TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Juzuu 22

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 19906
Pakua: 2195


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 19906 / Pakua: 2195
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Juzuu 22

Mwandishi:
Swahili

24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

وَلَقَدْ آتَيْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿١٦﴾

16. Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu.

وَآتَيْنَاهُم بَيِّنَاتٍ مِّنَ الْأَمْرِ فَمَا اخْتَلَفُوا إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿١٧﴾

17. Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliokuwa baina yao. Hakika Mola wako atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika waliyokuwa wakikhitalifiana.

ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَىٰ شَرِيعَةٍ مِّنَ الْأَمْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٨﴾

18. Kisha tukakuweka juu ya sharia katika amri, basi ifuate. wala usifuate matamanio ya wasiojua.

إِنَّهُمْ لَن يُغْنُوا عَنكَ مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُتَّقِينَ ﴿١٩﴾

19. Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni mawalii wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni walii wa wenye takua.

هَـٰذَا بَصَائِرُ لِلنَّاسِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ ﴿٢٠﴾

20. Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni mwongozo, na rehema kwa watu wanaoyakinisha.

WANA WA ISRAIL TENA

Aya 16 – 20

MAANA

Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu.

Katika Aya zilizotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja wazushi wenye dhambi ambao wamezikanusha dalili za Mwenyezi Mungu na wakaidharau haki na watu wake.

Kwa kuwa Wana wa israil ni mfano halisi wa sifa hizi, ndio akafuatishia kuwataja na yale waliyo nayo ya upinzani na madhambi; pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu aliwaneemesha kwa Tawrat na Injil alizoziashiria kwa neno Kitab. Akawafahamisha mawaidha na hukumu zilizomo ndani ya vitabu hivyo. Na hayo ndio makusudio ya ‘Hukumu.’

Akawafanyia mitume kutokana na wao na akawateremshia Manna na Salwa, alizoziashiria Mwenyezi Mungu kwa neno ‘Vitu vizuri.’ Pia akawafadhilisha juu ya watu wa Firauni pale alipowagharikisha na waisrail wakapumua kutokana na adhabu yao.

Na tukawapa maelezo wazi ya amri.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwafafanuliwa Wana wa Israil mahitaji yao ya mambo ya dini, hawakubakiwa na udhuru au visababu vya kutofautiana na kufarikiana.

Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliokuwa baina yao.

Waliyajua kwa yakini yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwa Musa, lakini wao wakajitia kutojua na wakayageuza kulingana na matamanio na masilahi yao:

مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ وَيَقُولُونَ سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا ﴿٤٦﴾

“Miongoni mwa mayahudi wako ambao hugeuza maneno kutoka mahali mwake na husema: tumesikia na tumeasi.” Juz. 5 (4:46).

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Basi hawakukhitalifiana,” inaashiria kuwako wachache kwa nadra waliothibiti katika haki.

Hakika Mola wako atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika waliyokuwa wakikhitalifiana.

Katika maisha ya duniani, mara nyingine asiyekuwa na haki humshinda mwenye haki, lakini akhera itakayokuwa juu ni haki peke yake; vinginevyo mwenye haki angekua ni mbaya kuliko asiyekuwa na haki.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:93).

WAISRAIL WAMEPIGWA NA UDHALILI KWA HUKUMU YA TAWRAT

Qur’an imewazungumzia Wana wa Israil kwa kusema: “Wamepigwa na udhalili popote wanapokutanikana” Juz. 4 (3:112). Huko tumezungumza kwa ufafanuzi zaidi kuhusu Aya hii na tukasema kuwa Israil ni kambi ya kijeshi ya ukoloni na kwamba itaisha tu, sasa au baadaye.

Hivi sasa tutanukuu kitabu kitakatifu kwa Mayahudi yale yanayofahamisha kwa uwazi kuwa Mwenyezi Mungu amewaandikia Waisrail udhalili hadi siku ya mwisho: “Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israel sana…. Kwa hiyo BWANA akakitaa kizazi chote cha Israel, akawatesa.”

(2 Wafalme 17:18 – 20)

“Basi BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa nami nitawapa maji ya uchungu wanywe. Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao hao hawakuwajua; wala baba zao; nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza.” (Yeremia 9:15-16)

“Nanyi mtasalia wachache kwa hisabu…..Nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi” Kumbukumbu la (Torati 28: 62-63). Maneno katika nukuu zote hizo yanaelekwezwa kwa Wana wa Israil. Kuna nukuu nyinginezo zaidi ya hizi.

