TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 14333
Pakua: 2507


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 25 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14333 / Pakua: 2507
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI Juzuu 20

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

Sura Ya Ishirini Na Nane: Surat Al-Qasas. Tabrasi amesema imeshuka Makka. Ina Aya 88.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

طسم ﴿١﴾

1. Twaa Siin Miim.

تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿٢﴾

2. Hiyo ni Aya za Kitabu kinachobainisha.

نَتْلُو عَلَيْكَ مِن نَّبَإِ مُوسَىٰ وَفِرْعَوْنَ بِالْحَقِّ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٣﴾

3. Tunakuosomea habari za Musa na Firauni kwa haki kwa ajili ya watu wanaoamini.

إِنَّ فِرْعَوْنَ عَلَا فِي الْأَرْضِ وَجَعَلَ أَهْلَهَا شِيَعًا يَسْتَضْعِفُ طَائِفَةً مِّنْهُمْ يُذَبِّحُ أَبْنَاءَهُمْ وَيَسْتَحْيِي نِسَاءَهُمْ إِنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ ﴿٤﴾

4. Hakika Firauni alitakabari katika nchi akagawa watu wake makundi. Akidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wa kiume na akiwaacha watoto wao wa kike. Hakika yeye alikuwa katika wafisadi.

وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ ﴿٥﴾

5. Na tunataka kuwafadhili waliodhoofishwa katika ardhi na kuwafanya wawe ni viongozi na kuwafanya ni warithi.

وَنُمَكِّنَ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَنُرِيَ فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَجُنُودَهُمَا مِنْهُم مَّا كَانُوا يَحْذَرُونَ ﴿٦﴾

6. Na kuwamakinisha katika ardhi. Na kumuonyesha Firauni na Hamana na majeshi yao yale waliyokuwa wakiyahadhari kwao.

AYA ZA KITABU

Aya 1 – 6

TWAA SIIN MIIM.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1)

Hiyo ni Aya za Kitabu kinachobainisha.

Hiyo ni ishara ya Sura hii, Kitabu ni Qur’an na kubainisha ni kupambanua baina ya upotevu na uongofu.

Tunakuosomea habari za Musa na Firauni kwa ajili ya watu wanaoamini.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemsomea Mtume wake mtukufu habari mara kwa mara. Katika Juz. 16 kifungu cha ‘Kukaririka Kisa’ (20:9) tumeeleza lengo la kukaririka kisa cha Musa.

Hakika Firauni alitakabari katika nchi akagawa watu wake makundi.

Alipetuka mipaka na akajifanya jabari, akawagawa wananchi wake kwenye makundi wakigombana, ili udumu utawala wake.

Akidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wa kiume na akiwaacha watoto wao wa kike. Hakika yeye alikuwa katika wafisadi.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:49) na Juz. 9 (7:127).

KWA NINI FIRAUNI ALIWAKANDAMIZA WANA WA ISRAIL?

Mmoja katika wafasiri wa kisasa anasema: “Firauni aliwakandamiza wana wa Israil kwa sababu walikuwa na itikadi isiyoafikiana na itikadi yake. Wao walikuwa wakifuata dini ya babu yao Ibrahim na Ya’qub. Ingawa itikadi yao ilikuwa na upotofu, lakini walibakia na itikadi ya Mungu mmoja.”

Sisi tunamuuliza mfasiri huyu mpya: Umejua vipi kuwa mayahudi waliokuwa wakati wa Firauni walikuwa kwenye dini ya Ibrahim(a.s) na kwamba walibaki na itikadi ya Mungu mmoja? Je, umepata kujua kutokana na kuli yao: “Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu.” Au kauli yao: “Hatutakuamini mpakae tumwone Mungu wazi wazi.”

Au ni kutokana na kuabudu kwao ndama au kwa kuwaua kwao mitume? Ikiwa Firauni aliwakandamiza kwa sababu ya itikadi yao, kwa nini Mtume wao na mwenye ikhlasi zaidi, Musa aliwapa wasifa huu ufuatao? Ufuska, Juz. 6 (5:25), wapumbavu, Juz. 9 (7:155), wabatilifu Juz. 9 (7:153) na ujinga Juz. 9 (7:138). Kama amabavyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya kadhaa amewasifu kwa ufisadi, uovu na kwa kila aina ya hatia?

Qur’an imetaja kwamba Firauni aliwakandamiza wana wa isaril na kwam- ba yeye alipituka mpaka katika dhulma yake, lakini haikuashiria sababu.

Kwa hiyo maulama wametofautiana katika kuielezea. Kuna waliosema kuwa kuhani alimwambia Firauni kuwa atazaliwa mtoto katika wana waisrail, atakayekuja mvua ufalme wake, wengine wakasema kuwa mitume waliokuwa kabla yake walitoa bishara ya kuja kwake.Firauni alipojua hivyo akahofia na kuanza kuwachinja watoto wa kiume wa wana wa israil. Na sikuona yoyote aliyesema kuwa Firauni aliwakandamiza kwa sababu ya kuwa kwenye dini ya Ibrahim.

