TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA Juzuu 16

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10618
Pakua: 2682


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10618 / Pakua: 2682
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA Juzuu 16

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

Sura ya Kumi na Tisa: Surat Maryam. Imeshuka Makka ina Aya 98.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu.

كهيعص ﴿١﴾

1. Kaaf Haa Yaa A’yn Swaad.

ذِكْرُ رَحْمَتِ رَبِّكَ عَبْدَهُ زَكَرِيَّا ﴿٢﴾

2. Huu ni ukumbusho wa rehema ya Mola wako kwa mja wake Zakariya.

إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا ﴿٣﴾

3. Alipomuomba Mola wake kwa siri.

قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا ﴿٤﴾

4. Akasema: Mola wangu! Mfupa wangu umedhoofika, na kichwa kiname remeta kwa mvi. Mola wangu! Sikuwa mwenye bahati mbaya kwa kukuomba wewe.

وَإِنِّي خِفْتُ الْمَوَالِيَ مِن وَرَائِي وَكَانَتِ امْرَأَتِي عَاقِرًا فَهَبْ لِي مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا ﴿٥﴾

5. Na Mimi nahofia jamaa zangu baada yangu na mke wangu ni tasa, Basi nipe mrithi kutoka kwako.

يَرِثُنِي وَيَرِثُ مِنْ آلِ يَعْقُوبَ وَاجْعَلْهُ رَبِّ رَضِيًّا ﴿٦﴾

6. Atakayenirithi mimi na arithi ukoo wa Ya’qub, Ewe Mola wangu mjaaliye mwenye kuridhisha.

ZAKARIYA

Aya 1-6

MAANA

Kaaf Haa Yaa A’yn Swaad.

Umetangulia mfano wake pamoja na tafsiri katika Juz. 1, mwanzo wa Sura Baqara

Huu ni ukumbusho wa rehema ya Mola wako kwa mja wake Zakariya.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamsimulia Mtume wake mtukufu, katika Aya hizi, jinsi alivyompa rehema Zakariya na akamneemesha kwa mtoto wake Yahya. Zakariya anatokana na kizazi cha Suleiman bin Daud. Alimuoa khalat (mama mdogo) wa Maryam. Naye alikuwa ni mlezi wa Maryam, Yametangulia maelezo ya hayo katika Juz; 3 (3:38), Inasemekana kuwa Zakriya alikuwa seremala.

Alipomuomba Mola wake kwa siri Alimuomba Mola wake akiwa peke yake na akasema: Mola wangu! Mfupa wangu umedhoofika, na kichwa kinameremeta kwa mvi. Mola wangu! Sikuwa mwenye bahati mbaya kwa kukuomba wewe.

Zakariya alizeeka bila ya kuwa na mtoto, kwa hiyo akamnyenyekea Mola wake, akimshtakia udhaifu wake na uzee wake. Miongoni mwa aliyoyasema ni: “Mola wangu usiniache peke yangu na Wewe ndiye mbora wa wanaorithi” (21:89). Ninakuomba ewe Mola wangu, nikiwa na matarajio ya rehema yako bila ya kukata tamaa. Vipi nikate tamaa na hali hujawahi kuyaangusha matarajio yangu kwako.

Na mimi nahofia jamaa zangu baada yangu na mke wangu ni tasa. Basi nipe mrithi kutoka kwako atakayenirithi mimi na arithi ukoo wa Ya’qub, Ewe Mola wangu mjaaliye mwenye kuridhisha.

Neno la kiarabu ‘mawalii’ lililofasiriwa jamaa, lina maana ya ndugu wa upande wa baba. Kwa hiyo Zakariya akiwa mzee na mkewe akiwa tasa, alihofia kurithiwa na binamu zake ambao ni wana wa Israil. Inasemekena walikuwa ni waovu.

Na hilo si mbali kwa Waisrail, kuwa wakirithi watawafanyia uovu watu na kuwafanyia ufisadi kwenye dini yao na dunia yao. Pamoja na uzee wake Zakariya na utasa wa mke wake, bado alikuwa na mategemeo makubwa kwa muumba wake, ndio maana akamuomba amtimizie haja yake.

يَا زَكَرِيَّا إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ اسْمُهُ يَحْيَىٰ لَمْ نَجْعَل لَّهُ مِن قَبْلُ سَمِيًّا ﴿٧﴾

7. Ewe Zakariya! Hakika sisi tunakubashiria mwana, jina lake ni Yahya, hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake.

قَالَ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَكَانَتِ امْرَأَتِي عَاقِرًا وَقَدْ بَلَغْتُ مِنَ الْكِبَرِ عِتِيًّا ﴿٨﴾

8. Akasema: Ewe Mola wangu! Vipi nitakuwa na mwana na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimekwishafikia ukongwe katika uzee?

قَالَ كَذَٰلِكَ قَالَ رَبُّكَ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ وَقَدْ خَلَقْتُكَ مِن قَبْلُ وَلَمْ تَكُ شَيْئًا ﴿٩﴾

9. Akasema, ndio hivyo hivyo Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi. Na hakika nilikuumba wewe zamani na hukuwa kitu.