Tunawauliza wazayuni: Ikiwa nyinyi ni taifa teule la Mwenyezi Mungu, kama mnavyodai, basi kwa nini nyinyi na kizazi chenu Mwenyezi Mungu amewahukumia udhalili, kufukuzwa hadi kung’olewa kabisa? Vipi Mola akatoa ahadi kuwa ataifanya Jerusalem ni magofu na makao ya mbweha? Kama ilivyoelezwa katika Yeremia 9:11, “Nami nitafanya Yerusalem kuwa magofu, makao ya mbweha; Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, isikaliwe na mtu awaye yote.”

Ni kipi hicho Kitabu kitakatifu kwa ajili ya dola yenu ya kidini ya kiubaguzi, kama alivyosema Pompidou, raisi wa ufaransa? Je, ni Tawrat iliyowasifu nyinyi na mji wenu kwa kusema: “Bwana asema hivi; mji – yaani Yerusalem – umwagao damu ndani yake…Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu.”

(Ezekieli 22: 3,6.)

Vile vile umeshutumiwa mji wa Jerusalemu, kwenye Luka mtakatifu 13:34: “Ewe Yerusalemu, Yerusalemu, wewe uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako!”

Inasema Biblia kuwa kila mahali na kila wakati Mayahudi ni washirika wa hatia ya mababu zao waliomsulubu Bwana Masih, kwa sababu wanaliridhia hilo kwa vitendo vyao kwa kusema kuwa Yeye ni mwanaharamu.

Hayo yanaafikiana na msingi wa kiislamu unaosema kuwa mwenye kufanya dhulma, mwenye kuisaidia na mwenye kuiridhia wote ni washirika.

Ndio maana kanisa la Khufti (Coptic), likaingilia kati kumpinga Baba mtakatifu, wakati yeye na wasaidizi wake walipotoa tamko rasmi la kukisafisha kizazi cha kiyahudi na damu ya Bwana Masih.

Ieleweke kuwa Baba mtakatifu alitoa tamko hili kabla ya muda mchache Israil kuvamia miji ya Kiarabu.

Kisha tukakuweka juu ya sharia katika amri, basi ifuate.

Neno sharia katika Lugha lina maana ya chemchem ya maji. Kisha likaazimwa kutumiwa kwenye hukumu za dini. Kwa sababu zinaipa uhai roho; kama maji yanayvoupa uhai mwili. Makusudio ya amri hapa ni dini. Maana ni kuwa Ewe Muhammad tumekujaalia kwenye itikadi ya Tawhid na kuing’oa shirki na tukakupa sharia nyepesi, basi shikamana nayo. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:wala usifuate matamanio ya wasiojua, maana yake ni kuwa wakosefu hawafuati isipokuwa matamanio na lengo.

Na wala usizichukulie lawama za mwenye kulaumu, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) atakutosha na vitimbi vya wenye vitimbi na shari za wenye njama.

Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu anayeshindwa kujikinga yeye mwenyewe hawezi kumsaidia mwingine.

Na hakika wenye kudhulumu ni mawalii wao kwa wao.

Mwenye hatia duniani hapati wa kumsaidia na kumnusuru isipokuwa aliye kama yeye katika hatia na dhambi, na walio wema ni maadui zake na wagomvi wake. Lakini huko Akhera, wenye hatia watalaniana wao kwa wao.Na Mwenyezi Mungu ni walii wa wenye takua, duniani na Akhera.

Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni mwongozo, na rehema kwa watu wanaoyakinisha.

Ni dalili zinazowaonyesha haki na njia ya uongofu. Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kufuata Qur’an anakuwa na yakini kwamba yeye yuko kwenye uongofu Kutoka kwa Mola na kuingia kwenye rehema yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:203).

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ﴿٢١﴾

21. Je, wanadhani wanaotenda maovu kuwa tutawafanya kama walioamini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni mabaya wanayohukumu.

وَخَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَلِتُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٢٢﴾

22. Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki. Na ili kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma. Nao hawatadhulumiwa.

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّـهِ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٢٣﴾

23. Je, umemwona aliyefanya hawaa yake kuwa ndio mungu wake? Basi nani atamwongoza baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ وَمَا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ ﴿٢٤﴾

24. Na walisema: Hapana ila uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana kinachotuhilikisha isipokuwa dahari. Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu.

