TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 14093
Pakua: 2360


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 25 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14093 / Pakua: 2360
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Mwendelezo Wa Sura ya Ishirini Na Saba.

أَمَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا بِهِ حَدَائِقَ ذَاتَ بَهْجَةٍ مَّا كَانَ لَكُمْ أَن تُنبِتُوا شَجَرَهَا أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ بَلْ هُمْ قَوْمٌ يَعْدِلُونَ ﴿٦٠﴾

60. Au ni nani yule aliyeziumba mbingu na ardhi na akawateremshia maji kutoka mbinguni na kwayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuotesha miti yake. Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu waliopotoka.

أَمَّن جَعَلَ الْأَرْضَ قَرَارًا وَجَعَلَ خِلَالَهَا أَنْهَارًا وَجَعَلَ لَهَا رَوَاسِيَ وَجَعَلَ بَيْنَ الْبَحْرَيْنِ حَاجِزًا أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٦١﴾

61. Au ni nani yule aliyefanya ardhi mahali pa kutua? Na akaweka ndani yake mito na akaiwekea milima. Na akaweka kizuizi baina ya bahari mbili. Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

62. Au ni nani yule anayemjibu aliyedhikika pale anapomwomba na akaiondoa dhiki? Na akawafanya ni warithi wa ardhi? Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayoyazingatia.

أَمَّن يَهْدِيكُمْ فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَن يُرْسِلُ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ تَعَالَى اللَّـهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٦٣﴾

63. Au ni nani yule anayewaongoza katika giza la bara na bahari? Na ni nani yule azipelekaye Pepo kuleta bishara kabla ya rehema yake? Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya yale wanayoyashirikisha.

أَمَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَمَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٦٤﴾

64. Au ni nani yule anayeuanzisha uumbaji kisha akaurejesha? Na ni nani anayewaruzuku kutoka mbinguni na ardhini? Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Sema: Leteni dalili zenu kama nyinyi ni wakweli.

JE, KUNA MUNGU MWINGINE?

Aya 60–64

MAANA

Makusudio ya Aya hizi na ile iliyoishia mwisho wa juzuu iliyopita ni kuwatahayariza washirikina na kuwarudi kwa njia ya maswali yasiyohitajia jawabu isipokuwa kusalimu amri; kama yafutavyo:

1.Je, Mwenyezi Mungu ni bora au wale wanaowashirikisha naye?

Aya hii imeishia mwisho wa juzuu ya kumi na tisa tumeileta tena kwa sababu inaungana na hapa Maana ni kuwa ni nani aliye bora na adhimu; ni Mwenyezi Mungu ambaye imetukuka hekima yake au ni mizimu na mengineyo mnayoyaabudu?

Jibu : ni Mwenyezi Mungu hilo halina shaka hata kwa washirikina, kwa sababu hawakanushi kuweko muumba, isipokuwa wanamuomba pamoja na wengine.

2.Au ni nani yule aliyeziumba mbingu na ardhi kwa nidhamu yake na mpangilio wake wa ajabu na wa hali ya juu ambao unafahamisha kuweko mjuzi mwenye hekima? Na akawateremshia maji kutoka mbinguni na kwayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza?

Mwenyezi Mungu huteremsha mvua kutoka mbinguni kwa sababu zake za kimaumbile. Vile vile huotesha kwenye ardhi kila aina ya mimea ya kupendeza kwa sababu za kimaumbile.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba hayo maumbile na viliyvomo ndani yake, ndio ikasemewa kuwa Yeye ndiye aliyeteremsha mvua na kuotesha bustani.

Nyinyi hamna uwezo wa kuotesha miti yake , bali hata kujua chimbuko la uhai wa mimea na mengineyo, isipokuwa mkifasiri kuweko Mola muweza anayekiambia kitu: ‘Kuwa,’ kikawa.

Mfano wa Aya hi ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

أَفَرَأَيْتُم مَّا تَحْرُثُونَ ﴿٦٣﴾ أَأَنتُمْ تَزْرَعُونَهُ أَمْ نَحْنُ الزَّارِعُونَ ﴿٦٤﴾

“Je, mnaona mnayolima? Ni nyinyi mnayoyaotesha au ni sisi tunayoyaotesha? (56:63 – 64).

Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu waliopotoka kwenye haki, kwa sababu wanamlinganisha Mwenyezi Mungu na wengineo.

3.Au ni nani yule aliyefanya ardhi mahali pa kutua?

