TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA Juzuu 16

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10448
Pakua: 2455


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10448 / Pakua: 2455
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA Juzuu 16

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكَ إِنَّكَ لَن تَسْتَطِيعَ مَعِيَ صَبْرًا ﴿٧٥﴾

75. Akasema: Sikukuambia kuwa wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?

قَالَ إِن سَأَلْتُكَ عَن شَيْءٍ بَعْدَهَا فَلَا تُصَاحِبْنِي قَدْ بَلَغْتَ مِن لَّدُنِّي عُذْرًا ﴿٧٦﴾

76. Akasema: Nikikuuliza tena kitu baada ya haya usifuatane nami kwani umekwishapata udhuru kwangu

فَانطَلَقَا حَتَّىٰ إِذَا أَتَيَا أَهْلَ قَرْيَةٍ اسْتَطْعَمَا أَهْلَهَا فَأَبَوْا أَن يُضَيِّفُوهُمَا فَوَجَدَا فِيهَا جِدَارًا يُرِيدُ أَن يَنقَضَّ فَأَقَامَهُ قَالَ لَوْ شِئْتَ لَاتَّخَذْتَ عَلَيْهِ أَجْرًا ﴿٧٧﴾

77. Basi wawili hao wakaondoka, mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja, wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka akausimamisha, Akasema (Musa): Ungelitaka ungelichukua ujira kwa haya.

قَالَ هَـٰذَا فِرَاقُ بَيْنِي وَبَيْنِكَ سَأُنَبِّئُكَ بِتَأْوِيلِ مَا لَمْ تَسْتَطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٧٨﴾

78. Akasema: “Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Nitakueleza taawili ya yale uliyokuwa huwezi kuyavumilia.

أَمَّا السَّفِينَةُ فَكَانَتْ لِمَسَاكِينَ يَعْمَلُونَ فِي الْبَحْرِ فَأَرَدتُّ أَنْ أَعِيبَهَا وَكَانَ وَرَاءَهُم مَّلِكٌ يَأْخُذُ كُلَّ سَفِينَةٍ غَصْبًا ﴿٧٩﴾

79. Ama ile jahazi iikuwa ni ya maskini wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuitia kasoro, kwani nyuma yao kulikuwa na mfalme anayenyang’anya majahazi yote.

وَأَمَّا الْغُلَامُ فَكَانَ أَبَوَاهُ مُؤْمِنَيْنِ فَخَشِينَا أَن يُرْهِقَهُمَا طُغْيَانًا وَكُفْرًا ﴿٨٠﴾

80. Ama yule kijana wazazi wake walikuwa waumini, tukahofia asiwahangaishe kwa uasi na kufuru.

فَأَرَدْنَا أَن يُبْدِلَهُمَا رَبُّهُمَا خَيْرًا مِّنْهُ زَكَاةً وَأَقْرَبَ رُحْمًا ﴿٨١﴾

81. Basi tulitaka Mola wao awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika na aliye karibu zaidi kwa huruma.

وَأَمَّا الْجِدَارُ فَكَانَ لِغُلَامَيْنِ يَتِيمَيْنِ فِي الْمَدِينَةِ وَكَانَ تَحْتَهُ كَنزٌ لَّهُمَا وَكَانَ أَبُوهُمَا صَالِحًا فَأَرَادَ رَبُّكَ أَن يَبْلُغَا أَشُدَّهُمَا وَيَسْتَخْرِجَا كَنزَهُمَا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ وَمَا فَعَلْتُهُ عَنْ أَمْرِي ذَٰلِكَ تَأْوِيلُ مَا لَمْ تَسْطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٨٢﴾

82. Na ama ukuta ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini, na chini yake ilikuwako hazina yao, na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako alitaka wafikie kukomaa na wajitolee hazina yao. Nirehema itokayo kwa Mola wako. Hayo sikuyatenda kwa amri yangu, Hiyo ndiyo tafsiri ya ambayo hukaweza kuyavu milia.

HUWEZI KUVUMILIA

Aya 75 – 82

MAANA

Juzuu ya 15, imeishia na Aya ya kuuliwa kijana na mshangao wa Musa kwa tendo hilo. Kwenye Aya hii swahibu wa Musa anamkumbusha kuhusu walivyoahidiana:

Akasema: “Sikukuambia kuwa wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?

Anamkumbusha tena lile sharti na Musa naye anaomba tena msamaha akasema:Nikikuuliza tena kitu baada ya haya usifuatane nami.

Hapo mwanzo yule mtu alimuwekea sharti Musa, hivi sasa Musa anajiwekea mwenyewe sharti kwamba asisuhubiane naye tena kama atamuuliza, na waumini wanalazimiana na masharti yao; sikwambii tena mitume.

Kwani umekwishapata udhuru kwangu; Sababu zote zitakuwa zimekwisha.

Basi wawili hao wakaondoka, mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja.

Huu ni ushahidi wa tatu wa kuwa ni wachache wanaovumilia. Ushahidi wa kwanza na wa pili umekwishapita kwenye Juzuu ya 15. Inasemekana mji huo walioufikia ni Antioch. Katika riwaya iliyopokewa kwa Imam Jafar As-Swadiq, inasema kuwa ni Nazarethi[1] .

Wakawaomba watu wake wawape chakula, lakini nao wakakataa kuwakaribisha.

Wafasiri wanasema kuwa Mwenyezi Mungu amesema walikataa kuwakaribisha, badala ya walikataa kuwapa chakula, kwa vile watu wa mji ule walikuwa wabaya sana. Kwani hakuna anayemkataa mgeni ila mtu mbaya, hasa ikiwa mgeni ni wa mbali.

Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, akausimamisha.

Hapo, ni hapo kwenye mji. Aliyeusimamisha, ni yule mja mwema. Kutaka kuanguka, ni kukurubia kuanguka. Maana ni kuwa Musa na mwenzake walikuta ukuta unakaribia kuanguka, yule mwenzake akautengeneza bila ya malipo yoyote.

Ndipo Musa akastaajabu na akasema: Ungelitaka ungelichukua ujira kwa haya.

Unafanya kazi ya bure tu kwa watu waliokataa hata kutukaribisha tukiwa na shida. Kutoboa jahazi na kuua kijana ni mifano miwili yenye dhahiri ya ubaya na kusimamisha ukuta ni kinyume cha mifano hiyo miwili.

Akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Nitakueleza taawili ya yale uliyokuwa huwezi kuyavumilia.

Mja mwema alitoa sharti kwa Musa la kutoulizwa, Musa akakubali, lakini pamoja na hayo akauliza, Alipokumbushwa akaomba msamaha, Tena akauliza baada ya msamaha. Alipokumbushwa mara ya pili akajiwekea sharti yeye mwenyewe la kutofuatana naye kama atauliza tena. Lakini bado akauliza, ingawaje alikuwa na hamu sana ya kufuatana naye.

Musa hana lawama yoyote katika yote aliyoyauliza; Kwa sababu nafsi yake inaweza kuvumilia mambo ya kheri na mazuri, lakini yale anayoyaona ni mabaya, hakuweza wala hataweza kuvumilia; hata kama hilo litapelekea kuvunja masharti na maelewano. Ni kipimo gani cha masharti kinachoweza kupimwa kuacha mema na kukataza mabaya.

Imani sahihi haiwezi kuzuiwa na kitu chochote, si msukumo wa nafsi wala mengineyo. Hakuna kitu kigumu zaidi kuliko imani sahihi; na atakayeshindwa na kitu chochote katika hivyo basi hana imani sahihi; hata akiswali, kufunga na kuhiji Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu.

Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe , ushike njia yako nami nishike yangu, Hivyo ndivyo alivyomwambia Musa. Lakini kabla ya kutengana, yule mja mwema alimwambia Musa hekima ya yale aliyoyapinga, kama ifuatavyo:

Ama lile jahazi lilikuwa ni la maskini wafanyao kazi baharini. Nilitaka kulitia kasoro, kwani nyuma yao kulikuwa na mfalme anayenyang’anya majahazi yote.

Mwenye akili anavumilia madhara kwa ajili ya kuondoa madhara makubwa; kama anavyosema mshairi: “Nimevumilia nusu shari kihofia shari yote.”

Kuanzia hapa ndio mafaqihi wakaafikiana kuwa dhara kubwa inakingwa na dhara hafifu na yakiingiliana maovu mawili litaangaliwa lile lenye madhara zaidi kwa lile lililo na machache. Kutokana na kawaida hii wametoa hukumu nyingi, kama vile kuruhusiwa kukata kiungo ikiwa kitamletea mtu maangamizi.

Ama yule kijana wazazi wake walikuwa waumini, tukahofia asiwahangaishe kwa uasi na kufuru. Basi tulitaka Mola wao awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika na aliye karibu zaidi kwa huruma.

Imepokewa riwaya kutoka kwa Imam Jafar As-Swadiq(a.s) kuwa huyo kijana aliuawa katika rika la balehe na alikuwa kafiri. Akifanya juhudi kuwaingiza wazazi wake kwenye ukafiri, sawa na wanavyofanya baadhi ya vijana wa kileo.

Tumewahi kuwona maulama wengi wa kidini waliokuwa ni tegemeo kubwa la watu, lakini mara tu walipobalehe vijana wao, wakabomoa yote waliyojenga baba zao kwa muda mrefu.

Kuna kauli mashuhuri ya Imam Ali(a.s) :“Zubeir aliendelea kuwa nasi mpaka alipokuwa na kijana wake Abdullah”

Ahmad Amin wa Misr, katika kitabu Hayati (maisha yangu), anasema: “Hivi sasa mimi na uzee wangu ninakubali kila ambalo nilikuwa nikilikataa na huwa ninaacha misimamo niliyokuwa nayo kwa sababu ya watu na mazungumzo yao na wingi wa watoto.”

• Udogo sikutaka Hawa nafsi yangu

• Zama zikakatika kawa na mvi zangu

• Hawa zikanishika kinyume matakwa yangu

• Laitani ngezalika nao ukubwa wangu

• Udogo wa marika kupinga nafsi yangu

Na ama ukuta ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini, na chini yake ilikuwako hazina yao, na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako alitaka wafikie kukomaa na wajitolee hazina yao. Ni rehema itokayo kwa Mola wako. Hayo sikuyatenda kwa amri yangu, Hiyo ndiyo tafsiri ya ambayo hukaweza kuyavumilia.”

Kwa ufupi ni kuwa ukuta ulikua wa watoto wawili na chini yake kulikuwa na dafina yao. Mwenyezi Mungu akataka kuilinda mali hiyo isipotee, kwa kubakia ukuta, mpaka wawe wakubwa au wawe na akili, kisha wajitolee mali yao wao wenyewe; na mzazi wao alikuwa mtu mwema “Na wema wa mtu mumini, Mwenyezi Mungu huufanya kwa mtoto wake na mtoto wa mtoto wake.”

