TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Juzuu 17

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA33%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 9667 / Pakua: 4397
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA Juzuu 17

Mwandishi:
Swahili

1

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ وَأُحِلَّتْ لَكُمُ الْأَنْعَامُ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ وَاجْتَنِبُوا قَوْلَ الزُّورِ ﴿٣٠﴾

30. Ndivyo hivyo! Na anayeitukuza miiko ya Mwenyezi Mungu hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake. Na mmehalalishiwa wanyama howa ila wale mliosomewa. Basi jiepusheni na uchafu wa mizimu na mjiepushe na kauli ya uzushi.

حُنَفَاءَ لِلَّـهِ غَيْرَ مُشْرِكِينَ بِهِ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَكَأَنَّمَا خَرَّ مِنَ السَّمَاءِ فَتَخْطَفُهُ الطَّيْرُ أَوْ تَهْوِي بِهِ الرِّيحُ فِي مَكَانٍ سَحِيقٍ ﴿٣١﴾

31. Kwa kumtakasia imani Mwenyezi Mungu bila ya kumshirikisha. Na anayemshrikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukampeleka mahala mbali.

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾

32. Ndivyo hivyo! Na anayezitukuza nembo za Mwenyezi Mungu. Basi hiyo ni katika takua ya nyoyo.

لَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ثُمَّ مَحِلُّهَا إِلَى الْبَيْتِ الْعَتِيقِ ﴿٣٣﴾

33. Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda uliowekwa kisha mahali pake ni nyumba ya kale.

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ جَعَلْنَا مَنسَكًا لِّيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ ﴿٣٤﴾

34. Kila umma tumeujaalia mihanga ya ibada, ili wamtaje Mwenyezi Mungu katika vile alivyowaruzuku katika wanyama howa. Basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, Kwa hiyo jisalimisheni kwake. Na wabashirie wanyenyekevu.

الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَالصَّابِرِينَ عَلَىٰ مَا أَصَابَهُمْ وَالْمُقِيمِي الصَّلَاةِ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣٥﴾

35. Ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka na walio na subira kwa yale yaliyowasibu, na wanao-simamisha Swala, na wanatoa katika tulivyowaruzuku.

MIIKO YA MUNGU NA NEMBO ZAKE

Aya 30 -35

MAANA

Ndivyo hivyo! Na anayeitukuza miiko ya Mwenyezi Mungu hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake.

Kutukuza kuko aina nyingi kutegemea na anayetukuzwa na namna ya kutukuzwa inayokubaliana naye.

Hakuna kitu kinachokubaliana na kumtukuza muumba isipokuwa kumtii na kufuata amri yake katika kila jambo. Atakayemtii Mwenyezi Mungu na akafuata amri zake na kuacha makatazo yake, basi atakuwa ametukuza na kuadhimisha miiko yake na nembo zake. Taadhima hii au utiifu huu unamwinua aliyeutenda kwa muumba wake, sio kuwa unamwinua muumbaji, kwa sababu Yeye hawahitajii walimwengu.

Ndio maana akasema:‘Hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake’ yaani kutukuza hukumu za Mwenyezi Mungu kwa kumtii ni kheri ya huyo mtiifu.

Na mmehalalishiwa wanyama howa ila wale mliosomewa.

Mwenyezi Mungu amemharamishia anayehiji kuwinda akiwa katika Ihram yake, pengine anaweza akadhania kuwa ameharamishiwa kula nyama ya wanyama wa kufugwa. Ndio akabainisha kuwa hakuna uhusiano baina ya mawili hayo; na kwamba walioharamishwa ni mfu na waliochinjiwa mizimu. Angalia Juz. 6 (5:3).

Basi jiepusheni na uchafu wa mizimu.

Jiepusheni nayo na msiiabudu, kama mnavyojiepusha na uchafu, kwa sababu yote ni uchafu, ndio maana ikafasiriwa uchafu wa mizimu, ingawaje kuna herufi min, ambayo hapa imekuwa ya kueena na sio ya baadhi, kama inavyokuwa mara kwa mara.

Na mjiepushe na kauli ya uzushi.

Kauli ya uzushi inachanganya kila lilioharamishwa; iwe ni uongo, kusengenya, shutuma na ufyosi. Uzushi mbaya zaidi ni kuleta ushahidi wa uongo, kwa sababu unanyima haki ya Mungu na ya watu. Mtume(s.a.w.w) anasema: “Uzushi umelinganishwa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu,” kisha akasoma Aya hii.

Kwa kumtakasia imani Mwenyezi Mungu bila ya kumshirikisha.

Yaani kushikamana na dini ya haki na kuachana na dini potofu. Bila ya kumshirikisha ni msisitizo wa hayo. Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 15 (17:107).

Na anayemshrikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukampeleka mahala mbali.

Hiki ni kinaya cha dhambi ya shirki kwamba haifanani na dhambi yoyote, na kwamba adhabu ya mshirikina haishindwi na adhabu yoyote. Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an na Sunna za Mtume ataona kuwa mshirikina ana dhambi kubwa zaidi kuliko mlahidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Inawezekana siri ya hilo ni kuwa mlahidi hathibitishi upungufu wa muumba, kwa sababu yeye hakubali kabisa kuwa yuko. Hii pia ni dhambi kubwa, hilo halina shaka, lakini dhambi ya mshirikina ni kubwa zaidi, kwa sababu ni kumshirikisha muumba kwa upande mmoja na ni kuthibitisha upungufu kwa muumba kwa upande wa pili.

Ndivyo hivyo! Na anayezitukuza nembo za Mwenyezi Mungu. Basi hiyo ni katika takua ya nyoyo.

Nembo za Mwenyezi Mungu na miiko yake zina maana moja. Tumezungumzia kuhusu miiko katika Aya iliyotangulia. Hakuna mwenye shaka kwamba hawatii amri za Mwenyezi Mungu isipokuwa wenye takua na ikhlasi.

Miongoni mwa kutukuza nembo za Mwenyezi Mungu na kutii hukumu yake ni kuchinja mnyama aliyenona asiye na kasoro yoyote siku za Hijja. Mtume(s.a.w.w) anasema: “Hafai aliye kiguru, wala aliyekonda, wala aliyetobolewa sikio wala aliyekatwa sikio wala aliyevunjika pembe.”

Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda uliowekwa.

Katika hao ni hao wa kuchinjwa kwenye Hijja. Muda uliowekwa ni wakati wa kuchinjwa. Maana ni kuwa mwenye kuhiji anaruhusiwa kunufaika na maziwa na mgongo wa mnyama wa kuchinja mpaka wakati wa kuchinja.

Katika Tafsiru-Razi imeelezwa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimpitia mtu akimkokokota mnyama na yeye mwenyewe amechoka. Mtume akamwambia: “Mpande.” Yule mtu akasema: “Huyu ni wa kuchinja kwa ajili ya Hijja ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!” Akasema Mtume: “Ole wako, mpande!”

Anaendelea kusema Razi: “Abu Hanifa hajuzishi hilo, akatoa hoja kuwa haijuzu kumkodisha kwa hiyo haijuzu kumpanda.” Razi akamjibu Abu Hanifa kwamba hoja hii ni dhaifu, kwa sababu, mjakazi aliyezaa na mmiliki wake hauzwi, lakini inajuzu kunufaika naye.

Kisha mahali pake ni nyumba ya kale.

Yaani mahali pake pa kuchinjwa ni nyumba ya Mwenyezi Mungu takatifu na makusudio yake ni haram yote ikiwemo Mina. Katika Hadith imeelezwa. Mina yote ni machinjioni.

Kila umma tumeujaalia mihanga ya ibada.

Makusudio ya mihanga ya ibada hapa ni kuchinja wanyama kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu,Ili wamtaje Mwenyezi Mungu katika vile alivyowaruzuku katika wanyama howa, iliyokuja moja kwa moja. Maana ni kuwa hakuna bid’a (uzushi) katika kuchinja mnyama, ilikuweko katika dini zilizotangulia.

Basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Kwa hiyo msimtaje mwengine katika dhabihu zenu.

Kwa hiyo jisalimisheni kwake .Yaani fuateni amri yake na mumfanyie ikhlasi katika kauli na vitendo.

Na wabashirie wanyenyekevu, ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na walio na subira kwa yale yaliyowasibu, na wanaosimamisha Swala na wanatoa katika tulivyowaruzuku.

Mpe habari njema ya Pepo, ewe Muhammad, yule anayemnyenyekea Mwenyezi Mungu, akamwogopa akawa na uthabiti kwenye dini wakati wa raha na dhiki, akamwabudu bila ya unafiki wala ria na akatoa mali yake katika kumtii Mungu na kutaka radhi yake. Hakuna shaka kwamba mwenye kukusanya sifa hizi atakuwa na daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu na ya watu.

وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ كَذَٰلِكَ سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٣٦﴾

36. Na ngamia wa kunona tumewafanyia kuwa ni miongoni mwa nembo za Mwenyezi Mungu, kwao mna kheri. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanaposimama safu. Na wanapoanguka ubavu, basi kuleni na mlisheni aliyekinai na aombaye. Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mpate kushukuru.

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٧﴾

37. Nyama zao hazimfikii wala damu zao, lakini inamfikia takua kutoka kwenu. Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyowaongoa. Na wabashirie wenye kufanya mema.

NGAMIA WANONO

Aya 36 -37

MAANA

Na ngamia wa kunona tumewafanyia kuwa ni miongoni mwa nembo za Mwenyezi Mungu, kwao mna kheri.

Neno ‘Budna’ ni ngamia hasa; kama ilivyoelezwa katika Tafsiri Razi, na Baydhawi. Hufananishwa naye ng’ombe katika hukumu si katika jina.

