TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 14317
Pakua: 2503


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 25 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14317 / Pakua: 2503
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

Mwandishi:
Swahili

21

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَاءَتْكُمْ جُنُودٌ فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا وَجُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا ﴿٩﴾

9. Enyi ambao mmeamini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu; pale yalipowafikia majeshi, tukayapelekea upepo na majeshi msiyoyaona na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

إِذْ جَاءُوكُم مِّن فَوْقِكُمْ وَمِنْ أَسْفَلَ مِنكُمْ وَإِذْ زَاغَتِ الْأَبْصَارُ وَبَلَغَتِ الْقُلُوبُ الْحَنَاجِرَ وَتَظُنُّونَ بِاللَّـهِ الظُّنُونَا ﴿١٠﴾

10. Walipowajia kutoka juu yenu na kutoka chini yenu; na macho yakakodoka na nyoyo zikapanda kooni. na mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali.

هُنَالِكَ ابْتُلِيَ الْمُؤْمِنُونَ وَزُلْزِلُوا زِلْزَالًا شَدِيدًا ﴿١١﴾

11. Hapo waumini walijaribiwa na wakatikiswa mtikiso mkali.

وَإِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ مَّا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ إِلَّا غُرُورًا ﴿١٢﴾

12. Na waliposema wanafiki na wale ambao wana maradhi katika nyoyo zao, Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakutuahidi ila udanganyifu.

وَإِذْ قَالَت طَّائِفَةٌ مِّنْهُمْ يَا أَهْلَ يَثْرِبَ لَا مُقَامَ لَكُمْ فَارْجِعُوا وَيَسْتَأْذِنُ فَرِيقٌ مِّنْهُمُ النَّبِيَّ يَقُولُونَ إِنَّ بُيُوتَنَا عَوْرَةٌ وَمَا هِيَ بِعَوْرَةٍ إِن يُرِيدُونَ إِلَّا فِرَارًا ﴿١٣﴾

13. Na kundi moja miongoni mwao liliposema: Hapana pa kukaa nyinyi leo, basi rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume wakisema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa ni tupu; hawakutaka ila kukimbia tu.

وَلَوْ دُخِلَتْ عَلَيْهِم مِّنْ أَقْطَارِهَا ثُمَّ سُئِلُوا الْفِتْنَةَ لَآتَوْهَا وَمَا تَلَبَّثُوا بِهَا إِلَّا يَسِيرًا ﴿١٤﴾

14. Na lau wangeingiliwa kwa pande zake, kisha wakatakiwa fitna, wangelifanya, na wasingelisita isipokuwa kidogo tu.

وَلَقَدْ كَانُوا عَاهَدُوا اللَّـهَ مِن قَبْلُ لَا يُوَلُّونَ الْأَدْبَارَ وَكَانَ عَهْدُ اللَّـهِ مَسْئُولًا ﴿١٥﴾

15. Na kwa hakika walikuwa wamemwahidi Mwenyezi Mungu kabla kwamba hawatageuza migongo. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.

AHZAB

Aya 9 – 15

MUHTASARI WA KISA CHA AHZAB

Aya hizi tulizo nazo na zinazofuatia hadi 27, zilishuka kuhusu vita vya Ahzab (makundi), ambavyo pia vinaitwa vita vya Khandaq (handaki).

Kwa ufupi ni kuwa kikundi katika viongozi wa kiyahudi waliwahimiza makuraishi na makabila mengine ya waarabu kupigana na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Walitoa mali nyingi sana na wakaweza kuunda jeshi ambalo halikuwahi kutokea katika bara Arabu. Basi jeshi, likiongozwa na Abu Sufyan, likaelekea Madina.

Mtume(s.a.w.w) , alipojua makusudio yao, aliaamrisha lichimbwe shimo kwa ushauri kutoka kwa Salman Al-Farisi. Mtume(s.a.w.w) akafanya kazi kwa mkono wake, na waislamu wengine wenye ikhlasi pia wakafanya kazi. Salmani alikuwa akiwatia hamasa kwa kuwasimulia ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa wanaofanya matendo na wapiganaji jihadi. Wanafiki walikuwa wakijaribu kuivunja azma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na wakiponyoka bila ya Mtume kujua.

Lakini handaki lilikamilika, na vikosi vya majeshi vikaanza kuja kwa maelfu. Waislamu walipowaona, wengi wakajawa na hofu na wakaona wamefikwa na balaa, wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana nyingi. Fazaa yao ilizidi pale Bani Quraydh, kabila la kiyahudi waliokuwa wakikaa na Mtume(s.a.w.w) Madina wakiwa na ahadi ya kutosaidia adui, na kuendelea na ahadi yao hiyo, lakini lilipokuja jeshi la Ahzab wakavunja ahadi na kutangaza vita katika wakati mgumu sana kwa waislamu.

Hivi ndivyo walivyo Mayahudi kila wakati na kila mahali. Wanajidhalilisha kama mbwa, wakiwa hawana nafasi, lakini mara tu wanapoipata wanaanza kuuma. Mtume(s.a.w.w) alimtuma Sa’d Bin Muadh na maswahaba wengine kujaribu kuwaambia Bani Quraydha wasivunje ahadi, lakini wakang’angania kuivunja. Basi Waislamu wakawa wamezungukwa na adui wa nje na wa ndani. Juu kuna adui na chini kuna adui.

Katika kitabu Fiqhu ssira cha Sheikh Ghazali, anasema: “Amru bin Wud, Ikrima bin Abu Jahl na Dhirar bin Al-Khattwab walipitapita wakaona sehemu finyu kwenye handaki, Wakawarusha farasi wao na wakajitoma. Waislamu wakahisi hatari sana. Wapanda farasi wakiongozwa na Ali bin Abu Twalib, wakenda haraka kuziba mwanya.

