TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 14896
Pakua: 2111


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 19 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14896 / Pakua: 2111
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO Juzuu 15

Mwandishi:
Swahili

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَكَذَٰلِكَ بَعَثْنَاهُمْ لِيَتَسَاءَلُوا بَيْنَهُمْ قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ كَمْ لَبِثْتُمْ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَـٰذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَىٰ طَعَامًا فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ وَلْيَتَلَطَّفْ وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ أَحَدًا ﴿١٩﴾

19. Na kama hivyo tuliwainua ili waulizane. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu anajua zaidi muda mliokaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi pesa zenu aende mjini akaangalie chakula kipi kilicho kisafi zaidi awaletee riziki katika hicho, na awe mwangalifu, wala asiwajulishe kwa yeyote.

إِنَّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا ﴿٢٠﴾

20. Kwani wao wakiwajua watawapiga mawe au watawarudisha katika mila yao na hamtafaulu kabisa.

وَكَذَٰلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا ﴿٢١﴾

21. Na kama hivyo tuliwajulisha kwa watu wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli na kwamba saa haina shaka. Walipogombania jambo lao wao kwa wao, walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao anawajua zaidi, Wakasema wale walioshinda katika shauri lao. Hakika tutawajengea msikiti juu yao.

سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيلٌ فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاءً ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا ﴿٢٢﴾

22. Watasema ni watatu na wanne wao ni mbwa wao. Na wanasema ni watano na wa sita wao ni mbwa wao, kwa kuvurumisha ya ghaibu. Na wanasema ni saba na wa nane wao ni mbwa wao. Sema Mola wangu ndiye anayejua zaidi idadi yao, Hawawajui isipokuwa wachache. Basi usibishane juu yao ispokuwa mabishano ya juu juu; wala usiulize habari zao kwa yeyote yule.

NA KAMA HIVYO TULIWAINUA

Aya 19 – 22

SEHEMU YA TATU

Tumeishiria, katika maelezo yaliyotangulia, kuwa Aya zinazofungamana na watu wa pango zinagawanyika kwenye sehemu nne. Timekwishataja mbili na sasa tunaendelea na sehemu mbili za mwisho. Katika sehemu ya tatu ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na kama hivyo tuliwainua ili waulizane.

Waliendelea na usingizi wao kwa muda wa miaka 309; kama itakvyoelezwa kwenye Aya ya 25. Kisha akawaamsha kutoka kwenye usingizi mrefu wa ajabu. Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu aliwaamsha ili waulizane muda wa usingizi wao, na watakapofahamu hakika, imani yao kwa Mwenyezi Mungu na ufufuo itazidi.

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, katika Aya ya 16, kuwa lengo la kuwaamsha ni kuwa wajue muda wao wale waliozozana kabla ya kuamka. Na katika Aya hii anasema kuwa aliwaamsha ili waulizane wao wenyewe. Je kuna wajihi gani wa Aya hizi mbili?

Jibu : hakuna kugongana baina ya Aya mbili. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaamsha watu wa pango kwa mambo mawili: moja ameliashiria katika Aya iliyotangulia na jingine akaliashiria katika Aya hii. Kwa hiyo, maana ya Aya zote mbili ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwaamsha ili wajue wao na wengine kuwa Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kufufua wafu hata muda ukirefuka.

Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu ana- jua zaidi muda mliokaa.

Walipoamka walianza kuulizana, je mnajua mmekaa muda gani? Baadhi yao wakajibu kuwa tumekaa siku moja au baadhi ya siku. Kauli hii ni kuashiria kuwa hakuna kilichobadilika katika vitu vyao; si nguo wala nywele au kucha, nyuso, mili na hata rangi yao; ingawaje walikaaa muda mrefu. Lau kingebadilika kitu katika hivyo basi kingeonekana na wala asingesema msemaji miongoni mwao kuwa tumekaa siku moja au sehemu ya siku; kama asemavyo Razi.

Kisha wakasema tuachane na maswali haya, hakuna ajuae muda tuliokaa ila Mwenyezi Mungu.

Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi pesa zenu aende mjini akaangalie chakula kipi kilicho kisafi zaidi awaletee riziki katika hicho. na awe mwangalifu, wala asiwajulishe kwa yeyote. kwani wao wakiwajua watawapiga mawe au watawarudisha katika mila yao na hamtafaulu kabisa.

Pesa ilikuwa na sura ya mfalme wa wakati wao. inasemekana kuwa jina lake lilikuwa ni Dacianus na jina la mji lilikuwa ni Daqsus.

Waliamka na wakahisi njaa baada ya kukaa muda mrefu. Hivyo wakamtuma mmoja wao awanunulie chakula na wakamuusia awe na hadhari ili asitambuliwe na yeyote wasije wakauawa na mataghuti au wawafitini na dini yao. Hawajui kama wao wako kwenye zama nyingine

SEHEMU YA NNE

Na kama hivyo tuliwajulisha kwa watu wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli na kwamba saa haina shaka. Walipogombania jambo lao wao kwa wao, walisema: Jengeni jengo juu yao, Mola wao anawajua zaidi. Wakasema wale walioshinda katika shauri lao. Hakika tutawajengea msikiti juu yao.

‘Kama hivyo’ ni ishara ya kwamba kama tulivyozidisha uongofu na kutia nguvu kwenye nyoyo zao, tukawalaza kisha kuwaamsha, basi vile vile tuliwadhihirisha kwa watu au watu wa mji uliokuwa karibu na pango.

Waliogombania ni watu wa mji uliokuwa karibu na pango. Walihitalifiana watu wa mji huo kuwa je, watu wa pango wamelala au wamekufa? Hiyo ni baada ya kuona pesa ya zamani aliyokuwa nayo yule aliyetaka kununua chakula. Wakaenda pangoni na wakaona miili imelala chini haitingishiki wala kuzungumza.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wale walioshinda’ inaonyesha kuwa watu wa mji waligawanyika, kuhusiana na watu wa pango. Kuna waliosema tuwaache kama walivyo, waliosema tulizibe pango na wale waliosema tuwajengee msikiti utakoswaliwa na watu; na hili ndilo lililoshinda.

