TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 26475
Pakua: 2631


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 26475 / Pakua: 2631
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

25

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

نَحْنُ خَلَقْنَاكُمْ فَلَوْلَا تُصَدِّقُونَ ﴿٥٧﴾

57. Sisi tumewaumba; basi mbona hamsadiki?

أَفَرَأَيْتُم مَّا تُمْنُونَ ﴿٥٨﴾

58. Je, mnaiona mnayoitoneza?

أَأَنتُمْ تَخْلُقُونَهُ أَمْ نَحْنُ الْخَالِقُونَ ﴿٥٩﴾

59. Je, mnaiumba nyinyi, au tunaiumba Sisi?

نَحْنُ قَدَّرْنَا بَيْنَكُمُ الْمَوْتَ وَمَا نَحْنُ بِمَسْبُوقِينَ ﴿٦٠﴾

60. Sisi tumewawekea mauti. Na Sisi hatushindwi,

عَلَىٰ أَن نُّبَدِّلَ أَمْثَالَكُمْ وَنُنشِئَكُمْ فِي مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٦١﴾

61. Kuwaleta wengine badala yenu na kuwaumba nyinyi kwa umbo msilolijua.

وَلَقَدْ عَلِمْتُمُ النَّشْأَةَ الْأُولَىٰ فَلَوْلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

62. Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, tena mbona hamkumbuki?

أَفَرَأَيْتُم مَّا تَحْرُثُونَ ﴿٦٣﴾

63. Je, Mnaona mnayolima?

أَأَنتُمْ تَزْرَعُونَهُ أَمْ نَحْنُ الزَّارِعُونَ ﴿٦٤﴾

74. Je, ni nyinyi mnayoyaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?

لَوْ نَشَاءُ لَجَعَلْنَاهُ حُطَامًا فَظَلْتُمْ تَفَكَّهُونَ ﴿٦٥﴾

75. Tungelitaka tungeliyafanya mapepe, mkabaki mnastaajabu,

إِنَّا لَمُغْرَمُونَ ﴿٦٦﴾

66. Hakika sisi tumegharamika.

بَلْ نَحْنُ مَحْرُومُونَ ﴿٦٧﴾

67. Bali sisi tumenyimwa.

أَفَرَأَيْتُمُ الْمَاءَ الَّذِي تَشْرَبُونَ ﴿٦٨﴾

68. Je, mnayaona maji mnayoyanywa?

أَأَنتُمْ أَنزَلْتُمُوهُ مِنَ الْمُزْنِ أَمْ نَحْنُ الْمُنزِلُونَ ﴿٦٩﴾

69. Je, ni nyinyi mnayoyateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?

لَوْ نَشَاءُ جَعَلْنَاهُ أُجَاجًا فَلَوْلَا تَشْكُرُونَ ﴿٧٠﴾

70. Tungelipenda tungeliyafanya ya chumvi kali. Basi mbona hamshukuru?

أَفَرَأَيْتُمُ النَّارَ الَّتِي تُورُونَ ﴿٧١﴾

71. Je, mnauona moto mnaouwasha?

أَأَنتُمْ أَنشَأْتُمْ شَجَرَتَهَا أَمْ نَحْنُ الْمُنشِئُونَ ﴿٧٢﴾

72. Ni nyinyi mliouumba mti wake au Sisi ndio Wenye kuuumba?

نَحْنُ جَعَلْنَاهَا تَذْكِرَةً وَمَتَاعًا لِّلْمُقْوِينَ ﴿٧٣﴾

73. Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa wenye kusikiliza.

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ ﴿٧٤﴾

74. Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

JE, MNAONA MAKULIMA MNAYOYAPANDA

Aya 57 – 74

MAANA

Sisi tumewaumba; basi mbona hamsadiki?

Waliamini na wakakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba, lakini wakakana na kukadhibisha kwamba wao baada ya mauti watarudishwa kwa ajili ya hisabu na malipo. La kwanza kwa itikadi, linawezekana ama la pili kwao ni muhali.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawarudi kuwa kuanza kuumba na kurudisha baada ya mauti ni hali moja tu, kulingana na uweza wa Mwenyezi Mungu; bali kurudisha ni rahisi zaidi. Kwani kuumba ni kuleta kitu kisichokuwepo kabisa, na kurudisha ni kukusanya viungo vilivyotawanyika.

Kwa hiyo basi inawalazimu moja ya mambo mawili: Ama muamini yote mawili au muyakate yote. Mwenye kuamini moja na akaacha jingine atakuwa amejipinga yeye mwenyewe. Hii inaitwa dalili ya kulazimiana baina ya vitu viwili, haiepukani na nyingine. Kwa hiyo moja inaitolea dalili nyingine kichanya na kihasi.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akapiga mifano ya kuumba kwake inayofahamisha uwezekano wa kuweko ufufuo; kama ifutavyo:-

1.Je, mnaiona mbegu ya uzazi mnayoitoneza? Je, mnaiumba nyinyi, au tunaimba Sisi?

Ni nani aliyewaumba kutokana na manii yenu kuwa mtu aliyekamilika viungo vyake na silika yake. Ni nyinyi au Mwenyezi Mungu? Mmeshusha manii katika mfuko wa uzazi wa mwanamke tu na kazi yenu ikaisha. Ni nani aliyeyageuza manii kuwa pande la damu nalo kuwa pande la nyama kisha kuwa mifupa na mifupa kuvikwa nyama n.k.? Ikiwa mtasema yote hiyo ni kazi ya asili ya maumbile peke yake, tutawauliza:

Ni nani aliyeyaleta hayo maumbile? Mkijubu kuwa yamejileta yenyewe, tutawauliza: Ni nani aliyempa mtu uhai, hisia na utambuzi? Mkisema ni hayo maumbile, tutawauliza: Hayo yana uziwi na upofu, na asiyekuwa nacho hawezi kutoa.