Yaani ni mahali pa kutulia kulingana na ilivyo kwa umbo lake, kimo chake, vitenda kazi vyake, vituo vyake na mengineyo ambayo hayawezi kuwa isipokuwa kwa mpangilio wa mjuzi mwenye elimu.

Na akaweka ndani yake mito wanayonufaika nayo viiumbena akaiwekea milima ili isiwayumbishe[1] .

Na akaweka kizuizi baina ya bahari mbili ya maji chumvi na maji tamu. Kizuizi ni kuinama sehemu moja zaidi ya nyingine. Vinginevyo maji tamu yangeliharibika. Tazama Juz. 19 (25:53)[2] .

Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu anayeshirikiana naye katika hayo?Bali wengi wao hawajui, lakini wako wanaojua isipokuwa wanafanya kiburi na inadi kuhofia chumo lao.

4.Au ni nani yule anayemjibu aliyedhikika pale anapomwomba na akaiondoa dhiki?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) humpa msaada na tawfiki yule anayemkimbilia Yeye kwa kumtegemea. Humwandalia sababu ambazo zitatekeleza haja zake na humwondolea dhiki na uovu ikiwa ataihangaikia kwa mahangaiko yake yaliyozoeleka. Na yule mwenye kujifungia mahali pake bila ya kuhangaika atakuwa ameidhulumu nafsi yake.

Na akawafanya ni warithi wa ardhi, mkipokezana kizazi baada ya kizazi katika kuimiliki ardhi na kuiendesha.

Hivi karibuni wanasayansi wamegundua kwamba ingawa aina mbili hizi za maumbo ya maji huweza kukutana wakati mto ukiishia baharini, lakini hayawezi kamwe kuchanganyikana kwa vile kuna kizuizi kisichoonekana ambacho huweka aina mbili hizi za maji mbali mbali na tabia zao za wazi.

Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayoyazingatia.

Makusudio ya kuzingatia hapa ni kuzitumia dalili, kunufaika na maonyo na kuwaidhika na mazingatio.

5.Au ni nani yule anayewaongoza katika giza la bara na bahari?

Kupitia milima, nyota na mengineyo yanayoingia kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَعَلَامَاتٍ وَبِالنَّجْمِ هُمْ يَهْتَدُونَ ﴿١٦﴾

“Na alama nyingine. Na kwa nyota wao wanajiongoza.” Juz.14 (16:16).

Na ni nani yule azipelekaye pepo kuleta bishara kabla ya rehema yake?

Umetangulia mfano wake katika Juz.8 (7;57) na Juz. 19 (25:48).

Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya yale wanayoyashirikisha na kuyazua kwa kumnasibishia ushirika na mtoto.

6.Au ni nani yule anayeuanzisha uumbaji kisha akaurejesha?

Mpangilio mzuri katika kuumba unafahamisha kuwa unatokana na mwenye hekima na mpangiliaji. Ikithibitika kuwa uumbaji umeanzia kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi ndio imethibiti kuwa Yeye ndiye mwenye kuurudisha.

Kwa sababu kurudisha ni kwepesi zaidi kuliko kuanzisha, kama isemavyo Aya hii:

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ ﴿٢٧﴾

“Na yeye ndiye ambaye anaanzisha uumbaji kisha ataurudisha mara nyingine. Na hili ni jepesi zaidi kwake.” (30:27).

Na ni nani anayewaruzuku kutoka mbinguni na ardhini kwa kuteremsha mvua na kuotesha mimea?Je, yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Sema: Leteni dalili zenu kama nyinyi ni wakweli kuwa Mwenyezi Mungu ana mshirika au mtoto.

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta dalili na hoja nyingi kwamba yeye yupo na yuko peke yake. Amezifafanua kwa kila mfumo. Basi anayepinga au kumfanya ana mshirika, alete dalili moja tu ya upinzani wake au ya ushirika wake.

Aina hii ya mjadala na mwito wa hukumu ya akili ni dalili mkataa kuwa Uislamu umejikita kwenye umbile ambalo Mwenyeezi Mungu amewaumbia watu. Ni kwa ajili hii ndo Mwenyezi Mungu akausifu kuwa ni dini iliyonyooka.

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ ﴿٦٥﴾

65. Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipokuwa Mwenyezi Mungu; wala wao hawajui lini watafufuliwa.

