TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 26038
Pakua: 3251


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 26038 / Pakua: 3251
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

Mwandishi:
Swahili

21

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا ﴿١٨﴾

18. Na hakika misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuombe yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.

وَأَنَّهُ لَمَّا قَامَ عَبْدُ اللَّـهِ يَدْعُوهُ كَادُوا يَكُونُونَ عَلَيْهِ لِبَدًا ﴿١٩﴾

19. Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu aliposimama kum­womba, wao walikuwa karibu kumzonga!

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا ﴿٢٠﴾

20. Sema: Hakika mimi namwom­ba Mola wangu tu, wala simshirikishi na yeyote.

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا ﴿٢١﴾

21. Sema: Mimi sina mamlaka ya kuwadhuru wala kuwaon­goza.

قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّـهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٢﴾

22. Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitap­ata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu.

إِلَّا بَلَاغًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِسَالَاتِهِ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ﴿٢٣﴾

23. Ila kwa kufikisha Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.

حَتَّىٰ إِذَا رَأَوْا مَا يُوعَدُونَ فَسَيَعْلَمُونَ مَنْ أَضْعَفُ نَاصِرًا وَأَقَلُّ عَدَدًا ﴿٢٤﴾

24. Hata watakapoyaona wanayoahidiwa, ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.

قُلْ إِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ مَّا تُوعَدُونَ أَمْ يَجْعَلُ لَهُ رَبِّي أَمَدًا ﴿٢٥﴾

25. Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayoahidiwa, au Mola wangu atayawekea muda mrefu.

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾

26. Ni Mwenye kujua ghaibu, wala hamdhihirishii yeyote ghaibu yake.

إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَدًا ﴿٢٧﴾

27. Isipokuwa Mtume aliyemridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

لِّيَعْلَمَ أَن قَدْ أَبْلَغُوا رِسَالَاتِ رَبِّهِمْ وَأَحَاطَ بِمَا لَدَيْهِمْ وَأَحْصَىٰ كُلَّ شَيْءٍ عَدَدًا ﴿٢٨﴾

28. Ili ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao, Na anajua vyema yote waliyo nayo na amedhibiti idadi ya kila kitu.

HAKIKA MISKITI NI YA MWENYEZI MUNGU

Aya 18 – 28

MAANA

Na hakika misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuombe yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.

Wametofautiana kuwa kauli hii ni ya Mwenyezi Mungu au ni ya majini? Vyovyote iwavyo maana ni moja, kwamba sehemu zote za kuabudu ni kwa ajili ya kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumtii Yeye tu; iwe zime­jengwa na kuimarishwa na waislamu au wengineo.

Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu aliposimama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga!

Makusudio ya mja wa Mwenyezi Mungu hapa ni Muhammad(s.a.w.w) , aliyemuomba, ni Mwenyezi Mungu; na waliomzonga ni maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Maana ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alipotoa mwito wa haki vilijitokeza vikundi vya upotevu na kumzonga kutokana na wingi wao; kama nywele au sufu zinapojizonga zonga. Katika hilo Imam Ali (a.s) anasema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) aliingia kwenye kila majonzi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Ndugu zake wa karibu walimbadilikia na wa mbali wakaungana dhidi yake.

Waarabu walilegeza hatamu zao dhidi yake na wakamvalia njuga kumpiga vita, mpaka wakamjia maadui kutoka sehemu mbali mbali.

Linalofahamisha kuwa haya ndio makusudio yake ni kauli yake Mwenyezi Mungu moja kwa moja:

Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu tu, wala simshirikishi na yeyote.

Sema ewe Muhammad kuwaambia wale walioungana kukupiga vita: Je, nimewakosea nini? Je, nimewataka ujira au nimetaka cheo? Hapana isipokuwa ninamwabudu Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi. Yeye ndiye aliyoyeumba ulimwengu wote pamoja na ardhi yake na mbingu yake, je hii ni dhambi isiyosameheka?

