TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 26036
Pakua: 3250


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 30 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 26036 / Pakua: 3250
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE Juzuu 24

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sitini Na Tatu: Surat Al- Munafiqun. Imeshuka Madina. Ina Aya 11.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

ذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ ﴿١﴾

1. Wanapokujia wanafiki huse­ma: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika wewe ni Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanafiki ni waongo.

اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢﴾

2. Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ ﴿٣﴾

3. Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao nao hawafahamu.

وَإِذَا رَأَيْتَهُمْ تُعْجِبُكَ أَجْسَامُهُمْ وَإِن يَقُولُوا تَسْمَعْ لِقَوْلِهِمْ كَأَنَّهُمْ خُشُبٌ مُّسَنَّدَةٌ يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ هُمُ الْعَدُوُّ فَاحْذَرْهُمْ قَاتَلَهُمُ اللَّـهُ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٤﴾

4. Na unapowaona, miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao. Kama kwamba wao ni magogo yaliy­oegemezwa. Wao hudhania kila ukelele ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; jihadhari nao.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا يَسْتَغْفِرْ لَكُمْ رَسُولُ اللَّـهِ لَوَّوْا رُءُوسَهُمْ وَرَأَيْتَهُمْ يَصُدُّونَ وَهُم مُّسْتَكْبِرُونَ ﴿٥﴾

5. Na wanapoambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghufira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi.

سَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَسْتَغْفَرْتَ لَهُمْ أَمْ لَمْ تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ لَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ ﴿٦﴾

6. Ni sawa kwao, ukiwatakia maghufira au usiwatakie maghufura, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki.

HAO NI MAADUI JIHADHARI NAO

Aya 1-6

MAANA

Qur’an imewasifia maswahaba na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na ikawasifia kwa nguvu daraja zao na vyeo vyao. Vile vile imezungumzia aina za wanafiki katika sura kadhaa na jinsi walivyong’ang’ania kuufanyia vitimbi Uislamu na manabii wake. Masimulizi kuhusiana na wanafiki hayana ukomo, kwa sababu uwongo wao na mbinu zao chafu hazina mpaka.

Kwa hiyo si ajabu kukaririka masimulizi yao, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwahusisha na sura kamili katika Kitabu chake na kuwasi­fia kwa sifa mbaya; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-

Wanapokujia wanafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika wewe ni Mtume wake.

Walidhamiria kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumfanyia uadui Nabii wake mtukufu, wakadhihirisha mapenzi na imani kwake na kwa risala yake.

Na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanafiki ni waongo.

Makusudio ya kushuhudia kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni kujua. Maana ni kuwa wanafiki wanasema kwa ndimi zao yale yasiyo nyoyoni mwao; na Mwenyezi Mungu anajua wanayoyaficha na wanayoyadhi­hirisha naye anawangojea tu.

Vile vile Nabii anajua hakika yao, lakini ameamrishwa kuwachukulia kwa dhahiri na sio kwa uhalisia; akasema: “Nimeamriwa kupigana na watu mpaka waseme: Lailahaillallah Muhammadur-rasurullah. (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu) wakishasema basi imehifadhika nami damu zao na mali zao, isipokuwa kwa haki yake, na hisabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu.”

Ufasaha zaidi niliousoma kuhusiana na maudhui haya ni kauli ya Imam Ali(a.s ) :“Ulimi wa mumin uko nyuma ya moyo wake na moyo wa mnafiki uko nyuma ya ulimi wake.” Yaani ulimi wa mumin unafuata moyo wake, hasemi isipokuwa analoliamini. Lakini mnafiki moyo wake unafuata ulimi wake na ulimi wake unazunguka na hawaa yake na malengo yake. Natija ya hayo ni kuwa mnafiki hana moyo isipokuwa hawa na matamanio.

Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu.

Mara nyingi njama za wanafiki zilikuwa zikifichuka, nao kila walipokuwa wakizungumza wanafanya kiapo ndio kinga yao kuzuia kughadhibikiwa na Mtume(s.a.w. w ) na kuficha njama zao dhidi ya Mtume na upinzani wao kwa risala yake.

Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya ya vitimbi, hadaa na kuwa vigeugeu.

Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao nao hawafahamu lolote.

Makusudio ya waliamini ni kuwa walijulikana na watu kwamba wameami­ni. Vinginevyo ni kuwa wao hawakuwahi kuamini hata chembe. Na makusudio ya wakakufuru ni kujulikana kuwa kumbe walidhihirisha imani na wakaficha ukafiri. Ama makusudio ya kupigwa muhuri juu ya nyoyo zao ni kuwa hawaongoki kwenye heri baada ya kupofushwa na hawaa na upotevu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:137).