بَلِ ادَّارَكَ عِلْمُهُمْ فِي الْآخِرَةِ بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ مِّنْهَا بَلْ هُم مِّنْهَا عَمُونَ ﴿٦٦﴾

66. Bali ujuzi wao umefikia kuijua Akhera. Bali wao wamo katika shaka nayo. Bali wao ni vipofu nayo.

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا وَآبَاؤُنَا أَئِنَّا لَمُخْرَجُونَ ﴿٦٧﴾

67. Na wakasema wale ambao wamekufuru: Tutakapokuwa mchanga, sisi na baba zetu, hivyo kweli tutakujatolewa?

لَقَدْ وُعِدْنَا هَـٰذَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا مِن قَبْلُ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٦٨﴾

68. Haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni ngano za watu wa kale.

قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُجْرِمِينَ ﴿٦٩﴾

69. Sema: Nendeni katika ardhi na tazameni ulikuwaje mwisho wa wakosefu.

وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُن فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ ﴿٧٠﴾

70. Wala usiwahuzunikie wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazozifanya.

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٧١﴾

71. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini ikiwa mnasema kweli.

قُلْ عَسَىٰ أَن يَكُونَ رَدِفَ لَكُم بَعْضُ الَّذِي تَسْتَعْجِلُونَ ﴿٧٢﴾

72. Sema: Asaa ikawafikia sehemu ya yale mnayoyahimiza.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَشْكُرُونَ ﴿٧٣﴾

73. Na hakika Mola wako ni mwenye fadhila kwa watu, lakini wengi wao hawashukuru.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَيَعْلَمُ مَا تُكِنُّ صُدُورُهُمْ وَمَا يُعْلِنُونَ ﴿٧٤﴾

74. Na hakika Mola wako anayajua yanayoficha vifua vyao na wanayoyatangaza.

وَمَا مِنْ غَائِبَةٍ فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٧٥﴾

75. Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika kitabu kinachobainisha.

MJUZI WA GHAIBU NA UFUFUO

Aya 65 – 75

MAANA

Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipokuwa Mwenyezi Mungu; wala wao hawajui lini watafufuliwa.

Wapinzani walimtaka Mtume(s.a.w.w) awawekee muda maalum wa ufufuo, ndio Aliye Mtukufu na kutukuka akamwambia: Waambie kuwa hakuna yeyote katika watu majini na hata malaika anayejua ghaibu na muda wa ufufuo isipokuwa Mwenyezi Mungu tu, na kwamba wao watafufuliwa bila ya kujua.

Bali ujuzi wao umefikia kuijua Akhera.

Yaani Mitume waliwapa habari washirikina, lakini hawakumwaamini; watakapofufuliwa na kuiona Akhera kwa macho watajua kuwa yale waliyoelezwa na mitume kuwa ni kweli.

Bali wao wamo katika shaka nayo.

Vipi wanaulizia wakati wa Akhera na hali wao hawaiamini?

Bali wao ni vipofu nayo.

Nyoyo zao zimekuwa na upofu wa Akhera kwa sababu ya upotevu wao na inadi yao.

Na wakasema wale ambao wamekufuru: Tutakapokuwa mchanga, sisi na baba zetu, hivyo kweli tutakujatolewa? Haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni ngano za watu wa kale.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:5) na Juz. 18 (23: 35 – 36 na 82 – 83).

Sema: Nendeni katika ardhi na tazameni ulikuwaje mwisho wa wakosefu.

Haya ni makemeo kwa yule anayekadhibisha utume wa Muhammad(s.a.w.w) , kuwa atapatwa na maangamizi kama yaliyowapata wengine katika umma zilizotangulia ambao waliwakadhibisha mitume wao.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:137).

Wala usiwahuzunikie wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazozi- fanya.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 14 (16:127).

Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini ikiwa mnasema kweli.

Mtume(s.a.w.w) aliwahadharisha makuraishi na mwisho mbaya wa kukadhibisha kwao na uasi wao, wao wakamwambia kwa kumfanyia maskhara: Hilo litakuwa lini? Kila Mtume alisikia jawabu kama hili la dharau kutoka kwa watu wake pale alipowahadharisha.

Sema: Asaa ikawafikia sehemu ya yale mnayoyahimiza.

Huenda adhabu iko nyuma yenu na nyinyi hamjui. Maana ya Aya hii yako kwenye Aya: “Na watasema: lini hayo? Sema: asaa yakawa karibu.” Juz. 15 (17:51).

