• Anza
  • Iliyopita
  • 8 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 6287 / Pakua: 1377
Kiwango Kiwango Kiwango
HIDAYA YA RAMADHANI

HIDAYA YA RAMADHANI

Mwandishi:
Swahili

HIDAYA YA RAMADHANI

Kitabu hiki kinazungumzia kufunga na kufungua katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na vile Muislamu anatakiwa awe katika mwezi huu.

Kimeandaliwa na: Ahlulbayt Organization

KHUTBATU SHAABAANIYYA

Khutba hii ilitolewa na Mtume Muhammad(s.a.w.w) katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Shaabaan.

Imepokewa na Imam Ali(a.s) amesema; "Mtume(s.a.w.w) alituhutubia siku hiyo na alisema:

'Enyi watu! kwa hakika umewakaribieni mwezi wa Mwenyezi Mungu, kwa baraka na rehma na maghfira, (huo ni) mwezi ambao mbele ya Mwenyezi Mungu ni bora ya miezi yote, na masiku yake ni bora ya masiku yote, na usiku zote, na masaa yake ni bora ya masaa yote. Huo ni mwezi ambao mmealikwa ndani yake katika dhifa ya Mwenyezi Mungu, na mmefanywa kuwa ni watu wenye karama ya Mwenyezi Mungu.

“Pumzi zenu katika mwezi huo ni tasbihi, na usingizi wenu katika mwezi huo ni ibada, na amali zenu katika mwezi huo ni zenye kukubaliwa, na du'a zenu ni zenye kujibiwa, basi muombeni Mwenyezi Mungu, Mola wenu kwa niyya zenye ukweli, na mioyo misafi ili awawezeshe kuufunga mwezi huo na kukisoma kitabu chake, kwani yule aliyepata hasara ni yule aliyekosa maghfira ya Mwenyezi Mungu katika mwezi huu mtukufu. Na kumbukeni kwa njaa yenu na kiu yenu katika mwezi huo, njaa na kiu ya siku ya kiyama.

“Wapeni sadaka mafakiri wenu na masikini wenu, na waheshimuni wakubwa wenu, na wahurumieni wadogo wenu, na dumisheni undugu wenu, na chungeni ndimi zenu, na kifungieni macho kile ambacho hakifai kutizamwa na macho yenu, na kile ambacho hakifai kusikizwa na masikio yenu, wafanyieni upole mayatima wa watu wengine ili nao wawafanyie upole mayatima wenu. Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu madhambi yenu, na mnyanyulieni mikono yenu mnapo omba du'a katika nyakati za sala zenu, kwani hizo ni nyakati bora zaidi, Mwenyezi Mungu huwatizama waja wake katika nyakati hizo kwa upole, huwajibu pindi wanapomuomba, huwapa wanapomuuliza.

“Enyi watu, hakika nafsi zenu zimewekwa rehani kwa amali zenu, basi zifungueni kwa kuomba kwenu msamaha, migongo yenu ni mizito kwa mizigo yenu ya madhambi, ipunguzieni uzito huo kwa kurefusha sajda zenu, na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu ameapa kwa utukufu wake kuwa hatawaadhibu wenye kusali na kusujudu, na kwamba hatawaadhibu kwa moto siku watakapo simama watu kwa Mola wa walimwengu.

“Enyi watu, mwenye kumfuturisha mtu mu'umin aliyefunga miongoni mwenu katika mwezi huu, jambo hilo mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na kumuachilia mtumwa huru, na husamehewa madhambi yake yaliyopita.

Ikasemwa:-

'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sio wote kati yetu wanaoweza jambo hilo.'

Mtume(s.a.w.w.) akasema:-

'Ogopeni moto japo (mfuturishe) kwa tende moja, ogopeni moto japo kwa kunywesha maji'.

“Enyi watu! mwenye kuifanya tabia yake iwe nzuri miongoni mwenu katika mwezi huu, malipo yake ni kuweza kupita katika Swiraat kwa usalama siku ambayo miguu ya watu wengine itakapokuwa ikiteleza. Na mwenye kumpunguzia katika mwezi huu kazi, mjakazi ambaye amemumiliki kwa mkono wake wa kulia, Mwenyezi Mungu atampunguzia hesabu (madhambi) zake.

“Na atakayezuia shari yake katika mwezi huu, Mwenyezi Mungu atazuia ghadhabu zake siku atakayo kutana naye. Na atakayemkirimu yatima katika mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamkirimu mtu huyo siku ya Kiyama. Na atakaye dumisha undugu katika mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamdumishia rehma zake siku atakayokutana naye. Na atakayevunja undugu ndani yake, Mwenyezi Mungu atamvunjia rehma zake siku atakayokutana naye.

“Na atakaye sali sunna ndani yake, Mwenyezi Mungu atamwandikia awe mbali na moto. Na atakayetimiza faradhi moja ndani yake, atakuwa na thawabu amabazo atakuwa sawa na atakayetimiza faradhi sabini zenye kuwa sawa katika miezi mingine. Na mwenye kukithirisha kuniswalia mimi ndani ya mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamfanyia uwepesi mizani yake siku itakayokuwa ni mzito mizani nyengine (kwa madhambi). Na atakayesoma ndani yake aya moja ya Qur'ani malipo yake yatakuwa ni sawa na yule aliyehitimisha Qur'ani katika miezi mingine isiyokuwa Ramadhani.

Enyi watu! hakika milango ya pepo katika mwezi huu iko wazi, basi muombeni Mola wenu asiifunge kwenu nyinyi. Na milango ya moto imefungwa, muombeni Mwenyezi Mungu asiifungue kwenu. Na Mashetani wamefungwa, basi muombeni Mola wenu wasije wakawatawala juu yenu..."

Imam Ali Ibn Abi Talib(a.s) alimuuliza Mtume(s.a.w.w) :

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni tendo gani lililo bora kabisa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani?"

Mtume Mtukufu(s.a.w.w) alijibu:

"Ewe Abu'l Hasan, bora ya matendo yote katika mwezi huu Mtukufu ni kujiweka mbali kabisa na yale yaliyoharamishwa na Allah s.w.t.

“Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu, Siku chache tu (kufunga huko). Na atakaye kuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi (atimize) hisabu katika siku nyingine.

Na wale wasioweza, watoe fidia kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake. Na (huku) kufunga ni bora kwenu. Ikiwa mnajua (haya sasa basi fuateni).