Na unapowaona, miili yao inakupendeza , Wana mandhari mazuri na hisia mbaya. Kwa ibara ya Imam Ali(a.s ) :“Nyoyo zao zina maradhi na nyuso zao ni safi.”

Na wakisema, unasikiliza usemi wao , kwa sababu wanazungumza maneno ya wenye ikhlasi na wanaizungumzia dunia kwa maneno ya wenye zuhudi.

Kama kwamba wao ni magogo yaliyoegemezwa . Ni mfano wa magogo, lakini wanakula na kunywa. Kila mwenye kupofu­ka na uongofu, basi ni maiti hai.

Wao hudhania kila ukelele ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; jihadhari nao.

Wana roho za woga wa kufichuka siri zao, hawasikii sauti ila wanadhani ni sauti ya adhabu itakayowanyakuwa bila ya kujua. Woga huu ume­wazidishia lawama na uadui kwenu enyi wenye ikhlasi, basi jihadharini na njama zao na msiwape fursa kadiri mtakavyoweza.

Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanageuzwa?

Hii ni shutuma kwa tamko la kuduia na kushangaa. Maana ni kuwa wao wamelaaniwa kwa vile wameiacha haki kwa inadi na jeuri.

Kila sifa walizosifiwa wanafiki wakati wa Mtume(s.a.w. w ) ni sura iliyoko kwa vibaraka wa leo wanaokula njama na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa nchi kwa kuufanyia vitimbi uma wao.

Hakuna hatia kubwa kama kuufanyia hiyana uma, na hakuna fedheha kama mtu kumuuza mtu mwenzake.

Na wanapoambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghufira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi.

Mtu akiwanasihi na kuwaambia tubieni mliyo nayo na Mwenyezi Mungu atawaghufiria, basi wao wanag’ang’ania batili na kuipinga haki, waki­inamisha vichwa vyao kwa dharau na kiburi. Kwa vile wao ni wakubwa kuliko wanayoyahitajia kwa Mtume; kama wanavyodai.

Ni sawa kwao, ukiwatakia maghufira au usiwatakie maghufira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria.

Hakuna faida ya kuwataka watengenee; kwa hiyo hakuna haja ya kuwatakia maghufira.

Ni kweli Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira mwenye kurehemu, hilo halina shaka, na rehema ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuenea katika kila kitu, isipokuwa kwa mwenye kuikataa na akaifanyia kiburi. Kwa hiyo itakuwa si huruma kumfanyia yule anayeona kuwa haihitajii huruma yako.

Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki , maadamu wanang’ang’ania ufuska.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (9: 80).

هُمُ الَّذِينَ يَقُولُونَ لَا تُنفِقُوا عَلَىٰ مَنْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ حَتَّىٰ يَنفَضُّوا وَلِلَّـهِ خَزَائِنُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَفْقَهُونَ ﴿٧﴾

7. Hao ndio wanaosema: Msitoe kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili wawaondokee. Na hazina za mbingu na ardhi ni za Mwenyezi Mungu, lakini wanafiki hawafahamu.

يَقُولُونَ لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٨﴾

8. Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanafiki hawajui.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٩﴾

9. Enyi mlioamini! Zisiwa­shughulishe mali zenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio wenye hasara.

وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠﴾

10. Na toeni katika tulichowapa kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, kisha aseme: Mola wangu! Mbona hukuni­akhirishia muda kidogo nika­toa sadaka, na kuwa katika watu wema?

وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١١﴾

11. Wala Mwenyezi Mungu hata­iakhirisha nafsi yoyote inapofika ajali yake; na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

MWENYE NGUVU ATAMFUKUZA MNYONGE

Aya 7 – 11

MAANA

Hao ndio wanaosema: Msitoe kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili wawaondokee.

Wanaosema ni wanafiki na walioko kwa Mtume ni wahajiri walio mafukara. Matajiri wa Kianswar walikuwa wakiwasaidia hawa, ndio wanafiki wakawaambia matajiri msitoe mali zenu kwa muhajiri yoyote ili wapate kuona vibaya waweze kuondoka. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawarudi kwa kuwaambia:

Na hazina za mbingu na ardhi ni za Mwenyezi Mungu, lakini wanafiki hawafahamu.

Mnawaamuru ubahili wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na wakafanya juhudi katika njia yake, na hali Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa viumbe na ndiye anayevimiliki pamoja na mali zao na ndiye mwenye kuviruzuku! Yeye anaweza kuwatajirisha waumini kwa fadhila yake, lakini nyinyi hamjui.

Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge.

Wafasiri wamesimulia kisa cha Aya hii kinachohusiana na kiongozi wa wanafiki Abdallah bin Ubayya na vita vya Bani Mustaliq.