Na hakika Mola wako ni mwenye fadhila kwa watu, lakini wengi wao hawashukuru.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anawafadhili kwa kuwapa muda na kuwacheleweshea adhabu ili watubie na warudi kutoka kwenye upotevu wao. Ilikuwa ni wajibu wao washukuru hilo, lakini badala yake wanahimiza adhabu kwa dharau.

Na hakika Mola wako anayajua yanayoficha vifua vyao na wanayoy- atangaza.

Walitangaza kumshirikisha Mwenyezi Mungu na wakaficha njama na shari dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyaficha na wanayoyadhihirisha.

Naye atawalipa tu kwa haya na yale kulingana na wanavyostahili.

Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika kitabu kinachobainisha.

Hakuna siri katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu hilo halina shaka, lakini makusudio ya kulieleza hilo ni onyo na hadhari kwa wahaini na vibaraka ambao wanajificha nyuma ya pazia la unafiki na ria.

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَقُصُّ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَكْثَرَ الَّذِي هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٧٦﴾

76. Hakika hii Qur’an inawasimulia wana wa Israil mengi wanayohitilafiana.

وَإِنَّهُ لَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٧٧﴾

77. Nayo hakika ni uongofu na rehema kwa waumini.

إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُم بِحُكْمِهِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ ﴿٧٨﴾

78. Hakika Mola wako atakata baina yao hukumu yake naye ni mwenye nguvu, Mjuzi.

فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ إِنَّكَ عَلَى الْحَقِّ الْمُبِينِ ﴿٧٩﴾

79. Basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika wewe uko kwenye haki iliyo wazi.

إِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ ﴿٨٠﴾

80. Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka kurudi nyuma.

وَمَا أَنتَ بِهَادِي الْعُمْيِ عَن ضَلَالَتِهِمْ إِن تُسْمِعُ إِلَّا مَن يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا فَهُم مُّسْلِمُونَ ﴿٨١﴾

81. Wala huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao. Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanaoziamini ishara zetu, basi hao ndio watiifu.

وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لَا يُوقِنُونَ ﴿٨٢﴾

82. Na itakapowaangukia, tutawatolea mnyama katika ardhi atakayewasemeza, kwamba watu walikuwa hawana yakini na ishara zetu.

وَيَوْمَ نَحْشُرُ مِن كُلِّ أُمَّةٍ فَوْجًا مِّمَّن يُكَذِّبُ بِآيَاتِنَا فَهُمْ يُوزَعُونَ ﴿٨٣﴾

83. Na siku tutakapowakusanya watu kutoka kila umma, kundi katika wanaokadhibisha ishara zetu. Nao watagawanywa mafungu mafungu.

حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوا قَالَ أَكَذَّبْتُم بِآيَاتِي وَلَمْ تُحِيطُوا بِهَا عِلْمًا أَمَّاذَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨٤﴾

84. Hata watakapofika, atasema: Je, nyinyi si mlizikanusha ishara zangu pasipo kuzijua vyema, au mlikuwa mkifanya nini?

وَوَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِم بِمَا ظَلَمُوا فَهُمْ لَا يَنطِقُونَ ﴿٨٥﴾

85. Na kauli itawaangukia kwa vile walivyodhulumu. Basi wao hawatasema lolote.

QUR’AN INASIMULIA

Aya 76 – 85

MAANA

NEMBO YA ISRAIL NI: ‘TUMESIKIA NA TUMEASI’

Hakika hii Qur’an inawasimulia wana wa Israil mengi wanayohitalifiana.

Qur’an imezungumzia na kuyakariri mambo ya kushangaza ya wana wa Israil. Imezungumzia mambo yanayohusiana nao, nembo yao na yale waliyohitalifiana wakati wa Nabii Musa na baadaye.

Nembo yao wanayoifuata bila ya kuicha ni: ‘Tumesikia na tumekataa,’ kama ilivyoelezwa katika Juz. 1(2:93) na Juz. 5 (4:46). Yaani tumemsikia Mwenyezi Mungu na mtume wake na tumemuasi Mwenyezi Mungu na mitume wote. Waliendelea na nembo hii wakati wa Nabii Musa(a.s) mpaka akawashtakia kwa Mola wake na akawapa sifa ya ufuska, akisema kwa masikitiko:

رَبِّ إِنِّي لَا أَمْلِكُ إِلَّا نَفْسِي وَأَخِي فَافْرُقْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ ﴿٢٥﴾

“Ewe Mola wangu! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu; basi tutenge na watu hawa mafasiki.” Juz. 6 (5:25).