Al Baqarah 2: 183 – 184.

HIDAYA YA RAMADHANI

SAUMU NI AMRI YA MUNGU

Sisi kama Waislamu, hatufuati amri yeyote ile ila sharti iwe imenasiwa katika Qur'ani ama katika Hadithi tukufu za Mtume wetu(s.a.w.w)

Saumu katika Qur'ani imetajwa kutoka Aya ya 183 ya Sura ya pili 'Albaqarah' hadi Aya ya 187 ya Sura hiyo hiyo.

Mwenyezi Mungu ametufunza kama ifuatavyo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

"Enyi mlioamini, mmelazimishwa kufunga Saumu kama walivyolazimishwa wa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu."

أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٨٤﴾

183. Ni siku chache tu (zinazohesabiwa) lakini miongoni mwenu awaye mgonjwa au katika safari, basi atimize hesabu katika siku zingine. Na wale wanaoweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake basi ni bora kwake, na mkifunga ni bora kwenu mkiwa mnajua.

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٨٥﴾

185. (Mwezi mnaoambiwa kufunga) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa mwongozo kwa watu na ishara zilizo wazi za mwongozo na kipambanuzi. Basi miongoni mwenu atakayeuona mwezi (au atakayekuwa mkazi asiwe msafiri pindi mwezi ufikapo) afunge Saumu na mwenye kuwa mgonjwa au safarini basi atimize hesabu katika siku zingine. Mwenyezi Mungu Huwatakieni mepesi wala Hawatakieni yaliyo mazito, na kamilisheni hesabu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwaongozeni na ili mpate kumshukuru.

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

186. Na waja wangu watakapokuuliza juu yangu basi hakika Mimi nipo karibu, Nayaitika maombi ya mwombaji anaponiomba, basi waniitikie na waniamini ili wapate kuongoka.

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿١٨٧﴾

187. Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuwaingilia wake zenu (yaani kutangamana nao) wao ni nguo kwenu na nyinyi ni (kama) nguo kwao, Mwenyezi Mungu amejuwa kuwa mlikuwa mkizihini nafsi zenu, kwa hivyo amewakubalieni toba zenu na amewasameheni, basi sasa changanyikeni nao (yaani laleni nao) na takeni aliyowaandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni, mnyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe katika uzi mweusi wa Alfajiri, kisha timizeni Saumu mpaka usiku, wala msitangamane nao na hali mnakaa itikafu misikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu basi msiikaribie. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyobainisha hoja zake kwa watu ili wapate kumcha.

Maneno hayo ufasaha usioweza kukabiliwa na mfasaha yeyote, ndiyo asili na misingi ya Saumu. Yeyote abishanaye au kukaidi Amri tunamjibu na kumlainisha kwa nasaha hiyo.

FUNGA UKIUONA

Fungeni Mkiuona Na Fungueni Mkiuona (Mtume(s.a.w.w).

Ndugu Mwislamu, yakupasa kujua kwamba kufunga mwezi wa Ramadhani hakutegemei kuwa sikia watu wakizungumza kwamba "Kesho ni Saumu, kesho ni Saumu...." Na hujui sababu ya hao watu na usemi wao huo, bali na wewe mwenyewe wahitajika kujua matukio ya dini yako:

a. Utakapouona mwezi umeandama, ni lazima juu yako kuamkia kufunga na sawa watu wengine wamefunga au hawakufunga, kwako si halali kula hata kidogo na ukila ni juu yako kuilipa siku hiyo na kafara.

b. Habari zikienea mitaani, mijini au barabarani kwamba mwezi umeandama na ukaonekana, na kukawa hakuna uwezekano wa wao kusema uongo, basi ni lazima kuanza Saumu mara moja asubuhi yake.

c. Habari zikitoka mji mwengine ambao si wa mbali sana (kama hapa Kenya na Tanzania na mfano wake) kwa njia ya Radio au simu kwa ushahidi unaoaminika au kutegemewa, Saumu italazimu.

d. Watu wawili unaowaamini watakapokupa habari za kuonekana Hilal (mwezi mwandamo) utalazimika kuwaamini na kuamkia Saumu ingawa wewe mwenyewe hukuona.

e. Pengine kunaweza kuwa na mawingu ambayo yanaweza kuzuia kuonekana kwa mwezi, hapa basi lililo lazima kwako ni kutimiza 30 za Sha’bani na baadaye kuzingatia kuonekana kwa mwezi kutakuwa hakuhitajiki.

ANGALIZO

Kauli ya mnajimu (yaani mtu mwenye utaalamu wa kinyota) akitoa hukumu yake ya kinyota kuhusu kuonekana kwa mwezi hazingatiwi.

SOMA DUA HIZI UKIUONA MWEZI

Ukiuona mwezi umeandama, simama wima huku umeelekea Kibla, na usome:

"Ee Mwenyezi Mungu! Tunakuomba Utuukaribishie mwezi huu kwa amani, imani, na kwa Uislamu kamili (na tunakuomba katika mwezi huu) afya bora, riziki pana, na utuondolee maradhi. Ee Mola wetu! Tujaalie tuufunge wote, tusimame kwa Ibadati, tusome Qur'ani kwa wingi, tujaalie tuupokee, (nao mwezi) Utupokee, na tunakuomba Utuvushe salama.

Pia ni vizuri kusoma Dua hii ya Amiril Muuminina Aly Bin Abi Talib (a.s) baada ya kuuona mwezi.

“Ee Mola wetu! Ninakuomba heri za mwezi huu na heri za mwanzo wake na ninakuomba mwangaza wake, pia nusura yake, baraka zake, utufuku wake na riziki zake. Pia ninakuomba heri zilizomo katika mwezi huu na heri zijazo, na ninajilinda kwako na shari zitakazokuwemo katika mwezi huu na shari zitakazokuja baada yake.

“Ee Mwenyezi Mungu! Ulete kwetu kwa amani, imani, usalama, na kwa Uislamu, pia tunakuomba baraka, na Utujaalie tukuogope zaidi katika mwezi huu, na mambo yetu yawe ni yenye kuwafikiana na Uyapendayo na Ukayaridhia.”

Dua hizi ni bora zaidi kwa Mwislamu kuzisoma punde tuu baada ya kuonekana mwezi. Na wakati wa kuzisoma ni bora zaidi uwe umeelekea Kibla - yaani huko Makkah.