Hawa walikuwa ni sehemu ya Khuza’a na walikuwa wakiishi karibu na Makka. Waliona kuwa Uislamu utakuwa na nguvu katika Bara Arabu, hivyo wakajiandaa kupigana vita na Mtume(s.a.w.w) wakiongozwa na kiongozi wao Harith bin Abu Dhirar. Mtume(s.a.w.w) alipojua hilo akaharakisha kuwatokea na jeshi lake kabla ya wao kufika Madina.

Ibn Ubayya naye akatoka pamoja na jeshi la waislamu kwa tamaa ya ngawira. Basi Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mtume wake dhidi ya maadui zake, wakapata mali nyingi ya ngawira. Mtume(s.a.w.w)

akawaongezea mafukara wahajiri katika ngawira ili kupunguza pengo baina ya mafukara na matajiri. Ibn Ubayya akaona vibaya, akawa anawa­chochea Answar; miongoni mwa aliyoyasema ni: “Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge.”

Mtukufu anajikusudia yeye mwenyewe na mnyonge anamkusudia Mtume(s.a.w.w) . Ndio ikashuka Aya hii na Ibn Ubayya akafedheka. Wafasiri wengi wamesema kuwa Ibn Ubayya alisema neno hili la kufuru kutokana na mzozo uliotokea baina ya mmoja wa wafuasi wake na mfanyakazi wa Umar bin Al-Khattab.

Abdallah bin Ubayya alikuwa na mtoto mwema aliyekuwa akiitwa Abdallah pia. Alipojua kuhusu baba yake, alimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na kumwambia: “Umekwishajua alivyofanya baba yangu. Ukiwa unataka kumuua basi niamuru mimi nimuue, ili nisije nikashindwa kujizuia kumuona aliyemuua baba yangu, nikamuua mumin kwa sababu ya kafiri, nikaingia motoni.”

Mtume(s.a.w.w) akamjibu:“Tutamuhurumia baba yako na tutaishi naye kwa wema muda ule atakaobakia nasi.”

Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu -Yeye, na Mtume wake, na Waumini.

Hii ni kumrudi Ibn Ubayya aliyejisifu kuwa mtukufu zaidi. Utukufu wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni kuwa yeye ndiye mtukufu zaidi kwa waja wake, utukufu wa Mtume ni dini yake kushinda dini nyingine zote na kuwashinda maadui zake, na utukufu wa waumini ni kushinda haki na watu wake.

Lakini wanafiki hawajui kwamba utukufu ni kwa imani na takua. Enyi mlioamini! Zisiwashghulishe mali zenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio wenye hasara.

Mwenye kuitaamali Aya hii na ile iliyo kabla yake ataona kuwa makusudio ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu hapa ni jihadi.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwanza ametaja utukufu wake, wa Mtume na wa waumini; kisha akawakataza na kuwahadharisha waumini, dunia isiwasahaulishe kumkumbuka Mwenyezi Mungu na akajaalia natija ya hayo ni hizaya na udhalili duniani na Akhera.

Hakuna mwenye shaka kwamba hizaya na udhalili ni natija ya kuipenda dunia na kuhofia jihadi na mauti. Hakuna linalosadikisha hakika hii kuliko maisha ya waislamu na waarabu hivi sasa jinsi yalivyo.

Na toeni katika tulichowapa kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, kisha aseme: Mola wangu! Mbona hukuniakhirishia muda kidogo nikatoa sadaka, na kuwa katika watu wema?

Makusudio ya kufikiwa na mauti ni kudhihiri alama zake na utangulizi wake. Maana ni kuwa chukueni fursa ya kutoa kile alichowapa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kupuuza akangoja mpaka siku zake za mwisho mwisho atauma vidole kwa kujuta na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu ampe muda kidogo, lakini wapi! Yaliyopita hayarudi.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14:44).

Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapofika ajali yake; na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

Ajali imekwishaamriwa haiwahi wala haichelewi. Mwenye kupoteza fursa hana jingine isipokuwa hasara na majuto. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:145) kifungu cha ‘Ajali haina kinga.’ Na Juz. 8 (7:34).

MWISHO WA SURA YA SITINI NA TATU: SURAT AL- MUNAFIQUN

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA ISHIRINI NA NNE

Sura Ya Sitini Na Nne: Surat At – Taghabun. Imeshuka Madina Ina Aya 18.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾

1. Vinamsabihi vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi, Ufalme ni wake, na sifa njema ni zake. Na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُمْ فَمِنكُمْ كَافِرٌ وَمِنكُم مُّؤْمِنٌ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٢﴾

2. Yeye ndiye Aliyewaumba. Miongoni mwenu yupo aliye kafiri, na yupo aliye Muumini. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ ﴿٣﴾

3. Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na akawapa sura, na akazifanya nzuri sura zenu Na marejeo ni kwake.

يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُسِرُّونَ وَمَا تُعْلِنُونَ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٤﴾

4. Anajua vilivyomo mbinguni na ardhini, na anajua mnayoy­afanya siri na mnayoy­atangaza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَبَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَبْلُ فَذَاقُوا وَبَالَ أَمْرِهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٥﴾

5. Kwani haikuwajia habari ya waliokufuru kabla, wakaonja ubaya wa mambo yao? Na wao wana adhabu iliyo chungu.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُ كَانَت تَّأْتِيهِمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَقَالُوا أَبَشَرٌ يَهْدُونَنَا فَكَفَرُوا وَتَوَلَّوا وَّاسْتَغْنَى اللَّـهُ وَاللَّـهُ غَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿٦﴾

6. Hayo ni kwa kuwa walikuwa wakiwajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, nao wakase­ma: Hivi binadamu ndio atuongoze? Basi wakakufuru, na wakageuka upande. Mwenyezi Mungu si muhitaji. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, naye ni Msifiwa.

MIONGONI MWENU KUNA KAFIRI NA MUUMIN

Aya 1 – 6

MAANA

Vinamsabihi vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi.

Baadhi ya viumbe vinamsabihi kwa lugha ya maneno na vingine kwa lugha ya hali. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyonayo, mwanzo wa sura 62.Ufalme ni wake, humpa amtakaye na humvua amtakaye.

Na sifa njema ni zake. Kwa utukufu wa ihsani yake na uangavu wa dalili zake.Na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu bila ya nyenzo wala kufikiria, bali ni kwa neno ‘kuwa.’

Yeye ndiye Aliyewaumba. Miongoni mwenu yupo aliye kafiri, na yupo aliye Muumini. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

Mtu katika mtazamo wa kiislamu ni kwa uhuru wake na utashi wake. Hakuna utu bila ya uhuru. Anayo hiyari ya kuchagua imani hata kama wazazi wake ni makafiri, na ana hiyari ya kuchgua ukafiri hata kama wazazi wake ni waumini; wala haifai kabisa yeyote kumlazimisha mwingine - hakuna kulazimishana katika dini; vinginevyo taklifa, hisabu na thawabu zitakuwa ni batili.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumpa mja wake uhuru, unaomfanya kuwa mtu, akamwamuru kufuata imani na kufanya heri na akamkataza ukafiri na kufanya shari, akamwekea dalili za uzuri wa aliyomwamrisha na ubaya wa aliyomkataza; kutokana na akili yake na maumbile yake. Wakaamini baadhi ya watu na wakakufuru waliokufuru; na kila mmoja atapata thawabu au adhabu kulingana na imani na matendo yake.

Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki,

Yaani kwa hikima ya hali ya juu; wala hakuna chochote katika ulimwengu huu kilichoko kwa mchezo, wala hakuna tofauti baina ya kusema kuwa vitu vimepatikana kwa sadfa na kusema kuwa kila kitu, hata nidhamu, kimejileta chenyewe.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (16:3).

Na akawapa sura, na akazifanya nzuri sura zenu.

Msanii anaweza kutengeneza sura ya chochote na kwa ufundi na ustadi wa hali ya juu, lakini kazi yake kubwa inakuwa ni kupamba na kuweka shepu tu; sawa na mjengaji anayeweka jiwe juu ya jiwe jingine, lakini nyenzo za ujenzi na kutengeneza sura inatoka kwa anayekiambia kitu kuwa na kikawa.

Mwenyezi Mungu aliiumba mada ya mtu kwa neno ‘kuwa’ akaitia sura zaidi kuliko viumbe vingine. Umetangulia mfano wake katika Juz. 18 (23:14)

Na marejeo ni kwake awambie mliyokuwa mkiyafanya, na mwenye kuepushwa na moto atakuwa amefuzu.

Anajua viliomo mbinguni na ardhini, na anajua mnayoyafanya siri na mnayoyatangaza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliomo vifuani. Maana yako wazi. Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

Kwani haikuwajia habari ya walio kufuru kabla, wakaonja ubaya wa mambo yao? Na wao wana adhabu iliyo chungu.

Swali ni la kutahayariza, na maneno yanaelekezwa kwa washirikina waliomkufuru Muhammad(s.a.w. w ) na wakatangaza vita naye na mwito wake. Amewakumbusha Mwenyezi Mungu yaliyowapata waliokuwa kabla yao; kama vile kaumu ya Nuh, A’d na Thamud - waliwakadhibisha mitume yakawasibu maangamizi duniani na adhabu ya Akhera ni kali zaidi na ya kufedhesha.

