TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE Juzuu 18

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 11214
Pakua: 2121


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 11214 / Pakua: 2121
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE Juzuu 18

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

Sura Ya Ishirini Na Tatu: Al-Mu’minun. Imeshuka Makka ina Aya 118.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾

1. Hakika wamefaulu waumini.

الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾

2. Ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao.

وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾

3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.

وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾

4. Na ambao kwa Zaka ni watendaji.

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾

5. Na ambao wanazilinda tupu zao.

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾

6. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume. Kwani si wenye kulaumiwa.

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾

7. Lakini anayetaka kinyume cha hayo basi hao ndio wapetukao mipaka.

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾

8. Na wale ambao wanachunga amana zao na ahadi zao.

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾

9. Na ambao Swala zao wanazihifadhi.

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾

10. Hao ndio warithi.

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

11. Watakaorithi Firdausi, wadumu humo.

HAKIKA WAMEFAULU WAUMINI

Aya 1-11

MAANA

Kila mwenye kusema: Lailaha illa llah Muhammadur rasulullah (Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu) atastahiki yale yanayowastahiki waislamu, naye atawapatia wanayostahiki waislamu kutoka kwake. Hiyo ni katika maisha ya hapa duniani. Ama maisha ya akhera, hiyo peke yake haitatosha kumpatia thawabu za Mwenyezi Mungu na radhi zake mpaka awe amekusanya mambo yafutayo:-

1.Hakika wamefaulu waumini ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao.

Kunyenyekea ni kinyume cha kiburi na kujikweza. Mwenyezi Mungu anasema: "Wananyeyekea kwa udhalili." (42:45). Kunyenyekea katika Swala ni natija ya kuwa na yakini na Mwenyezi Mungu na kuhofia adhabu yake. Swala bila ya yakini si chochote wala lolote. Imam Ali(a.s ) anasema: "Kulala na yakini ni bora kuliko kuswali na shaka."

2. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.

Mumin wa kweli upuuzi na batili haimfanyi aache Mwenyezi Mungu. Imam Ali(a.s) anasema:"Hakika mawalii wa Mungu ni wale ambao wanaangalia ndani ya dunia wakati watu wanapoangalia nje yake na wanajishugulisha na ya baadaye wakati watu wakijishughulisha na ya sasa." Akasema tena:"Mwenye kuangalia kasoro zake hatajishugulisha na kasoro za wengine."

3.Na ambao kwa Zaka ni watendaji.

Angalia tuliyoyaandika kuhusu Zaka katika Juz. 3 (2:272-274).

4.Na ambao wanazilinda tupu zao isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume. Kwani si wenye kulaumiwa.

Makusudio ya iliyowamiliki mikono yao ya kuume ni wajakazi. Hivi sasa hawako tena. Zina ni miongoni mwa madhambi makubwa na uchafu katika sharia ya kiislamu. Kwenye jamii yoyote zina ikienea basi inabomoka.

Lakini anayetaka kinyume cha hayo basi hao ndio wapetukao mipaka.

Yaani atakayetaka kumwingilia asiyekuwa mkewe au mjakazi, basi atakuwa amepituka mipaka ya Mwenyez Mungu na anastahiki ghadhabu yake na adhabu yake.

Unaweza kuuliza kuwa : je, kauli yake Mwenyezi Mungu:"Lakini anayetaka kinyume cha haya" inachanganya kujitoa manii kwa mkono kunakojulikana kwa jina la punyeto (Kujipuli)?

Jibu : ndio. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amehalalisha mke na mjakazi na akaharamisha kinyume cha hivyo kwa namna yoyote ile itakayokuwa. Ndio maana mafakihi wote wakaharamisha, isipokuwa Hanafi na Hambali wamesema inaruhusiwa kwa yule anayehofia kuingia kwenye haramu. Tazama Ruhulbayan cha Ismail Haqqiy.

Imam Jafar Sadiq(a.s) aliulizwa kuhusu punyeto (Kujipuli). Akasema:ni dhambi kubwa. Muulizaji akamuuliza iko wapi kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Imam akasoma:Lakini anayetaka kinyume cha hayo … Kisha akasema:Ponyeto ni kinyume cha hayo.