Ali akamwambia Amru bin Wud, Shujaa mkubwa, mwenye uzoefu: ‘Ewe Amru! Ulimwahidi Mwenyezi Mungu kuwa mwanamume yote wa kikuraishi hatakupa mwito wa mojawapo ya mambo mawili ila utauchukua.” Akasema: “Ndio.” Ali akamwambia: “Ninakupa mwito uje kwa Mwenyezi Mungu kwenye Uislamu.” Akasema: “Sina haja.” Ali akasema. “Ninakuita kwenye mapambano.” Akasema: “Kwa nini ewe mwana wa ndugu yangu. Wallah mimi sipendi kukuua-alisema hivi kwa kumdharau - Ali akamwambia wallahi mimi ninapenda kukuua.

Basi Amru akakasirika, akaruka kutoka kwenye farasi wake, na akapiga uso wake; kisha akamkabili Ali wakaanza kupambana; Ali akamuua. Wakatoka wapanda farasi wa washirikina wakiwa wameshindwa hawana lolote.”

Jeshi la washirikina lilipoona halina mahali pa kuvuka handaki wakaanza kurusha mishale yao kwa waislamu. Mshale mmoja ukampata Sa’ad Bin Mua’dh na ukamjeruhi sana kwenye mboni ya jicho. Mtume(s.a.w.w) akaamuru apelekwe kwa mwanamke anayeitwa Rafida, aliyekuwa akiwatibu majeruhi wa kiislamu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Sa’ad alipoona jeraha lake linaweza kumuua, aliomba dua kwa kusema: “Ewe Mola wangu, Ikiwa bado umebakisha vita na Makuraishi basi nibakishe, kwani hakuna watu ninaopenda kuwapiga jihadi kuliko hawa waliomuudhi Mtume, wakamkadhibisha na kumfukuza. Na ikiwa vita umevimaliza baina yetu na wao basi nibakishe wala usiniue mpaka jicho langu litulie kwa Bani Quraydha.”

Basi Mwenyezi Mungu akamwitikia dua yake akamfanya ni hakimu kwa Bani Quraydha, akawauwa wanume wao na akateka wake zao. Ufafanuzi utakuja kwenye Aya 26 inshallah.

Waislamu wakaendelea kuzingirwa kwa kiasi cha siku ishirini; hakuna kitu isipokuwa kutupiana mishale na mawe. Mara ukaja upepo mkali uliopondaponda kambi ya Ahzab, ukaizua mahema yao, na kila kitu kikaharibika, wakarudi wamedhalilika wakiongozwa na Abu Sufyan.

Mwenyezi Mungu akampa nguvu Mtume wake kwa ushindi; akawa anasema: Lailaha ill- lallha, wahdahu, swadaqa wa’dahu wanaswara abdahu, wa a’zza jundahu wahazama l-a’hzaba wahadau, fala shay-unba’dah” (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, amesma kweli kiaga chake na akamusuru mja wake na akawatia nguvu askari wake na akavishinda makundi akiwa peke yake, basi hakuna kitu baada yake).

Wapokezi wameafikiana kuwa vita hivi vilikuwa mwaka wa tano wa Hijra na wakatofautiana katika mwezi. Kuna waliosema ni Dhul qaada (mfunguo pili) na waliosema ni Shawwal (mfunguo mosi). Kwa ujumla hivyo ndivyo vilivyokuwa vita vya Ahzab (makundi). Ufafanuzi wake ni kama ufuatavyo katika ufafanuzi wa Aya:

Enyi ambao mmeamini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu; pale yalipowafikia majeshi, tukayapelekea upepo.

Kumbukeni enyi waumini mliokuwa pamoja na Mtume(s.a.w.w) katika vita vya Khandaq, mkizungukwa na maadui kila upande. Kumbukeni hilo na mshukuru neema ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa na ikhlasi na subira, pale alipowapelekea madui zenu upepo mkalina majeshi msiyoyaona na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

Wafasiri wanasema walikuwa ni malaika. Inawezekana kuwa ni kinaya cha khofu na utishio alioutia Mwenyezi Mungu kwenye nyoyo za majeshi ya Ahzab.

Katika Bahrul-muhit ya Abu Hayan Al-Andalusi imeelezwa kuwa jeshi la wa Ahzab lilikuwa na watu 15,000 na waislamu walikuwa 3000.

Wafasiri na watu wa sera wameafikiana kwamba ulitokea mwamba ndani ya handaki wakati wa kuchimba, ukavunja vyuma na kukawa na uzito. Mtume(s.a.w.w) akachukua sururu kutoka kwa Salman akaupiga mwamba ukatoa cheche, akapiga mara ya pili ukatoa cheche na mara ya tatu pia ukatoa cheche. Mtume(s.a.w.w) akasema:“Kwenye cheche za kwanza nimeona Madain mji wa mfalme Kisra, mara ya pili nikaona kasri ya Kaizari na mara ya tatu nikaona kasri ya Sanaa. Na Jibril amenipa habari kuwa umma wangu utaingia kote huko, basi furahini.”

Yote aliyoyasema, Bwana wa majini na watu, yalitokea.

Walipowajia kutoka juu yenu na kutoka chini yenu.

Yaani jeshi la Ahzab liliwazingira waislamu bila kuwapa mwanya wowote. Kundi la wafasiri wamesema kuwa walikuja Ghatafan, Banu Quraydha na Banun Nadhir katika Mayahudi kutoka upande wa mashariki, wakaja Makuraishi, Banu Kinana na watu Tihama kutoka upande wa magharibi.

Na macho yakakodoka na nyoyo zikapanda kooni.

Hiki ni kinaya cha hofu kubwa na fazaa.

Na mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali.

Baadhi ya walioamini walidhani kuwa Mwenyezi Mungu hatainusuru dini yake na Mtume wake. Baadhi ya wanafiki wakasema Muhammad anatuahidi hazina za Kaizari na leo mtu hawezi hata kwenda chooni.