FAIDA ZA SAUMU

Limekuwa jambo jema kueleza faida za Saumu ili kila afungaye ajuwe hasa masumbuko yake ni kwa sababu gani? Kwani si vyema mtu kutaabika na hali hajui matokeo ya shughuli zake, na pengine huenda akaingia katika kundi la wale waliotajwa na mshairi mmoja kwamba:

Mfisada mkubwa ni mjuzi mwenye kupotosha (bila kujua) na aliye muovu zaidi ni mjinga mwenye (kupenda) ibada. Hao watu wa aina mbili hizi ni fitina kubwa kwa watu na hasa kwa mtu aliyeshikamana na dini kwa kuwafuata. Jee, vipi utamfuata mtu ambaye hajui?

Mshairi mwengine amenena:

Ewe mtu (mjinga) unayemfundisha mwenzako, jee wewe nafsi yako unajua unachofundisha? Wampa dawa mtu aliyokonda na mwenye maradhi ili apone (kwa hizo dawa) na hali wewe ni mgonjwa?"

Faida za kufunga ni nyingi mno, miongoni mwazo ni: kutekeleza mojawapo ya amri za Mwenyezi Mungu Alizotufaradhia kwetu sisi na faida ya utekelezaji huu ni kuingia peponi.

Faida ya pili ya Saumu ni kujizoeza subira, yaani katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, mtu anajifunza jinsi ya kuweza kuvumilia na kustahamilia njaa, kiu, na kila matamanio ya kimwili. Mtume(s.a.w.w) amenena:

"Huo mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kusubiri, na hakika subira malipo yake ni pepo tu".

Faida ya tatu ni kuwa na uadilifu na kujifundisha usawa baina ya tajiri na maskini.

Imam Ja'far As-sadiq(a.s ) alisema:

"Hakika si jingine, Mwenyezi Mungu amefaradhisha kufunga ili wapate kulingana tajiri na maskini (katika shida ya njaa na kiu) basi akapenda viumbe vyake wawe sawa, na Amwonjeshe tajiri maumivu ya kushikwa na njaa ili apate kumhurumia mnyonge, na apate kumsikitikia mwene njaa".

Faida ya nne na ambayo ni muhimu zaidi ni kughufiriwa katika mwezi huu na kusamehewa madhambi yote ya mwaka ikiwa mwenye kufunga ameyafuata masharti yote na kufunga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Mtume(s.a.w .w ) katika mojawapo ya hotuba alizozitoa kwa minajili ya mwezi huu akasema:

"Enyi watu! Hakika umewaelekeni nyinyi, mwezi wa Mwenyezi Mungu (mwezi wa Ramadhani) kwa baraka, rehema na msamaha. Mwezi ambao ni bora mbele ya Mwenyezi mungu kuliko miezi yote, na siku zake ni bora kuliko siku zote, na masiku yake ni bora kuliko masiku mengine yote na masaa yake ni bora na muhimu kuliko masaa yote."

AFYA

Faida ya tano ya Saumu inahusu upande wa afya. Kwa kawaida chochote kifanyacho kazi sharti kipumzike kwa muda. Hata mitambo, kwa mfano, ambayo imeundwa kwa vyuma imara tena vyenye nguvu, hufika wakati ambao huwa lazima kusimama kwa marekebisho ili ipate nguvu zingine za kuendelea upya. Jee vipi kwetu sisi ambao tumeumbwa wadhaifu tusivipumzishe baadhi ya viungo vyetu na hasa tumbo ambalo huendelea na kazi mfululizo kva miezi kumi na moja? Hapo utauona ulazima wa kuyapumzisha matumbo yetu ili kuhifadhi siha zetu.

MADAKTARI

Madaktari wote wakuu ulimwenguni, wamekariri na kuthibitisha faida hii, na wote wa nyuma ya Daktari wetu mkuu(s.a.w.w) Aliposema:

"Fungeni ili mpate siha nzuri." Naye lmam Ja'far As-sadiq(a.s.) anasema:"Kila kitu kina utakaso, na kitakaso cha mwili ni kufunga (Saumu).”

"Ni wajibu juu ya kila mtu mgonjwa ajizuie kula ijapokuwa kwa muda wa siku moja tu katika kila mwaka". Haya yalisemwa na daktari wa Kimarekani aitwaye Dr. CAR. Pia akaongeza "Vijidudu viambukizavyo maradhi huendelea na kunawiri maadam mwenye mwili anaendelea na kula na kuvilisha na hivyo basi vitaendelea kukua. Ama lau utajizuia kula vitadhoofika.”

Madaktari wote Waislamu na wasio Waislamu wameliwafiki shauri hili. Miongoni mwao ni Dr. Abdul Aziz bin Ismail aliyesema kwamba kufunga siku moja ni kinga ya maradhi ya mwaka. Isitoshe kwa siku hizi kumetokea hospitali mbali mbali ambazo zimehimiza na kusisitiza umuhimu huu, kadhalika mara nyingi tunashuhudia wagonjwa wengi sana ambao huzuiwa kula kwa manufaa ya afya zao.

Mwalimu wa Cairo University aitwaye Dr Muhammad Dhawahir asema: "Ugonjwa wa kuzidi maji mwilini, unene, moyo, ini, pafu, n.k. huzuiwa na kufunga (Saumu)."

HIDAYA YA RAMADHANI

MAANA YA 'SAUMU'

Neno 'Saumu' ki lugha ya Kiarabu lina maana ya kujizuia. Pia ni neno ambalo lilitumika kabla ya zama za Uislamu. Baadaye Uislamu ulipokuja ukalijaalia neno hili kuwa ni moja kati ya maneno yatumikayo kiibada.

Ama maana ya neno hili Kisheria, ni kujizuia kutokana na mambo yanayobatilisha Saumu yaitwayo 'al-Muftiraat'.

Kinyume cha watu wengi wanavyodhani kwamba Saumu hasa ni kujizuia kula na kunywa tu. La Hasha! Bali Saumu ni kukihifadhi kila kiungo chako kutokana na mambo yasiyotakikana.

Amesema lmam Ja'far As-sadiq(a.s.) :"Kufunga siko kujilinda na kula na kunywa tu, bali utakapofunga hifadhi (chunga) macho yako, ulimi wako, tumbo lako, masikio yako na uchi wako. Vile vile ilinde mikono yako, pendelea sana kunyamaza ila katika heri tu (kama kusoma Qur'ani n.k.) na umhurumie mtumishi wako."