Katika Aya nyingine amewapa sifa ya upumbavu:

قَالَ رَبِّ لَوْ شِئْتَ أَهْلَكْتَهُم مِّن قَبْلُ وَإِيَّايَ أَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ السُّفَهَاءُ مِنَّا ﴿١٥٥﴾

“Alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeliwaangamiza wao na mimi zamani. Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wapumbavu katika sisi?” Juz. 9 (7:155).

Bado wanaendelea na nembo yao hii hadi leo. Mnamo mwaka 1967, Umoja wa Mataifa, unaowakilisha mataifa yote duniani, kuanzia mashariki hadi magharibi, ulipitisha azimio la kuitaka Israil ijiondoe katika ardhi ya Quds.

Jibu la mjumbe wake lilikuwa ni: “Umoja wa Mataifa ni debe la takataka,” kama ilivyonukuliwa katika magazeti.

Ama yale ambayo walihitilafiana ni walivyoifanyia Tawrat wakati wa Musa mpaka Mwenyezi Mungu akawainulia jabali na kuwatishia kuwaangamiza:

وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَكُمْ وَرَفَعْنَا فَوْقَكُمُ الطُّورَ خُذُوا مَا آتَيْنَاكُم بِقُوَّةٍ وَاسْمَعُوا قَالُوا سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا ﴿٩٣﴾

“Na tulipochukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu: Kamateni kwa nguvu haya tuliyowapa na sikilizeni. Wakasema: “Tumesikia na tumekataa” Juz 1(2:93)[3] .

Walihitalifiana katika mitume waliokuja baada ya Musa(a.s) . Miongoni mwao ni Bwana Masih(a.s) , kundi moja lilimkadhibisha na kundi moja likataka kumuua; kama ilivyoelezwa katika Juz. 1 (2:87).

Vilevile walihitalifiana kuhusu utume wa Muhammad. Hawakumwamini isipokuwa wachache. Kama wangelikuwa ni watafutaji kweli wa haki wangeliafikiana kuichukua Qur’an ambayo imesimama kwa dalili na hoja juu ya ukweli wake.

Nayo hakika ni uongofu na rehema kwa waumini.

Ni uongofu kwa mwenye kutaka kuongoka na rehema kwa kutumia hukumu zake na mafunzo yake.

Hakika Mola wako atakata baina yao hukumu yake naye ni mwenye nguvu, Mjuzi.

Siku ya Kiyama batili zitaondoka na Mwenyezi Mungu atawahukumu waisrail na wengineo katika yale waliyohitalifiana katika mambo ya dini na dunia.

Basi mtegemee Mwenyezi Mungu.

Mwenye kukimbilia kwake basi yuko katika ngome imara na kizuizi cha nguvu.

Hakika wewe uko kwenye haki iliyo wazi.

Na mwenye haki hajali yanayosemwa juu yake.

Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka kurudi nyuma. Wala huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao.

Jumla hizi zina lengo moja, kwamba kuna sifa zinazoua moyo na kumfanya mtu anga’ang’anie ukafiri, unafiki na upotevu. Zinamfanya yeye na maiti ni sawasawa; hafaidiki na mawaidha wala maonyo. Miongoni mwa sifa kuu hizo ni tamaa na pupa ya chumo na cheo.

Maana haya yamekaririka kwa mifumo mbalimbali; miongoni mwayo ni Aya hizi zifuatazo:-

Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi. Hao ndio walioghafilika. Juz. 9 (7:179).

Je, wewe unaweza kuwasikilizisha viziwi ingawa hawafahamu? Je, wewe unaweza kuwaogoza vipofu ingawa hawaoni? Juz.11 (10 42–43).

Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanaoziamini ishara zetu, basi hao ndio watiifu.

Anayekusikiliza na kukutii wewe Muhammad ni yule anayeitafuta haki kwa ajili ya haki, kiasi ambacho akipata dalili na hoja anaiamini na kuifuata. Ama watu wa masilahi na tamaa wanakupa mgongo.

Na itakapowaangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama katika ardhi atakayewasemeza, kwamba watu walikuwa hawana yakini na ishara zetu.

Kuwaangukia, ni kuwathibitikia. Makusudio ya kauli hapa ni yale aliyoyaahidi Mwenyezi Mungu ya kutokea Kiyama. Makusudio ya watu ni makafiri.