Tukiangalia sera ya wana wa israil kwa Mtume wao Musa(a.s) na mitume wengine waliokuja baada ya Musa; ambapo walikuwa wakikadhibisha wengine na wengine wakiwaua. Pia tukiangalia sera yao katika miji wanayoiteka jinsi wanavyoleta fitna, kupanga njama, kujaribu kutawala nyenzo na propaganda zote.

Tukiangalia yote haya basi tunakubaliana na Sheikh Maraghi aliyesema: “Firauni aliwakandamiza wana wa israil kwa vile aliwahofia wanaume ambao walikuwa na ufundi na mikononi mwao mlikuwa na hatamu za uchumi; kuwa muda ukiendelea watakuwa juu kiuchumi waje wawashinde wamisri. Na uchumi ndio wenye nguvu kiutawala.”

Ni kweli kuwa Firauni alipetuka mpaka katika dhulma kwa kuwachinja watoto wa kiume na kuwafanya watumwa watoto wa kike wa wana wa israil, lakini sababu ya yote haya ni wayahudi.

Kwa hiyo lawama ni la wote wawili. Mayahudi kwa sababu ya chuki yao, tabia yao na malengo yao mabaya na pia kwa Firauni kwa sababu aliwatesa wasiokuwa na hatia kwa sababu ya wenye hatia.

LINI MWENYEZI MUNGU ATAWAFADHILI WALIODHOOFISHWA?

Na tunataka kuwafadhili waliodhoofishwa katika ardhi.

Waliodhoofishwa katika ardhi ni wale waliokandamizwa na wenye nguvu, waliotawala nyenzo zao na nguvu zao kimabavu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawafadhili uhuru na kujikomboa kwenye ukandamizaji ikiwa watafanya juhudi na kujitolea kwa ajili ya maisha yao na heshima yao; sawa na mgonjwa atapona ikiwa atafanya matibabu mazuri na mkulima atapata mavuno akilima vizuri.

Mwenyezi Mungu ana desturi katika maumbile yake, na wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu kabisa. Kila mwenye kufuata njia atafika, awe mumin au kafiri. Ama malipo ya kafiri na mumin ni siku ya Kiyama, si katika maisha haya.

Basi atakayemnyenyekea dhalimu, Mwenyezi Mungu humdhalilisha na humwachia atakayemdhulumu, hata kama ataswali, kufunga na kuhiji. Kwa sababu ameidhalilisha haki na akisaidia batili na akhera hana kitu.

Na mwenye kujikomboa kutoka kwa dhalimu na watu wake, na akajitolea mhanga kwa ajili ya heshima yake, Mungu humpa nusra kuwashinda mad- halimu na wababe; kwa sababu atakuwa amekutana na utashi wa Mwenyezi Mungu na amri yake, kwa jihadi na uimara.

Hatuna haja ya kurudia historia ya mbali kutafuta ushahidi wa hakika hii. Kwani ukakamavu wa wananchi wa Vietnam mbele ya taifa hilo na nguvu kubwa ya shari na ufisadi, ni dalili kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na mwenye kudhulumiwa anayepigana jihadi aliye mvumilivu, kwa namna yoyote ile atakayokuwa.

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu hapigani kwa ajili ya waliodhoofishwa, lakini anakuwa nao na kuwapa msaada wake, ikiwa watapigana na kupinga kwa lengo la haki, uadilifu na kujikomboa kutoka kwenye makucha ya ukoloni na dhulma. Mwenyezi Mungu yuko pamoja na hawa, kwa sababu, yuko pamoja na kila mwenye kufanya juhudi na akatenda kwa ajili ya maisha.

Haya tumeyafafanua zaidi katika Juz. 13 (13:11).

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwangamiza Firauni na watu wake, akawaokoa wana wa israil na adhabu yao na ukandamizwaji wao. Hii inamaanisha kuwa Mwenyezi Mungu anapigana kwa ajili ya wanyonge; bali kuna Aya isemayo:

إِنَّ اللَّـهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا ﴿٣٨﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini.” Juz. 17 (22:38)?

Jibu : Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwangamiza Firauni na watu wake kwa sababu ya shirki yao na kuwakadhibisha kwao mitume na sio kuwasaidia wana wa israili; sawa na alivyoangamiza kaumu ya Nuh na washirikina wengineo.

Kwa hiyo wana wa israil na wengineo wakapona na dhulma na ukandamizwaji. Ama makusudio ya walioamini, wanaokingwa na Mwenyezi Mungu ni wale wanopigana jihadi. Na wavivu wako kwenye dini ya wale waliomwambia Musa:

فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ ﴿٢٤﴾

“Nenda wewe na Mola wako mkapigane, hakika sisi ni wenye kukaa hapa.” Juz. 6 (5:24)

Na kuwafanya wawe ni viongozi.

Yaani tuwafanye mitume miongoni mwao.

Na kuwafanya ni warithi na kuwamakinisha katika ardhi.

Mwenyezi Mungu anawafanya huru kwa muda mrefu baada ya kuwa utumwani.

Na kumuonyesha Firauni na Hamana na majeshi yao yale waliyokuwa wakiyahadhari kwao.

Kwao ni kwa hao wana wa israil. Maana ni kuwa Firauni na watu wake walihofia utawala wao usiingie mikononi mwa wana wa israil, ndio wakachukua hadhari, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaingiza kwenye yale waliyoyahofia.

