TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Juzuu 17

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 8253
Pakua: 2189


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 8253 / Pakua: 2189
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Juzuu 17

Mwandishi:
Swahili

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

Sura Ya Ishirini Na Mbili: Surat Al-Hajj.

Baadhi ya Aya zake zimeshuka Makka na nyingine Madina. Ina Aya 78.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ ﴿١﴾

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu. Hakika tetemeko la saa ni jambo kuu.

يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ ﴿٢﴾

2. Siku mtakapoiona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshae na kila mwenye mimba ataiharibu mimba yake. Na utawaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.

وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّبِعُ كُلَّ شَيْطَانٍ مَّرِيدٍ ﴿٣﴾

3. Na miongoni mwa watu kuna anayejadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya elimu na anamfuata kila shetani muasi.

كُتِبَ عَلَيْهِ أَنَّهُ مَن تَوَلَّاهُ فَأَنَّهُ يُضِلُّهُ وَيَهْدِيهِ إِلَىٰ عَذَابِ السَّعِيرِ ﴿٤﴾

4. Ameandikiwa kwamba anayemtawalisha shetani, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza katika adhabu ya moto mkali.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّنَ الْبَعْثِ فَإِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ مِن مُّضْغَةٍ مُّخَلَّقَةٍ وَغَيْرِ مُخَلَّقَةٍ لِّنُبَيِّنَ لَكُمْ وَنُقِرُّ فِي الْأَرْحَامِ مَا نَشَاءُ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ثُمَّ نُخْرِجُكُمْ طِفْلًا ثُمَّ لِتَبْلُغُوا أَشُدَّكُمْ وَمِنكُم مَّن يُتَوَفَّىٰ وَمِنكُم مَّن يُرَدُّ إِلَىٰ أَرْذَلِ الْعُمُرِ لِكَيْلَا يَعْلَمَ مِن بَعْدِ عِلْمٍ شَيْئًا وَتَرَى الْأَرْضَ هَامِدَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ وَأَنبَتَتْ مِن كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ ﴿٥﴾

5. Enyi watu! Ikiwa mna shaka ya kufufuliwa, basi kwa hakika tuliwaumba kutokana na udongo kisha kutokana na tone kisha kutokana na pande la damu kisha kutokana na pande la nyama lenye umbo na lisilokuwa na umbo. Ili tuwabainishie. Na tunaliweka katika matumbo ya kizazi mpaka muda uliowekwa. Kisha tunawatoa hali ya kuwa mtoto mchanga kisha mfikie kukomaa kwenu. Na wapo miongoni mwenu wanaokufa na wapo miongoni mwenu wanorudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa hata asijue kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imekufa, lakini tunapoyateremsha maji juu yake, husisimka na kututumka na kumea kila aina ya mimea mizuri.

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّهُ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَأَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٦﴾

6. Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ni haki na kwamba hakika yeye ndiye Mwenye kuhuisha wafu na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

وَأَنَّ السَّاعَةَ آتِيَةٌ لَّا رَيْبَ فِيهَا وَأَنَّ اللَّـهَ يَبْعَثُ مَن فِي الْقُبُورِ ﴿٧﴾

7. Na kwamba saa itakuja hapana shaka kwa hilo, na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.

UFUFUO

Aya 1 – 7

MAANA

Katika Aya hizi kuna kutahadharisha kuhusu siku ya Kiyama pamoja na kuashiria vitu na shida za siku hiyo. Vile vile kuwashutumu wale walioghafilika nacho; kisha kutoa dalili ya ufufuo.

Ufafanuzi ni kama ufuatavyo:

1.Enyi watu! Mcheni Mola wenu. Hakika tetemeko la saa ni jambo kuu.

Makusudio ya saa ni siku ya Kiyama. Kimeitwa hivyo kwa sababu kila mtu atakifikia; kama anavyosema Mulla Sadra katika kitabu Al-Asfar.

Maana ya tetemeko la kiyama ni kuharibika ulimwengu ikiwa ni pamoa na ardhi yake na mbingu yake. Hizo zitachanganyika na pia bara na bahari na vizuizi vitaondoka. Miili itatoka makakburini kama picha isiyo na roho.

Siku mtakapoiona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshae na kila mwenye mimba ataiharibu mimba yake. Na utawaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.

Hiki ni kinaya cha vituko vya siku ya Kiyama na shida zake; ambapo hakutakuwa na mnyonyeshaji wala mwenye mimba sku hiyo. Yaani, lau angelikuwako mwenye kunyonyesha basi angelimsau mwanawe na mwenye mimba angelizaa. Na watu wote watagongana huku na huko kama walevi.

MJADALA WAKIJINGA NA UPOTEVU

2.Na miongoni mwa watu wako wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya elimu.

Mtu yeyote atakuwa ni mmoja wapo kati ya wawili: Ama atakuwa hajui au atakuwa ni mjuzi. Huyo mjuzi naye yuko katika hali mbili: Ama atakuwa ni mwenye insafu au atakuwa mpotevu. Mwenye insafu ni yule anayesema yale anayoyajua na kuyanyamazia asiyoyajua. Mwenyezi Mungu ameueleza wadhifa wa asiyejua kwa kusema:

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧﴾

“Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.” (21:7).

Ikiwa atauepuka wadhifa huu, basi atakuwa amehusika na kauli ya Imam Ali(a.s) :“Yu mjinga, anatangatanga gizani bila ya mwongozo.”