Sema: Mimi sina mamlaka ya kuwadhuru wala kuwaongoza ; yaani kuwanufaisha. Maana ni kuwa sema ewe Muhammad kuwaambia washirikina: Mimi ni mtu kama nyinyi tu sidai kuwa na uweza wa hatima yenu, wala madhara na manufaa yenu; amri yote ni ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu. Ila kwa kufikisha Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akizembea kufikisha ujumbe alioaminiwa nao basi atakuwa hana pa kumkimbia Mwenyezi Mungu.

Aya hii ni miongoni mwa makumi ya Aya yanayofahamisha kwa uwazi kuwa Uislamu unakataa fkra ya kuweko wasta (wa katikati) baina ya Mwenyezi Mungu na mja wake, na inamweka mja mbele ya Mola wake moja kwa moja; azungumze naye, amnong’oneze vile atakavyo na ajikurubishe kwake kwa kufanya heri bila ya kuweko muombezi wala mgombezi.

Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.

Hili ni onyo, hadhari na kiaga kwa waasi waliopituka mipaka, kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapasa kutiiwa, hata kama hakutoa tahadhari na onyo; sikwambii tena akitoa onyo na tahadhari kama hii.

Hata watakapoyaona wanayoahidiwa, ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.

Washirikina walikuwa wakiwaona dhaifu wasisidizi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na wakiwaona ni wachache, wakimwambia: sisi ni zaidi yako wewe kwa mali na watu. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia kesho mtajua ni nani aliye na nguvu na ninani aliye dhalili. Amesema kweli Mwenyezi Mungu mtukufu, hazikupita siku Uislamu ukawa na nguvu na akawainua waislamu kwa uweza wake na makafiri watakuwa na adhabu ya kuungua huko Akhera.

Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayoahidiwa, au Mola wangu atayawekea muda mrefu.

Washirikina waliposikia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi,’ wal­imuuliza Mtume(s.a.w.w) : yatakuwa lini hayo; ndio Mwenyezi Mungu akamwamrisha Nabii wake awaambie ilimu yake iko kwa Mola wangu na wala sijui iko karibu au iko mbali.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Au atayawekea muda inafupishwa na neno mbali; kama ilivyo katika kauli yake:

وَإِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ أَم بَعِيدٌ مَّا تُوعَدُونَ ﴿١٠٩﴾

“Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa. Juz. 17 (21:109).

Ni Mwenye kujua ghaibu, wala hamdhihirishii yeyote ghaibu yake, isipokuwa Mtume aliyoemridhia.

Ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu na yule aliyemwamini kwa wahyi wake na akamchagua kupeleka ujumbe wake kwa waja wake, huyo anaweza kujua ghaibu aliyojulishwa na Mwenyezi Mungu: “Utakatifu ni wako hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha.” Juz. 1 (2:32).

Kundi la wafasiri, akiwemo Ar-Razi na Al-Maraghi wamesema asiyekuwa Mtume anaweza kujua ghaibu na kuitolea habari, lakini kauli hii haifikia­ni na dhahiri ya kauli yake isipokuwa Mtume aliyemridhia.

Ndio, ni kweli kuwa kuna baadhi ya watu wanaweza kutabiri mambo yatakayotokea mbele na wakawa wakweli katika nyingi ya dhana zao, lakini hayo wanayatoa kutokana na vigezo na alama zinazowadhihirikia kwa ufahamu na ilimu. Sasa ni wapi na wapi haya na ilimu ya ghaibu ambayo haidhihirishi Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa mitume na manabii?

Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

Yanayokuja haraka kwenye ufahamu wetu kutokana na Aya hii, ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawalinda manabii wakiwa wanatekeleza ujumbe wake na anawahifadhi na kila kikwazo cha kufikisha ujumbe kwa njia yake; ni sawa kizuizi hicho kiwe kinatoka ndani, kama vile kupuuza na kusahau, au kiwe kinatoka nje, kama vile ushawishi wa maadui nk. Kwa maneno mengine ni kuwa Aya hii inathibitisha umasumu wa manabii kati­ka utekelezaji wa wahyi.

Ili ajue yaani ifichuke ilimu ya Mwenyezi Mungu na uhakika wake,kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao, kwa uhalisia wakena Yeye anayajua vyema yote walio nayo . Yaani kila waliyosema manabii; haimpiti hata herufi moja. Fauka ya hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amevizunguka kwa ujuzi viumbe vyake vyote vidogo na vikubwa.