قَالَ رَبِّ اجْعَل لِّي آيَةً قَالَ آيَتُكَ أَلَّا تُكَلِّمَ النَّاسَ ثَلَاثَ لَيَالٍ سَوِيًّا ﴿١٠﴾

10. Akasema: Mola wangu nijaalie ishara. Akasema, ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima.

فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَأَوْحَىٰ إِلَيْهِمْ أَن سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيًّا ﴿١١﴾

11. Akawatokea watu wake kutoka mihirabuni, akawaashiria kuwa mumsabihi asubuhi na jioni.

BISHARA YA YAHYA

Aya 7 – 11

MAANA

Ewe Zakariya! Hakika sisi tunakubashiria mwana, jina lake ni Yahya, hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake.

Mwenyezi Mungu aliitikia dua ya Zakariya na akampa habari njema ya kuzaliwa mtoto wa kiume, na kwamba Mwenyezi Mungu amemuita Yahya akiwa bado yuko kwenye uti wa mgongo wa baba yake. Na hakuna aliyewahi kuitwa jina hilo kabla yake. Inasemekana Yahya ndiye Yohana amabye ni maarufu kwa wakiristo kwa jina la Yohana mbatizaji).

Akasema: “Ewe Mola wangu! Vipi nitakuwa na mwana na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimekwishafikia ukongwe katika uzee?

Kusema hivi sio kuona kuwa haiwezekani, bali ni kuadhimisha na kushukuru neema za Mwenyezi Mungu na uweza wake ambao umekiuka desturi na mazoweya. Yeye ni mzee na mkewe ni tasa tena ni mzee, lakini pamoja na yote hayo Mwenyezi Mungu amemneemesha kupata mtoto.

Akasema: ndio hivyo hivyo Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi. Na hakika nilikuumba wewe zamani na hukuwa kitu.

Anayesema kauli zote mbili ni mmoja, naye ni Mwenyezi Mungu. yaani Mwenyezi Mungu anamwambia Zakariya kuwa Mola wako amesema. Desturi hii wanaitumia watungaji wengi wa kiislamu.

Mtu anaweza kusema: “Amesema Muhammad yeye ni Bin Malik” akijikusudia yeye Mwenyewe. Mfano mwingine ni wa Tabariy akijizungumzia yeye mwenyewe: “Amesema Abu Jafar Muhammad bin Jarir At-Tabariy”

Aliposema Mwenyezi Mungu haya kwangu ni mepesi, ni kuwa kwa Mungu hakuna kitu chochote kilicho kigumu. Vitu vyote kwake ni sawa tu; hahitajii isipokuwa neno ‘Kuwa’

Akasema: Mola wangu nijaalie ishara. Akasema, ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima. Akawatokea watu wake kutoka mihirabuni, akawaashiria kuwa mumsabihi asub- uhi na jioni.

Makusudio ya kuwaashiria ni kuwaashiria kwa mkono wake au kwa maandishi, kwa sababu yeye amezuiliwa kuzungumza, Umetangulia ufafanuzi wake katika Juz; 3 (3:41).

يَا يَحْيَىٰ خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ وَآتَيْنَاهُ الْحُكْمَ صَبِيًّا ﴿١٢﴾

12. Ewe Yahya! Kishike kitabu kwa nguvu, Na tulimpa hukumu angali mtoto.

وَحَنَانًا مِّن لَّدُنَّا وَزَكَاةً وَكَانَ تَقِيًّا ﴿١٣﴾

13. Na tukampa huruma itokayo kwetu na utakaso na alikuwa ni mwenye takua.

وَبَرًّا بِوَالِدَيْهِ وَلَمْ يَكُن جَبَّارًا عَصِيًّا ﴿١٤﴾

14. Na mwema kwa wazazi wake wala hakuwa jeuri muasi.

وَسَلَامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا ﴿١٥﴾

15. Na amani iwe juu yake, siku alipozaliwa na siku atakapokufa na siku atakapofufuliwa.

YAHYA

AYA 12 – 15

MAANA

Ewe Yahya!

Kauli hii inaelezea moja kwa moja kuwa Yahya amekwishazaliwa, amekuwa na akili ya kufahamu na kutia maanani na ana uwezo wa kutumia Tawrat ambayo ndiyo aliyoikusudia Mwenyezi Mungu aliposema:

Kishike kitabu kwa nguvu.

Maana ya kukishika kwa nguvu ni kukitumia kwa bidii na ikhlasi. Kisha akamsifu Yahya kwa sifa zifuatazo:

Na tulimpa hukumu angali mtoto na tukampa huruma itokayo kwetu na utakaso na alikuwa ni mwenye takua na mwema kwa wazazi wake wala hakuwa jeuri muasi.

Makusudio ya kupewa hukumu udogoni ni kujua dini mapema udogoni. Hii ni neema Mwenyezi Mungu aliyomhusisha nayo Yahya; kama alivyomhusisha kwa kuzaliwa na wazazi wazee. Mwenyezi Mungu humhusisha kwa rehema yake amtakaye. Baadhi ya riwaya zinasema kuwa siku moja watoto walimwambia Yahya: “Twendeni tukacheze.” Yahya akasema: “Hatukuumbwa kwa ajili ya kucheza, twendeni tukaswali.”

Makusudio ya upole ni upole kwa waja. Utakaso ni utwahara na utakatifu. Takua ni kumtii Mwenyezi Mungu. Kuwatendea wema wazazi wawili ni kinyume cha kuwaudhi.

Kauli yake Mwenyezi Mungu:Wala hakuwa ni jeuri muasi ni kuunganisha kwa kufafanua. Kwa sababu Mwenye utakaso na takua hawezi kuwa jeuri muasi.

