TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA Juzuu 21

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 25571
Pakua: 3256


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 32 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 25571 / Pakua: 3256
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA Juzuu 21

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾

41. Enyi ambao mmeamini! Mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi.

وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٤٢﴾

42. Na mumtakase asubuhi na jioni.

هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا ﴿٤٣﴾

43. Yeye ndiye anayewaswalia na malaika wake, ili awatoe vizani na kuwatia kwenye nuru. Naye ni mwenye kuwarehemu waumini.

تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا ﴿٤٤﴾

44. Maamkuzi yao siku ya kukutana naye yatakuwa ni Salaam na amewaandalia malipo yenye heshima.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿٤٥﴾

45. Ewe Nabii! Hakika sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na muonyaji.

وَدَاعِيًا إِلَى اللَّـهِ بِإِذْنِهِ وَسِرَاجًا مُّنِيرًا ﴿٤٦﴾

46. Na mlinganiaji kwa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa iangazayo.

وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ بِأَنَّ لَهُم مِّنَ اللَّـهِ فَضْلًا كَبِيرًا ﴿٤٧﴾

47. Wape bishara waumini ya kwamba wanafadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

وَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَالْمُنَافِقِينَ وَدَعْ أَذَاهُمْ وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا ﴿٤٨﴾

48. Wala usiwatii makafiri na wanafiki na acha udhia wao na mtegemee Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا ﴿٤٩﴾

49. Enyi ambao mmeamini! Mkiwaoa wanawake waumini kisha mkawaacha kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayoihisabu. Hivyo wapeni cha kuwaliwaza na waacheni muachano mzuri.

NDIYE ANAYEWAREHEMU

Aya 41 – 49

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi na mumtakase asubuhi na jioni.

Hii ni amri ya kudumu kwenye Swala tano na kumkumbuka, Mwenyezi Mungu wakati wote, kwa kumbukumbu nzuri.

Yeye ndiye anayewaswalia na malaika wake.

Kuswalia kukitoka kwa Mwenyezi Mungu, maana yake ni maghufira na rehema na kukitoka kwa mwenginewe ni kuombea maghufira na rehema. Kwa hiyo inampasa kila mtu kumswalia na kumwombea amani kila mwenye kuamini na katenda mema.

Ni vizuri kudokeza kwamba Sunni, aghlabu wakimtaja sahaba mtukufu au imam mkuu husema: Radhiallah anh (Mwenyezi Mungu awe radhi naye). Shia wao husema: Alayhissalam (amani ishuke juu yake). Chimbuko la kauli zote mbili ni moja – Qur’an. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Awe radhi nao Mwenyezi Mungu na wao wawe radhi naye.” Juz. 7 (5:119) na akasema:“Amani kwa Ilyasin” (37:130) na amesema kwenye Aya hii tuliyo nayo: “Yeye ndiye anayewaswalia na malaika wake.”

Katika Tafsir Ruhul-bayan imeelezwa: “Bani Israil walimuuliza Musa: “Mola wetu naye anaswali? Basi hili likawa zito kwa Musa.” Hilo si ajabu kwa Waisrail.

Ili awatoe vizani na kuwatia kwenye nuru.

Makusudio ya viza hapa ni viza vya moto; na nuru ni nuru ya neema; yaani Mwenyezi Mungu na malaika wake wanawaswalia waumini ili wawe mbali na adhabu ya moto na waingie kwenye raha. Imesekana kuwa makusudio ya viza ni ukafiri na nuru ni nuru ya imani, lakini hii haiafikiani na kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia:

Naye ni mwenye kuwarehemu waumini.

Vile vile haiafikiani na kuwa Mwenyezi Mungu na malaika wake hawarehemu makafiri ili awatoe kwenye imani.

Maamkuzi yao siku ya kukutana naye yatakuwa ni Salaam na amewaandalia malipo yenye heshima.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:10) Juz. 13 (14:23).

Ewe Nabii! Hakika sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na muonyaji na mlinganiaji kwa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake.

Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad(s.a.w. w ) kulingania haki na akamsheheneza hoja za kutosha, kumpa habari njema ya pepo yule mtiifu na kumwonya na adhabu chungu yule mwenye kuasi. Kesho atakuwa shahidi wa huyu kwamba alipinga na akatupilia mbali na atakuwa shahidi wa yule kwamba alisikia na akatii.

Kwenye Nahjul-balagha kuna maelezo haya: “Alimtuma kuwa ni mlingania kwenye haki na shahidi kwa viumbe. Akafikisha ujumbe wa Mola wake bila ya kubweteka wala kuzembea, na akapigana jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na maadui zake bila ya kudhoofika wala kutafuta visababu. Ni imamu wa mwenye takua na busara ya mwenye kutaka kuongoka.

Na taa iangazayo inayowaongoza wanaohangaika kwenye ufukwe wa salama.

Wape bishara waumini ya kwamba wanafadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Umepita mfano wake katika Juz.11 (9-112)

Wala usiwatii makafiri na wanafiki.

Imetangulia neno kwa neno katika Juzuu iliyopita mwanzo wa sura hii tuliyo nayo.

Na acha udhia wao.