Na amedhibiti idadi ya kila kitu. Atashindwaje kuwadhibiti wajumbe wake kwenye kauli zao na pumzi zao na hali wao wanafikisha risala yake kwa waja wake? Lengo la msisitizo huu ni kutanabahisha kwamba manabii wamelindwa; hawakosei katika kufikisha wahyi ‧ hawapunguzi herufi wala kugeuza herufi kwa herufi nyingine.

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

“Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni wahyi uliotolewa.” Juz. 27 (53: 3-4).

MWISHO WA SURA YA SABINI NA MBILI: SURAT AL-JINN

22

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sabini Na Tatu: Surat Al Muzzammil. Imeshuka Makka Ina Aya 20.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehmu.

يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ ﴿١﴾

1. Ewe uliyejizongazonga nguo!

قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٢﴾

2. Simama usiku, ila kidogo tu!

نِّصْفَهُ أَوِ انقُصْ مِنْهُ قَلِيلًا ﴿٣﴾

3. Nusu yake, au ipunguze kidogo.

أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا ﴿٤﴾

4. Au izidishe, na soma Qur’an kwa utaratibu.

إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا ﴿٥﴾

5. Hakika tutakuteremshia kauli nzito.

إِنَّ نَاشِئَةَ اللَّيْلِ هِيَ أَشَدُّ وَطْئًا وَأَقْوَمُ قِيلًا ﴿٦﴾

6. Hakika kuamka usiku kunakanyaga zaidi, na ni vizuri zaidi kutamka.

إِنَّ لَكَ فِي النَّهَارِ سَبْحًا طَوِيلًا ﴿٧﴾

7. Kwani hakika mchana una shughuli nyingi.

وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ وَتَبَتَّلْ إِلَيْهِ تَبْتِيلًا ﴿٨﴾

8. Na lidhukuru jina la Mola wako, na ujitupe kwake kujitu­pa kabisa.

رَّبُّ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَاتَّخِذْهُ وَكِيلًا ﴿٩﴾

9. Mola wa mashariki na magharibi, hapana mungu isipokuwa Yeye, basi mfanye kuwa Mtegemewa.

EWE MWENYE KUJIZONGAZONGA NGUO

Aya 1 – 9

MAANA

Ewe uliyejizongazonga nguo!

Aya hii na zinazofuatia ni miongoni mwa Aya za mwanzo mwanzo kumshukia Mtume(s.a.w.w) . Ama Aya ya mwanzo kabisa au Sura ya kwanza, yatakuja maelezo yake katika Juzuu inayofuatia sura 96.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa amemwita Nabii wake mtukufu hivyo, kwa sababu alikuwa amejizongozonga nguo kutokana na sababu fulani. Ndio maana Mtukufu akamwita kwa sifa aliyokuwa nayo kwa kuzungumza naye kwa upole. Katika mfano kama huu ni kauli yake Mtume(s.a.w.w) kumwambia Ali: “Simama ewe Abu Turab (Baba wa mchanga),” kwa sababu alikuwa amelala mchangani. Pia kauli yake Nabii kumwambia Hudhayfa Al-Yamani: “Simama ewe mlalaji,” kwa vile alikuwa amelala.

Simama usiku, ila kidogo tu!

Wacha kujifunika nguo ewe Muhammad! Na ukeshe usiku kwa Swala na ibada nyingine, isipokuwa sehemu ndogo ya usiku utakayopumzika kwenye kitanda chako kwa usingizi. Kwa maneno mengine ni kuwa usiku wako ugawanye sehemu mbili; sehemu ya Mola wako na sehemu nyingine ya nafsi yako. Msemaji mmoja amesema kuwa kwa hili Mwenyezi Mungu alitaka kumwandaa Nabii mtukufu kwa jihadi ndefu, kuvumilia matatizo ya ufik­shaji na maudhi atakayopambana nayo kutoka kwa washirikina.

