TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 26032
Pakua: 3249


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 26032 / Pakua: 3249
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

Mwandishi:
Swahili

18

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sabini: Surat Al- Maa’rij. Ina Aya 44. Imeshuka Makka.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

سَأَلَ سَائِلٌ بِعَذَابٍ وَاقِعٍ ﴿١﴾

1. Mwenye kutaka alitaka adhabu itakayotokea.

لِّلْكَافِرِينَ لَيْسَ لَهُ دَافِعٌ ﴿٢﴾

Kwa makafiri, hapana awezaye kuizuia.

مِّنَ اللَّـهِ ذِي الْمَعَارِجِ ﴿٣﴾

3. Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye daraja.

تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ ﴿٤﴾

4. Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka hamsini elfu!

فَاصْبِرْ صَبْرًا جَمِيلًا ﴿٥﴾

5. Basi subiri kwa subira njema.

إِنَّهُمْ يَرَوْنَهُ بَعِيدًا ﴿٦﴾

6. Hakika wao wanaiona iko mbali.

وَنَرَاهُ قَرِيبًا ﴿٧﴾

7. Na Sisi tunaiona iko karibu.

يَوْمَ تَكُونُ السَّمَاءُ كَالْمُهْلِ ﴿٨﴾

8. Siku ambayo mbingu zitakuwa kama shaba iliyoyayuka.

وَتَكُونُ الْجِبَالُ كَالْعِهْنِ ﴿٩﴾

9. Na milima itakuwa kama sufi.

وَلَا يَسْأَلُ حَمِيمٌ حَمِيمًا ﴿١٠﴾

10. Wala jamaa hatamuuliza jamaa.

يُبَصَّرُونَهُمْ يَوَدُّ الْمُجْرِمُ لَوْ يَفْتَدِي مِنْ عَذَابِ يَوْمِئِذٍ بِبَنِيهِ ﴿١١﴾

11. (Ingawa) watafanywa wao­nane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe.

وَصَاحِبَتِهِ وَأَخِيهِ ﴿١٢﴾

12. Na mkewe, na nduguye.

وَفَصِيلَتِهِ الَّتِي تُؤْوِيهِ ﴿١٣﴾

13. Na ukoo wake uliokuwa ukimzunguka.

وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا ثُمَّ يُنجِيهِ ﴿١٤﴾

14. Na wote waliomo ardhini, kisha aokoke.

كَلَّا إِنَّهَا لَظَىٰ ﴿١٥﴾

15. Sivyo! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa.

نَزَّاعَةً لِّلشَّوَىٰ ﴿١٦﴾

16. Unaobabua ngozi ya kichwa!

تَدْعُو مَنْ أَدْبَرَ وَتَوَلَّىٰ ﴿١٧﴾

17. Utamwita kila aliyoegeuza mgongo na akageuka.

وَجَمَعَ فَأَوْعَىٰ ﴿١٨﴾

18. Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi.

KADIRI YAKE NI MIAKA HAMSINI ELFU

Aya 1- 18

MAANA

Mwenye kutaka alitaka adhabu itakayotokea.

Neno kutaka tumelitarjumu kutokana na neno la kiarabu sa-ala ambalo mara nyingi hutumiwa kwa maana ya kuuliza, lakini pia huwa na maana ya kutaka au kuomba. Huko nyuma tumewahi kueleza kuwa washirikina waliupinga mwito wa Mtume(s.a.w.w) kwa sababu zifuatazo:

1. Ulikua unapingana na chumo na faida zao.

2. Kwamba Mwenyezi Mungu hawezi kumtuma mtu kuwa Mtume, na kama hakuna budi basi atamtuma tajiri sio fukara, kama Muhammad bin Abdillah. Tatu, Muhammad anaamimi Mungu mmoja na wao wanaamini miungu mingi. Nne, kuwa Muhammad anawahofisha na adhabu na ufufuo.

Hili ndilo walilokuwa wakilipinga sana:

أَئِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿٤٧﴾

“Tutakapokufa na tukawa udongo na mifupa, ati ndio tutafufuliwa?” Juz. 27 (56:47).

Na kama Nabii akisisitiza kuuelezea ufufuo, wao husema:

مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٨﴾

“ Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?” Juz. 23 (36:48).