Huu ndio ujinga alioukusudia Mwenyezi Mungu kwenye kauli yake hii na pia kauli itakayokuja kwenye Aya ya 8 ya Sura hii: “Na katika watu wapo wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilmu wala uongufu wala Kitabu chenye nuru.”

Hajui njia ya kumjua Mwenyezi Mungu, lakini anabishana kuhusu Mungu, huku akisema: lau Mwenyezi Mungu angelikuwako tungelimuona. Kwa mantiki haya, anataka kufasiri mada kwa isiyokuwa mada, kuona kwa macho kile kinachonekana kwa akili tu na kumgusa kwa mkono muumba wa mbingu na ardhi.

Huyu hana tofauti na yule anayetaka kufanya mtihani wa nadhariya ya ‘ushahidi ni wa mwenye kudai na kiapo ni kwa mwenye kukanusha’ kwenye kiwanda. Au kutaka kufanya mtihani wa kuendesha gari kutokana na hisia zake.

Wakati nikiandika maelezo haya nimekumbuka tulipokua Najaf tukisoma, kiasi cha miaka arobaini iliyopita. Siku moja tulipokuwa kwenye darasa tukisiliza mhadhara wa mwalimu, mmoja wa wanafunzi akamkatiza mwalimu na akatoa ushahidi usiokuwa na uhusiano wowote na maudhui kwa umbali wala karibu. Basi mwalimu akaachana naye akawaangalia wanafunzi wengine na akasema:

“Hapo zamani kulikuwa na mtu mmoja mwenye akili punguani, jina lake ni Bau. Siku moja alipita barabarani akaona watu wamekusanyika. Akauliza, kulikoni? Akaambiwa fulani ameanguka kutoka juu ya nyumba, amaevunjikavunjika viungo hatujui kama ataishi na watu wake hawana la kufanya.

Basi Bau akasema: “Mimi nina suluhisho, mfungeni kamba mumkaze sawasawa kisha avutwe mpaka juu ya nyumba kule alikotokea, atapona tu.” Watu walipomcheka, alitoa hoja kwamba mwaka jana fulani alianguka kisimani, wakamfunga kamba na wakamtoa, akasalimika.”

Mantiki haya hasa ndiyo ya yule anayekana kuweko Mungu kwa vile hamuoni. Ulimwengu huu na nidhamu yake anauona, lakini bado anadai kuwa haufahamishi kuwako aliyeutengeneza na kuuwekea nidhamu.

Sisi tunaamini ushahidi na majaribio, lakini tunaamini vilievile kuwa majaribio haya hayawezi kuwa kwenye kila kitu, bali yanakuwa kwenye baadhi ya vitu vya kimaada. Ama vitu vya kiroho na vya kibinadamu vina njia nyingine ya kujua.

Tunasema hivi tukiwa na uhakika kwamba hivi viwili vinakwenda pamoja vikikamilishana na kwamba mtu anahitajia maada. Misimamo kama vile haki na kheri haina budi iwe na athari inayoonekana, vinginevyo ingelikuwa ni matamshi tu yasiyokuwa na maana yoyote.

Lakini hii haimaanishi kuwa ndio njia ya maarifa peke yake; bali inatofautiana kwa kutofautiana vitu. Kwa hiyo ushahidi na majaribio ni sababu ya kujua vitu vya kimaada na akili ni sababu ya kujua vinginevyo visivyokuwa maada.

Tumezungumzia kuhusu maarifa na sababu zake katika Juz. 1(2:3-5)

Kwa ufupi ni kuwa mwenye kusema: Simwamini Mungu mpaka nimuone, amekiri yeye mwenyewe kwamba hataki kumwamini Mwenyezi Mungu, hata kama ataletewa dalili elfu na moja. Maana yake ni kuwa anakubali kuwa yeye ni mjinga mwenye kiburi.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu hawezi kuonekana kwa macho na kwamba njia ya kujua haikomei kwenye macho tu. Mwenyezi Mungu anamtaka binadamu afanye utafiti, uchunguzi, mjadala na mdahalo, lakini kielimu na kuchunga haki, sio kiujinga na kiupofu.

Na anamfuata kila shetani muasi.

Kila anayeweza kuvunga na kuficha hakika yake, basi huyo ni shetani. Shetani asi ni yule ambaye vitendo vyake na kauli zake zote zimejaa ufisadi. Shetani huyu akiingia kwenye akili ya mtu tu humuongoza kwenye upotevu na maangamizi. Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Ameandikiwa kwamba anayemtawalisha shetani, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza katika adhabu ya moto mkali.

Upotevu na adhabu ya moto hawezi kuepukana nayo yule mwenye kufuata wapotevu na wafisadi, ambao wanayapotoa maneno ya Mwenyezi Mungu, wakihalalisha na kuharamisha kwa hawa zao na matakwa yao.

3.Enyi watu ikiwa mna shaka ya kufufuliwa, basi kwa hakika tuliwaumba kutokana na udongo.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumhadharisha yule anayebishana kuhusu Mwenyezi Mungu bila ya elimu, sasa anataja dalili za ufufuo ambao mjinga anauifikiria kuwa hauwezekani.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezileta dalili hizi kwa mifano yenye kuhisiwa, nayo ni kuwa: Hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mtu kutokana na mchanga moja kwa moja, au kupitia kitu kingine.