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّ مُوسَىٰ أَنْ أَرْضِعِيهِ فَإِذَا خِفْتِ عَلَيْهِ فَأَلْقِيهِ فِي الْيَمِّ وَلَا تَخَافِي وَلَا تَحْزَنِي إِنَّا رَادُّوهُ إِلَيْكِ وَجَاعِلُوهُ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧﴾

7. Na tulimpa wahyi mama wa Musa kuwa mnyonyeshe. Na utakapomhofia basi mtie mtoni. Na usihofu wala usihuzunike. Hakika sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa mitume.

فَالْتَقَطَهُ آلُ فِرْعَوْنَ لِيَكُونَ لَهُمْ عَدُوًّا وَحَزَنًا إِنَّ فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَجُنُودَهُمَا كَانُوا خَاطِئِينَ ﴿٨﴾

8. Basi wakamwokota watu wa Firauni aje kuwa adui kwao na huzuni. Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa.

وَقَالَتِ امْرَأَتُ فِرْعَوْنَ قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ لَا تَقْتُلُوهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾

9. Akasema mke wa Firaun: Ni kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa au tumfanye kuwa mtoto wetu. Wala wao hawakutambua

وَأَصْبَحَ فُؤَادُ أُمِّ مُوسَىٰ فَارِغًا إِن كَادَتْ لَتُبْدِي بِهِ لَوْلَا أَن رَّبَطْنَا عَلَىٰ قَلْبِهَا لِتَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠﴾

10. Moyo wa mamake Musa ukawa mtupu. Alikuwa karibu kudhihirisha, lau tusingeliuimarisha moyo wake ili awe miongoni mwa waumini.

وَقَالَتْ لِأُخْتِهِ قُصِّيهِ فَبَصُرَتْ بِهِ عَن جُنُبٍ وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١١﴾

11. Akamwambia dadake (Musa) mfuatie. Basi akawa anamwangalia kiupande upande na wao hawatambui.

وَحَرَّمْنَا عَلَيْهِ الْمَرَاضِعَ مِن قَبْلُ فَقَالَتْ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ أَهْلِ بَيْتٍ يَكْفُلُونَهُ لَكُمْ وَهُمْ لَهُ نَاصِحُونَ ﴿١٢﴾

12. Na tukamharamishia wanyonyeshaji tangu mwanzo. Akasema (dadake): Je, niwaonyeshe watu wa nyumba watakaowalelea na watakuwa wema kwake?

فَرَدَدْنَاهُ إِلَىٰ أُمِّهِ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلَا تَحْزَنَ وَلِتَعْلَمَ أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٣﴾

13. Basi tukamrudisha kwa mama yake ili yaburudike macho yake na ajue kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Lakini watu wengi hawajui.

MAMA WA MUSA

Aya 7 – 13

MAANA

Na tulimpa wahyi mama wa Musa kuwa mnyonyeshe.

Makusudio ya wahyi hapa ni ilhamu; ni mfano kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na Mola wako akampa wahyi nyuki.” Juz. 14 (16:68). Katika Juz. 9 (7: 103 -112).

Tumenukuu kutoka kitabu Qisasul-qur’an, kwamba jina la mama yake Musa ni Yukabid (Jochebed). Kisha tukasoma katika Tawrat kuwa hilo ndilo jina lake na kwamba aliolewa na Amram, mtoto wa kaka yake. Musa ndiye mdogo katika watoto wa baba yake, akiwa ni watatu, baada ya Maryam na Harun.

Na utakapomhofia basi mtie mtoni.

Makusudio ya mto hapa ni mto Nile. Maana ni akimhofia kuchinjwa amtie mtoni kwa mkono wake! Itakuwaje, mwenye akili aweze kujitupa motoni?

Lakini akaambiwa: Na usihofu wala usihuzunike. Hakika sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa mitume.

Usimhofie, hakika Mwenyezi Mungu ndiye mhifadhi na mlinzi. Yule ambaye ameujaalia moto kuwa baridi na salama kwa Ibrahim, ataijalia bahari kuwa amani kwa Musa. Alimpa habari ya usalama wa mtoto wake na kwamba yeye atamlea na pia akampa habari njema kuwa amemchagua kwa risala yake na kumhusu kwa rehema yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:38).

Basi wakamwokota watu wa Firauni aje kuwa adui kwao na huzuni.

Walimwokota na kumlea kwa kumfanya mtoto wao, lakini akaja akawa ni adui wa itikadi yao na desturi yao. Akaingiza huzuni nyoyoni mwao na mwisho wa ufalme wao ukawa mikononi mwake.

Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa, wapotevu katika vitendo vyao vyote; hasa kuua maelefu ya vijana ili kujiepusha na Musa, lakini ikawa wao wanamwepusha Musa na mauti ili aje awamalize. Katika kamusi ya Kitabu kitakatifu[4] , imeelezwa kuwa maisha ya Musa katika nyumba ya Firauni hayakujulikana kwa ufafanuzi na kwamba wanahistoria wametofautiana kuhusu wakati wake alioishi. Wengine wakasema ni wakati wa Firauni Amenophis (Amenhotep II) (1411 – 1436 Bc), wengine wakasema ni Ramesses II (1223 – 1290 Bc). Pia kuna waliosema ni wakati wa Mernptsh ( 1211 – 1223 Bc).