Mara nyingine wanaifanyia haraka adhabu kwa masikhara na kusema:

وَإِذْ قَالُوا اللَّـهُمَّ إِن كَانَ هَـٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِندِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣٢﴾

“Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni haki itokayo kwako, basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.” Juz. 10 (8:32).

Ndio maana wafasiri wengi wamesema kuhusu Aya hii tuliyo nayo kuwa ni ishara ya kutaka kuharakishiwa adhabu, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) naye akawajibu kwa kusema:Kwa makafiri, hapana awezaye kuizuia . Yaani adhabu itashuka tu kwa wapinzani, hapana awezaye kuizuia, wawe wameitaka kwa haraka au kwa muda ujao.

SHETANI NA UTAFITI WA GHAIBU

Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye daraja.

Ni sifa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Makusudio yake ni utukufu. Mfano wake ni: “Ndiye Mwenye daraja za juu, Mwenye Arshi” Juz. 24 (40:15). Imesemekana kuwa maana ya neno maarij, tulilolitarjumu kwa daraja, lina maana ya mbingu.

Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka hamsini elfu!

Makusudio ya Roho hapa ni Jibril. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemhusisha kumtaja, japo yeye ni miongoni mwa malaika, kwa sababu ya cheo chake kikuu. Kwake ni kwenye yale yaliyo maalum mbele yake na kwa malaika. Miaka hamsini elfu ni kinaya cha urefu wa muda.

Ustadh Ahmad Amin Al-Iraqi, ameitaja Aya hii katika kitabu chake Attakamulu fil islam. Akaeleza kuwa malaika wanakwenda kwa kasi kuliko sauti.

Hivyo ni kwa kuwa upeo wa ulimwengu hauna kikomo. Inatosha kuwa ni dalili ya hakika hii, kwamba baadhi ya nyota mwanga wake umeanza kuja ardhini tangu mamilioni ya miaka iliyopita na bado haujafika; ambapo kasi ya mwanga ni kilomita 300000 kwa sekunde. Kwa hiyo basi malaika wasingeweza kukata masafa yaliyo mapana zaidi, kama wasingekua na kasi zaidi sana.

Katika kufasiri Aya 18 ya Sura iliyo kabla ya hii tuliyo nayo: “Na wanane juu ya hawa siku hiyo watabeba Arshi ya Mola wako,” tulisema kuwa maudhui haya na yanayofanana na haya hayathibiti ila kwa nukuu wazi inayofahamisha kwa mkato, bila ya taawili kwa hali yoyote ile.

Lakini ingelikuwa ni katika masuala ya halali na haramu, basi dhana ya faqih ingelikuwa na mwelekeo kama ingelitegemezwa kwenye dhahiri ya Kitabu au Sunna.

Baadhi ya masufi wanasema makusudio ya miaka hamsini elfu sio ile miaka tunayoijua, bali makusudio ni mizunguko. Sufi mwingine naye akasema kuwa siku za Mwenyezi Mungu ziko kama vile anavyotaka, akitaka anazifanya elfu na akitaka anazifanya maelfu na mamilioni.

Hiyo ni ghaibu ndani ya ughaibu. Sisi hatuna majukumu na ilimu ya Mwenyezi Mungu wala hatukalifishwi kuifanyia utafiti isipokuwa shetani.

Imam Ali(a.s) anasema:“Na ilimu ambayo shetani amekutwisha na wajibu wake kwako hauna athari katika Kitabu wala Sunna ya Nabii (s.a.w.w) na maimamu, basi iwakilishe kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa huo ni mwisho wa haki ya Mwenyezi Mungu kwako. Jua kuwa wale waliozama katika elimu ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewatosheleza kwa kutoivamia milango iliyofungiwa ghaibu .

Kukiri jumla ya wasiyoyajua ni tafsiri ya ghaibu iliyofichikana. Mungu akawasifu kwa kukiri kushindwa kutambua yale wasiyoyajua. Amekuita kuacha kuzama katika wasiyokalifishwa, kwa kutafuta kumjua alivyo, kuwa ni kuimarika. Basi tosheka na hayo, wala usiupime utukufu wa Mwenyezi Mungu kwa kipi­mo cha akili yako usije ukawa katika walioangamia.”

Basi subiri kwa subira njema. Hakika wao wanaiona siku ya adhabu kuwaiko mbali, na Sisi tunaiona iko karibu.