Mtume hakuwaudhi, ispokuwa washirikina ndio waliomuudhi, kiasi cha kufikia kusema: “Hakuudhiwa Nabii mfano wa nilivyoudhiwa mimi.” Kwa hiyo maana ni, achana nao, usikushughulishe ujinga na upumbavu wao.

Na mtegemee Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi.

Kwenye Nahjul-balagha imesemwa: “ Mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu anamtoshea na mwenye kumwomba atampa na mwenye kumkopesha atamlipa, na mwenye kumshukuru atampa jaza yake.

Enyi ambao mmeamini! Mkiwaoa wanawake waumini kisha mkawaacha kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakyoihisabu. Hivyo wapeni cha kuwaliwaza na waacheni muachano mzuri.

Kabla ya kuwagusa ni kabla ya kuwaingilia. Cha kuwaliwaza kisharia ni kitu anachokitoa mtaliki akiwa hajamwingilia na hakutaja mahari yake. Ikiwa ametaja itakuwa ni wajibu kutoa nusu ya mahari. Tazama Juz. 2 (2:236 – 237).

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَحْلَلْنَا لَكَ أَزْوَاجَكَ اللَّاتِي آتَيْتَ أُجُورَهُنَّ وَمَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ مِمَّا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَيْكَ وَبَنَاتِ عَمِّكَ وَبَنَاتِ عَمَّاتِكَ وَبَنَاتِ خَالِكَ وَبَنَاتِ خَالَاتِكَ اللَّاتِي هَاجَرْنَ مَعَكَ وَامْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِيِّ إِنْ أَرَادَ النَّبِيُّ أَن يَسْتَنكِحَهَا خَالِصَةً لَّكَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ قَدْ عَلِمْنَا مَا فَرَضْنَا عَلَيْهِمْ فِي أَزْوَاجِهِمْ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ لِكَيْلَا يَكُونَ عَلَيْكَ حَرَجٌ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٠﴾

50. Ewe Nabii! Hakika sisi tumekuhalalishia wake zako ambao umewapa ujira wao, na uliowamiliki kwa mkono wako wa kuume katika aliokupa Mwenyezi Mungu, na mabinti wa ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako na mabinti wa khalat zako waliohama pamoja nawe, na mwanamke mumin akijitoa mwenyewe kwa Nabii ikiwa Nabii anataka kumuoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa waumini wengine. Tunajua tuliyowafaradhishia wao kuhusu wake zao na wale waliomilikiwa na mikono yao ya kuume. Ili isiwe dhiki juu yako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

تُرْجِي مَن تَشَاءُ مِنْهُنَّ وَتُؤْوِي إِلَيْكَ مَن تَشَاءُ وَمَنِ ابْتَغَيْتَ مِمَّنْ عَزَلْتَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكَ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن تَقَرَّ أَعْيُنُهُنَّ وَلَا يَحْزَنَّ وَيَرْضَيْنَ بِمَا آتَيْتَهُنَّ كُلُّهُنَّ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا فِي قُلُوبِكُمْ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَلِيمًا ﴿٥١﴾

51. Unamwakhirisha umtakaye katika wao na na unamsogeza kwako umtakaye. Na unayemtaka katika uliyemtenga si vibaya kwako. Hivyo itakuwa ni karibu zaidi kuburudika macho yao wala wasihuzunike na wawe radhi juu ya kile unachowapa wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.

لَّا يَحِلُّ لَكَ النِّسَاءُ مِن بَعْدُ وَلَا أَن تَبَدَّلَ بِهِنَّ مِنْ أَزْوَاجٍ وَلَوْ أَعْجَبَكَ حُسْنُهُنَّ إِلَّا مَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ رَّقِيبًا ﴿٥٢﴾

52. Hawakuhalalikii wanawake baadaye wala kuwabadilisha kwa wake wengine, ijapo uzuri wao utakupendeza; isipokuwa uliyemmiliki kwa mkono wako wa kuume. Na Mwenyezi Mungu ni Mchungaji wa kila kitu.

TUMEKUHALALISHIA WAKE ZAKO

Aya 50 – 52

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya hii ametaja aina ya wanawake walio halali kwa Mtume(s.a.w. w ) na kumwachia hiyari ya kumlalia na kutomlalia anayemtaka. Kisha akamharamishia kuzidisha wale aliokuwa nao au kubadilisha mwingine. Wakati huo alikuwa na wake tisa. Ufuatao ni ufafanuzi:

Ewe Nabii! Hakika sisi tumekuhalalishia wake zako ambao umewapa ujira wao.

Makusudio ya ujira hapa ni mahari. Na kuwapa hayo mahari kunakuwa ni lazima. Aya inaashiria kuwa Mtume anaweza kuoa idadi yoyote anayoitaka. Haya ni katika mambo yanayomuhusu yeye tu.

Unaweza kuuliza : kufunga ndoa kunaswihi hata kama mahari hayakuta- jwa, kwa nini basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameufunga uhalali kwa mahari?

Jibu : Ulazima hapa ni wa kuyatoa hayo mahari sio kuyataja kwenye ndoa. Ikiwa mahari hayakutajwa kwenye ndoa, basi ni lazima kutoa mahari kifani; yaani yanayofana na mwingine wa aina yake. Mahari ya mtume, wakati huo, yalikuwa ni Dirhamu 500. wamekadiria Dirhamu moja kuwa ni sawa na Lira 25 za dhahabu.