Hapana mwenye shaka kuwa daima kuna udhuru kwa wanafiki. Lakini mwenye kuamini kisha akajiuliza huku akikereka: Kwa nini Mwenyezi Mungu asiwadidimize madhalimu ardhini au awateremshie kimondo kutoka mbinguni, huyu hatumshangai kuwa yeye ni mwenye kusamehewa kwa Mungu, maadamu anamwamini kwenye moyo wake.

Hapo waumini walijaribiwa na wakatikiswa mtikiso mkali.

Uhakika wa nafsi ulivyo haujitokezi ila wakati wa shida na mtihani wa mambo ya kuhofisha na ya kuchukiza. Vita vya Khandaq vilikuwa ni mtihani mkubwa sana kwa waumini na wanafiki; ambapo hakika ya kila mmoja ilijitokezawaliposema wanafiki walioficha unafiki na kudhihirisha imanina wale ambao wana maradhi katika nyoyo zao . Hawa ni wale wenye imani dhaifu waliowaamini wanafiki bila ya kufikiria. Hawa na wale wakasema:

Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakutuahidi ila udanganyifu.

Hao hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Mtume wake. Kwa sababu mumin hawezi kusema maneno haya ya kufuru. Waliyasema haya ili kuwatia shaka wapumbavu na wenye akili dhaifu.

Na kundi moja miongoni mwao liliposema: Hapana pa kukaa nyinyi leo, basi rudini.

Mtume(s.a.w.w) na maswahaba walipoanza kuchimba handaki, kundi moja la wanafiki likasema: “Handaki litafaa nini na vita hivi, halifai lolote hilo.” Walisema hivi kabla ya kufika majeshi. Yalipokuja majeshi wakasema: “Hamuliwezi jeshi hili kubwa wala hamponi isipokuwa kukimbia na kujisalimisha.”

Wakati nikifafanua Aya hizi nimekumbuka vibaraka wa wazayuni na wa wakoloni wanavyoeneza hofu na fazaa kutoka kwa waisrail. Nimekumbuka hivyo kwa kujua kuna wanaofanana nao katika zama zilizopita na kwamba vita vya maneno vilianza zamani; wala havikuanza na uzayuni na ukoloni; lakini la umuhimu ni kuwa hahadaiki nayo isipokuwa mwenye akili finyu na asiyekuwa na mtazamo wa mbali [8] .1

Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume wakisema: Hakika nyumba zetu ni tupu.

Wanafiki walikuwa wakitafuta vijisababu vya kukimbia kambi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kwa kusema kuwa wataibiwa kwa vile nyumba zao hazina watu, lakini Mwenyezi Mungu akafichua uwongo na unafiki wao kwa kusema:wala hazikuwa ni tupu. Hawakutaka ila kukimbia tu kutoka kwenye jihadi na kuinusuru haki.

Na lau wangeingiliwa kwa pande zake, kisha wakatakiwa fitna, wan- gelifanya, na wasingelisita isipokuwa kidogo tu.

Makusudio ya fitna hapa ni kurtadi. Yaani lau jeshi la washirikina lingeingia Madina na likauzingira mji kila upande, na washirikina wawambie wanafiki wartadi na kutangaza shirk, basi wangeliitika haraka sana bila ya kusita au wangelisita kidogo tu.

Ilivyo ni kuwa mumin wa kweli hawezi kurtadi itikadi yake, bali anaipigania akiwa anajua kuwa mwema ni yule anayeigombania dini, vyovyote itakavyokuwa; kama walivyo mashahidi, hawaogopi silaha za wauaji.

Na kwa hakika walikuwa wamemwahidi Mwenyezi Mungu kabla kwamba hawatageuza migongo.

Walitumia uongo kukwepa jeshi la Mtume baada ya kutoa ahadi kwamba watashiriki hadi mauti. Katika Tafisir Tabariy imesemwa: “Bani Haritha na Bani Salama, walidhamiria waislamu washindwe siku ya Uhud; kisha wakamwahidi Mwenyezi Mungu kuwa hawatarudia milele; ndipo Mwenyezi Mungu akawakumbusha ahadi hii waliyoitoa wenyewe.” Tazama Juz. 4 (3:122).

Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa siku ya Kiyama kuhusu utekelezwaji wake,

فَمَن نَّكَثَ فَإِنَّمَا يَنكُثُ عَلَىٰ نَفْسِهِ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللَّـهَ فَسَيُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿١٠﴾

“Basi mwenye kuvunja ahadi kwa hakika anaivunjia nafsi yake tu, na anayetekeleza aliyomwahidi Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.” (48:10).

قُل لَّن يَنفَعَكُمُ الْفِرَارُ إِن فَرَرْتُم مِّنَ الْمَوْتِ أَوِ الْقَتْلِ وَإِذًا لَّا تُمَتَّعُونَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٦﴾

16. Sema: Hakutawafaa kukimbia; ikiwa mnakimbia kifo au kuuawa. Na hata hivyo hamtastareheshwa isipokuwa kidogo tu.

قُلْ مَن ذَا الَّذِي يَعْصِمُكُم مِّنَ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَ بِكُمْ سُوءًا أَوْ أَرَادَ بِكُمْ رَحْمَةً وَلَا يَجِدُونَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴿١٧﴾

17. Sema, ni nani atakayewalinda na Mwenyezi Mungu akiwatakia uovu au akiwatakia rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الْمُعَوِّقِينَ مِنكُمْ وَالْقَائِلِينَ لِإِخْوَانِهِمْ هَلُمَّ إِلَيْنَا وَلَا يَأْتُونَ الْبَأْسَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٨﴾

18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanaozuilia na wanaowaambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.