Akasema mke wa Firaun: Ni kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuue! Huenda akatufaa au tumfanye kuwa mtoto wetu. Wala wao hawakutambua.

Kuburudika macho ni furaha. Mke wa Firauni ni Asiya bint Muzahim. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemsifu pale aliposema:

وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا لِّلَّذِينَ آمَنُوا امْرَأَتَ فِرْعَوْنَ إِذْ قَالَتْ رَبِّ ابْنِ لِي عِندَكَ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَنَجِّنِي مِن فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿١١﴾

“Na Mwenyezi Mungu amewapiga mfano walioamini – mke wa Firauni, aliposema: “Mola wangu! Nijengee kwako nyumba Peponi na uniokoe na Firauni na vitendo vyake na uniokoe na watu madhalimu.” (66:11).

Na katika Hadith imesemwa kuwa wanawake bora ni wane: Maryam binti Imran, Asiya binti Muzahim, Khadija bint Khuwaylid na Fatima bint Muhammad. Firauni alipomwangalia mtoto alishtuka na kusema, imekuaje huyu mtoto wa ki Hebrew amepona kuchinjwa? Majasusi hawakumuona au wamenificha?

Mkewe akamtuliza na akamfanya ampende mtoto ili awe kiburudisho cha macho yao, lakini akawa ni kero ya macho yao na huzuni ya nyoyo zao.

Moyo wa mamake Musa ukawa mtupu. Alikuwa karibu kudhihirisha, lau tusingeliuimarisha moyo wake ili awe miongoni mwa waumini.

Alimtupa mtoto wake baharini akiwa na matumaini ya kuukotwa na ambaye atamwepusha na Firauni. Mara kadari ikamtoa baharini hadi nyumbani kwa Firauni!

Alipopata habari kuwa ameanguka mikononi mwa mchinjaji, alijua mtoto wake amekwisha.

Akafazaika sana na akajisahau na ahadi aliyoahidiwa na Mungu kuwa atamrudisha kwake; akawa karibu adhihirishe fazaa yake kwa kutamka jina la kipenzi chake, lakini Mwenyezi Mungu akampa utuvu, akaufanya thabiti moyo wake ili awe miongoni mwa wanaoamini ahadi yake. Kwa hiyo akawa na subira na akatulia.

Akamwambia dadake (Musa), mfuatie na uchunguze habari yake.

Akaenda na akamkuta kwa Firauni.

Basi akawa anamwangalia kiupande upande na wao hawatambui.

Wengine wamefasiri alimwangalia kwa mbali.

Maana ni kuwa alimwangalia kama vile hataki wala hamkusudii yeye, huku watu wa Firauni hawajui lengo lake au kuwa yeye ni dada wa mtoto waliyemuokota ufukweni.

Na tukamharamishia wanyonyeshaji tangu mwanzo.

Firauni alimsikiliza mkewe, akamwacha mtoto baada ya Mwenyezi Mungu kutia mahaba moyoni mwake na akaamrisha atafutwe mnyonyeshaji atakayemlea na kumtunza.

Wakaletwa wanyonyeshaji kutoka huku na huko, kila mmoja anapendelea akubali matiti yake ili apate hadhi mbele ya Firauni. Lakini mtoto aliwakataa wote.

Akasema (dadake): Je, niwaonyeshe watu wa nyumba watakaowalelea na watakuwa wema kwake.

Dadake Musa alipoona kuduwaa kwa watu wa Firauni kuhusu mtoto alijitokeza kuwaelekeza atakayekubali matiti yake na kumshughulikia bila ya kuzembea. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:40).

Basi tukamrudisha kwa mama yake ili yaburudike macho yake.

Vile vile umetangulia mfano wake katika Juzuu hiyo hiyo.

Na ajue kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli.

Yaani mamake Musa ajue kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kurudishiwa mwanawe na kuwa miongoni mwa mitume, ni kweli.

Lakini watu wengi hawajui, mipangilio yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na undani wa hekima yake.

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI

وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَاسْتَوَىٰ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١٤﴾

14. Na alipofikilia kukomaa kwake na akastawi, tulimpa hukmu na elimu. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

وَدَخَلَ الْمَدِينَةَ عَلَىٰ حِينِ غَفْلَةٍ مِّنْ أَهْلِهَا فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَـٰذَا مِن شِيعَتِهِ وَهَـٰذَا مِنْ عَدُوِّهِ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ قَالَ هَـٰذَا مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ عَدُوٌّ مُّضِلٌّ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾

15. Na akaingia mjini wakati wenyeji wake wako kwenye mghafala. Akakuta humo watu wawili wanapigana – huyu ni katika kundi lake na huyu ni katika adui zake. Yule aliye katika kundi lake alimtaka msaada dhidi ya yule aliye katika adui zake. Musa akampiga, akammaliza. Akasema: Hiki ni kitendo cha shetani; hakika yeye ni adui mpotezaji dhahiri.

قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي فَغَفَرَ لَهُ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿١٦﴾

16. Akasema: Mola wangu! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

قَالَ رَبِّ بِمَا أَنْعَمْتَ عَلَيَّ فَلَنْ أَكُونَ ظَهِيرًا لِّلْمُجْرِمِينَ ﴿١٧﴾

17. Akasema: Mola wangu! Kwa ulivyonineemesha, sitakuwa msaidizi wa wakosefu.

فَأَصْبَحَ فِي الْمَدِينَةِ خَائِفًا يَتَرَقَّبُ فَإِذَا الَّذِي اسْتَنصَرَهُ بِالْأَمْسِ يَسْتَصْرِخُهُ قَالَ لَهُ مُوسَىٰ إِنَّكَ لَغَوِيٌّ مُّبِينٌ ﴿١٨﴾

18. Akapambaukia mjini akiwa na hofu na hadhari, mara yule aliyemtaka msaada jana anampigia kelele. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mpotevu dhahiri.

فَلَمَّا أَنْ أَرَادَ أَن يَبْطِشَ بِالَّذِي هُوَ عَدُوٌّ لَّهُمَا قَالَ يَا مُوسَىٰ أَتُرِيدُ أَن تَقْتُلَنِي كَمَا قَتَلْتَ نَفْسًا بِالْأَمْسِ إِن تُرِيدُ إِلَّا أَن تَكُونَ جَبَّارًا فِي الْأَرْضِ وَمَا تُرِيدُ أَن تَكُونَ مِنَ الْمُصْلِحِينَ ﴿١٩﴾

19. Basi Musa alipotaka kumkamata kwa nguvu, yule aliye adui yao akasema: Ewe Musa! Unataka kuniua, kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki ila kuwa jabari katika ardhi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wema.

ALIPOFIKIA KUKOMAA

Aya 14 – 19

MAANA

Na alipofikilia kukomaa kwake na akastawi, tulimpa hukmu na elimu. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 12 (12:22). Kule imekuja kwa wasifu wa Yusuf na hapa ni wa Musa.

Na akaingia mjini wakati wenyeji wake wako kwenye mghafala. Akakuta humo watu wawili wanapigana – huyu ni katika kundi lake na huyu ni katika adui zake. Yule aliye katika kundi lake alimtaka msaada dhidi ya yule aliye katika adui zake. Musa akampiga, akam- maliza.

Makusudio ya mji hapa ni mji wa Misri.

Siku moja Musa aliingia mitaani bila ya kujulikana na yeyote. Akawaona watu wawili wanagombana na kupigana – mmoja ni Mkibti katika wafuasi wa Firauni na mwingine ni Mwisrail katika jamaa za Musa. Kwa ujumla Wakibti walikuwa wakiwakandamiza waisrail na wakiwahisabu ni watumishi na watumwa wao.

Basi yule Mwisrail akamtaka msaada Musa. Musa naye akampiga ngumi au fimbo kwa kukusudia kumtia adabu na kukinga dhulma, si kwa kukusudia kuua na yule akaanguka ni maiti. Huku kunaitwa kuua kimakosa.

Akasema: Hiki ni kitendo cha shetani; hakika yeye ni adui mpotezaji dhahiri.

Anakusudia kile kitendo cha kugombana wale wawili sio pigo alilopiga Musa. Maana ni kuwa mapigano baina ya wawili, chanzo chake ni wasi-wasi wa shetani na hadaa yake ya kuingiza kwenye uasi na madhambi.

Akasema: Mola wangu! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Mitume na mawili wanajiona mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wapungufu. Hiyo ni katika aina ya kunyenyekea na dua. Hilo halifahamishi kuweko dhambi wala upungufu.

Kwa sababu anayemjua Mwenyezi Mungu kisawasawa huwa anaituhumu nafsi yake kuwa na upungufu wa kumtii Mwenyezi Mungu na kumwabudu.

Ndio maana humwomba msamaha wa dhambi. Wa kale walisema: “Uovu wa watu wema ni wema wa waovu.” Tazama tuliyoyaeleza kwa anuani ya ‘Toba na maumbile’ katika Juz. 4 (4:17-18).

Akasema: Mola wangu! Kwa ulivyonineemesha, sitakuwa msaidizi wa wakosefu.

Musa alimuomba msamaha Mola wake na akamwahidi kuwa atawapiga vita mataghuti na wakosefu; kama vile Firauni na jeshi lake na kumsaidia kila mumin.

Akapambaukia mjini akiwa na hofu na hadhari.

Musa alihofia kuuawa kwa sababu ya Mkibti na kutarajia shari kutoka kwa Firauni na watu wake.

Wakati akiwa katika hali hiyo, mara yule aliyemtaka msaada jana anampigia kelele. Anampigia kelele za kumtaka msaaada. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mpotevu dhahiri.

Wewe kazi yako ni kugombana na Wakibti na kutusababishia matatizo. Hebu chunga upotevu wako!

Basi Musa alipotaka kumkamata kwa nguvu yule aliye adui yao,

Musa alitaka kumkamata Mkibti, kwa sababu wakibti ndio waliokuwa wakiwachokoza waisrail na kuwachukulia kuwa ni watumwa wao, kama tulivyoashiria mwanzo. Mkibti alidhani kuwa Musa anataka kumuua, kwa hiyo akasema:

Ewe Musa! Unataka kuniua, kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki ila kuwa jabari katika ardhi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wema.

Jana ulimuua mtu na leo unataka kuniua mimi, je wewe ni mbabe au mtu mwema? Hii inaashiria kwamba Musa alikuwa ni katika watu wema mwenye tabia nzuri na kwamba kuua hakuendani na tabia yake.

وَجَاءَ رَجُلٌ مِّنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ يَسْعَىٰ قَالَ يَا مُوسَىٰ إِنَّ الْمَلَأَ يَأْتَمِرُونَ بِكَ لِيَقْتُلُوكَ فَاخْرُجْ إِنِّي لَكَ مِنَ النَّاصِحِينَ ﴿٢٠﴾

20. Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akaipiga mbio, akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanapanga kukuua. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanaokupa nasaha.

فَخَرَجَ مِنْهَا خَائِفًا يَتَرَقَّبُ قَالَ رَبِّ نَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢١﴾

21. Basi akatoka mjini akiwa na hofu na hadhari. Akasema: Mola wangu! Niokoe na watu madhalimu.

وَلَمَّا تَوَجَّهَ تِلْقَاءَ مَدْيَنَ قَالَ عَسَىٰ رَبِّي أَن يَهْدِيَنِي سَوَاءَ السَّبِيلِ ﴿٢٢﴾

22. Alipoelekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu akaniongoza njia iliyo sawa.

وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِّنَ النَّاسِ يَسْقُونَ وَوَجَدَ مِن دُونِهِمُ امْرَأَتَيْنِ تَذُودَانِ قَالَ مَا خَطْبُكُمَا قَالَتَا لَا نَسْقِي حَتَّىٰ يُصْدِرَ الرِّعَاءُ وَأَبُونَا شَيْخٌ كَبِيرٌ ﴿٢٣﴾

23. Alipoyafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wakinywesha (wanyama wao), na akakuta nyuma yao wanawake wawili wanazuia (wanyama wao). Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi mpaka wamalize hao wachunga na baba yetu ni mzee sana.

فَسَقَىٰ لَهُمَا ثُمَّ تَوَلَّىٰ إِلَى الظِّلِّ فَقَالَ رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ ﴿٢٤﴾

24. Basi akawanyweshea kisha akarudi kivulini na akasema: Mola wangu! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayoniteremshia.

فَجَاءَتْهُ إِحْدَاهُمَا تَمْشِي عَلَى اسْتِحْيَاءٍ قَالَتْ إِنَّ أَبِي يَدْعُوكَ لِيَجْزِيَكَ أَجْرَ مَا سَقَيْتَ لَنَا فَلَمَّا جَاءَهُ وَقَصَّ عَلَيْهِ الْقَصَصَ قَالَ لَا تَخَفْ نَجَوْتَ مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٥﴾

25. Basi mmoja wa wale wanawake wawili akamjia naye anatembea akiona haya. Akasema: Baba yangu anakuita akulipe ujira wa kutunyweshea.Basi alipomjia na kumsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwishaokoka na watu madhalimu.

قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ ﴿٢٦﴾

26. Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumwajiri ni mwenye nguvu na mwaminifu.

قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٢٧﴾

27. Akasema: Mimi ninataka kukuoza mmoja wa mabinti zangu hawa wawili kwa kunifanyia ajira ya miaka minane na kama ukitimiza kumi hiyari yako. Mimi sitaki kukutaabisha. Inshaallah utanikuta miongoni mwa watu wema.

قَالَ ذَٰلِكَ بَيْنِي وَبَيْنَكَ أَيَّمَا الْأَجَلَيْنِ قَضَيْتُ فَلَا عُدْوَانَ عَلَيَّ وَاللَّـهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌ ﴿٢٨﴾

28. Akasema: Hayo yamekwishakuwa baina yangu na yako. Muda wowote kati ya miwili nitakoumaliza nisifanyiwe ubaya na Mwenyezi Mungu ni wakili juu ya haya tunayoyasema.

NJAMA

Aya 20 – 28

MAANA

Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akaipiga mbio, akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanapanga kukuua. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanaokupa nasaha.

Firauni na wapambe wake walijua yaliyotokea baina ya Musa na Mkibti wa kwanza aliyemuua kimakosa na wa pili aliyemwambia unataka kuniua. Kwa hiyo wakashauriana kuhusu mambo ya Musa na kuazimia kumuua. Mmoja wa waumini alipojua hilo alikimbia kwa Musa kumpa habari na akamshauri awakimbie madhalimu.

Wafasiri wengi wamesema kuwa mumin huyu ni yule aliyeashiriwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

“Na akasema mumin aliyekuwa mmoja katika watu wa Firauni aliyeficha imani yake: Mtamuua mtu kwa kusema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu naye amewajia na hoja zilizo wazi?” (40:28).

Basi akatoka mjini akiwa na hofu na hadhari. Akasema: Mola wangu! Niokoe na watu madhalimu.

Musa alitoka mjini bila ya maandalizi yoyote; hana chakula wala maji, au yeyote wa kuongozana naye. Alitoka kwa hadhari akihofia asionekane na chinjachinja wa Firauni. Zaidi ya hayo alikuwa hajui anakwenda wapi? Basi akamkimbilia Mola wake, akamwachia Yeye mambo yake na akamwomba kuongoka na kuokoka na Firauni na watu wake.

Alipoelekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu akaniongoza njia iliyo sawa.

Musa alitembea bila ya kujua anakwenda wapi, lakini ana yakini kuwa Mola wake atamwongoza njia iliyo sawa ambayo itampelekea kuokoka na kufaulu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamshika mkono na kumwelekeza Madyana, mji wa Shua’yb, ambao baina yake na Misri pana masafa ya mwendo wa siku nane katika jangwa pana sana.

Basi Musa akakata mbuga kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa akila mimea ya ardhini. Jana alikuwa ikulu ya Firauni akistarehe. Mimea ya ardhi na hofu ni bora mara elfu kwa wenye ikhlasi kuliko starehe pamoja na dhulma; kama alivyosema Imam Husein(a.s) : “Wallahi! Sioni mauti ila ni wema; na sioni kuishi pamoja na madhalimu ila ni uovu.”

Alipoyafikia maji ya Madayana alikuta umati wa watu wakinywesha (wanyama wao) na akakuta nyuma yao wanawake wawili wanazuia (wanyama wao). Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi mpaka wamalize hao wachunga na baba yetu ni mzee sana.

Mwendo wa Musa uliishia kwenye kisima. Akakuta kundi la watu waki-wanywesha maji wanyama wao na akawaona wanawake wawili pembeni wakiwa na kondoo wao wanataka kunywa maji, lakini wao wanawazuia.

Musa akashtuliwa na hali hii, akawauliza, kwa nini mnawazuia nao wana kiu? Wakasema sisi ni wanawake dhaifu, hatuwezi kusukumana na wanaume. Tunangoja mpaka wamalize ndio nasi tupate nafasi, na baba yetu ni mzee sana, hawezi kuja kuchota maji. Nafsi ya Musa ikataharaki kidini na kiubinadamu, akawasaidia.

Hakuna ajabu kwa Musa kuwasaidia wanawake dhaifu; wala si ajabu kwa Shua’yb na mabinti zake kuishi kwa jasho lao.

Hii ndiyo sera ya mitume na makhalifa wao wenye takua, tangu zamani na baadaye. Bali ajabu ni kuwa roho hii ya Qur’an haina athari yoyote katika nafsi zetu sisi tunaodai kumjua Mwenyezi Mungu, Kitabu chake, na sera ya mitume wake. Ajabu ya maajabu ni kwamba tunashindana katika kuitafuta dunia na mapambo yake.

Basi akawanyweshea, kisha akarudi kivulini na akasema: Mola wangu! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayoniteremshia.

Musa aliwapatia maji wanyama wa wasichana wawili, kisha akaenda chini ya mti kupata kivuli, akiwa na uchovu na njaa. Akamwomba Mwenyezi Mungu fadhila na ukarimu wake. Wala hakung’angania sana au kuomba zaidi, kwa sababu alichokitaka ni kuziba tumbo tu.

Kama angelikuwa anaomba akhera angeling’ang’ania. Katika Nahjul balagha imeelezwa: “Wallahi hakumuomba isipokuwa mkate wa kula tu. Rangi ya kijani ya majani ilikuwa ikionekana kwenye ngozi ya tumbo lake kwa wembamba wake na kutengana na nyama yake.”

Basi mmoja wa wale wanawake wawili akamjia naye anatembea akiona haya. Akasema: Baba yangu anakuita akulipe ujira wa kutunyweshea.

Wale wasichana wawili walirudi kwa baba yao na wakamwelezea yaliyotokea. Basi akamwambia mmoja wao: Nenda kamwite tuje tumlipe hisani yake. Basi akaenda msichana akiwa amegubikwa na haya, ustahi na heshima na kumweleza alivyosema baba yake.

Basi alipomjia na kumsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwishaokoka na watu madhalimu.

Musa alikubali mwito, na mzee akamkaribisha na kumshukuru kwa kitendo chake. Musa alipotulia na kumwamini yule mzee, alimsimulia yaliyompitia kwa Firauni na watu wake. Yule mzee akamwambia usihofu, umefika. Hapa kwetu ni ngome ya amani, haifikiwi na Firauni wala mfano wake katika madhalimu.

Wafasiri wametofautiana kuhusu mzee huyu ni nani? Wengi wao wamesema ni Shuaib na wengine wakasema siye. Hakuna ya kutegemewa kwa hawa wala wale. Nasi hatuna haja na tofauti hizi madam hazina uhusiano wowote na imani wala maisha.

Sisi tumechagua jina la Shua’yb kiasi cha kumwelezea huyo mzee tu, sio kuwa tumekubaliana na jina hilo na pia kwa kuwa ni jina liloenea kwa wengi; kama lilivoenea baina ya wanafunzi na ulamaa wa Najaf.

Akasema mmoja katika wale wanawake ambaye alimwita kwa baba yake: Ewe baba! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumwajiri ni mwenye nguvu na mwaminifu.

Tunasema aliyesema ni yule aliyemwita kutokana na kauli yake ‘mwenye nguvu’ pale alipowasaidia kuchota maji na ‘mwaminifu’ pale alipokuwa na staha wakati wakielekea kwa baba yake.

Akasema: Mimi ninataka kukuoza mmoja wa mabinti zangu hawa wawili kwa kunifanyia ajira ya miaka minane na kama ukitimiza kumi hiyari yako. Mimi sitaki kukutaabisha. Inshaallah utanikuta miongoni mwa watu wema.

Musa mkimbizi, fukara asiyekuwa na chochote, ambaye kwa siku kadhaa, ameishi kwa kula mimea ya ardhi; mpaka akamuomba Mola wake tonge ya kumwezesha kuishi, leo anahiyarishwa kuchagua mke amtakaye. Bila shaka hapa kuna siri ya utu wa Musa na utukufu wake uliomgusa mzee na mabinti zake. Vile vile katika masimulizi yake na sera yake kwa Firauni na watu wake.

Mzee alitambua, kutokana na akili yake safi, kwamba mtu huyu atakuwa na athari ya mbali. Kwa sababu matendo ya mtu aghlabu yanatoka kwenye chimbuko moja. Kwa hiyo mzee, hapa alifuzu kutokana na ukwe huu. Kuna faida gani kubwa zaidi ya kuwa mkwe wa Mtume na mwenye takua.

SHARIA YA KIISLAMU IMEFUTA SHARIA ZOTE

Mafaqihi wamezungumza mengi kuhusiana na Aya hii, wakaitolea dalili kuwa walii wa mwanamke ndiye atakayetamka tamko la ndoa. Lakini ilivyo ni kuwa inafaa kwa mwanamume au mwanamke mwenyewe kutam- ka. Hilo linafahamika kimsingi bila ya kuhitaji nukuu. Shafii na Imamiya wamesema kuwa ndoa haifungiki isipokuwa kwa tamko la ziwaj na nikah. Hii ni baada ya kuiunganisha Aya hii, yenye tamko la nikah, na ile yenye tamko la ziwaj.

فَلَمَّا قَضَىٰ زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَاكَهَا ﴿٣٧﴾

“Basi Zaid alipokwisha haja naye tulikuoza wewe” (33:37).

Malik na Hambal wakasema pia ndoa inafungika kwa neno hiba, kutokana na Aya yenye neno hiba:

وَامْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِيِّ ﴿٥٠﴾

“Na mwanamke mumin akijitoa mwenyewe kwa Nabii.” (33:50).

Hanafi naye akasema kuwa ndoa inafungika kwa neno lolote linalofahamisha kutaka kuoana.

Mafaqihi wengi wamesema kuwa muda wa kuchunga wanyama miaka minane au kumi haukuwa mahari au sehemu yake. Bali mahari yalikuwa mbali; na kwamba kauli ya mzee: “kunifanyia ajira” maana yake ni kuwa ukichunga wanyama kwangu kwa ajira, nitakuoza mmoja wa mabinti zangu kwa mahari; sawa na kusema: ‘Ukifanya hivi nami nitafanya hivyo.’

Haya ndio maana sahihi ya Aya. Kwa vyovyote iwavyo, hakuna hoja yoyote, katika Aya hii kwa, waliyoyasema mafaqihi. Kwa sababu hizo ni simulizi za sharia zilizotangulia. Nasi tuna uhakika kwamba sharia ya Kiisalmu imefuta sharia zote zilizotangulia, wala haifai kutumia hukumu yoyote miongoni mwa hukumu hizo zilizotangulia, isipokuwa kwa dalili maalum au ya kiujmla kutoka katika Kitab au Sunna. Na hapo itakuwa ni kukitumia Kitab au Sunna, sio kuitumia sharia hiyo.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ ﴿٣٨﴾

“Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote.” Juz. 7 (6:38).

Na kauli yake:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ ﴿٨٩﴾

Na tumekuteremshia Kitabu hiki kubainisha kila kitu.” Juz.14: (16:89),

Yaani kila kitu katika misingi ya kiislamu na sharia yake.

Mtume(s.a.w.w) naye anasema: “Hakuna kitu kitakachowakurubisha nyinyi Peponi isipokuwa nimewaamrisha, na hakuna kitu kitakachowaweka mbali na moto isipokuwa nimewakataza.”

Akasema: Hayo yamekwishakuwa baina yangu na yako. Muda wowote kati ya miwili nitakoumaliza nisifanyiwe ubaya na Mwenyezi Mungu ni wakili juu ya haya tunayoyasema.

Haya ni maneno ya Musa. Muda wa kwanza ni Hijja nane na wa pili ni Hijja kumi. Maana ni kuwa Musa alimwambia mzee, nimekubali na kuridhia kuoa na kuchunga wanyama.

Mimi nitakuwa na hiyari ya kumaliza nane au kumi. Muda wowote nitakaoumaliza basi usiwe na hoja kwangu na Mwenyezi Mungu ndiye shahidi juu ya haya uliyojiwajibishia na niliyojiwajibishia.

Kuna Hadith isemayo kuwa Musa alichagua muda wa kumi. Wafasiri wengi wanasema kuwa yeye alimchagua mdogo naye ndiye aliyesema, baba yangu anakuita. Na pia kumwambia baba yake, hakika yeye ana nguvu na ni mwaminifu.