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ مَّا كَانَ حُجَّتَهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٥﴾

25. Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wakweli.

قُلِ اللَّـهُ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يَجْمَعُكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢٦﴾

Sema: Mwenyezi Mungu anawapa uhai, kisha anawafisha, kisha anawakusanya, Siku ya Kiyama isiyo na shaka.

AMEIFANYA HAWA YAKE NDIO MUNGU WAKE

Aya 21 – 26

MAANA

Je, wanadhani wanaotenda maovu kuwa tutawafanya kama walioamini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni mabaya wanayohukumu.

Inawezekana mwema na muovu wawe na daraja sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na katika mtazamo wa kiakili? Basi kutakuwa na haja gani ya kuitwa mwema na mwengine muovu? Nini itakuwa tofauti ya heri na shari?

Wataalamu wa ilimu ya teologia wamechukua madhumuni ya Aya hii na wakasema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaahidi watiifu thawabu na akawahidi waasi adhabu, na duniani hakutokei kitu katika hayo. Kwa hiyo basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibisha kurudisha uhai baada ya mauti ili upatikane utekelezaji wa ahadi yake.

Vile vile Mwenyezi Mungu ni mwadilifu, hilo halina shaka, na tunamuona dhalimu akimaliza maisha yake bila ya kulipizwa kisasi na yoyote aliyedhulumiwa. Lau si kurudi kwa hisabu na malipo, basi mdhulumiwa angelikuwa na hali mbaya zaidi ya dhalimu na Mwenyezi Mungu angelikuwa dhalimu. Ametakata sana Mwenyezi Mungu na hayo.

Ama neema za dunia sio alama ya kuridhia Mwenyezi Mungu. Wala shida ya dunia sio dalili ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Imam Ali (a.s.) anasema: “Enyi watu! Hakika dunia ni ya kupita na akhera ni ya kutulia, basi chukueni kutulia kwenu katika mapito yenu…nyoyo zenu zitoeni duniani kabla hazijatoka milini mwenu. Kwenye hiyo dunia mnapewa mtihani na mmeumbwa kwa ajili ya kwengine sio duniani.”

Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki.

Hii ni sababu ya kutofanywa sawa mwema na muovu. Ubainifu wake ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ulimwengu kwa haki na uadilifu; vinginevyo ingelikuwa kuumbwa ulimwengu ni kwa mchezo na ubatilifu.

Kwa sababu mwenye kufanya mchezo kwenye jambo moja anaweza kufanya kwenye jambo jingine.

Na ili kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma. Nao hawatadhulumiwa.

Hii ndio njia ya usawa – njia ya haki na uadilifu; mwenye kufanya heri kwa uzani wa chembe ataiona, na mwenye kufanya shari kwa wizani wa chembe ataiona. Tazama Juz. 11 (10:4) kifungu cha: ‘Hisabu na malipo ni lazima.’

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu ana hekima na ameepukana na makosa, na hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu inapelekea kuwafufua watu baada ya mauti, ili kumpambanua mwema na muovu na kumlipa kila mmoja stahiki yake. Kama si hivyo basi kuumbwa ingelikuwa ni kwa mchezo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki.” yaani ametakasika na mchezo. Juz. 18 (23:115-116)

Je, umemwona aliyefanya hawa yake kuwa ndio mungu wake?

Miongoni mwa watu kuna yule ambaye haamini chochote isipokuwa nafsi yake na masilahi yake tu. Anaweza kuwa anasoma tahlili na takbira; bali anaweza pia kuwa anafunga na kuswali, madamu hilo haliingiliani na anayoyapenda na kuyatamani. Hawa yake ndiyo muabudiwa wa haki peke yake, mengineyo ni nyenzo tu, sio lengo; au ni mazoweya tu sio ibada. Haya ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘aliyefanya hawa yake kuwa ndio mungu wake.’

Neno hawa limetokana na neno la kiarabu linalotamkwa hivyo hivyo ‘Hawaa’ lenye maana pia ya kuanguka chini. Kuna mmoja amesema, hali hiyo imeitwa hawa kwa sababu inamwangushwa kwenye Jahannam aliye nayo. Msemaji amechukua fikra hii kutokana kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٤٠﴾ فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ﴿٤١﴾

“Na ama yule mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake, na akaikataza nafsi na hawa, basi hakika Pepo ndio makazi (yake).” (79:40-41).