Alimuumba Adam, baba wa watu, moja kwa moja kutokana na mchanga na akatuumba sisi wana wa Adam kupitia kitu kingine. Kila mmoja wenu anakuwa kutokana na manii na damu navyo vinatokana na chakula ambacho kinatokana na mchanga na maji. Kwa hiyo mchanga ndio msingi wa kupatikana mtu, kisha kutokana na tone la manii; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

أَلَمْ يَكُ نُطْفَةً مِّن مَّنِيٍّ يُمْنَىٰ ﴿٣٧﴾

“Je, hakuwa ni tone la manii lililoshushwa?” (75:37).

Kisha kutokana na pande la damu. Tone la manii linageuka kuwa kipande cha damu iliyoganda,kisha kutokana na pande la nyama. Pande la damu nalo linabadilika kuwa pande la nyamalenye umbo na lisilokuwa na umbo. Yaani baadhi yake imetimia umbo na sehemu haijatimia.Ili tuwabainishie uwezo wetu wa kufufua na mengineyo.

Na tunaliweka katika matumbo ya kizazi mpaka muda uliowekwa wa kuzaliwa mtoto.

Kisha tunawatoa hali ya kuwa mtoto mchanga kisha mfikie kukomaa kwenu . Kukomaa ni kukamilika mtu nguvu za kimwili na kiakili.

Na wapo miongoni mwenu wanaokufa kabla ya kukomaa au baada ya kukomaa kabla ya uzee na umri mbaya.

Na wapo miongoni mwenu wanorudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa hata asijue kitu baada ya kuwa anakijua.

Ni uzee na ukongwe, udhaifu wa kimwili, kiakili na kumbukumbu. Inapodhoofika akili matamanio yanachukua nafasi na kuzidi kufanya mambo ya kipuuzi.

Mabadiliko haya ya kukua kwa binadamu, kutoka hali duni hadi hali ya juu; kutoka mchanga hadi manii, kisha pande la damu, la nyama, utoto hadi kukomaa, yanafahamisha waziwazi kwamba binadamu ana nguvu na maandalizi yatakayompeleka kwenye ukamilifu na ubora, ikiwa hakutakuwa na vizuizi vya kuzuia kufikia lengo hili.

Na unaiona ardhi imekufa, lakini tunapoyateremsha maji juu yake, husisimka na kututumka na kumea kila aina ya mimea mizuri.

Maji yakishuka kwenye ardhi iliyokufa hutaharaki na kupumua kwa uhai, kisha inatoa aina kwa aina za mimea inayovutia macho na yenye ladha kwa walaji.

Hakuna mwenye shaka kwamba ardhi ni maandalizi ya kuukabili uhai, lakini mpaka kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu kila kitu kinaishia kwenye kauli yake ‘kuwa na kinakuwa’ Baadhi ya masufi wanasema: Makusudio ya ardhi iliyokufa ni ujinga, maji ni elimu na aina mbalimbali za mimea ni sifa za ukamilifu za Mwenyezi Mungu.

Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ni haki na kwamba hakika yeye ndiye Mwenye kuhuisha wafu na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu na kwamba saa itakuja hapana shaka kwa hilo na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.

Hayo ni ishara ya mambo yalivyo. Maana ya kuwa Mwenyezi Mungu ni haki ni kwamba hukumu na ufalme ni wake yeye peke yake bila ya kushirikiana na yeyote na kwamba hakuna kupatikana isipokuwa kutokana na yeye.

Hiyo ikiwa na maana kwamba yeye ndiye mwanzishaji na mrudishaji na ufufuo utakuwako tu kama ulivyokuwako uumbaji; bali huo uumbaji ni nyenzo na njia ya kufikia ufufuo ambao ndio lengo la malengo yote.

Kwa sababu mtu anarejea kwa muumba wake kuhisabiwa na kulipwa na pia hapo ndio pa kubakia, lakini kule kuumbwa kwa kwanza kuliisha. Kwisha ni nyenzo ya kubakia.

Hapa ndio tunakuta tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

“Na sikuumba majini na watu ila waniabudu.” (51:56).

Yametangulia maelezo ya ufufuo katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz. 1 (2:28-29) kifungu cha ‘Ufufuo,’ Juz. 5 (4:85-87) kifungu cha ‘Njia mabalimbali za kuthibitisha marejeo (ufufuo) na Juz. 13 (13: 5-7) kifungu cha ‘Wanaoamini maada na maisha baada ya mauti.’

وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ ﴿٨﴾

8. Na katika watu wapo wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu wala uongufu wala Kitabu chenye nuru.

ثَانِيَ عِطْفِهِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ لَهُ فِي الدُّنْيَا خِزْيٌ وَنُذِيقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿٩﴾

9. Anayegeuza shingo yake ili awapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya na siku ya Kiyama tutamuonjesha adhabu ya kuungua.

ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ يَدَاكَ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿١٠﴾

10. Hayo ni kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yako na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١١﴾

11. Na katika watu wapo wanaomwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni. Ikimfika kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amepata hasara ya dunia na Akhera; hiyo ndiyo hasara iliyo wazi.

يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُ وَمَا لَا يَنفَعُهُ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ ﴿١٢﴾

12. Anaomba, badala ya Mwenyezi Mungu, kile kisichomdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotelea mbali.

يَدْعُو لَمَن ضَرُّهُ أَقْرَبُ مِن نَّفْعِهِ لَبِئْسَ الْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ الْعَشِيرُ ﴿١٣﴾

13. Anamuomba yule ambaye hakika dhara iko karibu zaidi kuliko nafuu yake. Hakika ni mlinzi mbaya na ni rafiki mbaya.

إِنَّ اللَّـهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ ﴿١٤﴾

14. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitazo mito chini yake. Hakika Mwenyezi Mungu hufanya ayatakayo.

SABABU YA MAARIFA KATIKA AYA MOJA

Aya 8 – 14

MAANA

Na katika watu wapo wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu wala uongufu wala Kitabu chenye nuru.

Wewe unaona hii ndiyo haki na ile ni batili, lakini ni lipi lililokujulisha kwamba rai yako ni sahihi na salama? Una dhamana gani ya usahihi huo? Inawezekekana kuwa ile unayoiona ni haki kumbe ni batili na ile unayoiona ni batili kumbe ni haki.

Hakuna njia ya kujua maarifa sahihi isipokuwa kwa kurejea kwenye chimbuko lake na sababu iliyotokana nayo. Ikiwa sababu ni sahihi basi maarifa nayo yatakuwa sahihi; vinginevyo yatakuwa batili. Kwa sababu tawi lina- fuata shina.

Swali linarudi tena : Je, ni ipi hiyo sababu ya maarifa sahihi? Utaitambuaje?

Jamaa katika wanafalsafa wanasema kuwa: sababu ya maarifa sahihi inakuwa kwenye majaribio ya hisia tu. Wengine wakasema ni akili; na hisia ni vyombo tu. Ama Qur’an, katika Aya tunayoifasiri, imetaja sababu tatu za maarifa: Kwanza ni majaribio ya hisiya yaliyotajwa kwa neno ‘ilimu’ Ya pili ni akili iliyoitwa ‘Uongofu’ Ya tatu ni Wahyi iliyokusudiwa kwenye neno ‘Kitabu chenye nuru’.

Majaribo ya hisia yanakuwa ni sababu ya kujua vitu vya kimaada tu. Kwa sababu ndivyo vinavyoweza kuhisiwa na kufanyiwa majaribio. Tena majaribio haya huwa yanahitajia akili, kwa sababu hisia haziwezi kutambua kitu ila kwa msaada wa akili.

Ni akili pekee ndiyo inayoweza kujua na kuthibitisha kuweko Mungu. Ama utume unathibitika kwa akili na kwa miujiza. Ukitaka ibara ya ndani zaidi sema: Utume unathibitika kwa miujiza inayothibitishwa na akili na kuikubali kuwa imetoka mbinguni sio ardhini.

Ama wahyi ni sababu ya kujua kila uliyokuja nayo. Wahyi ndio njia pekee ya kujua mambo ya ghaibu; kama majini, Malaika, Kiyama, namna ya hisabu na na malipo kwenye ufufuo n.k.

Anayegeuza shingo yake ili awapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na siku ya Kiyama tutamuonjesha adhabu ya kuungua.

Kugeuza shingo ni kinaya cha kiburi.

Yeye hajui kitu, anajadili kuhusu Mungu bila ya ujuzi, ana kiburi kinachomuhadaa na ni mpotevu na mpotezaji. Hakuna malipo ya wajinga weneye kiburi isipokuwa kudharaulika na kupuuzwa na watu na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hayo ni kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yako na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja. Kwa sababu amewaondolea udhu- ru kwa kuwapa akili, kuwapelekea mitume na akateremsha vitabu.

Na katika watu wapo wanaomwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemtaja anayemkufuru Mwenyezi Mungu na kumjadili bila ya elimu. Hapa anamtaja yule anayemwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni.

Wafasiri wametofautiana katika makusudio ya kabudu ukingoni. Kuna waliosema kuwa ni kumwabudu Mwenyezi Mungu pamoja na shaka katika dini. Wengine wakasema ni kumwabudu kwa ulimi tu sio kwa moyo na kauli nyingine.

Hakuna haja ya kutofautiana huku wakati Mwenyezi Mungu amekwisha mbainisha anayemwabudu ukingoni kwa kusema:

Ikimfika kheri hutulia kwayo na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake.

Makusudio ya kheri hapa ni mambo ya kufurahisha na misukosuko ni madhara. Kutulia ni kuwa na raha na kuendelea na ibada, na kugeuza uso ni kurtadi dini. Maana ni kuwa anayemwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni ni yule anayeweka sharti kwa ibada yake, mpaka apate kitu ndio anaabudu vinginevyo humkufuru Mungu, vitabu vyake na mitume yake.

Na yoyote mwenye kumkufuru basi malipo yake ni Jahannam na ni mwisho mbaya.

Amepata hasara ya dunia na Akhera; hiyo ndiyo hasara iliyo wazi.

Amepata hasara ya nyumba mbili: ambapo mwanzo ni balaa na madhara. Pili, atafika kwa Mola wake akiwa anamkufuru. Kuna hasara kubwa zaidi ya ufukara duniani na adhabu akhera.

Ufafanuzi zaidi wa Aya hii ni riwaya inayosema kwamba baadhi ya mabedui walikuwa wakifika kwa Mtume(s.a.w.w) wakihama kutoka ubeduini kwao.