Naye Mtume(s.a.w.w) amesema:"Mambo matano hutengua Saumu ya mtu: Uongo, kuseng'enya, kufitinisha, kula viapo vya uongo na (mwanamke) kumkazia macho mwanamume asiye maharimu wake au (mwanamume) kumkazia macho mwanamke asiye maharimu wake kimatamanio.”

Kuseng'enya kumekatazwa katika kauli hii ya Mtume(s.a.w.w) na badala yake tunahimizwa na hadithi nyingi tujiepushe na lolote la kutuharibia Saumu zetu.

Mtume(s.a.w.w) anasema:"Mwenye kufunga huwa ibadani wakati wowote hata kama analala madamu hajaitengua Saumu yake kwa kusengenya".

Kwa hapa utaona kwamba, kule kutokula na mfano wake kama tulivyo yabaini hapo mbeleni siko kufunga hasa kunakotakikana, bali kufunga ni kujizuia na makatazo yote na mabaya.

NYAMA MDOMONI

Siku moja Mtume(s.a.w. w ) alimsikia mwanamke mmoja akisengenya na hali amefunga. Mtume(s.a.w. w ) akamwitishia chakula ili ale. Yule mwanamke akasema: "Mimi nimefunga". Mtume akaendelea kuhimiza chakula iletwe mara moja ili yule bibi ale naye, yule bibi azidi kukariri kuwa angali anafunga.

Hapo Mtume akamwambia:

"Unafungaje na hali menoni mwako mna kipande cha nyama? Yule mwanamke akazidi kubishana na huku Mtume amwambia"Hebu tia mkono wako kinywani mwako" na kweli alipouingiza mkono wake menoni, alitoa kipande cha nyama. Hapo Mtume(s.a.w. w ) akamwambia"Waona? Wataka kula nyama ya nduguyo aliyekufa?” Yaani kusengenya ni sawa na kula nyama ya mfu tena nduguyo.

Hapo waona ndugu? Kwa hakika kile kipande cha nyama mdomoni mwa yule bibi kilipatikana kwa kule kusengenya, na yeyote asengenyaye huwa Saumu yake si sawa na huwa amekula nyama ya mfu tena nduguye.

PIA KUTUKANANA

Siku moja Mtume(s.a.w. w ) alimsikia mwanamke mmoja akimtusi msichana wake - mfanya kazi - na yule bibi alikuwa amefunga. Mtume(s.a.w. w ) akaitisha maji ampe yule bibi afuturu (na ilikuwa ungali mchana).

Yule bibi akasema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nimefunga". Mtume(s.a.w. w ) akajibu,"Unawezaje kumtusi mtu au kumteta na hali umefunga? Wewe tayari Saumu yako ni batili, yaani si makbuli.”

Viungo vyako ni hadiya ya Mwenyezi Mungu kwako, kwa hivyo haifai kuvifanyia hiana.

Katika masiku haya ya Saumu, na mengine pia ambayo ni heshima kuu na utukufu kwa Waislamu, ni lazima kujilinda.

Miguu : Isielekee kulikokatazwa ambako kunajulikana kama Makadara, kwenda disco, kwenda sinema na kadhalika, na badali yake ni muhimu lau tutakwenda misikitini, kutembeleana kwa heri kama alivyotuhimiza Mola wetu kwa kutuambia: "Saidianeni katika mema na kwa kumcha Mwenyezi Mungu, lakini msisaidiane katika kumwasi Mola na kufanyiana uadui.” Na kujilinda huku kuendelee hata baada ya Ramadhani.

Mikono : Izuie kuwadhuru watu kwa kuwaibia, kuua, kupiga na kadhalika, na badala yake ishikishe Qur'ani, iamkize jamaa na kadhalika.

Macho : Usiyatizamishe ulichokatazwa. Kuwaangalia watu wasio wa maharimu yako, kutamani kisicho chako na kadhalika bali fungua Msahafu usome.

Masikio : Usisikilize upuzi uliokatazwa kama nyimbo, kusengenya, udaku na kadhalika na badala yake nenda ukasikilize mawaidha na kama hayo ambayo ndani yake mna radhi ya Allah (s.w.t).

MASHARTI YA SAUMU

Saumu Ni Wajibu Kwa Masharti Manane

Mwenyezi Mungu amesema:

"Basi atakayekuwa katika mji (asiwe msafiri) katika mwezi huu afunge". Qur'ani 2:185.

Wakati tunapojiandaa kwa kuianza Ramadhani, tunapaswa kujua kwamba, amri ya kufunga ni yake Mwenyezi Mungu. Na wala amri hii haikuwa ya yeyote yule kati ya viumbe. Muda huu wa Saumu mtu hutakiwa kufanya ibada kwa wingi. Kuomba, kusoma dua mbali mbali na kuomba maghfira.

Na masharti yafuatayo ukiwa umeyakamilisha utalazimika kuanza Saumu, na wala hutokuwa na udhuru wowote ukuzuiao kufunga.

1. Al-Islam: Uislamu ni shuruti moja katika shuruti za kukubaliwa Saumu na ibada zote. Ijapokuwa juu ya kafiri pia ni wajibu kufunga na kufanya ibada zote, lakini kwa vile yeye si Mwislamu basi haitasihi na kukubaliwa ibada zake.

Mwenyezi Mungu anaamrisha wasali lakini shuruti (watawadhe au watayammamu). Basi kafiri pia inampasa afunge, lakini shururti za kusihi hiyo saumu yake ni kukubali Islamu, na Kafiri anaweza kusilimu.

2. Baleghe: Ukiwa umebaleghe (mwanamume) kwa kutimiza miaka kumi na mitano na mwanamke kwa kutimiza miaka tisa; au ukiwa wewe ni mwanamke aliyewahi kutokwa na damu ya mwezi, au ukiwa umewahi kuota ndoto kama unatangamana na mke (ukiwa mume) au na mume (ukiwa mke) na kutokwa na manii kwa ndoto hiyo, utalazimika kuanza kufunga.

3. Nia: Ni makusudio ya kutenda, nayo ni fardhi kwa kila ibada na ni sharti katika ibada zote. Lazima kunuia kujizuia na kila kinachobatilisha Saumu, na si lazima wakati wa nia kuzikumbuka zote kwa jina, inatosha kuweka nia ya kujitenga na kila kinacho haribu na kubatilisha Saumu.

