TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 26546
Pakua: 2657


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 26546 / Pakua: 2657
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

هُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوكُمْ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَالْهَدْيَ مَعْكُوفًا أَن يَبْلُغَ مَحِلَّهُ وَلَوْلَا رِجَالٌ مُّؤْمِنُونَ وَنِسَاءٌ مُّؤْمِنَاتٌ لَّمْ تَعْلَمُوهُمْ أَن تَطَئُوهُمْ فَتُصِيبَكُم مِّنْهُم مَّعَرَّةٌ بِغَيْرِ عِلْمٍ لِّيُدْخِلَ اللَّـهُ فِي رَحْمَتِهِ مَن يَشَاءُ لَوْ تَزَيَّلُوا لَعَذَّبْنَا الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿٢٥﴾

25. Hao ndio waliokufuru na wakawazuia msiingie Msikiti Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao pa kuchinjwa. Na lau si wanaume waumini na wanawake waumini msiowajua kuwa mtawasaga na mkaingia matatani kutokana nao bila ya kujua. Ili amuingize amtakaye katika rehema yake. Lau wangelipambanuka bila ya shaka tungeli waadhibu waliokufuru kwa adhabu chungu.

إِذْ جَعَلَ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي قُلُوبِهِمُ الْحَمِيَّةَ حَمِيَّةَ الْجَاهِلِيَّةِ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَأَلْزَمَهُمْ كَلِمَةَ التَّقْوَىٰ وَكَانُوا أَحَقَّ بِهَا وَأَهْلَهَا وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٢٦﴾

26. Pale wale ambao wamekufuru walipotia katika nyoyo zao hasira, hasira za kijinga, Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya waumini, na akawalazimisha neno la takua. Na wao walikuwa ndio wenye haki nalo na wenye kustahili. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

WALIOWAZUIA NA MSIKITI MTAKATIFU

Aya 25 – 26

MAANA

Hao ndio waliokufuru na wakawazuia msiingie Msikiti Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao pa kuchinjwa.

Katika kufasiri Aya ya 10 ya sura hii tulisema kuwa mnamo mwaka wa sita wa Hijra washirikina walimzuia Mtume(s.a.w. w ) na maswahaba wasiuzuru Msikiti Mtakatifu. Inasemekana walikuwa na ngamia sabini wa kuchinja Makka. Hao ndio aliowakusudia Mwenyezi Mungu kwa kusema: “na wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao pa kuchinjwa.”

Vile vile katika Aya 24 tukasema kuwa waislamu waliiteka Makka bila ya vita mnamo mwaka wa nane. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alitizitia hofu nyoyo za washirikina kutokana na waislamu.

Aya tuliyo nayo hivi sasa inaelezea maana haya na kusisitiza kuwa watu wa Makka hawakujizuia kupigana na Mtume(s.a.w. w ) na maswahaba wake, walipoingia Makka, isipokuwa ni kwa kuwaogopa waislamu. Dalili ya hilo – kama ilivyoweka wazi Aya – ni kuwa hawa ndio walewale waliowazuia waislamu jana kuingia Msikiti Mtakatifu na kuchinja ili wale mafukara.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaashiria baadhi ya faida za kutopigana Makka, kwa kusema:

1.Na lau si wanaume waumini na wanawake waumini msiowajua kuwa mtawasaga na mkaingia matatani kutokana nao bila ya kujua.

Mtume(s.a.w. w ) alipoingia Makka kuiteka, hapo walikuweko waislamu wanaume na wanawake, waliokuwa hawajulikani wala huwezi kuwatofautisha na wshirikina kwa vile walikuwa wakificha imani yao kuhofia maadui wa uislamu. Lau vita vingechachamaa, madhara yake yangeliwakumba waislamu na makafiri. Hilo lingeliwatia tabu waislamu; kama vile kutoa fidia ya kuua kwa makosa, kuongezea maadui watapata la kusema kuwa waislamu wanauana wenyewe kwa wenyewe.

2.Ili amuingize amtakaye katika rehema yake.

Makusudio ya rehema hapa ni Uislamu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliizuia mikono isipigane Makka, kwa sababu anajua kuwa baadhi ya wakazi wake washirikina wataongoka na kusilimu. Na ilitokea hivyo kweli.

Lau wangelipambanuka bila ya shaka tungeliwaadhibu waliokufuru kwa adhabu chungu.