Hizi ni njozi tu, kwani Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikwishamwandaa Muhammad, kwa ajli ya amana kubwa atakayoichukua, kwa maumbile yake tangu siku aliyozaliwa.

Nusu yake, au ipunguze kidogo, au izidishe kidogo pia.

Huu ni ubainifu na tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘sima­ma usiku ila kidogo.’ Maana yake ni kuwa ewe Muhammad unaweza kusi­ma nusu yote ya usiku au chini yake kidogo au zaidi kidogo. Tafsiri hii, kikanuni ya nahw, inatubainishia kuwa nusu yake ni bada ya usiku na sio ya uchache. Pia inawezekana kuwa ni bada ya uchache na siyo ya usiku, na maana yawe unaweza kulala nusu yote ya usiku au upunguze au uzidishe kidogo. Hakuna tofauti ya maana baina ya irabu mbili hizi za kinahw.

Wafsiri wengi wameleta natija kutokana na neno kidogo katika Aya hii kuwa nusu inatakikana isizidi theluthi na ziada isizidi nusu mbili, kwa hiyo hiyari inakuwa baina ya nusu, theluthi au theluthi mbili na Aya ya 20 ya Sura hii imeeleza nyakati hizi tatu.

Na soma Qur’an kwa utaratibu.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w) , lakini makusudio ni kwa wote. Maana ni kuwa usifanye haraka kusoma, kwani lengo la kusoma Qur’an ni kuzingatia msomaji maana yake na malengo yake, anufaike na hukumu zake, mawaidha yake na ahadi zake, aweze kuhisi hofu ya adhabu chungu kutokana na maasi na kutumaini thawabu nyingi kutokana na utiifu; vinginevyo kutingisha ulimi na kuzitoa herufi kwa matokeo yake tu, sio malengo.

HAIBA YA MTUME MTUKUFU

Hakika tutakuteremshia kauli nzito.

Qur’an kwa maana yote yaliyo katika maneno haya, ni nzito kwa vile imeshinda na imedumu. Pia ni nzito katika itikadi na sharia yake na kupigana vita kwake dhidi ya wafisadi wenye nguvu na mataghuti wapenda anasa.

Wafasiri wengi wamesema Qur’an ni nzito kwa sababu ya taklifa zake zenye mashaka; mfano kudumisha Swala tano, kuamka mwisho wa usiku kwa jli ya Swala ya alfajiri, kutawadha na kuoga kwa maji baridi mara nyingi, kufunga siku za joto, kuamka mwisho wa usiku, kuhiji na masha­ka yake ya ihramu kufanya sa’yi na tawafu.

Hakuna mwenye shaka kwamba haya ni mazito isipokuwa kwa wenye kunyenyekea, lakini kubwa na zito zaidi ya hayo yote ni taklifa ya jihadi ambayo iko namna nyingi, na iliyo nzito zaidi ni jihadi ya kubadilisha nyoyo na hisia, kubadilisha imani mbovu zilizorithiwa na kung’oa mizizi ya ufisadi.

Haya ndiyo aliyobebeshwa Abul-Qasim, Muhammad mwana wa Abdillah. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimtuma kukamilisha maadili mema ya utu wote na awatoe watu kutoka gizani kuwapeleka kwenye nuru. Je, kuna mzigo mzito na wenye tabu kuliko huu?

Ni nani anayeweza kugeuza maadili ya mkewe na watoto wake, hasa kati­ka zama za ujahilia, zilizokuwa na ufisadi wa kupindukia na kupituka mipaka zaidi? Lakini Muhammad aliweza kuyakamilisha hayo. Siri ya hilo inakuwa katika haiba ya Muhammad(s.a.w. w ) , nguvu yake, ukuu wake na uvumilivu wake wa kushangaza katika maudhi kwenye njia ya mwito wake. alikuwa akizidi kuwa na subira na upole kila waasi walivyozidisha maudhi. Hakuwa akizidisha kauli yake: “Ewe Mwenyezi Mungu waseme­he watu wangu, hakika wao hawajui… ikiwa wewe hunikasirikii basi sijali.” Hapa ndio tunapata tafsiri sahihi zaidi ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ﴿١٢٤﴾

“Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujum­be wake.” Juz. 8 (6:124).