5.Na wale ambao wanachunga amana zao na ahadi zao.

Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu amana na wajibu wa utekelezaji wake katika Juz. 5 (4:58). Ahadi ni kila aliloliamrisha Mwenyezi Mungu na kulikataza. Mwenyezi Mungu anasema: "Na tekelezeni ahadi yangu. Nitatekeleza ahadi yenu" Juz. 1(2: 40).

6.Na ambao Swala zao wanazihifadhi wakidumu nazo kwa wakati wake.

Tumefafanua kuhusu Swala katika Juz. 1 (2:3, 110).

Hao ndio warithi, watakaorithi Firdausi, wadumu humo.

Mumin yoyote atakayekuwa na mambo hayo yaliyotajwa, basi atastahiki Pepo, kama anavyostahiki mrithi mirathi kutoka kwa jamaa yake wa karibu. Wapi na wapi urithi wa dunia unaoisha na mabalaa yake na urithi wa akhera na neema zake za kudumu!

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾

12. Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.

ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾

13. Kisha tukamjaalia awe tone katika makao yaliyo makini.

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾

14. Kisha tukaumba tone kuwa pande la damu na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama, na pande la nyama tukaliumba kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji.

ثُمَّ إِنَّكُم بَعْدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ ﴿١٥﴾

15. Kisha hakika nyinyi baada ya hayo ni maiti.

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ ﴿١٦﴾

16. Kisha hakika nyinyi siku ya Kiyama mtafufuliwa.

وَلَقَدْ خَلَقْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعَ طَرَائِقَ وَمَا كُنَّا عَنِ الْخَلْقِ غَافِلِينَ ﴿١٧﴾

17. Hakika tumeumba juu yenu tabaka saba. Nasi katika kuumba si wenye kughafilika.

KUUMBWA MTU NA MBINGU

Aya 12 -17

MWENYEZI MUNGU NA MTU

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria kwenye Aya nyingi kuhusu kuumbwa mtu; sio kwa kuwa tujue tumetoka wapi, tumepatikana vipi na tuko vipi tu, iwe ni basi. Hapana! Bali ni tuuatumbue ukuu wa muumbaji katika kutuumba kwetu, kama tunavyoutambua katika kuumba mbingu na ardhi.

Tunapaswa tumwamini na tuende na mwongozo wake kwa kutumai kupata thawabu zake na kuepukana na adhabu yake.

Miongoni mwa Aya hizo ni ile isemayo:

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا ﴿١﴾

"Hivi ulimfikia mtu wakati fulani hakuwa kitu kinachotajwa?" (76:1).

Ndio! Hakuwa kitu kinachotajwa kisha akawa kitu. Ama yule ambaye amemfanya aweko kutoka asikokuwako, anatutanabahisha pale aliposema:

'Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.'

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu Mtukufu ameonyesha chimbuko la mtu, vipi alivyomgurisha kutoka hali moja hadi nyingine. Lengo la kwanza katika hilo ni kujua dalili za kuweko muumba na utukufu wake, tufikirie na tumwangalie kiumbe huyu wa ajabu katika sura yake, umbile lake, akili yake na utambuzi wake.

Mtu huyu Mwenye historia na maendeleo, kiumbe huyu ambaye ana nguvu na uwezo kuliko kiumbe yeyote mwengine, ambaye wajuzi wameileza taadhima yake hii kwa neno: "Na kwako wewe umekunjwa ulimwengu mkubwa," ametokea wapi na ameumbwa kutokana na nini?

Aya inatujibu kwamba yeye ameumbwa kutokana na udongo uliotokana na mchanga na maji, katika asili ambayo imeumbiwa wadudu na mimea. Hapa ndio pana dalili na hoja. Kwani inavyojulikana ni kuwa kitu kimoja hakiwezi kutoa vitu viwili vinavyopingana, utambuzi na kutotambua; upofu na kuona. Kwa hiyo hapa kuna siri wala hakuna tafsiri ya siri hii isipokuwa kwa nguvu yenye uwezo na yenye ujuzi wa kitu hicho.