Mkiendelea kusema kuwa uhai umetokea kwenye maada bila ya makusudio, nasi tutawaambia kuwa maneno haya nayo yametokea bila ya makusudio. Na akili haikubali tafsiri yoyote ya maisha na nidhamu ya ulimwengu isipokuwa kwa sababu ya kiakili iliyofanya. Na haiwezekani kuweko sababu zizizokuwa na ukomo; vinginevyo kupatikana kusingekuwa na athari.

Sisi tumewawekea mauti.

Mwenye kumiliki mauti ndio huyo huyo anayemiliki uhai.

Na Sisi hatushindwi kuwaleta wengine badala yenu na kuwaumba nyinyi kwa umbo msilolijua.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) hashindwi, wala hapitwi na lolote; na yeye ni muweza wa kila jambo. Na kwa uweza wake amehamisha kukosekana kwenye kupatikana. Lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwabadilisha waasi kuwa watu wengine wanaomtii, angelifanya hilo wala hakuna wa kulizuia analolitaka.

Hapa kuna makemeo na kiaga kwa yule anayepinga mwito wa haki:

وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم ﴿٣٨﴾

“Na mkigeuka atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.”

Juz. 26 (47:38).

Na bila ya shaka mlikwishajua umbo la kwanza, tena mbona hamkumbuki?

Mmejua kuumbwa kwenu kusikotokana na kitu chochote; sasa je tutashindwa kuvikusanya viungo vyenu na kuvirudisha kama vilivyokuwa baada ya baada ya kutawanyika?

Tafsiri fasaha zaidi ya Aya hii ni kauli ya Imam Ali(a.s) : “Nashangazwa na yule anayepinga ufufuo wa mwisho na hali anaona ufufuo wa kwanza!”

2.Je, Mnaona mnayolima? Je, ni nyinyi mnayoyaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?

Mtu anatafuta mbegu, analima anapanda na kumwagilia maji, hilo halina shaka. Lakini hiyo mbegu, miche, maji, ardhi na mengineyo, kama jua na hewa yametoka wapi? Wakisema; yametokana na kitendo cha maada isiyokuwa na akili, nasi tutawajibu: Kauli yenu hiyo inatokana na asiyekuwa na akili.

Tungelitaka tungeliyafanya mapepe, mkabaki mnastaajabu, Mkisema: Hakika sisi tumegharimika.

Yaani tumetaabika sana na kugharimika kutayarisha mashamba na wala hatukunufaika na chochote. Na mtaendelea kusema: Bali sisi tumenyimwa riziki. Hakuna kitu kinachotia uchungu kwenye nafsi kuliko kuhisi kunyimwa.

3.Je, mnayaona maji mnayoyanywa? Je, ni nyinyi mnayoyateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashiria kuwa Yeye ndiye aliyeleta maumbile yanayosababisha mvua. Maana ni kuwa maji haya, ambayo ni asili ya uhai, na ambayo mtu hana budi nayo kwa hali yoyote, ni nani aliyesababisha kupatikana kwake na kuyapangilia? Ni nyinyi au ni yule ambaye ameumba kila kitu na akakipangilia?

Mwenyezi Mungu amezindua, kwenye Aya nyingi. kwamba Yeye atafufua wafu; kama anavyoifufua ardhi kwa mvua:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٣٩﴾

“Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi imetulia, lakini tunapoiteremshia maji mara unaiona inashtuka na kututumka. Bila ya shaka aliyeihuisha ardhi ndiye atakayehuisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza juu ya kila kitu.” Juz. 24 (41:39).

Tungelipenda tungeliyafanya ya chumvi kali. Basi mbona hamshukuru?

Neno chumvi kali tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu ujaj lenya maana ya chumvi kali iliyofikia kufanya kitu kiwe kichungu.

Maana ni kuwa lau Mwenyezi Mungu angelitaka angeliyafanya maji kuwa na chumvi sana yasiyoweza kuwa na manufaa ya kunywewa wala kulimi- wa, lakini ameyafanya tamu baridi, kwa ajili ya kuwahurumia. Pamoja na kuwa neema hii inataka kushukuriwa, lakini bado Mwenyezi Mungu anamlipa mwenye kushukuru.

4.Je, mnauona moto mnaouwasha?

Moto ni neema sawa na maji. Lau si huo mtu asingeliweza kupiga hata hatua moja katika maisha yake; mpaka siku yake ya mwisho angelibakia akiishi na wanyama mwituni.

Ni nyinyi mliouumba mti wake au Sisi ndio Wenye kuuumba?

Moto unasabishwa na vitu mbali mabali; miongoni mwavyo ni kuni, makaa ya mawe, mafuta umeme na mengineyo watakayoyagundua wataalamu baadae au wasiyagundue, Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi.

Umetajwa mti katika Aya kwa njia ya kufananisha tu. Wafasiri wamesema kuwa waarabu walikuwa wakipekecha vijiti kutoa moto, ndio maana Mwenyezi Mungu akaleta mfano unaoendana na maisha ya wakati huo.

Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa wenye kusikiliza.

Neno kusikiliza tumelifasiri kutokana na neno muqwin ambalo wafasiri wametofatiana katika tafsiri yake. Tabari anasema: “Wametofautiana wafasiri katika maana ya neno muqwin. Kuna waliosema ni wasafiri na waliosema ni wasikilizaji.”

Sisi tumechagua wenye kusikiliza kwa vile moto unawanufaisha wasafiri na wasiokuwa wasafiri.

Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wakikusudiwa watu wote. Maana ni mtukuze na umtakase Muumba Mkuu na kila yasiyofanana na ukuu wake. Waislamu wanaisoma tasbihi katika rukui zao. Ama kwenye sujudi zao wanasoma tasbihi iliyoko (87:1).

فَلَا أُقْسِمُ بِمَوَاقِعِ النُّجُومِ ﴿٧٥﴾

75. Basi naapa kwa maanguko ya nyota.

وَإِنَّهُ لَقَسَمٌ لَّوْ تَعْلَمُونَ عَظِيمٌ ﴿٧٦﴾

76. Na hakika bila ya shaka hiki ni kiapo kikubwa, lau mngelijua!

إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ ﴿٧٧﴾

77. Hakika hii bila ya shaka ni Qur’an Tukufu,

فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ ﴿٧٨﴾

78. Katika Kitabu kilichohifadhiwa.

لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ ﴿٧٩﴾

79. Hapana akigusaye ila waliotakaswa.

تَنزِيلٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٨٠﴾

80. Ni uteremsho unaotoka kwa Mola wa walimwengu wote.

أَفَبِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَنتُم مُّدْهِنُونَ ﴿٨١﴾

81. Je, ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayafanyia udanganyifu?

وَتَجْعَلُونَ رِزْقَكُمْ أَنَّكُمْ تُكَذِّبُونَ ﴿٨٢﴾

82. Na mnafanya riziki yenu kuwa mnakadhibisha?

فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ ﴿٨٣﴾

83. Basi mbona itakapofika kwenye koo.

وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ ﴿٨٤﴾

84. Na nyinyi wakati huo mnatazama,

وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾

85. Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi, lakini hamuoni,

فَلَوْلَا إِن كُنتُمْ غَيْرَ مَدِينِينَ ﴿٨٦﴾

86. Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka,

تَرْجِعُونَهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٨٧﴾

87. Kwa nini hamuirudishi, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

فَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٨٨﴾

88. Basi akiwa miongoni mwa waliokaribishwa.

فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ ﴿٨٩﴾

89. Itakuwa ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.

وَأَمَّا إِن كَانَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٩٠﴾

90. Na akiwa katika watu wa kuume.

فَسَلَامٌ لَّكَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٩١﴾

91. Basi ni Salama kwako uliye miongoni mwa watu wa kuume.

وَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُكَذِّبِينَ الضَّالِّينَ ﴿٩٢﴾

92. Na ama akiwa katika waliokadhibisha wapotovu,

فَنُزُلٌ مِّنْ حَمِيمٍ ﴿٩٣﴾

93. Basi karamu yake ni maji yanayochemka,

وَتَصْلِيَةُ جَحِيمٍ ﴿٩٤﴾

94. Na kutiwa Motoni.

إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ حَقُّ الْيَقِينِ ﴿٩٥﴾

95. Hakika hii ndiyo haki yenye yakini.

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ ﴿٩٦﴾

96. Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

HAPANA AIGUSAYE ILA WALIOTAKASWA

Aya 75 – 96

MAANA

Basi naapa kwa maanguko ya nyota, na hakika bila ya shaka hiki ni kiapo kikubwa, lau mngelijua!

LUGHA

Wafasiri wengi wamesema kuwa herufi la hapa ni ziyada kiirabu ya nahau; kama ilivyo katika Aya ya mwisho ya Juzuu hii tuliyo nayo (57:29) na “Nini kilichokuzuia kumsujudia.” Juz. 8 (8:12). Wengine wamesema kuwa herufi La hapa ni ya asili, na kwamba maana yake ni ‘Siapi,’ kwa vile jambo liko wazi nilislohotajia kiapo.

Kauli sahii ni ya mwanzo, kwa dalili ya kuli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na hakika bila ya shaka hiki ni kiapo kikubwa, lau mngelijua!” inayofahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ameapa hasa.

Katika Juz. 23 (37:1), tumesema kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kuapia chochote katika viumbe wake, kwa sababu kila kiumbe kinafahamisha kuweko muumba, ujuzi wake na hikima yake; sikwambii tena ikiwa kinachoapiwa athari yake inaonyesha zaidi mpangilio wa ulimwengu na nidhamu yake na kuhifadhika kwake na kubakia; kama vile kuwekwa nyota sehemu zake na mpangilio wake; kiasi ambacho lau itasogea moja tu kutoka sehemu yake kwa nafasi ya unywele mmoja tu, basi kila kitu kitaharabika. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘lau mngelijua!,’ inaashiria kuwa watu wengi hawajui hakika hii; hasa wale wa zama za mwanzomwanzo.

UISLAMU NA WANAFIKRA WAKUU WA ULAYA

Hakika hii bila ya shaka ni Qur’an Tukufu.

Ndio! Hii ni Qur’an tukufu inayotosheleza miongozo na dalili zote, ni ponyo la ugonjwa wa ujinga na upotevu, inaongoza kwenye vituo vya heshima na salama na ni mkombozi wa vifungo vya dhulma na utumwa.

Siri ya sifa zote hizi na nyinginezo ni kuwa Qur’an inatekeleza mahitajio yote ya maisha, na inafungamanisha dini na matendo, katika maisha ya dunia, kwa ajili ya maisha mazuri ya usawa yasiyokuwa na matatizo wala uadui. Hata wema wa Akhera pia hawezi kuupata ila mwenye ikhlasi na akafanya matendo mema. Kabisa! Hakuna njia ya kwenda kwa Mwenyezi Mungu wala kuokoka isipokuwa kwa matendo yenye kunufaisha:

فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ﴿١٧﴾

“Ama povu linakwenda bure; ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi.” Juz. 13 (13:17).