Kuweka nia ni wajib. Ikiwa kwa mfano, siku moja kabla ya kuingia Ramadhani mtu bila ya nia ya kufunga akalala na asizindukane ila baada ya magharibi ya usiku wa pili wa mwezi wa Ramadhani, basi kukosa kula na kunywa siku hiyo moja ya Ramadhani bila ya nia haitasihi, na lazima baadaye ailipe.

Mtu anaweza kila usiku wa Ramadhani kuweka nia ya kufunga kesho yake, na ni vizuri usiku wa kwanza wa mwezi wa Ramadhani aweke nia ya mwezi mzima.

WAKATI WA KUWEKA NIA

Wakati wa kuweka nia ya Saumu ni kutoka mwanzo wa usiku hadi adhana ya asubuhi (Alfajiri) kwa saumu za fardhi, ama saumu za sunna huanzia mwanzo wa usiku, hadi kiasi cha kunuia kumebaki kufikia magharibi, ikiwa mpaka wakati ule hakutenda kitu cha kuvunja saumu, basi hapo aweke nia ya saumu, na saumu itasihi.

Ikiwa mtu bila ya kuweka nia kabla ya Alfajiri akalala, na akaamka kabla ya adhuhuri na hapo akiweka nia, saumu yake itasihi, ikiwa saumu ya fardhi au ya sunna; lakini akizindukana baada ya adhuhuri, basi hapo hawezi kuweka nia ya saumu ya fardhi. Ikiwa kabla ya alfajiri kanuia na akalala na asiamke ila baada ya magharibi, saumu hiyo itasihi haidhuru neno.

AL-KHULUUS

Lil-Laahi Ta'ala, maana yake, kufunga kwake iwe Lil-Laahi, Ta'ala tu, lau akiongeza Riya (kwa kujipendekeza) tu hapa saumu yake haitasihi.

4. Ukiwa (wewe mke) unayo damu ya mwezi au ya uzazi, unashauriwa kusubiri hadi itakapokoma ndipo uanze kufunga, hata hivyo utalazimika kuzilipia siku ambazo zimekupita.

5. Kwa aliye na kichaa na wazimu huyo anasamehewa Saumu zitakazompita muda wa udhuru wake huo.

6. Ukiwa umgonjwa hulazimiki kufunga hadi utakapopata nafuu, hata hivyo ni ugonjwa usiokuwezesha kufunga tu ndio unaokusudiwa kwa hapa, kama mtu mwenyewe anajihisi udhaifu, na kutovumilia Saumu atafuturu.

7. Ujue vile vile kwamba, msafiri (safari yenye umbali maalumu) si halali kwake kufunga hadi arudipo uwenyejini.

8. Pia kwa aliye na ugonjwa wa kifafa halazimiki kufunga na badala yake anaruhusiwa kula.

MZEE NA NAHODHA

Mzee mkubwa, na kadhalika vikongwe wasio na uwezo wa kustahamilia Saumu, wanaruhusiwa na sheria wasifunge na watoe sadaka ya kibaba (sawa na kilo kasorobo) kwa kila siku. Kibaba hiki kiwe ni cha chakula kitumiwacho sana na watu wa sehemu hiyo, na pia hukumu hii humhusu mwanamke anayenyonyesha na aliye na mimba wakijichelea au kuchelea wana wao, wanaruhusiwa na sheria kufuturu.

Isipokuwa hawa wawili wa mwisho watalazimika kulipa nyudhuru zao zikiisha kabla ya Ramadhani nyengine kufika.

Msafiri asafiriye umbali wa Km. 48 halazimiki kufunga, bali atafuturu ingawa haambiwi ale bali atajizuia vivyo hivyo na kulipa baada ya Ramadhani kumalizika. Na safari, sharti iwe ya halali; pia isiwe kazi yake kama kondakta, dereva nahodha n.k. asiwe atakaa huko zaidi ya siku 10 akiwa atakaa zaidi ya siku 10 atafunga hata huko huko safarini.

Kafiri wa kuzaliwa akisilimu halazimiki kulipa Saumu zilizompita alipokuwa ukafirini. Kadhalika mtoto akibaleghe, na aliyekuwa na kicha (wazimu). Ama aliyepitiwa na Saumu kwa kuwa na hedhi, nifasi, ugonjwa,n.k. hulipa.

PIA SALA

Ili kuthibitisha utiifu wetu kwa Mwenyezi Mungu na ili Saumu zetu zikubaliwe, ni sharti tutekeleze amri zake zote pasina kuziacha zingine. Sala ni mojawapo wa mahimizo makubwa kwa Mwislamu na lau atajisumbua kwa kuumwa na njaa bure pasina kusali, ajuwe kuwa hana fungu lolote katika Saumu yake. Kwa hivyo tukiwa tunataka thawabu zaidi na zaidi ni lazima sala hata tusiziache.

Sala ni nguzo ya pili katika nguzo za Islamu, na tukumbuke kwamba, tukiwa na sala pungufu, hata mali zetu zi katika mafungu yasiyotakikana, na zikiwa kamili, hata ibada zinginezo zitakuwa makbuli Inshaallah.

'NAFSI' NI ADUI

Mwenyezi Mungu Anasema,"Na kiwe katika nyinyi (Waislamu) kipote ambacho kitawalingania watu katika mambo ya kheri, kiwe kinaamrisha mema na kinakataza maovu.”

Kuamrishana mema na kukatazana maovu ni jambo la lazima kwa kila mwislamu awaye mume au mke, na hasa wakati wa Ramadhani.

Ingawa mwezi huu mashetani hufungwa kama ilivyopokewa katika hadithi, pana adui mwengine kwa mwanadamu ambaye husononeka sana anapomwona mwanadamu katika mwangaza wa utiifu, na ye si mwengine bali ni "Nafsi".

Mwenyezi Mungu Anasema:"Nafsi ni yenye kuamrisha (sana) maovu."

Mmoja wa wanavyuoni anasema: "Nafsi ni kitu kiovu zaidi ya mashetani elfu."

Nafsi hii hii ndiyo ambayo huwaghafilisha baadhi ya watu wasifunge mwezi huu, wala wasikumbuke kabisa adhabu ziwasubirizo wasiofunga.

Mtume(s.a.w. w ) alisema"Watu wasiofunga hufungwa miguu yao kwa pingu kisha wakaninginizwa vichwa vyao chini na miguu yao juu na huku wapigwa na kucharazwa mijeledi kemkem, pia huwa nyuma yao wale wanaokula kabla ya wakati maalum wa kufuturu haujafika."