Baada ya kubainisha makusudio ya matamko ya Aya tuanze ufafanuzi:

Ni kawaida ya Qur’an kuacha kutaja kila maneno ambayo yataweza kufahamika kutokana na mfumo wa maneno ulivyo au mambo ambayo yanalazimiana na hali ya tukio. Kwa misingi hii ndio kukawa kuna jumla nyingi hazipo kwa vile zinajulikana kutokana na mazingira yalivyo. Muhtasari wa jumla zisizokuwepo:

Mmoja wao alikwenda mjini kununua chakula na alikuwa na hadhari, kama alivyousiwa na wenzake. Lakini yeye akatokewa na jambo ambalo hakulifikiria; pale alipotoa pesa kwa muuza chakula na akasema hii ni hela ya zamani haitumiki hivi sasa ni ya mfalme Dacianus; kama ilivyosemekana. Yule mwenye hela akasema: itakuwaje jana na leo tu.

Habari zikaanza kuenea mjini, Walipomuuliza kuhusu habari yake na ya pesa aliyokuwa nayo, aliwaambia kuwa yeye na wenzake walikimbia na dini yao kutoka kwa mataghuti na wakaeleka kwenye pango. Mmoja wa waliokuwa pale akasema ndio nimesikia kuwa zamani kuna watu walikimbia na dini yao kwa kumhofia mfalme Dacianus aliyechorwa kwenye pesa hii na wakakimbilia pangoni, Inawezekana ndio hawa. Watu wakamiminika pangoni baada ya yule mwenye pesa kuwahi pangoni na kuwaeleza wenzake.

Hatimaye baada ya kugunduliwa, walinyenyekea kwa Mwenyezi Mungu; kama walivyonyenyekea mwanzo, walipoingia pangoni. Wakamtaka Mwenyezi Mungu awape rehema yake na awachagulie lile ambalo linamridhisha Yeye Mwenyezi Mungu. kabla hawajamaliza dua yao walianguka wote na roho zao takatifu zikahamia kwenye rehema ya Mola wao kwenye neema ya milele, Watu wakawajengea msikiti.

Ushahidi katika kisa hiki ni dalili yake ya hisia kwa yale aliyoyadokeza Mwenyezi Mungu (s.w.t) “watu wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli na kwamba saa haina shaka” na kwamba binadamu ni wa milele akitoka kwenye nyumba hii na kuhamia nyumba nyingine. Ole wake tena ole wake yule anayeicha nyumba isiyoisha kwa nyumba inayoisha.

Watasema ni watatu na wanne wao ni mbwa wao. Na wanasema ni watano na wa sita wao ni mbwa wao, kwa kuvurumisha ya ghaibu. Na wanasema ni saba na wa nane wao ni mbwa wao.

Watu wametofautiana mahali palipokuwa na pango. Ikasemekana lilikuwa Palestina karibu na Baytul-muaqaddas, Ikasemekana lilikuwa Musel. Pia imesemekana lilikuwa Hispania upande wa Granada na kauli nyingi nyenginezo.

Vile vile wametofautiana kuhusu wakati wa tukio, Kuwa je lilikuwa kabla ya Bwana Masih au baada yake? Pia wametofautiana kuhusu chakula alichoambiwa anunue, kuwa je kilikuwa tende, zabibu au nyama? Bali hata wametofautiana katika rangi ya mbwa kuwa je alikuwa rangi ya kahawia au wa madoadoa, Na tofauti nyingi nyenginezo. Kwa hiyo si ajabu kutokea tofauti katika idadi ya watu wa pango.

Katika Tafsir ya Razi na Tabrasi imeelezwa kuwa ulipokuja ujumbe wa wakristo wa Najrani kwa Mtume(s.a.w.w) yalipita mazungumzo kuhusu watu wa pango. Akasema mmoja katika wakiristo, anayeitwa Ya’qubiya: “Walikuwa watatu na wa nne wao ni mbwa wao.” Akasema Nasturiya: “Walikuwa ni watano na wa sita wao ni mbwa wao.” Wakasema waislamu: “Walikuwa ni saba na wa nane wao ni mbwa.”

Kisha Razi akaendelea kusema: Wafasiri wengi wamesema kuwa wao walikuwa saba na wa nane wao ni mbwa. Akataja njia nne za kusihi kauli hii. Tatu katika hizo ni za kuangaliwa na ya nne ina mwelekeo. Kwa ufupi kauli hiyo inasema kuwa kauli ya tatu na ya tano, Mwenyezi Mungu amesema huko ni kuvurumisha yasiyojulikana, lakini alipotaja ya saba akanyamaza, kwa hiyo inawajibisha kuwa ndiyo ya sawa.

Sema: Mola wangu ndiye anayejua zaidi idadi yao, Hawawajui isipokuwa wachache.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuishiria tofauti za watu kuhusu idadi ya watu wa pango na kwamba kauli zote au baadhi yake ni kusema tu bila ya uhakika, sasa anamwambia Mtume wake mtukufu:

Tofauti zote hizi hazina umuhimu; na kwamba ni juu ya kila mtu kumwachia Mungu, kuzingatia yale yaliyowapitia watu wa pango na kuyachukulia kuwa ni dalili ya ufufuo; sio kujadili idadi, mahali au wakati. Kwa sababu lengo la kisa hiki ni mazingatio na mawaidha; bali hili ndilo lengo la visa vyote vya Qur’an; ndilo la kwanza na la mwisho:

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١١١﴾

“Kwa hakika katika simulizi zao mna mazingatio kwa wenye akili,” Juz;13 (12:111).

Basi usibishane juu yao ispokuwa mabishano ya juu juu; wala usiulize habari zao kwa yeyote yule.

