TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 26019
Pakua: 3246


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 26019 / Pakua: 3246
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

Mwandishi:
Swahili

17

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sitini Na Tisa: Surat Al-Haqqa. Imeshuka Makka. Ina Aya 52.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

الْحَاقَّةُ ﴿١﴾

1. Tukio la haki.

مَا الْحَاقَّةُ ﴿٢﴾

2. Nini hilo Tukio la haki?

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْحَاقَّةُ ﴿٣﴾

3. Na nini kitachokujulisha tukio la haki ni nini?

كَذَّبَتْ ثَمُودُ وَعَادٌ بِالْقَارِعَةِ ﴿٤﴾

4. Thamudi na A’di walikad­hibisha tukio linalogonga.

فَأَمَّا ثَمُودُ فَأُهْلِكُوا بِالطَّاغِيَةِ ﴿٥﴾

5. Basi Thamudi waliangamizwa kwa tukio kubwa mno.

وَأَمَّا عَادٌ فَأُهْلِكُوا بِرِيحٍ صَرْصَرٍ عَاتِيَةٍ ﴿٦﴾

6. Na ama A’di waliangamizwa kwa upepo mkali wenye nguvu.

سَخَّرَهَا عَلَيْهِمْ سَبْعَ لَيَالٍ وَثَمَانِيَةَ أَيَّامٍ حُسُومًا فَتَرَى الْقَوْمَ فِيهَا صَرْعَىٰ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ خَاوِيَةٍ ﴿٧﴾

7. Aliowapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magogo ya mitende yalio wazi ndani.

فَهَلْ تَرَىٰ لَهُم مِّن بَاقِيَةٍ ﴿٨﴾

8. Basi je, unamwona mmoja wao aliyebaki?

وَجَاءَ فِرْعَوْنُ وَمَن قَبْلَهُ وَالْمُؤْتَفِكَاتُ بِالْخَاطِئَةِ ﴿٩﴾

9. Na Firaun na waliomtangulia, na miji iliyopinduliwa chini juu, walileta hatia.

فَعَصَوْا رَسُولَ رَبِّهِمْ فَأَخَذَهُمْ أَخْذَةً رَّابِيَةً ﴿١٠﴾

10. Wakamuasi Mtume wa Mola wao, ndipo akawakamata kwa mkamato uliozidi nguvu.

إِنَّا لَمَّا طَغَى الْمَاءُ حَمَلْنَاكُمْ فِي الْجَارِيَةِ ﴿١١﴾

11. Maji yalipofurika tuliwapan­disha katika Jahazi.

لِنَجْعَلَهَا لَكُمْ تَذْكِرَةً وَتَعِيَهَا أُذُنٌ وَاعِيَةٌ ﴿١٢﴾

12. Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalosikia liyahifadhi.

فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ نَفْخَةٌ وَاحِدَةٌ ﴿١٣﴾

13. Na itapulizwa parapanda mpulizo mmoja.

وَحُمِلَتِ الْأَرْضُ وَالْجِبَالُ فَدُكَّتَا دَكَّةً وَاحِدَةً ﴿١٤﴾

14. Na ardhi na milima ikaondole­wa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja.

فَيَوْمَئِذٍ وَقَعَتِ الْوَاقِعَةُ ﴿١٥﴾

15. Siku hiyo Tukio litatukia.

وَانشَقَّتِ السَّمَاءُ فَهِيَ يَوْمَئِذٍ وَاهِيَةٌ ﴿١٦﴾

16. Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa.

وَالْمَلَكُ عَلَىٰ أَرْجَائِهَا وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ ﴿١٧﴾

17. Na Malaika watakuwa kandoni mwake; Na wanane juu ya hawa siku hiyo watabeba Arshi ya Mola wako.

يَوْمَئِذٍ تُعْرَضُونَ لَا تَخْفَىٰ مِنكُمْ خَافِيَةٌ ﴿١٨﴾

18. Siku hiyo mtahudhurishwa ­haitafichika siri yoyote yenu.

TUKIO LA HAKI

Aya 1 – 18

MAANA

Tukio la haki. Nini hilo Tukio la haki?