Ndio maana Waislamu wamekongamana kwa kauli moja kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuweka sharia wala hataweka sharia ila kwa heri ya mtu na masilahi yake, na kwamba haiwezekani kabisa kuweka sharia itakayokuwa na madhara kwa mtu yoyote vyovyote awavyo.

Ikiwa itadaiwa kuwa ni sharia ya Qur’an na haiendani na misingi hii, basi hiyo itakuwa imetokana na ujinga wa wajinga au wasingiziaji wanaobandika mambo. Aya zinazofahamisha hivyo zinahisabika kwa makumi; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:

Kauli yake Mwenyezi Mungu kupitia Nabii wake Shua’yb:

إِنْ أُرِيدُ إِلَّا الْإِصْلَاحَ ﴿٨٨﴾

“Sitaki ila kutengeneza.” Juz. 12 (11:88).

مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ ﴿٦﴾

“Mwenyezi Mungu hapendi kuwatia katika taabu lakini anataka kuwatakasa na kutimiza neema yake juu yenu.” Juz.6 (5:6).

إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٤٣﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu, kwa watu, ni Mpole, Mwenye kurehemu.” Juz. 2 (2:143).

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٠﴾

“Basi uelekze uso wako sawa sawa kwenye dini – ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini ya sawa sawa, lakini watu wengi hawajui.” Juz. 21 (30:30).

Huu ndio uhakika wa Uislamu na uhalisia wake, ulio katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na ujuzi wake. Hakuna kitu ndani yake isipokuwa kile anachokihitajia mtu kwa silika yake na maumbile safi aliyozaliwa nayo yanayomtofautisha na viumbe vingine vyote, lakini sio kujiingiza kwenye tamaa dhulma uchokozi n.k.

Hakika hii wameigundua wanafalsafa na wanafsihi wengi wa Ulaya. Wakautukuza Uislamu na wakamsifia Mtume(s.a.w. w ) ; si kwa lolote ila ni kwa msukumo wa heri, haki na uadilifu.

Lau tungelikuwa na nafasi tungelitaja kauli zao nyingi, lakini yasiyowezakana yote hayaachwi yote. Tutachagua kauli za baadhi yao; kama vile: Mjarumani Goeth, Mfaransa Amrtin, Mrusi Tolstoy na Mwingereza Bernad Show. Wote hawa kama unavyooona wanatofautiana katika uta- maduni, mwelekeo na jinsia zao.

Goethe alisoma Qur’an, akatambua yaliyomo ndani yake na akaitukuza. Alifanya hafla usiku wa Laylatul-qadr ambao Qur’an iliteremshwa. Alisoma Historia ya Mtume(s.a.w. w ) , akatunga kasida ya Muhammad na akaandika tamthilia ya Muhammad(s.a.w. w ) .

Miongoni mwa kauli zake ni: “Ikiwa Uislamu ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu na sio kwenye hawa na matamanio, basi tuishi kwenye Uislamu na tufeni kwenye Uislamu.”

Amrtin, Mshairi mkubwa wa Kifaransa, anasema: “Maisha ya Muhammad(s.a.w. w ) yote yanafahamisha kuwa hakudhamiria kudanganya au kuishi kwenye ubatilifu… Hakika yeye ni mwongozi wa watu kwenye akili na ni muasisi wa dini isiyokuwa na uzushi.”

Tolstoy, mwanafalsafa ya binadamu kutoka Urusi, anasema: “Katika mambo yasiyo na shaka ni kuwa Muhammad ameihudumia jamii kwa huduma tukufu. Inatosha kuwa ni fahari, kwamba yeye ameongoza mamia ya mamilioni kwenye nuru ya haki utulivu na amani na akaupa ubinadamu njia ya maisha. Hiyo ni kazi kuu ambayo haiwezi isipokuwa yule aliyepewa nguvu na ilhamu kutoka mbinguni.”

Mwanafisihi wa kimataifa kutoka Uingerza, Bernad Show anasema: “Ni lazima isemwe kuwa Muhammad ni mwokozi wa mtu… Mimi ninaamini kwamba lau hivi sasa angelitawala ulimwengu mtu mfano wake, angelifaulu kutatua matatizo kwa namna ambayo ingeuleta ulimwengu kwenye amani na raha…Hakika Muhammad ni mkamilifu zaidi ya watu waliopita na watakaokuja, wala haifikiriwi kupatikana mfano wake katika watakaokuja.”

Kauli ya Show kuwa Muhammad ni mkamilifu zaidi ya watu waliopita na watakaokuja, inamaanisha kuwa risala ya Muhammad(s.a.w. w ) haifikiwi na risala ya manabii waliotangulia; hata Isa na Ibrahim.

Na aliposema: “Wala haifikiriwi kupatikana mfano wake katika watakaokuja.” Maana yake ni kuwa hakuna yeyote baada ya Muhammad(s.a.w. w ) anayeweza kuleta jipya lenye faida au manufaa zaidi ya alilolileta Muhammad.

Vile vile anamaanisha kuwa mwito wa Muhammad hauhitajii dini wala sharia au nidhamu nyingine; bali hizo nyingine ndizo zinauhitajia.

Kila mmoja wetu anajua kuwa Bernad Show ni katika wanafikra wakubwa wa ulaya aliyetokea katika karne ya ishirini, karne ya maendeleo ya atom na anga; na kwamba ushahidi wake huu ni matokeo ya utafiti mrefu, fikra ya kina na upembuzi yakinifu.

Ushuhuda huu wa Bernad ni ibara au tafsiri nyingine ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾

“Na hatukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote.” Juz. 17 (21:107).