أَشِحَّةً عَلَيْكُمْ فَإِذَا جَاءَ الْخَوْفُ رَأَيْتَهُمْ يَنظُرُونَ إِلَيْكَ تَدُورُ أَعْيُنُهُمْ كَالَّذِي يُغْشَىٰ عَلَيْهِ مِنَ الْمَوْتِ فَإِذَا ذَهَبَ الْخَوْفُ سَلَقُوكُم بِأَلْسِنَةٍ حِدَادٍ أَشِحَّةً عَلَى الْخَيْرِ أُولَـٰئِكَ لَمْ يُؤْمِنُوا فَأَحْبَطَ اللَّـهُ أَعْمَالَهُمْ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴿١٩﴾

19. Wana choyo juu yenu. Ikija hofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka kama ambaye amezimia kwa mauti, lakini hofu inapoondoka wanawaudhi kwa ndimi kali, na wanaifanyia choyo kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amezipomosha amali zao. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.

يَحْسَبُونَ الْأَحْزَابَ لَمْ يَذْهَبُوا وَإِن يَأْتِ الْأَحْزَابُ يَوَدُّوا لَوْ أَنَّهُم بَادُونَ فِي الْأَعْرَابِ يَسْأَلُونَ عَنْ أَنبَائِكُمْ وَلَوْ كَانُوا فِيكُم مَّا قَاتَلُوا إِلَّا قَلِيلًا ﴿٢٠﴾

20. Wanadhani yale makundi hayajaondoka. Wanatamani wangelikuwa jangwani pamoja na mabedui wakiuliza habari zenu. Na lau wangelikuwa pamoja nanyi wasingelipigana isipokuwa kidogo tu.

KUKIMBIA HAKUTAWAFAA

Aya 16 – 20

MAANA

Sema: Hakutawafaa kukimbia; ikiwa mnakimbia kifo au kuuawa.

Walikimbia jihadi kwa kuhofia mauti, na mtu hawezi kuepuka kifo kwa kukimbia, wala mwenye kukipenda pia hawezi kubakia.

Na hata hivyo hamtastareheshwa isipokuwa kidogo tu.

Ikiwa mtasalimika kifo kwenye uwanja wa vita, basi mtakutana nacho baada ya muda mchache tu, kisha muingie motoni. Lakini mashahidi watakwenda kwenye Pepo yenye neema. Imam Ali(a.s) anasema:“Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, mapigo elfu moja ya panga kwangu ni mepesi zaidi kuliko kufa kitandani.”

Sema, ni nani atakayewalinda na Mwenyezi Mungu akiwatakia uovu au akiwatakia rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Tutaifasiri na kauli yake nyingine Mwenyezi Mungu: “Sema ni nani awezaye kuwasaidia chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka kuwadhuru au akitaka kuwanufaisha?” (48:11). Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:11).

Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanaozuilia na wanaowaambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawajua wanafiki na kwamba wao wanawazuia watu wasiende vitani na kuwaambia: Kuna haja gani ya vita njooni tule raha. Wanapofichuka basi wanakwenda vitani kwa kujisukuma, kama vile wanapelekwa machinjioni, wanapigana kidogo kidogo na kuwa wazito. Watu wa aina hii wanapatikana kila wakati.

Wana choyo juu yenu kwa mali na ushindi, ubakhili wote Mwenyezi Mungu anausamehe; isipokuwa ubakhili wa jihadi na mali.

Ikija hofu utawaona wanakutizama na macho yao yanazunguka kama ambaye amezimia kwa mauti, lakini hofu inapoondoka wanawaudhi kwa ndimi kali.

Aya hii inaelezea woga wa wanafiki na udhaifu wao kwenye kifo. Wana jeuri ya ya dhambi wakiwa salama, lakini ukianguka mshindo macho yao yanazunguka kwa fazaa na woga, wakishasalimika ndimi zao zinaanza kuwauma waumini wanaopigana jihadi.

Katika Nahjul-balagha kuna maelezo haya:“Hakika mnafiki anazungumza yanayomjia kwenye ulimi wake: hajui anayostahiki na yaliyo wajibu kwake.” Mtume naye anasema:“Haiwi sawa imani ya mja mpaka uwe sawa moyo wake, wala hauwi sawa moyo wake mpaka uwe sawa ulimi wake.”

Na wanaifanyia choyo kheri.

Makusudio ya kheri hapa ni ngawira. Yaani wao wakati wa vita ni waoga, lakini wakati wa kugawanya ngawira wanapandisha sauti kwa kuhoji na kwamba wao wana haki zaidi kuliko wote. Hao hawakuamini; bali walidhihirisha imani wakaficha kufuru, wakapi- gana pamoja nanyi kwa unafiki na riya.

Basi Mwenyezi Mungu amezipomosha amali zao.

Yaani amebatilisha kupigana kwao kwa sababu kulikuwa ni kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Kuna Hadith inayosema: “Yeyote ambaye kuhama (kuhajiri) kwake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kuhama kwake ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ambaye kuhama kwake ni ili aipate dunia au mwanamke wa kumuoa, basi kuhama kwake ni kwa lile alilolihamia.”

Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.

Hilo la kupomosha kupigana kwao. Ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa sababu Yeye si dhalimu.

Wanadhani yale makundi hayajaondoka.

Makundi yaliondoka bila ya kurejea, lakini wanafiki hawamini macho yao; si kwa lolote ila ni kwa kuwa wanatamani lau makundi yale yangelimfyeka Mtume na sahaba zake. Matamanio yao haya yakawapa picha kuwa makundi yale bado yako yameuzingira mji wa Madina na kwamba watawamaliza Waislamu kesho au keshokutwa.

Wanatamani wangelikuwa jangwani pamoja na mabedui wakiuliza habari zenu.

Wanafiki wakihakikisha kuwa makundi yameshindwa; kisha yarudi tena mara ya pili Madina, basi watatamani wanafiki lau wangelikuwa mbali na Madina wakikaa jangwani wawe wakiuliza tu yaliyowapata waislamu.