Juu yao ni kuhusu hao watu wa pango. Yaani ewe Muhammad! Usiwe na haja kabisa ya kujadiliana na yeyote katika watu wa Kitab kuhusu idadi ya watu wa pango wala usimuulize ulama katika wao, kwani suala hilo sio lenyewe hasa; bali yule mwenye kubishana mwambie kwa upole tu; mfano Mungu ndiye ajuaye au mjadala huu hauna faida n.k.

وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾

23. Wala kamwe usiseme kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho;

إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَىٰ أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لِأَقْرَبَ مِنْ هَـٰذَا رَشَدًا ﴿٢٤﴾

24. Isipokuwa akipenda Mwenyezi Mungu. Na mkumbuke Mola wako pale unaposahahu, na sema: Asaa Mola wangu akaniongoza kwenye uongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.

وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا ﴿٢٥﴾

25. Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu na wakazidisha tisa.

قُلِ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ مَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾

26. Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda waliokaa. Ni zake siri za mbingu na za ardhi. Kuona kulikoje kwake na kusikia, Hawana mlinzi isipokuwa Yeye; wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.

INSHAALLAH

Aya 23-26

MAANA

Wala kamwe usiseme kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifaya hilo kesho; isipokuwa akipenda Mwenyezi Mungu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwambia usibishane, alimwamrisha afungamanishe kila jambo lake na matakwa ya Mungu.

Mtu anaweza kupitiwa akafanya lile aliloliazimia kuliacha au akaacha lile aliloliazimia kulifanya; Hili linaweza kumtokea hata maasumu, maadamu sio la kumwasi Mungu; kwa sababu isma haiwezi kuwa pamoja na maasi kwa hali yoyote ile; sawa na ambavyo elimu haiwezi kuwa pamoja na ujinga.

UTASHI MKUU

Mazingira yana athari, hilo halina shaka, lakini sio kila kitu kwa binadamu, Ni mtu gani ambaye kila analolitaka analipata? Hata awe na uwezo au cheo kiasi gani! Ni nani ambaye ameweza kumfanya mkewe au mwanawe vile anavyotaka awe kiumbo na kitabia? Ongezea mifano mingine kadiri unavyotaka, Hakuna yeyote ambaye amenyookewa na kila analolitaka; hata katika mazungumzo na usingizi.

Kwa hiyo utashi wa mtu upo na una athari yake, lakini utashi huu unahukumiwa na utashi wa Mwenyezi Mungu ambaye anasema: ukitaka jambo litafute kwa sababu zake na njia zake za kimaumbile ambazo nimeziweka, lakini angalia usinisahau; Kwani wewe unatembea kwenye njia yangu. Mimi ndiye niliyekuumba, nikakutengenezea njia na nikakupa mwongozo wa njia hiyo, tena nikakuamrisha uifuate.

Vile vile usisahau kuwa njia niliyokutengeneza haiwezi kukufikisha, kwa hali yoyote ile, kwenye matakwa yako; hata ukijitahidi kiasi gani. Kwa sababu mimi vile vile nimetengeneza vikwazo kwenye njia hiyo; Si wewe wala mwingine mwenye uwezo navyo; Kwa sababu viko mikononi mwangu. Ni mimi ndiye ninayevizuia na ni mimi ndiye ninayeviachia. Usikate kabisa kuwa wewe utafika kila unapotaka; isipokuwa kwa matakwa ya juu. Tazama kifungu cha ‘Siri na matukio ya ghafla’ katika Juz.2 (2:210).

Na mkumbuke Mola wako pale unaposahahu.

Kila mtu hutokewa na kusahau; hasa akiwa ametingwa na shughuli na huzuni. Hata imesemekana neno la kiarabu insan lililo na maana ya mtu, linatokana na neno nasiya lenye maana ya mwenye kusahau.

Mwenyezi Mungu ametuamrisha tumkumbuke tunaposahau na akatu- fundisha namna ya kukumbuka pale aliposema:na sema: Asaa Mola wangu akaniongoza kwenye uongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.

Yaani kama Mwenyezi Mungu hatanikumbusha yale niliyoyasahau. Basi yeye atanikumbusha yaliyo na masilahi na manufaa zaidi kuliko haya. Na kusahau baadhi ya mambo kuna faida zake nyingi.

Kwa mnasaba wa Aya hii tutaje kisa ambacho ni nadra kutokea cha kuhusudiana watu wa elimu ya dini; kama wanavyohusudiana wafanyakazi na wafanyabiashara:

Imepokewa riwaya kwamba Mansur alikuwa akimfadhilisha sana Abu Hanifa kuliko wanafiqh wengine. Muhammad bin Is-haq akamuonea wivu. Siku moja wakakutana wote mbele ya Mansur, Muhamad akamuuliza Abu Hanifa akikusudia kumshinda na kumnyamazisha, kama ifuatavyo:-

Muhammad: Unasemaje kuhusu mtu aliyeapa akanyamaza kwa muda, kisha akasema inshaallah.

Abu Hanifa: Kiapo chake kitafaa na atalazimiana nacho, kwa sababu kauli yake ya inshaallah imetengana na kiapo, lau haikutengana basi kiapo hak itafaa.

Muhammad: Vipi na babu wa Amir Al-muminin – akimkusudia Mansur – hasemi hivyo?

Mansur akamgeukia Abu Hanifa: Eti ni kweli babu alisema hivi?

Abu Hanifa: Ndio

Mansur: Sasa unampinga babu yangu ewe Abu hanifa?

Abu Hanifa: Kauli ya babu yako ni sahihi lakina kuna taawili, inayoitoa kwenye ushahihi. Huyu Muhammad na wenzake hawakuoni kuwa wewe unastahiki ukhalifa; Kwa sababu wao wanakubai, kisha wakitoka wanasema inshaallah. Maana yake ni kuwa katika madhehebu yao wao hawakukubali kuwa wewe ni khalifa kwa kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu hakutaka wewe uwe khalifa.

Basi Mansur akakasirika sana akawaambia maaskari wake mchukueni huyu, akimwashiria Muhammad bin Is-haq. Basi ule mtandio wake wakauweka shingoni mwake wakamburura hadi korokoni.