Yaani walimwengu wote kila wakati na kila mahali. Vile vile tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ﴿٤٠﴾

“Bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa mitume.” Juz. 22 (33:40).

Vile vile ushahidi wa Show, ni dalili mkataa ya ukweli wa waislamu katika itikadi yao, kwamba Muhammad ni mkamilifu zaidi ya watu waliopita na watakaokuja, wala haifikiriwi kupatikana mfano wake katika watakaokuja; kama anavyosema.

Je, baada ya hayo yote wanasemaje vijana wanokana dini ya mababa na mababu zao, kuhusiana na kauli ya Bernad Show? Je, wao wana ujuzi zaidi, wana hamu zaidi ya ubinadamu kuliko yeye au wao wanazungumza kwa kutumia fikra za maadui wa Uislamu na ubinadamu bila ya kujitambua?

Katika Kitabu kilichohifadhiwa.

Wametofautiana katika kuhifadhiwa Kitabu. Kuna waliosema kimehifad- hiwa na mchanga na vumbi; kama ilivyoelezwa katika Tafsir Attabari. Wengine wakasema kimehifadhiwa katika Lawh mahfudh.

Tuonavyo sisi ni kuwa hakuna haja ya mzozo huu, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebaainisha maana ya hifadhi hii kwa kusema:

Hapana akigusaye ila waliotakaswa. Ni uteremsho unaotoka kwa Mola wa walimwengu wote.

Yaani Qur’an ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu sio kutoka kwa shetani, wala si uchawi au ngano za watu wa kale; kama wanavyodai walahidi.

Wameafikiana wana fikh wa madhehbu kuwa ni haramu kugusa maandishi ya Qur’an isipokuwa kwa aliyetwahara mwenye udhu. Wakatofautiana katika kuiandika na kuisoma kwa asiyekuwa twahara.

Hanafi wamesema haifai kuiandika, lakini inajuzu kuisoma kwa moyo. Shafii wakasema haijuzu kuiandika wala kuisoma isipokuwa kama ni kwa kukusudia dhikri; kama kusoma Bismillah kwenye chakula. Maliki nao wakasema haijuzu kuiandika, lakini inajuzu kusoma kwa moyo au kwa kuiangalia. Hambali wamesema haijuzu kuiandika, lakini inajuzu kuichukua kwa kuiziba na kizuizi.

Shia Imamiyah wamesema si haramu kwa mwenye janaba kusoma Qur’an na inajuzu kuandika, isipokuwa sura nne za Azaim, zenye sijda ya wajib, ambazo ni: Alaq. Annajm, Alif lamim Sajjda na Sajda (96, 53, 41 na 32).

Je, ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayafanyia udanganyifu?

Makusudio ya maneno hapa ni Qur’an. Kauli hii inaelekezwa kwa wanafiki ambao walifanya udanganyifu; wakadhihirisha kuikubali Qur’an na nyoyoni wanaikataa.

Na mnafanya riziki yenu kuwa mnakadhibisha?

Makusudio ya riziki hapa ni neema na kukadhibisha ni kuikataa. Maana ni kuwa Qur’an ni neema kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu enyi wadanganyifu, vipi mnaikabili kwa kuikana na kuikufuru.

Kundi katika wafasiri wamesema: mvua iliponyesha walikuwa wakisema: hii ni kazi ya maumbile, kwa hiyo ikawa huko ni kukufuru neema ya Mwenyezi Mungu, na ndio wakateremshiwa Aya hii.

Lakini kauli hii iko mbali na maana. Kwa sababu mazungumzo yanahusiana na Qur’an si mvua.

Basi mbona itakapofika kwenye koo, na nyinyi wakati huo mnatazama!

Itakapofika kwenye koo ni roho. Hilo limefahamika kutokana na mfumo wa maneno unavyokwenda. Nyinyi wanaambiwa waliokaribu na anayekata roho, awe ni katika jamaa zake au la.

Maana ni mtakuwaje nyinyi wanafiki mmoja wenu akifikiwa na mauti na roho ikafika kooni huku mnamwangalia mkitamani aendelee kuishi, je mtakuwa na uwezo na kumrudishia uhai na afya yake?

Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi, lakini hamuoni.

Naye ni huyo anayekata roho. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anayajua yanayompitia mwenye kukata roho, na jinsi nyinyi mnavyoshindwa kumwokoa na mnavyoona uchungu kumkosa, lakini nyinyi hamjui kuwa Mwenyezi Mungu yuko kila mahali kwa ilimu yake na uweza wake.

Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka, kwanini hamuirudishi, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

Ikiwa nyinyi mko huru, kama mnavyodai, na hamtaulizwa lolote wala hakuna yoyote anayeweza kuwalazimisha kitu, basi kwanini hamyazuii mauti na mkazirudisha roho kwenye mili yenu? Kwa sababu mnavyomaanisha ni kuwa Mwenyezi Mungu hamiliki mauti, uhai, ufufuo wala hisabu.

Basi akiwa miongoni mwa waliokaribishwa, itakuwa ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.

Mwanzoni mwa sura hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewagawanya watu siku ya kiyama kwenye aina tatu, waliotangulia wenye kukaribishwa, watu wa kuume na wa kushoto.

Katika Aya hii anataja kuwa mwenye kukata roho akiwa ni katika waliotangulia basi atakuwa mwenye amani na neema ya milele. Aliyowaandalia wenye kutangulia ameyataja katika Aya ya 12 na zinazofuatia katika sura hii tuliyo nayo.

Na akiwa katika watu wa kuume, basi ni Salama kwako uliye miongoni mwa watu wa kuume.

