumzo ni dalili ya kuvunja kauli ya wale wasemao kuwa Qur’an ni ya tangu zama.

Hakuna mwenye shaka kuwa Mtume anamtakia heri kila mtu bila ya kubagua; kama vile wewe uanvyomtakia heri mtoto wako na mimi ninavyomtakia heri mtoto wangu. Mtume alikuwa akihuzunika na kusononeka sana pindi mtu anapofuata njia ya upotevu na maangamizi.

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anamkataza Mtume wake mtukufu kuwa asijitie simanzi, akajiangamiza bure kwa ajili ya wanaopinga uongofu na kufuata haki. Akamwambia usihuzunike:

إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ ﴿٢٥﴾ ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم ﴿٢٦﴾

“Hakika ni kwetu sisi marejeo yao na hakika ni juu yetu hisabu yao.” (88:25-26).

Hakika tumevifanya vilivyo katika ardhi kuwa ni pambo lake ili tum- jaribu ni nani kati yao mwenye vitendo vizuri zaidi.

Vipambo hapa vinakusanya cheo mali na watoto na kila lile wanalokufia watu na kuvurugana kwa ajili yake. Ghururi hizi ndizo zinazomtambulisha mwema na muovu.

Mwenye kukinai na fungu lake na akaishi kwa jasho lake basi huyo ni mwema aliye karimu.

Na mwenye kujaribu kufanya ulanguzi na kuishi kwa jasho la wengine; hata kama ni kwa kuanzisha vita na kuleta fitna, basi huyo ni muovu mwenye dhambi.

Maana ya majribio ya Mwenyezi Mungu kwa watu katika vipambo vya ardhi ni kuzidhihirisha sababu zake na vitendo vyao ambavyo vitastahiki thawabu au adhabu. Tumezungumzia hilo kwa ufafanuzi Juz. 7 (5:94) kifungu cha ‘Maana ya kujaribu kwa Mwenyezi Mungu’.

Hakika sisi tutavifanya vilivyo juu yake kuwa nchi iliyo kame.

Juu yake ni juu ya ardhi; Yaani kila kilicho juu ya ardhi kitatoweka ibaki tupu. Mwema ni yule atakyemtii Mwenyezi Mungu na muovu ni yule atakayetii hawaa yake.

أَمْ حَسِبْتَ أَنَّ أَصْحَابَ الْكَهْفِ وَالرَّقِيمِ كَانُوا مِنْ آيَاتِنَا عَجَبًا ﴿٩﴾

9. Kwani unadhani kwamba watu wa pango na maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?

إِذْ أَوَى الْفِتْيَةُ إِلَى الْكَهْفِ فَقَالُوا رَبَّنَا آتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً وَهَيِّئْ لَنَا مِنْ أَمْرِنَا رَشَدًا ﴿١٠﴾

10. Pale vijana walipokimbilia kwenye pango wakasema: Mola wetu! Tupe rehema itokayo kwako na tutengenezee uongofu katika jambo letu.

فَضَرَبْنَا عَلَىٰ آذَانِهِمْ فِي الْكَهْفِ سِنِينَ عَدَدًا ﴿١١﴾

11. Basi tukayaziba masikio yao pangoni kwa miaka kadhaa.

ثُمَّ بَعَثْنَاهُمْ لِنَعْلَمَ أَيُّ الْحِزْبَيْنِ أَحْصَىٰ لِمَا لَبِثُوا أَمَدًا ﴿١٢﴾

12. Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi kati ya makundi mawili lililohisabu sawa muda waliokaa.