Basi mmoja wao akiwa na mali nyingi huswali na kufunga. Akipatwa na masaibu au akicheleweshewa sadaka basi huritadi. Nimeyashuhudia yanayofanana na haya nilipokuwa nikiishi na baadhi ya wanakijiji.

Baada ya hayo, hakika mumin wa kweli ni yule anayemfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na kumtegemea katika hali zote; anakuwa na subira wakati wa shida na anashukuru wakati wa raha.

Katika Nahjul balagha kuna maelezo haya: “Haiwi kweli imani ya mja mpaka yawe yaliyo mikononi mwa Mwenyezi Mungu anayategemea zaidi kuliko yaliyo mikononi mwake.”

Anaomba, badala ya Mwenyezi Mungu, kile kisichomdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotelea mbali.

Maana ya Aya hii yametangulia kwenye Aya nyingi, yenyewe pia iko wazi.

Anamuomba yule ambaye hakika dhara iko karibu zaidi kuliko nafuu yake. Hakika ni mlinzi mbaya na ni rafiki mbaya.

Unaweza kuuliza kuwa : katika Aya ya kwanza Mwenyezi Mungu amekanusha kuweko manufaa na madhara kwa yale wanayoyaabudu washirikina, kisha katika Aya hii anathibitisha kuweko manufaa ya mbali na madhara ya karibu. Je, kuna wajihi gani baina ya Aya mbili hizi?

Jibu : makusudio ya chenye kuabudia katika Aya ya kwanza ni mawe; hayanufaishi wala hayadhuru. Na makusudio katika Aya ya pili ni kuwatii viongozi mataghuti na kuwataka usaidizi kwa kukusudia kupata faida na manufaa, na ukubwa wa manufaa ya duniani si chochote kulinganisha na ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Kwa maneno mengine ni kwamba wao wanamtii kiumbe kwa kumuasi muumba kwa ajili ya manufaa ya dunia, hawajui kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali na kubwa zaidi.

Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitazo mito chini yake.

Aya iko wazi na pia imekwishatangulia katika Juz. 1 (2: 25).

Hakika Mwenyezi Mungu hufanya ayatakayo katika kuwapa thawabu wema na kuwaadhibu waovu. Na amekwishapitisha kuwa waliofanya mema atawalipa mema na wabaya atawalipa ubaya kutona na waliyoyafanya.

8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

مَن كَانَ يَظُنُّ أَن لَّن يَنصُرَهُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ فَلْيَمْدُدْ بِسَبَبٍ إِلَى السَّمَاءِ ثُمَّ لْيَقْطَعْ فَلْيَنظُرْ هَلْ يُذْهِبَنَّ كَيْدُهُ مَا يَغِيظُ ﴿١٥﴾

15. Anayedhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru katika dunia na Akhera, basi na afunge kamba mbinguni kisha aikate, aone je, hila yake itaondoa yale yaliyomghadhabisha?

وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ وَأَنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يُرِيدُ ﴿١٦﴾

16. Na namna hiyo tumeiteremsha kuwa ni Aya zilizo wazi na kwamba Mwenyezi Mungu humuongoza anayetaka.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالصَّابِئِينَ وَالنَّصَارَىٰ وَالْمَجُوسَ وَالَّذِينَ أَشْرَكُوا إِنَّ اللَّـهَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿١٧﴾

17. Hakika wale ambao wameamini na ambao ni mayahudi na wasabai na wanaswara na wamajusi na wale washirikishao, hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya kila kitu.

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَسْجُدُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِّنَ النَّاسِ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَابُ وَمَن يُهِنِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّكْرِمٍ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ﴿١٨﴾

18. Je huoni kuwa vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini na jua na mwezi na nyota na milima na miti na wanyama na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahili adhabu. Na anayetwezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumheshimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.

AJINYONGE

Aya 15 -18

LUGHA

Wengi wamesema kuwa makusudio ya mbingu hapa ni dari ya nyumba, kukata ni kujinyonga na hila yake ni huko kujinyonga kwake. Kwa hiyo maana yatakuwa: Anayedhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru katika dunia na Akhera, basi na afunge kitanzi ajinyonge aone je huko kujinyonga kutamuondolea ghadhabu yake?

MAANA

Anayedhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru katika dunia na Akhera, basi na afunge kamba mbinguni kisha aikate, aone je, hila yake itaondoa yale yaliyomghadhabisha?

Wafasiri wengi wamesema kuwa dhamiri ya ‘hawatamnusuru’ inamrudia Muhammad(s.a.w.w) na maana yawe: Anayedhani katika washirikina kuwa Mwenyezi Mungu hatamnusuru Mtume wake Muhammad(s.a.w.w) , basi na amnyonge aone kama Mwenyezi Mungu hatamnusuru Mtume wake.

Lakini dhahiri ya mfumo wa Aya inaonyesha kuwa dhamiri inamrudia huyo anayedhani, kwa sababu Muhammad(s.a.w.w) hakutajwa katika Aya. Na maana yanakuwa:

Ambaye ameshukiwa na balaa na akachukia kadha ya Mwenyezi Mungu na kadari yake, akakata tamaa kwamba Mwenyezi Mungu atamsaidia duniani na kumpa thawabu akhera kwa sababu ya kuvumilia kwake, atakayekuwa hivyo basi hatakuwa na la kufanya isipokuwa kujinyonga kwa kujifunga kamba kwenye dari ya nyumba yake; kisha aangalie je, hilo ndilo suluhisho?