Funzo la kisa hiki ni kwamba mtu asijione ni yeye tu na asifanye haraka kujiamulia jambo kwa kuangalia upande mmoja, bali ni lazima aangalie pande zote kwa undani na kulinganisha kisha aangalie ulio bora zaidi; kwani masilahi huwa yanasigana na madhara.

Hakuna jambo lolote la manufaa isipokuwa lina baadhi ya madhara ndani yake; kama ambavyo hakuna jambo lolote ila lina baadhi ya manufaa. Siku zote mazingatio ni kwa lililo na wingi.

وَيَسْأَلُونَكَ عَن ذِي الْقَرْنَيْنِ قُلْ سَأَتْلُو عَلَيْكُم مِّنْهُ ذِكْرًا ﴿٨٣﴾

83. Na wanakuuliza kuhusu Dhul-qarnain, Waambie nitawasimulia baadhi ya habari zake.

إِنَّا مَكَّنَّا لَهُ فِي الْأَرْضِ وَآتَيْنَاهُ مِن كُلِّ شَيْءٍ سَبَبًا ﴿٨٤﴾

84. Hakika sisi tulimmakinisha katika ardhi na tukampa sababu ya kila kitu.

فَأَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٨٥﴾

85. Basi akafuata sababu.

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَغْرِبَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَغْرُبُ فِي عَيْنٍ حَمِئَةٍ وَوَجَدَ عِندَهَا قَوْمًا قُلْنَا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِمَّا أَن تُعَذِّبَ وَإِمَّا أَن تَتَّخِذَ فِيهِمْ حُسْنًا ﴿٨٦﴾

86. Hata alipofika machweo ya jua aliona linatua kwenye chemchem yenye matope meusi, Na hapo akawakuta watu, tukasema: Ewe Dhul-qarnain! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.

قَالَ أَمَّا مَن ظَلَمَ فَسَوْفَ نُعَذِّبُهُ ثُمَّ يُرَدُّ إِلَىٰ رَبِّهِ فَيُعَذِّبُهُ عَذَابًا نُّكْرًا ﴿٨٧﴾

87. Akasema: “Ama aliyedhulumu, basi tutamwadhibu adhabu na kisha atarudishwa kwa Mola wake amuadhibu adhabu isiyojulikana.

وَأَمَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُ جَزَاءً الْحُسْنَىٰ وَسَنَقُولُ لَهُ مِنْ أَمْرِنَا يُسْرًا ﴿٨٨﴾

88. Na ama mwenye kuamini na akatenda mema tutamlipa malipo mazuri na tutamwambia lililo jepesi katika amri yetu.

ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٨٩﴾

89. Kisha akafuata sababu.

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَطْلِعَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَطْلُعُ عَلَىٰ قَوْمٍ لَّمْ نَجْعَل لَّهُم مِّن دُونِهَا سِتْرًا ﴿٩٠﴾

90. Mpaka alipofika mawiyo ya jua aliona linawachomozea watu tusiowawekea sitara ya kuwakinga nalo.

كَذَٰلِكَ وَقَدْ أَحَطْنَا بِمَا لَدَيْهِ خُبْرًا ﴿٩١﴾

91. Kama hivyo tulizijua vizuri habari zake.

ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٩٢﴾

92. Kisha akafuata sababu.

DHUL-QARNAIN

Aya 83 – 92

MAANA

Na wanakuuliza kuhusu Dhul- qarnain, Waambie nitawasimulia baadhi ya habari zake.

Wametofautiana kuhusu Dhul-qarnaini huyu kuwa ni nani? Ikasemekana kuwa alikuwa miongoni mwa Malaika, lakini hili ni jambo la kushangaza, Ikasemekana alikuwa Mtume.

Imepokewa kutoka kwa Imam Ali(a.s) kwamba yeye alikuwa ni mja mwema. Hakuna shaka ya wema wake, kwani vitendo vyake na kauli zake, alizozisajili Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika kitabu chake, zinatoa ushahidi wa ubora wake na wema wake.

Pia imesemekana kuwa ni Alexandre wa Macedonia (The great Alexandre), mwanafunzi wa Aristotle. Lakini hili nalo ni la kushangaza zaidi, kwa sababu Alexandre alikuwa ni mwabudu masanamu na Dhul-qar-nain alikuwa akimwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Amenukuu Razi na Abu Hayyani Al-Andalusi (Mhispania), kutoka kwa Abu Rayhan Al-Biruni, kuwa Dhul-qarnaini alikuwa ni mwarabu wa Yemen kutoka kabila la Himayr na jina ake ni Abu Bakr.

Vilevile wametofautiana, kuwa kwa nini aliitwa Dhul-qarnain (mwenye pembe mbii)? Ikasemekana ni kwa kuwa yeye aikuwa ni mtukufu wa wazazi wawili.

Ikasemekana kuwa ni kwa vile alikuwa na misokoto miwili ya nywele. Pia ikasemekana ni kwa vile yeye alimiliki mashariki na magharibi na mengineyo katika kauli za kutofautiana.

Ni ajabu kwa wafasiri kujishughulisha na kuwashughulisha watu kwa jambo lisilokuwa na faida yoyote ya kidunia wala akhera. Tangu lini Qur’an ikajishughulisha na majina na sababu zake? Kama hilo lingekuwa na faida basi Qur’an isingelinyamazia.

Ni kwa ajili hii ndio sisi tukatosheka na dhahiri ya Qur’an na tunasema: watu walimuuliza Mtume mtukufu(s.a.w.w) kuhusu mtu aliyeitwa Dhul-qarnain, Mwenyezi Mungu akamwamrisha awaambie waulizaji kuwa nitawaambia baadhi ya habari zake.

