TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Juzuu 22

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 19745
Pakua: 2110


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 19745 / Pakua: 2110
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI Juzuu 22

Mwandishi:
Swahili

15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَـٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ ﴿٢٧﴾

27. Na lau Mwenyezi Mungu angeliwakunjulia riziki waja wake basi bila ya shaka wangeliasi katika dunia, lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona.

وَهُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ الْغَيْثَ مِن بَعْدِ مَا قَنَطُوا وَيَنشُرُ رَحْمَتَهُ وَهُوَ الْوَلِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٢٨﴾

28. Naye ndiye anayeiteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Walii Mwenye kuhimidiwa.

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِن دَابَّةٍ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ ﴿٢٩﴾

29. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza humo. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo.

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ ﴿٣٠﴾

30. Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu. Naye anasamehe mengi.

وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿٣١﴾

31. Na nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Na hamna walii wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

وَمِنْ آيَاتِهِ الْجَوَارِ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ ﴿٣٢﴾

32. Na katika Ishara zake ni vyombo baharini kama vilima.

إِن يَشَأْ يُسْكِنِ الرِّيحَ فَيَظْلَلْنَ رَوَاكِدَ عَلَىٰ ظَهْرِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ ﴿٣٣﴾

33. Akitaka, huutuliza upepo navyo husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.

أَوْ يُوبِقْهُنَّ بِمَا كَسَبُوا وَيَعْفُ عَن كَثِيرٍ ﴿٣٤﴾

34. Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyoyatenda. Naye husamehe mengi.

وَيَعْلَمَ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِنَا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ ﴿٣٥﴾

35. Na ili wajue wale wanaojadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia.

RIZIKI NI KWA KUFANYA KAZI SIO KWA DUA

Aya 27 – 35

MAANA

Na lau Mwenyezi Mungu angeliwakunjulia riziki waja wake basi bila ya shaka wangeliasi katika dunia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameitegemeza riziki kwa waja wake kwa kuchuma kwao na kufanya kazi si kwa matakwa yao na matamanio; vinginevyo ingelienea vurugu na kufanya ufisadi katika ardhi.

Lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho.

Yaani anamrukuzu kwa kadiri ya utendaji wake wa kazi. Mara nyingine Mwenyezi Mungu hutoa riziki nyingi kwa kazi chache au riziki chache kwa kazi nyingi kulingana na hekima anayoijua Yeye zaidi. Ama utajiri unaotokana na haramu; kama vile kughushi na kupora, hiyo ni riziki ya shetani sio ya kutokana na kutoa kwa Mwingi wa rehema; vipi isiwe hivyo na hali mwenye riziki hiyo amepewa kiaga cha adhabu chungu?

Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona.

Anamjua anayeishi kwa hisabu ya kupora na anayeishi kwa jasho lake. Wa kwanza amemwahidi hizaya na adhabu na wa pili ni heshima na thawabu.

Naye ndiye anayeiteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na hueneza rehema yake.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja riziki, anasema kuwa sababu za hizo riziki, kama vile mvua, ziko mikononi mwake. Huipeleka anapotaka na huizuia anapotaka. Basi ikichelewa kidogo, wao hukata tamaa, lakini anawawahi kwa rehema yake iliyoenea katika kila kitu.

Naye ndiye Walii anayewasimamia waja wake kwa wemaMwenye kuhimidiwa anyestahiki sifa njema na kushukuriwa.Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza humo.

Makusudio ya mbingu ni kilicho juu, iwe sayari au anga; na makusudio ya wanyama hapa ni kila mwenye uhai wakiwemo malaika ndege au yoyote mwenye uhai anayeishi nchi kavu au baharini na kwenye anga au kwenye nyota. Wote hao wanaonyesha kuweko mtengenezaji wake na mtia sura wake.Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo; sawa na alivyoweza kuwaumba na kuwaeneza mbinguni na ardhini.

Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu.

Aya hii inafahamisha waziwazi, wala haikubali taawili yoyote, kuwa dhulma na ufukara unatokana na watu sio Mwenyezi Mungu na wala hautokani na hukumu ya Mwenyezi Mungu na sharia yake; hata kahati na kuzuilika mvua, sababu yake ni dhulma na ufisadi; kama ilivyoelezwa katika Hadith na katika kitabu cha Mwenyezi Mungu: “Lau wangelisimamisha Tawrat na Injil na yale yaliyoteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao, kwa hakika wangelikula vya juu yao na vya chini ya miguu yao. ‘Juz. 6 (5:66), kifungu cha ‘Riziki na ufisadi’

Naye anasamehe mengi katika madhambi isipokuwa shirki na dhulma, kwa sababu Yeye ndiye aliyesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ﴿٤٨﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika, lakini husamehe yasiyokuwa hayo.” Juz. 5 (4:48).