WATU WA PANGO

Aya 9 – 12

UTANGULIZI

Tutafisiri Aya zinazofungamana na watu wa pango (As-habulkahf) kutokana na dhahiri ya zinavyofahamisha Aya au kutokana na dalili ya mazingira; kwa mfano kusema kiulize kijiji kwa maana ya waulize watu wa kijiji. Tutaachana na rejea au ngano nyenginezo. Kwani tumesema mara nyingi kwamba matukio ya historia na mfano wake hayathibiti ila kwa nukuu ya Qur’an au kwa Hadith iliyopokewa kwa njia nyingi (Mutawatir) Na kwamba Hadith iliyopokewa kwa njia moja (Ahad) si kitu, hata kama yakisihi mategemezi yake; isipokuwa katika hukumu ya sharia.

MAANA

Kwani unadhani kwamba watu wa pango na maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?

Makusudio ya maandishi hapa ni ubao ulioandikwa majina ya watu wa pango. La kushangaza ni kauli ya anayesema kuwa neno raqim, tuliolifasiri kwa maana ya maandishi, ni jina la mbwa wao; na hali inajulikana na ni maarufu kuwa jina la mbwa wao ni Qitmir.

Vyovyote iwavyo ni kuwa kisa cha watu wa pango kilielezwa katika vitabu vya kale na waliokisoma au kukisikia wakashangaa kuwa itakuwaje watu walale usingizi mrefu wa miaka kiasi hicho na wabaki bila ya chakula?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia kila anayeshangazwa na kisa hiki kuwa usistaajabu na hayo, kila ishara ya Mwenyezi Mungu ni ya ajabu. Yule aliyewafanya watu wa pango ndiye yuleyule aliyeufanya ulimwengu na vilivyomo. Kwa hiyo kwake kuwabakisha vijana usingizini kwa mda mrefu kisha kuwaamsha ni jambo rahisi sana, lakini watu wengi hawajui.

Pale vijana walipokimbilia kwenye pango wakasema: Mola wetu! Tupe rehema itokayo kwako na tutengenezee uongofu katika jambo letu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaishria katika Aya hii na nyingine mbili zinazofuatia kuhusu kisa cha watu wa pango kwa ujumla, kisha anaanza kufafanua. Katika Aya hii tuliyonayo anasema kuwa hapo zamani za kale kulikuwa na vijana walioacha kila kitu katika maisha haya na wakakimbilia pangoni; wakamtaka Mwenyezi Mungu awahurumie na awatengenezee mambo yao wakiwa pangoni.

Hakudokeza Mwenyezi Mungu, katika Aya, hii sababu iliyofanya vijana hao waache kila kitu na kujiingiza pangoni, huku wakimtaka Mwenyezi Mungu awaangalilie mambo yao. Tunavyofahamu, kutokana na tafsiri ya mazingira na inavyoashiria Aya inayofuatia, ni kuwa vijana waliongozwa na maumbile yao salama kuwa watu wao wako katika upotevu wa kuabudu masanamu na kwamba wao walikataa kuabudu yale wanayoaabudu wazazi wao.

Kwa hiyo kama kawaida ya wenye siasa kali walitaka kwaua vijana au kuwafitini na dini yao. Vijana walipokosa njia zote waliamua kukimbilia pangoni na kumwambia Mwenyezi Mungu kuwa tumeudhiwa kiasi hiki unachoona nasi tunahitaji sana msaada wako na huruma zako. tunaomba msaada kwako wewe tu, si kwa mwengine.

Basi tukayaziba masikio yao pangoni kwa miaka kadhaa.

Yaani tuliwalaza usingizi ambao hawawezi kusikia chochote kwa muda wa miaka kadhaa, Itaelezwa idadi ya miaka hiyo kwenye Aya ya 25.

Kisha tukawazindua yaani tuliwaamshaili tujue ni lipi kati ya makundi mawili lililohisabu sawa muda waliokaa.