Na uliowamiliki kwa mkono wako wa kuume katika aliokupa Mwenyezi Mungu katika mateka waliowatekwa nyara na waislamu kati- ka vita na washirikina, ambao wanaitwa masuria. Mwenyezi Mungu amemuhalishia Mtume wake na umma wake, wanawake hawa.

Na mabinti wa ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako na mabinti wa khalat zako waliohama pamoja nawe.

Unaweza kuuliza : Mabinti wa ami, wa shangazi, wajomba na wa khalat (dada wa mama) si wanaingia katika aina ya kwanza ya wanawake, sasa kuna haja gani ya kuhusishwa kutajwa?

Jibu : Inawezekana kuwa makusudio ya kutajwa ni kuwa inavyopendeza ni kuwa hadhi ya Mtume ni kuoa makuraishi aliohama nao kutoka mji wa ukafiri hadi mji wa Uislamu. Ama waumimi wengine ni bora kutowaoa.

Swali la pili : Watu wa sira wamesema kuwa Mtume alikuwa na ami tisa: Abbas, Hamza, Abu Twalib, Zabeir, Harith, Hijla, Muqawwam, Dhirar na Abu Lahab. Na shangazi sita: Swafiya, Ummu Hakim al-baydhau, Atika, Umayma, Arwa na Barra (Assiratu nnabaawiya cha Ibn Hisham).

Na wakasema: “Mtume hakuwa na wajomba wala khalat (mama wadogo au wakubwa), kwa sababu mama yake Amina bint Wahb(a.s) hakuwa na kaka wala dada.” (Tafsir Ruuhul-bayan).

Sasa kuna wajihi gani wa Mwenyezi Mungu kusema: ‘Na mabinti wa ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako na mabinti wa khalat zako?’

Jibu : Makusudio ya wajomba na khalat wa Mtume ni ukoo wa mama yake unaoitwa Bani Zuhra, ambao walikuwa wakisema: “Sisi ni wajomba zake Mtume.”

Na mwanamke mumin akijitoa mwenyewe kwa Nabii ikiwa Nabii anataka kumuoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa waumini wengine.

Katika mambo yanayomuhusu Mtume tu ni kumuoa mwanamke, akitaka, ikiwa atajitoa mwenye kwa Mtume bila ya mahari, kwa masharti ya kuwa mumini. Ndio! Inajuzu kwa mwinginewe kuoa kwa mahari, kisha mke asamehe mahari, kama anavyosamehe mtu yoyote mali yake kwa mwingine.

Tunajua tuliyowafaradhishia wao kuhusu wake zao na wale waliomi- likiwa na mikono yao ya kuume. Ili isiwe dhiki juu yako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu, ameweka idadi ya wake waungwana na akaharamisha mwanamke kujitoa mwenyewe bila mahari. Lakini akaliruhusu hilo kwa Mtume ili isiwe dhiki juu yake.

Vile vile kufahamisha utukufu wa cheo chake na juhudi zake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye anayejua zaidi li lilo na masilahi zaidi kwa watu, akiwa anawahurumia na kuwaghufuria.

Unamwakhirisha umtakaye katika wao na na unamsogeza kwako umtakaye.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amempa uhuru Mtume wake mtukufu katika idadi ya wanawake na katika Aya hii amempa hiyari ya kuongeza au kupunguza zamu ya yeyote anayemtaka.

Na unayemtaka katika uliyemtenga si vibaya kwako.

Yaani anaweza kumrudia aliyemaliza zamu naye na kumwacha aliyekuwa kwenye zamu yake. Kwa ibara ya wanaoimudu lugha ni, anaweza kumtanguliza wa mwisho na kumweka mwisho wa kwanza.

Hivyo itakuwa ni karibu zaidi kuburudika macho yao wala wasihuzunike na wawe radhi juu ya kile unachowapa wao wote.

‘Hivyo’ ni huko kuachiwa hiyari Mtume(s.a.w.w) . Maana ni kuwa wao wakijua kuwa hiyari ni yako sio yao ya zamu sawa, basi kila mmoja ataridhia na vile utakavyokuwa kwake kwa siku kidogo au nyingi kwa kujua kuwa ziada hiyo imetokana na wewe wala si wajibu kwako. Pamoja na hayo, lakini Mtume alikuwa akikaa siku sawa baina ya wake zake.

Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu ya kupondokea zaidi kwa baadhi ya wake zenu kuliko wengine. Mwenyezi Mungu hayachukulii mapenzi yaliyo moyoni au chuki; isipokuwa anachukulia matendo. Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.

Hawakuhalalikii wanawake baadaye wala kuwabadilisha kwa wake wengine, ijapo uzuri wao utakupendeza.

Wafasiri wametaja maana tatu za Aya hii; iliyo karibu zaidi na maana ya dhahiri ni ile isemayo kuwa Mwenyezi Mungu baada ya kumhalalishia Mtume wanawake aliowaishiria katika Aya iliyotangulia, amewajibisha katika Aya hii kutosheka na alio nao ambao walikuwa tisa na akaharamishiwa kumwacha yeyote katika wao na kuweka mwingine mahali pake, hata kama atakuwa amempendeza.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Ijapo uzuri wao utakupendeza’ inafahamisha kuwa mwanamume anaruhusiwa kumwangalia mwanamke anayetaka kumuoa.