Hali yoyote iwayo, mtu ni natija ya mambo mengi, yakiwemo mazingira anayoishi. Waarabu, kwa karne nyingi, wakati wa jahiliya na baadaye, wameishi pamoja na ngamia na alikuwa ni sehemu ya maisha yao; wakila nyama yake, kunywa maziwa yake , kuvaa manyoya yake, kubebea mizigo kutoka mji mmoja hadi mwingine n.k. Tazama Juz. 14 (16: 6).

Kwa ajili hii ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamtaja kwenye Aya kadha, kwa tamko la kiujumla; kama vile wanyama howa, au kwa tamko mahususi; kama ilivyo katika Sura 88 na hii Aya tuliyo nayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaneemesha waja wake kwa ngamia na akamfanya ana manufaa mengi; yakiwemo kujikurubisha mja kwa Mwenyezi Mungu kwa kumchinja katika nyumba yake takatifu. Kuleta ibara ya nembo kwa dhabihu hii ni kufahamaisha kuwa hiyo ni twaa na ibada bora zaidi.

Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanaposimama safu.

Katika masharti ya kuchinja ni kusoma Bismillah na kuelekezwa chinjo upande wa Qibla, na ngamia kuwa na aina yake ya kuchinjwa (nahr) ambayo ni maalum kwa ngamia:

Anachomwa kisu au kitu chochote chenye ncha kwenye maungio ya shingo na kifua, akiwa ngamia amesimama au kupiga magoti au amelala ubavu, kwa sharti ya kuwa sehemu zote za mbele ya mwili wake zielekee Qibla.

Njia bora ni kumchinja ngamia kwa namna ilivyoelezwa katika Riwaya ambayo ni kusimamishwa ngamia na kufungwa mmoja wa miguu yake ya mbele na asimame mchinjaji kuelekea Qibla vile vile kisha amchome kwenye maungio ya shingo na kifua. Riwaya hii inaweza kufaa kuwa ni tafsiri ya neno ‘wanaposimama safu.’

Na wanapoanguka ubavu, yaani wanapoanguka chini na kukata roho,basi kuleni na mlisheni aliyekinai na aombaye.

Aliyekinai ni yule anayeridhia unachompa bila ya kuomba.Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mpate kushukuru.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewafanya wanyama tuwatumie, hata kuwachinja pia. Kwa hiyo ni wajibu wetu kushukuru.

Nyama zao hazimfikii wala damu zao.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosha na walimwengu, hawahitajii, sikwambii nyama zilizochinjwa na damu; bali haihitajii chochote. Imesemekana hii ni kuwarudi washirikina ambao walikuwa wakitapakaza damu ya dhabihu kwenye masanamu yao na kuta za Al-Kaaba.

Lakini inamfikia takua kutoka kwenu.

Unaweza kuuliza kuwa : maana ya takua ni kumcha Mungu katika yale aliyoyaharamisha; ambapo thawabu yake na manufaa yake yanarudi na kumfikia mtendaji tu. Sasa nini maana ya kuwa inafika kwa Mungu?

Jibu : Makusudio ya takua hapa ni kumridhisha Mwenyezi Mungu, na radhi ya Mwenyezi Mungu haiepukani na mwenye takua, zinakwenda sambamba. Kwa hiyo maana ni kinachomfikia Mwenyezi Mungu katika dhabihu zenu ni kule kuridhiwa na Mungu sio kukasirikiwa. Inafanana na kumwambia mwanao: kufaulu kwako darasani kunanifanya ni kupende na kukuridhia, na haya ndiyo ninayoyapata kutokana na masomo na kufaulu kwako.

Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyowaongoa.

Amewadhalilisha wanyama kwa waja wake na akawaongoza kujikurubisha kwake kwa kuwachinja ili wamsifu kwa sifa zake njema, wamuad- himishe kwa ujuzi wake na uweza wake, wahofie adhabu yake na kutumai thawabu zake.

Wabashirie wenye kufanya mema wote; wawe wamefanya mema kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuchinja au kwa jambo jinginelo. Kwani aina za wema hazina idadi. Bora zaidi ni kupigana jihadi na madhalimu na wapotevu japokuwa kwa tamko la haki na uadilifu.

إِنَّ اللَّـهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ خَوَّانٍ كَفُورٍ ﴿٣٨﴾

38. Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini, mwenye kukufuru sana.

أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا وَإِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ ﴿٣٩﴾

39. Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.

الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّـهُ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّـهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّـهِ كَثِيرًا وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٤٠﴾

40. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila tu kwa kuwa wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu. Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi yangelivunjwa mahekalu na makanisa na (sehemu) za kuswalia na misikiti ambayo ndani yake hutajwa jina la Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.

الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ وَلِلَّـهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ ﴿٤١﴾

41. Wale ambao tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha Swala na wakatoa Zaka na wakaamrisha mema na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.

MWENYEZI MUNGU HUWAKINGA WALIOAMINI

Aya 38 – 41

MAANA

Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini mwenye kukufuru sana.

Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazuia ukafiri na utaghuti kwa waumini katika maisha haya na siku ya mwisho. Aya iliyo wazi zaidi katika hilo ni: “Hakika bila shaka tutawanusuru Mitume wetu na walioamini katika uhai wa duniani na siku watakaposimama mashahidi.” (40:51).

Pamoja na hayo Mwenyezi Mungu ameashiria kwenye Aya kadhaa, kwamba mayahudi walikuwa wakiwaua manabii bila ya haki. Miongoni mwazo ni: Juz.3 (3: 21), Juz. 4 (3:112, 181) na Juz 6 (4:154). Kuongezea Historia ya mwanadamu, tangu zamani na sasa, imejaa dhulma na kufanyiwa uadui wale wenye takua na ikhlasi.

Sasa je, kuna wajihi wa kukusanya baina ya zinazofahamisha kuuliwa watu wema na zile zinazofahamisha kunusuriwa watu wa haki?

Jibu :Kwanza : Aya za nusra zinawahusu baadhi ya mitume; kama vile: Nuh, Hud, Swaleh, Lut na Muhammad. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono kwa nusra yake amtakaye.” Juz.3 (3:13).

Na Aya hii tuliyo nayo inafahamisha kuwa Muhammad (s.a.w.) na maswahaba ndio wanokusudiwa kwenye kauli yake ‘Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamni.’ Kwa sababu wao ndio waliotolewa majumbani mwao si kwa lolote ila ni kwa kuwa wamesema: ‘Mola wetu ni Mwenyezi Mungu.”

Katika vitabu vya Hadith (As-sihah) imeelezwa kwamba Aya hizi zilishuka wakati Mtume alipofanya hijra (kuhama) kutoka Makka kwenda Madina.

Pili : Mwenye haki na ikhlasi hawezi kukosa wa kumuunga mkono na kumsaidia kwa mkono wake, mali yake au ulimi wake. Wala hatujawahi kusikia jamii ambayo kwa pamoja imekuwa dhidi ya mwenye kutamka tamko la haki na uadilifu.

Ndio, ni kweli kwamba watetezi wa haki wengi wameuawa, wakatekwa na wakafukuzwa, lakini Mwenyezi Mungu anawapa wasaidizi wanotangaza misimamo yao na kuwatukuza na wakiwakabili maadui zao kwa hoja na dalii mkataa. Hii ni aina ya nusra. Kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini’ ni sababu ya kauli yake: ‘Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamni.’

Sababu hii inafahamisha kuwa ni wajibu kwa anayemwamini Mwenyezi Mungu kumsaidia mumin kwa kila alichonacho kinachoweza kumsaidia, angalau kumtetea anapotajwa kwa ubaya; vinginevyo atakuwa ni mhaini mwingi wa kukanusha. Kuna Hadith sahih isemayo: “ Mwenye kuinyamazia haki ni shetani bubu.

Tatu : Lau ingekuwa mtu akiamini tu, basi anaondokewa na muadui na matatizo, basi wangeliamini watu wote imani ya kibiashara; kama vile anayeiuza dhamiri yake kwa kila mwenye kutoa thamani.

Nne : Imani ya haki ni kumtii Mwenyezi Mungu katika maamrisho yake na hukumu zake zote. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuamrisha, tukitaka kufanya jambo, tufuate sababu za kimaumbile ambazo amezifanya zitekeleze matakwa yetu. Ameziweka sababu za ushindi kuwa ni umoja na kuandaa nguvu, akasema: “Wala msizozane, msije mkavunjika moyo na zikapotea nguvu zenu.” Na akasema: “Na waandalieni nguvu vile muwezavyo.” Juz. 10 (8: 46, 60).

Katika Futuhatul-Mkkiya, Ibnul A’arabiy ameziletea sababu hizi ibara ya mkono wa Mungu. Ameichukua ibara hii katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Je, hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyama wa mifugo wakawa wenye kuwamiliki.” (36:71). Tazama maelezo kwa anuani ya ‘Dini haioteshi ngano’ katika Juz.3 (8: 1-4).

Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.

Waislamu kule Makka walikuwa ni wanyonge, wakipata kila aina ya maudhi na ukandamizwaji kutoka kwa washirikina; na walikuwa hawawezi kujitetetea. Walikuwa wakimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na wakimshitakia dhulma, naye akiwa hana lolote la kuwaambia isipokuwa kuwausia subra. Miongoni mwa aliyokuwa akiwaambia ni: “Mimi sijaamriwa kupigana.”

Mtume alikatazwa kupigana na washirikina katika zaidi ya Aya 70, alipokuwa Makka. kwa sababu kupigana wakati huo ilikuwa ni sawa na kujimaliza. Tazama Juz.5 (4:77).

Baada ya Mtume na Waislamu kuhamia Madina, wakawa na nguvu, ndipo ikashuka Aya hii. Inasemekana kuwa ndio Aya ya kwanza kushuka kuhu- siana na vita.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha sababu ya kutoa ruhusa hii; kwamba washirikina wamewachokoza waislamu, wakawatoa kwenye miji yao kwa dhulma na kwa uadui na akawaahidi waislamu ushindi kwa maadui zao, pale aliposema: “Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.”

Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa kosa pekee la Mtume na swahaba zake kwa washirikina ni kule kusema: “Hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu.” Dhahiri hii ndio walioichukua wafasiri wote; bali mmoja wa wafasiri wapya alisema, ninamnukuu: “Hakuna upinzani kuliko kupinga maisha haya yaliyojikita kwenye tamaa, kupingana masilahi, kutofautiana mielekeo na kugongana matamanio.”

Mara nyingi tumeashiria huko nyuma kwamba utaghuti wa kishirikina uli- upiga vita ujumbe wa Muhammad na neno la Tawhid si kwa lolote isipokuwa linataka kuondoa manufaa, matamanio, masilahi yao na kuwe- ka usawa baina ya watu. Angalia tuliyoyaandika kwa anuani ya ‘Masilahi ndio sababu’ katika Juz. 1 (2: 92-96).

Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi yangelivunjwa mahekalu na makanisa na (sehemu) za kuswalia na misikiti ambayo ndani yake hutajwa jina la Mwenyezi Mungu kwa wingi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwaruhusu waumini, wanaochokozwa, kupigana na washirikina, sasa anabainisha sababu ya ruhusa hiyo; kwamba lau si kuweko na nguvu ya upinzani, basi ingeenea vurugu na ufisadi katika ardhi kwa sababu ya unyang’nyi, uporaji na kumwagika damu; hasa baina ya vikundi na watu wa dini.

Mwenyezi Mungu ameielezea fitna baina ya mataifa kwa ibara ya kuvunjwa sehemu zake za kuabudu. Kwa sababu ndio sehemu muhimu kwa mataifa; na zina alama maalum zinazotofautiana na nyingine. Mahekalu ni ya mayahudi, makanisa ni ya wanaswara (wakiristo), na sehemu za kuswalia ni zamataifa mengineyo. Msikiti unatofautiana na sehemu nyingine kwa kuwa Swala humo ni mara tano, usiku na mchana.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu anawazuwiya waumini na makafiri. Kama itakuwa ni sawa tafsiri hiyo, haiwezi kufaa kila wakati. Usahihi hasa ni tuliouelezea, kuwa ili kuhifadhika amani na nidhamu ni lazima kuweko na nguvu ya upinzani; ni sawa nguvu hiyo iwe mikononi mwa waumini au makafiri.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Hapana budi watu wawe na kiongozi mwema au muovu, atatumiwa na mumin na kafiri, Mwenyezi Mungu atafikisha kwaye muda. Watu watajikusanya kwake waweze kumpiga adui, nia zitakuwa na amani kwaye, mwenye nguvu atakamatwa kwa ajili ya kumuonea mnyonge ili astarehe na kila muovu.”

Kauli hii ya Imam Ali, ilikuwa ni kuwarudi Khawariji waliposema: “Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu.” Angalia tuliyoyaandika kwa anuani hii, kwenye Juz. 12 (12:40).

Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.

Hiki ni kichocheo cha kupigana jihadi ya kuinusuru haki na watu wake.

Wale ambao tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha Swala na wakatoa Zaka na wakaamrisha mema na wakakataza mabaya.

Makusudio ya kumakinishwa hapa ni utawala. Mwenyezi Mungu ameapa kwa msisitizo kwamba Yeye atawasaidia watawala, kwa sharti ya kuweko mambo mawili:

Kwanza : wao wenyewe watekeleze haki ya ibada kwa ukamilifu; kama vile Swala, Saumu na kuamrisha mema na kukataza maovu. Ibada ya kimwili ameileta kwa ibara ya Swala na ibada ya kimali kwa Zaka.

Jambo la pili : ni kufanya uadilifu baina ya watu, kuisimamisha haki na kuibatilisha batili. Hayo ndio makusudio ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Akivunja moja tu ya mawili haya, Mwenyezi Mungu humpuuza na humwacha.

Unaweza kuuliza : Tumewaona watawala wengi wasiomwamini Mungu kabisa, sikwambii kumwabudu kwa kuswali na kutoa Zaka, lakini pamoja na hayo utawala wao umestawi na kufuatwa na raia kwa vile wametimiza malengo ya raia na kuwatumikia, wala raia hawaangalii imani yao. Kwa hiyo, inaonyesha, suala la imani sio sharti la kudumu utawala na ustawi wake?

Jibu : Makusudio ya nusra ya Mwenyezi Mungu, katika Aya, ni kuustawisha utawala katika dunia na thawabu za akhera; bali hii ndio nusra ya kiuhakika. Kwa sababu ufalme wa dunia unaondoka, lakini neema za akhera ni za kudumu bila ya kuwa na ukomo na ni msafi na wa raha kwa pande zake zote.

Mtawala wa dunia anaweza kuustawisha utawala wake duniani akiwa mwadilifu, lakini Akhera akapata adhabu ya kuungua kwa kukufuru kwake dalili za kilimwengu ambazo zinaonyesha kuweko mtengenezaji.

Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.

Yeye peke yake ndio Mfalme wa wafalme, huumpa ufalme amtakaye na humnyima ufalme amtakaye, na yeye ni Muweza wa kila kitu.

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَعَادٌ وَثَمُودُ ﴿٤٢﴾

42. Wakikukadhibisha, basi wamekadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh na kina A’d na Thamud.

وَقَوْمُ إِبْرَاهِيمَ وَقَوْمُ لُوطٍ ﴿٤٣﴾

43. Na kaumu ya Ibrahim na kaumu ya Lut.

وَأَصْحَابُ مَدْيَنَ وَكُذِّبَ مُوسَىٰ فَأَمْلَيْتُ لِلْكَافِرِينَ ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿٤٤﴾

44. Na watu wa Madyan na Musa alikadhibishwa. Nikawapa muda makafiri kisha nikawatia mkononi, basi kulikuwaje kukanya kwangu?

فَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ فَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَبِئْرٍ مُّعَطَّلَةٍ وَقَصْرٍ مَّشِيدٍ ﴿٤٥﴾

45. Na miji mingapi tuliyoiangamiza iliyokuwa ikidhulumu. Ikaangukiana mapaa yake na visima vilivyoachwa na makasri yaliyo madhubuti?

أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾

46. Je, hawatembei katika ardhi ili wapate akili za kuzingatia na masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَن يُخْلِفَ اللَّـهُ وَعْدَهُ وَإِنَّ يَوْمًا عِندَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٤٧﴾

47. Wanakuharakisha ulete adhabu na hakika Mwenyezi Mungu hakhalifu miadi yake. Na hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnavyohisabu.

وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَمْلَيْتُ لَهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ ثُمَّ أَخَذْتُهَا وَإِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿٤٨﴾

48. Ni miji mingapi nimeipa muda na hali ilikuwa imedhu- lumu, kisha nikaitia mkononi? Na kwangu mimi ndio marejeo yote.

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا أَنَا لَكُمْ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٤٩﴾

49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni muonyaji kwenu niliye dhahiri.

فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٥٠﴾

50. Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watapata maghufira na riziki za heshima.

وَالَّذِينَ سَعَوْا فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ ﴿٥١﴾

51. Na wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa motoni.

WAKIKUKADHABISHA

Aya 42 -51

MAANA

Wakikukadhibisha, basi wamekadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh na kina A’d na Thamud na kaumu ya Ibrahim na kaumu ya Lut na watu wa Madyan na Musa alikadhibishwa.

Makuraishi walimkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) na wakamtoa nyumbani kwake, Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake, kwa kumtuliza na kumpoza moyo, kwamba hakuna la ajabu katika yanayokutokea. Kila Nabii alipambana na hayo uliyopamabana nayo.

Kisha akamtajia idadi ya manabii, kwa njia ya mfano tu; akiwemo Hud na watu wake walioitwa A’d, Swaleh na watu wake walioitwa Thamud. Ama watu wa Madyana hao ni watu wa Shuayb. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:34).

Nikawapa muda makafiri kisha nikawatia mkononi, basi kulikuwaje kukanya kwangu?

Makusudio ya kukanya hapa ni adhabu, kwa maana ya kukanya kwa vitendo sio kwa maneno. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwacheleweshea makafiri adhabu mpaka ulipofika muda wake, akawapatiliza kwa upatilizo wa mwenye uweza asiyeshindwa. Aya inaashiria kwamba mwenye akili hatakikani kuharakisha mambo kabla ya kufikia muda wake.

Na miji mingapai tuliyoiangamiza iliyokuwa ikidhulumu.

Baada ya Mwenyezi Mungu kusema kuwa anawapa muda makafiri mpaka wakati maalum, sasa anaishiria kuangamia kwa miji ambayo watu wake wamedhulumu, ambayo ni mingi, kama inavyoashiria kauli yake: ‘Miji mingapi?’ Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:4).

Ikaangukiana mapaa yake?

Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:259) na Juz. 15 (18:42).

Na visima vilivyoachwa na makasri yaliyo madhubuti.

Yote haya yameachwa bila watu; yaani miji ya madhalimu imekuwa mahame, haina watu, ambapo hapo zamani ilikuwa imesheheni wenyeji na wageni wanaoitembelea.

Je, hawatemebei katika ardhi ili wapate akili za kuzingatia na masikio ya kusikilia?

Wanaambiwa wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w. w ) . Yaani hawapati funzo kwa waliyowafikia wakadhibishaji na kuona jinsi miji yao ilivyokuwa mitupu? Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:137) na Juz. 14 (16: 36).

Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.

Kuna faida gani ya kusikia na kuona ikiwa moyo umepofuka? Kwa sababu masikio na macho ni nyenzo na akili ndio asili.

Wanakuharakisha ulete adhabu.

Wanaohimiza ni washirikana na anayehimizwa ni Muhammad(s.a.w.w) . Mtume alikuwa akiwapa kiaga cha adhabu ikiwa watang’ang’ania ushirikina.