Ndio! Mwenyezi Mungu anajua kuwa haiba ya Muhammad ina nguvu zaidi kuliko imani na itikadi na watu wote, ndio maana akamtuma kuka­milisha tabia njema: “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya alivyoipa.” Juz. 28 (65:7). Hakika hii ameigundua mwanafasihi mashuhuri wa kimataifa, Bernard Show, pale aliposema; “Lau Muhammad bin Abdillah angelikuwa kwenye karne ya ishirini angemaliza ufisadi na upotevu.”

Hakika kuamka usiku kunakanyaga zaidi, na ni vizuri zaidi kutamka.

Katika Bahrf Al-muhit, imeelezwa kuwa maana ya kuamka usiku ni saa yake, kukanyaga zaidi, ni mashaka zaidi, na vizuri zaidi kutamka, ni kutamka kwa usawa na uthabiti.

Ni kama kwamba muulizaji ameuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu akamwamuru Nabii wake mtukufu kuabudu sehemu ya usiku? Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajibu, kwa sababu mtu kuacha kitanda chake baada ya utulivu wa usiku kuna mashaka makubwa zaidi katika nafsi, na bora ya amali ni ile yenye mashaka zaidi. Na kwa kuwa moyo wa mtu usiku unakuwa safi na mtulivu zaidi, basi kisomo chake kinakuwa sahihi na uthabiti zaidi. Vile vile kinakuwa na mwitikio zaidi pamoja na Aya.

Imesemekana kuwa neno watw’a, tulilolifasiri kwa maana ya kukanyaga, hapa lina maana ya kuafikiana baina ya moyo na ulimi.

Kwani hakika mchana una shughuli nyingi.

Neno shughuli tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu sabhU lenye maana ya kuogelea; yaani mtu anajigeuzageuza kwenye shghuli za hapa na pale, kama anayeogelea.

Usiku ni wa ibada na tahajudi na mchana ni wa kufanya kazi na kuhangai­ka kutafuta maisha, nao ni mrefu unaotosheleza mahitaji ya mtu.

Sheikh Abdul-Qadir Al-Maghribi, katika kufasiri Aya hii, anasema: “Mpingaji anaweza kusema kuwa kuamka usiku kunadhoofisha. Hilo amelijibu Bwana wetu Ali (r.a) kwa kusema: ‘Kama mtu akisema: ikiwa hali ya mwana wa Abu Twalib ni hii basi hataweza kupamabana na mashujaa. Juweni kwamba mti wa msituni una mbao laini na matawi ya kijani yana magome laini, na mti wa mbugani una kuni ngumu na zinazochelewa kuzimika. Mimi na Mtume wa Mwenyezi Mungu ni kama mwanga unao­tokana na mwanga, na kama pacha, na kama kigasha na sehemu ya juu ya mkono.’

Yaani yeye na Bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ni asili moja katika utendaji na mfumo wa maisha; kwa hiyo hali ya ke ni kama hali ya Mtume, shujaa, mwenye azma ya nguvu, ingawaje maisha yake yalikuwa magumu.”

Na lidhukuru jina la Mola wako, na ujitupe kwake kujitupa kabisa.

Makusudio ya kumdhukuru Mwenyezi Mungu hapa ni kumlingania. Neno kujitupa tumelifasiri kutokana na neno abattul, linalotokana na batl. Neno hili hutumika katika kuachana na dunia; miongoni mwayo ni Batul, msimbo wa Bibi Maryam.

Maana ni kuwa baada ya kukesha sehemu ya usiku kwa ibada ewe Muhammad na kupumzika, basi lingania haki na kufanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu peke yake. Kama kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamfahamisha Mtume wake mtukufu kuugawanya usiku mafungu matatu: Fungu la ibada, la jihadi na la kupumzika ili aweze kuendelea na ibada yake na juhudi zake.

Mola wa mashariki na magharibi, hapana mungu isipokuwa Yeye, basi mfanye kuwa Mtegemewa.