Ni nguvu hii ambayo imefarikisha na kupamabanua baina ya vitu viwili vinavyopingana ambavyo vimeumbwa kwa asili moja. Baada ya kuashiria malengo ya Aya zinazozungumzia kuumbwa kwa mtu, sasa tunabainisha makusudio ya Aya tulizonazo.

MAANA

Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.

Makusudio ya mtu hapa ni mwanadamu, sio Adam mwenyewe. Kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia: 'Kisha tukamjaalia awe tone' inafahamisha hivyo. Adamu na wanawe wote wanatokana na udongo uliotokana na mchanga na maji. Tofauti ni kuwa Adam ameumbwa kutokana na mchanga na maji, moja kwa moja; na wanawe ni kupitia chakula kinachozalikana kutokana na ardhi na maji.

Kisha tukamjaalia awe tone katika makao yaliyo makini katika uti wa mgongo wa baba hadi kwenye mfuko wa uzazi wa mama.

Kisha tukaumba tone kuwa pande la damu na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:5).

Na pande la nyama tukaliumba kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama.

Pande la nyama akaligawanya mifupa, mishipa na nyama, kisha kwenye mkusanyiko huo akaumba aina mbali mbali. Ufafanuzi uko katika elimu ya upasuaji.

Kisha tukamfanya kiumbe mwengine mtu aliye kamili kama siye yule aliyekuwa tone damu nyama n.k.

Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji.

Wala hakuna kitu kinachofahamisha hakika hii kuliko kuumbwa ulimwengu na nidhamu yake na kuumbwa mtu na ubainifu wake, moyo wake, akili yake n.k. Tunakariri tuliyoyasema mara kwa mara, kwamba imekuwa ni desturi ya Qur'an Tukufu kutegemeza mabadiliko ya ulimwengu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Yeye, ambaye umetukuka utukufu wake, ndiye sababu ya kuumbwa ulimwengu.

Kisha hakika nyinyi baada ya hayo ni maiti.

Na anayekufa marejeo yake ni kwa muumba wake.

Kisha hakika nyinyi siku ya Kiyama mtafufuliwa muulizwe mliyokuwa mkiyafanya.

MAANA YA MBINGU SABA

Hakika tumeumba juu yenu tabaka saba. Nasi katika kuumba si wenye kughafilika.

Wakati wa kufasiri Juz. 1 (2: 29), nilisema kuwa kutajwa mbingu saba hakufahamishi kuwa ni hizo hizo tu, na kwamba sababu ya kutajwa kwake huenda ikawa ni kwa mambo yanayohusika hapo. Nilitosheka na kauli hiyo wakati huo, kwa sababu mimi si mjuzi zaidi wa hilo, kwani si mtaalamu wa elimu ya falaki.

Nilipofikia kufasiri Aya hii tuliyo nayo nikasoma makala ya kisayansi katika jarida la Misr liitwalo Akhbar la tarehe 17 Julai 1969, yenye kichwa cha maneno 'Mwenyezi Mungu na mtu na mwezi,' kama ifutavyo:-

"Imethibitishwa kisayansi kwamba katika anga za mbali kuna aina za ulimwengu zaidi ya ulimwengu huu tunaoishi - yaani mkusanyiko wa sayari tunazoziona kwa macho makavu au kwa darubini - na kwamba kila ulimwengu katika aina hizo una jua lililo na nguvu zaidi ya hili jua letu linaongaza kila siku kwenye ardhi; na pembezoni mwake kunazunguka nyota kadhaa.

Haiwezekani kufikia kwenye sayari yoyote katika sayari hizo pamoja na kwamba tuna vyombo vilivyoweza kugundua sehemu hizo, kutokana na umbali wa kasi ya mwanga kufikia huko. Jua na nyota za sehemu hizo ziko mbali nasi kwa mwendo wa kasi ya mwanga ya mamilioni ya miaka. Lau kama tutakadiria mtu kusafiri kufikia huko, basi itamchukua mamilioni ya miaka kwa kasi ya mwanga kuweza kuifikia sayari iliyo karibu zaidi ya ulimwengu huo. Hii ndio hakika iliyothibitishwa na sayansi na wamekubaliana nayo wataalam wa kisasa."