Jee ndugu waona!!! Lakini lao kubwa ni kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Hakika wao wanaoiona (siku ya kiama) iko mbali nasi Tunaiona iko karibu sana."

Pia wanaofunga na huku hawasali, wao ni mfano mbaya sana kwa umma wa Kiislamu. Allah Anasema,"Adhabu kali sana itawathibitikia wale wanaosali na ambao wao katika sala zao hughafilika."

Waliokusudia hapa ni watu ambao wao husali leo kesho hawasali, husali asubuhi jioni hawasali na kadhalika. Ikiwa Mwenyezi Mungu Amekasirika hivyo hadi kufikia hatua ya kuapa kuwatia adabu wasiosali sawasawa, waonaje kwa yule asiyesali kabisa? Ama wasiosali wamewekeana mkataba na Mwenyezi Mungu wa kusameheana?

HIDAYA YA RAMADHANI

YANAYOHARIBU SAUMU

Kwa kuwa Mwislamu huwa na hamu kubwa ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhani, kadhalika anatakiwa kuwa na hamu ya kujichunga na mambo ambayo huenda yakamharibia saumu yake. Na mambo yenyewe ni haya:

1. Kula japo kitu kidogo sana;

2. Kunywa hata kama ni tone moja;

3. Kumwingilia mwanamke mchana hata kama manii hayakutoka;

4. Kujitoa manii kwa kujichezesha, au kwa kumchezesha mwanamke hata kama ni mkeo pia kunatengua;

5. Kutooga Janaba, Hedhi, au Nifasi hadi alfajiri pasina sababu ya udhuru maalumu pia kunabatilisha Saumu;

6. Kujifikisha vumbi - zito - kooni makusudi na kadhalika moshi wa sigara pia hubatilisha;

7. Enema-Kupigwa bomba yenye kitu cha majimaji (dawa) kwenye tundu ya nyuma pia kutaharibu;

8. Kujitapisha makusudi;

9. Kumkadhibisha Mwenyezi Mungu au Mtume wake Mohammad(s.a.w.w) au Maimamu watakatifu kuwa katika jambo fulani walisema hivi hali ni uongo kunabatilisha Saumu;

10. Kujitosa majini makusudi kwa kupiga mbizi, au kukitumbukiza tu kichwa pekee majini pia kunaharibu Saumu.

MASWALA TOFAUTI

Ingawa kula kunabatilisha Saumu lakini kunasamehewa kwa mtu yeyote aliyekula kwa kusahau, vile vile kunywa. Ama kuyameza mate yaliyojaa kinywani, hakuna makosa.

Kuyameza mabaki yaliyaliyosalia menoni wakati wa kula ama kunywa, kunabatilisha.

Kukiangalia chakula kwa hali ya kukitamani na hali umefunga hakubatilishi Saumu. Lakini ni vizuri zaidi kutokiangalia ukiwa wakitamani.

Kudungwa sindano si makosa kwa mtu aliyefunga. Naam, ni vizuri kutumia Ihtiyat (yaani kujitoa mashakani) kwa kutodungwa sindano iliyo na chakula.

Kumbuka kwamba nia ni muhimu sana na Saumu haisihi pasina kutia nia. Kunuia huku ni kusema moyoni. "Nia yangu ni kufunga kesho kwa ajili ya Mwenyezi Mungu". Kadhalika amali zote za ibada hazisihi pasina nia maalum kama alivyosema Mtume(s.a.w .w ) :"Matendo yote hufanywa kwa nia" . Na hivyo basi nia ni muhimu sana.

Mwenye Saumu akiazimia usiku kwamba mimi kesho sito funga basi Saumu ya siku hiyo haitasihi hata kama atabadili dhamira na kufunga tena hivyo basi atalazimika kuilipa siku hiyo. Na tukumbuke tena kwamba, mtu yeyote aliyeitengua Saumu haimfalii kula au kuendelea na vitendo vilivyokatazwa, bali analazimika kujizuia.

Kusukutua wakati wa kutawadha hakukatazwi lakini ni bora kukuepuka maana huenda maji yakakutangulia pasina kutegemea. Ama kule kupiga mswaki nako ni hivyo hivyo.

Mtume(s.a.w. w ) alisema "Harufu ya mdomoni wa mwenye kufunga ni bora na yenye manukato zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko marashi yoyote yale".

Ukimlazimisha mkeo kumwingilia na hali yeye mwenyewe hayuko radhi utalazimika kulipa na kutoa kafara, na pia kuaziriwa kwa kupigwa viboko 50. Na lau nyote mtaridhiana mtalazimika kulipa, kutoa kafara na kuaziriwa kwa kupigwa viboko 25 kila mmoja.

Ingawa tulieleza kwamba kutoka manii kwa kujimai (kuingiliana mke na mume) kunabatilisha Saumu na wanaohusika na kitendo hivyo huwa na janaba, hukumu hii haimhusu aliyetoka manii mchana wa Ramadhani kwa kuota usingizini, bali ataoga tu na Saumu yake haina dosari.

Udhuru wa kutokwa damu ya hedhi ukitokea japo bado kidogo tu magharibi kuingia Saumu yako itakuwa batili, na hivyo basi utalazimika kuirudia.

Kuteta katika mchana wa Saumu na hatimaye kupigana ni jambo baya sana na hasa kwa kuwa mwezi huu ni wa kusameheana, kuhurumiana n.k. Pindi ufungapo unapomuona mtu yeyote akikukabili na upuzi wowote ule, sema: "Innii Saaim", yaani:

“Hakika yangu mimi nimefunga” na ukifanya hivyo utakuwa umeukimbia uovu wote ambao huletwa na shetani.

Kutengua Saumu kwa jambo lolote la haramu kama kuzini, kulewa, na kadhalika, adhabu yake ni:

a. Kulipa siku 60 kwa siku mmoja iliyotenguliwa;

b. Kuwalisha maskini 60;

c. Kumwacha huru mtumwa.

HESHIMA YA RAMADHANI

"Mwezi wa Ramadhani ni ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa mwongozo kwa watu..." (Qur'ani: 2:185)

Waislamu kote ulimwenguni hufunga mwezi ambao ni mwema kuliko miezi yote, ulio na masiku bora kuliko masiku yote, wenye masaa ya baraka kuliko masaa yote na amali zifanyikazo katika mwezi huo ni makbuli kuliko baki ya maombi. Nao ni mwezi wa Ramadhani.

Mwezi huu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa tisa wa miezi wa Kiislamu, ni mwezi wa pekee wa aina yake kwa utukufu. Ni mwezi wa kusameheana, kuombeana heri na hata kufanya ibada kwa wingi na kwa usahali kabisa.

Mwezi huu una matukio mbali mbali ya kihistoria ambayo hayatasahaulika, na ambayo vile vile hupambanua wazi utukufu wake.

Imam Ja'far As-sadiq(a.s.) alisema kutoka kwa Babuye, Mtume(s.a.w. w ) "Taurati ilishuka na kumfikia Nabii Musa(a.s.) tarehe 6 Ramadhani, nayo Injili iIiteremshiwa Nabii Isa(a.s.) tarehe 12 za Ramadhani, kadhalika Zaburi ya Nabii Daud(a.s.) iliteremshwa mnamo tarehe 18 za Ramadhani, vile vile Qur'ani Takatifu iliteremka katika usiku wa Laylatul Qadri ambao kwa kawaida huwa katika mwezi huu wa Ramadhani."

Bila shaka hiyo ni heshima kuu kabisa. Na umejionea mwenyewe, hakuna kitabu kati ya vitabu vitukufu vinne kutoka kwa Mungu kilichoshuka ila kilishuka mwezi huu wa Ramadhani, na hayo yote ni kuonyesha utukufu wa mwezi huu. Kwa hivyo lazima vitendo vyetu katika mwezi huu viwe vitukufu kama mwezi wenyewe ulivyo.

Na katika Historia, tunasimuliwa baadhi ya matukio ya mwezi huu huu wa Ramadhani, kwa mfano:

1. Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib(a.s.) mwanawe Sayyidna Ali(a.s.) wa kwanza, na Mjukuu wa Mtume(s.a.w. w ) alizaliwa mwezi huu wa Ramadhani tarehe 15 mwaka wa 3 wa tangu Mtume kugura toka Makkah kuja Madina. Mtume mwenyewe ndiyo aliyemfanyia Akiki kwa kumchinjia mbuzi alipotimiza siku 7. Sayyidna Hasan(a.s.) , kama ilivyokuja katika Historia, alimfanana sana Babuye, Mtume(s.a.w. w ) sehemu ya juu. Naye Mtume(s.a.w. w ) alimnbashiria kuwa"Bwana wa vijana wa peponi".

2. Vita vya Badr vinavyojulikana zaidi (vita vikuu vya Badr, au Ghazwatul Badr) vilitukia siku ya Ijumaa mwezi wa Ramadhani tarehe 17 mwaka wa 624 A.D. Vita hivi ndivyo vilivyopambanua baina ya wakweli na waongo. Mushirikina (waabudu masanamu) waliharibikiwa sana na Waislamu ndio walioibuka na ushindi.

3. Katika mwezi huu huu, Mtume(s.a.w. w ) aliirudisha Makkah chini ya himaya ya Kiislamu tarehe 10 mwaka wa 630 A.D. Baada ya kuiteka Makkah, dini ya Islamu ilizidi mno nguvu na makafiri kuharibikiwa.

4. Imam, Sayyidna Ali bin Abi Talib(a.s.) , bin Ami yake Mtume(s.a.w. w ) aliyezaliwa katika Kaaba, alipigwa upanga na adui wa Uislamu, Abdu Rahmani bin Muljim tarehe 19 ya mwezi huu wa Ramadhani mwaka wa 40 Hijria.

Alipigwa upanga msikitini huko Kufa, Iraq alipokuwa amekwenda kusali sala ya Alfajiri, na alifariki siku ya tatu yake, yaani tarehe 21 Ramadhani.

Sayyidna Ali(a.s.) , Simba wa Mungu alishirikiana sana na Mtume(s.a.w. w ) na kuhudhuria vita vyote pasina kukimbia na ndiye aliyebaki kitandani cha Mtume(s.a.w. w ) alipokuwa akihamia Madina.

NASAHA KWA VIJANA

Vijana wa Kiislamu! Mwezi wa Ramadhani umetuwadia, hatuna wakati mwengine tuutarajiao tena na kuutumaini katika kufuzu kwetu usio huu. Balaa zote za kutuletea maafa hapo kesho (Akhera) tuziepuke na tuwe mbali kabisa nazo.

Katika mwezi huu hakuna masingizio yoyote, ambayo tunaweza kujisingizia nayo kama vile kudai kwamba 'O'..... Shetani ametushika sana! Kwani Mtume(s.a.w. w ) ametudokezea kwamba, "Mwezi wa Ramadhani unapoingia, milango yote ya rehema huwa wazi (kuwapokea wanaotaka kuingia), milango yote ya Jahannam hufungwa na Mashetani wote hutiwa minyororo ili wasiwahangaishe."

Ajabu kubwa zaidi ni kijana wa Kiislamu kuvaa ushanga, mikufu na bangili namna wafanyavyo wanawake. Ni hadi lini watajisitahi na kuwa na haya juu ya haya wayafanyayo?

Ni aibu kubwa kwa vijana wa Kiislamu kuhalifu sheria za dini yao hasa katika mwezi huu. Kwa kila aliye na uchunguzi, atastaajabu sana kumwona mtu aliyekuwa mnyenyekevu mchana kutwa, msalihina, kubadili hali hiyo na kuufanya usiku kuwa sitara ili kumdumishia maasi yake.

Ikiwa hawatajinasihi katika muda huu wa rehma na maghfira wakumbuke kuwa wamo hatarini ya kupoteza imani.

Badala ya kuketi mabarazani kusengenyana na kufitiniana, tunahimizwa kuingia misikitini na kuendesha ibada mbali mbali na tukisome kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa wingi yaani Qur'ani. Kwani pasi na kufanya hivyo, tutakuwa tunaupoteza wakati wetu ambao ni wa thamani sana kama ilivyopokelewa katika kauli za wahenga wa kiarabu kwamba: 'Wakati ni kama upanga, usipouvunja, (mwishowe) utakukata.'

KWA AKINA DADA

Dada wapendwa wa Kiislamu, mwezi mtukufu wa Ramadhani hutujia mara moja tu kwa mwaka. Tunapokaribia kuumaliza mwezi wa Sha’bani, huwa na furaha tele nyoyoni mwetu ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhani. Na kwa wakati huu hatunalo ila kumshukuru Mumba wetu aliyetuongoza kwenye njia yake nyofu (ya Kusilimu), maana lau si Yeye, kamwe hatungeongoka.