Ufalme katika mashariki na magharibi na mbinguni na ardhini ni wake peke yake, hana mshirika. Ikiwa viumbe wote ni wa Mwenyezi Mungu basi ni wajibu kwa mja kumtegema Yeye tu na wala asikimbilie kwa yey­ote asiyekuwa Yeye.

Hapa kuna ishara kwamba viumbe wanafahamisha kuweko muuumbaji na kwamba kunyenyekea viumbe kwenye siri ya maumbile yenye kuthibiti bila kugeuka ni dalili wazi kuwa muumba ni mmoja katika dhati yake na sifa zake.

وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاهْجُرْهُمْ هَجْرًا جَمِيلًا ﴿١٠﴾

10. Na vumilia hayo wayasemayo, na jitenge nao kujitenga vizuri.

وَذَرْنِي وَالْمُكَذِّبِينَ أُولِي النَّعْمَةِ وَمَهِّلْهُمْ قَلِيلًا ﴿١١﴾

11. Na niache Mimi na wanaokadhibisha, walioneemeka, na wape muda kidogo!

إِنَّ لَدَيْنَا أَنكَالًا وَجَحِيمًا ﴿١٢﴾

12. Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unaowaka kwa ukali!

وَطَعَامًا ذَا غُصَّةٍ وَعَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٣﴾

13. Na chakula kinachokwama kooni, na adhabu inayoumiza.

يَوْمَ تَرْجُفُ الْأَرْضُ وَالْجِبَالُ وَكَانَتِ الْجِبَالُ كَثِيبًا مَّهِيلًا ﴿١٤﴾

14. Siku ambayo ardhi itatikisika na milima, na milima itakuwa kama tifutifu la mchanga.

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا ﴿١٥﴾

15. Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu yenu, kama tulivyomtuma Mtume kwa Firauni.

فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا ﴿١٦﴾

16. Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamtesa mate-so mazito.

فَكَيْفَ تَتَّقُونَ إِن كَفَرْتُمْ يَوْمًا يَجْعَلُ الْوِلْدَانَ شِيبًا ﴿١٧﴾

17. Basi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na Siku ambayo itawafanya watoto wawe wazee?

السَّمَاءُ مُنفَطِرٌ بِهِ كَانَ وَعْدُهُ مَفْعُولًا ﴿١٨﴾

18. Mbingu zitapasuka! Ahadi yake itakuwa imetekelezwa.

إِنَّ هَـٰذِهِ تَذْكِرَةٌ فَمَن شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ سَبِيلًا ﴿١٩﴾

19. Kwa hakika haya ni ukum­busho. Mwenye kutaka atashika njia ya kwendea kwa Mola wake.

JITENGE NAO KWA UZURI

Aya 10 -19

MAANA

Na vumilia hayo wayasemayo, na jitenge nao kujitenga vizuri.

Maadui wa Mwenyezi Mungu walisema mengi juu ya Muhammad(s.a.w. w ) , ndio Mwenyezi Mungu akamwamuru avumilie na aachane nao bila ya kuwafanya lolote.

Hayo yalikuwa mwanzo mwanzo mwa utume ambapo waislamu walikuwa kidogo na makafiri ni wengi; mpaka ilipofikia Hijra na waislamu wakawa na nguvu ndipo Mwenyezi Mungu alipowaruhusu kuwahami wadhulumiwa kutokana na madhalimu.

Umetangulia mfano wake katika Aya kdhaa ikiwemo Juz. 9 (7:199).

Na niache Mimi na wanaokadhibisha, walioneemeka, na wape muda kidogo!

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwambia Nabii wake mtukufu kuwa aachane nao hao wanaomkadhibisha na kumpa sifa ya uchawi, mwendawazimu na mshairi, sasa anamwambia niachie nao mimi hawa waliolevyeshwa na mali na kuwapofua wasione kitu isipokuwa starehe na anasa zao. Waache wala wasikushughulishe, ni hivi karibuni tu itawapata adhabu na maangamizi.

Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unaowaka kwa ukali! Na chakula kinachokwama kooni, na adhabu inayoumiza.

Haya ndiyo aliowaahidi Mwenyezi Mungu: mbingu, moto ambao kuni zake ni watu na mawe, chakula cha miba kisichoshuka kooni wala kutoka na aina nyinginezo za adhabu, kama vile nguo za moto na makomeo ya chuma.