Na amani iwe juu yake, siku alipozaliwa na siku atakapokufa na siku atakapofufuliwa

Hili ni fumbo la kuwa Yahya ni Mwenye kuridhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu duniani na Akhera. Ilivyo ni kuwa kumridhia kwake Yahya (a.s.) ni matokeo ya sifa alizomsifu nazo Mwenyezi Mungu.

Unaweza kuuliza : Kwanini Mwenyezi Mungu amemuhusisha Yahya na sifa hizi tele akiwa bado angali mdogo?

Jibu : Hakika Mwenyezi Mungu ana mambo yake kwa viumbe vyake. Anaweza akampa fadhila mdogo na akamnyima mkubwa. Na kila kutoa kwake na kuzuia kwake kuna hekima ambayo akili inaweza kujua na isiweze kujua. Lakini akili huwa inajaribu; kama ifuatavyo:

Sio mbali kuwa makusudio ya kusifika Yahya na sifa hizi katika rika hilo ni kutoa hoja kwa Wana wa Israil, watakapohitilafiana naye na wasikilize nasaha zake na mwito wake, Alimuumba Isa bila ya baba, “ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu na rehema itokayo kwetu” Itakuja Aya hii sehemu inayofuatia hii.

Pamoja na hoja hii ya kunyamazisha, lakini bado walimuasi Yahya na wakamfanyia uadui; mwisho wakamuua yeye na baba yake, si kwa lolote isipokuwa ni kwa kuwakataza mabaya. Hili si ajabu kwa yule aliyesema kuwa mikono ya Mwenyezi Mungu imefunga au Mungu ni fukara na sisi ni matajiri. Rudia Juz. 6 (5:64).

Katika kitabu Qasasul-anbiya (Visa vya mitume) imeelezwa kuwa Herod mfalme wa Palestina, wakati huo, alimpenda Herodias, binti wa kaka yake, kutokana na uzuri wake, na akataka kumuoa. Yahya alipopinga hilo

Herodias alichukia na akatoa sharti kwa ami yake kuwa mahari yake yawe kichwa cha Yahya. Kwa hiyo Mfalme akamchinja Yahya na akampelekea mpenzi wake zawadi hiyo ya kichwa.

Kuna riwaya mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Ali bin Husein bin Ali(a.s) kwamba baba yake, alipokuwa akielekea Iraq, alikuwa akimkumbuka sana Yahya na akisema: “Ni katika utwevu wa dunia kwa Mwenyezi Mungu, kwamba kichwa cha Yahya bin Zakariya kitolewe zawadi kwa kahaba miongoni mwa makahaba wa ki bani Israil.”

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ مَرْيَمَ إِذِ انتَبَذَتْ مِنْ أَهْلِهَا مَكَانًا شَرْقِيًّا ﴿١٦﴾

16. Na mtaje Maryam katika Kitabu, alipojitenga na watu wake mahali upande wa mashariki.

فَاتَّخَذَتْ مِن دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا ﴿١٧﴾

17. Na akaweka pazia kujikinganao, Tukampelekea roho wetu, Akajifananisha kwake sawa na mtu.

قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَـٰنِ مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا ﴿١٨﴾

18. Akasema: Hakika mimi najilinda kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mwenye takua.

قَالَ إِنَّمَا أَنَا رَسُولُ رَبِّكِ لِأَهَبَ لَكِ غُلَامًا زَكِيًّا ﴿١٩﴾

19. Akasema: Mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu.

قَالَتْ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ وَلَمْ أَكُ بَغِيًّا ﴿٢٠﴾

20. Akasema: Nitakuwaje na mwana hali hajanigusa mtu yoyote wala mimi si malaya.”

قَالَ كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ وَلِنَجْعَلَهُ آيَةً لِّلنَّاسِ وَرَحْمَةً مِّنَّا وَكَانَ أَمْرًا مَّقْضِيًّا ﴿٢١﴾

21. Akasema; Ndivyo hivyo hivyo, Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi! Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu na rehema itokayo kwa kwetu. Nahilo ni jambo lililokwishapitishwa.

MARYAM

Aya 16-21

MAANA

Na mtaje Maryam katika Kitabu, alipojitenga na watu wake mahali upande wa mashariki, Na akaweka pazia kujikinga nao.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Maryamu alijitenga na watu na akawa peke yake upande wa mashariki na kaweka sitara baina yake na wao, kiasi ambacho hawamuoni wala yeye hawaoni wao.

Kwa nini Maryamu alijitenga? Je, ni kwa kuwa aliona mambo yanayomchukiza au ni kwa kujitenga kwa ajili ya kufanya ibada au ni kwa ajili ya jambo jengine? Je, makusudio ya mahali upande wa mashariki ni kunakotokea jua au ni mashariki ya Baytul-maqdis au ni upande wa mashariki wa nyumba ya watu wake. Pia je, ni aina gani ya pazia aliyoweka, ni ukuta au kibanda?

Hakuna kitu, katika Aya, kinachoashiria majibu ya maswali haya; Kwa sababu hayahusiani na itikadi wala maisha. Sio mbali kuwa Mwenyezi Mungu alimpa ilhamu ya kujitenga huko ili apewe habari na Jibril kuhusu kuzaliwa Isa(a.s) akiwa kando na watu.

Tukampelekea roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu

Makusudio ya roho wetu, ni Jibril. Alijifananisha na mtu kamili. Imeelezwa katika baadhi ya Tafsiri kwamba alikuja na umbo la mtu ili asimwogopeshe. Tafsiri nyingine inasema kuwa aliogopa na akafadhaika, kwa mshtukizo huu.

Mgeni ajitome ndani bila ya hodi na yeye yuko peke yake! Jambo la kushangaza, Kauli hii, ya pili, ina nguvu na usahihi zaidi ya ile nyingine, kwa dalili ya kuwa yeye alifazaika na akasema:

Hakika mimi najilinda kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ukiwa ni Mwenye takua.”

Yaani nataka hifadhi kwa Mwenyezi Mungu na shari yako ikiwa wewe unamwamini Yeye na hisabu yake na adhabu yake. Alimuhofisha na Mwenyezi Mungu, kwa sababu hakuwa na nyenzo nyingine yoyote ya kumzuia hapo alipo, isipokuwa hiyo. Vinginevyo yeye ana hifadhi ya Mwenyezi Mungu akiwa anamtegemea Yeye; ni sawa huyo anayemuhofisha ni mwenye takua au muovu.

Akasema: Mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu.” Akasema: Nitakuwaje na mwana hali hajanigusa mtu yoyote wala mimi si malaya?

Unanipa habari ya mtoto, vipi na kutoka wapi? Sina mume wala sijafanya uasharati.

Akasema: Ndivyo hivyo hivyo Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi! Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu na rehema itokayo kwetu. Na hilo ni jambao lililokwishapitishwa.

Roho mwaminifu alimwambia kuwa sababu za kuzaa, kwa Mungu, sio kuonana na mtu tu. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu anafanya vitu kwa sababu zake zilizozoeleka, vile vile anafanya vitu kwa neno ‘kuwa’ sawa na alivyofanya ulimwengu bila ya kitu chochote na Adamu bila ya baba wala mama.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alitaka azaliwe mtoto kuonyesha dalili wazi ya ukuu wa muumba na utume wa atakayezaliwa, awe ni rehema kwa ubi- nadamu na hoja ya kunyamazisha wana wa Issrail ambao walijaribu kumuua. Tumeyaeleza hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 3 (3: 45)

فَحَمَلَتْهُ فَانتَبَذَتْ بِهِ مَكَانًا قَصِيًّا ﴿٢٢﴾

22. Basi akachukua mimba yake akaondoka nayo mahali mbali.

فَأَجَاءَهَا الْمَخَاضُ إِلَىٰ جِذْعِ النَّخْلَةِ قَالَتْ يَا لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَـٰذَا وَكُنتُ نَسْيًا مَّنسِيًّا ﴿٢٣﴾

23. Uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: Laiti ningelikufa kabla ya haya nikawa mwenye kusahaulika kabisa.

فَنَادَاهَا مِن تَحْتِهَا أَلَّا تَحْزَنِي قَدْ جَعَلَ رَبُّكِ تَحْتَكِ سَرِيًّا ﴿٢٤﴾

24. Pakanadiwa kutoka chini yake kwamba usihuzunike; hakika Mola wako amejaalia chini yako kijito cha maji.

وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا ﴿٢٥﴾

25. Na litikise kwako shina la mtende utakuangushia tende freshi zilizo mbivu.

فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا ﴿٢٦﴾

26. Basi kula na kunywa na uburudishe jicho. Na pindi ukimuona mtu yeyote basi sema hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kufunga. Kwa hiyo leo sitasema na mtu.

MIMBA YA ISA

Aya 22 – 26

MAANA

Basi akachukua mimba yake akaondoka nayo mahali mbali

Inasemekana kuwa Jibril alimpulizia kwenye gauni lake, ikawa ndiyo sababu ya kushika mimba; Rejea ya kauli hii ni dhahiri ya Aya hii:

وَالَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهَا مِن رُّوحِنَا ﴿٩١﴾

“Na (mwanamke) aliyelinda tupu yake na tukampulizia katika roho yetu” (21:91)

وَمَرْيَمَ ابْنَتَ عِمْرَانَ الَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهِ مِن رُّوحِنَا ﴿١٢﴾

“Na Maryam Binti Imrani aliyelinda tupu yake na tukampulizia humo kutoka roho yetu,” (66:12).

Mara kwa mara tumeishiria kuwa Qur’an inajifasiri yenyewe; yaani Aya zinafasiri Aya nyingine. Kwa sababu chimbuko lake ni moja. Tukiangalia msingi huu tutafahamu, kwa ujumla wake wote kuwa makusudio ya kupulizia ni kuumba na kutengenezwa mimba, na makusudio ya Roho ni Isa mwenyewe; kama inavyofahamisha Aya hii: “Masih Isa bin Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na neno lake tu alilompelekea Maryam, na ni roho iliyotoka kwake.” Juz.6 (4:171)

Maana ya ‘neno lake’ ni neno ‘kuwa,’ambalo anaumbia nalo vitu. Na maana ya ‘alilompelekea Maryam’ ni kuwa Maryam au tumbo lake ndio mahali pa kuumbwa; Kwa ufafanuzi zaidi angalia huko. Kwa vyovyote ilivyo ni kwamba Maryam alipojihisi ana mimba alijitenga kando na watu wake kwa kuona haya.

Uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: Laiti ningelikufa kabla ya haya nikawa mwenye kusahaulika kabisa.

Haya ni maneno anayoyasema mtu yeyote anapozongwa na matatizo makubwa, anatamka kupunguza msongo wa moyo na huzuni yake.

Pakanadiwa kutoka chini yake kwamba usihuzunike; hakika Mola wako amejaalia chini yako kijito cha maji.

Yanayokuja akilini mwanzo, kutokana na mfumo wa maneno, ni kuwa aliyenadi ni Isa(a.s) na wala sio Jibril, kama wanavyodai wafasiri wengi. Kunadi huku ni miongoni mwa miujiza ya Isa; sawa na kuzaliwa na kufufua kwake wafu.

Isa aliendelea kumwambia mama yake:

Na litikise kwako shina la mtende utakuangushia tende freshi zilizo mbivu.

Inasemekana huo haukuwa msimu wa tende. Kwa hiyo kupatikana tende ilikuwa ni muujiza. Hili haliko mbali, kwa sababu kila kitu hapa ni muujiza tu na tamko lenyewe pia linafahamisha hivyo.

Basi kula tende na kunywa kutoka kwenye kijito na uburudishe jicho.

Yaani poa moyo kwa kupata mtoto mwenye kubarikiwa.

Na pindi ukimuona mtu yeyote na akakuuliza kuhusu mtoto,basi sema kwa ishara kuwahakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kufunga kwa kunyamaza, Hiyo ndiyo iliyokuwa Swaumu ya waisrail wakati huo.

Kwa hiyo leo sitasema na mtu.

Hapana haja ya ufafanuzi hapa, isipokuwa kufasiri matamshi, kwa sababu akili haina nafasi katika maudhui haya maadamu dhahiri ya maneno haigongani na hukumu ya kiakili katika maudhui haya; Tazama Juz; 3 (3:45–51) kifungu cha ‘Lisilowezekana kiakili na kidesturi.

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA

فَأَتَتْ بِهِ قَوْمَهَا تَحْمِلُهُ قَالُوا يَا مَرْيَمُ لَقَدْ جِئْتِ شَيْئًا فَرِيًّا ﴿٢٧﴾

27. Akaenda naye kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu.

يَا أُخْتَ هَارُونَ مَا كَانَ أَبُوكِ امْرَأَ سَوْءٍ وَمَا كَانَتْ أُمُّكِ بَغِيًّا ﴿٢٨﴾

28. Ewe dada wa Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu wala mama yako hakuwa kahaba.

فَأَشَارَتْ إِلَيْهِ قَالُوا كَيْفَ نُكَلِّمُ مَن كَانَ فِي الْمَهْدِ صَبِيًّا ﴿٢٩﴾

29. Ndipo Akashiria kwake, Wakasema: Tutamsemezaje aliye bado mdogo susuni?

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا ﴿٣٠﴾

30. Akasema: Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu amenipa Kitabu na amenifanya nabii.

وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾

31. Na amenijaalia ni mwenye popote pale niwapo. Na ameniusia Swala na Zaka muda wa kuwa niko hai.

وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا ﴿٣٢﴾

32. Na kumtendea mema mama yangu, Wala hakunifanya niwe jeuri muovu.

وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا ﴿٣٣﴾

33. Na amani iwe juu yangu, siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakay- ofufuliwa.

ذَٰلِكَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ قَوْلَ الْحَقِّ الَّذِي فِيهِ يَمْتَرُونَ ﴿٣٤﴾

34. Huyo ndiye Isa Mwana wa Maryam, kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.

مَا كَانَ لِلَّـهِ أَن يَتَّخِذَ مِن وَلَدٍ سُبْحَانَهُ إِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٣٥﴾

35. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu Kuwa na mwana, Yeye ametakasika! Anapolipitisha jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.

UMELETA KITU CHA AJABU

Aya 27 – 35

MAANA

Akaenda naye kwa jamaa zake amembeba.

Baada ya Maryam kuzaa, alimbeba mwanawe kwenda naye kwa watu wake, akiwa na utulivu bila ya kuwa na wasiwasi; kwani mimba ambayo ilikuwa ni sababu ya kutuhumiwa kwake, sasa ndiyo yenye ushahidi wa kweli wa usafi wake.

Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu kwa kudai kupata mimba bila ya kuguswa na mtu, huo ni uzushi.

Ewe dada wa Harun ! Huyu ni nduguye Musa, na yeye Maryam ni katika kizazi chao. Makusudio ya kumtaja ni kuwa asili yake ni watu wema na kwamba shina likiwa zuri matawi pia yanatakiwa yawe mazuri, sasa imekuwaje kutokewa na yaliyomtokea ambayo hakuna mfano aliyetokewa na hayo?

Baba yako hakuwa mtu muovu wala mama yako hakuwa kahaba.

Unafanana na nani wewe kwa kitendo chako hiki? Hawezi kufanya hivi ila binti wa muovu au wa mama muovu.

Ndipo akaishiria kwake

Yaani kwa mtoto aweze kushuhudia usafi wake naye ni mkweli zaidi ya wanaoshuhudia, kwa sababu anatamka kwa lugha ya Mwenyezi Mungu.

Wakasema kwa mshangao; Tutamsemezaje aliye bado mdogo susuni?

Lakini yule aliye susuni alianza kuwasemesha kabla wao hawajaanza na akasema:

Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu amenipa Kitabu na amenifanya ni nabii.