Watu walijua kisa cha watu wa pango wakiwa bado kwenye usingizi wao. Habari zikaenea na watu wakatofautiana katika muda wa kukaa kwao. Kuna waliosema muda mchache na waliosema mwingi. Mwenyezi Mungu akawainua watu wa pango. Ili makundi mawili yajue muda waliokaa waweze kuamini awazidishie imani yao kuhusu uweza wa Mwenyezi Mungu wa kuwafufua wafu. Kusema kwake Mwenyezi Mungu “ili tujue’ maana yake ni ili idhihiri elimu yetu kwa watu kiasi cha muda waliokaaa. Umepita mfano wake katika Juz 4. (3:140).

Unaweza kuuliza : Watu walijuaje muda wao na hali wenyewe walipoamka hata hawakuujua; bali walianza kuulizana, wengine wakasema tumekaa siku moja tu au nusu siku?

Jibu : Watu walijua muda wao kutokana na pesa walizokuwa nazo. Mmoja wao alikwenda mjini kununua chakula na watu wa mji walipoona ile pesa walijua ilikuwa ni wakati wa mmoja wa wafalme waliopita. Utakuja ufafanuzi wake kwenye Aya 19.

نَّحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ نَبَأَهُم بِالْحَقِّ إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى ﴿١٣﴾

13. Sisi tunakusimulia habari zao kwa haki. Hakika hao ni vijana waliomwamini Mola wao na akawazidisha uongofu.

وَرَبَطْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ إِذْ قَامُوا فَقَالُوا رَبُّنَا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَن نَّدْعُوَ مِن دُونِهِ إِلَـٰهًا لَّقَدْ قُلْنَا إِذًا شَطَطًا ﴿١٤﴾

14. Na tukazitia nguvu nyoyo zao, waliposimama, wakasema: Mola wetu ni Mola wa mbingu na ardhi, Hatutamuomba Mungu mwingine badala yake, Hakika tutakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.

هَـٰؤُلَاءِ قَوْمُنَا اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً لَّوْلَا يَأْتُونَ عَلَيْهِم بِسُلْطَانٍ بَيِّنٍ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ﴿١٥﴾

15. Hawa watu wetu wamefanya waungu badala yake; Kwa nini hawawaletei dalili bayana? Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo?

وَإِذِ اعْتَزَلْتُمُوهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ إِلَّا اللَّـهَ فَأْوُوا إِلَى الْكَهْفِ يَنشُرْ لَكُمْ رَبُّكُم مِّن رَّحْمَتِهِ وَيُهَيِّئْ لَكُم مِّنْ أَمْرِكُم مِّرْفَقًا ﴿١٦﴾

16. Na mkijitenga nao na vile wanavyoviabudu badala ya Mwenyezi mungu, basi kimbilieni pangoni, atawafungulia Mola wenu rehema yake na atawafanyia wepesi mambo yenu.

وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ ذَٰلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ مَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِ وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا ﴿١٧﴾

17. Na unaliona jua linapochomoza linaelemea kuumeni mwao mbali na pango lao; na lipokuchwa linawahepa kushotoni na wao wamo katika uwazi wake. Hayo ni katika ishara zake. Ambaye Mwenyezi Mungu anamuongoza basi yeye ndiye aliyeongoka, na anayempoteza hutampatia mlinzi (wala) mwongozi.

وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًا وَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا ﴿١٨﴾

18. Utawadhania wako macho na hali wamelala, na tunawageuza kuume na kushoto na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini lau ungeliwatokea bila shaka ungeligeuka kuwakimbia na ungelijazwa hofu.

HABARI ZAO ZA KWELI

Aya 13-18

MAANA

Sisi tunakusimulia habari zao kwa haki.

Kabla ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , watu walikuwa wakielezana habari za kisa cha watu wa pango. Kikaandikwa kwenye vitabu na pia kwenye mashairi. Miongoni mwa kaswida ya Umayya bin Abu Swalat:

Hakuna isipokuwa raqimu aliye jirani watu na mbwa wao wamelala pangoni.

Mtume alikuwa akiwataka watu wamsomee shairi la Bin Abu swalat, Basi husikilza kisha anasema, huyu mtu aliamini kwa ulimi wake na akakufuru kwa moyo wake.