Kwa hiyo basi makusudio ya mbingu saba ni ulimwengu (dunia) wa aina saba na sio sayari saba, kwamba kila ulimwengu una sayari na nyota zake zisizokuwa na idadi na kwamba mtu hawezi kuzifikia kwa sababu hawezi kuishi mamiloni ya miaka. Ama ardhi saba zilizoashiriwa katika (65:12) ni kuwa katika ulimwengu huo wa aina saba kila mmoja una sayari ya ardhi.

وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَسْكَنَّاهُ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّا عَلَىٰ ذَهَابٍ بِهِ لَقَادِرُونَ ﴿١٨﴾

18. Na tumewateremshia kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza ardhini. Na hakika sisi ni wenye uwezo wa kuyaondoa.

فَأَنشَأْنَا لَكُم بِهِ جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ لَّكُمْ فِيهَا فَوَاكِهُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿١٩﴾

19. Basi kwa maji hayo tukawafanyia bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi na katika hayo mnakula.

وَشَجَرَةً تَخْرُجُ مِن طُورِ سَيْنَاءَ تَنبُتُ بِالدُّهْنِ وَصِبْغٍ لِّلْآكِلِينَ ﴿٢٠﴾

20. Na mti utokao katika Mlima Sinai unaotoa mafuta na kitoweo kwa walaji.

وَإِنَّ لَكُمْ فِي الْأَنْعَامِ لَعِبْرَةً نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهَا وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٢١﴾

21. Na hakika katika wanyama howa mna mazingatio. Tunawanywesha katika vile vilivyomo matumboni, na mnapata katika hao manufaa mengi, Na katika hao mnawala.

وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ ﴿٢٢﴾

22. Na juu yao na juu ya majahazi mnabebwa.

TUKATEREMSHA MAJI KUTOKA MBINGUNI

Aya 18 – 22

MAANA

Na tumewateremshia kutoka mbinguni maji kwa kiasi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa hatukughafilika na viumbe, alipigia mfano wa hilo kwa kuteremsha maji kutoka mbinguni kwa kiasi kile kinachowafaa watu; si kingi cha kuwadhuru wala kichache cha kudhuru mimea.

Na tukayatuliza ardhini katika chemchemi, visima, mabawa na mito, ili yawafae watu wakati wa kiangazi.

Na hakika sisi ni wenye uwezo wa kuyaondoa.

Yule aliyeweza kuyaleta bila shaka anaweza kuyaondoa kwa kuyazuia au kuyakausha yasiweze kuwafaa, lakini hakufanya hivyo kwa kuwahurumia.

Basi kwa maji hayo tukawafanyia bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi na katika hayo mnakula.

Imehusishwa kutajwa mitende na mizabibu kwa sababu waarabu wakati huo walikuwa hawajui kingine zaidi yake.

Na mti utokao katika Mlima Sinai unaotoa mafuta na kitoweo kwa walaji.

Makusudio ya mti utokao Mlima Sinai ni mzaituni. Mlima Sinai ni ule mlima aliozungumza Musa na Mola wake na kitoweo ni mafuta ambayo hutengenezwa siagi ya kutowelea mkate.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kutaja aina hizi tatu kwa sababu ni miti mitukufu zaidi na ina manufaa mengi, lakini ukweli ni kuwa ilikuwa ndio iliyoenea zaidi kwa waarabu.

Umetangulia mfano wake mara nyingi. Angalia kwenye Juz. 14 (16:10).

Na hakika katika wanyama howa; ngamia ng'ombe, mbuzi na kondoo,mna mazingatio mtakayoyazingatia.

Tunawanywesha katika vile viliomo matumboni, maziwa na mnapata katika hao manufaaa mengi, yakiwa ni pamoja sufu, manyoya na ngozi zake. Na katika hao mnawala nyama yake.

Na juu yao na juu ya majahazi mnabebwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Umetangulia mfano wake katika Aya nyingi. Angalia Juz. !4 (16:5).

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٢٣﴾

23. Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je, hamna takua?

فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُرِيدُ أَن يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً مَّا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي آبَائِنَا الْأَوَّلِينَ ﴿٢٤﴾

24. Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu. Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, hakika angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.

إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ بِهِ جِنَّةٌ فَتَرَبَّصُوا بِهِ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٢٥﴾

25. Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi ngojeni kwa muda.

قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٢٦﴾

26. Akasema: "Mola wangu! Nisaidie kwa kuwa wamenikadhibisha.

فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ فَاسْلُكْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ مِنْهُمْ وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ ﴿٢٧﴾

27. Tukampa wahyi: Tengeneza jahazi mbele ya macho yetu. Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize wa kila namna dume na jike, wawili na ahli zako, isipokuwa ambaye kauli imekwishatangulia juu yake katika wao. Wala usinitajie hao waliodhulumu, Hakika wao watagharikishwa.

فَإِذَا اسْتَوَيْتَ أَنتَ وَمَن مَّعَكَ عَلَى الْفُلْكِ فَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي نَجَّانَا مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٨﴾

28. Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, sema, sifa njema (Alhamdulillah) ni za aliyetuokoa na watu madhalimu.

وَقُل رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ ﴿٢٩﴾

29. Na sema, Mola wangu! niteremshe mteremsho wenye baraka na wewe ndiwe mbora wa wateremshaji.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ وَإِن كُنَّا لَمُبْتَلِينَ ﴿٣٠﴾

30. Hakika katika hilo kuna ishara na kwa hakika sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.

NUH

Aya 23-30

MAANA

Kila yaliyokuja kwenye Aya hizi yametangulia kutajwa katika Juz. 12 (11: 25-49) yamemaliza zaidi ya kurasa 22, kwa hiyo hapa tutazipitia juu juu tu.

Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je, hamna takua?

Aliwalingania kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake na kuwahadharisha na shirki. Wale wapenda anasa wakahofia vyeo vyao na chumo lao. Wakaanzisha kampeni za uongo na kuwatatiza watu kwa shubha za ubatilifu. Mwenyezi Mungu amezitaja tatu miongoni mwazo:

1.Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu.

Walisema, vipi Nuh awe ni nabii naye ni mtu kama nyinyi. Yeye hana lengo la utume katika mwito wake isipokuwa anataka kuwa raisi na nyinyi muwe raia wake. Hii ndio lugha ya wafanyi biashara, wanafasiri faida katika kila kitu.

2.Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, hakika angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.

Hawakusikia kuwa Mwenyezi Mungu alituma mitume, vilevile hawakusikia kuwa Mungu wa ulimwengu wote ni mmoja. Kwa hiyo Nuh si Mtume na miungu ni mingi, yakiwemo masanamu yao. Hakuna tofauti baina ya mantiki haya na mantiki ya anayesema: mimi siamini kuweko kwa sayari ya Mars kwa sababu sijafika huko.

3.Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu.

Walileta uongo huu wakijua fika kuwa ni uongo; kama walivyokuwa maquraishi na uhakika wa wa uzushi wao pale waliposema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) amerogwa na ni mwendawazimu.

Basi ngojeni kwa muda. Yaani mngojeni Nuh afe au awache mwito wake.

Akasema: "Mola wangu! Nisaidie kwa kuwa wamenikadhibisha.

Alikimbilia kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu na akamtaka msaada baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.

Tukampa wahyi: Tengeneza jahazi mbele ya macho yetu.

Ni kinaya cha kuichunga kwake Mwenyezi Mungu safina. Na wahyi wetu yaani na amri yetu.

Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri; yaani maji yatakapochimbuka kutoka ardhini.

Hapo waingize wa kila namna dume na jike, wawili na ahli zako, isipokuwa ambaye kauli imekwishatangulia juu yake katika wao.

Yaani isipokuwa mke wake Nuh na mwanawe ambaye inasemekana jina lake ni Kanani.

Wala usinitajie hao waliodhulumu, Hakika wao watagharikishwa.

Yaani usiniombe kuokoka wale ambao neno la adhabu limekwishahakika kwao; hata mkeo na mwanao pia.

Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, sema, sifa njema (Alhamdulillah) ni za aliyetuokoa na watu madhalimu.