Akiwa mkata roho ni katika aina ya pili ambayo ni watu wa upande wa kuume, basi malaika watampa bishara ya salama na raha. Mwenyezi Mungu ameyataja aliyowaandalia hawa katika Aya 27 na zinazofutia katika sura hii tuliyo nayo.

Na ama akiwa katika waliokadhibisha wapotovu, basi karamu yake ni maji yanayochemka, na kutiwa Motoni.

Anayekata roho akiwa ni katika aina ya tatu ambao ni watu wa kushoto, basi makazi yake ni Jahannam ambayo ni makazi mabaya kabisa. Maandalizi ya hawa, Mwenyezi Mungu ameyataja katika Aya 41 na zinazofuatia katika sura hii tuliyo nayo.

Hakika hii ndiyo haki yenye yakini isiyokuwa na shaka yoyote. Katika baadhi ya vitabu vya kisufi imeelezwa kuwa utambuzi uko mafungu matatu: Utambuzi wa ilimu ya yakini; kama kujua kuweko moto kutokana na moshi unaofuka, kujua kwa jicho la yakini; kama kuuona moto wenyewe hasa na kujua kwa haki ya yakini; kama kuungua kwenye huo moto.

Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Aya ya 75 ya sura hii.

MWISHO WA SURA YA HAMSINI NA SITA: SURAT AL-WAAQIA

26

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Sura Ya Hamsini Na Saba: Al-Hadid. Imeshuka Madina. Ina Aya 29.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

سَبَّحَ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١﴾

1. Vinamsabihi Mwenyezi Mungu vilivyo katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢﴾

2. Yeye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Anahuisha na anafisha. Na Yeye ni Mwenye uweza wa kila kitu.

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾

3. Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhahiri na wa Batini, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٤﴾

4. Yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akastawi juu ya Arshi. Anayajua yanayoingia katika ardhi, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo. Naye yuko pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayoyatenda.

لَّهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿٥﴾

5. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake. Na mambo yote yanarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu.

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَهُوَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٦﴾

6. Huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku. Na Yeye ni Mwenye kuyajua yaliomo vifuani.

آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَأَنفِقُوا مِمَّا جَعَلَكُم مُّسْتَخْلَفِينَ فِيهِ فَالَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَأَنفَقُوا لَهُمْ أَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿٧﴾

7. Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyowafanyia nyinyi kuwa ni waangalizi wake. Basi walioamini miongoni mwenu, na wakatoa, wana malipo makubwa.

NDIYE WA MWANZO NA NDIYE WA MWISHO

Aya 1 – 6

MAANA

Katika Juz. 14 (16:49), Mwenyezi Mungu anasema: “Vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.”

Kumsabihi Mwenyzi Mungu na kumsujudia ni kukiri uweza wa Mwenyezi Mungu mtukufu na hikima yake. Kukiri huku kunakua katika hali mbili: Moja ni kwa lugha ya kusema na nyingine ni kwa lugha ya hali. Mtu huwa anatumia hali zote mbili, lakini viumbe vingine visivyoweza kutamka huwa vinasujudi na kusabihi kwa lugha ya hali. Kwa sababu hakuna kiumbe chochote isipokuwa kinafahamisha kuweko mwenye kukifanya na kukipa sura. Tazama Juz. 15 (15:44) kifungu cha ‘Kila kitu kinamsabihi.’

Katika vitabu vya sera, Hadith na Tafsiri imeelezwa kuwa Fatima binti wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa akifanya kazi zote za nyumbani yeye mwenyewe, akimuhudumia mumewe na watoto wake. Siku moja akamweleza baba yake hali yake, naye akaona athari ya juhudi yake kwenye mikono yake. Basi akamtaka ampatie mjakazi katika mateka wa vita ili amsaidie kazi za nyumbani.

Mtume akasema: sitakupa mjakazi na hali kuna mwingine anafunga tumbo lake kwa njaa. Kisha akaendelea kusema: Unaonaje nikikufahamisha jambo lilio na heri zaidi kuliko mjakazi – kusabihi Mwenyezi Mungu mara 33, kumhimidi mara 33 na kumfanyia takbira mara 34. Fatima akasema: Nimeridhia ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Tasbihi hii inajulikana kwa jina la Tasbih Zahra.

Yeye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Anahuisha na anafisha.

Kama kwamaba muulizaji ameuliza kwanini vikamsabihi Mwenyezi Mungu vilivyo katika ardhi na mbingu?Na Yeye ni Mwenye uweza wa kila kitu . Analolitaka hua na asilolitaka haliwi.

Yeye ndiye wa Mwanzo bila ya kuanza kulikokuwa kabla yake na kutoka kwake ndio chanzo cha kila kitu.Na ndiye wa Mwisho, bila ya kuweko na ukomo baada yake na kwake Yeye ndio mwisho wa kila kitu.

Naye ndiye wa Dhahiri kwa athari na vitendo sio kwa kuhisiwa.Na wa Batini, akili na dhana haziwezi kufikiria hakika yake; isipokuwa anadhihiri kwa athari zake.

Kwenye Nahjul-balagha imesemwa: “Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ameonyesha athari za mamlaka yake na ukuu wa ukubwa wake, zilizozubaisha mboni za macho kwa maajabu yake na kuzuia dhana za nafsi kujua hakika ya sifa zake... amekuwa karibu akawa mbali na amekua juu akawa chini. Kuwa kwake kumetangulia nyakati, na kupatikana kwake kumetangulia kukosekana, na ukale wake umetangulia kuanza.”

Naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.

Ni mjuzi wa kila kitu kwa vile ameumba kila kitu.

Yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akastawi juu ya Arshi.