Na akasema:

يَوْمَ لَا يَنفَعُ الظَّالِمِينَ مَعْذِرَتُهُمْ وَلَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ ﴿٥٢﴾

“Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao watapata laana, na watapata makazi mabaya kabisa.” Juz. 24 (40:52).

Na nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Na hamna walii wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 20 (29:22)

Na katika Ishara zake ni vyombo baharini kama vilima.

Ikiwa jahazi limetengenezwa na mtu lakini maji linayoyapitia na upepo unaolisukuma ni katika matengenezo yake Mwenyezi Mungu na hata miti iliyotengenezewa nk. Pia ndege zinazopaa kwenye anga ya Mwenyezi Mungu, magari yanayotembea kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu na vingenevyo hata mtu mwenyewe pia. Vyote hivyo vinadhihirisha uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na rehema zake.

Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu ya bahari.

Akizuia upepo au akiyagandisha maji basi majahazi yatasimama tu.

Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.

Mwenye kuwa na subira ya tafakuri na kuutazama ulimwengu na maajabu ya siri zake, hana budi kuishia kwenye imani ya Mwenyezi Mungu na utukufu wake, na atamshukuru kwa fadhila zake na mwongozo wake.

Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyoyatenda hao watu.Naye husamehe mengi; yaani hawaharakishi pamoja na dhambi zao nyingi.

Na ili wajue wale wanaojadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia.

Wanaojadiliana katika ishara za Mwenyezi Mungu ni wale wanaosema kuwa hakuna kitu kinachofahamisha kuwa Mwenyezi Mungu yuko. Maana ni kuwa makafiri hawamuamini Mwenyezi Mungu na kupinga kila dalili inayotamka kuweko kwake.

Hata hivyo iko njia moja ya kuamini na kukiri kwao ambayo ni kuona maangamizi kwa macho yao na kujua kuwa hakuna pa kukimbilia; mfano jahazi likisimama baharini au upepo mkali. Kwa maneno mengine hawaamini mpaka waone adhabu.

فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٣٦﴾

36. Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu zaidi. Kwa ajili ya walioamini na wakawa wanamtegemea Mola wao.

وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ ﴿٣٧﴾

37. Na wanayaepuka madhambi makubwa na mambo machafu na wanapokasirika wao husamehe.

وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣٨﴾

38. Na wanaomwitikia Mola wao na wakasimamisha Swala. Na mambo yao ni kwa kushauriana baina yao na wanatoa katika yale tuliyowapa.

وَالَّذِينَ إِذَا أَصَابَهُمُ الْبَغْيُ هُمْ يَنتَصِرُونَ ﴿٣٩﴾

39. Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ ﴿٤٠﴾

40. Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.

وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَـٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ ﴿٤١﴾

41. Na wanaojitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu.

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٤٢﴾

42. Bali njia ya lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.

وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿٤٣﴾

Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.

KILICHOKO KWA MWENYEZI NI BORA NA KITABAKIA

Aya 36 – 43

MAANA

Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu,

Starehe za dunia ni kila kinachostarehesha katika maisha haya; kama vile afya cheo, mali, wanawake, watoto, majengo, samani na mengineyo. Anasa za dunia hata zikiwa nyingi, zinaondoka na kuisha. Ama neema za Akhera zinabaki kwa kubakia kwake:

مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ ﴿٩٦﴾

“Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobakia.”

Juz. 14 (16:96).

Anaendelea kusema Mwenyezi Mungu:lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu zaidi.

Kila amali itakayotekeleza haja yoyote katika maisha basi hiyo ni akiba mbele ya Mwenyezi Mungu kwa Masharti yafuatayo:-

1.Kwa ajili ya walioamini Mwenyezi Mungu. Ama wale waliomkufuru hawana chochote mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa adhabu, kwa vile wao hawakiri isipokuwa kuweko kwake. Kuna Hadithi inayosema: “Mwenye kumfanyia amali asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamwachia aliyemfanyia amali, na kesho ataambiwa: chukua malipo yako kwa uliyemfanyia.”