Walikuwa wakisema yale waliyosema waliowatangulia kuwaambia mitume kila wanapowakataza ushirikina: “Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni mkweli.”

Na hakika Mwenyezi Mungu hakhalifu miadi yake.

Kuharakisha au kuchelewesha si muhimu madamu ahadi itakuwa. Kuwa hakika ni kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwapa thawabu watiifu ni haki ya wale watiifu, hawezi kuihalifu.

Ama ahadi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ya adhabu kwa waasi, hiyo ni haki yake Mwenyezi Mungu, akitaka anaweza kuitekeleza na akipenda anaweza kusamehe, ila ikiwa imetanguliwa na neno ‘Hatahalifu’ kama ilivyo katika Aya hii tuliyo nayo; ambapo amekanusha kutotekeleza aliyowaahidi makuraishi kutokana na msimamo wao kwa Mtume wa rehema.

Na hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnavyohisabu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia washirikina; kuna haja gani ya kuharakisha adhabu ya Akhera na siku moja kwake ni kali kwenu kuliko adhabu ya miaka elfu katika miaka ya kiduniani? Kwa ufupi ni kuwa miaka elfu ni fumbo la vituko vya siku ya mwisho.

Ni miji mingapi nimeipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, kisha nikaitia mkononi? Na kwangu mimi ndio marejeo yote.

Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii na Sura hii tuliyo nayo Aya 45 na pia sehemu hii tuliyo nayo. Mwenyezi Mungu amerudia kwa kusisitiza na kutoa hadhari.

Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni muonyaji kwenu niliye dhahiri.

Huu ndio umuhimu wa mitume, kufikisha ujumbe na kutoa onyo kwa yule mwenye kuupinga. Maana haya yamekaririka kwa mifumo mbalimbali.

Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watapata maghufira na riziki za heshima.

Maana yako wazi, na yametangulia kwenye Aya kadha, ikiwemo Juz. 1 (2:25).

Na wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa motoni.

Yaani washirikina wataingia motoni kwa muda usiokuwa na ukomo kwa sababu ya kumfanyia inadi Mtume na kujitahidi kumpinga kufikisha ujumbe wa Mola wake na kuwazuilia nao watu.

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ وَلَا نَبِيٍّ إِلَّا إِذَا تَمَنَّىٰ أَلْقَى الشَّيْطَانُ فِي أُمْنِيَّتِهِ فَيَنسَخُ اللَّـهُ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ ثُمَّ يُحْكِمُ اللَّـهُ آيَاتِهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٢﴾

52. Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii anaposoma ila shetani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayoyatumbukiza shetani; kisha Mwenyezi Mungu huzi- makinisha Aya zake na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, mwenye hekima.

لِّيَجْعَلَ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ فِتْنَةً لِّلَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَفِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ ﴿٥٣﴾

53. Ili alifanye lile alilolitumbu iza shetani ni mtihani kwa wale wenye maradhi katika nyoyo zao na wale ambao nyoyo zao zimesusuwaa. Na hakika madhalimu wamo katika uasi wa mbali.

وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَيُؤْمِنُوا بِهِ فَتُخْبِتَ لَهُ قُلُوبُهُمْ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهَادِ الَّذِينَ آمَنُوا إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٤﴾

54. Ili wajue wale ambao wamepewa elimu kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako na zinyenyekee kwake nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye awaongozaye wale ambao wameamini kwenye njia iliyonyooka.

وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي مِرْيَةٍ مِّنْهُ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً أَوْ يَأْتِيَهُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَقِيمٍ ﴿٥٥﴾

55. Na wale ambao wamekufuru hawataacha kuwa katika wasiwasi katika hilo mpaka saa iwafikie ghafla au iwafikie adhabu ya siku tasa.

الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٥٦﴾

56. Ufalme siku hiyo ni wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina yao. Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watakuwa katika Bustani zenye neema.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٥٧﴾

57. Na wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu watapata adhabu ifedheheshayo.

KUSOMA KWA MTUME NA KUJIINGIZA SHETANI

Aya 52 -57

MAANA

Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii anaposoma ila shetani hutumbukiza katika masomo yake.

Wametofautiana wafasiri kuhusu neno Nabii na Mtume, (Nabiy na Rasul)[6] kuwa je, ni ibara zenye maana moja au kila moja ina maana yake?

Kauli iliyo karibu zaidi ni ile isemayo kuwa hakuna tofauti baina yake; kwa vile kila mmoja kati yao anatanabahishwa na Mwenyezi Mungu kwa lile analolitaka. Kwa hiyo akitanabahishwa na kuamrishwa kufikisha yale aliyotanabahishwa, huyo anaitwa Nabii kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtanabahisha na pia anaitwa Mtume kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtumma kufikisha.

Ikiwa amemtanabahisha tu bila ya kumwamuru kufikisha, basi huyo atakuwa ni Nabii tu. Hiyo ni kusema kuwa kila Mtume ni Nabii, lakini sio kila Nabii ni Mtume.

Kuna riwaya inayosema kuwa sababu ya kushuka Aya hii ni kwamba Mtume(s.a.w.w) aliwasomea makuraishi Sura Najm, alipofikia kwenye Aya isemayo:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ ﴿١٩﴾ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ ﴿٢٠﴾

“Je, mmewaona Lata na Uzza na Manata mwingine wa tatu” (53: 19 – 20)

basi shetani aliingiza katika kisomo cha Mtume maneno haya: “Hao ni wazuri watukufu na kwamba maombezi yao bila shaka yanatarajiwa,” yani haya masanamu ni mazuri na uombezi wao unatarajiwa kwa Mwenyezi Mungu.

Maulama wahakiki wamekanusha riwaya hii na wakakata kauli kuwa hiyo ni miongoni mwa uzushi wa wazandiki wanaotaka kukitia ila Kitabu cha Mwenyezi Mungu na utume wa Muhammad(s.a.w.w) .

Wametegemea, katika hilo, kwenye dalili mkataa za kiakili na kinakili. Mtume ambaye ametumwa na Mwenyezi Mungu kupiga vita ushirikina na kuabudu mizimu, halafu huyo huyo arudi kuisifia kwa sifa za ukamilifu! Vipi iwe hivyo na ulimi wa Mtume unamtarjumu na kumbainisha Mwenyezi Mungu? Shetani anaweza kupata nafasi kwenye ubainifu na tafsiri hii ya kimungu?

Usahihi wa maana ya Aya ni kuwa ukomo wa usomaji wa Mtume yeyote, ni kuwafahamisha watu uhakika wa risala yake ili waweze kuifahamu na kuongoka nayo, lakini wenye tamaa wanaingilia kati kwa kuvungavunga na kueneza kila aina ya propaganda.

Haya tumeyashuhudia na kuyaona hasa. Haya ndio maana ya kutumbukiza shetani katika usomi wa Nabii. Nabii anawatakia heri watu na shetani muharibifu anawazuia wasiipate.

Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayoyatumbukiza shetani; kisha Mwenyezi Mungu huzimakinisha Aya zake na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, mwenye hekima.

Wabatilifu wanaunda njama na kuzitangaza, lakini Mwenyezi Mungu huondoa ubatilifu wao na kuufedhehi uwongo wao kwenye ndimi za wakweli na mikononi mwa wapigania jihadi. Aya nyingine yenye maana hii ni ile isemayo:

يُرِيدُونَ أَن يُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّـهُ إِلَّا أَن يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿٣٢﴾

“Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywavyao. Na Mwenyezi Mungu amekataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wamechukia.” Juz.10 (9:32).

Ili alifanye lile alilolitumbukiza shetani ni mtihani kwa wale wenye maradhi katika nyoyo zao na wale ambao nyoyo zao zimesusuwaa.

Wenye maradhi katika nyoyo ni wezi wanaoishi kwa unyang’anyi, uporaji, ghushi na utapeli. Ama waliosusuwaa nyoyo zao ni wale ambao ni bendera hufuata upepo. Maana ni kuwa kampeni za uwongo hazina nafasi isipokuwa kwa wezi na walio na bendera.

Popote utakapoelekea utakuta picha hii waziwazi; hasa kwenye magazeti, idhaa, vitabu, michezo ya kuigiza na katika mazungumzo ya vibaraka na wale wanaodanganywa ambao wanaamini kila wanayoambiwa bila ya kuchunguza; tena ni wengi.

Kisha kampeni za uwongo, hata kama zitakuwa zina madhara kwa upande fulani, lakini zina manufaa kwa upande mwingine. Kwa sababu zinamtambulisha muhaini na mwenye ikhlasi, vile vile mjinga na mjuzi. Haya ndio makusudio ya neno mtihani.

Na hakika madhalimu wamo katika uasi wa mbali.

Kila mwenye kuvungavunga na akafanya uzushi basi ni dhalimu, na kila mwenye kuusadikisha uwongo na uzushi bila ya kuuchuunguza pia huyo ni dhalimu.

Ili wajue wale ambao wamepewa elimu kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako na zinyenyekee kwake nyoyo zao.

Neno ‘hiyo’ hapa ni hiyo Qur’an. Pia inaweza kufasirika ‘huyo’ kwa maana ya huyo Nabii. Maana ni kuwa, ikiwa mtu atasadikisha uwongo juu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi wenye maarifa na ikhlasi, wanajua hakika ya uwongo na uzushi huo; jambo ambalo linawazidishia imani na mshikamano kwa Mwenyezi Mungu, mitume yake na vitabu vyake na pia unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu.

Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye awaongozaye wale ambao wameamini kwenye njia iliyonyooka.

Anawaongoza Mwenyezi Mungu kwenye njia yake na kuifuata kwa kujikurubisha kwake hata kukiwa na kampeni za uwongo na vikwazo kiasi gani.