Hakika sisi tulimmakinisha katika ardhi na tumpa sababu ya kila kitu

Makusudio ya kummakinisha hapa ni nguvu na utawala. Na sababu ni nyenzo zinazomfikisha mtu kwenye yale anayoyataka; kama vile elimu, uwezo, afya, mali, watu na zana. Zaidi ya hayo ni tawfiki ya Mungu na msaada wake, Nyenzo zote hizi alikuwa nazo Dhul-qarnain. Kwa hiyo akawa ni mwenye nguvu, Hii ndiyo maana ya kummakinisha katika ardhi. Aya inafahamisha waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) analeta vitu kwa sababu zake.

Basi akafuata sababu

Mwenyezi Mungu alimwandalia njia naye akazitumia katika kheri na matendo mema. Miongoni mwazo ni kwenda kwake magharibi ambako amekuashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika kauli yake:

Hata alipofika machweo ya jua aliona linatua kwenye chemchem yenye matope meusi.

Makusudio ya machweo ya jua ni miji ya magharibi, Ni wazi kuwa jua haliwezi kuingia kwenye chemchem. Kwa hio makusudio ni chemchem yenye matope meusi ya bahari ambayo yanaonekana na watu kama Jua linatua ndani yake. Bahari hii ni miongoni mwa bahari za miji ya magharibi, lakini ni bahari gani hiyo? Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi wa hilo. Sheikh Maraghi anasema ni bahari ya Atlantic.

Na hapo akawakuta watu, tukasema: Ewe Dhul-qarnain! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.

Makusudio ya hapo ni hapo kwenye chemchem. Dhahiri ya Aya, ikiwa peke yake, inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwachia Dhul-qarnain afanye atakavyo kwa watu wa mji huo, akitaka atawaadhibu na akitaka awafanyie hisani.

Na ilivyo hasa ni kuwa jambo hilo haliafikiani na uadilifu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kafiri na washirikina, ikiwa watang’ang’ania kufru na shirk, tutapata kuwa watu aliowakuta Dhul-qar-nain huko magharibi walikuwa ni makafiri na kwamba yeye aliwelezea imani wakaikataa.

Unaweza kuuliza : kuwa je, inafaa kuwafanyia wema makafiri?

Jibu : Inafaa ikiwa hawakutupiga vita kwenye dini yetu wala hawakututoa majumbani mwetu. Mwenyezi Mungu anasema:

لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ ﴿٨﴾

“Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakuwafukuza katika miji yenu; Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanya uadilifu.” (60:8).

Akasema (Dhul-qarnain): Ama aliyedhulumu, basi tutamwadhibu adhabu na kisha atarudishwa kwa Mola wake amuadhibu adhabu isiyojulikana. Na ama mwenye kuamnini na akatenda mema tutamli- pa malipo mazuri na tutamwambia lililo jepesi katika amri yetu.

Hii ndio desturi ya hukumu Dhul-qarnain na utawala wake. Kwa ufupi ni kuwa, upanga ni kwa mwenye kuasi na wema ni kwa mtiifu. Hakika mali, elimu, na utawala ni neema kubwa anayowapa mtihani Mwenyezi Mungu kwayo waja wake.

Basi neema hiyo huwazidisha washari ukafiri na kupitua mipaka, lakini watu wazuri huifanya neema hiyo kuwa ni nyenzo ya kumtii Mwenyezi Mungu na kumridhisha, kama alivyofanya Dhul-qar- nain.

Kisha akafuata sababu, Yaani akafuata njia, Dhul-qarnain alirejea kutoka magharibi na akaelekea mashariki ambako Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekuashria kwa kauli yake:

Mpaka alipofika mawiyo ya jua aliona linawachomozea watu tusiowawekea sitara ya kuwakinga nalo.

Makusudio ya mawiyo ya jua hapa ni upande wa mashariki, na sitara ni jengo na mfano wake, kama hema, vibanda na mapango. Maana ni kuwa Dhul-qarnain alipowasili miji ya mashariki aliwakuta watu wanaishi kwenye nchi iliyo wazi ikifikiwa na jua, wakiishi maisha ya kiporini, kama wanyama.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa nchi hiyo ilikuwa ufuoni mwa Afrika mashariki, Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutaja alichofanya Dhul-qarnain huko; kuwa je alimfanyia wema mwenye kuamini na aka- tenda mema na kumwadhibu mwenye kunga’ang’ania ukafiri na inadi au aliwaacha kama walivyo? Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi.

Kama hivyo tulizijua vizuri habari zake.

Yaani hii ndiyo habari ya Dhul-qarnain, tunaijua yote.

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ بَيْنَ السَّدَّيْنِ وَجَدَ مِن دُونِهِمَا قَوْمًا لَّا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ قَوْلًا ﴿٩٣﴾

93. Hata alipofikia baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wakifahamu kauli.

قَالُوا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِنَّ يَأْجُوجَ وَمَأْجُوجَ مُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ فَهَلْ نَجْعَلُ لَكَ خَرْجًا عَلَىٰ أَن تَجْعَلَ بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمْ سَدًّا ﴿٩٤﴾

94. Wakasema: Ewe Dhul-qar-nain! Hakika Juju na Majuju wanafanya ufisadi katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?