2.Na wakawa wanamtegemea Mola wao katika mambo yao yote, wala hawajienzi isipokuwa kwa kumcha Mwenyezi Mungu na radhi yake.

3.Na wanayaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, ikiwemo dhulma, uongo na ufisadi. Tazama Juz. 5 (4:31) na Juz. 8 (6:151)

4.Na wanapokasirika wao husamehe; yaani si wepesi wa kukasirika na wasiokasirika isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu.

5.Na wanaomwitikia Mola wao, hawamuasi katika amri yake wala makatazo yake.

6.Na wakasimamis ha Swala. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameihusisha kuitaja hapa kwa vile ndio nguzo ya dini, na Mtume(s.a.w. w ) alikuwa akiita ‘kitulizo cha jicho.’ Baadhi ya wataalamu wameiita ‘Uhakika wa Mwislamu’

7.Na mambo yao ni kwa kushauriana baina yao.

Kauli ‘mambo yao’ inaashiria mambo mema ya uma na kwamba wao wanasaidiana kuufanyia kazi uma. Kushauriana huku si katika halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake, kwa sababu zinatokana na Mwenyezi Mungu tu peke yake. Tazama Juz. 4 (3:159). Katika Nahjul-balagha amesema: “Kutaka ushauri ni jicho la mwongozo na amejiingiza kwenye hatari anayetosheka na rai yake.”

8.Na wanatoa katika yale tuliyowapa, katika mali.

9.Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.

Unaweza kuuliza : Tutaichanganya vipi Aya hii na ile isemayo: ‘Na wanapokasirika wao husamehe?’

Jibu : Kusamehe uovu ni vizuri ikiwa kutasababisha muovu kujirekebisha na kutubia au ikiwa ni kukinga ugomvi na fitina, lakini si kuzuri ikiwa kutasababisha ujeuri na usafihi kwa muasi. Imam Ali(a.s ) anasema:“Kuwatekelezea ahadi wavunja ahadi ni kuvunja ahadi mbele ya Mwenyezi Mungu na kuvunja ahadi kwa wavunja ahadi ni kutekeleza ahadi.”

Tumeelezea hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 24 (41:34).

Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo.

Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ ﴿١٩٤﴾

“Anayewachokoza nanyi mchokozeni kwa kadiri alivyowachokoza.” Juz.2 (2:194).

Lakini mwenye kusamehe na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu.

Mfano wake ni

وَأَن تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ﴿٢٣٧﴾

“Na kusamehe ndiko kuliko karibu zaidi na takua” Juz. 2 (2:237).

Vile vile:

فَمَن تَصَدَّقَ بِهِ فَهُوَ كَفَّارَةٌ لَّهُ ﴿٤٥﴾

“Lakini atakayesamehe itakuwa kafara kwake.” Juz. 6 (5:45).

Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.

Makusudio ya madhalimu hapa ni wale wanaopita mpaka wa kisasi.

Na wanaojitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu kabisa wala hakuna kuadhibiwa, kwa sababu mwenye kuanza ndiye dhalimu, na mwenye kudhulimiwa anayo haki ya kujitetea; bali akimnyamazia aliyemdhulumu basi atakuwa ni mshirika katika dhulma, kwa sababu kumnyamazia dhalimu kunamtia mori. Na lau dhalimu atajua kuwa mdhulumiwa ataitetea heshima yake basi atajizuia.

Bali njia ya lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.

Huko nyuma tumewahi kueleza kuwa dhalimu anahukumiwa kuwa ni kafiri mbele ya Mwenyezi Mungu, ajapotamka shahada mbili. Ndio! Hapa duniani atachukuliwa kama Mwislamu, lakini Akhera atakuwa pamoja na madhalimu. Hilo ni kwa ushahidi wa Aya kadhaa, zinazomwita kafiri kuwa ni dhalimu na dhalimu kuwa ni kafiri. Tazama Juz. 3 (2:254) na Juz. 9 (25:55-62).

Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa; yaani ni mambo mazuri ya kuazimiwa kufanywa. Aina bora ya subira ni kuvumilia udhia katika kuithibitisha haki na kuitangaza. Na aina bora zaidi ya kusamehe ni kule kutakakosababisha kuondoa fitina na ufisadi.

16

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA MBILI

وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن وَلِيٍّ مِّن بَعْدِهِ وَتَرَى الظَّالِمِينَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ يَقُولُونَ هَلْ إِلَىٰ مَرَدٍّ مِّن سَبِيلٍ ﴿٤٤﴾

44. Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, hana walii baada yake. Na utawaona madhalimu watakapoiona adhabu watasema: Je, ipo njia ya kurudi?