Nabii(s.a.w.w) aliwahadharisha washirikina na siku ya adhabu, lakini wakaiharakisha kwa dharau, basi kuwa na subira ewe Muhammad na dha­rau yao hii subira isiyokuwa na malalamiko, wala usione kuwa nusra inachelewa. Siku ya adhabu itakuja tu haina shaka, hata kama wanaibadil­isha kuwa ngano, na kila linalokuja liko karibu.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akasifu siku hiyo waliyooahidiwa na kuidharau kuwa niSiku ambayo mbingu zitakuwa kama shaba iliyoyayuka .

Gimba la mbingu litayeyuka na kuwa kama matope ya mafuta. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَإِذَا النُّجُومُ انكَدَرَتْ ﴿٢﴾

“Na nyota zitakapopukutika.” (81:2).

Na milima itakuwa kama sufi.

Mwenye kuiangalia ataiona kama ni sufi iliyochanguliwa; mfano wake ni kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَبُسَّتِ الْجِبَالُ بَسًّا ﴿٥﴾

“Na milima itaposagwasagwa.” Juz 27 (56:5).

Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake, kwa sababu kila mtu ana shughuli yake itakayomshughulisha. Mwema siku hiyo ni yule atakayejiwekea akiba ya mambo mema.

Ingawa watafanywa waonane.

Yaani hakuna atakayemuuliza mwenzake siku ya Kiyama, hata kama ni marafiki na ndugu, ingawaje wanajuana, lakini watakimbiana kutokana na balaa na majanga ya siku hiyo.

Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwa­toa fidia wanawe, na mkewe, na nduguye, na ukoo wake uliokuwa ukimzunguka, na wote waliomo ardhini, kisha aokoke.

Neno ‘kisha’ linaashiria umbali wa kuokoka. Maana ni kuwa mateka wa Jahannam atatamani lau atafidiwa na watu wote, hata mke na watoto ambao jana alikuwa akiwafidia kwa nafsi yake na kujingiza kwenye hatari kwa ajili yao.

Huu ni ufasaha zaidi wa kuleta picha ya masikitiko ya mkosefu kutokana na yaliyoompita.

Sivyo Enyi wakosefu!Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa, Unaobabua ngozi ya kichwa!

Unaondoa viungo kutoka sehemu yake, kisha unavirudisha tena na unaviondoa, bila ya kikomo:

لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُم مِّنْ عَذَابِهَا كَذَٰلِكَ نَجْزِي كُلَّ كَفُورٍ ﴿٣٦﴾

“Hawahukumiwi wakafa wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyomlipa kila mwenye kuzidi ukafiri” Juz. 22 (35:36).

Utamwita kila aliyegeuza mgongo na akageuka duniani na kuacha mwito wa haki. Makusudio ya kuita Moto ni kuwa hakuna pa kuukimbia.

Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi.

Aya inatoa hadhari na kiaga kwa mwenye kukusanya mali na akawa na pupa nayo na wala asitoe kwa utiifu wa Mwenyezi Mungu.

Kuwachanganya mwenye kulimbikiza mali na mwenye kukadhibisha mwito wa haki, kunajulisha kuwa wote wako sawa mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya hisabu na malipo.

إِنَّ الْإِنسَانَ خُلِقَ هَلُوعًا ﴿١٩﴾

19. Hakika mtu ameumbwa na papara.

إِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ جَزُوعًا ﴿٢٠﴾

20. Inapomgusa shari hupapatika.

وَإِذَا مَسَّهُ الْخَيْرُ مَنُوعًا ﴿٢١﴾

21. Na inapo mgusa kheri huizuil­ia.

إِلَّا الْمُصَلِّينَ ﴿٢٢﴾

22. Isipokuwa wanaoswali,

الَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ دَائِمُونَ ﴿٢٣﴾

23. Ambao wanadumisha Swala zao.

وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَّعْلُومٌ ﴿٢٤﴾

24. Na ambao katika mali yao iko haki maalumu.

لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ ﴿٢٥﴾

25. Kwa mwenye kuomba na anayejizuia.

وَالَّذِينَ يُصَدِّقُونَ بِيَوْمِ الدِّينِ ﴿٢٦﴾

26. Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo.

وَالَّذِينَ هُم مِّنْ عَذَابِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ ﴿٢٧﴾

27. Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao.

إِنَّ عَذَابَ رَبِّهِمْ غَيْرُ مَأْمُونٍ ﴿٢٨﴾

28. Hakika adhabu ya Mola waosi ya kusalimika nayo.

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٢٩﴾

29. Na ambao wanazilinda tupu zao.

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٣٠﴾

30. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume, kwani si wenye kulaumiwa.

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٣١﴾

31. Lakini anayetaka kinyume cha hayo basi hao ndio wapetukao mipaka.

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٣٢﴾

32. Na wale ambao wanachunga amana zao na ahadi zao.

وَالَّذِينَ هُم بِشَهَادَاتِهِمْ قَائِمُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao.

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٣٤﴾

34. Na ambao wanazihifadhi Swala zao.

أُولَـٰئِكَ فِي جَنَّاتٍ مُّكْرَمُونَ ﴿٣٥﴾

35. Hao ndio watakuwa Peponi wakiheshimiwa.

NI NANI HAO WANAOSWALI?

Aya 19 - 35

MAANA

Hakika mtu ameumbwa na papara. Inapomgusa shari hupapatika. Na inapo mgusa kheri huizuilia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa anaashiria kuwa mtu ni dhaifu kwa maumbile yake; kama alivyosema:

وَخُلِقَ الْإِنسَانُ ضَعِيفًا ﴿٢٨﴾

“Na mtu ameumbwa hali ya kuwa dhaifu.” Juz. 5 (4:28)

Na akasema tena:

اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ ضَعْفٍ ﴿٥٤﴾

“Mwenyezi Mungu ndiye ambaye amewaumba katika udhaifu.” Juz. 21 (30:54).

Udhifu huu huwa unajitokeza kwenye sababu zake, kama utajiri na ufukara. Akiwa anajitosheleza basi anakuwa na ubahili na mali yake akihofia ufukara, na akiwa fukara hukata tamaa.

Lakini mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu kikwelikweli na akamategemea Yeye kwa rehema zake, huwa anaushinda udhaifu huu, anakuwa na subira wakati wa shida, kwa subira ya kiungwana akingoja wepesi na faraja na akipata anakuwa mkarimu wa kutoa, akiamini kuwa yalioko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na yenye kubaki.

Kisha Mwenyezi Mungu anataja sifa za waumini kama ifuatavyo:­

1.Isipokuwa wanaoswali, ambao wanadumisha Swala zao.

Hii inafahamisha kuwa hawa hawamo katika kundi la wenye papara na kufazaika. Inafahamaisha wazi kuwa wenye kumswalia Mwenyezi Mungu kiukweli ni wale wanaomtegemea Yeye tu peke yake wala hawamnyenyekei yeyote asiyekuwa Yeye:

“Wewe tu tunakuabudu na wewe tu tunakuomba msaada.”

Ama wale wanasoma takbira na tahalili, kisha wakarukuu na kusujudi kwa ajili ya watu wa jaha na mali kwa tamaa ya yaliyomo mikononi mwao, hawa hawaswali, hata kama watadumu kila siku kwenye faradhi na suna.

2.Na ambao katika mali yao iko haki maalumu kwa mwenye kuomba na anayejizuia.

Maana ni kuwa wanatoa kwa njia ya utiifu na kheri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, hawataki kulipwa wala shukrani. Umetangulia mfano wake katika Juz. 26 (51:19).

3.Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo.

Wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wanafanya kwa mujibu wa imani hii; vinginevyo itakuwa imani ya nadharia tu haifai kitu.

4.Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao. Hakika adhabu ya Mola wao si ya kusalimika nayo.

Mumin anakuwa na matarajio na hofu, anaitazama Pepo kwa makini na Moto pia anautizama kwa makini. Anauhofia huu na wala hakati tamaa na ile. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema: “Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.” Juz. 9 (7:99). Akaendelea kusema:

إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾

“Hakika hawakati tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri.”

Juz. 13 (12:87).

Aliye na dhana nzuri zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni yule anayemhofia zaidi; kama alivyosema Imam Ali(a.s) ; yaani kumhofia Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kiasi cha kujua utukufu wake.

5.Na ambao wanazilinda tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume. Kwani si wenye kulaumiwa. Lakini anayetaka kinyume cha hayo basi hao ndio wapetukao mipaka.