Makusudio ya tukio la haki ni Kiyama. Kimeitwa hivyo kwa sababu ni wajibu kutokea kwake. Ama kuuliza na kukaririka, ni kwa ajili ya kuhofisha ukali wake na vituko vyake; kwamba ni tukio ambalo masikio hayajawahi kusikia, macho haya­japata kuona wala akili haijawahi kuwazia. Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akalirudia swali kwa kusema: Na nini kitakujulisha nini hilo Tukio la haki?

Thamudi na A’di walikadhibisha tukio linalogonga.

Thamud ni watu wa Swaleh na A’d ni watu wa Hud. Tukio linalogonga ni katika majina ya Kiyama, kama tukio la haki.

Basi Thamudi waliangamizwa kwa tukio kubwa mno, ambalo ni ukelele wa adhabu. Umeitwa hivyo kwa sababu ya ukali wake.

Na ama A’di waliangamizwa kwa upepo mkali wenye nguvu, wenye kuangamiza.

Aliowapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo.

Upepo uliendelea kwa muda huo bila ya kusita.

Utaona watu wamepinduka ardhinikama kwamba ni magogo ya mitende yalio wazi ndani.

Kila aliye maiti ni gogo lilio wazi; hata kama amevaa hariri.

Basi je, unamwona mmoja wao aliyebaki?

Hapana! Hakuna atakayebaki. Yametangulia maelezo kuhusu A’d na Tahamud kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 8 (7:65-79), Juz. 12 (11:50-68) na Juz. 19 (26:123-1590).

Na Firaun na waliomtangulia, na miji iliyopinduliwa chini juu, walile­ta hatia. Wakamuasi Mtume wa Mola wao, ndipo akawakamata kwa mkamato uliozidi nguvu.

Miji iliyopinduliwa ni miji ya watu wa Lut. Maana yake kwa ufupi ni kuwa Firaun na watu wake na mfano wao katika wale waliotangulia, wakiwemo watu wa Lut, waliwakadhibisha manabii wa Mwenyezi Mungu na mitume wake, na wakafanya vitendo vya hatia; ndio Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa adhabu iliyopita kiasi cha kufikiriwa. Aya na Sura za kumzungumzia Firaun na watu wake ni nyingi; zikiwemo zile zilizo katika Juz. 9 (7:103-137). Vile vile yametangulia maelezo kuhusu Lut na watu wake mara kadhaa; yakiwemo yale yaliyo katika Juz. 8 (7:80-84).

Maji yalipofurika tuliwapandisha katika Jahazi.

Makusudio ya jahazi hapa ni Safina ya Nuh. Hapa kuna maneno ya kukadiriwa; yaani tuliwachukua mababu zenu waumini katika Safina ya Nuh. Vile vile masimulizi kuhusu Nuh na Safina yake, yametangulia mara kadhaa; kama, katika Juz. 8 (7:59-64).

Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu.

‘Hayo’ ni hayo ya kisa cha Nuh na Safina yake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyakariri kwenye Kitabu chake ili ajue kila mtu kwamba lau si Safina ya Nuh, Adam na Hawa wasingebakiwa na watoto baada ya Tufani. Abul­A’lai ameenda mbali pale alipodai angelikuwa tasa mama yetu Hawa. Kwa sababu kuweko sisi ni neema; kama alivyosema Aristotle na wanafunzi wake.

Na kila sikio linalosikia liyahifadhi.

Kwenye tafsri nyingi za kale na za sasa; ikiwemo ya Razi na ya Sheikh Maraghi, imeelezwa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alimwambia Ali bin Abu Twalib: “Mimi nimemuomba Mwenyezi Mungu ajalie masikio yako ewe Ali.” Imam Akasema: “Sikusikia chochote nikakisahau, na wala sikuwa ni mwenye kusahau.”

Na itapulizwa parapanda mpulizo mmoja.

Kupulizwa parapanda ni kinaya cha ukelele wa kutoka makaburini. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ ﴿٤٢﴾

“Siku watakaposikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kutoka.” Juz. 26 (50:42).

Katika Juz. 24 (39:68), tumetaja maoni ya wafasiri kuhusiana na Parapanda, na kwamba mipulizo itakuwa mitatu: Mpulizo wa fazaa, wa mauti na wa kufufuliwa.

Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja.

Hiki ni kinaya cha kuharibika ardhi na vilivyomo ardhini siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Na milima itakuwa kama tifutifu la mchanga.” (73:14). Yaani itakuwa kama michanga inayokwenda na upepo.

Siku hiyo Tukio litatukia.

Parapanda ikipulizwa na ardhi na majabali yakivunjwavunjwa, hapo ndio kitasimama Kiyama na wakadhibishaji watajua kuwa ni haki isiyokuwa na shaka.

Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa.

Kitachoipata ardhi na mbingu vile vile kitaipata mbingu:

يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ﴿٤٨﴾

“Siku itakapobadilishwa ardhi kuwa ardhi nyingine na mbingu (pia).” Juz. 14 (14:48).

Yaani mbingu pia itabadilishwa.

Na Malaika watakuwa kandoni mwake ; yaani kandoni mwa mbingu. Maana ni kuwa baada ya kuharibika ardhi na mbingu Malaika watatawan­yika huku na huko katika pambizo za anga.

WABEBAJI ARSHI

Na wanane juu ya hawa siku hiyo watabeba Arshi ya Mola wako.

Je, Mwenyezi Mungu ana kiti cha enzi anachokikalia, kama wafanyavyo masultani na watawala? Watu wadhahiri ya herufi wanasema: Ndio, Yeye ana masikio, macho, mguu na viungo vinginevyo.

Abu Amir Alqurashi amenasibishiwa kauli ya kuwa: Mwenyezi Mungu ni mfano wangu na wako katika umbo lake na sura yake.

Hili haliwezekani kabisa; lau angelikuwa na mwili angelihitajia kuwa na mahali, na muumba hahitajii chochote; isipokuwa chochote ndio kinamhi­tajia Yeye. Vile vile hili litahitajia awe na mahali pawe na zama, na hakuna uzamani ila Mwenyezi Mungu; na mengineyo waliyooyataja wana filosofia na wanateolojia.

Wengine wakasema: “Sisi hatujui Arshi ilivyo wala itakavyobebwa, na wala Mwenyezi Mungu hakutukalifisha kulijua hilo.” Kauli hii ni ya kujitoa shakani (Ihtiyat), kama wasemavyo mafaqihi wenye takua.

Tulipotaamali maana ya Aya hii tulifunukiwa kuwa makusudio ya Arshi (kiti cha enzi) ni utawala; kama tulivyotangulia kuashiria katika Juz. 8 (7:54) na makusudio ya wabebaji arshi ni viumbe vinavomilikiwa na Mwenyezi Mungu. Hilo linatambulika kutokana na yaliyosemwa kwenye

ahjul-balagha: “Na lau si mbingu kumkubali Mwenyezi Mungu kwa uungu na kumtii, asingelizijaalia ni mahali pa Arshi Yake.” Yaani lau sikuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anazitumia mbingu vile atakavyo, zisingelikuwa ni milki Yake. Kwa hiyo kutumia atakavyo ni dalili ya umiliki; kama amabavyo umiliki unapelekea utumizi huu.

Kwa hiyo basi kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na watabeba Arshi ya Mola wako,” inashabihiana na jawabu la swali la anayeuliza: Kama mbingu na ardhi ikiondoka itamaanisha ufalme wa Mwenyezi Mungu umeondoka na hakuna kitu anachokitawala?

Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajibu: Hapana! Kuna viumbe vingine visivyokuwa mbingu na ardhi ambavyo ni vinane, vikiwa kwenye amani na salama, anavitumia Mwenyezi Mungu (s.w.t) vile apendavyo baada ya kupomoka ardhi na mbingu.

Tunasema hivi, kama fikra tuliyoitoa kutoka kwenye neno: ‘Watabeba.’ Fikra hii ‧ kama uinavyo ‧ inawezekana, lakini hii na mfano wake haithibiti isipokuwa kwa nukuu wazi inayofahamisha kwa mkato. Lau ingelikuwa ni katika mlango wa halali na haramu, ingelikuwa dhana ya mwanafiqhi ina njia, kama itategemezwa kwenye dhahiri ya kitabu au sunna.

Siku hiyo mtahudhurishwa -haitafichika siri yoyote yenu.

Viumbe watahudhurishwa kwa Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama, kwa ajili ya hisabu na kutekelezewa kila mtu malipo yake. Na Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamjua zaidi aliyeongoka na aliyepotea njia yake.

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَءُوا كِتَابِيَهْ ﴿١٩﴾

19. Basi ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!

إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ ﴿٢٠﴾

20. Hakika nilijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu.

فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ ﴿٢١﴾

21. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhia.

فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ ﴿٢٢﴾

22. Katika Bustani ya juu.

قُطُوفُهَا دَانِيَةٌ ﴿٢٣﴾

23. Matunda yake yako karibu.

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا أَسْلَفْتُمْ فِي الْأَيَّامِ الْخَالِيَةِ ﴿٢٤﴾

24. Kuleni na kunyweni kwa fura­ha kwa sababu ya mlivyotan­guliza katika siku zilizopita.

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ ﴿٢٥﴾

25. Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto, Basi atasema: Laiti nisingelipewa kitabu changu!

وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيَهْ ﴿٢٦﴾

26. Wala nisingelijua nini hisabu yangu.

يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ ﴿٢٧﴾

27. Laiti (mauti) yangelimaliza.

مَا أَغْنَىٰ عَنِّي مَالِيَهْ ﴿٢٨﴾

28. Mali yangu hayakunifaa kitu.

هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيَهْ ﴿٢٩﴾

29. Madaraka yangu yamenipotea.

خُذُوهُ فَغُلُّوهُ ﴿٣٠﴾

30. Mshikeni na mumtie pingu!

ثُمَّ الْجَحِيمَ صَلُّوهُ ﴿٣١﴾

31. Kisha mtupeni Motoni!

ثُمَّ فِي سِلْسِلَةٍ ذَرْعُهَا سَبْعُونَ ذِرَاعًا فَاسْلُكُوهُ ﴿٣٢﴾

32. Tena mtieni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabini!

إِنَّهُ كَانَ لَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ الْعَظِيمِ ﴿٣٣﴾

33. Hakika yeye alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu.

وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿٣٤﴾

34. Wala hahimizi kulisha masiki­ni.

فَلَيْسَ لَهُ الْيَوْمَ هَاهُنَا حَمِيمٌ ﴿٣٥﴾

35. Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu.

وَلَا طَعَامٌ إِلَّا مِنْ غِسْلِينٍ ﴿٣٦﴾

36. Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni.

لَّا يَأْكُلُهُ إِلَّا الْخَاطِئُونَ ﴿٣٧﴾

37. Chakula hicho hawakili ila wenye hatia.

LAITI YANGELIKUWA NI YAKUMALIZA

Aya 19 – 37

MAANA

Basi ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu! Hakika nilijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameeleza kuwa siku hiyo watu watahudhurisha. Hapa anabainisha tofauti baina ya watu wa kulia na wa kushoto. Makusudio ya kulia ni heri na kushoto ni shari, kwa kuangalia desturi ya waarabu na istilahi yao. wao wanaita kulia ni heri na kushoto ni shari. Walikuwa wakitabiri kwa kumrusha ndege, akiruka upande wa kuliawanona ni heri na akiruka upande wa kushoto wanaona ni shari[7] .

Kwa hiyo basi maana ni kuwa wema siku ya Kiyama watajitangaza wenyewe kwa fakhri na utukufu, na watamwambia watakayemuona au atakayewauliza hali zao: Ona tulivyo! Hebu soma daftari la matendo yetu! Sisi tulikuwa tukimwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na tulikuwa tukiwekeza kwa ajili ya siku hiyo.

Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhia, yaani yenye kuridhiwa, yasiyokuwa na bughdha yoyote.Katika Bustani ya juu, matunda yake yako karibu. Waambiwe:

Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa sababu ya mlivyotanguliza katika siku zilizopita . Huu ni ufafanuzi baada ya ujumla; kama kwamba mtu ameuliza: Ni maisha gani hayo ya kuridhiwa? Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajibu kuwa ni Pepo ya daraja ya juu, matunda yake yako chinichini kuweza kuchumwa na kuliwa na Malaika watawaambia watu wa Peponi: Kuleni matunda ya Peponi na kunyweni katika kinywaji chake kwa raha, yakiwa ni malipo ya mema mliyoyatenda.

Mwenyezi Mungu ameanzia na tamko la mmoja, kwa kusema atakuwa katika maisha ya kuridhia, na kumalizia na tamko la wengi kwa kusema: Kuleni; kwa kuangalia maana yake ambayo ni wengi.

Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto.

Huyu ni yule aliyoekadhibisha hisabu na malipo, akapituka mipaka na kuwafanyia dhulma waja. Mwenyezi Mungu amemueleza kwa ibara ya kushoto kwa kuashiria kuwa matendo yake yatamrudia kwa shari; kama tulivyotangulia kueleza.

Basi atasema: Laiti nisingelipewa kitabu changu! Wala nisingelijua nini hisabu yangu. Laiti (mauti) yangelimaliza. Mali yangu hayakuni­faa kitu, madaraka yangu yamenipotea.

Atatamani lau asingelikuwa ameumbwa au asingelifufuliwa kutoka kaburi­ni kwake. Atatamani hivyo baada ya kuwa na uhakika wa adhabu isiy­oweza kukingwa kwa mali wala jaha. Wala si hoja kuwa anamiliki vyote hivyo; isipokuwa ni matamanio ya kukata tamaa.

Hakuna kitu chochote baada hayo isipokuwa kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:Mshikeni na mumtie pingu! Mfungeni mikono yake kwenye shingo yake.Kisha mtupeni Motoni! Kwenye Jahannam.

Tena mtieni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabini!

Dhiraa sabini ni kinaya cha uchungu wa adhabu yake. Na ukali wake unapimwa kwa matendo yake na athari aliyoiacha katika jamii. La kushangaza ni kauli ya mfasiri mmoja aliyesema: “Wametofautiana kuhusu dhiraa hii. Ikasemekana ni dhiraa hasa inayojulikana.

Ikasemekana ni dhi­raa ya malaika wa adhabu. Pia imesemekana dhiraa moja ni kipimo cha kuanzia Makka hadi Kufa.” Sijui aliyeyasema hayo ni mtu wa Makka au Kufa?

Hakika yeye alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Wala hahimizi kulisha masikini.

Huu ni ubainifu wa sababu inayowajibisha adhabu kali; kwamba ni kufuru, uasi na kutohimiza kutoa. Hapa kuna ishara ya kuwa matajiri wanatakikana watoe na wahimize kutoa.

Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu.

Hakuna wa karibu wa kunufaisha wala yeyote wa kuombea.

Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni, unaotoka kwenye mili yao.

Chakula hicho hawakili ila wenye hatia , waliokuwa duniani wakila vyakula vya wanyonge.