Na ndio mafakihi wakalitolea fatwa hilio kwa kutegemea Aya hii na Hadith za Mtume mtukufu(s.a.w. w ) .

Isipokuwa uliyemmiliki kwa mkono wako wa kuume, aliokupa Mwenyezi Mungu katika mateka.

Na Mwenyezi Mungu ni Mchungaji wa kila kitu, hata kilicho siri na kwenye dhamiri:

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ﴿٤﴾

“Naye yu pamoja nanyi popote mlipo.” (57:4).

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَـٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ وَاللَّـهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّـهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمًا ﴿٥٣﴾

53. Enyi ambao mmeamini! Msiingie majumba ya Mtume ila mkipewa ruhusa ya kwenda kula, sio kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni. Na mkisha kula, tawanyikeni wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii, naye anawastahi nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa haki. Na mnapowaomba chombo cha nyumbani, basi waulize nyuma ya mapazia. Hilo linasafisha zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao. Haiwafalii nyinyi kumuudhi Nabii wala kuwaoa wake zake kabisa. Hakika hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

إِن تُبْدُوا شَيْئًا أَوْ تُخْفُوهُ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٥٤﴾

54. Mkidhihirisha chochote au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

لَّا جُنَاحَ عَلَيْهِنَّ فِي آبَائِهِنَّ وَلَا أَبْنَائِهِنَّ وَلَا إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ أَخَوَاتِهِنَّ وَلَا نِسَائِهِنَّ وَلَا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ وَاتَّقِينَ اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا ﴿٥٥﴾

55. Hapana ubaya kwao kwa baba zao, wala watoto wao, wala kaka zao, wala watoto wa kaka zao, wala watoto wa dada zao, wala wanawake wao, wala wale waliomilikiwa na mikono yao ya kuume. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu.

MKISHAKULA TAWANYIKENI

Aya 53 – 55

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Msiingie majumba ya Mtume ila mkipewa ruhusa ya kwenda kula, sio kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni. Na mkisha kula, tawanyikeni wala msiweke mazungumzo.

Yaani msikae kabisa si kwa mazungumzo wala kwa jambo jingine. Yametajwa mazungumzo kwa vile mara nyingi mtu anakaa kwa kupiga gumzo.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa baadhi ya maswahaba walikuwa wakiingia nyumba ya Mtume(s.a.w. w ) bila ya idhini kama ilivyo ada ya kijahiliya; na kwamba wakiona chakula kinapikwa basi wanakingoja na baada ya kula walikuwa wakipiga gumzo.

Hakuna mwenye shaka kwamba aina hii ya upuzi na kukosa adabu inamuudhi binadamu yeyote, awe Mtume au si Mtume. Ni kwa ajili hii Mtume(s.a.w. w ) aliwafundisha adabu mswahaba na wengineo kuwa wasiingie nyumba yoyote bila ya idhini ya wenyewe - hayo yamedokezwa kwenye Juz. 18 (24:28) – na kwamba wasiende kula ila wakiitwa, tena chakula kiwe kimeandaliwa na wakishamaliza kula wasingoje tena.

Haya hayahusiki na nyumba ya Mtume peke yake; isipokuwa Mwenyezi Mungu amemtaja yeye kwa vile ndio sababu ya kushuka Aya. Mara nyingi tumesema kuwa sababu ya kushuka Aya haiifungi na hilo lililoishukia.

Hakika hayo yanamuudhi Nabii, naye anawastahi nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa haki.

Makusudio ya haki aliyokuwa akiistahi Mtume ni haki yake ya kiutu – kuwatoa wapuuzi nyumbani kwake. Mtume aliwanyamazia kwa kuwaonea haya; ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akatanabahisha kwamba kubaki kwao baada ya chakula kunamuudhi Mtume, vile vile kuingia kwao nyumbani kwake bila ya idhini yake.

Kuna Hadith isemayo: “Haya ni tawi la imani na asiyekuwa na haya hana dini.” Kuna Hadith nyingine isemayo:“Hakukubakia katika mifano ya mitume isipokuwa kauli ya watu: Kama huna haya basi fanya utakavyo.”

Katika maelezo ya wasifu wa Mtume(s.a.w. w ) ni kuwa yeye alikuwa na haya kuliko mwanamwali kwenye ushungi wake. Katika Nahjul-balagha imesemwa:“Hakuna imani kama haya na subira.” Farazdaq katika kumsifu Imam Zaynul-abdin anasema:

Hufumba macho kwa haya kwa haiba yake. Hazungumzi ila kuonekana tabasamu yake Maajabu ni yale yaliyoandikwa kwenye kitabu Muhadharatul-udabai cha Asfahaniy:

“Doezi mmoja alilaumiwa kwa kudoea kwake, akasema akijitetea: “Ala! Ikiwa bani Israil walimdoea Mungu, je sisi tusidoee watu?”

Na mnapowaomba chombo cha nyumbani, basi waulize ni nyuma ya mapazia. Hilo linasafisha zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao.