Hayo ni kwa kuwa walikuwa wakiwajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, nao wakasema: Hivi binadamu ndio atuongoze? Basi wakakufu­ru, na wakageuka upande.

‘Hayo’ ni ishara ya adhabu iliyowafika uma zilizopita kwa vile wali­wakadhibisha mitume. Waliwajia na dalili mkataa juu ya utume wao, lakini bado wao waling’ang’ania kufuru, si kwa lolote ila ni kuwa mitume ni watu kama wao watawaongozaje!

Hawajui kuwa uongozi unatokana na ilimu? Ajabu ni kuwa walipopewa mwito wa tawhid walisema ‘mtu kama sisi atuongoze?’ lakini hawakumwambia hivi aliyewaita kwenye ibada ya mawe, bali walimsikiliza na kumtii bila ya ubishi. Hili si la kushangaza, ndio tabia ya ujinga.

Kadiri nitakavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka kuwa wenye busara lau watahiyarishwa baina ya upofu pamoja na ilimu, na ujinga pamoja na uoni, basi wangelichagua upofu, kwa sababu hauwezi kulikaribisha la mbali wala kulibaidisha la karibu, wala hausawirishi weusi kuwa weupe au weupe kuwa weusi. Lakini ujinga unasawirisha uongofu kuwa ni upotevu, upotevu kuwa uongofu, haki kuwa batili na batili kuwa haki.

Mwenyezi Mungu si muhitaji. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, naye ni Msifiwa.

Kila kilichoko kinashuhudia kwa lugha ya maneno na lugha ya hali kuwa Mwenyezi Mungu hawahitajii viumbe na utiifu wao, mwenye kusifiwa katika sifa zake zote na vitendo vyake.

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿٧﴾

7. Waliokufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Naapa kwa Mola wangu! Hapana shaka mtafu­fuliwa, na kisha hapana shaka mtaambiwa mliyoyatenda. Na hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.

فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَالنُّورِ الَّذِي أَنزَلْنَا وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿٨﴾

8. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru tuliyoiteremsha. Na Mwenyezi Mungu kwa mnay­oyatenda anazo habari.

يَوْمَ يَجْمَعُكُمْ لِيَوْمِ الْجَمْعِ ذَٰلِكَ يَوْمُ التَّغَابُنِ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ وَيَعْمَلْ صَالِحًا يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّئَاتِهِ وَيُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٩﴾

9. Siku atakayowakusanya kwa ajili ya Siku ya Mkusanyiko; hiyo ni siku ya hasara. Na anayemwamini Mwenyezi Mungu na akatenda mema, atamfutia maovu yake, na atamuingiza katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ خَالِدِينَ فِيهَا وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿١٠﴾

10. Na waliokufuru na waka­ kadhibisha Ishara zetu, hao ni watu wa Motoni, watadumu humo milele. Na hayo ndiyo marudio mabaya.

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١١﴾

11. Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu huuongoza moyo wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَإِنَّمَا عَلَىٰ رَسُولِنَا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿١٢﴾

12. Na mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume. Mkigeuka, basi hakika juu ya Mtume wetu ni kufikisha kwa uwazi tu.

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١٣﴾

13. Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Na juu ya Mwenyezi Mungu nawategemee Waumini.

HII NI SIKU YA HASARA

Aya 7-13

MAANA

Waliokufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Naapa kwa Mola wangu! Hapana shaka mtafufuliwa, na kisha hapana shaka mtaambiwa mliyo yatenda. Na hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.

Tumebainisha njia ya Qur’an katika ufufuo na kuzirudi shaka shaka za wakanushaji na kwamba mwenye kufanya kitu bila ya mali ghafi basi ni rahisi zaidi kwake kuvikusanya viungo baada ya kutawanyika kwake. Tumefafanua kwa mifumo mbali mbali katika kufasiri Aya za ufufuo; kama vile Juz. 11 (10:4) ‘Hisabu na malipo ni lazima.’

Unaweza kuuliza : Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alitoa mwito wa ufufuo kwa kiapo wakampinga waabudu masanamu; na kimsingi ni kuwa ushahidi ni wa mwenye kudai na kiapo ni cha mwenye kupinga. Msingi huu ni wa kibinadamu uliokubaliwa na sharia zote. Kwa hiyo basi Mtume(s.a.w. w ) anatakiwa alete ushahidi, sio aape. Sasa je, kuna wajihi gani wa Mtume kuleta kiapo na alitakiwa alete hoja za kuwanyamazisha. Je ufufuo utathibitika kwa kuapa tu?