وَتَرَاهُمْ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا خَاشِعِينَ مِنَ الذُّلِّ يَنظُرُونَ مِن طَرْفٍ خَفِيٍّ وَقَالَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَلَا إِنَّ الظَّالِمِينَ فِي عَذَابٍ مُّقِيمٍ ﴿٤٥﴾

45. Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walioamini watasema: Hakika waliopata hasara ni hao waliohasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! Hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya kudumu.

وَمَا كَانَ لَهُم مِّنْ أَوْلِيَاءَ يَنصُرُونَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن سَبِيلٍ ﴿٤٦﴾

46. Wala hawatakuwa na walii wa kuwanusuru asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemepoteza, basi hana njia yoyote.

اسْتَجِيبُوا لِرَبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَكُم مِّن مَّلْجَإٍ يَوْمَئِذٍ وَمَا لَكُم مِّن نَّكِيرٍ ﴿٤٧﴾

47. Mwitikieni Mola wenu kabla haijafika siku isiyoepukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha kukataa.

فَإِنْ أَعْرَضُوا فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا إِنْ عَلَيْكَ إِلَّا الْبَلَاغُ وَإِنَّا إِذَا أَذَقْنَا الْإِنسَانَ مِنَّا رَحْمَةً فَرِحَ بِهَا وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَإِنَّ الْإِنسَانَ كَفُورٌ ﴿٤٨﴾

48. Na wakipuuza, basi hatukukupeleka uwe mwenye kuwalinda. Si juu yako ila kufikisha tu. Na hakika tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.

لِّلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ يَهَبُ لِمَن يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَن يَشَاءُ الذُّكُورَ ﴿٤٩﴾

49. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume.

أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا وَيَجْعَلُ مَن يَشَاءُ عَقِيمًا إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ ﴿٥٠﴾

50. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.

MWENYE HASARA NI YULE ALIYEJIHASIRI MWENYEWE

Aya 44 – 50

MAANA

Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, hana walii baada yake.

Mwenye kufuata njia ya upotevu kwa uchaguzi wake mbaya, basi atakuwa ni katika wapotevu. Wala hakuna wa kumlaumu ila yeye mwenyewe. Ambaye Mwenyezi Mungu amemuhizi hawezi kupata wa kumuokoa na hizaya hii.

Na utawaona madhalimu watakapoiona adhabu watasema: Je, ipo njia ya kurudi?

Walijikuza, wakafanya kiburi na kutakabari katika maisha ya dunia, lakini watakapofufuliwa wakiwa dhalili, watanyenyekea na watatafuta njia ya kuokoka na adhabu au kurudi duniani mara nyingine.

Hivi ndivyo walivyo mataghuti, wanajikuza ikiwa hakuna nguvu ya kuwarudi na wananyewa ikiwadhihirikia dalili yake.

Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho.

Wataukabili moto kwa matendo yao, wataichungulia Jahannam wakiwa wanatetemeka kwa hofu kuu, na hapo mwanzo walikuwa wakiifanyia mzaha.

Na walioamini watasema: Hakika waliopata hasara ni hao waliohasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! Hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya kudumu.

Waumini watayasema haya watakapowaona wakosefu wakisukumwa kwenye mwisho wa matendo yao, watamshukuru Mwenyezi Mungu aliyewaokoa na hizaya hii. Umetangulia mfano wake katika Juz. 23 (39:15).

Wala hawatakuwa na walii wa kuwanusuru asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Sharti la kwanza la walii (mlinzi) atakayeweza kusaidia, ni kuwa yeye mwenyewe awe na nguvu za kujikinga na kujisadia au kumsadia mwingine. Siku hiyo hakutakuwa na yeyote atakayekuwa na uwezo au nguvu.

Na ambaye Mwenyezi Mungu amemepoteza, basi hana njia yoyote ya kuokoka na moto.

Hapa tutaufasiri upotevu kwa maana ya moto, kwa sababu mfumo wa maneno unaishiria hilo; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Juz. 24 (40:34): “Kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza yule aliyepita kiasi mwenye shaka.” Yaani anamwadhibu.