Yaani mnapowaomba haja wakeze Mtume. Kutaja chombo cha chumbani ni kutolea mfano tu, sio kuhusisha na kuondoa hukumu kwa vingine. Hilo linafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Hilo linasafisha zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao.” Inayotambulisha kuwa kuchanganyika na kuondoa pazia baina ya wanawake na wanaume kunaleta ufisadi na fitna.

Maana yake ni kuwa kuchanganyika ni haramu, au angalau ni bora kuacha. Hapa inatubainikia kuwa kuchanganyika ni sababu ya kuleta matamanio ya kijinsiya, na wala sio kumtia adabu mwanamke na kumkandamiza; kama wanavyodai wale wasemao: “Mungu amesema hivyo na mimi nasema hivi” Ni nani aliye mkweli zaidi kwa mazungumzo kuliko Mwenyezi Mungu?

Haiwafalii nyinyi kumuudhi Nabii wala kuwaoa wake zake kabisa. Hakika hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hukumu hii inamuhusu Mtume tu peke yake. Kwa sababu wakeze wako katika daraja ya mama wa waumini. Imeelezwa katika Tafsir Arrazi na Ruhul-bayan ya Ismail Haqiy: “Hakika Aya hii ilishuka pale aliposema Twalha bin Abdallah Attaymiy:“Akifa Muhammad(s.a.w. w ) nitamuoa Aisha.”

Hilo linataliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Mkidhihirisha chochote au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Hilo ni karipio kwa yule aliyedhamiria kuoa wake za Mtume baada yake.

Hapana ubaya kwao kwa baba zao, wala watoto wao, wala kaka zao, wala watoto wa kaka zao, wala watoto wa dada zao, wala wanawake wao, wala wale waliomilikiwa na mikono yao ya kuume. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuamrisha kuzungumza na wanawake nyuma ya pazia (hijabu) hapa anavua wale ambao hawawezi kuoana nao, ambao ni: baba, mtoto, kaka, mtoto wa kaka na mtoto wa dada, mtumwa na wanawake. Lakini Mwenyezi Mungu amesema wanawake wao, yaani wanawake wenzao walio waumini, kwa sababu wasiokuwa waumini watawasifia wanaume zao.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 18 (24:31).

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

56. Hakika Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi ambao mmeami- ni! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu.

إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا مُّهِينًا ﴿٥٧﴾

57. Hakika wale ambao wanamuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha.

وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴿٥٨﴾

58. Na wale ambao wanawaudhi waumini wanaume na waumini wanawake pasi na wao kufanya, hakika wamebeba dhulma kubwa na dhambi kubwa.

MSWALIENI MTUME

Aya 56 – 58

MAANA

Hakika Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi ambao mmeamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu.

Makusudio ya Mwenyezi Mungu kumsalia Mtume ni kumridhia kumrehe- mu na kumsifu kwa kila kheri, swala ya malaika ni kumsifu, na kutoka kwa waumini ni kumwombea dua ya kuwa na daraja ya juu. Imam Ar-Ridha(a.s) aliulizwa kuhusu maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu: malaika na waumini humswalia Mtume, akasema:“Swala kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni rehema, kutoka kwa malaika ni kumsifu na kutoka kwa waumni ni kumwombea.”

Kuswaliwa huku hakuhusiki na risala ya Muhammad(s.a.w. w ) peke yake. Kila mtu anayetumia desturi ya risala ya Muhammad(s.a.w. w ) , kuifundisha au kuijulisha au kutaja fadhila yoyote katika fadhila zake basi atakuwa amemswalia, awe mumin au sio mumin, akitaka hilo au asitake.

Imam Ja’far As-Sadiq(a.s) anasema: “Mtu kumswalia Muhammad(s.a.w. w ) ni kama kusema:“Subhanallah walhamdulillah walailaha illaha wallahu akbar” (Kutakasika ni kwa Mwenyezi Mungu na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu na hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mkubwa).

Imam hapa anakusudia kuwa thawabu za kumswalia Mtume ni sawa na thawabu za tasbih, tahmid, tahlil na takbir. Imepokewa Hadith kutoka kwa Mtume mtukufu(s.a.w. w ) , amesema:“Bakhili wa kweli ni yule ambaye nikitajwa mbele yake haniswalii” .

VIPI TUTAMSWALIA MTUME?

Katika Sahih Al-Bukhariy Juz. 8, mlango wa kumswalia mtume, Tafsir At- Tabariy, Tafsir Ar-Raziy, Tafsir Al-Maraghi na wafasiri wengineo, pia katika vitabu vya Hadith, kuna maelezo haya: “Mtume aliulizwa: Vipi tutakuswalia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?Akasema: semeni:

Allahumma swalli a’la muhammdi wa a’la aali Muhammad, kama swal-layta a’la Ibrahima wa a’laa aali Ibrahim, Innaka hamidum majiid Allahumma barik ala muhammdi wa a’la ali Muhammad, kama barakta a’la Ibrahima wa a’la ali Ibrahim, Innaka hamidum majid.