Siku ambayo ardhi itatikisika na milima, na milima itakuwa kama tifutifu la mchanga.

Huu ndio wasifu wa siku ya Kiyama na vituko vyake: ardhi itatetemeka na milima iwe kama rundo la mchanga unaotawanyika kwa sababu ndogo tu.

Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu yenu.

Maneno yaneelekezwa kwa wakadhibishaji walioneemeka, makusudio ya mtume na shahidi ni Muhammad(s.a.w. w ) ; kama ilivyo katika Juz. 7 (4:41). Yaani Muhammad(s.a.w. w ) atatoa ushuhuda kuwa aliwafikishia ujumbe wa Mola wao, lakini wakaukadhibisha na kuupuza.

Kama tulivyomtuma Mtume kwa Firauni. Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamtesa mateso mazito.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapiga mfano wa Firauni na wale walioneeme­ka waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w. w ) , kuwa hali yao ni sawa na hali ya watu wa Firauni walivyokuwa na Musa. Mwenyezi Mungu anawahad­harisha, kama wataendelea na upotevu yatawapata yaliyompata Firauni na watu wake; maangamizi na adhabu chungu duniani na Akhera.

Basi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na Siku ambayo itawafanya watoto wawe wazee? Mbingu zitapasuka! Ahadi yake itakuwa imetekelezwa.

Makusudio ya mkikufuru ni mkibakia kwenye ukafiri. Maana ni kuwa mta­jiokoa na nini nyinyi mnaopituka mipaka na adhabu kubwa siku itakapopa­suka mbingu na mtoto kuwa mzee kutokana na vituko vya siku hiyo. Siku hiyo itafika tu, hilo halina shaka, kwa sababu Mwenyezi Mungu hakhalifu kiaga. Ilivyo ni kuwa kuzeeka ni fumbo la yatakayowapata wakosefu, kwa sababu watoto hawatahisabiwa wala kuadhibiwa.

Kwa hakika haya ni ukumbusho. Mwenye kutaka atashika njia ya kwendea kwa Mola wake.

Haya ni hayo yaliyotangulia ya Aya za maonyo na kiaga. Ukumbusho ni mazingatio na mawaidha. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anabainisha njia mbili za heri na shari. Akaamrisha hili na kuliahidia thawabu na akakataza lile na kuliahidia adhabu; kila mtu atajichagulia neema au moto.

إِنَّ رَبَّكَ يَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُومُ أَدْنَىٰ مِن ثُلُثَيِ اللَّيْلِ وَنِصْفَهُ وَثُلُثَهُ وَطَائِفَةٌ مِّنَ الَّذِينَ مَعَكَ وَاللَّـهُ يُقَدِّرُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ عَلِمَ أَن لَّن تُحْصُوهُ فَتَابَ عَلَيْكُمْ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ عَلِمَ أَن سَيَكُونُ مِنكُم مَّرْضَىٰ وَآخَرُونَ يَضْرِبُونَ فِي الْأَرْضِ يَبْتَغُونَ مِن فَضْلِ اللَّـهِ وَآخَرُونَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنْهُ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا وَاسْتَغْفِرُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾

20. Hakika Mola wako anajua ya kuwa hakika wewe unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya watu walio pamoja nawe. Na Mwenyezi Mungu anaukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuwe­ka hisabu, basi amewasamehe. Basi someni kilicho chepesi katika Qur’an. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni kilicho chepesi humo. Na simamisheni Swala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina ujira mkubwa sana. Na mtakeni maghufira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kure­hemu.

SOMENI KILICHOCHEPESI KATIKA QUR’AN

Aya 20

MAANA

Hakika Mola wako anajua ya kuwa hakika wewe unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya watu walio pamoja nawe.

Mwanzoni mwa sura Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamuru Nabii wake mtukufu na walio pamoja naye wafanye ibada theluthi mbili za usiku au nusu yake au hata theluthi, ni hiyari ya mtu.

