HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU 0%

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU Mwandishi:
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi: Tarehe

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi: Jopo La Waandishi Wa Vitabu Vya Kiada
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi:

Matembeleo: 8631
Pakua: 2657

Maelezo zaidi:

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 8631 / Pakua: 2657
Kiwango Kiwango Kiwango
 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi:
Swahili

HISTORIA NA SIRA YA VIONGOZI WAONGOFU

MTUNZI: JOPO LA WAANDISHI WA VITABU VYA KIADA

MTARJUMI: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI

Utangulizi

Hamna shaka kuwa historia ya mwanadamu ndio chemchemu na chanzo cha maarifa, chanzo ambacho mataifa yanakihitaji katika safari yake yenye kuendelea. Na ndio chanzo pekee chenye uwezo wa kuhuisha na kulisukuma taifa mbele na kulipa sifa na hadhi maalum huku kikilifunganisha taifa hilo na mizizi yake ya ustaarabu ambayo hulizuwia taifa dhidi ya mmong'onyoko.

Qur'ani imemhimiza kila mwanadamu ikamtaka azame ndani ya his- toria ya mwanadamu na azingatie yaliyomo ili awaidhike na kuongoka, hivyo Mwenyezi Mungu akasema:

"Je, hawatembei katika ardhi ili wapate nyoyo za kufahamia au masikio ya kusikilizia? "[1]

Baada ya Mwenyezi Mungu kutoa historia ya Adi, Thamudi, Firauni, watu wa miji iliyopinduliwa na watu wa Nuh akasema:

"Ili tuifanye ukumbusho kwenu na sikio lisikialo lisikie ."[2]

Historia ya ujumbe mbalimbali wa Mwenyezi Mungu imejaa masomo na mazingatio, masomo ambayo yameonyesha jinsi manabii watukufu walivyojali mataifa yao ili kuyaokoa toka kwenye matatizo mbalimbali.

Pia ujumbe huo umeonyesha lengo na mwelekeo wake wenye kujaa nuru na manufaa. Kwa ajili hiyo sera ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w ) na kizazi chake huwa ni tafsiri ya kivitendo ya misingi na sheria za kiislamu.

Hivyo kusoma sera yao na historia ya maisha yao ni chanzo muhimu cha kuifahamu Qur'ani na Sunna, na ni chemchemu ya maarifa ya wanadamu wote, kwa sababu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu alioutuma kwa wanadamu huku Nabii wa mwisho na mawasii wake wateule wakiwa ni viongozi wa wanadamu wote bila kubagua.

Tumeona ni vizuri tuweke silabasi kwa ajili ya kusoma historia ya kiislamu kwa kufuata hatua moja baada ya nyingine, kwani masomo ya historia ya nukuu hutangulia kabla ya masomo ya uchambuzi.

Na kwa kuwa umma wote umekongamana juu ya wema na utakaso wa viongozi wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu basi inafaa tuingize historia ya maisha yao ndani ya maisha ya wanafunzi, kwani Qur’ani imetamka wazi kuhusu umaasumu na utakaso wao ili wawe ni kiigizo chema kwa yule anayetarajia fadhila za Mwenyezi Mungu na malipo mema ya Siku ya Kiyama.

LENGO LA SILABASI YA KITABU HIKI

Kitabu “Masomo ya utangulizi katika historia na sera ya viongozi wema” kimetungwa ili kiwe hatua ya mwanzo ya kuelekea kwenye masomo mbalimbali ya lengo la kina zaidi, huku kikitegemea kufikia lengo hilo kwa kutumia wepesi wa ibara, usalama wa nukuu na vyanzo vyenye kukubalika ili kitoe picha ya wazi isiyokuwa na utata, shaka au hisia ambazo huenda zikamchanganya msomaji wa sera na historia mwanzoni tu mwa safari yake hii.

Masomo haya sitini yataanza kuzungumzia historia na sera kwa mtazamo wa Qur’ani, kisha yatatoa maisha binafsi na ya kijamii ya kila mmoja kati ya maasumina kumi na wanne(a.s ) , na mwisho yataishia kwenye uwanja kati ya viwanja vya urithi wao wenye kunukia manukato.

Mwisho kabisa tutatoa faida ya maisha yao ya ujumbe huku tukionyesha mavuno ambayo yamepatikana ndani ya karne tatu bali ni zaidi ya karne kumi na nne za mapambano yenye kuendelea kwa ajili ya kuuokoa umma wa kiislamu na jamii ya wanadamu toka kwenye yale yaliyowapata na waliyonasa ndani yake.

Na ili yawe maandalizi mema yenye kuunea na mapinduzi ya kiulimwengu ambayo yanamsubiri kiongozi wake wa kiroho, Imam angojewaye Al-Mahdi(a.s ) ambaye Mwenyezi Mungu aliwaahidi watu wa mataifa yote, ili aje kuunganisha nguvu na kuzifanya vizuri hali zao huku akiwaokoa wanadamu toka kwenye upotevu na kutimiza matarajio ya manabii na akitimiza wema wa ubinadamu, wema ambao bado binadamu anaendelea kuutolea juhudi zake usiku na mchana.