(Ewe Mwenyezi Mungu mswalie Muhammad na kizazi cha Muhammad, kama ulivyomswalia Ibrahim na kizazi cha Ibrahim, hakika wewe ni mwenye kusifiwa mwenye kutukuzwa. Ewe Mwenyezi Mungu mbariki Muhammad na kizazi cha Muhammad, kama ulivyombariki Ibrahim na kizazi cha Ibrahim. Hakika wewe ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa. )

Katika tafsir Ruhul-bayan ya Ismail Haqiy, amesema: “Inatakikana mwenye kuswali aseme: Allhumma swali a’la Muhammad wa a’la AliMuhammad” kwa kulirudia neno ‘a’la’; kwani Sunni wanaweka neno hilo kabla ya aali, kuwapinga Shia ambao hawaliweki neno hilo.

Sisi hatuoni tofauti yoyote baina ya anayesema: neno hilo na asiyelisema. Ama kuhusu ile Hadith isemayo:“Mwenye kutenganisha baina yangu na kizazi changu, hatapata shafaa yangu,” Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi usahihi wake.

Imam Shafii naye amesema katika shairi lenye maana hii: Enyi watu wa nyumba ya Mtume pendo lenu ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu amelieleza katika Qur’an. Inawatosha kuwa ni cheo kikuu kwamba nyinyi asiyewaswalia hana Swala

Hakika wale ambao wanamuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha.

Makusudio ya kumuudhi Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kumghadhabisha, na sababu yenye kuwajibisha hilo ni kumpinga, kumnasibishia mshirika au mtoto, au kuasi hukumu miongoni mwa hukumu zake. Na kuumuudhi Mtume(s.a.w. w ) ni kupinga utume wake au kupuuza mwenendo wake.

Laana kutoka kwa Mungu ni kwa kuwekwa mbali na rehema yake na kutoka kwa watu ni shutuma na kuombewa mabaya. Katika Nahjul-balagha imeelezwa:“Mwenyezi Mungu amewalaani wanaoamrisha mema na kuacha kuyatenda na wanaokataza maovu na wanayoyatenda.”

Na wale ambao wanawaudhi waumini wanaume na waumini wanawake pasi na wao kufanya, hakika wamebeba dhulma kubwa na dhambi kubwa.

Pasi na wao kufanya, yaani kufanya kosa linalostahili udhia. Kuudhi kunakuwa ni kwa kusengenya, vitimbi, uzushi n.k. Kuna Hadith zisemazo:

“Mwislamu ni yule ambaye watu wamesalimika na mkono wake na ulimi wake.”

“Utukufu wa mumin ni kwa kujizuia na kuwaudhi watu.”

“Aliye dhalili zaidi katika watu ni yule anayewadharau watu.”

Imam Ali(a.s) anasema: Mwenye hali mbaya zaidi katika watu ni yule asiyemwaamini yeyote kwa dhana zake mbaya, na asiyeaminiwa na yeyote kwa vitendo vyake vibaya.”

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MOJA

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

59. Ewe Nabii! Waambie wake zako na wake za waumini, wajiteremshie jalbab zao. Hilo ni karibu zaidi kuweza kujulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

لَّئِن لَّمْ يَنتَهِ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْمُرْجِفُونَ فِي الْمَدِينَةِ لَنُغْرِيَنَّكَ بِهِمْ ثُمَّ لَا يُجَاوِرُونَكَ فِيهَا إِلَّا قَلِيلًا ﴿٦٠﴾

60. Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na wale wanaoeneza fitna Madina, hawataacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.

مَّلْعُونِينَ أَيْنَمَا ثُقِفُوا أُخِذُوا وَقُتِّلُوا تَقْتِيلًا ﴿٦١﴾

61. Wamelaaniwa! Popote waonekanapo, na wakamatwe na wauliwe kabisa.

سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٦٢﴾

62. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

WAJIBU WA HIJABU

Aya 59 – 62

LUGHA

Kuna kauli nyingi kuhusu neno Jalbab: kuna wanaosema kuwa ni nguo inayomfunika mwanamke kutoka kichwani hadi nyayoni. Wengine wakasema ni ushungi unaofunika kichwa cha mwanamke na uso wake. Kauli hii ndio aliyo nayo mwenye Majmaul-Bayan.

MAANA

Zimekwishatangulia Aya mbili zinazofahamisha wajibu wa hijabu kwa wanawake:

Ya kwanza ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Wala wasidhihirishe uzuri wao ila kwa waume zao.” Juz. 18 (24: 31). Ya pili ni ile Aya ya 53, katika Sura hii tuliyo nayo: “Na mnapowaomba chombo cha nyum- bani, basi waulizeni nyuma ya mapazia.”

Aya iliyo wazi zaidi ya hizi mbili ni hii tuliyo nayo, isemayo:

Ewe Nabii! Waambie wake zako na wake za waumini, wajiteremshie nguo zao.

Kusema kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘wajiteremshie nguo zao’ inaenea kusitiri na kufunika sehemu zote za mwili, kikiwemo kichwa na uso. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Hilo ni karibu zaidi kuweza kujulikana wasiudhiwe.

Waislamu, mwanzoni walikuwa wakitoka bila ya kujitanda, kama ilivyokuwa desturi ya kijahiliya, ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamtaka Mtume wake mtukufu, katika Aya hii, awaamrishe wake zake kujisitiri na kuvaa hijabu. Na amri inafahamisha wajibu. Kwa hiyo hijabu ni wajibu.