Mwitikieni Mola wenu kabla haijafika siku isiyoepukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha kukataa

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewakalifisha waja yale yaliyo na manufaa kwao na heri yao, akawapa uwezo wa kuyatekelza yale aliyowakalifisha, akawapa muda wa kuyatenda na kutubia na akwahadharisha na matokeo ya kupuuza na uzembe – hakumwachia yeyote hoja ya kukimbilia siku ile ambayo mtu hataweza kurudishwa kwenye maisha yake ya kwanza wala hataweza kuyakana yaliyofanywa na mikono yake.

Na wakipuuza, basi hatukukupeleka uwe mwenye kuwalinda. Si juu yako ila kufikisha tu.

Maana yako wazi. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; kama vile: Juz. 5 (4:80) na Juz. 7(6:107).

Na hakika tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.

Makusudio ya rehema ni neema; kama vile afya na mali, na ovu ni balaa; kama vile ufukara na maradhi. Ama Makusudio ya mtu ni wengi katika wao sio kila mtu; vinginevyo ingelikuwa mtu hana taklifa yoyote, ikiwa ndio hivyo alivyo; kama tulivyobainisha katika Juz.13 (14:32-34).

Maana ni kuwa mjinga mwenye hasara huwa anafurahi kwa starehe za dunia akizipata na anakufuru akikosa kitu, hata kama ni kwa rai yake mbaya na matamanio ya nafsi yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 12 (11:9-10).

Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apen- davyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.

Hakuna mwenye shaka kwamba mtu hana hiyari wala uweza wowote wa kupata watoto wa kike tu au wa kiume tu au mchanganyiko. Ni Mwenyezi Mungu tu ndiye mwenye uwezo wa kumpa mtu watoto wa kike, wa kiume, mchanganyiko au kumfanya asizae kabisa. Mpaka sasa bado madaktari hawajaweza kutibu utasa kwa mwanamume au kwa mwanamke. Waliloweza ni kuchukua mbegu za mwanamume mwingine, bila ya kufanyika tendo la kujamiaana, na kuzitia kwa mke wa mume tasa.

Tumeweka mlango maalum wa hilo katika kitabu chetu Al-islamu walhay-at (Uislamu na maisha) na tukatoa fatwa ya kuharamisha hilo na kwamba mtoto atakayezaliwa katika njia hiyo hawezi kuwa wa mume, kwa ijimai, na atakuwa ni wa mama.

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ ﴿٥١﴾

51. Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi, au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humletea wahyi ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا مَا كُنتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٢﴾

52. Na hivyo ndivyo tulivyokupa roho kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumeifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunamwongoza tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoza kwenye njia iliyonyooka.

صِرَاطِ اللَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ أَلَا إِلَى اللَّـهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ ﴿٥٣﴾

53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Ehe! mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.

SURA YA MAWASILIANO BAINA MWENYEZI MUNGU NA MITUME WAKE

Aya 51 – 53

MAANA

Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi, au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humletea wahyi ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.

Maneno ya Mwenyezi Mungu yana maana nyingi; miongoni mwayo ni haya yafuatayo:

Kadha yake na kadari yake: “Na lau si neno lilikwishatangulia kutoka kwa Mola wako.” Aya 45

Kuuumba:

إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّـهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِّنْهُ ﴿١٧١﴾

“Hakika Masih Isa bin Maryamni Mtume wa Mwenyezi Mungu ni neno lake tu alilompelekea Maryam, Juz. 6 (4:171)

Haki:

وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ﴿٤٠﴾

“Na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu.” Juz. 10 (9:40).

Ulimwengu aliouleta kwa neno

كُن ﴿٨٢﴾

“kuwa” Juz. 23 (36:82)

Ilhamu kama inavyoelezewa kwenye Aya hii tuliyo nayo: “kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi.”

Maneno yanayosikiwa:

أَفَتَطْمَعُونَ أَن يُؤْمِنُوا لَكُمْ وَقَدْ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَسْمَعُونَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ يُحَرِّفُونَهُ مِن بَعْدِ مَا عَقَلُوهُ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿٧٥﴾

“Je mnatumaini ya kwamba wataamini na hali baadhi yao walikuwa wanasikia maneno ya Mwenyezi Mungu kisha wanayabadili baada ya kuwa wameyafahamu na hali wanajua? Juz. 1 (2:75).

Maneno haya ndiyo anayoyasikia Mtume nyuma ya pazia au kupelekewa mjumbe.

Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja njia tatu za kuzungumza kwake Mwenyezi Mungu na mitume na namna ya kuwasiliana nao:

1. Kuyaingiza maana katika moyo wa Mtume moja kwa moja bila ya kuweko kati chochote. Hii ndiyo iliyokusudiwa katika kauli yake: ‘Ila kwa wahyi’

2. Kuumba Mwenyezi Mungu maneno, kama anavyoumba vitu vingine na kuyasikia mtume nyuma ya pazia; yaani bila ya kumuona mzungumzaji. Ndio makusudio ya kauli yake:

وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا ﴿١٦٤﴾

“Na Musa akanena na Mwenyezi Mungu maneno.” Juz. 6 (4:164).

3. Kumpeleka Mwenyezi Mungu (s.w.t) Malaika kwa Mtume wake, atakayemfikishia risala ya Mola wake. Mula Sadra anasema katika Asfar: “Usije ukadhani Mtume(s.a.w. w ) alipokea maneno ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Jibril kama unavyosikia wewe kutoka kwa Mtume, au kusema kuwa Mtume(s.a.w. w ) alikuwa akimwiga Jibril.”

Hakuna mwenye shaka kuwa hakuna anayedhania au kusema hivi isipokuwa mjinga tu. Kwa sababu Jibril aliyomfikishia Muhammad(s.a.w. w ) ni maneno ya Mwenyezi Mungu hasa na Mtume(s.a.w. w ) akayaelewa kiuhakika wake.

Kwa hiyo basi kule kujua Mtume maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ndio maneno ya Mwenyezi Mungu, na maneno ya Mwenyezi Mungu ndio kujua Mtume.

Na hivyo ndivyo tulivyokupa roho kwa amri yetu.

Makusudio ya roho hapa ni Qur’an, kwa sababu hiyo ni uhai wa roho na mwili vile vile. Imam Ali(a.s ) anasema:“Kitabu cha Mwenyezi Mungu mnaona kwacho, mnatamka kwacho na manasikia kwacho”

Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala imani.

Makusudio ya Kitabu ni Qur’an na imani ni sharia ya Mwenyezi Mungu ambayo ameibainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa Nabii wake mtukufu baada ya kumchagua Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa risala yake. Wametofautiana katika tafsiri ya Aya hii kwenye kauli ambazo Razi ameishilizia tano. Yenye nguvu zaidi – kama tuonavyo – ni kauli ya Sheikh Ismail Haqqi, katika Tafsir Ruhul-bayan, ninamnukuu:

“Makusudio ya imani ni ufafanuzi uliokuja kwenye Qur’an ambao akili hauwezi kuupata, sio ile imani ambayo inakuwa kwenye akili na maarifa. Kwa sababu uzoefu wa Mtume(s.a.w. w ) hauna shaka.

Wamekongamana watu wa Usul – kwenye maarifa ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake – kwamba mitume walikuwa ni waumini kabla ya wahyi, wakiwa wamehifadhika (maasumu) na madhambi makubwa na madogo ambayo yangeliweza kuwafanya watu wawakimbie kabla na baada ya utume, zaidi ya kwamba hawakuwa makafiri.”

Lakini tumeifanya hiyo Qur’ankuwa ni Nuru ambayo kwayo tunamwongoza tumtakaye katika waja wetu ambao wametafuta uongofu kwa nia safi na wakaitafuta haki kwa haki. Ama yule aliyeasi na akafanya jeuri, Mwenyezi Mungu anaachana naye:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ ﴿٣﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu hamwongozi aliye mwongo kafiri.” Juz. 23 (39:3).

Na hakika wewe unaongoza kwenye Njia Iliyonyooka, njia ya Mwenyezi Mungu.

Nabii(s.a.w. w ) anatoa mwito wa Uislamu, dini ya Mwenyezi Mungu na njia yake iliyonyooka. Mwenye kufuata njia hii atakuwa amefuata njia ya wazi itakayompeleka kwa Mwenyezi Mungu na atasalimika na mwisho mbaya.

Ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Ehe! mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.

Mwito wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio njia ya kueleka kwa Mfalme wa ulimwengu Ambaye atawakusanya Siku isiyo na shaka. Basi mwenye kuusikiliza mwito wa Mtume na akauitikia, kesho atakuwa pamoja na wakweli na manabii.

Hao ndio marafiki wazuri. Na mwenye kuuacha, akajiweka mbali nao, atakuwa katika Jahannam na rafiki yake shetani.

MWISHO WA SURA YA ARUBAINI NA MBILI: SURAT ASH-SHURA