Mwenye akili anapotokewa na balaa, hufanya juhudi na bidii kuiondoa huku akitaka msaada kwa Mwenyezi Mungu, akifaulu ni sawa, la sivyo humwachia Mwenyezi Mungu mambo yote huku akingoja fursa.

Na namna hiyo tumeiteremsha kuwa ni Aya zilizo wazi na kwamba Mwenyezi Mungu humuongoza anayetaka.

Dhamiri katika iliyoteremshwa inarudia Qur’an. Mwenyezi Mungu (s.w.t) humwongoza anayetaka kuongoka kwa Kitabu chake na humwongoza kwenye wema wa nyumba mbili yule anayetafuta mwongozo kwake na kwa Mtume wake.

Na mwenye kutafuta upotevu na ufisadi ataipata njia yake kwa wafisadi na wapotevu.

Hakika wale ambao wameamini na ambao ni mayahudi na wasabai na wanaswara na wamajusi na wale washirikishao, hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya kila kitu.

Wasabai wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, lakini wanaamini kuwa baadhi ya nyota zina athari katika kheri na shari, wamajusi wanaabudu moto kwa kusema kuwa kheri inatokana na nuru na shari inatokana na giza na wanaswara ni wakristo.

Mwenyezi Mungu anayajua makundi yote haya sita na atayapambanua kesho siku ya Kiyama na kumlipa kila mmoja kwa vile alivyofanya. Kafiri atamwingiza motoni na mumin atamwingiza Peponi. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 1 (2:117).

Je huoni kuwa vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini na jua na mwezi na nyota na milima na miti na wanyama.

Wamesema jamaa katika wafasiri kwamba makusudio ya kusujudi wanyama mimea n.k. Ni kutii amri yake na kwamba yeye anawafanyia vile atakavyo.

Katika Juz. 15 (17:44) tumeeleza kuwa makusudio ya kusujudi vitu visivyo na harakati, miti na mimea ni kule kufahamisha kwake kuweko muumba wake na utukufu wake. Mulla Sadra katika kitabu Al-Asfar anasema: “Vitu vyote vina akili, vinamfahamu Mola wake na kumjua muumba wake, vinasikia maneno yake na kufuata amri yake”

Haya hayako mbali, akili inakubali na dhahiri ya nukuu inalithibitisha. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤٤﴾

“Na hapana kila kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake, lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake.” Juz. 15 (17:44).

Sayansi itagundua hakika hii hivi karibuni au baadaye.

Na wengi miongoni mwa watu wanamwamini na wanamsujudia.Na wengi miongoni mwaoimewastahili adhabu .

Hao ni wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu wanaowadharau wale wanaomwamini Mungu. Ilikuwa inafaa kwa mwenye kitabu Al-Asfar, awavue wanaomkana Mungu katika viumbe.

Na anayetwezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumheshimu.

Kabisa! Hakuna wa kumuinua aliyeangushwa na kudhalilishwa na Mwenyezi Mungu, wala hakuna wa kumdhalilisha aliyetukuzwa na kuenziwa na Mwenyezi Mungu, na hakuna utukufu mbele ya Mwenyezi Mungu ila kwa wenye takua.

Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo kuwatukuza wema na kuwatweza wapotevu na wafisadi.

Baada ya hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ana desturi katika viumbe vyake haiachi; nayo ni kuwa mwenye kufuata nji ya maangamizi ataangamia, na mwenye kufuata njia ya usalama atasalimika. Njia ya usalama mbele ya Mwenyezi Mungu ni imani ya kweli na matendo mema; na njia ya kufedheheka na kupuuzwa ni unafiki na ufisadi katika ardhi.

هَـٰذَانِ خَصْمَانِ اخْتَصَمُوا فِي رَبِّهِمْ فَالَّذِينَ كَفَرُوا قُطِّعَتْ لَهُمْ ثِيَابٌ مِّن نَّارٍ يُصَبُّ مِن فَوْقِ رُءُوسِهِمُ الْحَمِيمُ ﴿١٩﴾

19. Hawa mahasimu wawili waliohasimiana kwa ajili ya Mola wao. Basi waliokufuru watakatiwa nguo za moto na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka.

يُصْهَرُ بِهِ مَا فِي بُطُونِهِمْ وَالْجُلُودُ ﴿٢٠﴾

20. Kwayo vitayeyushwa vilivyo matumboni mwao na ngozi.

وَلَهُم مَّقَامِعُ مِنْ حَدِيدٍ ﴿٢١﴾

21. Na yatakuwako makomeo ya chuma kwa ajili yao.

كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا مِنْ غَمٍّ أُعِيدُوا فِيهَا وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿٢٢﴾

22. Kila wanapotaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo; na onjeni adhabu ya kuungua.

إِنَّ اللَّـهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ ﴿٢٣﴾

23. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitiwazo na mito chini yake. Watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu na mavazi yao humo ni hariri.

وَهُدُوا إِلَى الطَّيِّبِ مِنَ الْقَوْلِ وَهُدُوا إِلَىٰ صِرَاطِ الْحَمِيدِ ﴿٢٤﴾

24. Na wataongozwa kwenye maneno mazuri na kuongozwa kwenye njia ya mwenye kuhimidiwa.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاءً الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُّذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٢٥﴾

25. Hakika wale waliokufuru na wakawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti mtakatifu ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawa sawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakayefanya upotofu humo kwa dhulma tutamwonjesha adhabu chungu.