Hata hivyo uso na viganja viwili havimo kwenye wajibu huu, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ﴿٣١﴾

“Wala wasionyeshe uzuri wao, isipokuwa unaodhihirika.” Juz. 18 (24:31).

Hilo ni karibu zaidi kuweza kujulikana kutokana na kujistahi na kujichunga. Kwani hijabu ni kinga baina ya mwanamke na tamaa ya watu wenye shakashaka na mafasiki,wasiudhiwe kwa kuangaliwa na mafasiki.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Anasamehe yaliyopita na anamuhurumia mwenye kutubia na kurejea nyuma.

Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na wale wanaoeneza fitna Madina, hawataacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.

Wanafiki walificha ukafiri na wakadhihirisha imani. Wanaoeneza fitna ni watu katika wananfiki waliokuwa wakieneza propaganda dhidi ya Mtume(s.a.w. w ) na maswahaba na wakawatia shaka wale wadhaifu wa imani ambao Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaletea ibara ya wenye mardhi nyoyoni mwao. Aya inatoa onyo la kuuawa na kufukuzwa wanafiki, waeneza fitna na wale watakaowasikiliza, ikiwa hawatajizuia na upotevu na ufisadi wao.

VITA VYA NAFSI

Siku hizi kueneza fitna kunaitwa ‘vita vya nafsi.’ Nguvu ya shari imetafuta njia nyingi sana za kueneza uongo na mambo ya ubatilifu kwa kila nyenzo. Kuanzia magazeti, radio, runinga, sinema, hotuba, vipeperushi, shule, vyuo, vitabu n.k.

Vyombo hivi vimekaririka masikioni mwa watu kila siku, kiasi ambacho uhakika haupati nafasi kwa watu na wenye ikhlasi, isipokuwa kwa mwamko mkamilifu na elimu itakayotangulia propaganda za wakoloni na wazayuni.

Nimesoma kwenye gazeti linaloitwa Akhabar Al-yawm la Misr, la 13/12/69, kwamba Israil ina magazeti ya propaganda yanayofikia 890 ulimwenguni kwa ajili ya kueneza habari za uongo. Zaidi ya hayo wametawala vyombo vingi vya habari ulimwenguni, kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja; kama vile runinga, radio n.k.

Kwenye mahisabu haya hayaingii magazeti ya Beiruti yenye uhusiano mkubwa na wakoloni na wazayuni.

Kwa vyovyote iwavyo, Alhamdu lillah, Israil imehisi mapigo kutoka kwa waarabu na kwamba propaganda zao zilizotengenezwa na Marekani, na kutangazwa na vibaraka, zimeanza kujulikana.

Wamelaaniwa! Popote waonekanapo na wakamatwe na wauliwe kabisa.

Wamelaaaniwa na kila ulimi, kwa sababu dini yao ni pesa na matendo yao ni udanganyifu, uwongo na hadaa. Hawana dawa isipokuwa kuuawa popote walipo; kama kiungo kilichoharibika, kisipokatwa kitaharibu mwili wote.

Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya desturi ya Mwenyezi Mungu hapa ni hukumu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa mpotevu anayepoteza, ambayo ni kuuliwa ambako amekuwekea sharia, ambaye imetukuka hekima yake, tangu zamani. Hukumu hii itabakia milele bila ya mabadiliko wala mageuzi.

يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا ﴿٦٣﴾

63. Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Na nini kitakachokujulisha? Pengine hiyo saa iko karibu.

إِنَّ اللَّـهَ لَعَنَ الْكَافِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمْ سَعِيرًا ﴿٦٤﴾

64. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri moto unaowaka.

خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا لَّا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴿٦٥﴾

65. Watadumu humo milele. Hawatapata mlinzi wala wa kuwanusuru.

يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا ﴿٦٦﴾

66. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Mwenyezi Mungu na tungelimtii Mtume!

وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾

67. Na watasema: Mola wetu! Hakika sisi tuliwatii mabwana zetu na wakubwa wetu, wakatupoteza njia.

رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا ﴿٦٨﴾

68. Mola wetu wape adhabu mara mbili, na walaani laana kubwa.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا ﴿٦٩﴾

69. Enyi ambao mmeamini! Msiwe kama wale ambao walimuudhi Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtaksa na waliyoyasema; naye alikuwa ni mwenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.

WANAKUULIZA KUHUSU SAA

Aya 63 – 69

MAANA

Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Na nini kitakachokujulisha? Pengine hiyo saa iko karibu.

Makusudio ya saa ni Kiyama Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:187).

Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri moto unaowaka. Watadumu humo milele. Hawatapata mlinzi wala wa kuwanusuru. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Mwenyezi Mungu na tungelimtii Mtume!

Makafiri na waasi kesho watasukumwa kwenye adhabu ya moto, hawatakuwa na msaidizi wala udhuru. Watauma vidole vyao kwa kujutia walivyomuasi Mwenyezi Mungu na Mtume, lakini ‘majuto ni mjukuu.’

Umetangulia mfano wake katika Juz. 19 (25:27).

Na watasema: Mola wetu! Hakika sisi tuliwatii mabwana zetu na wakubwa wetu, wakatupoteza njia. Mola wetu wape adhabu mara mbili, na walaani laana kubwa.

Makusudio ya mabwana na wakubwa ni viongozi wa dini na dunia. Laana ni kufedheheka. Wadhaifu watawageuzia adhabu na watamtaka Mwenyezi Mungu awaongezee adhabu.

Mwenye kuichunguza historia ataona kwamba aghlabu umma wa kijinga unaongozwa na mataghuti na waovu. Lakini watu wenye mwamko na maarifa hawaamini kuweka masilahi yao isipokuwa kwa waaminifu wenye ikhlasi.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:38).

Enyi ambao mmeamini! Msiwe kama wale ambao walimuudhi Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtaksa na waliyoyasema; naye alikuwa ni mwenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.

Waliomuudhi Musa(a.s) ni Wana wa Israil, hilo halina shaka; ambapo walimsifu sifa zisizokuwa za mitume.

Aya hii inaashiria kwamba badhi ya swahaba walimuudhi Mtume mtukufu(s.a.w.w) na wakambandika mambo asiyokuwa nayo, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawakataza waislamu hilo.

Kuna riwaya inayosema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) siku moja aliapa, basi mtu mmoja katika Answar akasema: “Kiapo hiki hakikusudiwa radhi ya Mwenyezi Mungu.” Hapo uso wa Mtume ukaiva wekundu na akasema:“Amrehemu Musa, hakika aliudhiwa zaidi ya hivi na akasubiri.”

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾

70. Enyi ambao mmeamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni kauli ya sawa.

يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾

71. Atawatengenezea matendo yenu na atawaghufiria dhambi zenu. Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amefuzu kufuzu kukubwa.

إِنَّا عَرَضْنَا الْأَمَانَةَ عَلَى السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالْجِبَالِ فَأَبَيْنَ أَن يَحْمِلْنَهَا وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا وَحَمَلَهَا الْإِنسَانُ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا ﴿٧٢﴾

72. Kwa hakika tulizitolea amana mbingu na ardhi na milima na vikakataa kuichukua na vikaiogopa, lakini mwanadamu akaichukua. Hakika yeye ni dhalimu mkubwa, mjinga sana,

لِّيُعَذِّبَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ وَيَتُوبَ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٣﴾

73. Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na washirikina wanaume na washirikina wanawake; na awapokelee toba waumini wanaume na waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

TULIZITOLEA AMANA

Aya 70 – 73

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni kauli ya sawa. Atawatengenezea matendo yenu na atawaghufiria dhambi zenu.

Kauli ya sawa ni kusema haki na ukweli, bila ya kuficha kitu; hata kama inamuhusu mwenyewe. Makusudio yake hapa ni ile inayowanufaisha watu kwa kulinganisha na kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Atawatengenezea amali zenu;’ ambapo Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejaalia kauli ya haki ni sababu ya matendo mema; kwa mfano kumwongoza aliyepotea kwenye njia ya heri na amani, kumsaidia aliyedhulumiwa kwa neno la usawa au kauli ambayo italeta suluhu baina ya watu wawili na mengineyo yanay- owanufaisha watu kwa namna moja au nyingine.

Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amefuzu kufuzu kukubwa.

Atafuzu duniani kwa kufaulu na kuwa na sera nzuri na katika Akhera atafuzu kwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake.

Kwa hakika tulizitolea amana mbingu na ardhi na milima na vikakataa kuichukua na vikaiogopa, lakini mwanaadamu akaichukua.

Wafasiri wametofautiana kuhusu maana ya amana. Kuna waliosema kuwa ni taklifa na twaa. Wengine wakasema ni tamko la Lailaha illahha (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu). Kuna waliosema ni viungo vya mwanadamu; kama masikio yake, macho yake, mikono yake na miguu yake. Kwamba ni juu yake kuvitumia kwa ajili ya lengo lilioumbiwa. Pia kuna wale waliosema kuwa ni amana katika mali.

Tuonavyo sisi maana yake ni kujitolea muhanga kwa ajili ya manufaa ya jamii, si kwa lololote isipokuwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na ya ubinadamu.

Kwa sababu kujitolea huku ni kuzito na kukubwa kiasi ambacho maumbile yenye nguvu zaidi, kama mbingu, ardhi na majabali yangelikataa kubeba, kama yangelikuwa na hisia.

Kwa hiyo lengo la kutaja mbingu na ardhi ni kuashiria ukubwa wa kuji- tolea huku, na kwamba binadamu ni kiumbe pekee anayeweza kupingana na nafsi yake na matamanio yake.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu:Hakika yeye ni dhalimu mkubwa, mjinga sana, maana yake ni kuwa binadamu atajidhulumu yeye mwenyewe na mwingine ikiwa ataifanyia hiyana amana hii na kutojua mwisho muovu utakotokana na hiyana yake hiyo.

Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ambao wanajionyesha kuwa wanatekeleza amana, lakini kumbe ni wahaini.

Na washirikina wanaume na washirikina wanawake. Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa vile kosa la ushirikina haliwezi kufutwa hata na kujitolea muhanga.

Na awapokelee toba waumini wanaume na waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Yaani anawaghufiria wenye kutubia na kuwahurumia wanyonge. Ewe Mwenyezi Mungu mrehemu Muhammad na kizazi chake, rehema ambayo atatuombea nayo siku tutakapohitajia.

MWISHO WA SURA YA THELATHINI NA TATU: SURAT AL-AHZAB