Na wale ambao wamekufuru hawataacha kuwa katika wasiwasi kati- ka hilo mpaka saa iwafikie ghafla au iwafikie adhabu ya siku tasa.

Makusudio ya saa ni ile saa ya kutoka watu kuelekea kwa Mola wao wakitokea makaburini (Kiyama). Siku tasa ni siku ya hisabu. Utasa ni kinaya cha makafiri kukata tamaa ya kuokoka.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kueleza, katika Aya iliyotangulia, kuwa wenye elimu wanaamini Qur’an na utume wa Muhammad(s.a.w.w) , kwenye Aya hii anasema kuwa makafiri wako katika shaka kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu na watendelea kuwa katika shaka hiyo mpaka siku ya kufufuliwa kwao makaburini au siku ya kusimama kwao mbele ya Mwenyezi Mungu kwa hisabu.

Na hapo ndipo itawafichukia hakika yao na watajua kuwa wao walikuwa kwenye upotevu.

Ufalme siku hiyo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake, hakuna kadhi au amiri wala raisi au waziri; kama ilivyo katika maisha haya ya duniani.Atahukumu baina yao . Yaani baina ya makafiri na waumini.

Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watakuwa katika Bustani zenye neema. Na wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu watapata adhabu ifedheheshayo.

Hawa watapata hizaya na moto na wale watapata Pepo na raha. Mfano wa Aya hizi umekwishatangulia mara nyingi.

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

وَدَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ إِذْ يَحْكُمَانِ فِي الْحَرْثِ إِذْ نَفَشَتْ فِيهِ غَنَمُ الْقَوْمِ وَكُنَّا لِحُكْمِهِمْ شَاهِدِينَ ﴿٧٨﴾

78. Na Daud na Suleiman walipohukumu juu ya shamba, walipolisha humo mbuzi wa watu usiku. Na sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao.

فَفَهَّمْنَاهَا سُلَيْمَانَ وَكُلًّا آتَيْنَا حُكْمًا وَعِلْمًا وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ وَكُنَّا فَاعِلِينَ ﴿٧٩﴾

79. Tukamfahamisha Suleiman na kila mmoja wao tukampa hukumu na elimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imsabihi (Mwenyezi Mungu). Na sisi tulikuwa ni wenye kuifanya.

وَعَلَّمْنَاهُ صَنْعَةَ لَبُوسٍ لَّكُمْ لِتُحْصِنَكُم مِّن بَأْسِكُمْ فَهَلْ أَنتُمْ شَاكِرُونَ ﴿٨٠﴾

80. Na tukamfundisha kutengeneza mavazi ya vita ili kuwakinga katika mapigano yenu. Je, mtakuwa wenye kushukuru?

وَلِسُلَيْمَانَ الرِّيحَ عَاصِفَةً تَجْرِي بِأَمْرِهِ إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا وَكُنَّا بِكُلِّ شَيْءٍ عَالِمِينَ ﴿٨١﴾

81. Na upepo mkali kwa ajili ya Suleiman, wendao kwa amri yake, katika ardhi tuliyoibariki. Na sisi ndio tunaojua kila kitu.

وَمِنَ الشَّيَاطِينِ مَن يَغُوصُونَ لَهُ وَيَعْمَلُونَ عَمَلًا دُونَ ذَٰلِكَ وَكُنَّا لَهُمْ حَافِظِينَ ﴿٨٢﴾

82. Na katika mashetani kuna wanompigia mbizi na kufanya kazi nyinginezo; Nasi tulikuwa walinzi wao.

DAUD NA SULEIMAN

Aya 78 – 82

MAANA

Na Daud na Suleiman walipohukumu juu ya shamba, walipolisha humo mbuzi wa watu usiku. Na sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao.

Kuna riwaya iliyo mashuhuri midomoni mwa wapokezi, kwamba watu wawili walikwenda kuamuliwa kwa Daud. Mmoja alikuwa na mimea na wa pili alikuwa na mifugo ya mbuzi na kondoo. Mwenye shamba akasema wanyama wa huyu bwana wamelisha kwenye mimea yangu usiku. Baada ya kumthibitikia hilo, Daud alitoa hukumu kuwa wanyama wawe wa mwenye shamba.

Suleiman alipojua hivyo akasema, ni vizuri mwenye shamba awachukue wanyama, anufaike nao lakini wasiwe wake kabisa, na mwenye wanyama achukue ardhi aishghulikie mpaka iwe kama ilivyokuwa kabla ya kuliwa. Kisha bada ya hapo kila mmoja achukue mali yake. Daud akapendezewa na hukumu ya mwanawe na akaitumia.

Dhahiri ya Aya inaafikiana na riwaya hii. Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kwamba yeye amesema: “Linaloafikiana na Qur’an lichukueni na linalokhalifiana nalo liacheni.”

Unaweza kuuliza : Kila mmoja kati ya Daud na Suleiman ni Nabii na Nabii ni maasumu; hasa katika hukumu ya sharia na hukumu ya sawa, sasa je kuna wajihi gani wa kupingana hukumu mbili hizi?

Baadhi wamejibu kuwa kauli ya Daud ilikuwa ni upatanishi sio hukumu. Lakini ijulikane kuwa upatanishi unakuwa kwa baadhi ya mali sio yote na Daud hakumbakishia mfugaji hata mnyama mmoja.

Wengine wakasema kuwa kila mmoja kati ya manabii wawili hao alihukumu kwa ijitihadi yake. Kauli hii vile vile ina kasoro; kwamba Nabii anatumia ijitihadi kama ulama wengine na inajulikana kuwa rai ya ijtihadi inakuwa kwa kukosekana nukuu (Nass) na ilivyo ni kuwa kauli ya Nabii ni nukuu ya haki; na kwamba ijitihadi ina uwezekano wa kupatia na kukosea, jambo ambalo haliswihi kwa maasumu.

Jamaa wamesema kuwa hukumu ilikuwa kama alivyopitisha Daud; kisha ikabadilishwa (naskh), na kauli ya Suleiman[2]

Kauli hii ina nguvu zaidi kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Tukamfahamisha Suleiman na kila mmoja wao tukampa hukumu na elimu.

Hapo Mwenyezi Mungu anashudia kuwa kila mmoja ni mjuzi wa hukumu. Kwa hiyo basi kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Tukamfahamisha Suleiman’ ni kwamba yeye alimpelekea wahyi wa kubadilisha hukumu ya baba yake. Mafaqihi wametofautiana kuwa je mwenye mifugo atalipa kilichoharibiwa na wanyama wake?

Maliki na Shafi wamesema kuwa atalipa kilichoharibiwa usiku sio mchana. Abu Hanifa akasema halipi kwa hali yoyote; iwe usiku au mchana.

Jamaa katika mafaqihi wa kishia wamesema kama alivyosema Maliki na Shafi na wahakiki katika wao wakasema kuwa litakaloangaliwa ni hali ya uzembe wa mfugaji au la; sio hali ya kuwa usiku au mchana. Ikiwa mfugaji atazembea au kufanya makusudi, basi atalipa. Na ikiwa atajichunga na asipuuze, ikatokea bahati mbaya basi hatalipa.

Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imsabihi (Mwenyezi Mungu). Na sisi tulikuwa ni wenye kuifanya.

Imekuwa mashuhuri kuwa Daud alikuwa na sauti nyororo. Majaribio yamethibitisha kuwa wanyama wengi wanaburudika na aina fulani ya nyimbo na muziki [3] 2. Niliwahi kusoma kwenye gazeti kwamba nyoka aliwahi kutoka kwenye tundu yake ili astarehe na nyimbo za Ummu Kulthum, katika moja ya hafla yake. Nyimbo ilipokwisha akarudi sehemu yake.

Ama tasbibih ya mlima ni kwa njia ya majazi na kusifia zaidi tu; kama kusema: Amelichekesha na kuliliza jiwe. Au inawezekana ni kiuhakika hasa. Kwa sababu yule aliyeweza kuufanya moto kuwa baridi na salama kwa Ibrahim, ndiye anaweza pia kulifanya jabali litoe tasbih pamoja na Daud.

Angalia Aya 69 ya Sura hii tuliyo nayo.

Na tukamfundisha kutengeneza mavazi ya vita ili kuwakinga katika mapigano yenu. Je, mtakuwa wenye kushukuru?

Makusudio ya mavazi ya vita hapa ni deraya. Aya inaonyesha kuwa Daud ndiye mtu wa kwanza kutengeneza deraya.

Kuna riwaya inayoelezea kwamba sababu ya hilo ni kuwa Daud alikuwa ni mfalme wa Israil na alikuwa ana desturi ya kupita mitaani kujulia hali za watu, bila ya yeye kujulikana. Siku moja akakutana na mtu akamuuliza kuhusu sera za mfalme Daud.

Yule mtu akasema: Ana sera nzuri sana, kama asingekuwa anakula kwenye hazina ya serikali. Daud akaapa kuwa kuanzia siku hiyo hatakula kitu isipokuwa kilichotokana na mikono yake na jasho lake.

Alipojua Mwenyezi Mungu ikhlasi yake na ukweli wa nia yake, alimalainishia chuma na kumfundisha kutengeneza deraya.

Iwe sahihi riwaya hii au la, ni kwamba inaashria wajibu wa kufanya bidii kubwa kuchunga masilahi ya watu na mali zao. Kuna Hadith mutawatir kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad(s.a.w.w) , alifariki akiwa ameweka rahani deraya yake kwa sababu ya kukopa kiasi fulani cha shayir, huku zikiwa mali za Bara arabu zote ziko mikononi mwake.

Na upepo mkali kwa ajili ya Suleiman, wendao kwa amri yake, kati- ka ardhi tuliyoibariki. Na sisi ndio tunaojua kila kitu.