Yaani atanifanya ni nabii baadaye, kwa sababu kitoto kichanga hakiwezi kuongoza watu na kuwa ni hoja kwao. Ikiwa yeye mwenyewe hana majukumu kwa kauli yake wala vitendo vyake. Atawezaje kuwa na majukumu ya kufikisha risala ya Mwenyezi Mungu kwa waja wa Mwenyezi Mungu?

Huko nyuma tumesema kuwa alitumwa kuwa Mtume akiwa na miaka 30; na kwamba alizungumza utotoni ili kumsafisha mama yake na tuhuma ya zina na uchafu; si kwa kuwa alikuwa ni nabii aliyetumwa, Angalia kifungu ‘Isa na utume wa utoto’ katika Juz.7 (5:109 –111).

Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo.

Kila anayewanufaisha watu kwa namna moja au nyingine basi ni mweye kubarikiwa na kila mwenye kumdhuru mtu mmoja - sikwambii watu wengi- basi huyo ni muovu na mfisadi.

Na ameniusia Swala na Zaka muda wakuwa niko hai na kumtendea mema mama yangu.

Yeye mwenyewe anakiri utumishi na utiifu kwa Mungu na kukana kuwa ni Mungu, mwana wa Mungu au mshirika wake; kama wanavyodai wanaswara (wakristo).

Wala hakunifanya niwe jeuri muovu; kama wanavyodai mayahudi. Bali ni mja mwema na Mtume; kama wanvyoitakidi waislamu.

Na amani iwe juu yangu, siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa.

Umepita punde mfano wake katika Aya 15 ya sura hii.

Huyo ndiye Isa mwana wa Maryam, kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.

Hili ndilo neno la kweli, la kielimu na la kiadilifu, kuhusu Bwana Masih.

Sio mjeuri kama wanavyosema mayahudi; wala si Mungu, mwanawe au mshirika wake; kama wasemavyo wanaswara. Yeye ni Nabii anayefikisha risala ya Mola wake na ni mja miongoni mwa waja wake, anaswali na kutoa Zaka. Vile vile yeye ni mwenye kubarikia anayewanufaisha watu. Pia ni mnyenyekevu anayemfanyia wema mama yake.

Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Yeye ametakasika! Anapolipitisha jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa

Lau Mwenyezi Mungu angelikuwa na watoto wangelijifichia kheri zote na baraka na kuzizuia wengine wasizipate. Pia wangeharibu yale aliyoten- geneza vizuri baba na ulimwengu wangeliujaza shari na upotevu; sawa na wanavyofanya baadhi ya watoto wa viongozi siku hizi. Umepita mfano wake katika Juz. 3 (3:59) na katika Juz.15 (18: 111).

وَإِنَّ اللَّـهَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٣٦﴾

36. Na Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na Mola Wenu, Basi muabuduni, Hii ndio njia iliyonyooka.

فَاخْتَلَفَ الْأَحْزَابُ مِن بَيْنِهِمْ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِن مَّشْهَدِ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٣٧﴾

37. Lakini Makundi yakahitilafiana baina yao, Basi ole wao waliokufuru kuhudhuria siku iliyo kuu.

أَسْمِعْ بِهِمْ وَأَبْصِرْ يَوْمَ يَأْتُونَنَا لَـٰكِنِ الظَّالِمُونَ الْيَوْمَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٣٨﴾

38. Watasikia na wataona vizuri vilioje siku watakayotufikia! Lakini madhalimu leo wako katika upotofu uliodhahiri.

وَأَنذِرْهُمْ يَوْمَ الْحَسْرَةِ إِذْ قُضِيَ الْأَمْرُ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ وَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٩﴾

39. Na waonye siku ya majuto itakapopitishwa amri nao wamo katika ghafla wala hawaamini.

إِنَّا نَحْنُ نَرِثُ الْأَرْضَ وَمَنْ عَلَيْهَا وَإِلَيْنَا يُرْجَعُونَ ﴿٤٠﴾

40. Hakika sisi tutairithi ardhi na walio juu yake na kwetu sisi wata rejeshwa.

NJIA ILIYONYOOKA

Aya 36 – 40

MAANA

Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni, Hii ndio njia iliyonyooka.

Aya hii inaungana na kauli ya Isa (hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu...) anawaamuru, kwenye kauli hii, wamwabudu Mungu mmoja wala wasimshirikishe na kitu chochote na kwamaba dini ya tawhid (kumpwekesha Mungu) ndio njia iliyo sawa; mwenye kuifuata ataokoka na mwenye kuiacha atapotea.

Lakini makundi yakahitilafiana baina yao.

Makundi hayo ni kaumu ya Isa. Kuna kundi lililosema kuwa Isa ni Mungu alishuka ardhini kisha akapanda mbinguni, kundi la pili likasema kuwa ni mwana wa Mungu na kundi la tatu likasema ni mja wa Mwenyezi Mungu. Tofauti ilikuwepo hapo zamani, lakini hivi sasa makundi yote yameafikiana kuwa Isa ni Mungu.

Basi ole wao waliokufuru kuhudhuria siku iliyo kuu

Makusudio ya waliokufuru hapa ni kundi la kwanza na la pili. Aya hii ni ibara nyingine ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ ﴿٢٧﴾

“Hiyo ni dhana ya waliokufuru ole wao waliokufuru na moto.”(38:27).