Ama kuhusu mnyama, maneno yamekuwa mengi kumuhusu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutubainishia ni yupi. Pia Hadith kutoka kwa maasum hazikuthibiti; hata kama mapokezi yake yatasihi hatuwezi kuitumia, kwa sababu itakuwa imekuja kwa njia moja (Khabarul-waahid) ambayo inakuwa hoja katika hukumu tanzu, si katika maudhui na misingi ya kiitikadi. Na kusema bila ya elimu ni haramu.

Kwa hiyo hakuna kilichobakia isipokuwa kuchukulia dhahiri ya Aya ambayo inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atakapowafufua watu kwa ajili ya hisabu atamtoa kiumbe kutoka ardhini atakayetangaza kuwa makafiri walizikana dalili wazi wazi na hoja mkataa za kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na mitume wake.

Unaweza kuuliza : kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubainisha hakika ya mnyama huyu akawaacha watu wameduwaa, mpaka wengine wakasema bila ya elimu na kuwazia tu?

Jibu : Lengo la kutajwa ni kuwatangaza makafiri na kwamba wao watafufuliwa kesho wakiwa madhalili wamefedheheka mbele ya ushahidi. Lengo hili linapatikana kiasi cha kudokeza tu kuwa kutakuwa na mnyama hata kama jina lake halijulikani wala hakika yake. Aya hii inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Siku ambayo nyuso zitang’aa na nyuso (nyingine) zitasawijika.” Juz. 4 (3:106).

Na siku tutakapowakusanya watu kutoka kila umma, kundi katika wanaokadhibisha ishara zetu.

Neno ‘katika’ ni la kubainisha sio la baadhi; ni kama mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Jiepusheni na uchafu katika mizimu.” akimaanisha mizimu yote sio baadhi.

Maana ni kuwa katika kila umma kuna wanaosadikisha ishara za Mwenyezi Mungu na wenye kuzikadhibisha. Mwenyezi Mungu (s.w.t) kesho atawakusanya wakadhibishaji wote kwa ajili ya hisabu na malipo. Inajulikana wazi kuwa Mwenyezi Mungu atawakusanya wasadikishaji na wakadhibishaji, lakini lengo la kutajwa wakadhibishaji ni ukemeo na kiaga.

Nao watagawanywa mafungu mafungu.

Malaika watawazuia kuumeni na kushotoni na watawachunga kwenda kwenye kisimamo, kama wanyama wakipelekwa machinjioni.

Hata watakapofika, atasema: Je, nyinyi si mlizikanusha ishara zangu pasipokuzijua vyema, au mlikuwa mkifanya nini?

Watakaposimama wakanushaji mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu atawaambia kwa kuwatahayariza, kwa nini mmewakadhibisha mitume wangu na kuacha kuitikia mwito wao? Ikiwa hamkujua ukweli wao kwanini mlipinga dalili za kuwajulisha na msiziangalie kwa mtazamo wa mwenye kutafuta haki kwa njia ya haki? Ni lipi lilo muhimu zaidi ya hilo?

Maulamaa wameafikiana, kwa kauli moja, kuwa akili inahukumiwa kwa wajibu wa kuangalia muujiza wa mwenye kudai utume. Wakasema: Akili haisamehewi kwa lile ambalo ni wajibu ikiwa inaweza kufanya utafiti na kupata maarifa. Kuna Hadith isemayo: “Mja ataambiwa siku ya Kiyama, je ulijua? Akisema, ndio, Ataulizwa tena, je ulifanya? Akisema sikujua (namna ya kufanya), ataulizwa, je ulijifundisha?

Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyodhulumu.

Ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu itawapata kwa sababu ya kufuru yao na uzembe wao wa kufanya utafiti na kuuliza.

Basi hao hawatasema lolote, kwa sababu ya kukatikiwa na hoja na mshangao wao kutokana na vituko vya siku ya Kiyama.

أَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا اللَّيْلَ لِيَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٨٦﴾

86. Je, hawaoni kwamba tumeufanya usiku ili watulie na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye kuamini.

وَيَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ ﴿٨٧﴾

87. Na siku itakapopuziwa parapanda, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote watamfikia nao ni wanyonge.

وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ ﴿٨٨﴾

88. Na unaiona milima unaidhania imetulia nayo inakwenda mwendo wa mawingu. Ni sanaa ya Mwenyezi Mungu aliyekitengeneza vizuri kila kitu. Hakika yeye ana habari za mnayoyatenda

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَهُم مِّن فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ ﴿٨٩﴾

89. Watakaokuja na wema watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mfazaiko wa siku hiyo.

وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَكُبَّتْ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٩٠﴾

90. Na wenye kuja na uovu, basi nyuso zao zitatupwa motoni. Kwani mnalipwa isipokuwa yale mliyoyatenda?

إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ رَبَّ هَـٰذِهِ الْبَلْدَةِ الَّذِي حَرَّمَهَا وَلَهُ كُلُّ شَيْءٍ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٩١﴾

91. Hakika nimeamrishwa kumwabudu tu Mola wa mji huu ambaye ameufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kunyenyekea.

وَأَنْ أَتْلُوَ الْقُرْآنَ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَقُلْ إِنَّمَا أَنَا مِنَ الْمُنذِرِينَ ﴿٩٢﴾

92. Na kwamba nisome Qur’an. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake tu na aliyepotea basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji tu.

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ سَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَتَعْرِفُونَهَا وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾

93. Na Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) Atawaonyesha ishara zake mtazijua. Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.

MILIMA INAKWENDA MWENDO WA MAWINGU

Aya 86 – 93

MAANA

Je, hawaoni kwamba tumeufanya usiku ili watulie na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wenye kuamini.

Imetangulia pamoja na tafsiri yake katika Juz. 11 (10:67).

Na siku itakapopuziwa parapanda, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu.

Parapanda itapuziwa kutangaza Kiyama, nyoyo za viumbe zitashtuka, kutokana na mpuzio huo, kwa hofu kuu; isipokuwa nyoyo za Mitume wasadikishaji, mashahidi na watu wema ambao Mwenyezi Mungu amewavua kwa kusema: ‘Ila amtakaye Mwenyezi Mungu.’ Hao aliowavua amewashiria katika kauli yake:

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا ﴿٦٩﴾

“Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na wasadikishaji na mashahidi na watu wema. Na hao ndio marafiki wema.” Juz. 5 (4:69).

Katika baadhi ya tafsiri imeelezwa kuwa Parapanda itapulizwa mara tatu; Mpulizo wa fazaa, wa kufa watu wote na ule wa ufufuo. Ufufuo wa kwanza unafahamishwa na Aya tuliyo nayo, wa pili na wa tatu unafahamishwa na Aya isemayo: “Na itapulizwa parapanda, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhini, ila aliyemtaka Mwenyezi Mungu. Kisha itapulizwa mara nyingine. Hapo watainuka wawe wanangojea.”

Na wote watamfikia nao ni wanyonge.

Yaani hao wanaohofia watafufuliwa kwa Mola wao wakiwa dhalili.

MILIMA NA HARAKATI ZA ARDHI

Na unaiona milima unaidhania imetulia nayo inakwenda mwendo wa mawingu.

Maudhui ya Aya hii na iliyo kabla yake ni mamoja, kuzungumzia Kiyama na vishindo vyake. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ataing’oa milima kutoka sehemu zake na kuiendesha angani, sawa na yanavyopita mawingu, lakini mtu atafikiria kuwa imetulia.

Hiyo inatokana na kuwa umbo kubwa likitembea kwenye mwelekeo mmoja ulionyooka, basi macho hayaoni harakati zake kutoka na ukubwa wake na umbali wa pembe zake; hasa ikiwa mtazamaji yuko mbalia nalo.

Hapa yanatubainikia makosa ya mwenye kuitumia aya hii katika kuthibitisha harakati ya ardhi. Kuna Aya nyingi zinazofahamisha kuwa makusudio ya kutembea milima, katika Aya hii, kutakuwa siku ya Kiyama; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-

وَيَوْمَ نُسَيِّرُ الْجِبَالَ وَتَرَى الْأَرْضَ بَارِزَةً وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا ﴿٤٧﴾

“Na siku tutakayoipitisha milima na utaiona ardhi iwazi. Na tutawafufua..” Juz. 15 (18:47).

وَسُيِّرَتِ الْجِبَالُ فَكَانَتْ سَرَابًا ﴿٢٠﴾

“Na ikaendeshwa milima ikawa sarabi.” (78:20).

يَوْمَ تَمُورُ السَّمَاءُ مَوْرًا ﴿٩﴾ وَتَسِيرُ الْجِبَالُ سَيْرًا ﴿١٠﴾

“Siku itakapotikisika mbingu mtikisiko. Na milima iwe inakwenda mwendo.” (52: 9 – 10).