Dhahiri ya Aya hii inafahamisha kuwa upepo ulikuwa ukimchukua Suleiman kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Wala hakuna haja ya kuleta taawili, maadamu akili inakubaliana na dhahiri hiyo.

Aya iliyo wazi zaidi ya hii ni ile isemayo: “Na Suleiman tukamtiishia upepo mwendo wake asubuhi ni mwezi mmoja na mwendo wake jioni yake ni mwezi mmoja.” (34:12) Yaani asubuhi unakwenda mwendo wa mwezi mmoja kwa kusafiri na ngamia na jioni vile vile.

Makusudio ya ardhi iliyobarikiwa ni ile iliyotajwa kwenye Aya ya 71 ya Sura hii.

Unaweza kuuliza : Hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema upepo mkali na mahali pengine anasema: pole pole: “Na tukamtiishia upepo uendao polepole kwa amri yake.” (38:36). Je, kuna wajihi gani wa Aya zote mbili?

Jibu : Huwa mara unakwenda kwa kasi na mara nyingine polepole kulin- gana na amri yake; sawa na gari au ndege.

Na katika mashetani kuna wanompigia mbizi baharini na kumtolea lulu na marijani.

Makusudio ya mashetani hapa ni majini

Na kufanya kazi nyinginezo ; kama kujenga mihirabu na picha:

يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِن مَّحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَّاسِيَاتٍ ﴿١٣﴾

“Wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu na picha na masinia makubwa, kama hodhi na masufuria makubwa yasiyoondolewa mahali pake.” (34:13).

Nasi tulikuwa walinzi wao, kwamba wasitoroke na kufanya ukorofi. Hatuna la kuongeza zaidi ya ulivyothibisha wahyi kuwepo majini na kwamba wao walimtumikia Suleiman na akili hailikatai hilo. Kwa hiyo basi hakuna haja yoyote ya kuleta taawili na kuyazungusha maneno. Imam Ali(a.s) amesema:“Lau kama mtu angeliweza la kumfanya adumu ulimwenguni au kuhepa mauti, basi angelikuwa Suleiman ambaye alitiishiwa ufalme, majini watu, utume na heshima kuu.”

وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٨٣﴾

83. Na Ayyub aliopomlingania Mola wake: Hakika mimi imenigusa dhara, nawe ndiye unayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu.

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَكَشَفْنَا مَا بِهِ مِن ضُرٍّ وَآتَيْنَاهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةً مِّنْ عِندِنَا وَذِكْرَىٰ لِلْعَابِدِينَ ﴿٨٤﴾

84. Basi tukamkubalia na tukamuondolea dhara na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema itokayo kwetu na ukumbusho kwa wafanyao ibada.

وَإِسْمَاعِيلَ وَإِدْرِيسَ وَذَا الْكِفْلِ كُلٌّ مِّنَ الصَّابِرِينَ ﴿٨٥﴾

85. Na Isamil na Idris na Dhulkifl, wote walikuwa miongoni mwa wanaosubiri.

وَأَدْخَلْنَاهُمْ فِي رَحْمَتِنَا إِنَّهُم مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿٨٦﴾

86. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao ni katika watu wema.

وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾

87. Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhabika na akadhani kuwa hatutamdhikisha. Basi aliita katika giza kwamba: Hapana Mola isipokuwa wewe, umetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

88. Basi tukamkubalia na tukamwokoa kutokana na ghamu. Kama hivyo tunawaokoa wenye kuamini.

وَزَكَرِيَّا إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ رَبِّ لَا تَذَرْنِي فَرْدًا وَأَنتَ خَيْرُ الْوَارِثِينَ ﴿٨٩﴾

89. Na Zakaria alipomwita Mola wake: Ewe Mola wangu! Usiniwache peke yangu na wewe ndiye mbora wa wanaorithi.

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ ﴿٩٠﴾

90. Basi tukamwitikia na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi kufanya kheri na wakituomba kwa hofu na walikuwa wakitunyenyekea.

وَالَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهَا مِن رُّوحِنَا وَجَعَلْنَاهَا وَابْنَهَا آيَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿٩١﴾

91. Na mwanamke aliyelinda tupu yake na tukampulizia katika roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni ishara kwa walimwengu.

NA AYYUB ALIOPOMLINGANIA MOLA WAKE

Aya 83 – 91

MAANA

Na Ayyub aliopomlingania Mola wake: Hakika mimi imenigusa dhara, nawe ndiye unayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu. Basi tukamkubalia na tukamuondolea dhara.

Makusudio ya dhara ni madhara ya nafsi, kama vile maradhi, kutokana na neno la kiarabu dhurr.

Likisomwa dharr ndio linakuwa na maana ya madhara ya kila kitu. Wafasiri na wapokezi wengi wamepokea riwaya nyingi zinazomuhusu Ayyub. Tunalolifahamu sisi, kutokana na Aya zinazomzungumzia kwa uwazi na kwa ishara hapa na pia katika Sura Swad (38), ni kwamba Ayyub alikuwa na afya yake nzuri akiwa hana matatizo yoyote. Kisha mabalaa yakaanza kumwandama kila upande, akawa ni wa kupigiwa mifano.

Masaibu yalimpata yeye mwenyewe binafsi; akavumilia uvumilivu wa kiungwana; na akabakia na yakini yake na kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu. Huzuni wala machungu hayakumfanya aache kumtii Mwenyezi Mungu. Lakini muda ulivyomzidi na machungu nayo yakazidi, alimshtakia

Mwenyezi Mungu mambo yake kwa maneno mawili tu: “Imenigusa dhara, nawe ndiye unayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu,” na wala hakulalamika kwa kusema balaa gani hii iliyoniandama.

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwitikia maombi yake na akamuondolea mabalaa na kumrudisha katika hali nzuri zaidi ya alivyokuwa.

Na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema itokayo kwetu na ukumbusho kwa wafanyao ibada.

Mwenyezi Mungu alimruzuku watoto na wajukuu zaidi ya wale aliowakosa, ikiwa ni rehema na malipo ya uvumilivu wake; na pia kukumbusha kwamba mwenye kuwa na subra na uvumilivu kama wa Ayyub, basi mwisho wake utakuwa kama wa Ayyub. Mwenyezi Mungu amehusisha kuwataja wenye kuabudu kwa kuashiria kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na mwenye subra aliye na ikhlasi kwa kauli yake na vitendo vyake.

Huu ndio ujumla wa maelezo ya Aya zinazofungamana na Ayyub; bila ya kuingilia ufafanuzi walioutaja wapokezi na wasimulizi. Kwani huo hauam- batani na itikadi wala uhai kwa mbali wala karibu. Miongoni mwa njia za Qur’an ni kukitaja kisa kwa yale yaliyo na mazingatio yenye kunufaisha na mawaidha ya kukanya.

Na Isamil Na Idris Na Dhulkifl, wote walikuwa miongoni mwa wanao- subiri. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao ni katika watu wema.

Ismail alifanya subra ya kukubali kuchinjwa na akawa na uvumilivu wa kukaa katika nchi isiyokuwa na mimea wala kinywewa. Idris tumemueleza katika Juz. 16 (19:56).

Ama Dhulkifl wengi wamesema alikuwa Mtume; na baadhi wakasema alikuwa ni mja mwema tu na sio Mtume. Sisi tunaamini kwamba yeye ni miongoni mwa waliokuwa na subira na waja wema, kwa kufuata Qur’an ilivyosema, na wala hatutaulizwa zaidi ya hayo.

Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhabika na akadhani kuwa hatutamdhikisha. Basi aliita katika giza kwamba: Hapana Mola isipokuwa wewe, umetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.

Dhun-Nun ni Yunus. Maana ya neno ‘Nun” ni samaki. Mwenyezi Mungu anasema:

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُن كَصَاحِبِ الْحُوتِ ﴿٤٨﴾

“Na vumilia hukumu ya Mola wako wala usiwe kama sahibu wa samaki” (68:48).

Hali ameghadhibika ni kuwaghadhibikia watu wake. Neno kudhikishwa limefasiriwa kutokana na neno Naqdira alyh; kama lilivyotumika mahali pengine:

وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ ﴿٧﴾

“Na yule ambaye imekuwa dhiki riziki yake” (65:7).

Makusudio ya katika giza hapa ni ndani ya tumbo la samaki.

Maana kwa ujumla ni: kumbuka ewe Muhammad habari ya Yunus alipowalingania watu wake, lakini hawakumwitikia mwito wake, akawaondokea kwa kuwakasirikia, akadhani kuwa hatutamdhikisha kwa kumzuia n.k. Alipomezwa na samaki akataka uokovu kutoka kwetu,basi tukamkubalia na tukamwokoa kutokana na ghamu. Kama hivyo tunawaokoa wenye kuamini.

Makusudio ya ghamu hapa ni tumbo la samaki; na kuokoka, ni kutolewa humo hadi kwenye nchi kavu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:98).

Na Zakaria alipomwita Mola wake: Ewe Mola wangu! Usiniwache peke yangu na wewe ndiye mbora wa wanaorithi. Basi tukamwitikia na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 ( 3: 38) na Juz. 16 (19:7).

Hakika wao walikuwa wepesi kufanya kheri na wakituomba kwa hofu na walikuwa wakitunyenyekea.

Wao ni Zakariya, mkewe na Yahya au wale Mitume waliotangulia kutajwa. Wote walifanya kheri kwa kutaka thawabu za Mwenyezi Mungu na kuhofia adhabu yake na walikuwa wakimfuata Mwenyezi Mungu katika kila jambo.

Na mwanamke aliyelinda tupu yake na tukampulizia katika roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni ishara kwa walimwengu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3: 45) na Juz. 16 (19: 16).

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SABA

إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ ﴿٩٢﴾

92. Hakika umma wenu huu ni umma mmoja, na mimi ni Mola wenu kwa hivyo niabuduni.

وَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ كُلٌّ إِلَيْنَا رَاجِعُونَ ﴿٩٣﴾

Na wakalivunja jambo lao baina yao. Wote watarejea kwetu.

فَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا كُفْرَانَ لِسَعْيِهِ وَإِنَّا لَهُ كَاتِبُونَ ﴿٩٤﴾

94. Na atendaye mema naye ni mumin, basi haitakataliwa bidii yake na hakika sisi tutamwandikia.

وَحَرَامٌ عَلَىٰ قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا أَنَّهُمْ لَا يَرْجِعُونَ ﴿٩٥﴾

95. Na ni haramu kwa mji tuliouangamiza kwamba wao hawatarejea.

حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُم مِّن كُلِّ حَدَبٍ يَنسِلُونَ ﴿٩٦﴾

96. Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju, wakawa wanateremka kutoka kila mlima.

وَاقْتَرَبَ الْوَعْدُ الْحَقُّ فَإِذَا هِيَ شَاخِصَةٌ أَبْصَارُ الَّذِينَ كَفَرُوا يَا وَيْلَنَا قَدْ كُنَّا فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا بَلْ كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٩٧﴾

97. Na miadi ya haki itakaribia, ndipo yatakapokodoka macho ya wale waliokufuru. Ole wetu! Hakika tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa ni wenye kudhulumu.

إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ ﴿٩٨﴾

98. Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.

لَوْ كَانَ هَـٰؤُلَاءِ آلِهَةً مَّا وَرَدُوهَا وَكُلٌّ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٩٩﴾

99. Lau haya yangelikuwa ni miungu yasingeliingia na wote watadumu humo.

لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَهُمْ فِيهَا لَا يَسْمَعُونَ ﴿١٠٠﴾

100. Lao humo ni kupiga mayowe na wala hawatasikika.

UMMA MMOJA

Aya 92 – 100:

MAANA

Hakika umma wenu huu ni umma mmoja, na mimi ni Mola wenu kwa hiyo niabuduni.

LUGHA

Maana ya neno umma ni watu wenye lugha moja na historia moja. Kisha neno hili likawa linatumika zaidi kwa maana ya dini na mila. Maana haya ndiyo yaliyokusudiwa hapa.

Umma wenu huu ni itikadi ya mitume ambayo ni tawhid pamoja na kufuata amri za Mwenyezi Mungu kwa kauli na vitendo. Msemo ‘wenu’ unaelekezwa kwa watu wote.

Maana ni kuwa enyi watu wote! Shikeni dini ya Tawhidi waliyokuwa nayo Mitume na mumwabudu Mungu mmoja aliye peke na mumfanyie ikhlasi katika kauli na vitendo.

Na wakalivunja jambo lao baina yao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamrisha wote wawe kwenye itikadi ya tawhidi, lakini wakagawanyika wakawa makundi ya wakana Mungu na washirikina. Hata wale wafuasi wa Mitume nao wanatukanana na kujitenga na wengine; bali hata wafuasi wa Mtume mmoja nao ni hivyo hivyo.

Wote watarejea kwetu.

Haya ni makemeo na hadhari kwa wale wanaofarikiana wakawa vikundi.

Na atendaye mema naye ni mumin, basi haitakataliwa bidii yake na hakika sisi tutamwandikia.

Imani pamoja na matendo mema ni njia ya Peponi na imani bila ya matendo haifai chochote. Hiyo ni kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ﴿١٥٨﴾

“Basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake.” Juz. 8 (6:158).

Ama matendo mema bila ya imani, humnufaisha mtendaji kwa namna moja au nyingine na huenda ikamfaa huko Akhera kwa kupunguziwa adhabu. Tumeyafafanua hayo katika Juz. 4 (3:158) kwenye kifungu ‘kafiri na amali njema’ Pia Umepita mfano wake katika Juz. 14 (16: 97)

Na ni haramu kwa mji tuliouangamiza kwamba wao hawatarejea.

Aya hii ni jawabu la swali la kukadiria, kwamba je, washirikina katika watu wa kijiji kilichoangamizwa na Mwenyezi Mungu kwa kufuru yao, watarudishwa tena kuwa hai na kuadhibiwa huko Akhera, kama walivyoadhibiwa duniani?

Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa watu wote, kesho watarejea kwa Mwenyezi Mungu; hata wale walioangamizwa duniani kwa dhambi zao na ni muhali kukosa kurejea kwa Mwenyezi Mungu baada ya mauti; bali hakuna budi lazima watafufuliwa.

Swali la pili : je inafaa kuadhibiwa akhera baada ya kuadhibiwa duniani? Huko si ni kuadhibu mara mbili kwa kosa moja?

Jibu : Hapana! Kuadhibiwa kwao duniani kulikuwa ni kwa ajili ya kuwakadhibisha kwao Mitume waliowajia na miujuza; kama zinavyofahamisha Aya hizi zifuatazo na nyinginginezo mfano wake:

وَقَوْمَ نُوحٍ لَّمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ ﴿٣٧﴾

“Na kaumu ya Nuh walipowakadhibisha Mitume tuliwagharikisha” (25:37)

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ ﴿١٢﴾ وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ ﴿١٣﴾ وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ ﴿١٤﴾

“Kabla yao walikadhibisha kamu ya Nuh na watu wa Rassi na Thamud na A’d na Firauni na ndugu wa Lut na watu wa vichakani na kaumu ya Tubbai, wote waliwakadhibisha Mitume, kwa hiyo kiaga kikathibitika juu yao.” (50: 12-14).

Ama adhabu ya Akhera ni ya ukafiri wenyewe na madhambi mengineyo; kama dhulma n.k.

Kwa hiyo adhabu zinakuwa nyingi kutokana na dhambi kuwa aina nyingi, sio kwa dhambi moja.

Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju, wakawa wanateremka kutoka kila mlima.

Katika Juz. 16 (18: 94) tuliwanukuu baadhi ya wafasiri wakisema kuwa Juju ni wa Tatars na Majuju ni Wamongoli. Vile vile tumesema huko kuwa ukuta wa Juju na Majuju hauko tena. Kwa hiyo basi makusudio ya kufunguliwa Juju na Majuju ni kuenea kwao katika mabara.

Vyovyote iwavyo sisi hatujawahi kusoma ya kutegemewa kuhusu Juju na Majuju, si katika tafsiri wala mahali penginepo. Kwa hiyo tutasimama kwenye dhahiri ya nukuu ya Qur’an tu na ufafanuzi tutawachia wengine.

Na miadi ya haki itakaribia, ndipo yatakapokodoka macho ya wale waliokufuru.

Makusudio ya miadi ya haki hapa ni Kiyama, hapo akili za waliokufuru zitapotea na macho yatatoka kutokana na vituko vya siku hiyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14: 42).

Ole wetu! Hakika tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.

Yaani watasema hivyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:5) na katika juzuu na Sura hii tuliyo nayo Aya 14 na 46.

Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.

Hapa wanaambiwa washirikina wa Makka. Makusudio ya mnayoyaabudu ni masanamu yao. Maana ni kuwa, enyi washirikina! Nyinyi na masanamu yenu mtakutana kwenye Jahannamu kesho. Kuna Hadithi isemayo: “Mtu yuko pamoja na anayempenda.”

Unaweza kuuliza : Kuna faida gani ya kutiwa masanamu kwenye Jahannamu na ni mawe yasiyokuwa na utambuzi wala hisiya?

Wafasiri wamejibu kuwa lengo ni kuwazidishia masikitiko wale wanaoyaabudu, kila watakapoyaona karibu nao. Lakini jawabu hili ni kiasi cha kuchukulia uzuri na hisia tu. Lilio bora ni kuicha Aya nyingine ijibu:

فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ﴿٢٤﴾

“Basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, uliowekewa makafiri.” Juz. 1 (2:24).

Kuna riwaya isemayo kuwa Ibn Az-Zab’ariy – mmoja wa washirkina wa kikuraishi na mshairi wao – aliingilia Aya hii kama mayahudi wanamwabudu Uzayr na wanaswara (wakristo) wanamwabudu Masihi na hawa wawili ni watu wa Peponi, kama anavyosema Muhammad, sasa vipi aseme kila kinachoabudiwa ni kuni?

Mtume akamjibu: Ni ujinga ulioje wako wewe kutojua lugha ya watu wako. Kwani huoni herufi ma (ambayo) ni ya visivyo na akili?

Zaidi ya hayo maneno yanawahusu washirikina wa kikurashi, kama tulivyotangulia kusema nao wanaabudu masanamu.

Lau haya yangelikuwa ni miungu yasingeliingia na wote watadumu humo.

Haya ni ishara ya masanamu. Maana ya Aya yako wazi, kwamba lau masanamu yangelikuwa miungu yasingeliiingia motoni. Ni kama kusema: Lau ungelikuwa mwaminifu usingelifanya khiyana, lakini umefanya khiyana kwahiyo wewe si mwaminifu. Mfano huu katika mantiki unaitwa kutoa dalili kwa kipimo cha kuvua (istithnaiyy).

Lao humo ni kupiga mayowe na wala hawatasikika.

Hapa anaambiwa kila mkosaji, awe mwislamu au kafiri. Humo ni humo ndani ya Jahannam. Maana ni kuwa kila mkosaji atakuwa katika Jahannam akilalama kwa machungu; hatasikia neno la upole wala huruma, bali atakayemuona atamtahayariza na kumsema:

وَقِيلَ لِلظَّالِمِينَ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْسِبُونَ ﴿٢٤﴾

“Na wenye kudhulumu wataambiwa onjeni yale mliyokuwa mkiyachuma.” (39:24).

إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ ﴿١٠١﴾

101. Hakika wale ambao umewatangulia wema kutoka kwetu, hao watatenganishwa na hayo.

لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ ﴿١٠٢﴾

102. Hawatasikia mvumo wake. Nao watudumu katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.

لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَـٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿١٠٣﴾

103. Hiyo fazaa kubwa haitawahuzunisha. Na Malaika watawapokea: Hii ndiyo siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.

يَوْمَ نَطْوِي السَّمَاءَ كَطَيِّ السِّجِلِّ لِلْكُتُبِ كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ وَعْدًا عَلَيْنَا إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ ﴿١٠٤﴾

104. Siku tutakapozikunja mbingu mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika sisi ni wenye kufanya.

وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِي الزَّبُورِ مِن بَعْدِ الذِّكْرِ أَنَّ الْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِيَ الصَّالِحُونَ ﴿١٠٥﴾

105. Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa Ardhi watairithi waja wangu walio wema.

إِنَّ فِي هَـٰذَا لَبَلَاغًا لِّقَوْمٍ عَابِدِينَ ﴿١٠٦﴾

106. Hakika katika haya kuna ujumbe kwa wafanyao ibada.

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾

107. Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.

ARDHI WATARITHI WAJA WANGU WALIO WEMA

Aya 101 – 107

MAANA

Hakika wale ambao umewatangulia wema kutoka kwetu, hao watatenganishwa na hayo.

Mwenyezi Mungu aliwaahidi wenye takua kuamiliana nao kwa wema. Miongoni mwa wema huo ni kuokoka na moto.

Hawatasikia mvumo wake.

Hii ni kusisitiza watakavyokuwa mbali nao.

Nao watudumu katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.

Watasalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu wakineemeshwa kwenye Pepo yake.

Hiyo fazaa kubwa haitawahuzunisha, sikwambii ndogo tena.

Kwani fazaa zina daraja, kuanzia machungu ya kukata roho, upweke wa kaburini, kisha kutoka makaburini kwa ajili ya hisabu hadi kuingia Jahannam.

Na Malaika watawapokea: Hii ndiyo siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.

Malaika watawapokea kwa takrima na kuwaambia kuwa Mwenyezi Mungu amewakusanya kwenye siku hii aliyowaahidi kwa ufalme wa daima na neema isiyokatika. Aya hizi tatu zinafupilizwa na neno:

هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ ﴿٦٠﴾

“Je, malipo ya hisani si ni hisani tu.” (55:60)

Au neno:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ﴿٢٦﴾

“Kwa wafanyao wema ni wema.” Juz.11 (10:26).

Siku tutakapozikunja mbingu mkunjo wa karatasi za vitabu.

Makusudio ya vitabu hapa ni maandishi ya matamko yanayoayaandikwa kwenye karatasi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atazikunja sayari, siku ya Kiyama, pamoja na ukubwa na wingi wake; kama inavyokunjwa karatasi yenye maandishi; kiasi ambacho kila sayari itafanana na herufi au neno lilo kwenye karatasi.

Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika sisi ni wenye kufanya.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amefananisha ufufuo na kuumba kwa kwanza; kwamba, kama kulivyowezekana kwa kwanza, basi kwa pili pia kuunawezekana. Si muhali kwa Mwenyezi Mungu kutekeleza ahadi yake.

Hilo halimshindi Mwenyezi Mungu; kwani mwenye kuumba ulimwengu basi hawezi kushindwa kuurudisha tena baada ya kuharibika na kutawanyika:

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ ﴿٢٧﴾

“Na Yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurudisha. Na hilo ni jepesi zaidi kwake” (30:27).

TENA MAHDI ANAYENGOJEWA

Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa Ardhi watairithi waja wangu walio wema.

Zaburi ni kitabu cha Daud na ukumbusho ni vitabu vya mbinguni vilivyotangulia; kama vile vitabu vya Ibrahim na Musa. Maana yake ni kuwa utawala wa dunia, ingawaje hivi sasa uko mikononi mwa mataghuti waovu, lakini Mwenyezi Mungu atauhamisha uende kwa walio wema. Hilo halina budi. Hapo amani na uadilifu utaenea ardhini na watu wote wataneemeka na kheri za Ardhi na baraka zake.

Kuna Hadithi nyingi zenye maana ya Aya hii; miongoni mwazo ni ile aliy- oipokea Abu Daud katika Kitabu cha Sunan, ambacho ni mojawapo ya Sahihi sita: “Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu:

Lau haitabakia katika dunia isipokuwa siku moja tu, basi Mwenyezi Mungu angeliirefusha siku hiyo mpaka amtume mtu kutoka katika watu wa nyumba yangu (Ahlu bayt) jina lake linafanana na jina langu, na jina la baba yake ni kama la baba yangu, ataijaza ardhi uadilifu baada ya kujazwa dhulma na jeuri” [4] .

Kanuni ya maisha hailikatai hilo, bali inalithibitisha na kulisisitiza. Ikiwa nguvu hivi sasa ziko mikononi mwa unyama wenye kudhuru wa umoja wa mataifa, baraza la usalama n.k. basi hakuna litakalozuia, siku moja kugeuka nguvu hiyo kutoka mikononi mwa madhalimu waovu hadi kwa watu wa haki na uadilifu; bali maumbile yanapenda kujikomboa na dhulma.

Pia kuna misingi isemayo: “Kila kilicho katika ardhi kina harakati, kama ilivyo na harakati ardhi na kwamba kudumu hali ni muhali.” Yote hayo yanapelekea kuwa hatimaye nguvu zitakuwa mikononi mwa wema wanao- faa.

Hakika katika haya kuna ujumbe kwa wafanyao ibada.

Haya ni haya ya kuwa ardhi itarithiwa na waja wema; hata kama ni baada ya muda. Makusudio ya wafanyao ibada hapa ni wale wanaopata mawaidha kwa kuzingatia na kunufaika na maonyo.

Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) . Risala yake ni rehema kwa wa mwanzo na wa mwisho. Huko nyuma tumeeleza mara nyingi kuhusu misingi ya risala hiyo na mafunzo yake.

Inatosha, kuthibitisha hilo, kauli za mwenye risala hiyo; kama vile: “Hakumwamini Mwenyezi Mungu yule ambaye watu hawamwamini. Likikuhuzunisha ovu na likakufurahisha jema, basi wewe ni mumin.”

Ni kwa hisia hizi ndio uadilifu utasimama, amani kuenea na maisha kuwa bora. Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu hilo katika Juz. 7 (6:92).

قُلْ إِنَّمَا يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَهَلْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٨﴾

108. Sema: Hakika umeletwa wahyi kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Je nyinyi mmesilimu?

فَإِن تَوَلَّوْا فَقُلْ آذَنتُكُمْ عَلَىٰ سَوَاءٍ وَإِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ أَم بَعِيدٌ مَّا تُوعَدُونَ ﴿١٠٩﴾

109. Kama wakikataa, basi sema: Nimewatangazia sawasawa. Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa.

إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ مِنَ الْقَوْلِ وَيَعْلَمُ مَا تَكْتُمُونَ ﴿١١٠﴾

110. Hakika Yeye anajua kauli ya dhahiri na anajua mnayoyaficha.

وَإِنْ أَدْرِي لَعَلَّهُ فِتْنَةٌ لَّكُمْ وَمَتَاعٌ إِلَىٰ حِينٍ ﴿١١١﴾

111. Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.

قَالَ رَبِّ احْكُم بِالْحَقِّ وَرَبُّنَا الرَّحْمَـٰنُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ ﴿١١٢﴾

Akasema: Mola wangu! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasifia.

HAKIKA MUNGU WENU NI MMOJA TU

Aya 108 – 112

MAANA

Sema: Hakika umeletwa wahyi kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Je nyinyi mmesilimu?

Mwenyezi Mungu alimwarisha Mtume wake awaambie washirikina kuwa Mwenyezi Mungu ameniletea wahyi kwamba Yeye ni mmoja tu hana mshirika katika kuumba kwake na wala katika ujuzi wake.

Ulimwengu huu na maajabu yake na kanuni zake unashuhudia kwa uwazi juu ya umoja, uweza na ukuu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Basi kwa nini hamuamini na kufuata amri yake? Kwanini mnadanganyika kuacha kumwabudu Yeye na kwenda kuabudu mawe yasiyodhuru wala kunufaisha?

Kama wakikataa, basi sema: Nimewatangazia sawasawa.

Baada ya kuwalazimu hoja ya kufikisha na maonyo, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu awaambie kuwa nimekishatekeleza wajibu wangu na nikafikisha risala ya Mola wangu. Kwa hiyo haukubaki udhuru wowote kwenu.

Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa.

Mimi nina yakini na adhabu yenu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameiahadi na kuwahadhirisha nayo, na ahadi yake Mwenyezi Mungu ni ya kweli na adhabu yake pia ni kali zaidi, lakini sijui itakuwa lini. Ni sawa iwe karibu au mbali, lakini ina wakati wake. Ngojeni nami niko pamoja nanyi katika wenye kungojea.

Hakika Yeye anajua kauli ya dhahiri na anajua mnayoyaficha.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:7).

Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.

Sijui kuna hekima gani ya kupewa kwenu muda na kucheleweshewa adhabu. Je Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaka kumdhirisha kila mmoja hakika yake, aweze kutubia mwema na aendelee mouvu au ametaka mustarehe siku zilizobakia kwenye umri wenu? Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye.

Akasema (Muhammad): Mola wangu! Hukumu kwa haki.

Yaani idhihirishe haki na uwanusuru watu wake kwa wale wanaoipinga.

Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasema kuwa masanamu yenu ni miungu na madai yenu kwangu kuwa ni mzushi.

Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wewe ni mtukufu kwa kila anayekuzulia. Wema ni wa yule anayekufuata, akachukua athari yako na akamwambia mzushi, kama vile ulivyosema wewe:

Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasifia.

MWISHO WA SURA YA ISHIRINI NA MMOJA


4

5

6