Watasikia na wataona vizuri vilioje siku watakayotufikia!

Makafiri watakapoiona adhabu siku ya Kiyama watasema:

رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ ﴿١٢﴾

“Mola wetu! Tumeshaona na tumeshasikia, Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwishakuwa na yakini”(32:12).

Walipokuwa wakilinganiwa kwenye haki walikuwa wakisema:

قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ ﴿٥﴾

“Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayotuitia na masikio yetu yana uziwi” (41:5)

Lakini madhalimu leo wako katika upotofu ulio dhahiri.

Makusudio ya leo hapa, ni siku ya Kiyama; na upotofu ni adhabu, kwa vile siku hiyo hakutakuwa na njia ya uongofu wala upotofu; bali ni hisabu na malipo, hakuna zaidi ya hivyo.

Na waonye siku ya majuto itakapopitishwa amri nao wamo katika ghafla wala hawaamini

Anaaambiwa Mtume(s.a.w.w) awaonye, Siku ya majuto ni Kiyama. Imeitwa hivyo kwa sababu nafsi yenye hatia siku hiyo itasema:

يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ ﴿٥٦﴾

“Ee majuto yangu kwa yale niliyoyapoteza upande wa Mwenyezi Mungu na hakika nilikuwa miongoni mwa wanofanya maskhara.”(39:56).

Amri itapitishwa siku hiyo ambapo hakutakuwa na kubatilika wala kurejea. Wao hivi sasa wameghafilika, kwani wanaweza kujirudi kufuru yao na upotevu wao, wamuombe Mwenyezi Mungu msamaha, lakini wao hawafanyi, na wameendelea na uasi wao.

Kauli yake Mwenyezi Mungu:wala hawaamini, ni kuwa wao hawaisadiki kauli yetu, kwamba wao watafufuliwa, bali wanapeta vichwa vyao huku wakifanya maskhara.

Hakika sisi tutairithi ardhi na walio juu yake na kwetu sisi watarejeshwa.

Ardhi na vilivyomo ni vya Mwenyezi Mungu, hakuna yeyote mwenye kumiliki kitu. Binadamu ni mpita njia tu. Na kila kilicho mikononi mwa mtu ni cha kuazimwa tu, ana majukumu na kuwajibika nacho ili ahisabiwe kwacho.

Kwa ufupi Aya hii inarudufu neno: “Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na Kwake Yeye tutarejea.” Juz. 2 (2:156). Makusudio yake ni kumhadharisha muasi, kumkemea na kupunguza huzuni ya Mtume(s.a.w.w) na uchungu wake kwa kupingwa mwito wake.

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِبْرَاهِيمَ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَّبِيًّا ﴿٤١﴾

41. Na mtaje Ibrahi mkatika Kitabu hakika yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا ﴿٤٢﴾

42. Alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini Unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa na chochote.

يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا ﴿٤٣﴾

43. Ewe baba yangu! Hakika imenifikia elimu isyokufikia wewe, Basi nifuate mimi nitakuongoza njia iliyo sawa.

يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ عَصِيًّا ﴿٤٤﴾

44. Ewe baba yangu! Usiabudu Shetani. Hakika shetani ni Mwenye kumuasi Mwingi wa rehema.

يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا ﴿٤٥﴾

45. Ewe baba yangu! Mimi nakuhofia isikupate adhabu ya Mwingi wa rehema ukawa ni walii washetani.

قَالَ أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾

46. Akasema: Unaichukia miungu yangu ewe Ibrahim! Kama hutakoma, Basi lazima nitakupiga mawe na niondokelee mbali kwa muda.

قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾

47. Akasema Ibrahim: Amani iwe juu yako (salamun alayka)! Nitakuombea msamaha kwa Mola wangu Hakika yeye ananihurumia sana.

وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾

48. Nami na ajitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyez Mungu na ninamuomba Mola wangu asaa nisiwe na bahati mbaya.

فَلَمَّا اعْتَزَلَهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَكُلًّا جَعَلْنَا نَبِيًّا ﴿٤٩﴾

49. Alipojitenga nao na yale wanayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimpa Is-haq na Ya’qub na kila mmoja tukamfanya nabii.

وَوَهَبْنَا لَهُم مِّن رَّحْمَتِنَا وَجَعَلْنَا لَهُمْ لِسَانَ صِدْقٍ عَلِيًّا ﴿٥٠﴾

50. Na tukawapa katika rehema zetu na tukawajaalia kuwa na sifa za kweli tukufu.

IBRAHIM

Aya 41-50

MAANA

Na mtaje Ibrahim katika Kitabu hakika yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.

Makusudio ya Kitabu hapa ni Qur’an. Ukweli ni sifa bora na ya ukamilifu zaidi. Tunalolifahamu kutokana na wasifu wa utume baada ya ukweli, ni kuwa yeye kwa maumbile yake ni mkweli hata kama si mtume.

Katika Juz; 7: (6:74) tumetaja tofauti za maulama katika makusudio ya baba wa Ibrahim, aliyetajwa katika Qur’an, kuwa je, ni baba yake wa hakika au ni baba wa kimajazi au ni ndugu wa baba? Tukasema huko, kuwa hakuna faida ya mzozo huu na kwamba lililo wajib kwa mwislamu ni kuamini utume wa Ibrahim(a.s) . Ama kuitakidi uislamu wa baba yake hilo halihusiani na dini; hasa kwa kuwa dhahiri ya Qur’an inafahamisha ukafiri wake.