Dada wapendwa, tunapaswa kukumbuka kwamba, kufunga siyo kutozingatia kula na kunywa tu na hatimaye kutayarisha futari, bali kufunga kunakotakikana ni kuzingatia maamrisho yake Sub'haanuhu Wata’ala na Mtumewe(s.a.w. w ).

Miongoni mwa maamrisho yake kwetu ni kuwatii waume zetu kwani Mwenyezi Mungu hako tayari kuzipokea Saumu zetu tukiwa na ufidhuli kwa waume zetu kwani Mola wetu Anatuambia katika Qur'ani:"Waume ndio wasimamizi wa wanawake."

Naye Mtume(s.a.w. w ) anasema kutufunza namna ya kutunza nyumba zetu kwamba"Mwanamke akifunga Saumu yake ya wajibu, asali sala zake fardhi na amtii mumewe, bila shaka ataingia peponi."

Huo ndio wajibu wetu. Ama mtindo wa kuwasengenya wenzetu, majirani zetu, waume zetu, au waume wa wenzetu ni kinyume cha dini ya Islam, na wakati wowote ule haitakikani kuendesha mikutano ya namna hii, na hasa katika Ramadhani, maana yanaweza kukuharibia Saumu yako.

Pia kujifahiri kubughudhiana, kukaripiana, kunyimana vifaa vya nyumbani kama shoka, chumvi, mwiko n.k. na kujiunga katika makundi ya karata hasa na waume ni dhambi isiyosameheka ila kwa kutubia hasa wakati kama huu wa Ramadhani.

JICHAGULIE MWENYEWE

Sote tukiwa Waislamu halisi na walio na gheri juu ya dini yetu tunapaswa kujihifadhi na kuutambua umuhimu wa uwajibu wetu. Katika Saumu hii ambayo huendelea nayo kila mwaka, tunapaswa kutambua kwamba wafungao wako makundi tofauti kadha wa kadha.

1. Wako watu ambao wao ni vijana wa Kiislamu, lakini kwa bahati mbaya wao hawajali na wala hawafungi kamwe wakidai eti kufunga kulianzishwa na Masheikh waliokuwa hawana chakula, na kwamba mtu aliye na chakula kufunga ni kama upumbavu.

2. Wapo watu wafungao lakini wao hufungana kujizuia chakula tu na kutotangamana na wake michana ya Ramadhani, ama katika mambo mengine wao huwa hawajali; kama kusengenya, kusema uongo, na kadhalika, huku wakiwa wamejisahaulisha kuwa hayo ni miongoni mwa yafuturishayo.

3. Kundi jengine hufunga na kufanya baadhi ya yatakikanayo, lakini huwa wao ni wenye kukereka na Saumu, na huwa wao ni wenye kuomba na kutaka Saumu imalizike haraka.

4. Kundi hili hufunga tena kwa unyenyekevu na hushinda misikitini, lakini ufikapo usiku ama Ramadhani imalizikapo, huanza vioja na kuanza upya kuyarejelea yaliyokuwa marufuku nyakati za Ramadhani, basi watu wa namna hii, ni sawa na mtu aliyeweka akiba ya Sh. 5000/- asubuhi, ili zimfae baadaye atakapopatwa na dhiki ya ghafla, na ufikapo usiku huzitumia zote katika starehe zisizo za lazima na kutobakisha kitu.

5. Wa mwisho, ni wale wafungao kwa Imani kamili na baada ya Ramadhani kumalizika wanaendelea na majonzi ya kusikitika kwani hawajui kama watajaaliwa tena kuifikia Ramadhani nyengine. Kundi hili ndilo la wafungao kikweli wajulikanao kama "Mo’ominoon" - yaani waumini halisi.

Ndugu mpendwa, unatakiwa kujikagua ili ujuwe kundi ulimo hivi sasa, la sivyo, kiri kutojitambua wewe mwenyewe.

Tunawatakieni nyinyi na sisi mwisho mwema ili tufungapo, tuimalize Saumu kwa baraka na amani ili iishapo tuwe kuendelea na utu wetu.

'SAUMU' KATIKA BIBLIA

Saumu kama ilivyopokewa katika Qur'ani kadhalika imepokewa katika vitabu vya dini mbali mbali.

Kulingana na ushahidi wa Aya tuliyoitaja huko nyuma inayosema "Enyi mlioamini, mmefaradhiwa kufunga kama walivyofaradhiwa wa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu! Ulazima wa Saumu kwa watu wote wa leo na wa kale umethibiti”

Ingawa katika Aya hiyo Mwenyezi Mungu atujulisha kama, jee Saumu tuliyofaradhiwa sisi ndiyo ile ile na kwa namna ile ile na kwa idadi zile zile walizofaradhiwa wa kabla yetu ama kwa namna iliyo tofauti? Hata hivyo si lazima juu yetu kujua.

Na Mwenyezi Mungu alitujulisha hili ili tusiwe na malalamiko (kama ilivyo ada ya mwanadamu) kuwa, kwa nini sisi tulazimishwe Saumu na hali wa kabla yetu hawakufunga na hali wao ni waja kama sisi? Ndiyo maana Akatujulisha mapema kabla ya nyudhuru zetu kutolewa. Ingawa ndugu zetu Wakristo wanatambua wazi Fardhi hii, kwa bahati mbaya wao hawakuijali bali wameyashughulikia mengine.

Hebu na tuangalie katika kitabu chao (Biblia - Agano jipya).

Katika Mathayo 6, kifungu cha 16 hadi 18 kumeandikwa hivi: "Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana, maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo jipake mafuta kichwani, unawe uso, ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini na Baba yako aonaye sirini atakujazi."

Pia katika Mathayo 4, kifungu cha 1-2 imeandikwa hivi: "Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Iblisi. Akafunga siku Arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa."

Ndugu mpendwa, jee pana udhuru wowote tena wa kutofunga kwa Wakristo baada ya ushahidi huu? Jee inafaa kutumia mbinu zozote zile za ulaghai ili kuupuza maamrisho ya Allah? Jee inasihi mtu kutangatanga mabarabarani akinadi kwa kila namna ya vishindo eti "Mimi nimeokoka.....Mimi nimeokoka..." Na hali anaihepa Saumu? Hasha Wakalla.......hilo haliwi.