Mumin anatakikana awe na subira na kuridhia mabinti wa Hawa aliopewa na Mwenyezi Mungu, na mumin mwanamke naye anatakiakana awe na subira na aridhie aliyoopewa na Mwenyezi Mungu katika watoto wa Adam. Mwenye kuvumilia na akashukuru basi malipo yake yako kwa Mwenyezi Mungu; vinginevyo mwisho wake ni kukosa Hurula’ini na Pepo. Aya hizi zimetangulia neno kwa neno katika Juz. 18 (23:5-7).

6.Na wale ambao wanachunga amana zao na ahadi zao.

Mumin akiahidi hutekeleza na akiaminiwa hafanyi hiyana, na asiyetekeleza ahadi hana dini wala dhamiri. Vile vile Aya hii imetangulia neno kwa neno katika Juz. 18 (23:8).

7.Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao.

Ushahidi ni amana ya Mwenyezi Mungu kwa shahidi, mwenye kuuficha au kuupindua, atakuwa amemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu:

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَتَمَ شَهَادَةً عِندَهُ مِنَ اللَّـهِ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿١٤٠﴾

“Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule afichaye ushahidi alio nao uto­kao kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na hayo mnayoyafanya.” Juz. 1 (2:140).

8.Na ambao wanazihifadhi Swala zao.

Unaweza kuuliza : Je, hii si ni kurudia Aya iliyotangulia - Ambao wanadumisha Swala zao?

Baahi ya afasiri wamejibu kuwa kudumumisha sio kuhifadhi. Kudumisha ni kuendelea kuswali kila siku na kila wakati wake, lakini kuzihifadhi ni kuzichunga kwa kuzileta kwa masharti yake.

Sisi hatuoni tofauti baina ya kudumisha na kuhifadhi, kwa sababu swala haiwezi kuwa bila ya kuchunga mafungu yake yote na masharti yake, likikosekana mojawapo basi swala imevunjika.

Lililokaribu na ufahamu ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amerudia Aya kwa kiasi cha kutilia mkazo swala na kuzindua kuwa hiyo ni nguzo ya Uislamu.

Hao ndio watakua Peponi wakiheshimiwa.

Hao ni watakaokuwa na sifa zilizotajwa, na kwamba wao watakuwa na daraja na heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.

فَمَالِ الَّذِينَ كَفَرُوا قِبَلَكَ مُهْطِعِينَ ﴿٣٦﴾

36. Wana nini wale waliokufuru wanakujia haraka?

عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ عِزِينَ ﴿٣٧﴾

37. Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto!

أَيَطْمَعُ كُلُّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ أَن يُدْخَلَ جَنَّةَ نَعِيمٍ ﴿٣٨﴾

38. Hivi anatumai kila mmoja wao kuingizwa katika Pepo ya neema?

كَلَّا إِنَّا خَلَقْنَاهُم مِّمَّا يَعْلَمُونَ ﴿٣٩﴾

39. Sivyo! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanachokijua.

فَلَا أُقْسِمُ بِرَبِّ الْمَشَارِقِ وَالْمَغَارِبِ إِنَّا لَقَادِرُونَ ﴿٤٠﴾

40. Basi naapa kwa Mola wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza

عَلَىٰ أَن نُّبَدِّلَ خَيْرًا مِّنْهُمْ وَمَا نَحْنُ بِمَسْبُوقِينَ ﴿٤١﴾

41. Kuwabadilisha kwa waliobora kuliko wao; na Sisi hatushindwi.

فَذَرْهُمْ يَخُوضُوا وَيَلْعَبُوا حَتَّىٰ يُلَاقُوا يَوْمَهُمُ الَّذِي يُوعَدُونَ ﴿٤٢﴾

42. Basi waache wapige porojo wakicheza, Mpaka wakutwe na hiyo siku yao wanayoahidiwa.

يَوْمَ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ سِرَاعًا كَأَنَّهُمْ إِلَىٰ نُصُبٍ يُوفِضُونَ ﴿٤٣﴾

43. Siku watakapotoka mak­aburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia kwenye mzimu.

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ذَٰلِكَ الْيَوْمُ الَّذِي كَانُوا يُوعَدُونَ ﴿٤٤﴾

44. Macho yao yatainama. uny­onge utawafunika. Hiyo ndiyo siku waliyokuwa wakiahidi­wa

WAACHE WAPIGE POROJO

Aya 36 – 44

MAANA

Wana nini wale waliokufuru wanakujia haraka? Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto!