Watu walitunga vigano kuhusu watu wa pango; kama walivyotunga kwa watu wengine waliopita. Ndio maana Mwenyezi Mungu akamwabia Mtume wake: ‘Sisi tunakusimulia habari zao kwa haki’ amabazo hazina shaka. Na ni nani aliye mkweli zaidi wa mazungumzo kumshinda Mwenyezi Mungu?

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuelezea kisa chao kwa ujumla katika Aya iliyotangulia, sasa anaanza kukichambua katika Aya zinazofuatia.

Kisa hiki kinagawanyika mafungu mane: Kwanza, kuelekea watu wa pango kwa Mwenyezi Mungu. Pili, hali yao na ya watu wao pamoja na kukimbia kwao, Tatu, kuamka kwao kutoka kwenye usingizi wao mazito. Nne, kufa kwao na kujengewa. Aya tuliyo nayo imechukua sehemu ya kwanza na ya pili na Aya zinazofuatia zimechukua sehemu mbili za mwisho.

SEHEMU YA KWANZA

Hakika hao ni vijana waliomwamini Mola wao na akawazidisha uon- gofu na tukazitia nguvu nyoyo zao.

Katika vijana wako wale ambao wamekomaa kiakili na kifikra; sawa na walivyokomaa kimwili. Aina hii ya vijana, ingawaje ni nadra kupatikana, lakini wapo, miongoni mwao ni watu wa pango. Walikuwa wakiishi katika jamii iliyojaa ufisadi na kuabudu masanamu, lakini wao walikataa na wakajiongoza kwa muwongozo wa usafi wa maumbile yao, Wakajiuliza, vipi mawe yanaweza kuwa miungu? Vipi wapenda anasa wanahodhi utajiri na nguvu na kuzitumia kwa wanyonge?

Shaka hii na maswali haya yaliwapeleka vijana hao kwenye itikadi ya tawhid na ufufuo. Mwenyezi Mungu alipoona ukweli wao wa nia na ikhlasi yao, aliwapa uthabiti katika imani yao na busara katika mambo yao.

Waliposimama.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubainisha walisimama wapi; Kwa hiyo wafasiri wametofautiana, Kuna waliosema kuwa walisimama mbele ya mfalme wao Decianus aliyejifanya jabari, Wengine wamesema kuwa walisimama kutoka usingizini.

Sio mbali kuwa makusudio ya kusimama kwao ni kutoka kwao kwenye ada ya watu wao na kuasi ushirikina na ufisadi. Hii ndio nembo ya mapinduzi yao.

Wakasema: Mola wetu ni Mola wa mbingu na ardhi, Hatutamuomba Mungu mwingine badala yake, Hakika tutakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka. Hawa watu wetu wamefanya waungu badala yake, Kwa nini hawawaletei dalili bayana? Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo?

Vijana waliamini Mungu mmoja aliye peke yake, Wakatangaza imani yao kwa watu na wakasema kuwa mataghuti katika watu wao wanamzulia Mwenyezi Mungu uongo na akili zao pia; kwa sababu wameyapa masanamu sifa ya Mungu huku wakijua kuwa hayadhuru wala kunufaisha. Wanawazuga wapumbavu kwamba hayo masanamu ndiyo yaliyowachgua wao na kuwapa nguvu juu ya watu. Na kwamba atakayewakhalifu malipo yake ni kuadhibiwa na kuuawa.

Ni kwa madai haya ndio mataghuti walitaka kuwauwa vijana hao, si kwa lolote ila ni kwa kuwa wao wamemwamini Mwenyezi Mungu na kuayakana masanamu kwa kuwaweka juu mataghuti na kuwakandamiza wanyonge.