فَلَا أُقْسِمُ بِمَا تُبْصِرُونَ ﴿٣٨﴾

38. Basi naapa kwa mnavoviona.

وَمَا لَا تُبْصِرُونَ ﴿٣٩﴾

39. Na msivyoviona.

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿٤٠﴾

40. Kwa hakika hii ni kauli ya Mjumbe mwenye hishima.

وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَاعِرٍ قَلِيلًا مَّا تُؤْمِنُونَ ﴿٤١﴾

41. Wala si kauli ya mshairi. Ni machache mnayoyaamini.

وَلَا بِقَوْلِ كَاهِنٍ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٤٢﴾

42. Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayoyakumbu­ka.

تَنزِيلٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٣﴾

43. Ni uteremsho utokao kwa Mola wa walimwengu wote.

وَلَوْ تَقَوَّلَ عَلَيْنَا بَعْضَ الْأَقَاوِيلِ ﴿٤٤﴾

44. Na lau kama angelituzulia baadhi ya maneno,

لَأَخَذْنَا مِنْهُ بِالْيَمِينِ ﴿٤٥﴾

45. Bila ya shaka tungelimshika kwa mkono wa kulia.

لَقَطَعْنَا مِنْهُ الْوَتِينَ ﴿٤٦﴾

46. Kisha kwa hakika tunge­limkata mshipa mkubwa wa moyo!

فَمَا مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ عَنْهُ حَاجِزِينَ ﴿٤٧﴾

47. Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeliweza kutuzuia naye.

وَإِنَّهُ لَتَذْكِرَةٌ لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٤٨﴾

48. Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wenye takua.

وَإِنَّا لَنَعْلَمُ أَنَّ مِنكُم مُّكَذِّبِينَ ﴿٤٩﴾

49. Na hakika bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanaokad­hibisha.

وَإِنَّهُ لَحَسْرَةٌ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٥٠﴾

50. Na hakika hii bila ya shaka itakuwa ni masikitiko kwa wanaokataa.

وَإِنَّهُ لَحَقُّ الْيَقِينِ ﴿٥١﴾

51. Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini.

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ ﴿٥٢﴾

52. Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

MNAVYOVIONA NA MSIVYOVIONA

Aya 38 – 52

MAANA

Basi naapa

Wafasiri wengi wamesema kuwa herufi lU hapa ni ziyada kiirabu ya nahau. Bali wengine wamesema kuwa herufi lU hapa ni ya asili, na kwamba maana yake ni ‘Siapi,’ kwa vile jambo liko wazi lisilohotajia kiapo. Maelezo zaidi yametangulia kwenye Juz. 27 (56:75)

Kwa mnavyoviona, na msivyoviona.

Hii inachaanganya ulimwengu wa ghaibu na unaoonekana; yaliyokuwa na yatakayokuwa duniani na Akhera. Hiyo hasa ni kuapa kwa ilimu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t), ambayo imekizunguka kila kitu; miongoni mwayo ni:

Kwa hakika hii Qur’anni kauli ya Mjumbe mwenye hishima. Wala si kauli ya mshairi. Ni machache mnayoyaamini. Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayoyakumbuka. Ni uteremsho utokao kwa Mola wa walimwengu wote.

Muhammad(s.a.w.w) ametamka Qur’an hilo hali shaka, lakini hakutamka kama mshairi au kuhani wala kwa sifa zozote za kibinadamu, isipokuwa aliitamka kama msemaji wa Mwenyezi Mungu. Tumezungumzia kwa ufufanuzi zaidi kuhusu ushairi na Mtume katika Juz. 19 (26:224).

Kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ni machache manyoyaamini, ni machache mnaoyakumbuka.” Maana ni kuwa hawaamini wala wahawaidhiki isipokuwa wachache. Imesemkana makusudio yake ni kuwa hawakuamini wala kukumbuka, wachache wala wengi.