Na lau wangelikuwa pamoja nanyi wasingelipigana isipokuwa kidogo tu.

Huu ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyotangulia ‘Wala hawaingii vitani ila kidogo tu.’

22

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾

21. Hakika nyinyi mna ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu – kwa mwenye kumtarajia Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi.

وَلَمَّا رَأَى الْمُؤْمِنُونَ الْأَحْزَابَ قَالُوا هَـٰذَا مَا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَصَدَقَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَمَا زَادَهُمْ إِلَّا إِيمَانًا وَتَسْلِيمًا ﴿٢٢﴾

22. Na waumini walipoyaona makundi walisema: Haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hayo hayakuwazidishia ila imani na utii.

مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّـهَ عَلَيْهِ فَمِنْهُم مَّن قَضَىٰ نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن يَنتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِيلًا ﴿٢٣﴾

23. Miongoni mwa waumini wapo wanaume waliotimiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea; wala hawakubadilisha ahadi yao hata kidogo.

لِّيَجْزِيَ اللَّـهُ الصَّادِقِينَ بِصِدْقِهِمْ وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ إِن شَاءَ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٢٤﴾

24. Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa ukweli wao na awaadhibu wanafiki, akipenda, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

وَرَدَّ اللَّـهُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِغَيْظِهِمْ لَمْ يَنَالُوا خَيْرًا وَكَفَى اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ الْقِتَالَ وَكَانَ اللَّـهُ قَوِيًّا عَزِيزًا ﴿٢٥﴾

25. Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha wale ambao wamekufuru na ghadhabu yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewakifia waumini, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye uwezo.

وَأَنزَلَ الَّذِينَ ظَاهَرُوهُم مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مِن صَيَاصِيهِمْ وَقَذَفَ فِي قُلُوبِهِمُ الرُّعْبَ فَرِيقًا تَقْتُلُونَ وَتَأْسِرُونَ فَرِيقًا ﴿٢٦﴾

26. Na akawateremsha wale waliowasaidia katika watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia hofu katika nyoyo zao. Badhi yao mkawa mnawaua na wengine mnawateka.

وَأَوْرَثَكُمْ أَرْضَهُمْ وَدِيَارَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ وَأَرْضًا لَّمْ تَطَئُوهَا وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرًا ﴿٢٧﴾

27. Na akawarithisha ardhi yao na majumba yao na mali zao na ardhi ambayo hamjaikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

RUWAZA NJEMA KWA MTUME

Aya 21 – 27

MAANA

Hakika nyinyi mna ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu – kwa mwenye kumtarajia Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi.

Makusudio ya ruwaza hapa ni mfano wa kuigwa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , na kumtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho ni kutaraji thawabu za Mwenyezi Mungu na neema za akhera; na kumkumbuka kwa wingi ni kinaya cha kuswali Swala tano.

Maneno ‘Hakika nyinyi’ yanaelekezwa kwa wale waliomwacha Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) katika vita vya Ahzab. Makusudio ni kuwatahayariza na kuwalalumu, kwa vile walimwacha Mtume wakati mgumu; wakiwa wao wanadai ni waislamu na kuswali na pia kudai wanamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.

Maana ya Aya hii ni kama ile isemayo: “Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio kandoni mwao kubaki nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; wala kujipendelea nafsi zao kuliko nafsi yake.” Juz. 11 (9:120).

Aya hii iaashiria kuwa mwislamu wa kweli hasa ni yule anayemfuata na kumwiga Mtume wake bila ya kumwasi na jambo lolote.

Unaweza kuuliza : mafakihi wameafikiana kuwa mwenye kusema: Lailaha illallah, Muhadur-rasulullah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu) atatendewa wanayotendewa waislamu, awe mtiifu au mwasi, sasa itakuwaje?

Jibu : Ndio atatendewa muamala wa kiislamu katika maisha haya ya dunia; kama vile kuozwa, urithi n.k. Lakini muamala katika maisha haya ni jambo jingine na kuzingatiwa kuwa yeye ni mwislamu mbele ya Mwenyezi Mungu ni jambo jingine.

Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa waislamu wanagawanyika mafungu mawili: Kuna mwislamu mbele za watu, lakini sio mbele ya Mwenyezi Mungu; naye ni yule aliyesema: Lailaha illallah, Muhadur-rasulullah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu) na huku anamwasi Mwenyezi Mungu na Mtume. Huyu atafanyiwa muamala wa Mwislamu duniani tu.

Mwingine ni yule aliyesema Lailaha illallah, Muhadur-rasulullah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu) na akamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Huyu atafanyiwa muamala wa Mwislamu duniani na akhera. Imam Ali (a.s.) anasema: “Ufukara na utajiri ni baada ya kuonekana kwa Mungu (Siku ya Kiyama).”

Na waumini walipoyaona makundi walisema: Haya ndiyo aliyotuahi- di Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hayo hayakuwazidishia ila imani na utii.

Wafsiri wa zamani wametaja kauli mbili kuhusiana na Aya hii. Ilio na nguvu zaidi ni ile isemayo kuwa Mtume alikuwa amewaahidi waislamu kupatwa na misukosuko aina kwa aina na kwamba makafiri na washirikina watajitokeza kuwapiga vita na kutaka kuwafyeka kabisa.

Ahadi hii imeelezwa katika Aya ismayo: “Au mnadhani kuwa mtaingia Peponi na hali hamjajiwa na mfano wa wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara” Juz. 2 (2:214).

Waislamu walipoona makundi ya majeshi yakiwazingira kila upande, walisema haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hali hiyo ikawazidishia imani na utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wakazidi imani juu ya imani. Ama wanafiki na wale walio na maradhi nyoyoni mwao walisema: ‘Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakutuahidi ila udanganyifu.’

Miongoni mwa waumini wapo wanaume waliotimiza waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu katika jihadi na uthabiti wakati wa kukutana na adui, mpaka wakati wa kufa.

Baadhi yao wamekwisha kufa kabla ya vita vya Ahzab; kama mashahidi wa vita vya Badrina baadhi wanangojea kufa shahid au ushindi;wala hawakubadilisha ahadi yao hata kidogo. Vile vile wanafiki na wenye maradhi nyoyoni, hawakubadilika; bali walikufa na unafiki.

Wafasiri wanasema kuwa Anas bin Annadhr hakuwepo kwenye vita vya Badr; akasikitika na akasema: sikuwepo kwa mashuhudio ya kwanza alioshuhudia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , lakini kama Mwenyezi Mungu Mtukufu bado ataniononyesha mashuhudio mengine pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , basi ataona nitakavyofanya.

Basi akawako kwenye vita vya Uhud. Akakutana na Sa’d bin Mua’dh, aka- muliza: “Mpaka wapi ewe Abu Amru?” Akajibu: “Nakimbila harufu ya Pepo. Wallah mimi ninaisikia Uhud.” Basi akapigana mpaka akauwawa. Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe kwake. Kwenye kiwiliwili chake kitukufu kulipatikana majeraha ya panga, mikuki na mishale karibu thamanini.

Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa ukweli wao na awaadhibu wanafiki, akipenda, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Pia ni Mwadilifu na Mwenye hekima; hafanyi upuzi wala mchezo katika matakwa yake na vitendo vyake. Humpa thawabu anayestahiki; kama vile wakweli na wenye imani, ikiwa wataendelea na ukweli wao na imani yao. Na atawaadhibu makafiri na wanafiki, ikiwa watang’ang’ania ukafiri na upotevu. Ikiwa watatubia basi atawapa rehema yake na atawasamehe yaliyopita.

Kusema kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na anawaadhibu wanafiki, akipenda,’ maana yake ni kuwa atawaadhibu ikiwa hawatatubia.

Dalili ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.’ Yaani wakitubia atawakubalia toba yao atawasamehe na atawapa rehema yake.

Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha wale ambao wamekufuru na ghadhabu yao.

Ni yale makundi yaliyokusanyika kumuua Mtume(s.a.w.w) kwa kuongozwa na Abu Sufyan. Hawakupata kheri yoyote; yaani lile walilodai kuwa ni kheri; kumuua Mtume na wale walioamini pamoja naye.

Na Mwenyezi Mungu amewakifia waumini na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye uwezo.

Yaani amewatoshea kwenye vita. Abu Hayani Al-Andalusi katika Tafsir yake Al-Bahrul- muhit anasema: “Mwenyezi Mungu aliwatoshea kwenye vita kwa kupeleka upepo na majeshi ambayo ni Malaika. Na imesekana ni Ali bin Abi Twalib na wale waliokuwa pamoja naye. Walipambana, na Ali akamuua Amr.”

Kuna Hadith isemayo: “Pigo la Ali la siku ya Khandaq ni bora kuliko amali za watu na majini.” Riwaya nyingine inasema: “Kupambana Ali na Amr ni amali bora zaidi katika umma wangu hadi siku ya Kiyama.”

Wamenukuu riwaya hizi Al-Hakim katika Mustadrak. Juz. 3 uk. 32, Sayyid Muhsin Al-Amin katika A’yanushia Juz. 2 na Sheikh Al-Mudhaffar katika Dalailussidq Juz. 2.

KISA CHA BANI QURAYDHA KWA UFUPI

Na akawateremsha wale waliowasaidia katika watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia hofu katika nyoyo zao. Badhi yao mkawa mnawaua na wengine mnawateka. Na akawarithisha ardhi yao na majumba yao na mali zao na ardhi ambayo hamjaikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

Yaani waliwasaidia maadui. Makusudio ya watu wa Kitabu hapa ni Bani Quraydha. Ama makusudio ya ardhi ambayo hamjaikanyaga ni bishara ya ushindi wa kiislamu.

Hapo nyuma kidogo tumeeleza kuwa Bani Quraydha walikuwa wakiishi na Mtume(s.a.w.w) huko Madina au kwenye vitongoji vyake na kwamba walikuwa wameahidiana na Mtume kutomsaidia adui. Lakini makundi yalipouzingira mji wa Madina walivunja ahadi na wakatangaza vita; kama ilivyo desturi ya mayahudi wa zamani na wa sasa.

Aya mbili hizi tulizo nazo zinadokeza yaliyowatokea Bani Quraydha baada ya kuvunja ahadi yao na kushindwa jeshi la washirikina; kwa ufupi ni kama ifuatavyo:

Mwenyezi Mungu alipowatoshea waislamu na vita vya Ahzab, msemaji wa Mtume alipiga mbiu ya kuwa watu wawatokee Bani Quraydha. Jeshi la waislamu lilipowafikia lilizingira ngome zao. Mtume akawakaribisha kwenye Uislamu; kwamba watastahiki kama wanavyostahiki waislamu wengine; vinginevyo atawazingira mpaka wasilimu au wapigane.

Kiongozi wao Ka’b bin Asad akawashauri kusilimu na kumwamini Muhammad(s.a.w.w) , akasema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu! imekwishawabainikia kuwa yeye ni Nabii aliyetumwa na kwamba yeye mnamkuta kwenye Tawrat.” Lakini walikataa na wakasema: “Hatutaiacha dini yetu.”