Yaani lau wangelijulina waislamu na makafiri, Mwenyezi Mungu angeliwaruhusu kupigana na na makafiri na angeliwateremshia adhabu kali.

Pale wale ambao wamekufuru walipotia katika nyoyo zao hasira, hasira za kijinga.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaashiria vigogo wa kishirikina waliomzuia Nabii(s.a.w. w ) kuzuru Msikiti mtakatifu. Si kwa lolote ila ni kwamba nyoyo zao zimejaa taasubi na kiburi.

Hili pekee linatosha kuruhusiwa kuuawa, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaizuia mikono ya waumini kuwachunga wale wanaoficha imani yao na waislamu watakaopatikana baadaye.

Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya waumini, na akawalazimisha neno la takua. Na wao walikuwa ndio wenye haki nalo na wenye kustahili.

Makusudio ya utulivu hapa ni kuridhia na subira nzuri. Kuwalazimisha ni kuwawajibishia. Ama neno la takua imesemekana ni tamko la ilaha illa Allah… (hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu….). lakini lenye nguvu ni kuwa makusudio yake ni kufanya takua.

Maana ni kuwa Mtume(s.a.w. w ) alikubali suluhu ya Hudaybiyya pamoja na kiburi cha washirikina na ujeuri wao. Baadhi ya maswahaba walichukia suluhu na wakataka kupigana tu, lakini Mwenyezi Mungu akawapa subira nzuri pamoja na ufedhuli wa washirikina, akawaamrisha wakubali suluhuu na wairidhie.

Wakasikia na wakafanya yanayowajibisha imani na takua. Hilo si la kushangaza kwa vile wao ndio wanaostahiki na ndio aula kulitumia. Walikwishapigana jihadi na wakajitolea mara nyingi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wakafanya subira ya kiungwana.

Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Anawajua wenye takua na wenye hatia, kila mmoja atamlipa kwa aliyoyachuma na wao hawatadhulumiwa.

لَّقَدْ صَدَقَ اللَّـهُ رَسُولَهُ الرُّؤْيَا بِالْحَقِّ لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ فَعَلِمَ مَا لَمْ تَعْلَمُوا فَجَعَلَ مِن دُونِ ذَٰلِكَ فَتْحًا قَرِيبًا ﴿٢٧﴾

27. Hakika Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ruiya ya haki. Bila ya shaka mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani, na hali mmenyoa vich- wa vyenu na mmepunguza. Hamtakuwa na hofu. Alijua msiyoyajua. Mbali na haya aliwapa ushindi ulio karibu.

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا ﴿٢٨﴾

28. Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na dini ya haki, ili aitukuze juu ya dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi.

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٢٩﴾

29. Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu na walio pamoja naye, wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakirukuu na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Tawrat na mfano wao katika Injili ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya shina lake, ukawapendeza wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walioamini na wakatenda mema katika wao maghufira na ujira mkubwa.

MRUIYA YA MTUME

Aya 27 – 29

MAANA

Hakika Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ruiya ya haki. Bila ya shaka mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani, na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza. Hamtakuwa na hofu.

Dhahiri ya Aya na Hadith mutawatir zinafahamisha kuwa Mtume(s.a.w. w ) aliota kuwa yeye na swahaba zake wameingia Makka kwa amani, wakatufu nyumba kongwe; vile wanavyotaka, wengine wakiwa wamenyoa na wengine wamepunguza. Basi Mtume akawaelezea swahaba zake alivyoona usingizini. Wakafurahi na kufikiria kuwa mwaka huhuo wataingia Makka. Mtume akaenda nao Makka lakini wakazuiliwa Hudaybiyya na wakarudi Madina; kama tulivyokwishaeleza.

Hapo wanafiki wakawa wamepata la kusema: “Haya iko wapi ndoto? Hatukunyoa, hatukupunguza wala hatukuona Msikiti? Wakasahau au wakajitia kusahau kuwa Mtume hakutaja muda. Mmoja akamuuliza Mtume: si umesema hakika utauingia Msikiti Mtakatifu kwa amani? Akasema ndio, lakini sikusema ni mwaka huu.

Mwaka uliofuatia, ambao ulikuwa ni mwaka wa saba wa Hijra, waislamu waliingia Makka kufanya Umra, wakatufu Al-Ka’aba wanavyotaka, akanyoa mwenye kunyoa na kupunguza mwenye kupunguza. Wakabaki hapo siku tatu kisha wakarejea Madina. Ndio ikashuka kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ruiya,” yalipojitokeza yale aliyoota Mtume na kuwaambia:

Alijua msiyoyajua.

Mwenyezi Mungu alijua masilahi ya kuuahirisha umra baada ya mkataba wa Hudaybiyya, jambo ambalo waislamu hawakulijua; ambayo ni kuepusha vita, kusilimu washirikina wengi waliomzuilia Mtume na maswahaba.

Mbali na haya aliwapa ushindi ulio karibu.

‘Haya’ ni kuhakika ndoto ya kuingia Makka kwa amani. Makusudio ya ushindi ni mkataba wa Hudaybiya au ni huo na kuichukua Khaybara. Maana ni kuwa suluhu hii na kuiteka Khaybara kulikofanyika baada siku kidogo, kulifanyika kabla ya kuhakikika ndoto. Mambo hayo mawili ni ushindi mkubwa sawa na kuingia Makka.

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki, ili aitukuze juu ya dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi.

Makusudio ya Mtume ni Muhammad(s.a.w. w ) . Uwongofu na dini ya haki ni Uislamu. Ulitukuka na kuenea mashariki mwa ardhi na magharibi yake. Kwa sababu unatoa mwito wa kutenda kwa ajili maisha bora na kukataza kila ambalo litakuwa ni kikwazo katika njia ya kufikia hilo.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (9:33).

MASWAHABA NA QUR’AN

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesimulia katika Kitabu chake Kitakatifu kuwa Musa Bin Imran aliwalingania wana wa Israil kwenye vita wakamwambia:

فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ ﴿٢٤﴾

“Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane, sisi tutakaa hapa.” Juz. 6 (5:24).

Pia alisimulia kuwa watu wa Bwana Masih walijaribu kumuua na kumsulubu na wanafunzi wake wakamwambia: Je Mola wako anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni; aliposema: Mcheni Mwenyezi Mungu. Wakasema: Tunataka kula katika hicho Tazama Juz. 7 (5:111-112).

Na akateremsha Sura nzima mbali ya Aya nyinginezo kadhaa kuwashutumu maswahaba wanafiki, lakini vile vile aliteremsha Aya nyingi za kuwasifu maswahaba wema wenye takua; miongoni mwa Aya hizo ni ya 18 ya sura hii tuliyo nayo, tuliyoifasiri punde tu na ile isemayo:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٠٠﴾

“Na waliotangulia wa kwanza katika wahajiri na Ansari, na wale waliowafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu yuko radhi nao na wao wako radhi naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” Juz. 11 (9:100).

Na pia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu na walio pamoja naye, wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao.

Waovu huungana katika kutafuta windo, na wanapolipata wanauana wao kwa wao kugombania kulila. Lakini wenye ikhlasi wao wako wako pamoja tu wakati wote, hawatofautiani. Ni ndugu katika dini wakihurumiana na kusaidiana; ni kama familia moja, wanasaidiana kwenye haki na watu wake na wanapiga vita ubatilifu na wanachama wake.

Hii ndio sifa halisi ya swahaba wa Muhammad(s.a.w. w ) kwa ushahidi wake Mwenyezi Mungu Mtukufu pale alipowasifu wao na Mtume kuwa wanakasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wanaridhia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Haya ameyatambua Dkt. Twaha Hussein, mwanafasihi ambaye huwa anafahamika kwa ishara na dalili. Anasema katika kitabu chake: Mir-atul-islam (Kioo cha uaislamu): “Uislamu wa manabii haukuwa ni twaa ya dhahiri isipokuwa uaislamu wao ulikuwa mpana wenye kina na wa ukweli zaidi ya inavyowezekana kuwa Uislamu. Na Uislamu wa waliokuwa wema katika Maswahaba haukuwa na ufinyu unaosimama mbele ya utii ulio dhahiri, isipokuwa ulikuwa ni mpana na wenye kina zaidi ya hivyo.”

Kisha Dkt. akampigia mfano Ammar Bin Yasir kwa Uislamu huu wa kina, akasema: “Ammar bin Yasir alikuwa akipigana pamoja na Ali katika Siffin kwa hamasa, naye akiwa ni mzee wa miaka tisini au kupita. Alikuwa akipigana kwa imani, yaani kwamba yeye anaitetea haki. Siku alipouawa alikuwa akiwahimiza watu huku akisema: Ni nani atakayekwenda Peponi? Leo nitakutana na wapenzi Muhammad na kikosi chake.”

Anaendelea kusema: “Kuuawa kwa Ammar kulikuwa ni kumthibitisha Ali na walio wema katika maswahaba zake na kumuweka kwenye shaka Muawiya na waliokuwa pamoja naye. Hiyo ni kwa sababu Wahajiri wengi na Answar walimuona Mtume(s.a.w. w ) akipapasa kichwa cha Ammar na kumwambia: Masikini ewe mwana wa Sumayya, kitakuua kikundi kiovu.”

Utawaona wakirukuu na kusujudu.

Yaani mandhari yanamfanya muangaliaji awaone kuwa wao ni watu wa kurukuu na kusujudu, hata kama wakati huo hawako hivyo.

Wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu.

Makusudio ya athari ya kusujudu hapa sio ile alama nyeusi inayoonekana kwenye paji la uso, hapana kwa sababu alama hizi nyingi ni za kinafiki na ria; isipokuwa makusudio yake ni usafi na uangavu unaonekana usoni kutokana na athari ya ibada.

Maana ni kuwa maswahaba walirukuu na kusujudu kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake na kuhofia ghadhabu zake na adhabu zake. Athari hiyo, ukiichunguza, inajitokeza katika nyuso zao kiuhakika, kwa sababu ibada ya ikhlasi ya Mungu inaleta utwahara na usafi katika nafsi ya mja mwenye ikhlasi na kujitokeza kwa ukamilifu usoni; sawa na inavyojitokeza huzuni na furaha.

Huu ndio mfano wao katika Tawrat na mfano wao katika Injili ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya shina lake.

Hiki ni kinaya cha maswahaba wa Mtume(s.a.w. w ) ; mwanzo wanakuwa wachache kisha wanazidi na kuwa wengi. Ufafanuzi wa mfano huu ni kuwa Tawrt na Injili zimetoa bishara ya Muhammad(s.a.w. w ) , zikawasifia maswahaba zake kama mmea unaokuwa, ukazaa matunda na yakawa mengi pamoja na matawi yake, yakashikana vizuri na ukawa una nguvu.Ukawapendeza wakulima kwa uzuri wake na kukua kwake.

Ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri.

Sio mbali kuwa makusudio ya wakulima hapa ni Mtume, maadamu mmea ni swahaba zake, kwa sababu yeye ndiye aliyewainua kufikia mahali walipo; na kwa fadhila yake wameshinda vita wakati wake na baadae. Na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja wakulima badala ya mkulima kwa kumtukuza Mtume(s.a.w. w ) .

Ikumbukwe kwamba tunayasema haya kwa njia ya uwezekano tu wa kukisia

Mwenyezi Mungu amewaahidi walioamini na wakatenda mema katika wao maghufira na ujira mkubwa.

Maana yake yako wazi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 6 (5:9).

JE, SHIA ITHANAASHARIA WANA TAFSIRI YA NDANI?

Mwanafasihi wa Misr, Dkt Mustafa Mahmud, alitoa mfulululizo wa makala 13, katika jarida la Sabahul-khayr. Katika makala hizo alizungumzia muujiza wa Qur’an, kisa cha kuumba[4] na maudhui mengine ya ghaibu.

Kisha yakakusanywa makala katika kitabu kilichoitwa: Muhawalatu lifahmi asriy lilqur’an (Kujaribu kuifahamu Qur’an kisasa). Kikachapishwa na kutolewa mnamo mwezi wa tatu au wa nne mwaka 1970.

Katika makala ya ‘Mungu mmoja na dini moja,’ mtungaji aliwachanganya Shia Ithnaashariya pamojana vikundi vinavyofasiri Qur’an kwa undani, na kwamba wao ni sawa na Al-babiyya na Al-khawarij, wakifasiri Qur’an kwa tafsiri ya undani.

Basi nikamwandikia barua kwamba Shia Ithanaasharia, wako mbali zaidi ya watu wote na fikra hii ya uzushi na upotevu na kwamba vitabu vyao vinashudia hilo na vimejaa kwa watu. Nikamtajia baadhi ya vitabu hivyo na jinsi masheikh wa Azhar wenye insafu walivyosema kuhusu Shia Imamia; kama vile marehemu Sheikh Shaltut na wengineo waliounukuliwa na jarida la Al-islam, linalotolewa Misr na Darut-taqrib.

Katika jioni ya 15-4-1970, nilisikia mlio wa simu, akawa ni Dkt. Mustafa Mahmud akizungumza kutoka Triumph Hotel ya Beirut…Tukawa pamoja kwa mara ya kwanza. Tukazungumza kuhusu kitabu chake Allahu wal-insan (Mwenyezi Mungu na mtu) na majibu yangu Allahu wal-aql (Mwenyezi Mungu na akili).

Basi nikamwalika nyumbani kwangu siku iliyofuatia. Mazungumzo yetu yalikuwa juu Uislamu na tafsiri za ndani. Miongoni mwa maneno aliyoyasema mwana fasihi huyu ni: “Baadhi ya Shia wanafasiri “Amezichanganya bahari mbili kwa kuzikutanisha[5] .” kuwa ni Ali na Fatima.”

Nikwambia: Je, ni mantiki na ni sawa kweli kulihusisha kundi lenye mamilioni ya wafuasi kwa kauli ya mmoja wao, anayejiwakilisha yeye mwenyewe tu? Je, ni lazima ikiwa sheikh mmoja atafasiri Aya ya Qur’an kwa undani, ndio taifa zima lihisabiwe wanafasiri Qur’an kwa undani? Ikiwa malenga mmoja wa Misr atafasiri ubeti wa shairi kialama, je, ni sawa kusema kuwa malenga wote wa Misri wanafasiri mashairi kialama? Niliendelea kumwambia: “Hakika Shia Ithnaasharia wana vitabu vya kiitikadi vinavyokubalika; kama vile Awail al-maqalat cha Sheikh Mufid, Qawaidul-aqai cha Nasruddin Attusi na sherehe yake cha Allama Hill na yaliyoelezwa katika Sharhut Tajrid minat Tawhid…”

Nilikuwa nikikutana na Tafsiri ya kiundani ya masheikh wa kisunni wakati nikifanya utafiti wa rejea, lakini nilikua nikizipuuza, kwa vile zilikuwa haziendani na malengo ya tafsiri yangu. Basi Dkt. Alipotoa hoja ya bahari mbili, nilijaribu sana kukumbuka angalau tafsiri moja tu ili nipinge manaeno ya Dkt. Lakini kumbukumbu zangu ziliniangusha wakati nilipokuwa nazihitajia sana. Basi tukaendelea na maudhi mengine.

Ilikuwa ni sadfa wakati tukijadilina, kuwa ninafasiri sura hii ya Al-fat-h. Siku iliyofuatia nikafika kwenye Aya isemayo: “Ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya shina lake,” Mara nikasoma tafsiri za Kissuni: Ruhul-bayan ya Isamil Haqqi na Ats-hil ya Alhafidh bin Ahamd Al-Kalabi. Wote ni wa kissuni, ninawanukuu: “Ni kama mmea uliotoa chipukizi lake Kwa Abu Bakr, kisha ukalitia nguvu kwa Umar, ukawa mnene kwa Uthman, ukasimama sawa juu ya shina lake kwa Ali.”

Basi niliyoyaona katika tafsiri hizi yakanikumbusha niliyoyasoma zamani katika kitabu Hayatu Al-imam Abu Hanifa (Maisha ya Imam Abu Hanifa) cha Sayyid Afifi, kwamba Suyut amesema: “Wamesema maulama kwamba Mtume(s.a.w. w ) alimbashiria Imam Malik katika Hadith isemayo: “Inakurubia watu kupiga matumbo ya farasi wakitafuta ilimu, hawatapata mwanachuoni aliye mjuzi zaidi kuliko mwanachuoni wa Madina.”

Akambashiria Shafii katika Hadith: “Msiwatukane makuraishi kwani mwanachuoni wake ataijaza ardhi ilimu.” Akambashiria Abu hanifa kwenye Hadith: “Lau kama ilimu itakuwa imeangikwa juu ya Thureya wangeliifuata watu katika wafursi.”

Basi hapo hapo nikampigia simu Dkt, nikamsomea tafsiri mbili na kumuuliza: je, utaniruhusu nizinasibishe tafsiri hizi kwa masunni wote, niwafanye wao na Wahabiy kuwa ni sawa, kama ulvyofanya wewe kwa Shia kwa kuwa tu mmoja wao amesema?

Basi hakunijibu kitu isipokuwa: “Tamam … tamam.” (sawa … sawa).

MWISHO WA SURA YA ARUBAINI NA NANE: SURAT AL-FATH