Kwa mnasaba huu tunadokeza kuwa mtu akisema: nimekuuzia kitu, inshaallah au mke wangu nimemtaliki inshaallah au pia kusema: wallahi sitafanya hivi inshaalllah n.k. Basi akisema hivyo ataangaliwa: ikiwa alikusudia kutabaruku na jina tu la Mwenyezi Mungu, basi atalazimiana na aliyoyasema, Itakuwa bei yake, talaka au kiapo chake kimefungika. Ama ikiwa amekusudia kuwa hilo ni sharti basi hatalazimika na kitu kwa sababu hilo sharti litakuwa limevunja alichokisema.

Unaweza kuuliza : Je, tutajuaje alichokikusudia?

Jibu : hilo litategema msemaje yeye mwenye. Kwa sababu makusudio hayakujulikana isipokuwa kwa yule aliyekusudiwa; na kadhi atachukua kauli yake.

Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu na wakazidisha tisa.

Baada ya kutoka nje kidogo Mwenyezi Mungu amerudia kisa cha watu wa pango na kubainisha kuwa wao walibaki kwenye usingizi kwa muda wa miaka 309.

Unaweza kuuliza : Kwa nini akasema na wakazidisha tisa badala ya kusema moja kwa moja, mia tatu na tisa?

Jibu : Baadhi ya wafasiri wamejibu kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema miaka 300 kwa hisabu ya miaka ya jua na 309 kwa miaka ya mwezi. Kwa sababu tofauti kati yake ni miaka mitatu kwa kila mia.

Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda waliokaa. Ni zake siri za mbingu na za ardhi.

Ndio anajua; Kwa sababu Yeye ndiye aliyewaumba, akawaongoza, akawalaza na akawaua, Na ametoa habari kuwa walikaa miaka 309. Kauli yake ni haki.

Kuona kulikoje kwake na kusikia.

Yaani anaona sana kila linaloonwa na anasikia sana kila linalosikiwa. Makusudio ni kuwa hakifichiki kwake kitu chochote.

Hawana mlinzi isipokuwa Yeye; wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.

Viumbe hawana mlinzi yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Maana ni kuwa hakuna wa kumsaidia aliyedhalilishwa na Mungu na hakuna wa kumdhalilisha aliyesaidiwa na Mungu na wala hakuna wa kuzuia alichokitoa na kutoa alichokizuia; Kwa sababu Yeye yuko peke yake hana mshirika. Ufalme uko mikononi mwake na Yeye ni muweza wa kila kitu.

14

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TANO

وَاتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِن كِتَابِ رَبِّكَ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ وَلَن تَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٧﴾

27. Na soma uliyopewa wahyi katika kitabu cha Mola wako, Hapana wa kubadilisha maneno yake, Wala hutapata makimbilio isipokuwa kwake.

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا ﴿٢٨﴾

28. Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanaomuomba Mola wao asubuhi na jioni, wakitaka radhi yake; wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya maisha ya dunia; wala usimtii tuliyemghafishilisha moyo wake asitukumbuke na akafuata matamanio yake na mambo yake yakawa yamepita kiasi.

وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمْ سُرَادِقُهَا وَإِن يَسْتَغِيثُوا يُغَاثُوا بِمَاءٍ كَالْمُهْلِ يَشْوِي الْوُجُوهَ بِئْسَ الشَّرَابُ وَسَاءَتْ مُرْتَفَقًا ﴿٢٩﴾

29. Sema hii ni kweli itokayo kwa Mola wenu, basi atakaye aamini na atakaye akufuru. Hakika sisi tumewaandalia wenye kudhulumu moto ambao hema lake litawazunguka, Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!

SOMA ULIYOPEWA WAHYI

Aya 27 -29

MAANA

Na soma uliyopewa wahyi katika kitabu cha Mola wako, Hapana wa kubadilisha maneno yake.

Anasema Mwenyezi Mungu kumwambia Mtume wake mtukufu: Fikisha tuliyokuteremshia yanayohusiana na watu wa pango na wengineo katika yaliyokuja kwenye Qur’an Tukufu. Kuwa na yakini na yale tunayokupa habari. Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake.

Siku na matukio yamethibitisha kuwa Muhammad(s.a.w.w) ni rehema iliyoongozwa kutoka mbinguni kwa ajili ya watu. Kila zama zinavyozidi kuendelea ndio unapatikana ushahidi wa hakika hii.

Wala hutapata makimbilio isipokuwa kwake.

Yaani huna pa kumkimbia Mungu, Maneno anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) . Maana yake ya dhahiri ni kuwa wewe Muhammad una majukumu mbele ya Mwenyezi Mungu wala hutapona ukiwa utatia shaka katika haki- ka ya Qur’an au kufanya uzembe katika kuifikisha.

Hasha! Haiwezekani kwa Mtume wa rehema kutia shaka au kufanya uzembe. Vipi iwe hivyo na hali Mwenyezi Mungu anajua zaidi pa kuuweka ujumbe wake! Isipokuwa makusudio ni kumweleza yule anayetia shaka katika utume wa Muhammad(s.a.w.w) au kuhalifu aliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanaomuomba Mola wao asubuhi na jioni, wakitaka radhi yake; wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya maisha ya dunia; wala usimtii tuliyemghafishilisha moyo wake asitukumbuke na akafuata matamanio yake na mambo yake yakawa yamepita kiasi.

Ikisemwa isuburishe nafsi yako pamoja na fulani; yaani kuwa naye. Makusudio ya wanaomuomba Mola wao ni wale waumini wenye ikhlasi. Asubuhi na jioni ni fumbo la kudumu kwenye twaa ya Mungu. macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya dunia; yaani usigeuze umuhimu wako kutoka kwa watu wa dini ukaenda kwa watu wa dunia. Walioghafishilishwa ni makafiri na wenye makosa. Kupita kiasi mambo ni kauli na vitendo kupituka haki na uadilifu.

Imepokewa kuwa Uyayna - mmoja wa viongozi wa washirikina - alikwenda kwa Mtume(s.a.w.w) akaona mafukara wamekaa naye, akiwemo Salmani Farisi akiwa na kilemba kilichojaa jasho na mkononi akiwa na jani la mtende.