Katika Aya hii kuna somo muhimu sana, nalo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapomwangamiza taghuti haitakikani kunyamaza yule aliyedhulumiwa; bali amuhimidi Mwenyezi Mungu kwa kuokoka kwake na kuangalia kuangamia kwake kuwa ni nyenzo tu sio lengo.

Na sema: Mola wangu! Niteremshe mteremsho wenye baraka na wewe ndiye mbora wa wateremshaji.

Niteremshe kutoka jahazini kwa namna ambayo utanihifadhi na uovu mimi na watu wangu na aliyeamini, kwani wewe ni mtermshaji na muhifadhi bora.

Hakika katika hilo kuna ishara na kwa hakika sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.

Yaani sisi tumewafanyia mtihani waja kwa kuwapelekea mitume na kuteremsha vitabu, ili kupambanua muovu na mwema na aonekane wazi wazi kila mmoja wao alipwe thawabu au adhabu, kiasi anachostahiki.

ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ ﴿٣١﴾

31. Kisha baada yao tukaanzisha karne nyingine.

فَأَرْسَلْنَا فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٣٢﴾

32. Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kwamba mumwabudu Mwenyezi Mungu! Hamna Mungu asiyekuwa Yeye, je hamuogopi?

وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِلِقَاءِ الْآخِرَةِ وَأَتْرَفْنَاهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يَأْكُلُ مِمَّا تَأْكُلُونَ مِنْهُ وَيَشْرَبُ مِمَّا تَشْرَبُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na wakuu katika watu wake waliokufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binadamu kama nyinyi, anakula mlacho na anakunywa mnywacho.

وَلَئِنْ أَطَعْتُم بَشَرًا مِّثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٣٤﴾

34. Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.

أَيَعِدُكُمْ أَنَّكُمْ إِذَا مِتُّمْ وَكُنتُمْ تُرَابًا وَعِظَامًا أَنَّكُم مُّخْرَجُونَ ﴿٣٥﴾

35. Je, anawaahidi ati mtakapokufa na mkawa mchanga na mifupa kwamba mtatolewa?

هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ لِمَا تُوعَدُونَ ﴿٣٦﴾

36. Hayawi! Hayawi hayo mnayoahidiwa.

إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ ﴿٣٧﴾

37. Hakuna ila maisha yetu ya dunia tu, tunakufa na tunaishi. Wala sisi si wenye kufufuliwa.

إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا وَمَا نَحْنُ لَهُ بِمُؤْمِنِينَ ﴿٣٨﴾

38. Huyo si lolote ila ni mtu anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo, wala sisi si wenye kumwamini.

قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٣٩﴾

39. Akasema: Mola wangu, ninusuru kwa wanavyonikanusha.

قَالَ عَمَّا قَلِيلٍ لَّيُصْبِحُنَّ نَادِمِينَ ﴿٤٠﴾

40. Akasema: Baada ya muda mchache hakika watakuwa ni wenye kujuta.

فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ بِالْحَقِّ فَجَعَلْنَاهُمْ غُثَاءً فَبُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٤١﴾

41. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki. Tukawafanya takataka zinazoelea juu ya maji, ikapotelea mbali kaumu ya madhalimu.

HUD

AYA 31-41

KISHA BAADA YAO TUKAANZISHA KARNE NYINGINE

Makusudio ya karne hapa ni watu. Mwenyezi Mungu hakuweka wazi ni akina nani hao. Wafasiri wamesema hao ni A'd, kaumu ya Hud. Na hii ni sawa kwa dalili ya yaliyokuja katika Juz.8 (7:65). Yametangulia maelezo katika Juz. 12 (11: 50 - 65). Kwa hiyo tutapita juu juu, kwenye Aya hizi, kama tulivyopita kwenye Aya zilizotangulia hizi.

Tukawapelekea Mtume mingoni mwao.

Mwenyezi Mungu alimtuma Hud kwa A'd naye ni miongoni mwao.

Kwamba mumwabudu Mwenyezi Mungu! Hamna Mungu asiyekuwa Yeye, je hamuogopi?

Aliwapa watu wake mwito wa tawhid na kuacha shirk kwa kutoa bishara ya radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake na kutoa onyo la hasira za Mweyezi Mungu na adhabu yake.