قَالَ مَا مَكَّنِّي فِيهِ رَبِّي خَيْرٌ فَأَعِينُونِي بِقُوَّةٍ أَجْعَلْ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ رَدْمًا ﴿٩٥﴾

95. Akasema: Yale Mola wangu aliyoniwezesha ni bora. Lakini nisaidieni kwa nguvu nijenge kizuizi baina yenu na wao.

آتُونِي زُبَرَ الْحَدِيدِ حَتَّىٰ إِذَا سَاوَىٰ بَيْنَ الصَّدَفَيْنِ قَالَ انفُخُوا حَتَّىٰ إِذَا جَعَلَهُ نَارًا قَالَ آتُونِي أُفْرِغْ عَلَيْهِ قِطْرًا ﴿٩٦﴾

96. Nileteeni vipande vya chuma, Hata alipojaza baina ya nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vuvieni. Hata alipokifanya moto akasema: Nileteeni shaba iliyoyeyuka niimwagie.

فَمَا اسْطَاعُوا أَن يَظْهَرُوهُ وَمَا اسْتَطَاعُوا لَهُ نَقْبًا ﴿٩٧﴾

97. Hawakuweza kuukwea wala hawakuweza kuutoboa.

قَالَ هَـٰذَا رَحْمَةٌ مِّن رَّبِّي فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ رَبِّي جَعَلَهُ دَكَّاءَ وَكَانَ وَعْدُ رَبِّي حَقًّا ﴿٩٨﴾

98. Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu, Itakapofika ahadi ya Mola wangu atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu ni ya kweli.

وَتَرَكْنَا بَعْضَهُمْ يَوْمَئِذٍ يَمُوجُ فِي بَعْضٍ وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَجَمَعْنَاهُمْ جَمْعًا ﴿٩٩﴾

99. Na siku hiyo tutawaacha wakisongana. Na parapanda itapuziwa na wote watakusanywa pamoja.

وَعَرَضْنَا جَهَنَّمَ يَوْمَئِذٍ لِّلْكَافِرِينَ عَرْضًا ﴿١٠٠﴾

100. Na siku hiyo tutawaonyesha wazi makafiri Jahannam waione.

JUJU NA MAJUJU

Aya 93 – 100

MAANA

Kisha akafuata sababu.

Dhul-qarnaini alirejea mji wa tatu ulioko katika Bahari nyeusi, unaokaliwa na Slaves[2] -kama ilivyosemekana - ambao Mwenyezi Mungu ameuashiria kwa kauli yake:

Hata alipofikia baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wakifahamu kauli.

Watu aliowakuta huko walikuwa hawafahamu lugha yake wala hakufaamu lugha yao, lakini walielewana kwa ishara au kwa mkalimani; kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Wakasema: “Ewe Dhul-qar-nain! Hakika Juju na Majuju wanafanya ufisadi katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?

Sheikh Maraghi anasema katika Tafsir yake: “Juju ni wa Tatars, na Majuju ni wa Mongoli. Asili yao wanatokana na baba mmoja anayeitwa Turk. Miji yao inaanzia Tibet na China hadi kwenye Bahri iliyoganda. Miongoni mwao ni Changez Khan na Halako.

Kisha akanukuu Maraghi Jarida la Al-Muqtatif la mwaka 1888, kwamba jengo la ukuta wa Dhul-qarnain liko nyuma ya Amou–Daria sehemu za Balkh. Jina lake hivi sasa ni mlango wa chuma na liko karibu na mji wa Tirmidh.

Mtaalamu mmoja wa kijerumani Cyllid Burger, amelitaja katika safari zake zilizokuwa mwanzoni mwa karne ya 15. Vilevile amelitaja mwana historia wa Kihispania Clavijo katika safari zake za mwaka 1402 A.D.

Vyovyote iwavyo ni kwamba watu walimtaka Dhul-qarnain awajengee ngome itakayowakinga na Juju na Majuju waliokuwa wakiishambulia nchi yao, wakiwapa adhabu mbaya ya kuwaua, kuwateka na kupora. Wakajiwekea sharti la kumlipa katika mali zao ikiwa atawajenega ngome.

Akasema: Yale Mola wangu aliyoniwezesha na akanipa utawala na malini bora kuliko yale aliyowapa Mwenyezi Mungu. Nyinyi wenyewe mna haja kubwa ya mali yenu, basi itumieni kwenye masilahi yenu.

Lakini nisaidieni kwa nguvu nijenge kizuizi baina yenu na wao.

Makusudio ya nguvu hapa ni wafanyikazi na vifaa vya ujenzi.

Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipojaza baina ya nafasi iliyo kati ya milima miwili.

Yaani alipoletewa vyuma alivipanga mpaka vikajaza nafasi iliyo baina ya milima miwili, kisha wakamletea kuni akawasha moto akaweka mifuoakasema: Vuvieni. Hata alipokifanya (chuma)moto akasema: Nileteeni shaba iliyoyeyuka niimwagie.

Wakamletea, akamwagia kwenye vyuma vilivyo moto, vikashikana, ukawa mlima wa chuma.

Hawakuweza kuukwea hao Juju na Majuju, kutokana na urefu na kutelezawala hawakuweza kuutoboa kutokana na ugumu wake na maki yake.

Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu.

Aliyesema ni Dhul-qarnain, akimshukuru Mola wake (s.w.t) kwa rehema na neema hii aliyoitimiza mikononi mwake, Hivi ndivyo anavyokuwa mumin mwenye ikhlasi. Anamnyenyekea Mwenyezi Mungu na kushukuru kila zinapokuwa neema za Mwenyezi Mungu kupitia kwake.

Kujengwa kwa ngome hii ni usadikisho wa mfano kuwa katika historia ya binadamu kulikuwa na kusaidiana baina ya mataifa makubwa na yale madogo yanayoendelea; baina ya taifa lililo na nyenzo za maendeleo na lile lisilokuwa nazo.