Maneno ya Qur’an ni mamoja, sehemu moja inaifafanulia nyingine.

Ndio! Watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w) , ambao wana elimu ya Kitabu na Sunna, waliweka wazi kuwa ardhi ina harakati kabla ya Companicus, kwa miaka elfu moja. Imam Ali(a.s) anasema katika Nahjul-balagha:Na akaiumba ardhi hewani na akiweka bila ya muhimili na akaiinua bila ya nguzo (khutba 186). Na mjukuu wake Imam Jafar Sadiq akasema:“Kufahamisha vitu kuzunguka na vilivyomo ndani yake zikiwamo sayari saba, ni kuwa ardhi ina harakati…”

Ni sanaa ya Mwenyezi Mungu aliyekitengeneza vizuri kila kitu , kuanzia kikubwa sana hadi kidogo sana. Ufundi, mpangilio na nidhamu ni ushahidi mkubwa wa kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na uwezo.

Hakika yeye ana habari za mnayoyatenda.

Ambaye amemuumba mtu kwa ufundi wa hali ya juu, anajua kila akitendacho kiumbe, kiwe cha heri au cha shari na yale yanayompitikia katika nafsi yake:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ ﴿١٦﴾

“Na hakika tumemuumba mtu nasi tunayajua yanayoitia wasiwasi nafsi yake na sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wake wa shingo.” (50:16).

Watakaokuja na wema watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mfazaiko wa siku hiyo. Na wenye kuja na uovu, basi nyuzo zao zitatupwa motoni. Kwani mnalipwa isipokuwa yale mliyoyatenda?

Inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na mwenye kufanya vibaya hatalipwa ila sawa na hivyo tu. Nao hawatadhulumiwa.” Juz. 7 (6:179).

Hakika nimeamrishwa kumwabudu tu Mola wa mji huu ambaye ameufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kunyenyekea.

Makusudio ya mji hapa ni Makka Tukufu. amaeuhusisha kuutaja, pamoja na kuwa yeye ni Mola wa ulimwengu wote, ili kuwabainishia makuraishi neema yake kwao kwa sababu ya mji huo. Walikuwa wakitegemeza ubora wao kuliko waarabu wengine kwa taadhima ya mji huo na utakatifu wake na kuwa na amani, kwa kuharamishwa kuua, kupigana, kuwinda, kukata miti na mengine yanayofahamisha utukufu na cheo chake.

Pamoja na yote haya makuraishi waliabudu masanamu wakaichafua Al-ka’ba kwayo, wakimshirikisha nayo Mola wa mji huu mtukufu ambaye amewalisha kutokana na njaa na akawasalimisha na hofu.

Kauli ya Mtume(s.a.w.w) : ‘Nimeamrishwa kumwabudu …’ ni kuwapinga makuraishi na kwamba wajibu wao ni kuacha ibada ya ya masanamu ambayo hayamiliki chochote, na wamwabudu Mola wa mji huu ambaye ndiye muumba, mfalme na mwenye amri. Na yeye ni muweza wa kila kitu na akawafadhili makuraishi kwa vitu vingi.

Na kwamba nisome Qur’an.

Makusudio ya kusoma Qur’an hapa ni kutoa mwito wa kuiamini na kwenda na sera yake.

Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake tu na aliyepotea basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji tu.

Mtume(s.a.w. w ) ametoa mwito wa uongofu. Mwenye kusikia na akatii, basi amejifanyia uzuri mwenyewe na atakuwa amefuata njia ya kheri na uokovu. Na mwenye kupinga basi atakuwa amejifanyia ubaya yeye mwenyewe na kujiingiza kwenye shari na maangamizi. Mtume(s.a.w.w) hana majukumu ya watu wa upotevu baada ya kuwanasihi na kuwafikishia risala ya Mola wake.

Na Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) kwa kuniwafikisha kufikisha risala yake kwa waja wake kama alivyopenda na kutaka.

Atawaonyesha ishara zake mtazijua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaonyesha dalili za ishara zake kwenye nafsi zao na kwenye pambizo, lakini wakazikana. Ndio akawaambia, leo mnazikana na kesho mtazikubali, ambapo kukubali kwenu hakutawafaa kitu.

Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.

Haya ni makemeo na kiaga cha kupinga kwao na kukana ishara za Mwenyezi Mungu na ubainifu wake.