Jibu : Kwanza, Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasimulia kuwa wakanushaji hapa walimwuliza Mtume kuhusu ufufuo kama wenye kuchunguza sio wenye kujadiliana; hawakusema:

مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ ﴿٧٨﴾

“Ni nani atakayeiuisha mifupa nayo imemung’unyika?” Juz. 23 (36:78).

Au kusema:

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿١٦﴾

“Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa?” Juz. 23 (37:16).

Kwa kuwa, katika Aya tuliyo nayo, wakanushaji walitosheka na kuuliza tu, sio kushangaa na kujadiliana, basi Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametosheka na kujibu tu pamoja na msisitizo wa kiapo.

Ndio maana pale waliposema: ‘Ni nani atakayeihuisha mifupa nayo imemung’unyika,” aliwaambia: “Ataihuisha yule Alieiumba mara ya kwanza. Na Yeye ni mjuzi wa kila jambo.” Jibu linakuja kulingana na swali.

Pili , wale waliokufuru pamoja na wanafiki walikuwa wakiamini kuwa Mtume(s.a.w. w ) hawatakii heri wala masilahi; isipokuwa anataka kujituku­za na kuwa juu yao; kama walivyoamini makafiri, hapo kabla, kwa Nabii Nuh:

فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُرِيدُ أَن يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ ﴿٢٤﴾

“Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu.” Juz. 18 (23:24).

Ndio akaapa Mtume kwamba mwito wake ni wa haki; akimaanisha kuwa hataki isipokuwa haki tu. Mfano wake ni kauli ya Shu’ayb kwa watu wake walipomdhania mabaya:

إِنْ أُرِيدُ إِلَّا الْإِصْلَاحَ مَا اسْتَطَعْتُ وَمَا تَوْفِيقِي إِلَّا بِاللَّـهِ ﴿٨٨﴾

“Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyoweza. Na tawfiki yangu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu.” Juz. 12 (11:88).

Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru tuliyoiteremsha.

Maadamu ufufuo ni haki na hisabu na malipo ni haki, basi ni juu ya kila mtu kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nuru; yaani Qur’an. Ameisifu kuwa ni nuru kwa vile inamtoa mtu kwenye giza la ujinga na kufuru kumpeleka kwenye nuru ya ilimu na imani na kumwongoza kwenye njia ya salama:

قَدْ جَاءَكُم مِّنَ اللَّـهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾ سُبُلَ السَّلَامِ وَيُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِهِ وَيَهْدِيهِمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿١٦﴾

“Hakika imekwishawafikia nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kitabu kinachobainisha. Mwenyezi Mungu huwaongoza kwacho wenye kufuata radhi yake katika njia za amani na huwatoa katika giza kuwapeleka kwen­ya nuru kwa amri yake, na huwaongoza katika njia iliyonyooka.” Juz.6 (5:15-16).

Na Mwenyezi Mungu kwa mnayoyatenda anazo habari. Siku atakayowakusanya kwa ajili ya Siku ya Mkusanyiko; hiyo ni siku ya hasara.

Neno ‘hasara,’ tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu taghabun ambalo wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio yake hapa ni kupunjana, ambapo siku ya Kiyama watu wa haki watawapunja watu wa batili, lakini tunavyofahamu sisi ni kuwa makusudio yake ni faida na hasara; ambapo wenye haki watapata faida na wabatilifu watapata hasara. Hata hivyo nati­ja ya maana zote mbili ni moja.

Mwenyezi Mungu anadhibiti kauli za waja wake, vitendo vyao, malengo yao na makusudio yao katika maisha ya dunia na kuyatumia siku ya Kiyama kwa hisabu.

Yakiwa ni heri basi ni heri na yakiwa ni shari basi ni shari. Siku ya mwisho imeitwa ya mkusanyiko kwa vile Mwenyezi Mungu atawakusanya viumbe kwa ajili ya hisabu na malipo.

Na anayemwamini Mwenyezi Mungu na akatenda mema, atamfutia maovu yake, na atamuingiza katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa. Na waliokufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ni watu wa Motoni, watadumu humo milele. Na hayo ndiyo marudio mabaya.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa Yeye atawakusanya watu siku isiyo na shaka, sasa anasema kuwa watu siku hiyo watakuwa aina mbili:

Ya kwanza : ni wale waliomwamini Mwenyezi Mungu, mitume wake na vitabu vyake na wakajitayarisha kwa matendo mema duniani kwa ajili ya Akhera yao. Aina hii ya watu ndio watakaofuzu kesho kwa kupata maghufira ya Mwenyezi Mungu na radhi yake na kwa kupata neema isiyo na ukomo wala kupungua kiwango chake.