Kwa vyovyote iwavyo, ni kuwa Ibrahim alimpa mwito baba yake, awe wa kimajazi au wa kihakika, wa uislamu na akamwambia katika yale aliyomwambia:

Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa na chochote?

Baba yake alikuwa akiabudu masanamu, kwa hiyo akamuhoji kwa manti- ki ya kiakili na kimaumbile. Mawe yaliyonyamaza, hayadhuru wala kunufaisha, unayaabudu na kuyasujudia? Iko wapi akili yako na fahamu yako?

Ewe baba yangu! Hakika imenifikia elimu isiyokufikia wewe, Basi nifuate mimi nitakuongoza njia iliyo sawa.

Kila anayekataa ibada ya masanamu anakuwa na ufahamu na akili zaidi kuliko wanayoyaabudu; sikwambii tena mitume wanaopata elimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa kutojua kunakuwa ni udhuru kwa yule asiyejua, lakini masanamu hayo yenyewe hayawezi kuacha udhuru kwa anayeyaabudu.

Ewe baba yangu! Usiabudu shetani. Hakika shetani ni Mwenye kumuasi Mwingi wa rehema.

Makusudio ya kumwabudu shetani ni kumtii, kwa sababu Mwenye kukitii kitu atakuwa amekiabudu; Kwa hiyo basi kila anayemuasi Mwenyezi Mungu atakuwa amemuabudu shetani.

Ewe baba yangu! Mimi nakuhofia isikupate adhabu ya Mwingi wa rehema ukawa ni walii wa shetani.

Walii wa shetani inaweza kuwa kwa maana ya kutawaliwa na shetani au kwa maana ya kuwa mtawala wa shetani katika kuabudu masanamu; sawa na kusema: watu wanajilinda na shetani na shetani anajilinda na watu. Katika makadirio yote, ni kuwa lengo ni kuhofisha na kuhadharisha kumtii shetani na kumfuata.

Akasema: Unaichukia miungu yangu ewe Ibrahim! kama hutakoma, basi lazima nitakupiga mawe na niondokelee mbali kwa muda.

Tulipokuwa tukisoma huko Najaf, siku moja tukiwa tumemzunguka mwal- imu wetu akifafanua maswala muhimu ya elimu ya misingi ya fiqh (Usuulul-fiqh) baada ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wake wote wamefahamu, alihitimisha darasa, lakini ghafla mmoja wa wanafunzi akamuuliza swali ambalo lilikuwa mbali kabisa na maudhui ya darasa. Basi mwalimu akaachana naye akawaangalia wanafunzi wengine na akasema:

“Hapo zamani palikuwa na mwanafunzi mmoja aliyejifundisha masuala ya Swaumu kwa mwalimu kwa muda wa zaidi ya mwezi. Baada ya kumaliza darasa yake mwalimu akadhania kuwa mwanafunzi wake ameelewa kila kitu kinachohusiana na Swaumu, lakini mwanafunzi akamwambia umeeleza sana na ukafafanua masuala ya Swaumu, lakini hatukufahamu kuwa Swaumu inakuwa usiku au mchana?!”

Haya hasa ndiyo yaliyompata Ibrahim pamoja na baba yake. Baada ya kumpa dalili zote na kumbembeleza kwa kumwambia ‘ewe baba yangu’ mara nne, lakini alimjibu kwa kumwambia kuwa kweli umeazimia kutowaabudu miungu pamoja nami? Ikiwa ni kweli umeazimia hivi, basi mimi sina jengine ila nikurujumu na kukuua au uniondokelee mbali nisikuone machoni mwangu.

Akasema Ibrahim: Amani iwe juu yako (salamun alayka)! Nitakuombea msamaha kwa Mola wangu, Hakika yeye ananihurumia sana”

Yaani Mwenyezi Mungu anamwitikia maombi yake, Umetangulia mfano wake katika Juz:11 (9:114).

Nami najitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu na ninamuomba Mola wangu asaa nisiwe na bahati mbaya.

Ibrahim aliwabughudhi watu wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na akawaondokea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akambadilisha familia bora kuliko wao, pale alipompa Is-haq na baada yake Ya’qub bin Is-haq na akawatukuza kwa utume.

Hayo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Alipojitenga nao na yale wanayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimpa Is-haq na baada ya Is-haq ni Ya’qub na kila mmoja tukamfanya Nabii.

Hakuna aliyeacha kitu katika mambo ya dunia kwa kutengeneza dini yake ila humbadilishia bora zaidi yake.

Na tukawapa katika rehema zetu

Mwenyezi Mungu hakubainisha aina ya alichowapa, kwa sababu neno rehema zetu linaashiria hilo. Inatosha kuwa ni zawadi radhi za Mwenyezi Mungu na neema zake.

Na tukawajaalia kuwa na sifa za kweli tukufu.

Makusudio ya sifa za kweli ni sifa wanazozikariri watu kizazi baada ya kizazi kusifia Ibrahim, Is-haq, Ismail na Ya’qub.

Aya hizi zinatia mkazo kwamba mwenye kumfanyia ikhlasi Mungu naye Mungu humsafisha na anakuwa pamoja naye popote alipo; sawa na alivyomfanyia Ibrahim(a.s) .