MAHASIMU WAWILI

Aya 19 – 25

MAANA

Hawa mahasimu wawili waliohasimiana kwa ajili ya Mola wao.

Kuna maelezo katika Tafsir At-Tabari kwamba Abu dharr alikuwa akiapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba Aya hii imeshuka kwa ajili ya watu sita katika makuraishi; watatu miongoni mwao ni waumini nao ni Hamza bin Abdul-Muttalib, Ali bin Abu Twalib na Ubayda bin Al-Harith.

Na watatu ni katika washirikina nao ni: Utba na Shayba, watoto wa Rabia na Walid bin Utba. Uhasama baina yao ulikuwa katika vita vya Badr walipobariziana; na Mwenyezi Mungu akawapa nusra waumini kuwashinda washirikina.

Jamaa katika wafasiri wamesema kwamba makusudio ya waliohasimiana ni kikundi cha waumini na kikundi cha makafiri ambao ni mayahudi, wanaswara, wasabai, majusi na washirikina. Kwa sababu wote hao wametajwa katika Aya iliyotangulia na kila kundi linasema lina haki kuliko jingine.

Vyovyvote iwavyo ni kwamba uhasama katika dini unatokea baina ya wanaoamini.

Basi waliokufuru watakatiwa nguo za moto na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka. Kwayo vitayeyushwa vilivyo matumboni mwao na ngozi. Na yatakuwako makomeo ya chuma kwa ajili yao. Kila wanapotaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo, na onjeni adhabu ya kuungua.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria uhasama wa waumini na makafiri anataja kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu mwisho wake ni Peponi na mwenye kumkufuru mwisho wake ni Jahannam, mwisho mbaya kabisa.

Na kwamba watu wake watavaa kivazi cha moto na watamiminiwa maji ya moto ambayo yatayeyusha mafuta, nyama matumbo na ngozi. Pia nguzo za chuma zitakuwa vichwani mwao kuwazuia kutoka kila wanapojaribu kukimbia. Inawezekena kukimbia hukumu ya Mwenyezi Mungu na matakwa yake? Umepita mfano wake katika Juz. 13 (14: 49 – 50) kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi’

Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitiwazo na mito chini yake. Watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu na mavazi yao humo ni hariri.

Makafiri watakuwa na mavazi ya moto, makomeo ya chuma, maji ya moto na waumini wenye ikhlasi watapata pepo yenye neema, mito yenye kinywaji cha ladha, nguo za hariri na vipambo vya dhahabu na lulu.

Na wataongozwa kwenye maneno mazuri.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria kwenye chakula na kinywaji chao, anataja kauli zao ambazo ni nzuri; mfano Alhamdulillah.Na kuongozwa kwenye njia ya mwenye kuhimidiwa. Hiyo ni njia yenye kunyooka waliyoifuata katika maisha ya dunia, ikawapeleka kwenye neema ya Akhera.

Hakika wale waliokufuru na wakawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti mtakatifu ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawa- sawa, kwa wakaao humo na wageni.

Washirikina wa kikuraishi walikuwa wakiwazuilia watu kuiingia kwenye Uislamu, kuhiji na kufanya umra kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo ameifanya ni mahali pa kuendewa na watu na mahali pa amani. Umepita mfano wake katika Juz. 1 (2:125).

Na kila atakayefanya upotofu humo kwa dhulma tutamwonjesha adhabu chungu.

Yaani atakayeacha yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu na akamfanyia uovu anayeikusudia nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu, basi Mungu atamwadhibu adhabu kubwa.

وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَاهِيمَ مَكَانَ الْبَيْتِ أَن لَّا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْقَائِمِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ ﴿٢٦﴾

26. Na tulipomwekea Ibrahim mahala penye ile nyumba kwamba usinishirikishe na chochote na uitwaharishe nyumba yangu kwa ajili ya wanozunguka na wakaazi na wanaorukui na wanaosujudi.

وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًا وَعَلَىٰ كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ ﴿٢٧﴾

27. Na watangazie watu Hijja; watakujia kwa miguu na juu ya kila mnyama aliyekonda kutoka kila njia ya mbali.

لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ ﴿٢٨﴾

28. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalum juu ya wanyama hawa aliowaruzuku.

ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ ﴿٢٩﴾

29. Basi kuleni katika hao na mumlishe mwenye shida aliye fukara, kisha wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao na waizunguke sana nyumba ya kale.

ITWAHARISHE NYUMBA YANGU

Aya 26 -29

MAANA

Na tulipomwekea Ibrahim mahala penye ile nyumba kwamba usin- ishirikishe na chochote na uitwaharishe nyumba yangu kwa ajili ya wanozunguka na wakaazi na wanaorukui na wanaosujudi.

Makusudio ya wakaazi ni wakaazi wa Makka na viunga vyake; na wanorukui wakisujudi ni wanaoswali.

Makuraishi walikuwa wakiabudu masanamu na wakisimamia Al-Kaaba. Baada ya Mwenyezi Mungu kumtuma Muhammad(s.a.w.w) walianza kuwa na uadui naye na kila anayemwamini, tena wakawazuilia waislamu kuizunguka (tawaf) na kuswali hapo; kama ilivyoelezwa kwenye Aya iliyotangulia. Pamoja na hayo Makuraishi walikuwa wakidai kwamba wako kwenye dini ya Ibrahim(a.s) .

Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao haya, kwamba yeye ndiye mwenye nyumba hiyo na alimpa wahyi kuwa aijenge na aifanye ni mahsusi kwa ibada ya wanaompwekesha Mungu wanaokaa hapo na wanaopita na pia kuwaweka mbali nayo washirikina na mizimu yao.

Haya ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Na uitwaharishe nyumba yangu’ lakini makuraishi waliipindua Aya, wakaijaza masanamu nyumba ya Mwenyezi Mungu, wakaihalalishia washirikina na wafisadi na wakawazulia nayo watu wa tawhid na wema.

Na watangazie watu Hijja; watakujia kwa miguu na juu ya kila mnyama aliyekonda kutoka kila njia ya mbali.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha kipenzi chake awaite watu kuhiji kwenye msikiti mtakatifu baada ya kusimamisha misingi yake na kutimia jengo. Akamwahidi kuwa watu watamwitikia na watamjia kwa kila hali; kutembea kwa miguu na kupanda ngamia au farasi waliokonda tena kutoka mbali, sikwambii karibu.

Ili washuhudie manufaa yao.

Hijja ni ibada pekee inayochanganya manufaa ya kidini na ya kidunia. Ama ya kidini ni kumtii Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza faradhi ya Hijja, kutubia na kutambua haiba ya Mwenyezi Mungu na utukufu. Ibn Al- Arabi anasema katika Kitabu Futuhatul- Makkiyya:

“Siku moja nilikuwa nikitufu Al-Kaaba nikaiona kama kwamba imenyanyuka kutoka ardhini, wallah, ikaniambia maneno niliyoyasikia: njoo uone nitakavyokufanyia, mara ngapi hadhi yangu unaiweka chini na ya binadamu unaiinua juu?.

Nasi tunasema kwa uhakika: hakuna yeyote anayefanya sa’yi au tawaf katika nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa ikhlas ila atahisi aina ya kitu kama hiki.

Na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalum juu ya wanyama howa aliowaruzuku, ambao ni ngamia ng’ombe na mbuzi na kondoo.

Kumtaja Mwenyezi Mungu kwenye wanyama ni kinaya cha kuchinja, kwa sababu kusoma Bismillah ni wajibu katika kuchinja. Makusudio ya siku maalum ni siku za kuchinja katika Hijja, kama inavyofahamisha Aya.

Mafakihi wametofautiana katika idadi ya siku hizo: Shia wamesema ni nne, mwanzo wake ni siku ya Idul-adh’ha na mwisho wake ni tarehe kumi na tatu ya Dhul-hijja. Mafakihi wa madhehbu mengine wamesema ni tatu kwa kuishia tarehe kumi na mbili. Ufafanuzi uko katika kitabu chetu Alfiqh ala madhahibil-khamsa [5] .

Razi anasema kuwa maulama wengi wanatofautisha baina ya siku maalum na siku za kuhisabiwa zilizotajwa katika Juz. 2 (2:203) na wanaona kuwa siku maalum ni siku kumi za mwezi wa Dhul-hijja na za kuhisabiwa ni siku za kuchinja.

Basi kuleni katika hao na mumlishe mwenye shida aliye fukara.

Wameafikiana mafakihi kuhusu wajibu wa kumlisha fukara mnyama wa Hijja na wakatofautina katika wajibu wa mwenyewe kula. Sisi tuko pamoja na wale wanaosema kuwa si wajibu kwa mwenyewe kula. Ni vile atavyoona, akipenda atakula na akipenda ataitoa sadaka yote. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu:‘Kuleni katika hao’ ni kwa ajili ya kuondoa fikra ya uharamu wa kula; ambapo wakati wa jahiliya walikuwa hawali wanyama hao wawachinjao wakidai kuwa ni haramu kwao. Ndipo Mwenyezi Mungu akawazindua kosa lao hilo.

Kisha wajisafishe taka zao.

Haijuzu kwa aliye kwenye Hijja akiwa kwenye ihram (Vazi maalum la Hijja) kunyoa, kukata kucha au kujipaka manukato; bali mafakihi au wengi wao wamesema kuwa hata kuua vidudu vya mwilini, kama vile chawa pia ni haramu. Zikiisha zile siku za Ihram basi inakuwa ni halali kwake yale yaliyokuwa ni haramu, basi hapo atanyoa, kukata kucha n.k. Ndipo kwa hili ameshiria Mwenyezi Mungu aliposema:

Kisha wajisafishe taka zao.

Na watimize nadhiri zao, ikiwa wameweka nadhiri siku za Hijja au kabla. Kwa sababu watu wengi huweka nadhiri ya kutoa sadaka ikiwa Mwenyezi Mungu atawaruzuku Hijja.

Na waizunguke sana nyumba ya kale. Kwa sababu ndio nyumba ya kwanza kuwekewa watu kwa ajili ya ibada.

Mwenyezi Mungu ameleta tamko la ‘sana’ kwa sababu ni Sunna kufanya tawaf mara nyingi; kama ambavyo pia ni Sunna kuswali sana. Kuna Hadithi mashuhuri kutoka kwa Mtume wa rehema, aliposema: “Kuizunguka Al-Kaaba ni Swala.’