Aina ya pili , ni waliopotezwa na dunia wanaoitafuta kwa njia yoyote itakayokuwa; hawajali dini wala dhamiri au halali wala haramu. Aina hi ya watu ndio watakaopata hasara, makazi yao ni Jahannam ambayo ni marejeo mabaya kabisa.

Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa shari yoyote ya duniani ni kwa kadha na kadari yake Mwenyezi Mungu. Na hii inapingana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ ﴿٣٠﴾

“Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu. Naye anasamehe mengi.” Juz. 25 (42:30).

Hili tumelijibu kwa ufafanuzi katika Juz. 5 (4:78-79). Ufupi wa jawabu ni kuwa majanga ya kimaumbile; kama vile tetemeko la ardhi kahati nk, yananasibika na maumbile moja kwa moja na yanasabishwa Kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa wasita; kwa vile Yeye ndiye Alieyaleta maumbe.

Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.” Na msiba wowote ambao chimbuko lake ni kupuuza na ufisadi, linanasibika kwenye uchaguzi mbaya wa kupuuza na ufisadi. Hii ndio iliyokusudia na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu.”

Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu huuongoza moyo wake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamchukulia mtu kwa vile inavyochagua nafsi yake. akijichagulia uongofu na heri na kufauata njia iliyonyoka, basi humshika mkono, kumsaidia na kumpatia thawabu za wenye kuongoka. Na akijichagulia upotevu na kuifuata njia yake, humwachilia mbali na kumtweza kisha anamtia kwenye adhabu ya moto.

Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Anamjua mwenye kujihurumia na anamuhurumia, na mwenye kujiangamiza kwa makusudi basi humwangamiza.

Na mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume. Mkigeuka, basi hakika juu ya Mtume wetu ni kufikisha kwa uwazi tu.

Wajibu wa Mtume ni kufikisha na wajibu wetu ni kusikiliza na kutii. Umetangulia mfano wake katika Aya kadha, ikiwemo ile iliyoko Juz. 7 (5:92).

Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipokuwa Yeye. Na juu ya Mwenyezi Mungu nawategemee Waumini.

Anawatoshea wenye kumtegemea Yeye na ni walii wa wenye ikhlasi.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ وَأَوْلَادِكُمْ عَدُوًّا لَّكُمْ فَاحْذَرُوهُمْ وَإِن تَعْفُوا وَتَصْفَحُوا وَتَغْفِرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٤﴾

14. Enyi mlioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu ni maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَاللَّـهُ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾

15. Hakika mali zenu na watoto wenu ni mtihani. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna ujira mkubwa.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا وَأَطِيعُوا وَأَنفِقُوا خَيْرًا لِّأَنفُسِكُمْ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٦﴾

16. Basi mcheni Mwenyezi Mungu vile muwezavyo, na sikieni, na tiini, na toeni, itakuwa heri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.

إِن تُقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعِفْهُ لَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللَّـهُ شَكُورٌ حَلِيمٌ ﴿١٧﴾

17. Mkimkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, atawazidishia maradufu, na atawaghufiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa shukrani, Mpole.

عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١٨﴾

18. Mwenye kujua ghaibu na dhahiri. Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

UADUI WA WAKE NA WATOTO

Aya 14 – 18

MAANA

Enyi mlioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu ni maadui zenu. Basi tahadharini nao.

Katika vitabu vya tafsiri na Hadith kuna maelezo kuwa kuna watu waliosilimu Makka na wakataka kuhamia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) , wake zao na watoto wao wakawazuia. Ndipo ikashuka Aya hii kuwahadharisha waumini wasiwatii baadhai ya wake zao na watoto.

Mara nyingi tumesema kuwa sababu ya kushuka haiihusishi Aya na tukio hilo, bali inaenea. Hiyo inakuwa ni sehemu tu miongoni mwa sehemu zake. Kwa hiyo basi kila mke asiyesaidiana na mumewe kwenye lile lilo na masilahi kwa pande zote mbili kidini na kidunia, basi huyo ni adui yake.

Pia mume atakuwa ni adui wa mke akiwa naye ni kikwazo kwa hilo. Vile vile kwa upande wa mtoto na mzazi bali mama na ndugu. Lolote linalofanywa na adui, akilifanya naye pi atakuwa ni adui, kwa hali yoyote itakavyokuwa.

Kwa mnasaba huu tunasema kuwa, kutoka mtu kwenye maisha ya useja kwenda kwenye maisha ya ndoa kunafanana na kwenda Akhera; itakuwa ni Peponi au motoni. Mara nyingi sana ni motoni sio kwenye neema. Kwani maisha ya familia wakati huu ni adhabu na Jahannam - mtoto hawezi kumridhia baba yake ila kwa kutiiwa yeye na kunyenyekewa, wala mke hamridhii mume ila awe yeye ndio mume na mume awe mke!

Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Hakuna tofauti baina ya msamaha, kupuuza na maghufira isipokuwa kwenye matamshi tu. Makusudio ya kuyachanganya matamko haya ni kiasi cha kusisitiza na kuhimiza tu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuhadharisha baadhi ya wake na wato­to kwa vile wanafanya wayafanyayo maadui akasema: Mkiwasamehe kwa kuwahurumia na kutumaini kurekebika kwao, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafanyia hivyo hivyo nanyi, kwa sababu Yeye humhurumia mwenye huruma na humsamehe mwenye kusamehe, lakini ni pale ikiwa kufanya hivyo ni vizuri; vinginevyo baadhi ya makosa haifai kuyasamehe kwa hali yoyote.

Aya inaashiria kwamba maisha ya famailia hayawezekani isipokuwa kwa subira na kusamehe. Na kwamba lau mtu atahisabu kila linalotoka kwa watoto wake basi mzozo usingemalizika na wangeliishi kwenye Jahannam.

Hakika mali zenu na watoto wenu ni mtihani. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna ujira mkubwa.

Kila litakalokuvutia na kukuzuia na majukumu ya kidunia na akhera, hilo ni mtihani; iwe ni mali, mtoto, mke, cheo, usanii n.k. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kutaja mali na watoto, kwa sababu ndiyo mambo yanayoongoza kwenye majaribu. Kadiri ladha ya dunia itakavyokuwa kubwa, lakini yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na yenye kubaki. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (8:28). Katika Tafsir Tabari na nyinginezo kuna maelezo haya: “Mtume(s.a.w. w )

alikuwa akihutubia, akaja Hasan na Husein wakiwa wamevaa kanzu nyekundu, wakijikunguwaa na kusimama. Basi Mtume akashuka akawachukua na kuwabeba mapajani mwake; kisha akasema: Amesema kweli Mwenyezi Mungu: Hakika mali zenu na watoto wenu ni mtihani. Nimewaona hawa na kukatisha mazungumzo yangu ili niwachukue. Kisha akaendelea na hutuba yake.

Basi mcheni Mwenyezi Mungu vile mwezavyo,

Fanyeni bidii kadiri mnavyoweza kuzichunga nafsi zenu na majaribio na mjiweke mbali na aliyoyaharimisha Mwenyezi Mungu wala msifanye chochote cha haramu kwa sababu ya mali au watoto.

Kuna mfasiri aliyesema kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha.” Juz. 4 (3:102) ni ya mkazo zaidi na kauli yake hii hapa ‘Basi mcheni Mwenyezi Mungu vile mwezavyo,’ ni ya tahafifu; kisha akaongezea hapo kuwa kauli hii imeondoa hukumu ya kauli ile.

Sisi hatuoni tofauti yoyote baina ya Aya mbili hizi, kwa sababu wajibu wa mtu ni kujikinga na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, kadiri atakavyoweza, wala yeye halazimiki na asichokiweza. Tazama Juz. 3 (2:286).

Na sikieni, na tiini, na toeni,

Sikieni mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na muuchunge kwa utiifu na takua, na toeni ziada ya mali yenu katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hiyo itakuwa heri kwa nafsi zenu; yaani:

إِنْ أَحْسَنتُمْ أَحْسَنتُمْ لِأَنفُسِكُمْ وَإِنْ أَسَأْتُمْ فَلَهَا ﴿٧﴾

“Mkifanya uzuri mnajifanyia wenyewe na mkifanya ubaya mnajifanyia wenyewe.” Juz. 15 (17:7)

Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.

Kutoa mali na nafsi ni njia ya kufaulu na kuokoka na kuifanyia ubahili mali na nafsi ni njia ya hasara. Kwa sababu ubahili na uchoyo ni katika nguvu kubwa inayopelekea kujiingiza kwenye maovu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juzuu hii tuliyo nayo (59:9).

Mkimkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, atawazidishia maradufu, na atawaghufiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa shukrani, Mpole.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anataka mkopo kwa waja wake na hali anazo hazina za mbingu na ardhi, anawazidishia malipo watiifu kwa hisani kutoka kwake, anawaghufiria wenye kutubia kwa kuwahurumia, anawashukuru wenye kufanya ihsani kwa kuwapa kingi kutokana na kichache walichotoa na anawapa muda waasi; kama kwamba amewasamehe. Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:245), Juz. 9 (5:12) na Juz. 27 (57:11).

Mwenye kujua ghaibu na dhaahiri hakifichiki kitu chochote kwake.Mwenye nguvu, isiyoshindwaMwenye hikima katika alivyoumba na kupangilia.

MWISHO WA SURA YA SITINI NA NNE: SURAT AT – TAGHABUN