Vikwazo viliendelea hadi siku ya ishiri na tano, wakawa karibu waangamie kwa kuchoka na hofu. Ndipo wakamtaka Mtume - kwa hiyari yao wenyewe- wahukumiwe na Sa’d bin Mua’dh, aliyekuwa kiongozi wa Aus waliokuwa na urafiki na Bani Quraydha. Mtume akawakubalia ombi lao na akamwita Sa’d akamwambia: “Hawa wametaka kuhukumia na wewe kwa hiyari yao, basi hukumu kwa unalopenda.” Sa’d akasema: “Na hukumu yangu itatekelezwa?” Mtume(s.a.w.w) akasema: “Ndio.”

Basi Sa’d akahukumu kwamba wanaume walioshiriki vitani wauawe. Mali yao ichukuliwe, watoto wao na wanawake wao wachukuliwe mateka na majumba yao yachukuliwe na Wahajiri sio Ansari, kwa sababu Ansar tayari wanayo majumba na Wahajiri hawana.

Basi Nabii(s.a.w.w) akaamuru wauliwe wanaume wale walioshika silaha na wale waliowachochea Bani Quraydha kuvunja ahadi; kama Hayy bin Akhtab, kiongozi wa Bani Nadhir. Kisha mali ikagawanywa, watoto na wanawake wakawa mateka; kama alivyohukumu Sa’d, aliyechaguliwa na Bani Quraydha wenyewe. Hapa ndipo panapoashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Badhi yao mkawa mnawaua na wengine mkawa mnawateka.’

Tumetangulia kuuleza kuwa mboni ya jicho la Saa’d ilidungwa na mshale wa majeshi ya Ahzab naye akaomba asife hadi aridhike kwa watakavyotiwa adabu Bani Quraydha. Basi baada ya kutekeleza hukumu yake kwao jeraha lilitutumka naye akafariki, radhi za Mungu ziwe kwake, moyo wake ukiwa umetulia kwa kufa shahidi na kukubaliwa dua yake.

JE MUHAMMAD ALIWADHULUMU BANI QURAYDHA?

Unaweza kuuliza : Ilikuwaje Mtume(s.a.w.w) aithibitishe hukumu ya Sa’d iliyokuwa ya nguvu na ukatili; kiasi ambacho maadui wa uislamu wamelifanya tukio hili ni nyenzo ya kuutuhumu na kuutusi Uislamu?

Jibu : Muhammad hakuwadhulumu Bani Quraydha; isipokuwa walijidhulumu wenyewe, kwa kujichagulia wao wenyewe mwishilio huu, kwa ushahidi ufuatao:

Kwanza : wao waliahidiana na Mtume na wakavunja ahadi katika wakati mgumu, kama ilvyo desturi ya mayahudi kuanzia zamani hadi sasa. Mwenyezi Mungu anasema: “Je, kila mara wanapofunga ahadi, kikundi katika wao huitupa? Juz. 1 (2:100).

Pili : Mtume(s.a.w.w) aliwaambia kuwa atawaacha bila ya kuwafanya lolote, kwa sharti waseme: Lailaha illallah, Muhadur-rasulullah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu). Kiongozi wao, Ka’b bin Asad aliwanasihi wamkubalie Muhammad na watamke shahada mbili, wakakataa.

Tatu : Bani Quraydha walikataa kuhukumiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na wakakubali hukumu ya Saa’d.

Nne, Saa’d aliwahukumu kwa sharia yao wanayohukumia watu na wanayoifuata hadi leo, inayosema: “Utakaposongea karibu ya mji kwenda kupigana juu yake, ndipo utakapowapigia ukelele wa amani.

Itakuwa watakapokujibu kwa amani, na kukufungulia, ndipo watu wote watakaoonekana humo, watafanya kazi ya shoka, na kukutumikia. Na kama hautaki kufanya amani nawe, lakini utafanya vita juu yako, ndipo uhusuru; na Bwana, Mungu wako, autiapo mkononi mwako, mpige kila mume aliyemo kwa makali ya upanga; lakini wanawake na watoto na wanyama wa mji, na vilivyo mjini vyote, navyo ni nyara zake zote, uvitwae viwe mateka; nawe utakula nyara za adui zako alizokupa Bwana, Mungu wako” (Kumbukumbu 20: 10 – 14)[9] .

Hii inafahamisha kuwa hukumu yao ni kali zaidi ya alivyohukumu Saa’d, kwa sababu hii inasema wazi kuwa mji ukikubli suluhu basi watu wake wote ni watumwa na ukikataa basi wanaume wote wauliwe kwa makali ya upanga, waliopigana na wale wasiopigana na kuchukua mali na kuwateka watoto na wanawake.

Kuna ibara nyingine iliyo kali zaidi ya hii, kwa sababu inaamuru wauliwe wakazi wote, mpaka wanawake na watoto, kisha mji uchomwe na vyote vilivyomo, kwa namna ambayo haitawezekana kujengwa tena; inasema:

“…Hakika yako uwapige wenyeji wa mji ule kwa makali ya upanga, kwa kuwaangamiza kabisa, pamoja na vitu vyote vilivyomo na wanyama na walio humo, kwa makali ya upanga na nyara zake zote uzikusanye katikati ya njia yake; na uuteketeze kwa moto na nyara zake zote, kuwe sadaka kamili ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wako, nao utakuwa magofu milele usijengwe tena” (Kumbukumbu 13:15 – 16).

Je, baada ya yote inafaa kusemwa kuwa Muhammad amewadhulumu Bani Quraydha na kwamba Saa’d aliwaonea kwa alivyowahukumu? Ni katika hukumu ya uadilifu kumpa mtu lile alilolitaka mwenyewe na kuhukumiwa kwa mujibu wa dini na itikadi yake.

Mayahudi wanaitakidi dini yao na kuifuata kwa matendo kwa kuwachinja wanaume kupora mali kuwateka wanawake, kuvunja majumba na kuchoma vijiji na miji kwa watu wote bila ya hata kuwa na vita nao au kuwa wamevunja ahadi au kufanyiwa hata chembe ya ubaya; kama wanavyowafanyia wapalestina hivi sasa.