Hiyo ni kufuata desturi ya waarabu wanaosema: “Ni mara chache kufanya; kwa maana hafanyi kabisa. Tafsiri ya kwanza ndio iliyo karibu zaidi na uhalisia, kwa sababu ilivyo ni kuwa baadhi ya washirikina walimwamini Mtume(s.a.w.w) kabla ya kuhamia Madina. Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (1:88).

Unaweza kuuliza : Je, kuapa tu kunathibisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa Muhammad(s.a.w.w) , na kukana ushairi na ukuhani?

Jibu : Kiapo hiki kimekuja baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataka wakadhibishaji walete mfano wa Qur’an, baada ya kushindwa na hoja. Kwa hiyo makusudio ya kuapa ni kusisitiza haki yenye kuthibiti na dalili, sio kuthibitisha haki kwa kiapo.

Zaidi ya hayo ni kuwa kujadiliana na mpinzani kuna mifumo mbalimbali na kunatofautiana kulingana na fikra na hali. Miongoni mwa mifumo hiyo ni kuleta dalili kwa hoja, kuleta maswali yanaolingana na itikadi na ufasaha wa mfumo. Vile vile kuapa huwa kunaleta hisia na athari.

Na lau kama angelituzulia baadhi ya maneno, bila ya shaka tungelimshika kwa mkono wa kulia, kisha kwa hakika tungelimkata mshipa mkubwa wa moyo! Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeliwe­za kutuzuia naye.

Yaani lau Muhammad angelituzulia tungelimfanya hivyo. Maana ni kuwa Muhammad(s.a.w.w) ni mwenye kutakaswa na wanayomanasibisha nayo washirikina kuwa anamzulia Mwenyezi Mungu uwongo. Lau angelifanya hivyo, basi Mwenyezi Mungu angelimwadhibu kwa adhabu kali kabisa wala kusingelikuwa na mshirikina au mwinginewe kuweza kumwokoa na adhabu.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu hakufanya hivyo, basi inamaanisha kuwa Muhammad(s.a.w.w) ni mkweli mwaminifu, na wazushi ndio waliom­nasibishia Muhammad(s.a.w.w) uzushi.

Unaweza kuuliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawaharakishii adhabu wanomkadhibisha Muhammad, kama atakavyomharakishia Muhammad(s.a.w.w) lau angekuwa muongo?

Jibu : Hakika utishio huu kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwa yule anayedai utume kwa uwongo na uzushi, sio kwa anayekadhibisha utume wa mitume. Tofauti ni kubwa sana baina ya wawili hawa. Zaidi ya hayo utishio wa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake ni kumsafisha Mtume mtukufu na yale wanayomnasibishia ya uzushi, kama tulivyoashi­ria.

Kwa hakika hii Qur’anni mawaidha kwa wenye takua.

Bila shaka ni mwongozo kwa anayetaka kuongoka na akataka kwa ukweli na ikhlasi kujiepusha na ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Na hakika bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanaokadhibisha.

Haya ni makemeo kwa anayemkadhibisha Mtume na Qur’an.

Na hakika hii Qur’anbila ya shaka itakuwa ni masikitiko kwa wanaokataa, kwa sababu inawalani na kuwafedhehsha na kwa sababu neno lake Mwenyezi Mungu liko juu na la makafiri liko chini. Na pia kwa vile ni hoja juu yao siku ya hisabu na malipo.

Na hakika hii Qur’an bila ya shaka ni haki ya yakini, isiyokuwa na shaka yoyote. Umetangulia mfano wake katika Juz. 27 (56:95).

Basi lisabihi jina la Mola wako aliye Mkuu.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) , na makusudio ni kwa wote. Maana ni mtakaseni Mwenyezi Mungu na yale yasiyokuwa laiki yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 27 (56:75).

MWISHO WA SURA YA SITINI NA TISA: SURAT AL-HAQQA