Nilizinduka wakati nikiandika maneno haya, kwenye tafsiri ya mfano hai wa kushangaza uliojitokeza katika miji yetu. Nao ni hili jeshi kubwa la masheikh wenye vilemba ambao hawana usheikh hata chembe. Nimegundua kuwa kuna mkono mchafu unaofanya kazi kwa siri. Wanatenga mali za kuwalipa vibaraka na za kuwaingiza kwenye safu ya maulama na kuwavisha vilemba. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kulinda masilahi ya mataghuti na wanyonyaji kwa jina la dini; sawa na walivyoyapa masananamu sifa ya Mungu ili wawambie watu mazuzu kuwa hayo masanamu ndiyo yaliyowateua wao kuwa viongozi wao na yakawapa wao mali na kuwanyima wanyonge.

SEHEMU YA PILI

Na mkijitenga nao na vile wanavyoviabudu badala ya Mwenyezi mungu, basi kimbilieni pangoni, atawafungulia Mola wenu rehema yake na atawafanyia wepesi mambo yenu.

Mataghuti waliwabana vijana waumini na wakajaribu kuwatia mtihani na dini yao. Wakaambiana kuwa hatutapona na watu madhalimu isipokuwa tuwakimbie wao na yale wanayoyaabudu na kuyafanya.

Baada ya kubadilishana mawazo na kushauriana waliafikiana wakimbilie Pangoni, Kwani walikuwa hawana pengine zaidi ya hapo. Wakaingia Pangoni na wakamwachia Mungu jambo lao; hata kama watakufa kwa njaa na kiu.

Hivi ndivyo anavyokuwa mumin wa kweli, anabakia na imani yake akiitekeleza kwa hamasa na uthabiti bila ya kujali tatizo litakalomtokea. Mtu akifikia hali hii, basi Mwenyezi Mungu anakuwa pamoja naye popote alipo na atampa faraja haraka sana; hata kama wa mbinguni na ardhini watamkalia vibaya; kama ilivyokuwa kwa watu wa pango, pale Mungu alipowachagulia raha na amani na kuwa huru na dhiki ya maisha, Akawapa usingizi usioweza kuamshwa wala kuhofia chochote.

Na unaliona jua linapochomoza linaelemea kuumeni mwao mbali na pango lao; na lipokuchwa linawahepa kushotoni na wao wamo katika uwazi wake.

Yaani uwazi wa hilo Pango. Lilikuwa ni kubwa lenye uwazi wa kupitisha hewa safi na mwanga wa jua. Miili yao haiweza kufikiwa na jua si wakati wa mawiyo wala machweo. Kwa sababu walikuwa kwenye sehemu ambayo haifikiwi na mwanga wa jua au kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa akiliepusha kwa kudura yake.

Hayo ni katika ishara zake.

Hayo ni pamoja na kutofikiwa na jua, kana kwamba ilikusudiwa kuwa hivyo. Pia kuwekwa katika hali ambayo si kuwa macho, kiasi ambacho wakati ulipita bila ya kujua; wala si mauti kwa kuwa na harakati na pumzi. Hakuna tafsiri ya haya isipokuwa uweza wa Mwenyezi Mungu na hekima yake.

Ambaye Mwenyezi Mungu anamuongoza basi yeye ndiye aliyeongoka na anayempoteza hutampatia mlinzi (wala) mwongozi.

Makusudio ya ambaye Mwenyezi Mungu anamuongoza ni watu wa pango na anayempoteza ni wale waliokusudia kuwatesa. Angalia Juz. 9 (7: 178).

Utawadhania wako macho na hali wamelala na tunawageuza kuume na kushoto na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini.

Macho yao yalikuwa wazi kama vile yanaangalia mbele na damu inatembea mishipani, wanageuka upande huu na huo. Mbwa wao akiwa pembeni au mlangoni mwa pango kama mlinzi.

Lau ungeliwatokea bila shaka ungeligeuka kuwakimbia na ungelijazwa hofu.

Kwa sababu wako katika hali ya kushangaza isiyokuwa na mfano.