Makusudio ya siku ni mikupuo, kustawi ni kutawala na arshi ni ufalme. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:54), 11 (10:3), 12 (11:7), 19 (25:59) na 21 (32:4).

Anayajua yanayoingia katika ardhi miongoni mwa hazina, mbegu na maji; hata milipuko ya mabomu ardhini wanayoilipua maadui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu, Mwenyezi Mungu anaijua hakika yake na atahri yake. Pia anajua lengo lake kuwa ni kutawala waja wa Mwenyezi Mungu na kuwawafanya wawanyenyekee na wakuze viwanda vya silaha.

Vile vile Mwenyezi Mungu anayajuana yanayotoka humo, ikiwemo mimea wadudu na maji. Hata mafuta pia Mwenyezi Mungu anajua yanatoka kwenye ardhi gani, mikono inayoyatoa, mashirika yanayoyapora na vita vinavyosababishwa nayo.Na yanayoteremka kutoka mbinguni, yakiwemo maji theluji, nuru na heri nyinginezo.

Pia amewajua wale waliokwenda kwenye mwezi ili waweze kupata nyenzo watakayoitumia kuhodhi baraka za mbinguni na kuwanyima waja wa Mwenyezi Mungu; sawa na walivyoifanyia ardhi na heri zake. Lakini Mwenyezi Mungu ambaye imetukuka hikima yake, aliwarudisha nyuma kwa visigino vyao kwenye jaribio la tatu na wakarudi utupu.

Na yanayopanda humo.

Vile vile Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua yanayoendelea kwenye anga za juu, hata ndege za ujajusi na zile zinazobeba makombora na setilaiti zinazozunguka juu ya ardhi kwa malengo ya kishetani; kama vile ujasusi, na ugaidi kwa walala hoi na kuwapora riziki zao.

Naye yuko pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayoyatenda. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake. Na mambo yote yanarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu.

Huu ni ukemeo na utisho kwa kila taghuti na dhalimu, kuwa matendo yake yamehifadhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba amewekwa rahani na atahisabiwa hisabu ya ndani na nzito na kuadhibiwa adhabu chungu.

Huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku. Na Yeye ni Mwenye kuyajua yaliomo vifuani.

Sayari zinataharaki na misimu inageuka, kuna msimu sehemu ya usiku inachukuliwa na mchana na mwingine mchana unachukuliwa na usiku na pia kuna siku unakuwa sawa usiku na mchana. Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3:27), 17 (22:61), 21: (31:29) na 22 (34:13).

وَمَا لَكُمْ لَا تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالرَّسُولُ يَدْعُوكُمْ لِتُؤْمِنُوا بِرَبِّكُمْ وَقَدْ أَخَذَ مِيثَاقَكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٨﴾

8. Na mna nini hata hamumwamini Mwenyezi Mungu na hali Mtume anawaita mumwamini Mola wenu? Naye amekwishachukua ahadi yenu, ikiwa nyinyi ni waumini.

هُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ عَلَىٰ عَبْدِهِ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ لِّيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ وَإِنَّ اللَّـهَ بِكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٩﴾

9. Yeye ndiye anayemteremshia mja wake Aya zinazobainisha wazi ili awatoe gizani muingie kwenye nuru. Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu ni Mpole, Mwenye kurehemu.

وَمَا لَكُمْ أَلَّا تُنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ أُولَـٰئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ أَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١٠﴾

10. Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu amewaahidi wema. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ ﴿١١﴾

11. Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu, na apate ujira mzuri.

TOENI KATIKA ALIVYOWAFANYA NI WAANGALIZI

Aya 7 – 11

MAANA

Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyowafanyia nyinyi kuwa ni waangalizi wake. Basi walio amini miongoni mwenu, na wakatoa, wana malipo makubwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehimiza kutoa na akapendekeza kwa mifumo mbali mbali. Akakemea na kumtishia kwa adhabu kali mwenye kufanya ubahili na akazuia. Miongoni mwa mifumo ya kuhimiza kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni Aya hii tuliyo nayo ambayo imeweka sawa imani ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kutoa.

Usawa huu unaashiria kwamba mwenye kufanya ubakhili na akazuia basi amemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake kimatendo; hata kama atawamini kinadharia. Vile vile Aya inaashiria kwamba wanachotoa matajairi sio mali yao; isipokuwa wao ni mawakala tu.

Imepokewa riwaya kutoka kwa sahaba mtukufu Abu dharr, kwamba yeye siku moja alitoka na Mtume kuelekea upande wa Uhud. Mtume(s.a.w. w ) akamwambia: Unauona mlima huu ewe Abu dharr? Akasema: ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mimi sipendi kuwa na dhahabu mfano wake, kisha nitoe katika njia ya Mwenyezi Mungu na nife nibakishe kareti mbili. Abu dhar akasema: sio mirundo miwili ya dhahabu ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Akasema: Hapana karati mbili[10] .

Tazama kifungu cha maneno ‘Matajiri ni mawakala sio wenyewe’ katika Juz. 4 (3:180).

Na mna nini hata hamumwamini Mwenyezi Mungu na hali Mtume anawaita mumwamini Mola wenu? Naye amekwishachukua ahadi yenu, ikiwa nyinyi ni Waumini.

Makusudio ya ahadi hapa ni amali kutokana na inavyofahamisha dalili mkataa. Dalili hizo ziko nyingi sana, tumetangulia kuzitaja pale tunapofasiri Aya za kilimwengu; miongoni mwazo ni zile tulizozitaja katika Juz. 15 (17:83) kifungu cha ‘Mwenyezi Mungu na ilimu ya chembe hai;’ kama ambavyo tumetaja dalili za utume wa Muhammad(s.a.w. w ) , katika kufasiri Aya zinazoashiria hivyo; ikiwemo tuliyoyataja punde katika Aya ya 77 ya sura iliyopita kwenye juzuu hii tuliyo nayo, kifungu cha ‘Uislamu na wanafikra wakuu wa Ulaya.’