Na wakuu katika watu wake waliokufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binadamu kama nyinyi, anakula mlacho na anakunywa mnywacho.

Maadamu yuko hivyo hivyo basi hana tofauti wala ubora, basi vipi mnamtii.

Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.

Wao ndio wako hasarani kiiudhahiri na kiuhalisi kutokana na kumuasi kwao Nabii. Lakini wamepindua na wakaufinika uhakika. Haya ndiyo mazoweya ya matwaghuti na wanaodeka kila mahali na kila wakati.

Je, anawaahidi ati mtakapokufa na mkawa mchanga na mifupa kwamba mtatolewa?

Makaburini kuwa hai kama mlivyo sasa. Hiki ni kitu cha ajabu.

Hayawi! Hayawi hayo mnayoahidiwa kuwa kuna ufufuo baada ya mauti. Hakuna ila maisha yetu ya dunia tu, tunakufa na tunaishi. Wala sisi si wenye kufufuliwa.

Kwa sababu aliyekufa na yake yamekwisha. Huu ni ubainifu wa yaliyotangulia, ya kuona kwao muhali kufufuliwa baada ya mauti, wakiwa wameghafilika kwamba aliyewaumba kwanza ndiye huyo huyo atakayewarudisha; na kwamba hilo ni rahisi zaidi kuliko kuanzisha, kama ni sawa ibara yao.

Huyo si lolote ila ni mtu anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo, wala sisi si wenye kumwamini.

Hawamwamini Hud kwa sababu anasema uongo juu ya Mwenyezi Mungu, lakini kuabudu kwao masanmu ndio ikhlasi ya kweli kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na takua!! Aliye mtupu zaidi katika watu ni yule anayefanya uovu kisha akajiona amefanya wema.

Akasema: Mola wangu, ninusuru kwa wanavyonikanusha.

Alisema hivi baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.

Akasema - Mwenyezi Mungu -baada ya muda mchache hakika watakuwa ni wenye kujuta, kutokana na shirki yao na uasi wao ambapo Mwenyezi Mungu atawapatiliza kwa mpatilizo wa mwenye nguvu mwenye uwezo.

Basi ukawanyakua ukelele kwa haki.

Makusudio ya ukelele ni adhabu. Kusema kwake kwa haki ni ishara ya kuwa wanastahili adhabu kutokana na waliyoyafanya.

Tukawafanya takataka zinazoelea juu ya maji.

Yaani wako sawasawa na vitu duni vinavyoelea kwenye maji.

Ikapotelea mbali kaumu ya madhalimu.

Wamepotelea mbali na Mwenyezi Mungu na twaa yake naye akawaweka mbali na fadhila zake na rehema zake.

ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قُرُونًا آخَرِينَ ﴿٤٢﴾

42. Kisha baada yao tukaanzisha karne niyingine.

مَا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٤٣﴾

43. Hapana umma unaoweza kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.

ثُمَّ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا تَتْرَىٰ كُلَّ مَا جَاءَ أُمَّةً رَّسُولُهَا كَذَّبُوهُ فَأَتْبَعْنَا بَعْضَهُم بَعْضًا وَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ فَبُعْدًا لِّقَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٤٤﴾

44. Kisha tukawapeleka mitume wetu mmoja baada ya mmoja. Kila umma alipowafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatishia baadhi yao wengine, ikapotelea mbali kaumu isiyoamini.

ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٤٥﴾

45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye Harun pamoja na ishara zetu, na hoja zilizo wazi.

إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا عَالِينَ ﴿٤٦﴾

46. Kwenda kwa Firaun na wakuu wake, lakini wakajivu- na na walikuwa ni kaumu waliojikweza.

فَقَالُوا أَنُؤْمِنُ لِبَشَرَيْنِ مِثْلِنَا وَقَوْمُهُمَا لَنَا عَابِدُونَ ﴿٤٧﴾

47. Wakasema: Je, tuwaamini watu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?

فَكَذَّبُوهُمَا فَكَانُوا مِنَ الْمُهْلَكِينَ ﴿٤٨﴾

48. Basi wakawakadhibisha wakawa miongoni mwa walioangamizwa.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٤٩﴾

49. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.

وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَىٰ رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ ﴿٥٠﴾

50. Tukamfanya mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni ishara. Na tukawapa kimbilio kwenda mahali palipoinuka, penye utulivu na chemchem za maji.

KILA UMMA ULIKANUSHA MTUME WAKE ALIPOWAFIKIA

Aya 42-50

MAANA

Kisha baada yao tukaanzisha karne niyingine.

Baada yao ni baada ya A'd na karne ni watu. Watu wa kwanza kuja baada ya A'd ni Thamud, kwa dalili ya yaliyoelezwa katika Juz. 8 (7:74)

Hapana umma unaoweza kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.

Kila kitu isipokuwa, Mwenyezi Mungu (s.w.t), kina muda wake hauchelewi wala kuja haraka. Miongoni mwa hayo ni kuangamia wale waliokadhibisha mitume yao. Adhabu ilikuwa ikawajia ghafla bila ya kutambua wala kuhisi.

Kisha tukawapeleka mitume wetu mmoja baada ya mmoja.

Mitume walikuwa wakija mmoja baada ya mwingine. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) alijaalia kila umma uwe na mtume.

Kila umma alipowafikia Mtume wao walimkanusha au kumuua. Si kwa lolote ila ni kwa kuwa amekuja na ambayo matamanio yao yanayakataa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Kila alipowajia Mtume kwa yale yasiyoyapenda nafsi zenu, mlijivuna, kundi moja mkalikadhibisha na kundi jingine mkaliua." Juz. 1 (2:87)

Tukawafuatishia baadhi yao wengine.

Yaani Mwenyezi Mungu aliangamiza umma uliomkadhibisha Mtume wake mmoja baada ya mwingine na akajaalia ni mazingatio kwa mwenye kuzingatia na habari watayoinukuu kizazi baada ya kizazi kingine.

Ikapotelea mbali kaumu isiyoamini haki wala kuitumia.

Kisha tukamtuma Musa na nduguye Harun pamoja na ishara zetu, kama vile fimbo kugeuka nyoka na kumeremeta mkono, na hoja zilizo wazi za kunyamazisha.

Kwenda kwa Firaun na wakuu wake, lakini wakajivuna na walikuwa ni kaumu waliojikweza.

Kuna kujikweza gani na majivuno makubwa zaidi ya kauli ya Firaun:

فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾

"Mimi ni Mola wenu mkuu." (79:24)

Au pale aliposema:

مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي ﴿٣٨﴾

"Simjui kwa ajili yenu mungu asiyekuwa mimi." (28:38).

Watu wengi wana moyo kama wa Firaun, wanaweza kudai uungu kama watakuwa na nyenzo na kupata watakaomwitikia kama alivyopata Firaun.

Wakasema: "Je, tuwaamini watu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?"

Firauni alidai uungu na akawaadhibu waisrail kwa kuwachinja watoto wao wa kiume na kuwaacha wa kike. Na Musa na Harun ni katika waisrail; vipi watawafuata?

Basi wakawakadhibisha wakawa miongoni mwa walioangamizwa. Kila anayepituka mipaka mwisho wake ni maangamizi tu. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.

Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat na wanaotakiwa kuongoka ni wana wa Israil, lakini hawakuongoka na wala hawataongoka kamwe baada ya kuipotoa Tawrat, wakafuata matamanio yao na wakaijaza dunia ufisadi na upotevu.

Kisa cha Musa kimekaririka mara nyingi kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Tumebainisha sababu ya kukaririka kisa katika Juz. 16 (20:9) Kifungu cha 'Kukaririka kisa cha Musa.'

Tukamfanya mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni ishara.

Yaani muujiza. Isa ni muujiza kwa sababu amezaliwa bila ya Baba na Mama yake ni mujiza kwa vile amezaa bila ya mume. Tazama Juz. 3 (3:45-51).

Na tukawapa kimbilio kwenda mahali palipoinuka. Makusudio ni Palestina, kwa sababu Bwana Masih alizaliwa hapo, napo ni penye utulivu na chemchem za maji.