Kuna tafsiri inayosema kuwa mshirikina aliye jahili, alikuwa akiangukia jiwe kuliabudu, kisha anaona jingeni analiangukia na kulitupa lile la kwanza. Ndio hivyo anayemtupa Mungu na kuangukia kwenye ‘hawa’ kuwa ndio Mungu wake.

Hakuna mwenye shaka kwamba mshirikina mpumbavu, hatia yake mbele ya Mwenyezi Mungu inazidiwa na kibaraka anyeiuza dini yake na dhamira yake kwenye mnada na kushikana na yule anayezidisha bei.

Na Mwenyezi Mungu akampoteza licha ya ilimu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hampotezi. Atampotezaji na hali Yeye ndiye aliyekataza upotevu na akautolea kiaga kikali? Lakini anyefuata njia ya upotevu kwa hiyari anamwachila mbali na upotevu wake, wala hapatwi na upole wake na msaada wake, baada ya kujua kwa mbali upotevu wake na inadi yake.

Ama kauli yake:na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akaweka kizibo machoni mwake, maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anampofusha na kumtia uziwi mwenye inadi baada ya kuitambua haki kwa macho yake na masikio yake, baada ya kubainishiwa na kuhimizwa, lakini akipinga bila ya sababu za maana. Mwenyezi Mungu nasema:

فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ ﴿٥﴾

“Lakini walipopotoka, Mwenyezi Mungu akazipotoa nyoyo zao, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki.” (61:5).

Basi nani atamwongoza baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?

Asiyenufaika na mawaidha ya Mwenyezi Mungu basi hayawezi kumfaa mwaidha na nasaha zote.

Na walisema: Hapana ila uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana kinachotuhilikisha isipokuwa dahari.

Wamaada au wadahari, vyovyote utakavyowaita, wanasema kuwa binadamu ni mchanaganyiko wa vitu vya kimaada vilivyokusanyika kutoka huku na huko na vikafanyika. Kwa hiyo akifa ndio amekwisha, hakuna chochote baada ya mauti, sawa na mimea na wadudu. Na kwamba hizi hisia na utambuzi tunaouna kwa binadamu zimezalishwa na mwili kutokana na mchanganyiko wa hali. Yaani akili ya mwanadamu ni mkondo wa pili usiokuwa na asili na chanzo.

Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu.

Yaani kauli yao hii ni madai yasiyokuwa na hoja; bali kuna hoja ya kuayavunja. Yule ambaye anaihukumu maada, kuipatia manufaa na kujua mengi zaidi kuihusu, lakini yenyewe isimjue yeye, hapana budi kuwa, mtu huyu wa ajabu, awe ni mkuu na yuko zaidi kuliko maada. Yametangulia maneno kuhisiana na hayo mara nyingi; kama vile kwenye Juz. 14 (16:78).

Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wakweli.

Hii ni sawa na anayesema, siwezi kuamini kuwa mtofahaa unaweza kuzaa matunda wakati wa kaskazi mpaka niuone una mimba wakati wa kusi. Mtoto huyu akishakuwa mkubwa, atajua kuwa kila kitu kina muda wake na kwamba kila ajali ina maandishi haikawii wala kuwahi. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo kwenye (44:36).

Sema: Mwenyezi Mungu anawapa uhai, kisha anawafisha, kisha anawakusanya, Siku ya Kiyama isiyo na shaka.

Ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye anayempa uhai mtu alipokuwa si chochote, atashindwa vipi kumpa uhai mara ya pili? Lakini watu wengi hawajui kuwa kurudishwa mara ya pili ni rahisi kuliko kuumbwa kwa kwanza. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa, zikiwemo: Juz. 1 (2:28) na Juz.17 (22:66).

25

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَخْسَرُ الْمُبْطِلُونَ ﴿٢٧﴾

27. Na ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na siku itaposimama Saa, siku hiyo watahasirika wenye batili.

وَتَرَىٰ كُلَّ أُمَّةٍ جَاثِيَةً كُلُّ أُمَّةٍ تُدْعَىٰ إِلَىٰ كِتَابِهَا الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٢٨﴾

28. Na utauona kila umma umepiga magoti. Kila umma utaitwa kwenye kitabu chake: Leo mtalipwa mliyokuwa mkiyatenda.

هَـٰذَا كِتَابُنَا يَنطِقُ عَلَيْكُم بِالْحَقِّ إِنَّا كُنَّا نَسْتَنسِخُ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٢٩﴾

29. Hiki kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyokuwa mkiyatenda.

فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَيُدْخِلُهُمْ رَبُّهُمْ فِي رَحْمَتِهِ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْمُبِينُ ﴿٣٠﴾

30. Ama wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaingiza katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi.

وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا أَفَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَاسْتَكْبَرْتُمْ وَكُنتُمْ قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿٣١﴾

31. Na ama wale waliokufuru: Kwani hamkuwa mkisomewa Aya zangu nanyi mkawa na kiburi, na mkawa watu wakosefu?

KILA UMMA UTAITWA KWENYE KITABU CHAKE

Aya 27 – 31

MAANA

Na ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anaashiria, kwa kauli hii, kwamba aliyeumba mbingu na ardhi na wala asichoke, bila shaka, ni muweza wa kuhuisha wafu.

Na siku itaposimama Saa ya Kiyama,siku hiyo watahasirika wenye batili, kwa sababu makazi yao ni motoni siku hiyo, wala hawatakuwa na wa kuwasaidia.

Na utauona kila umma umepiga magoti.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawafufua watu wakiwa wamepiga magoti wakingoja hisabu na malipo. Sio mbali kuwa hiki ni kinaya cha fazaa na hofu itakayojitokeza.

Kila umma utaitwa kwenye kitabu chake: Leo mtalipwa mliyokuwa mkiyatenda.

Makusudio ya kitabu hapa ni maandishi ya matendo. Maana ni kuwa kila umma na kila mtu atalipwa kwa aliyoyatenda. Kwenye Nahjul-balagha, Imam Ali(a.s ) anasema:“Anapokufa mtu watu husema alichokiacha, na Malaika husema alichokileta”

Hiki kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyokuwa mkiyatenda.

Kesho wakosefu wataambiwa haya ndiyo tuliyoyaandika kuhusiana na nyinyi. Picha kamili ya matendo haina nyongeza wala upungufu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Malaika kusajili vitendo vyenu na kuvihifadhi kwa pumzi zenu mlizozitumia kwenye maasi.

وَيُنذِرَ الَّذِينَ قَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا ﴿٤﴾

Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana. Juz. 15 (18:4).

Ama wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaingiza katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi.

Walifuata njia ya amani, Mwenyezi Mungu akawaongoza katika rehema yake. Imam Ali(a.s) anasema:“Hatafuzu kwa heri ila mwenye kuifanyia kazi, wala hatafedheheka na shari ila aliyeifanya.”

Na ama wale waliokufuru, wataambiwa: Kwani hamkuwa mkisomewa Aya zangu nanyi mkawa na kiburi, na mkawa watu wakosefu?

Kesho Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawambia waasi waliokuwa na inadi na kiburi, kwa kuwasuta na kuwatahayariza kuwa mliisikia sauti ya haki hamkuitika na mkaona dalili waziwazi mkazipinga kwa inadi na kiburi; mkastarehe kwenye ufisadi na upotevu, basi leo nyinyi ni katika waliohasirika.

وَإِذَا قِيلَ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَالسَّاعَةُ لَا رَيْبَ فِيهَا قُلْتُم مَّا نَدْرِي مَا السَّاعَةُ إِن نَّظُنُّ إِلَّا ظَنًّا وَمَا نَحْنُ بِمُسْتَيْقِنِينَ ﴿٣٢﴾

32. Na ikisemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, na Saa haina shaka, nyinyi mkisema: Hatuijui hiyo Saa, tunadhania dhana tu, wala hatuna yakini.

وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا عَمِلُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na ubaya wa waliyoyatenda utawadhihirikia, na yatawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

وَقِيلَ الْيَوْمَ نَنسَاكُمْ كَمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا وَمَأْوَاكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٣٤﴾

34. Na itasemwa: Leo tunawasahau kama mlivyosahau mkutano wa siku yenu hii; na mahali penu ni Motoni, wala hamna wa kuwanusuru.

ذَٰلِكُم بِأَنَّكُمُ اتَّخَذْتُمْ آيَاتِ اللَّـهِ هُزُوًا وَغَرَّتْكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فَالْيَوْمَ لَا يُخْرَجُونَ مِنْهَا وَلَا هُمْ يُسْتَعْتَبُونَ ﴿٣٥﴾

35. Hiyo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu; na maisha ya dunia yakawadanganya. Basi leo hawatatolewa humo wala hao hawatakubaliwa udhuru.