Maana yanayopatikana ya Aya tuliyo nayo ni: vipi nyinyi mnapinga mwito wa Mtume kwenye imani ya Mwenyezi Mungu au kwenye lile linalowapa maisha na hali zimekuwako dalili za kutosha za kuweko Mwenyezi Mungu na umoja wake na ukweli wa Mtume katika mwito wake na unabii wake?

Razi anasema: kutokana na dalili hizo zilivyohukumia wajibu wa kufanya amali, zimekuwa na msisitizo zaidi ya kiapo, ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akauita ahadi.

Yeye ndiye anayemteremshia mja wake Aya zinazobainisha wazi ili awatoe gizani muingie kwenye nuru.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemtuma Muhammad(s.a.w. w ) kwa hoja za kutosheleza na mawaidha ili awatoe kwenye utuiifu wa shetani kwenda kumtii Mwingi wa rehema – kutoka kwenye upotevu na ufisadi kwenda kwenye uongofu na utengeneo. Mtume akawahofisha na nguvu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake, kama wakipinga, na akawaahidi wema na thawabu nyingi kama wataitikia mwito na kumtiii; akawaambia:

Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu ni Mpole, Mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu ni mpole kwa waja, mwenye huruma, mwema na mkarimu.

Anawafanyia upole bila ya wao kujua na kuwaandalia njia ya heri bila ya kudhania na anawaneemesha, lakini wao wanafanya jeuri.

Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu?

Mali yote iliyo mikononi mwa mtu ni ya kuazima tu atawaachia wa baada yake. Inaendelea hivi mpaka mtu wa mwisho; akishaondoka atakuwa hana mrithi isipokuwa Mwenyezi Mungu: “Hakika sisi tutairithi ardhi na walio juu yake na kwetu sisi watarejeshwa,” Juz. 16 (19:40).

Ikiwa hali ni hiyo basi ubahili ni wa nini? Kwani kujizuia kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu? Katika Nahjul-balagha anasema: “Namshangaa bahili anayeulilia ufukara alioukimbia na unampita utajiri alioutaka. Duniani anaishi maisha ya kifukara na akhera atahisabiwa hisabu ya matajri.”

Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita.

Mkabala wake ni na waliotoa baada ya ushindi wa Makka.

Ufufanuzi wa maana ni kuwa kitu kinaweza kupimwa kwa vipimo na kwa aina; kama vyakula vinywaji, mavazi na vipambo. Thamani ya vitu hivi na mfano wake hukadiriwa kwa kipimo chake na kwa manufaa yake pamoja. Vingine vinapimwa kwa idadi tu; kama vile upigaji kura. Kura ya mjinga na mtaalamu, ya muovu na mwadilifu zote ni sawa katika kumfikisha mgombea kwenye uongozi au bungeni, au kutomfikisha.

Vingine vinapimwa kwa aina tu; kama vile dawa inayopimwa kwa athari ya kuponesha kwake au kinga yake.

Kutoa nako kuko namna kama hii. Mtu anaweza kutoa maelfu kwa ajili ya sehemu ya kuabudu, lakini asiwe na malipo ya yule aliyetoa mkate kumpa mwenye njaa.

Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akakana usawa wa aliyetoa na akapigana kabla ya ushindi wa Makka na aliyetoa baada ya ushindi wa Makka. Waislamu kabla ya ushindi wa Makka walikuwa na dhiki na haja sana na huku makafiri wakiwa kwenye utajiri na nguvu, lakini baada ya ushindi ilikuwa kinyume – ukafiri ulidhoofika na Uislamu ukawa na nguvu.

Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu amewaahidi wema. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

Hao ni ishara ya wale waliotangulia. Maana ni kuwa kila mmoja kati ya waliotangulia na waliofuatia ana ujira na thaawabu lakini kwa kutofautiana:

وَلِكُلٍّ دَرَجَاتٌ مِّمَّا عَمِلُوا وَلِيُوَفِّيَهُمْ أَعْمَالَهُمْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٩﴾

“Na wote watakuwa na daraja zao mbalimbali kwa waliyoyatenda na ili awalipe kwa vitendo vyao.” Juz. 26 (46:19).

Kwa maneno mengine ni kuwa waliotangulia wenye kukaribishwa ndio aina hii ya kwanza ambao Mwenyezi Mungu amewataja katika Aya ya 10 ya sura iliyotangulia. Na watu wa kuume ni katika aina hii ya pili. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja katika Aya ya 67 ya sura hiyo.

Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu, na apate ujira mzuri.

Makusudio ya kukopesha hapa ni kutoa, kwa sababu Mwenyezi Mungu haihitajii mkopo anajitosheleza. Katika Nahjul-balagha kuna maelezo haya: “Mwenyezi Mungu hakuwataka msaada kwa sababu ya unyonge wala hawataki mkopo kwa sababu ya kuishiwa.

Anawataka msaada na hali ana majeshi ya mbingu na ardhi na Yeye ni Mwenye nguvu Mwenye hikima. na anawataka mkopo na hali ana hazina za mbingu na ardhi na Yeye ni mwenye kujitosha msifiwa. Ametaka kuwajaribu ni nani mwenye matendo mazuri zaidi kwenu.”

Umetangulia mfano wake na tafsiri yake kwa ufafanuzi katika Juz. 2 (2:245).