Basi wakasikiliza na wakatii. Baadhi ya maswahaba wakawa wanaona uzito kuupanga wakati, kwa hiyo wakawa wanakesha usiku kucha, mpaka badhi yao wakavimba miguu kutokana na kusimama mda mrefu. Walifanya hivi kujitoa shaka kwenye dini yao na kumridhisha Mola wao.

Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu (s.w.t) anampa habari Mtume wake kwamba yeye na walio pamoja naye wamefikia ukomo wa kumwabudu na kumtii Mwenyezi Mungu na Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu atawalipa malipo bora na ya ukamilifu.

Na Mwenyezi Mungu anaukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amewasamehe. Basi someni kilicho chepesi katika Qur’an.

Kuweka hisabau ni hiyo theluthi mbili na nusu yake na theluthi yake. makusudio ya kuwasamehe ni kuwaondolea taklifa.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewafanyia usiku na mchana kwa kiwango maalum, lakini mswahaba walikuwa hawajui nyakati kwa kiwango chake; isipokuwa walikuwa wakitegema dhana tu na ijtihadi; ambapo wakati huo hakukua na saa za kudhibiti dakika na sekunde.

Kwa hiyo akawaondolea kisimamo cha usiku cha theluthi mbili za usiku, nusu yake au theluthi moja; kwamba wasome Qur’an kiasi watakachoweza.

Mwenye ajamul-bayaa amewanukuu wafasiri wengi wakisema kuwa makusudio ya kitakachokuwa chepesi ni Swala ya usiku.

Ni sawa iwe makusudio ni kisomo au Swala, lakini ieleweke kuwa amri hapa ni ya Sunna sio wajibu.

Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu.

Hii ni hikima ya pili ya kuhafifishwa na kuondolewa taklifa ya kusimama kwenye theluthi mbili za usiku au nusu yake au theluthi yake; nayo ni kuwa miongoni mwa waja watakuweko wagonjwa watakaokuwa na uzito wa kumaliza masaa mengi usiku kwa kuswali, vile vile kutakuweko wasafiri wanaotafuta maisha na bila shaka safari inahitaji mapumziko na kulala usiku, vinginevyo itakuwa uzito kufanya kazi mchana kwa msafiri. Vile vile kutakuwa na wapiganaji wanaohitajia mapumziko usiku ili wawe na nguvu za mapambano mchana.

Basi Mwenyezi Mungu akawawahafifishia wote kwa sababu ya hawa watatu. Aya inaashiria mambo mawili muhimu: Kwanza, hikima ya kuon­doa taklifa kwa wote hailazimishi kushindwa wote, bali inatosha tu kushindwa baadhi na kuondolewa kwa wote. Pili, kazi ya kutafuta riziki ya halali ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu; sawa na jihadi ya kupigana na maadui wa Mungu na wa ubinadamu.

Kwa hivyo someni kilicho chepesi humo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelikariri jambo hili kwa kukaririka sababu zake; ya kwanza ilikuwa ni kutodhibiti wakati na ya pili ni ugonjwa, safari na vita.

Na simamisheni Swala ; yaani Swala tano. Hizi haziondoki kwa hali yoyote ile, si kwa safari, wala ugonjwa au jihadi. Kila mtu ataitekeleza kulin­gana na uwezo wake.Na toeni Zaka ya wajibu katika mali zenu.Na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema . Yaani vile vile toeni kwa kujitolea katika njia za heri na hisani; kwani kutoa huku kunawarud­ishia ziada juu ya ziada.

Amri hii ya kutoa imekaririka mara saba mpaka sasa; ya kwanza ni ile iliyo katika Juz. 2 (2:245).

Na kheri yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina ujira mkubwa sana.

Kheri haihusiki na kutoa mali tu; kila lililo na masilahi kwa watu basi ni heri; iwe ni kauli au kitendo. Mwenye kufanya wema anajifanyia mwenyewe na mwenye kufanya ubaya pia ni juu yake.

Na mtakeni maghufira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Mwenye kuzembea na akapituka mipaka basi anamfungulia mlango wa toba, na ni muhali kuufunga mlango wa maghufira.

MWISHO WA SURA YA SABINI NA TATU: SURAT AL MUZZAMMIL