Wana nini hawa ambao wamekadhibisha risala yako ewe Muhammad(s.a.w.w) na kukadhibisha ufufuo, mbona wanakuja haraka kwenye vikao vyako makundi kwa makundi na kuchukua nafasi zao upande wa kulia na kushoto, wakisikiliza Aya za Mwenyezi Mungu kisha wanaambiana huku wakidharau ufufuo na hisabu na kusema, ikiwa haya ni kweli basi sisi ndio bora wa watu na ndio tunaofaa kuingia Peponi, kwa sababu tuna mali nyin­gi na ndio watukufu zaidi kuliko Muhammad.

Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibu kwa kusema:

Hivi anatumai kila mmoja wao kuingizwa katika Pepo ya neema?

Hapana! Hamna chenu, enyi wakadhibishaji, katika Pepo ya Mwenyezi Mungu wala thawabu zake. Nyinyi hamna chochote kutoka kwake isipokuwa mwisho mbaya. Vipi mnatumai Pepo na hali nyinyi mnaikadhibisha na mnam­fanyia dharau Mtume aliyoewapa mwito wa kuitumikia. Hivi mnadhani kwamba mali na masanamu yatawakurubisha kwa Mwenyezi Mungu?

Sivyo! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanachokijua.

Wanajua hakika kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba kutokana na maji hafifu: “Basi naatazame mtu ni kwa kitu gani ameumbwa. Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa kuruka.” (86:5-6).

Ikiwa asili ya mtu ni moja, basi iweje wengine wawe watukufu kuliko wengine mbele ya Mwenyezi Mungu? Au awe bora kuliko mwenzake? Hapana! Hakuna kuzuidiana kati ya mweupe na mweusi, wala tajiri na masikini, isipokuwa kwa takua na matendo mema.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘kutokana na wanachokijua’ ina madhumu­ni ya kuwaonyesha wakadhibishaji wa ufufuo, na kuwarudi kwa kuali yao, kwamba hakuna nguvu yoyote inayoweza kurudisha uhai kwa anayegeuka mifupa na udongo. Njia ya majibu ni ikiwa ameweza kuwaumba watu kutokana na maji hafifu basi hawezi kushindwa kuipa uhai mifupa iliyochakafuka.

Basi naapa kwa Mola wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza kuwabadilisha kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi.

Makusudio ya mashariki zote na magharibi ni mashariki na magharibi za sayari, au masahriki za jua na magharibi zake, ambalo linajitokeza machoni na kujificha kutokana na mzunguko wa ardhi mbele yake. Makusudio ya anayeweza kuwabadilisha ni wale waliokufuru.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) imetukuka hikima yake anaapa kuwa Yeye anaweza kuwaangamiza wakadhibishaji na kuwaleta wengine mahala pao wasiomuasi Mwenyezi Mungu kwa wanayoamriwa na kutenda wanayoamriwa, na kama akitaka Mwenyezi Mungu hilo hapana wa kurudisha matakwa yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 26 (47:38).

Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao wanayoahidiwa.

Hii ni tahadhari na kiaga. Maana yake ni, achana nao ewe Muhammad, wadharau wafanye sthizai kadiri wawezavyo, lakini mwisho wao ni moto na ni makazi mabaya.

Aya hii imetangulia neno kwa neno katika Juz. 25 (43:83).

Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia kwenye mzimu.

Watatoka haraka makaburini mwao kwenda kwenye mahojiano ya hisabu, kama walivyokuwa wakifanya jana kutoka haraka majumbani mwao kwenda kwenye masanamu na mizimu, lakini mambo ni tofauti baina ya siku mbili hizo. Duniani walikuwa wakiharakisha kwenda kwenye miungu yao wakiwa na amani na utulivu, lakini siku ya Kiyama wataenda haraka kwenda kwa Mwenyezi Mungu huku ardhi ikitetema chini ya nyayo zaoMacho yao yatainama, unyonge utawafunika.

Unyonge na utwevu utawagubika; kama zinavyogubikwa nyuso zao na kipande cha usiku wenye giza.Hiyo ndiyo Siku waliyokuwa wakiahidiwa ambayo walikuwa wakiifanyia dharau na kuiharakishia.

MWISHO WA SURA YA SABINI: SURAT AL- MAA’RIJ