Nguvu za Amerika zinafanana sana na nguvu za Dhul-qarnaini, kwa vile haziwezi kukabiliwa na yoyote, lakini kuna tofauti kubwa ya matokeo na natija. Wakati nguvu zote za Dhul-qarnain zilkuwa ni utawala wa kheri ya ubinadamu na ufanisi wake, lakini nguvu za Amerika ni za kuhami uovu wa uzayuni na kutawala nyenzo zote, masoko yote kwa masilahi ya ukoloni na kuwadumaza watu kwa kila namna.

Ushahidi wa hayo hauna idadi. Kuanzia kuusaidia uzayuni dhidi ya waarabu na ubaguzi wa rangi ndani ya Amerika hadi Rhodesia,[3] mapinduzi ya kijeshi katika nchi za kiafrika[4] na kuwapiga vita wapigania ukombozi huko Kongo na kila mahali, Ama huko Vietnam ndio haisemeki. Wamekusanya majeshi na kutumia kila walicho nacho, lakini ukakamavu wa wananchi wa Vietnam umetoa somo kwa Amerika, ambalo hawatalisahau maisha.

Kwa hiyo kila ushindi wanaoupata Amerika wajue huo ni wa muda tu, utaondoka kwa upinzani wa wananchi ambao unazidi siku baada ya siku.

Itakapofika ahadi ya Mola wangu atauvunja vunja.

Yaani huo mlima atauvunja vunja, Maana ni kuwa utakapokurubia wakati wa kutokea Juju na Mjuju nyuma ya ukuta, Mwenyezi Mungu ataleta sababu za kuvunjika kwake.

Na ahadi ya Mola wangu ni kweli haina shaka.

Shekh Maraghi anasema: “Ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ilifika kwa kutoka Changez Khan wakafanya ufisadi katika ardhi”.

Katika Tafsir Ar-Razi imeelezwa kuwa maana ya ahadi hapa ni siku ya Kiyama. Katika Tafsir At-Twabariy imeelezwa ni baada ya kuuliwa Dajjal.

Ama sisi tunapondokea kwenye kauli ya Maraghi, kwa sababu iko karibu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao.

Kwani tunafahamu kuwa Juju na Majuju wataenea katika ardhi baada ya kuharibika ngome na wataharibu maisha ya watu. Mwenyezi Mungu anasema:

حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُم مِّن كُلِّ حَدَبٍ يَنسِلُونَ ﴿٩٦﴾

“Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima.” (21:96).

Zaidi ya hayo ni kwamba lau ingelikuwa makusudio ya ahadi yake ni Kiyama au baada ya kufa Dajjal, ingelikuwa ngome bado ipo; na kama ipo basi ingelionekana, hasa kwa kuzingatia kuwa elimu imefanya dunia hivi sasa, pamoja na wakazi wake, ni kama familia moja inayoishi kwenye nyumba moja.

Na parapanda itapuziwa na wote watakusanywa pamoja.

Hii ndiyo siku ya mwisho kwa wale wa mwanzo na wa mwisho. Katika Tafsir Attwabariy imeelezwa kuwa Mtume(s.a.w.w) aliulizwa kuhusu Parapanda, akasema ni pembe itakayopuziwa.

Baada ya hayo yote, tunapenda kujulisha kuwa tuliyoyaeleza au kuyanukuu kutoka kwa wengine kuhusiana na Juju na Majuju, ni kwa njia ya kuleta karibu ufahamisho sio uhakika hasa.

Kwa vile hatukupata rejea za kutegemewa; Kwa sababu hiyo basi tutuatosheka na dhahiri ya Qur’an Tukufu na kuwaachia ufafanuzi wenzetu wengine.

الَّذِينَ كَانَتْ أَعْيُنُهُمْ فِي غِطَاءٍ عَن ذِكْرِي وَكَانُوا لَا يَسْتَطِيعُونَ سَمْعًا ﴿١٠١﴾

101. Wale ambao macho yao yalikuwa kwenye pazia ya kunitaja, Na wakawa hawawezi kusikia.

أَفَحَسِبَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن يَتَّخِذُوا عِبَادِي مِن دُونِي أَوْلِيَاءَ إِنَّا أَعْتَدْنَا جَهَنَّمَ لِلْكَافِرِينَ نُزُلًا ﴿١٠٢﴾

102. Je, wanadhani waliokufuru kuwafanya waja wangu ndio walinzi badala yangu? Hakika sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ni mashukio ya makafiri.

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾

103. Sema: je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo?

الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾

104. Ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kuwa wanafanya kazi nzuri?

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَلِقَائِهِ فَحَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا ﴿١٠٥﴾

105. Hao ndio ambao wamezikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye; Kwa hiyo vitendo vyao vimepomoka; nawala siku ya Kiyama hatutawapa uzito wowote.

ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُمْ جَهَنَّمُ بِمَا كَفَرُوا وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَرُسُلِي هُزُوًا ﴿١٠٦﴾

106. Hiyo Jahanamu ndiyo malipo yao kwa walivyokufuru na wakazifanyia kejeli ishara zangu na Mitume wangu.

JAHANNAMU NA WALIOHASIRIKA

Aya 101 – 106

MAANA

Na siku hiyo tutawaonyesha wazi Jahannam makafiri waione.

Wenye makosa, kesho, watashuhudia kwa macho yao Jahannam kabla ya kuingizwa humo, ili wachomeke kwa aina mbili za moto: Moto wa hofu na moto wa kuungua.

Wale ambao macho yao yalikuwa kwenye pazia ya kunitaja.