Uyayna akasema: “Huu uvundo wa hawa haukusumbui wewe. Sisi vigogo wa Mudhar tukisilimu watasilimu watu wengi, Hakuna kinachotuzuia isipokuwa wafuasi wako hawa tu, Hebu achana nao tukufuate sisi au uwafanyie kikao chao na sisi tuwe na kikao chetu” Ndipo ikashuka Aya hiyo.

Sisi hatujui usahihi wa mategemezi ya riwaya hii, lakini tunaitilia nguvu kwa sababu inaenda na muktadha wa hali; yaani hali ya wapenda makuu na kujifanya wakubwa wakiwadharau wanyonge. Hilo limenukuliwa na Qur’an:

وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ ﴿٢٧﴾

“Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni” Juz; 12, (11:27).

Kabla ya Mtume(s.a.w.w) kumjibu Uyayna na mfano wake kuwa ndio au hapana, aliye Mtukufu na kutuka akamwambia: kuwa pamoja na waumini, kwa vile wao wako pamoja nami, nami niko pamoja nao na uvumilie na wanayoyasema wapenda makuu. Kwa sababu subira yako kwao ni subira ya Mwenyezi Mungu na utiifu wake. Kwani huoni imani yao na ikhlasi yao kwangu na kwako katika kila kitu, wakitaka radhi yangu na thawabu zangu?

Ama waovu waliopofushwa na matamanio ya nyoyo zao, wanaofanya mambo kwa masilahi yao tu, wakikataa kuishi na wengine kwa haki na uadilifu, isipokuwa kiburi na kujikweza na kupituka mipaka yote ya Mwenyezi Mungu na ya binadamu, Hawa usiwasikilize. Kwani kauli yao hiyo ni ushenzi, uongo na upotevu; bali ni juu yako kupambana nao na kuwawekea ngumu kwa kauli na vitendo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قَاتِلُوا الَّذِينَ يَلُونَكُم مِّنَ الْكُفَّارِ وَلْيَجِدُوا فِيكُمْ غِلْظَةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴿١٢٣﴾

“Enyi mlioamini! Piganeni na wale walio karibu yenu katika makafiri na wakute kwenu ugumu; na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.” Juz, 11 (9:123).

Sema hii ni kweli itokayo kwa Mola wenu.

Anaambiwa Mtume awaambie wale walioghafilishwa nyoyo zao au watu wote. Hii ni usisitizo wa kauli iliyotangulia ya wasomee uliyopewa wahyi

Basi atakaye aamini na atakaye akufuru.

Hii ni sawa na kauli yake Mungu:

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا ﴿٣﴾

“Hakika sisi tumembainishia njia, Ama ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru” (76:3).

Aya hii inafahamisha kuwa mtu ana hiyari sio mwenye kuendeshwa, Lakini Razi amemrudi mwenye kutoa dalili kwa Aya hii kwamba utashi wa mtu haufanyi yeye mwenyewe, bali unafanywa na Mungu kwa hiyo kwake yeye mtu ni mwenye kuendeshwa hana hiyari.

Nasi tunamjibu: Hakika utashi wa mtu unatokana na sababu na mazingira yanayomzunguka. Mfano mtu kumuona mwanamke mzuri nafsi yake ikampondokea, na hali dini imewajibisha mtu kuizuiwa nafsi yake, katika hali hii.

Hakuna mwenye shaka kwamba hili liko chini ya uwezo wake mtu (anaweza kulizuia), Mtume wa Mwenyezi Mungu ameliita hilo ‘Jihadi kubwa’ Kuna riwaya isemayo kuwa Mtume alituma kikosi cha wapiganaji.

Kiliporudi, akasema: Karibuni watu waliomaliza jihadi ndogo na kubakiwa na jihadi kubwa.” Akaulizwa ni ipi jihadi kubwa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Jihadi ya nafsi. Hakika jihadi bora ni ya yule mwenye kufanya jihadi ya nafsi yake ambayo iko baina ya mbavu zake.

Hakika sisi tumewaaandalia wenye kudhulumu moto ambao hema lake litawazunguka. Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!

Hili ni onyo na hadhari kwa kwa yule anayeathirika na ukafiri kuliko imani na batili kuliko haki, kwamba adhabu itazunguka pande zote; sawa na hema linavyomzunguka mtu, na watendela kupata kila aina ya dhabu.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا ﴿٣٠﴾

30. Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya mazuri

أُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَيَلْبَسُونَ ثِيَابًا خُضْرًا مِّن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ نِعْمَ الثَّوَابُ وَحَسُنَتْ مُرْتَفَقًا ﴿٣١﴾

31. Hao wana bustani za milele zinazopita mito chini yake, watavaa nguo za kijani za hariri na atlasi, Huku wakiegemea juu ya makochi. Ni malipo bora yalioje na mahali pazuri palioje pa kupumzika.

UJIRA WA WATENDAO MEMA HAUPOTEI

Aya 30 – 31

MAANA

Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya mazuri.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja madhalimu na adhabu yao, sasa anataja wema na malipo yao. Akabainisha aina hii ya thawabu kwa kauli yake:

Hao wana bustani za milele zinazopita mito chini yake, watavaa nguo za kijani za hariri na atlasi, Huku wakiegemea juu ya makochi. Ni malipo bora yalioje na mahali pazuri palioje pa kupumzika.

Katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu anasema:

وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ﴿٧١﴾

“Na humo vitakuwemo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia” (43:71).

Imam Ali(a.s) anasema: “Kila neema isiyokuwa Pepo ni ya kudharauliwa na kila balaa isiyokuwa moto ni raha.” Umepita mfano wake katika Aya nyingi ikiwemo Juz. 1 (2: 82), Juz.4 (3:171) na Juz.5 (4:57).

Kauli ya kushangaza ni ile ya badhi ya masufi, kwamba makusudio ya kivazi ni tawhid, nguo za kijani ni sifa zinazoleta furaha, hariri ni vipawa, atlasi ni maadili na makochi ni majina ya Mwenyezi Mungu.

Wala hakuna ujeuri mkubwa kwa Mungu kuliko kutafsiri makusudio yake kwa njozi na mawazo au kwa hawaa na malengo mengine.

وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا رَّجُلَيْنِ جَعَلْنَا لِأَحَدِهِمَا جَنَّتَيْنِ مِنْ أَعْنَابٍ وَحَفَفْنَاهُمَا بِنَخْلٍ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمَا زَرْعًا ﴿٣٢﴾

32. Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimjalia vitalu viwili vya mizabibu na tukavizunguushia mitende na kati yake tukajaalia mimea ya nafaka.

كِلْتَا الْجَنَّتَيْنِ آتَتْ أُكُلَهَا وَلَمْ تَظْلِم مِّنْهُ شَيْئًا وَفَجَّرْنَا خِلَالَهُمَا نَهَرًا ﴿٣٣﴾

33. Hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hivyo kilichotindika. Na ndani yake tukapasua mito.

وَكَانَ لَهُ ثَمَرٌ فَقَالَ لِصَاحِبِهِ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَنَا أَكْثَرُ مِنكَ مَالًا وَأَعَزُّ نَفَرًا ﴿٣٤﴾

34. Naye alikuwa na mazao. Basi akamwambia mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda kwa mali na nguvu za watu.

وَدَخَلَ جَنَّتَهُ وَهُوَ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ قَالَ مَا أَظُنُّ أَن تَبِيدَ هَـٰذِهِ أَبَدًا ﴿٣٥﴾

35. Akaingia kitaluni kwake, naye ameidhulumu nafsi yake, akasema: Sidhani kuwa haya yataharibika milele.

وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِّنْهَا مُنقَلَبًا ﴿٣٦﴾

36. Wala sidhani kuwa hiyo saa (ya Kiyama) itatokea, Na kama nitarudishwa kwa Mola wangu bila shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya.

قَالَ لَهُ صَاحِبُهُ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا ﴿٣٧﴾

37. Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je, umemkufuru ambaye amekuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya kuwa mtu kamili?

لَّـٰكِنَّا هُوَ اللَّـهُ رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِرَبِّي أَحَدًا ﴿٣٨﴾

38. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, wala si mshirikishi na yeyote.

وَلَوْلَا إِذْ دَخَلْتَ جَنَّتَكَ قُلْتَ مَا شَاءَ اللَّـهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّـهِ إِن تَرَنِ أَنَا أَقَلَّ مِنكَ مَالًا وَوَلَدًا ﴿٣٩﴾

39. Na lau ulipoingi kitaluni kwako ungelisema, alitakalo Mwenyezi Mungu huwa (mashaallah!), hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe.

فَعَسَىٰ رَبِّي أَن يُؤْتِيَنِ خَيْرًا مِّن جَنَّتِكَ وَيُرْسِلَ عَلَيْهَا حُسْبَانًا مِّنَ السَّمَاءِ فَتُصْبِحَ صَعِيدًا زَلَقًا ﴿٤٠﴾

40. Basi huenda Mwenyezi Mungu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako na kukipelekea maafa kutoka mbinguni na kugeuka ardhi tupu inayoteleza.

أَوْ يُصْبِحَ مَاؤُهَا غَوْرًا فَلَن تَسْتَطِيعَ لَهُ طَلَبًا ﴿٤١﴾

41. Au maji yake yadidimie usiweze kuyagundua.

وَأُحِيطَ بِثَمَرِهِ فَأَصْبَحَ يُقَلِّبُ كَفَّيْهِ عَلَىٰ مَا أَنفَقَ فِيهَا وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُشْرِكْ بِرَبِّي أَحَدًا ﴿٤٢﴾

42. Yakaangamizwa matunda, akabaki anapinduapindua viganja vyake, kwa vile alivy - oyagharimia, nayo imeanguka juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingelimshirikisha Mola wangu na yoyote.

وَلَمْ تَكُن لَّهُ فِئَةٌ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَمَا كَانَ مُنتَصِرًا ﴿٤٣﴾

43. Wala hakuwa na kundi la kumsadia kinyume na Mwenyezi Mungu wala mwenyewe hakuweza kujisaidia.

هُنَالِكَ الْوَلَايَةُ لِلَّـهِ الْحَقِّ هُوَ خَيْرٌ ثَوَابًا وَخَيْرٌ عُقْبًا ﴿٤٤﴾

44. Huko usaidizi ni wa Mwenyezi Mungu, Mkweli. Yeye ni Mbora kwa malipo na mbora wa matokeo.

BAINA YA KAFIRI TAJIRI NA MUMIN FUKARA

Aya 32 – 44

MUHTASARI WA KISA

Tulipofasiri Aya 27 ya Sura hii tulitaja kuwa vigogo wa kishirikina walitoa sharti la kumwamini kwao Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kuwa awafukuze mafukara au awatengee vikao vyao ili wasichanganyike na mafakura, kwa vile wao ni mabwana na viongozi na watu wengine ni watumwa wao tu.

Aya tulizo nazo sasa zinaleta picha ya matajiri wenye kiburi, kwa mtu mmoja tajiri mwenye mali na mashamba na picha ya mafukara waumini, kwa mtu mmoja fukara asiye na chochote, lakini anajitukuza kwa maadili yake na tajiri anajitukuza kwa mali yake. Yanapita majibizano baina yao yanayowakilisha mvutano baina ya haki na batili. Hatimaye haki inashinda na batili inaanguka. Amesema kweli mwenye hekima aliyesema: “Mwenye kupigana na haki itampiga mweleka”

Kwa ufupi, maana ya Aya hizo ni: Yule anayejitukuza kwa mali yake, anamiliki mashamba mawili makubwa yenye miche ya ngano na nafaka nyinginezo. Pia mna miti mingi ya mitende na mizabibu. Mashamba yote mawili yana chemchem ya maji; mavuno yake ni mazuri na kamili. Ama yule anayejitukuza kwa maadili yake, hana kitu chochote.

Mwenye mashamba akamwambia yule fukara kwa kujisifu na kujinaki: Mimi nimekushinda na kila kitu – mali na jaha. Angalia mimea, miti, matunda na mito ya maji niliyo nayo. Hii ndio milki ya kudumu itakayoku- ja wafaa watoto na wajukuu; sio pepo mnayodai nyinyi masikini. Hivi baada ya mauti kweli kuna pepo na moto? Kama itakuwa ni kweli basi hadhi yangu huko itakuwa kubwa kuliko hapa duniani. Kwa sababu aliye tajiri hapa huko pia atakuwa tajiri .

Yule mumin akamjibu kwa kumjadili na kumlaumu: Hivi unasema haya kwa kumbughudhi na kumkufuru ambaye amekufanya uwe mtu? Umesahau asili yako? Wewe si umetokana na Adamu na Adam akatokana na mchanga? Hukuwa wewe ni tone la manii? Mimi mwenzako ninamwamini Mwenyezi Mungu na ninampwekesha, ninamsifu kwa kuniongoza kwenye njia yake na radhi zake. Kama ungekuwa na busara basi ungelimnyenyekea Mwenyezi Mungu na kumshukuru badala ya kujitia ujuvi kwa dhambi. Ni lipi liliokufanya ujiaminishe na mambo ya kushtukiza ya ghafla? Mungu akiwapa muda waasi kwa huruma zake huwa amewapa muda wa hasira zake na nakama yake.

Kabla ya hata kumaliza maneno yake yule mumin, mara miti ikaanza kuanguka, mito ikakauka, mimea ikateketea na kila kitu shambani kikaharibika. Mwenye shamba akasema: “Sikufikira kabisa itaharibika hii.” Baada ya kuona alivyofanya Mwenyezi Mungu na kukata tamaa ya mimea yake na miti yake alisema kwa masikitiko: “Laitani nisingemshirikisha Mola wangu na yeyote.” Lakini wapi! Hivi sasa na hali hapo mwanzo umemuasi na ukawa katika wafisadi?

Huu ndio muhtasari wa kisa. Na makusudio ya kisa hicho ni kuwa mtu aamini kwa kauli na vitendo kuwa hakuna hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu mmoja mwenye kushinda. Na kwamba Yeye ambaye imetukuka hekima yake saa yoyote anayotaka anaweza kumgeuza mtukufu kuwa dhalili na dhalili kuwa mtukufu. Vilevile tajiri kuwa fukara na fukara kuwa tajiri na afya kuwa ugonjwa na maumivu na kinyume chake. Vile vile mtu aamini kuwa milki ya mwenye kuumbwa si chochote kadiri itakavyokuwa ila akiibadilisha katika kazi za kheri.

Baada ya muhtasari huu sasa tuingilie ufafanuzi wa na tafsiri ya Aya ingawaje nyingi ziko wazi zisizohitaji ufafanuzi.

MAANA

Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimjalia vitalu viwili vya mizabibu na tukavizunguushia mitende na kati yake tukajaalia mimea ya nafaka, Hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hivyo kilichotindika. Na ndani yake tukapasua mito.

Anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) awambie washirikina waliosema kuwa awafukuze mafukara au amwambie kila mpenda makuu mwenye kiburi, Makusudio ya watu wawili ni tajiri na fukara ambao walikuwa na majibizano.

Ni maarufu Qur’an kuwa mara nyingi inaleta mifano ya fikra na misingi ya kiujmla na kufananisha na vitu vyenye kuhisiwa; kama kufananisha imani na nuru na ukafiri na giza. Pia mara nyingine inafananisha chenye kuhisiwa na chenye kuhisiwa kingine kilichowazi zaidi na kilicho na ubainifu zaidi; kama kufananisha mwenye kurtadi na mbwa mwenye kuhema kwa nguvu.

Lengo la yote hayo ni kufafanua na kuweka wazi, kuongezea mazingatio na mawaidha:

وَعَادًا وَثَمُودَ وَأَصْحَابَ الرَّسِّ وَقُرُونًا بَيْنَ ذَٰلِكَ كَثِيرًا ﴿٣٨﴾ وَكُلًّا ضَرَبْنَا لَهُ الْأَمْثَالَ وَكُلًّا تَبَّرْنَا تَتْبِيرًا ﴿٣٩﴾

“Na tuliwaangamiza kina watu A’d na Thamud na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyokuwa kati yao na wote tuliwapigia mifano.” (25:38-39).

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa amefananisha hali ya mataghuti wapenda makuu wenye kiburi na mtu mmoa kafiri mwenye kiburi mjinga aliye na vitalu viwiwili ambavyo ndani yake mna mto, mimea ya nafaka na miti inayobeba matunda bora ya wakati huo, ambayo ni tende na zabibu.

Mimea yote inatoa mazao kwa wakati wake kwa ukamilifu. Na akamfananisha mumin na mtu mmoja mnyeneykevu mwenye maarifa, lakini hana chochote ni fukara. Yakatokea majibizano baina ya wawili hao; kama ifuatavyo:-

Basi akmwambia mwenzake naye akibishana naye.

Aliyesema ni yule tajiri mwenye kiburi kumwambia mwenzake mumin mwenye adabu

Mimi nimekushinda kwa mali na nguvu za watu.

Aliona kuwa mali na jaha ndio kipimo cha utukufu, lakini imani na ikhlasi ni maneno matupu tu yasiyokuwa na maana. Hii ndio mantiki ya mafasiki na wovu, tangu zamani hadi leo. Thamani ya mtu kwao ni kile anachokimiliki, sio matendo mema wala elimu nzuri.

Mali ndiyo inayosababisha matatizo ya binadamu, Ndio kichocheo cha kwanza cha fitina ya silaha za maangamizi na kutumia mamilioni ya walalahoi kutengenezea silaha hizo. Wanyonyaji wanaiba mali ya wananchi na kuigeuza mabomu na maroketi kisha wayatupe kwa hao hao wananchi waliowanyanganya riziki zao na maliasili zao.

Akaingia kitaluni kwake, naye ameidhulumu nafsi yake kwa sababu aliyaitikia matamanio yake akaitia hatarini nafsi yake; sawa na anayemkubalia mwanawe mambo yatakayomdhuru na kumwangamiza.

Akasema: Sidhani kuwa haya yataharibika milele.

Razi anasema: “Vipi alisema kuwa sidhani kuwa haya yataharibika milele pamoja na kuwa hisia zinafahamisha kuwa dunia si yenye kubakia? Tunasema: alikusudia kuwa havitaharibika katika uhai wake”

Jibu sahihi ni kuwa ujinga na ghururi zilimpofusha mwenye shamba na kila kitu hata na vitu waziwazi na vyenye kuhisiwa. Anasema Mtukufu wa wasemao: “Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi, Hao ndio walioghafilika.” Juz. 9 (7:179).

Wala sidhani kuwa hiyo saa (ya Kiyama) itatokea.

Dhana hii haitegemei chochote isipokuwa majivuno ghururi na mambo ya kuwazia tu, kwamba neema yake ni ya milele haitaisha. Hii ndio tafsiri ya mataghuti wajivuni wanaokana hisabu na ufufuo.

Na kama nikirudishwa kwa Mola wangu bila shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya.

Kwa fikra yake anaona kuwa wapenda makuu huko pia wana nafasi, Anakisia ya ghaibu kwa ya sasa. Hajui kwamba uokovu kesho ni wa wamchao Mungu, sio mataghuti na wajivuni:

مَا أَغْنَىٰ عَنِّي مَالِيَهْ ﴿٢٨﴾ هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيَهْ ﴿٢٩﴾

“Mali yangu hayakunifaa, Madaraka yangu yamenipotea” (69:28-29).

Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je, umemkufuru ambaye amekuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kamili?

Mumini alimwambia kafiri kwa kumlaumu, kuwa unamkana aliyekuumba na dalili zake ziko wazi kwako? Umepata vipi uhai pamoja na akili yake na uoni wake? Si ulikuwa si chochote?

Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, wala si mshirikishi na yoyote.

Anaendelea kusema mumin, ama mimi nimeongoka kwa umbile langu na akili yangu kwa muumba wangu na muumba wa kila kitu na nimeamini kuwa Yeye pekee ndiye muumba mwenye kuruzuku.

Kisha muumin akamkumbusha yule kafiri neema ya Mwenyezi Mungu kwake na wajibu wa kumshukuru na kumsifu kwa kumwambia:

Na lau ulipoingia kitaluni kwako ungelisema alitakalo Mwenyezi Mungu huwa (mashaallah!), hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu.

Yaani lau ungelikuwa una busara ungelitambua kuwa kheri na fadhila ni kuongezeka ujuzi wako sio mali yako, ungeshindana na watu kwa maadili yako sio kwa jaha yako na kujua kuwa hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu mmoja mwenye nguvu na kushinda.

Ni Yeye pekee ndiye anayetoa enzi na jahaa na kubadilisha utajiri kwa ufukara na ufukara kwa utajiri; alitakalo huwa na asilolitaka haliwi.

Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, basi huenda Mwenyezi Mungu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako na kukipelekea maafa kutoka mbinguni na kugeuka ardhi tupu inayoteleza; au maji yake yadidimie usiweze kuyagundua.

Mumin aliendelea kumjia juu kafiri kwa mali yake, akamwambia kuwa utajiri na ufukara unatoka kwa Mungu na wewe hujui mimi nina utajiri zaidi wa kukushinda wewe alioniwekea akiba Mwenyezi Mungu kwenye nyumba ya milele kushinda hivi vitalu vyako unavyojifaharisha navyo.

Hujui wewe kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kunifanya tajiri mimi na kukufanya fukara wewe baina ya asubuhi na jioni.

Wewe unajigamba na mali yako, kwa sababu watu wanakusifia. Je sifa hizi ndio zitakukinga na mambo yanayofichwa na nyakati? Je, umejiaminisha na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu? Huogopi wewe na hivyo vitalu vyako kushukiwa na majanga kutoka mbinguni na ukabaki mtupu?

Yakaangamizwa matunda, akabaki anapinduapindua viganja vyake kwa vile alivyoyagharimia nayo imeanguka juu ya chanja zake.

Kupinduapindua viganja ni fumbo la kujuta. Mimea iliangamia, miti ikaanguka kila upande na maji yakauka mpaka tone la mwisho. Ardhi ikawa inateleza; kama kwamba hakukuwa na chochote.

Ufukara ukachukua nafasi ya utajiri, dhiki mahali pa faraja na udhalili na kuvunjikiwa mahali pa kujitukuza na kiburi. Haya ndio matunda ya ukafiri, dhulma na ufisadi – hasara na majuto ya juhudi na mali.

Akawa anasema: Laiti nisingelimshirikisha Mola wangu na yoyote.

Kama kwamba anakusudia, kwa kauli hii, kurudi kitalu chake, lakini wapi?

لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ﴿١٥٨﴾

“Basi nafsi haitaifaa imani yake ambayo haikuiamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake” Juz; 8 (6:158).

Wala hakuwa na kundi la kumsadia kinyume na Mwenyezi Mungu wala mwenyewe hakuweza kujisaidia.

Kabisa! Hakuna ndugu wala rafiki au jaha wala mali, isipokuwa Mwenyezi Mungu.

قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّـهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٢﴾

“Sema: Hakika hakuna yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake tu.” (72:22).

Huko usaidizi ni wa Mwenyezi Mungu, Mkweli. Yeye ni Mbora kwa malipo na mbora wa matokeo.

Huko ni ishara ya siku ya kiyama; yaani, ikiwa mtu katika maisha haya anapata wa kumtetea na kumsaidia, basi siku ya kiyama hatapata isipokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) peke yake.

Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua na amewaandalia ujira mwema na mahali pazuri.