Je, atahisabiwa ni dhalimu aliyewahukumu kwa wanavyowafanyia watu wengine? Tena Mtume(s.a.w. w ) aliwaua wale waliovunja ahadi tu na wakatangaza vita. Lakini wao wanaua na wanachoma si kwa lolote ila ni kwa kuwa kuua, kuchoma na ufisadi ndio dini yao.

Hata kama wasingevunja ahadi na kutangaza vita, wakahukumiwa kuuawa, kuporwa mali na kuchukuliwa mateka, bado isingelikuwa ni dhulma, kwa sabu wamehukumiwa kwa mujibu wa dini na wanavyofanya wao.

Sharia zote za dini za Mungu na kanuni za kutungwa zimeafikiana kuwa mwenye kufuata dini atalazimiwa na hukumu zake. Hapa ndio kuna siri ya kauli ya Mtume mtukufu(s.a.w.w) aliyomwambia Saa’d: “Umewahukumu kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu kutoka juu ya mbingu saba.”

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا ﴿٢٨﴾

28. Ewe Mtume! Waambie wake zako: Ikiwa nyinyi mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni niwape kitokanyumba na niwaache mwachano mzuri.

وَإِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٢٩﴾

29. Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia watenda mema, miongoni mwenu, malipo makubwa.

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ مَن يَأْتِ مِنكُنَّ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ يُضَاعَفْ لَهَا الْعَذَابُ ضِعْفَيْنِ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴿٣٠﴾

30. Enyi wake wa Mtume! Yeyote kati yenu atakayefanya uchafu dhahiri, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.

EWE NABII, WAAMBIE WAKE ZAKO

Aya 28 – 30

MAANA

Wake za Mtume(s.a.w.w) walimtaradhia Mtume matumizi zaidi na mapambo, kutokana na ngawira alizompa Mwenyezi Mungu, ndipo ikashuka Aya hii:

Ewe Mtume! Waambie wake zako: Ikiwa nyinyi mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni niwape kitoka-nyumba na niwaache mwachano mzuri. Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia watenda mema, miongoni mwenu, malipo makubwa.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu awahiyarishe wakeze mambo mawili: Ama awaache pamoja na kitoka-nyumba, ikiwa wanataka, wanayoyataka wanawake wengine, ya dunia.

Kitoka-nyumba ni kitu anachotoa mtaliki kumpa mtalaka wake, kwa kuangalia uwezo wa mwanamume. Tazama Juz. 2 (2:236 – 237).

Au waishi na Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kuvumilia shida [10] 1 na malipo yao mbele ya Mwenyezi Mungu huko akhera yatakuwa makubwa.

Basi wake za Mtume(s.a.w.w) wakachagua akhera na wakaiacha dunia na mapambo yake. Aya hii inaitwa Ayatut-takhyir (Aya ya kuhiyarisha).

MTUME NA WAKE WENGI

Aya ya takhyir ni dalili mkataa ya kukadhibisha madai ya wanaokuza mambo, kuwa Mtume alikuwa na wake kwa sababu ya matamnio ya nafsi. Kwa sababu mwenye pupa ya kustarehe na wanawake – kama alivyosema Mustafa Sadiq Rafi – hawezi kuwahiyarisha baina ya kuachana nao au kuishi maisha ya tabu mpaka siku ya mwisho; bali angeliwabembeleza na kuwaambia kuwa atafanya bidii awatimizie. Kuna mithali isemayo: “Tandiko la harusi liko ghali.”

Anasema Al- aqad katika kitabu chake: Abaqriyatul-Islamiyya: “Lau ladha ya hisia kama ingelikuwa ndio kichocheo cha kuoa baada ya kufa Khadija, basi angeliridhisha hisia zake kwa kuoa wasichana tisa wanaosifika kwa urembo huko Makka na Madina na Bara Arabu kwa ujumla. Na bila shaka angewataka wangelimkubali haraka na kwa kujionea fahari, pia mawalii wao wangeliuridhia na kuuonea fahari ukwe huu ambao haushindwi na ukwe wowote.”

Kisha Al-aqad akataja wake za Mtume mmoja baada ya mmoja na akabainisha sababu zilizopelekea kuwaoa na akasema: “Hakika wanaokuza mambo wamesahahu kila hakika miongoni mwa hakika za maisha haya ya ndoa na wakasahau kuwa Muhammad aliitwa mtakatifu na mtawa wakati wa ujana wake, na kwamba yeye alikaa miaka ishirini na tano na hakuchoka katika kuitafuta halali.

Pia wamesahau kwamba alipotaka kuoa katika miaka hiyo alimuoa mwanamke wa miaka 40 aliyemchagua kwa haja ya kuzoena, wala hakuchagua uzuri uliotakiwa kwa starehe. Wamesahau kwamba mtu waliyempa sifa za hisia za starehe, siku nyingine hakuwa akishiba na mkate wa shairi. Yote haya wameyasahau, na yamethibiti katika historia. Wameyasahau kwa vile wanataka kutia kasoro na kuupotosha uhakika.”

Enyi wake wa Mtume! Yeyote kati yenu atakayefanya uchafu dhahiri, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.

Makusudio ya uchafu hapa ni maasi ya aina yoyote na dhahiri ni waziwazi. Wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu wana daraja tukufu mbele ya Mwenyezi Mungu na ya watu kwa kuungana kwao na Mtume mtukufu(s.a.w.w) . Yeyote atakayefanya maasi atakuwa amehatarisha nafasi yake na kustahiki mara mbili zaidi ya anavyostahiki mwingine. Kwa sababu Mwenyezi Mungu huwahesabu watu kulingana na vyeo vyao; kama wanavyohisabiwa kadiri ya akili zao. Amewalaumu manabii kwa namna ambayo hamlaumu mwingine.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA JUZUU YA ISHIRINI