Kutajwa huwa kunasikiwa na masikio. Kwa hiyo hapa maana ya pazia ya macho ni mfundo wa makafiri kwa Mtume na waumini, na kwamba wao walikuwa hawawezi kumwangalia Mtume(s.a.w.w) wala waumini.

Na wakawa hawawezi kusikia utajo wa Mungu kutoka kwa Mtume wake Mtukufu.

Kwa maneno mengine ni kuwa wakosefu hawawezi kusikiza haki wala kuwatazama watu wa haki. Haya ndiyo tunayoyashuhudia kwa macho, ikiwa ni matokeo ya mzozo baina ya haki na batili na kheri na shari.

Je wanadhani waliokufuru kuwafanya waja wangu ndio walinzi badala yangu?

Makusudio ya waja wangu hapa ni viumbe ambao washirikina wali- wafanya ndio walinzi wao badala ya Mwenyezi Mungu. Hapa kuna maneno yanayokadiriwa kuwa: Je, wana dhani hawa kuwa tumeghafilika nao?Hapana! Hakika sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ni mashukio ya makafiri.

Mashukio ni mahali anapoandaliwa mgeni, vile vile linatumika neno hilo kwa maana ya nyumba. Maana ni kuwa tumewaandalia Jahannam kuwa ndio tosha yao. Hii ni sawa na kumwambia yule unayemdharau: unadhani mimi sikuwezi wewe nawe ni kama hiki kiatu?

THAMANI YA MTU

Sema je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo? Ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kuwa wanafanya kazi nzuri?

Ufupi wa maana ni kuwa mwenye hasara zaidi katika watu na mwenye kuhangaika bure, ni yule mjinga sana anayeuona ujinga wake kuwa ni elimu, shari yake kuwa ni kheri na uovu wake kuwa ni wema.

Hapana mwenye shaka kuwa huyo ni mwenye hasara duniani, kwa vile yeye anaishi asivyokuwa. Vile vile huko akhera, kwa vile atakutana na Mola wake akiwa na ujinga, ghururi na matendo maovu. Aya inaashiria kuwa thamani ya mtu haiwezi kupimwa kwa kuiona yeye mwenyewe; Kwa sababu mgomvi hawezi kujihukumu. Wala pia haiwezi kupimwa kwa mtazamo wa watu.

Ispokuwa mtu hupimwa kwa kipimo cha Qur’an na misingi yake na kushikamana na mafunzo yake na hukumu zake. Hupimwa kwa ukweli na uadilifu, kuinusuru haki na watu wake na kujitolea kwa hali na mali. Qur’an imejaa aina nyingi za mafunzo haya; kama vile kauli zake Mwenyezi Mungu Mtukufu zifuatazo: “...Na kuweni pamoja na wa kweli” Juz; 11 (9:119)

قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ ﴿١٣٥﴾

“....Kuweni Imara kwa uadilifu” Juz;. 5 (4:135)

كُونُوا أَنصَارَ اللَّـهِ ﴿١٤﴾

“...Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu (61:14)

كُونُوا رَبَّانِيِّينَ ﴿٧٩﴾

“...Kuweni watumishi wa Mwenyezi Mungu”Juz.3 (3:79)

وَجَاهِدُوا بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾

“...Na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu Juz.10 (9:41)

إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ﴿١٣﴾

“Hakika mtukufu wenu zaidi, kwa Mwenyezi Mungu, ni yule mwenye takua zaidi katika nyinyi” (49:13)

Unaweza kuuliza : Mkosaji anaweza kujiona kuwa amepatia na kwamba amefanya vizuri. Je atakuwa ni miongoni mwa waliohasirika; pamoja na kujua kuwa hakuna mwenye isma (kuhifadhiwa na madhambi) isipokuwa yule mwenye isma?

Jibu : Wenye kukosea wako aina mbili: Wa kwanza ni yule mwenye kukosea baada ya kutafiti na kuhakikisha; sawa na wanavyofanya wale wanaojitahidi, kiasi ambacho natija inayopatikana inaweza kuwa sawa na ya mtaalmu.

Hapana mwenye shaka kuwa mkoseaji huyu hawezi kuwa ni katika wale ambao juhudi zao zimepotea bure, au kuwa ni aibu ukoseaji wake; bali huyu analipwa thawabu kutokana na juhudi yake; kama ilivyoelezwa katika Hadith. Lakini kwa sharti awe na nia ya kujikosoa, yatakapofichuka makosa.

Aina ya pili, ni kukosea kulikotokana na kujiamini kwa juujuu, kulikotokana na mawazo, bila ya kufanya utafiti, kwa vile hajui misingi ya utafiti na elimu, Au anaweza kuwa anaijua, lakini asiitumie au aitumie nusunusu, aitumie kabla ya kuikamilisha. Huyu ndiye aliye miongoni mwa wale waliopata hasara katika kazi zao, hilo halina shaka. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ameamrisha kuwa na mazingatio na uthabiti na akakataza pupa na kusema bila ya ujuzi.

Baada ya hayo somo tunalolipata kutokana na Aya hii, ni kuwa tusijidanganye, tukajipa sifa tusizo nazo wala kujidanganya kwa maneno.

Vile vile ni wajibu tujihisabu nafsi zetu zinapokuwa na ghururi na kujitukuza, kabla hajatuhisabu Mwenyezi Mungu na watu. Pia rai zetu na kauli zetu tusizione kuwa ndio sawa mia kwa mia. Makosa yanatokea kwa yeyote.

Hao ndio ambao wamezikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye.

Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa makusudio ya wale waliokanusha ishara za Mola wao na kukutana naye ndio wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure; ni sawa wawe wameamini ufufuo au wameukanusha. Linalozingatiwa ni imani na matendo kwa pamoja; sio imani peke yake.

Kwa hiyo vitendo vyao vimepomoka na wala siku ya kiyama hatutawapa uzito wowote.

Yaani hatutawathamini, kwa sababu hakuna heshima mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa yule mwenye takua.

Hiyo Jahanamu ndiyo malipo yao kwa walivyokufuru na wakazifanyia kejeli ishara zangu na Mitume wangu.

Walimkufuru Mwenyezi Mungu na wakaifanyia masikhara haki na watu wake. Moto ndio mwisho na ukomo wa ufisadi na upotevu.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَانَتْ لَهُمْ جَنَّاتُ الْفِرْدَوْسِ نُزُلًا ﴿١٠٧﴾

107. Hakika wale ambao wameamini wakatenda mema, mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.

خَالِدِينَ فِيهَا لَا يَبْغُونَ عَنْهَا حِوَلًا ﴿١٠٨﴾

108. watadumu humo; hawatataka kuondoka.

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا ﴿١٠٩﴾

109. Sema: Lau bahari ingelikuwa ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingemalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tungeleta mfano wake kuongezea.

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

110. Sema: hakika mimi ni binadamu kama nyinyi tu, nimeletewa wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu mmoja. Mwenye kutarajia kukutana na Mola wake, basi na atende matendo mema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake.

WALIOAMNI NA WAKATENDA MEMA

Aya 108 – 110

MAANA

Hakika wale ambao wameamini wakatenda mema, mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwahidi makafiri moto, sasa anatoa ahadi ya Pepo kwa waumini. Firdausi ni katika Pepo ya daraja ya juu. Mtume Mtukufu(s.a.w.w) amesema: “Mkimuomba Mwenyezi Mungu muombeni Firdausi.”

Watadumu humo; hawatataka kuondoka.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawalipa wema yale ambayo hawatataka mengine, tosha kabisa! Yanatosheleza yote wanayoyataka. Aya inaashiria kuwa hakuna tamaa huko Akhera; vinginevyo ingelikuwa hakuna kutosheka. Kwani mwenye tamaa hatosheki.

Sema: Lau bahari ingelikuwa ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingemalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tungeleta mfano wake kuongezea.

Bahari ni jina la jinsi, linaenea kwenye bahari zote. Makusudio ya kabla ya kumalizika maneno, ni kuwa hayamaliziki na mfano wake ni mfano wa bahari. Maana ni kuwa lau tuchukulie kuwa bahari zote ni wino wa kuandika maneno ya Mwenyezi Mungu zisingetosha na maneno ya Mwenyezi Mungu yangelibakia bila ya kikomo.

Aya nyingine yenye maana hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na lau miti yote iliyomo ardhini ikawa ni kalamu na bahari (ikawa wino) na ikaongezewa bahari nyingine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelimalizika.” (31:27).

Makusudio ya maneno ya Mwenyezi Mungu hapa sio matamshi yanayotokana na herufi wala si amri ya kitendo inayotokana na ibara ya ‘kuwa na kikawa,’ kwa sababu amri hii haiingii kwenye mahisabu: “Na amri haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.” (54:51).

Isipokuwa makusudio ya maneno yake hapa, ni kuweza kuvileta vitu vyote, wakati wowote atakao; ni sawa iwe ni kwa kuviambia kuwa na vikawa au aviambie muda ujao, wa karibu au mbali. Uwezo huu hauna kikomo wala mwisho, lakini bahari, miti na mifano yake ina kikomo; na kila chenye kikomo kinakwisha.

Kwa maneno mengine ni kuwa kila kitu kilichopo kitakwisha na kukoma, isipokuwa uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kukifanya hicho kitu utabakia.

Tutaifafanua zaidi fikra hii kwa mfano huu: Mtu akiwa na maarifa ya kilimo, maarifa yake haya atakuwa nayo tu wakati wote atakaokuwa hai, lakini kile atakochokilima kitaisha. Uweza wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hauishi kwa vile hauna kikomo ni wa milele, lakini viumbe vyake vimepatikana na kila chenye kupatikana kina mwisho.

Sema: Hakika mimi ni binadamu kama nyinyi tu, sina tofauti na nyinyi isipokuwanimeletewa wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu mmoja.

Ibn Abbas anasema: “Mwenyezi Mungu, kwa Aya hii, amemfundisha Mtume wake unyenyekevu, akamwamrisha aseme yeye mwenyewe kuwa ni binadamu kama wengine, isipokuwa Mwenyezi Mungu amemtukuza kwa wahyi.”

Nasi tunaongezea kauli ya Ibn Abbas: Na ili waislamu wasimfanye Muhammad(s.a.w.w) kama wanaswara (wakristo) walivyomfanya Isa(a.s) .

Mwenye kutarajia kukutana na Mola wake, kwa hisabu, thawabu na adhabu,basi na atende matendo mema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake.

Kila mwenye kufanya amali kwa ajili ya mwengine atakuwa amemshirikisha Mwenyezi Mungu kwenye ibada; ni sawa aseme waungu ni wengi au asiseme.

Tofauti ni kuwa kauli ni shirki ya waziwazi na riya ni shirki ya kificho. Kuna Hadith inayosema:

“Mwenye kuswali kwa riya amefanya shirki na mwenye kufunga kwa riya amefanya shirk”

Fananisha mengine kwenye swala na saumu.

MWISHO WA SURA YA KUMI NA NANE