فَلِلَّـهِ الْحَمْدُ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَرَبِّ الْأَرْضِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٣٦﴾

36. Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa mbingu, na Mola wa ardhi, na Mola wa walimwengu wote.

وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٣٧﴾

37. Na ukubwa ni wake, mbinguni na katika ardhi, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

LEO TUNAWASAHAU

Aya 32-37

MAANA

Na ikisemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, na Saa haina shaka, nyinyi mkisema: Hatuijui hiyo Saa, tunadhania dhana tu, wala hatuna yakini.

Bado mazungumzo ya wakosefu yaaendelea. Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Saa haina shaka,’ ni ubaiinifu na tafairi ya ahadi ya Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa wakosfu walipokuwa wakiwaambiwa na waumini kuwa ufufuo ni kweli na hisabu na malipo ni kweli, wao walikuwa wakisema: sisi hatuna uhakika na ufufuo wala hatuji chochote kuhusiana nao isipokuwa dhana. Basi tuleteeni.dalili yake.

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwenye Aya 24 ya sura hii, amewasimulia kuwa wao walikana ufufuo kwa njia ya mkato, kama inavyofahamisha kauli yao: ‘hapana ila maisha yutu ya duniani,’ kisha hapa Mwenyezi Mungu anawasimulia kwamba wao wanadhania na hawana yakini, yaani hawakatai moja kwa moja. Vipi tutazichanganya Aya mbili hizi?

Razi anasema dhana kubwa ni kuwa wao walikuwa vikunndi viwili: kundi liliokanusha ufufuo kwa mkato na kundi jingine walikuwa na shaka.

Lakini sisi dhana yetu kubwa ni kuwa walikuwa kundi moja tu, na kwamba maana ya Aya zote mbili ni kuwa wao hawaamini ufufuo kwa vile wanadai hawana dalili inayoyakinisha isipokuwa ni mambo yaliyo mbali na wao.

Na ubaya wa waliyoyatenda utawadhihirikia, na yatawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

Duniani walipanda makosa na madhambi watayavuna matunda yake Akhera. Waliidharau Jahannam watakuwa ni kuni zake.

Na itasemwa: Leo tunawasahau kama mlivyosahau mkutano wa siku yenu hii; na mahali penu ni Motoni, wala hamna wa kuwanusuru.

Waliikana siku ya Kiyama na wakaifanyia dharau na wale wanaoiamini, Mwenyezi Mungu akawapa muda na wala hawatapata rehema ya Mwenyezi Mungu siku hiyo, bali atawaonjesha adhabu ya siku hiyo na atawaonyesha uweza wake na nguvu zake ndani ya siku hiyo waliyoitilia shaka. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:51).

Hiyo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu; na maisha ya dunia yakawadanganya.

‘Hiyo’ ni hiyo adhabu. Maana ni kuwa iliyosababisha adhabu yao ni kukanusha kwao siku ya mwisho, kuipinga Qur’an na kuzidharau Aya zako wanaposomewa na kujituliza kwao na dunia na strehe zake.

Basi leo hawatatolewa humo wala hao hawatakubaliwa udhuru.

‘Humo’ ni humo motoni. Maana ni kuwa wao watakaa milele humo, wala hawatatakiwa kumtaka radhi Mwenyezi Mungu kwa kauli au kitendo. Kwa sababu Akhera ni nyumba ya hisabu na malipo sio nyumba ya kuomba radhi.

Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa mbingu, na Mola wa ardhi, na Mola wa walimwengu wote.

Msifuni Mwenyezi Mungu peke yake, kwa sababu Yeye ni muumba wa kila kitu.

Na ukubwa ni wake, mbinguni na katika ardhi.

Makusudio ya ukubwa wake Mtukufu ni kwamba hakuna mkubwa anayehofiwa au kutarajiwa isipokuwa Yeye peke yake. Imam Ali(a.s.) akiwasifu wanaomjua Mwenyezi Mungu kwa kusema:“Amekuwa mkubwa Muumba katika nafsi zao akawa mdogo asiyekuwa Yeye machoni mwao.”

Naye ni Mwenye nguvu, ambaye hakimshindi chochote.Mwenye hikima katika mpangilio wa kuumba kwake.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI