TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 26465
Pakua: 2616


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 26465 / Pakua: 2616
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU Juzuu 23

Mwandishi:
Swahili

12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

Sura Ya Hamsini: Surat Qaf. Imeshuka Makka. Ina Aya 45.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

ق وَالْقُرْآنِ الْمَجِيدِ ﴿١﴾

1. Qaf. Naapa kwa Qur’an tukufu!

بَلْ عَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ فَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا شَيْءٌ عَجِيبٌ ﴿٢﴾

2. Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا ذَٰلِكَ رَجْعٌ بَعِيدٌ ﴿٣﴾

3. Je, tukifa na tukawa udongo? Marejeo hayo ni ya mbali!

قَدْ عَلِمْنَا مَا تَنقُصُ الْأَرْضُ مِنْهُمْ وَعِندَنَا كِتَابٌ حَفِيظٌ ﴿٤﴾

4. Hakika tunajua kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinachohifadhi.

بَلْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ فَهُمْ فِي أَمْرٍ مَّرِيجٍ ﴿٥﴾

5. Lakini waliikadhibisha haki ilipowajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.

أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ ﴿٦﴾

6. Je, Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyozijenga, na tukazipamba wala hazina nyufa.

وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ ﴿٧﴾

7. Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.

تَبْصِرَةً وَذِكْرَىٰ لِكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ ﴿٨﴾

8. Yawe ni busara na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.

وَنَزَّلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً مُّبَارَكًا فَأَنبَتْنَا بِهِ جَنَّاتٍ وَحَبَّ الْحَصِيدِ ﴿٩﴾

9. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa.

وَالنَّخْلَ بَاسِقَاتٍ لَّهَا طَلْعٌ نَّضِيدٌ ﴿١٠﴾

10. Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi.

رِّزْقًا لِّلْعِبَادِ وَأَحْيَيْنَا بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا كَذَٰلِكَ الْخُرُوجُ ﴿١١﴾

11. Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyokuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyokuwa ufufuo.

NAAPA KWA QUR’AN TUKUFU

Aya 1 – 11

MAANA

Qaf .

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).

Naapa kwa Qur’an tukufu!

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameapa kwa Qur’an kudhihirisha ukuu wake, na ameisifu ni tukufu kwa wingi wa manufaa na faida zake.

Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!

Ndio, ni ajabu katika mantiki ya wale wanaoona kila kitu ni mali, wala hawaoni ubora wowote isipokuwa benki na ardhi.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 11(10:2). Juz. 23 (38:4-5).

Je, tukifa na tukawa udongo? Marejeo hayo ni ya mbali!

Walikana ufufuo kwa sababu wao wanashindwa kuuelewa. Sisi tunaamini kushindwa kwao kuuelewa, lakini je, kushindwa kwao kulitambua jambo, ni dalili ya kutokuweko?

Ni mwenye akili gani anayechukia kushindwa kwake kuelewa kitu kuwa hakipo?

Kutatizika kwao kulikotokana na kutojua huku, walikokubainisha kwa kusema: “Ni nani huyo atakayeihuisha mifupa nayo imemung’unyika? Mwenyezi Mungu naye akawajibu:

وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ ﴿٧٨﴾ قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ ﴿٧٩﴾

“Sema: Ataihuisha aliyeiumba mara ya kwanza. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.”

Juz. (36:78-79).

Maana haya yamekaririka kwenye Aya kadhaa.

Hakika tunajua kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinachohifadhi.

Kitabu kinachohifadhi ni kinaya cha kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amekizunguka kila kitu kwa ujuzi. Aya hii ni jawabu la kutatizika kulikofanya wakanushe ufufuo. Ufafanuzi wake ni kuwa mwili wa mtu unaliwa na ardhi baada ya mauti na unakuwa chembechembe zinazotawanyika mashariki mwa ardhi na magharibi yake. Vipi zitakuswanywa na kurudishwa ulivyokuwa?

Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba Yeye anajua kwamba ardhi inakula mili ya wafu na kwamba inatawanyika mashariki mwa ardhi na magharibi yake, lakini pamoja na hayo Yeye anaweza kuikusanya na kuirudishia uhai wake.

MWENYE KULA NA MWENYE KULIWA

Wanafalsafa na wanatheologia wanakuita kutatizika huku ni kutatizika kwa ‘mlaji na mwenye kuliwa.’ Mulla Sadra amekutaja katika Juzuu ya nne ya kitabu chake, Al-asfar akasema: “Wametoa hoja kuwa: Ikiwa mtu atamla mtu mwingine, sehemu zilizoziliwa zikirudishwa kwenye mwili wa aliyekula hazitakuwa ni za aliyeliwa, na hapo atakuwa aliyeliwa ama ataadhibiwa au ataneemeshwa kutegemea na aliyemla.

Hayo yamejibiwa katika vitabu vya theologia kwamba ufufuo utakuwa kwa viungo vyao vile vilivyoanza kuumbwa ambavyo ni viungo vya asili kwao; na Mwenyezi Mungu anafihifadhi wala havifanyi ni viungo vya mwingine.”

Anaendelea kusema Mulla Sadra kwamba jawabu hili halitoshi. Ukweli ni kuwa kila linalowezekana kiakili na likafahamishwa na wahyi, ni wajibu kuliamini. Na ufufuo ni jambo linalowezekana kiakili na limethibiti kiwahyi. Kwa hiyo niwajibu kulisadiki na kuliamini. Ama wanafalsafa na watu wa mantiki sio maasumu.

Haya ndiyo aliyoyasema mwenye Al-asfar, nayo ndiyo tuliyoyategemea na kuyataja mara kdhaa huko nyuma. Masheikh wamejaribu kuthibitisha ufu- fuo wa kimwili kwa hukumu ya kiakili bila ya kuangalia wahyi, lakini hawakuzidisha ispokuwa uzito na kutatiza.

Lakini waliikadhibisha haki ilipowajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.

Makusudio ya haki ni Qur’an. Mwenyezi Mungu ameita, mkorogo hali ya wale waliomwambia Mtume kuwa ni mwenda wazimu, mara ni mchawi, tena ni kuhawani na hata pia wakamwita mshairi. Huko ndikokukorogeka na kuchanganyikiwa hasa.

Je, Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyozijenga, na tukazi- pamba wala hazina nyufa.

Makusudio ya kujenga hapa ni kuwa sayari za mbinguni zimepangiliwa kihekima katika kutengenezwa kwake, zimetulia kwenye nidhamu yake na zinakwenda kwa uhakika. Makusudio ya kuzipamba ni uzuri. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Hazina nyufa’ ni kuwa kila sayari katika sayari zake hakuna yenye kasoro; kama alivyosema:

هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ ﴿٣﴾

“Je, unaona kasoro?” (67:3).

Maana ni kuwa wakadhibishaji hawoni ufufuo kuwa jengo la sayari halifanani na jengo lolote la binadamu. Kwa sababu sayari kadiri itakavyokuwa kubwa, lakini inakuwa ni kitu kimoja kisichokuwa na maunganisho, lakini wajenzi huwa wanaweka tofali juu ya tofali jingine, kati yao kuna utengnisho na mistari, nao hawawezi kujenga jengo kubwa kama hilo la sayari.

Aya hii ni majibu wazi na hoja ya kumnyamzisha yule anayeiweka mbali na kuishangaa fikra ya ufufuo na kusema: “Je, tukifa na tukawa udongo? Marejeo hayo ni ya mbali!”

Majibu yenyewe ni kuwa yule ambaye ameumba sayari bila maunganisho hawezi kushindwa kumfufua mtu baada ya kufa kwake. Kwa sababu hili ni jepesi zaidi kuliko hilo:

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ ...﴿٥٧﴾

“Hakika umbo la mbingu na ardhi ni kubwa zaidi kuliko umbo la watu.” Juz. 24 (40:57).

Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.

Yaani tumeitandaza na tukaifanya iwe sawa kwa ajili ya binadamu, tukaweka humo milima ili isiyumbe na tukaotesha aina mbalimbali za mimea inayopendeza kuiona na yenye uzuri wa kuliwa.

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz.13 (13:3).

Yawe ni busara na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ulimwengu na yaliyomo ikiwemo nidhamu na mpangilio ili iwe ni ishara ya ukuu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mwenye busara na mazingatio. Hapo kuna ishara kuwa mfungamano wa mtu na ulimwengu anaoishi hauishii kwenye maada tu, bali ni kwa moyo pia.

Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa. Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyaita maji yenye baraka, kwa vile hakuna uhai wa roho wala viwiliwili bila ya maji. Na ameiita mitende mirefu kuashiria kuwa wakati wa kuota mitende inakuwa midogo, kisha inakuwa kwa sababu ambazo Mwenyezi Mungu amezipa maumbile.

Imam Ali(a . s) anasema:“Haikufahamisha dalili ila kwamba muumba wa chungu ndiye muumba wa mtende kwa umakini wa kukipangila kila kitu.” Yaani umakini wa mpangilio wa kutengenezwa chungu na mtende mkubwa unajulisha kuwa muumba ni mmoja.

Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Kwa vile hawawezi kujiruzuku wenyewe.Na tukaifufua kwa maji nchi iliyokuwa imekufa.

Hii ni mwanzo wa kusemaKama hivyo ndivyo utakavyokuwa ufufuo .

Kwa hiyo kufufua watu baada ya mauti ni sawa na kuufuua kwa maji mji uliokufa. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; kama vile Juz. 8 (7:57).

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ ﴿١٢﴾

12. Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuhu na watu wa Rassi na Thamudi.

وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ ﴿١٣﴾

13. Na A’di na Firauni na ndugu wa Lut.

وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ ﴿١٤﴾

14. Na watu wa Machakani na watu wa Tubbaa’. Wote waliwakanusha Mitume, kwa hivyo kiaga kikathibitika juu yao.

أَفَعَيِينَا بِالْخَلْقِ الْأَوَّلِ بَلْ هُمْ فِي لَبْسٍ مِّنْ خَلْقٍ جَدِيدٍ ﴿١٥﴾

15. Kwani tulichokakwa kuumba kwa kwanza? Bali wao wamo katika shaka juu ya umbo jipya.

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ ﴿١٦﴾

16. Na hakika tumemuumba mtu, na tunayajua yanayoitia wasiwasi nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingo.

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ ﴿١٧﴾

17. Wanapopokea wapokeaji wawili, walioko kuliani na kushotoni.

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ ﴿١٨﴾

18. Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.

وَجَاءَتْ سَكْرَةُ الْمَوْتِ بِالْحَقِّ ذَٰلِكَ مَا كُنتَ مِنْهُ تَحِيدُ ﴿١٩﴾

19. Na uchungu wa mauti utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْوَعِيدِ ﴿٢٠﴾

20. Na itapulizwa parapanda. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.

وَجَاءَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّعَهَا سَائِقٌ وَشَهِيدٌ ﴿٢١﴾

21. Na itakuja kila nafsi pamoja na na mpelekaji na shahidi.

لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ ﴿٢٢﴾

22. Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.

KWANI TULICHOKA KWA KUUMBA KWA KWANZA?

Aya 12 – 22

MAANA

Walikadhibisha kabla yao yaani kabla ya Muhammad(s.a.w. w ) kaumu ya Nuh

Kimetangulia kisa cha Nuh katika Juz. 12 (11:27-31).

Na watu wa Rassi.

Rassi ni kisima. Imetangulia ishara yao katika Juz. 19 (25:30-40).

Na Thamudi.

Hao ni watu wa Swaleh. Kisa chao kiko Juz. 12 (11:61-68).

Na A’di.

Hao ni watu wa Hud. Yametangulia masimulizi yao kwenye Juz. 12 (11:50-56).

Na Firauni.

Kisa chake pamoja na Musa na wana wa Israil, kimekaririka mara nyingi; miongoni mwazo ni Juz. 9 (7:103-112).

Na ndugu wa Lut.

Tazama Juz. 8 (7:80-84).

Na watu wa Machakani.

Imetangulia ishara yao katika Juz. 19 (26:176-191).

Na watu wa Tubbaa’.

Yametangulia maelezo yao katika Juz. 25 (45:37).

Wote waliwakanusha Mitume, kwa hivyo kiaga kikathibitika juu yao.

Hiyo ni adhabu ambayo Mwenyezi Mungu aliwaahidi kupitia Mitume wake.

Kwani tulichoka kwa kuumba kwa kwanza mpaka tuchoke na kuumba kwa pili?

“Kama tulivyoanza umbo la kwanza, tutalirudisha tena.” Juz. 17 (21:104).

Bali wao wamo katika shaka juu ya umbo jipya.

Umbo jipya ni ufufuo. Shaka ni nzuri, bali wakati mwingine ni dharura, ikiwa ni ya kufanya utafiti na kuchunguza, lakini kukanusha bila ya dalili na kutia shaka tu, huo ni ujinga na upotevu.

Na hakika tumemuumba mtu, na tunayajua yanayoitia wasiwasi nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingo.

Mwenyezi Mungu yuko karibu na kila kitu kwa kujua kwake, kwa sababu hakuna chochote ila kimetokana na Yeye. Kwa hiyo hakuna kitu kilicho mbali naye. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja mshipa wa shingo kwa vile uko karibu na mtu kuliko kiungo chochote kingine; kuongezea kuwa ni mhimili wa maisha.

Wanapopokea wapokeaji wawili, walioko kuliani na kushotoni. Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu anamwekea mtu waangalizi wawili; mmoja akiwa upande wa kulia na mwingine wa kushoto wakisajili kila analolitamka. Wafasiri wengi wamesema kuwa waangalizi hawa wawili ni malaika na kwamba yule wa kulia anaandika mema na yule wa kushoto maovu.

Pia inafaa kufasiri kuwa wawili hao ni kinaya cha kuwa mtu ataulizwa anayoyasema na anayoyafanya na kwamba yeye wakati wa hisabu hawezi kuficha au kupinga lolote katika uovu wake, kwa kuweko hoja juu yake.

Tumesema kuwa inafaa tafsiri hii kwa vile inaenda pamoja na ile ya kwanza inayofahamika kutokana dhahiri ya Aya, na natija zao ni moja.

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu kwa ilimu yake hana haja ya waangalizi na waaandishi. Sasa kuna Makusudio gani ya kuwaweka waangalizi?

Jibu : Makusudio ni kuwakabili Mwenyezi Mungu wakosefu kwa lile ambalo hawatakuwa ni hila wala njia ya kulikana. Na kwa mbali Aya inaashiria kuwa haifai kwa kadhi kuhukumu kwa kulijua kwake jambo. Tazama Juz. 24 (41:20).

Na uchungu wa mauti utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.

Uchungu wa mauti ni uchungu wa kutoka roho. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ‘kwa haki,’ inaashiria kuwa wakati wa kufa, uhakika utamfunukia yule mwenye kukata roho na atajua kwa uhakika kwamba ufufuo ni kweli isiyo na shaka. Neno ‘hayo’ ni ishara ya hayo ya kufufuliwa. Maneno hapa yanelekezwa kwa yule anayekana ufufuo. Makusudio ya kukimbia ni kukana.

Maana ni kuwa ataambiwa yule anayekana ufufuo wakati anapokata roho: huu ndio ufufuo uliokuwa ukiukana. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

هَـٰذَا يَوْمُ الْفَصْلِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ ﴿٢١﴾

“Hii ndiyo Siku ya upambanuzi mliyokuwa mkiikadhibisha.” Juz. 23 (37:21).

Na itapulizwa parapanda. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashiria Kiyama:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ ﴿٥١﴾

“Na itapulizwa parapanda mara watatoka makaburini wakikimbila kwa Mola wao.”

Juz. 23 (36:51).

Na itakuja kila nafsi pamoja na na mpelekaji na shahidi.

Mpelekaji ni wakuipeleka kwenye mkusanyiko na shahidi ni yule atakayeshuhudia matendo yake.

Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.

‘Haya,’ ni haya ya hisabu na malipo. Ama kuona kukali makusudio yake ni kuwa uhakika, kwa anayekana ufufuo, utajitokeza wakati wa kufa na baadae; atajua aliyoyakana na atayakana aliyoyajua.

Maana ni kuwa kesho ataambiwa mkanushaji: Ewe muovu! Uliikana siku hii ya leo na ukafuata hawa yako, ukaghafilika na uliyokusudiwa. Basi batili imekuondokea leo, umejua uhakika, lakini ni wakati ambao hakuna kimbilio la kujiepusha na kuungua.

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA TATU

وَقَالَ قَرِينُهُ هَـٰذَا مَا لَدَيَّ عَتِيدٌ ﴿٢٣﴾

23. Na mwenzake atasema: Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.

أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ ﴿٢٤﴾

24. Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inadi.

مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُّرِيبٍ ﴿٢٥﴾

25. Azuiaye heri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka.

الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ ﴿٢٦﴾

26. Ambaye amemfanya mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.

قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَـٰكِن كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ ﴿٢٧﴾

27. Mwenzake aseme: Ee Mola wetu! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotevu wa mbali.

قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ ﴿٢٨﴾

28. Aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikwishawatangulizia kiaga changu.

مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٢٩﴾

29. Kwangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja.

يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ ﴿٣٠﴾

30. Siku tutapoiambia Jahannamu: Je, umejaa? Nayo iseme Je, kuna ziada?

وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ غَيْرَ بَعِيدٍ ﴿٣١﴾

31. Na Pepo italetwa karibu kwa wenye takua, haitakuwa mbali.

هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِكُلِّ أَوَّابٍ حَفِيظٍ ﴿٣٢﴾

32. Haya ndiyo mnayoahidiwa. Kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu ajilindae.

مَّنْ خَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ وَجَاءَ بِقَلْبٍ مُّنِيبٍ ﴿٣٣﴾

33. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema kwa ghaibu, na akaja kwa moyo ulioelekea.

ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُلُودِ ﴿٣٤﴾

34. Ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima.

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ ﴿٣٥﴾

35. Humo watapata wakitakacho, na kwetu kuna ziada.

ANAYEKATAZA HERI

Aya 23 – 35

MAANA

Na mwenzake atasema: Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.

Mwenzake ni yule aliyetajwa katika Aya ya 17- Malaika anayeandika matendo ya yule aliye naye. Maana ni kuwa. Mwandishi huyu atamwambia Mwenyezi Mungu (s.w.t):

Hiki kitabu cha yale uliyonituma. Ndani yake mna mambo yote vile yalivyokuwa: “Na kitabu kitawekwa ndipo utawaona waovu wakiogopa kwa sababu ya yale yaliyomo. Na watasema:

وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا ﴿٤٩﴾

“Ole wetu! Kina nini kitabu hiki hakiachi dogo wala kubwa ila kinalihesabu? Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa. Na Mola wako hadhulumu yoyote.” Juz. 15 (18:49).

Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inadi, Azuiaye heri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka, ambaye amemfanya mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu.

Katika Aya 21, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema: “Na itakuja kila nafsi pamoja na mpelekaji na shahidi,” na katika Aya tuliyo nayo, anasimulia kuwa atamwambia mpelekaji na shahidi, mchukue kwenye Jahannam aliyenishirikisha, akaikufuru haki na akaifanyia inadi, akaipinga heri na akawazulilia watu nayo.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) atarudia na kusisitiza:Basi mtupeni katika adhabu kali.

Ilivyo ni kuwa hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amempa sifa ya mwenye kuzuia heri yule mwenye kuruka mipaka, anayetia shaka. Na mahali pengine amempa sifa ya mwenye dhambi:

مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ ﴿١٢﴾

“Azuiaye heri arukaye mipaka, mwenye dhambi” (68:12).

Tukiunganisha Aya hizi na ile isemayo:

إِنَّ شَجَرَتَ الزَّقُّومِ ﴿٤٣﴾ طَعَامُ الْأَثِيمِ ﴿٤٤﴾ كَالْمُهْلِ يَغْلِي فِي الْبُطُونِ ﴿٤٥﴾ كَغَلْيِ الْحَمِيمِ ﴿٤٦﴾

“Hakika Mti wa Zaqqum, Ni chakula cha mwenye dhambi, kama mafuta mazito, hutokota matumboni kama kutokota kwa maji ya moto.” Juz. 25 (44:43-46).

Tukiunganisha zote hizo inatubainikia kuwa kosa la kuzuia heri halina mfano na kosa lolote na kwamba adhabu yake haina kipimo.

Mwenzake aseme: Ee Mola wetu! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotevu wa mbali.

Mwenzake huyu sio yule mwenzake wa kwanza. Yule wa kwanza alikuwa ni katika waandishi wema, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.”

Ama huyu rafiki wa pili ni katika maibilisi ambao Mwenyezi Mungu amewaashiria kwa kauli yake: “Anayeifanyia upofu dhikri ya Mwingi wa rehema tutamwekea Shetani kuwa ndiye rafiki yake.” Juz. 25 (43:36).

Dalili ya kuwa marafiki ni tofauti ni kauli ya rafiki wa pili: “Sikumpoteza.” Kwa sababu yule rafiki wa kwanza haiwezekani kupoteza, kwa hiyo hawezi kukana, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemchagua kuandika kutokana na uaminifu wake.

Zaidi ya hayo ni kuwa kubishana kesho kutakuwa baina ya wakosefu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Msigombane mbele yangu.” Pia kauli yake: “Siku hiyo marafiki watakuwa maadui, wao kwa wao, isipokuwa wenye takua.” Juz. 25 (43:67).

Aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikwishawatangulizia kiaga changu.

Maneno yanatoka kwa Mwenyezi Mungu akiyaelekeza kwa mkosefu na rafiki yake shetani. Maana ni kuwa msianze kuambiana, wewe umenipoteza na mwingine naye aseme sikukupoteza. Kwani leo ni siku ya hisabu na malipo; wala mtu hatanufaika na maneno wala na mengine isipokuwa matendo mema tu; nami niliwawapa mwito wake na nikawahadharisha na siku ya leo kwa atakayehalifu, lakini mkakataa isipokuwa ukafiri.

Kwangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja.

Makusudio ya kauli hapa ni amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa mpelekaji na shahidi: “Mtupeni katika Jahannam kila kafiri mwenye inadi.”

Kutupwa huku kutakuwa tu na ni uadilifu. Kutakuwa, kwa vile ni amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) wala hakuna mabadiliko katika amri yake. Ni uadilifu kwa sababu mkosefu anastahiki hivyo.

Unaweza kuuliza : maulama wengi wamesema kuwa inawezekana kwa Mwenyezi Mungu kuhalifu kiaga (ahadi ya kuadhibu), lakini haiwezekani kuhalifu ahadi; (ahadi ya mazuri) kama ilivyo katika Hadith, aliposema:“Mwenye kumwahidi yoyote kumlipa uzuri, ni lazima atekeleze, na mwenye kumwahidi ubaya, basi ana hiyari.”

Zaidi ya hayo ni kuwa kiakili ni vizuri kutekeleza ahadi, lakini si vibaya kuhalifu kiaga. Sasa kuna wajihi gani wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: ‘Kwangu haibadilishwi kauli?’

Baadhi ya maulama wamejibu kuwa : Mwenyezi Mungu hasamehi hivi hivi tu, bali ni kwa sababu. Pia kusamehe si kubadilisha kauli. Nasi tunaongezea kwenye jawabu hili kuwa makusudio ya kiaga hapa ni kiaga cha adhabu ya mwenye kuzuia heri, na sio kila kiaga. Kwa sababu mruka mipaka huyu mwenye dhambi, tunavyodhani, ni kuwa hana kafara wala muombezi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Siku tutapoiambia Jahannamu: Je, umejaa? Nayo iseme Je, kuna ziada?

Hiki ni kinaya cha ukali wa muwako wake na ukali wa adhabu yake, na kwamba haiwi na msongomano wa wenye hatia kwa idadi yoyote watakayokuwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameipa Jahannam sifa kadhaa za kutisha zinazosisimua ngozi za wale wanaomwogopa Mola wao. Ama wale walio na maradhi nyoyoni mwao, wanadharau sifa hizo na wale wanaoziamini.

Na Pepo italetwa karibu kwa wenye takua, haitakuwa mbali.

Hii ni njia ya Qur’an, inaunganisha malipo ya muovu na mwema. Huko ni shida na machungu na hapa ni raha na nema na Pepo. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu: ‘Haitakuwa mbali,’ ni kutilia mkazo neno kuletwa karibu.Makusudio ya kuletwa karibu Pepo kwa wenye takua ni kuwa ni yao na wao ni wa hiyo.

Haya ndiyo mnayoahidiwa.

Mlijua enyi wenye takua ahadi ya Mwenyezi Mungu naye ameitekeleza. Basi chukueni neema hii isiyokuwa na mpaka wa sifa wala kufikiwa na akili.

Kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu ajilindae. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema kwa ghaibu, na akaja kwa moyo ulioelekea.

Sifa hizi nne ni alama za kujulisha mwenye takua: kuwa ni kutubia akijiweka mbali na maasi, kumhofia Mwenyezi Mungu na kudumu kumtii kwa kutumai thawabu zake, akiwa kwenye imani yake na ikhlasi yake kwenye njia moja; ni sawa awe mbele ya watu au akiwa mbali; kinyume na yule mwenye kujionyesha, mwenye ria.

Anakuwa mvivu akiwa peke yake na na anakuwa mchangamfu mbele ya watu. Huyo ndiye mwenye takua ambaye anamwelekea Mwenyezi Mungu kwa moyo ulio salama.

Kwa maneno mengine ya Imam akimsifu mwenye takua:

“Amemtii anayemwonogoza na akaijiepusha na anayempoteza; akapata njia salama kwa busara ya anayemuonyesha na kutii amri ya anayemwongoza. Akaharakisha kwenye uongofu kabla ya kufungwa milango yake na kuisha nyenzo zake.”

Ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima. Humo watapata wakitakacho, na kwetu kuna ziada.

Nyinyi wenye takua mtakuwa katika Pepo isiyokatika neema yake, hachoki mkazi wake, hazeeki anayedumu wala hakati tamaa mkazi wake. Mtapata zaidi ya manyoyatamani na kuyapendekeza.

Baada ya hayo, ni kuwa tofauti hii baina ya Pepo na Moto inafichua tofauti iliyopo baina ya wenye takua na wenye hatia na kwamba tofauti yao mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na tofauti ya Pepo na Moto.

وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هُمْ أَشَدُّ مِنْهُم بَطْشًا فَنَقَّبُوا فِي الْبِلَادِ هَلْ مِن مَّحِيصٍ ﴿٣٦﴾

36. Na karne ngapi tuliziangamiza kabla yao waliokuwa na nguvu zaidi kuliko wao. Nao walizunguka katika miji. Je, yako makimbilio?

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ ﴿٣٧﴾

37. Hakika katika hayo kuna ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.

وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ ﴿٣٨﴾

38. Na hakika tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita; na wala haukutugusa uchovu.

فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ ﴿٣٩﴾

39. Basi vumilia kwa hayo wasemayo na msabihi Mola wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ ﴿٤٠﴾

40. Na katika usiku msabihi na baada ya kusujudu.

وَاسْتَمِعْ يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ ﴿٤١﴾

41. Na sikiliza siku ataponadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu.

يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ ﴿٤٢﴾

42. Siku watakaposikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kutoka.

إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَإِلَيْنَا الْمَصِيرُ ﴿٤٣﴾

43. Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.

يَوْمَ تَشَقَّقُ الْأَرْضُ عَنْهُمْ سِرَاعًا ذَٰلِكَ حَشْرٌ عَلَيْنَا يَسِيرٌ ﴿٤٤﴾

44. Siku itapowapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.

نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِجَبَّارٍ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَن يَخَافُ وَعِيدِ ﴿٤٥﴾

45. Sisi tunajua sana wayasemayo. Wala wewe si jabari juu yao. Basi mkumbushe kwa Qur’an anayeogopa kiaga.

SIKU ATAKAPONADI MWENYE KUNADI

Aya 36 – 45

MAANA

Na karne ngapi tuliziangamiza kabla yao waliokuwa na nguvu zaidi kuliko wao. Nao walizunguka katika miji. Je, yako makimbilio?

Karne ni watu wa zama moja. Maana ni kuwa katika zama zilizopita kulikuwa na uma nyingi zilizokuwa na maendeleo, nguvu na idadi ya watu wengi kuliko wale waliokukadhibisha wewe Muhammad! Pia walikuwa na mawasiliano na miji mingine. Lakini yote hayo hayakuwafaa waliposhukiwa na adhabu, wala hawakupata pa kuikimbia amri ya Mwenyezi Mungu. Je, watu wako hawaogopi kuwasibu yaliyowasibu waliopita?

Maana haya yamekaririka kwenye Aya nyingi; ikiwemo: Juz. 21 (30:9).

Hakika katika hayo kuna ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye ni shahidi.

Hayo ni hayo ya kukumbushwa maangamizi ya waliopita. Mwenye moyo ni moyo salama. Kutega sikio ni kusikiliza kwa makini. Shahidi ni yule aliyepo kimoyo na kiakili. Maana ni kuwa yale tuliyoyataja ya maangamizi ni mawaidha tosha kwa mwenye busara na akazingatia.

Na hakika tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake katika siku sita; na wala haukutugusa uchovu

Siku sita ni kinaya cha mikupuo au maendeleo ya kugeuka ulimwengu kutoka hali moja hadi nyingine. Tazama Juz. 8 (7:54).

Basi vumilia kwa hayo wasemayo, ya ubatilifu na usafihi. Kwa sababu mwisho ni wa wenye kuvumilia uvumilivu wa kiungwana.

Na msabihi Mola wako kabla ya kuchomoza jua. Hiyo ni ishara ya swala ya Alfajiri.Na kabla ya kuchwa, ni swala ya adhuhuri na alasiri.

Na katika usiku msabihi, ni swala ya magharibi na isha. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:130).Na baada ya kusujudu, ni ishara ya uradi baada ya swala na swala za sunna baada ya kumaliza za wajibu.

Na sikiliza siku ataponadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu. Siku watakaposikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kutoka.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w. w ) . Siku atakayonadi, hapo kuna maneno ya kukadiriwa; yaani sikiliza masimulizi ya siku atakayonadi; na wala sio kusikiliza mnadi. Makusudio ya mahala karibu ni kuwa huo mwito watausikia wote; kama kwamba mnadi yuko karibu nao, ingawaje ukelele unatoka mbinguni.

Hapa ndio inatubainikia njia ya kuchanganya na kuafikiana baina ya Aya hii na ile isemayo:

أُولَـٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ ﴿٤٤﴾

“Hao wanaitwa kutoka mahali mbali.” Juz. 24 (41:44).

Maana ni kuwa, sikiza tunayokusimulia ewe Muhammad kuhusiana na ukulele wa ufufuo kwa ajili ya hisabu na malipo. Ukulele huu uko mbali, ukitokea mbinguni na uko karibu kwa kuwa unafika kwenye masikio yote, mpaka ya wafu, watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika:

هُنَالِكَ تَبْلُو كُلُّ نَفْسٍ مَّا أَسْلَفَتْ وَرُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٣٠﴾

“Huko kila nafsi itajua iliyoyatanguliza na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki, na yote waliyokuwa wakiyazua yatawapotea.” Juz. 11 (10:30)

Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.

Uhai na mauti yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye ndio marejeo ya viumbe. Umetangulia mfano wake mara nyingi; kama vile katika Juz. 11(10:56).

Siku itapowapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.

Ardhi itawapasukia wa kwanza na wa mwisho, watoke makaburini mwao upesi upesi; wakiwa ni wengi kuliko chunguchungu na machanga. Atakayekuwa na hali nzuri kuliko wengine ni yule atakayepata mahali pa kuweka unyayo wake na pa kuvutia pumzi zake; kama alivyosema Imam Ali(a . s) .

Sisi tunajua sana wayasemayo, ya kumkadhibisha Mtume na kukana ufufuo.Wala wewe si jabari juu yao, kuwalazimisha kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho. Wewe ni muonyaji tu.

Basi mkumbushe kwa Qur’an anayeogopa kiaga na yule asiyeogopa pia ili utoe hoja. Mwenyezi Mungu amemuhusisha kumtaja anayeogopa kwa kuashiria kuwa yeye ananufaika na ukumbusho zaidi kuliko asiyeogopa:

فَذَكِّرْ إِن نَّفَعَتِ الذِّكْرَىٰ ﴿٩﴾ سَيَذَّكَّرُ مَن يَخْشَىٰ ﴿١٠﴾ وَيَتَجَنَّبُهَا الْأَشْقَى ﴿١١﴾

“Kumbusha ikiwa kutafaa huko kukumbusha. Atakumbuka mwenye kucha na atajiepusha nako muovu.” 87: (9-11).

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Atajiepusha nako muovu,’ ni dalili mkataa kuwa amri ya kukumbusha ni ya ujumla, iwe kutafaa au hakutafaa.

MWISHO WA SURA YA HAMSINI: SURAT QAF