Hivyo mafunzo ya historia yamegawanywa katika sera binafsi na sera ya kijamii, huku yakiwa hayana uchambuzi wa matukio ya kihistoria wala kuzama sana ndani ya matukio makuu ya kihistoria, hiyo ni ili baadaye yafuatiwe na masomo mapana zaidi kuliko mafunzo haya.

Pia tumejiepusha na urudiaji huku tukikomea kwenye historia ya ujumbe wenyewe na yale yaliyopita katika mzunguko na vipindi vya ujumbe na kwenye matokeo yaliyopatikana ndani ya karne zilizopita ambazo ziliupitia Uislamu na waislamu.

Mada hizi zimetimia kwa kufuata uchambuzi wa kielimu dhidi ya matukio yaliyosajiliwa ndani ya vitabu vya historia au yaliyogunduliwa na watafiti. Katika hali zote mbili tumejaribu kutegemea juhudi za wale waliotutangulia, ambazo ni masomo ya waandishi na watafiti ili kupata matunda ya juhudi zao na kuunganisha kati ya watu wa zamani na kizazi cha sasa.

Pia ili tuwafunze vijana dharura ya kupitia rejea za kutegemewa za zamani na za sasa bila kudhulumu haki za waliyotangulia bali ili zionekane juhudi zao na jinsi walivyochangia katika uwanja wa elimu na maarifa ya jamii, na ili kuijua nafasi waliyonayo katika kunukuu urithi na kuvipelekea vizazi vyenye kufuata.

Waandishi wa zama hizi tutakaowataja ni Sheikh Baqir Sharifu Al- Qarashiy, Sayyid Murtaza Al-Askariy, marehemu Sheikh Asad Haydar, mashahidi wawili: Sayyid Muhammad Baqir As-Sadri na Sayyid Muhamad Baqir Al-Hakim. Kisha Sayyid Jafar Murtaza Al- Amiliy, Sheikh Muhammad Had Al-Yusufiy Al-Gharawiy na wengine ambao tumegusia vitabu vyao mwishoni mwa kila mada ambayo tumenukuu toka kwao.

Ni wajibu wetu kusema: Kitabu hiki ni mjumuisho wa mada mbalim- bali na utunzi unaolenga mafunzo ambayo yamezagaa ndani ya vitabu maalumu vilivyoteuliwa kufundisha sera ya kizazi cha Mtume (s.a.w.w.) ili iwe ni mali kwa mtafiti, mwanafunzi, mhutubu, mubali- hghiina, mlezi na mlelewa ili ajiandae na masomo ya juu zaidi katika historia ya Uislamu kwa ajili ya kupambana mapambano ya kielimu dhidi ya matukio ya kihistoria na kijamii, na ili tuzame ndani huku tukipata mafunzo toka humo ili yawe ni mazingatio kwa msomaji na mawaidha kwa mwenye mazingatio, insha’allah.

Kutokana na maelezo yaliyopita, kwa muhtasari tunatoa matokeo yafuatayo:

Kwanza : Katika hatua hii mwalimu anapofundisha historia asitege- mee kukutana na mafunzo ya kihistoria yenye mtiririko wa kuungana na kufuatana kwa maana iliyozoeleka. Kwa kuanzia jografia na histo- ria ya Bara la Uarabu, kisha utume wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w ) na dola yake, kisha dola ya makhalifa ambao walitawala kwa utaratibu maalumu. Hiyo ni kwa sababu sisi hatukusudii isipokuwa kusoma sera ya viongozi wema maasumina ambao ni lazima kuwaiga ili mwanafunzi afuate nyayo zao, awafuate na kuongoka kwa uongozi wao na sera yao katika maisha yake binafsi na ya kijamii.

Pili : Mwanafunzi anaweza kupata mafunzo muhimu ya kihistoria kupitia njia ya kutoa hatua za maisha ya kila mmoja kati ya maasumina kumi na wanne kwa kiwango kinachonasibiana na hatua ya mwanzo ya utangulizi ambayo imeishia kugusia nafasi na sehemu ya kizazi cha Mtume katika historia na harakati za Uislamu, kwa kuanzia nafasi yao maalumu ya kipekee aliyowapa Mwenyezi Mungu na kumalizia hali halisi ya kihistoria ambayo imetoa harakati zao na mwenendo wao muda wa karne tatu na zaidi.

Tatu : Kwanza hakika mafunzo ya historia ya Bara la Uarabu hayaingii yote katika historia ya Uislamu isipokuwa huwa kama utan- gulizi tu. Pili hutumiwa katika sehemu ya uchambuzi, jambo ambalo hatulikusudii katika hatua hii ya masomo haya. Zaidi ya hapo ni kuwa maelezo ya kizazi cha Mtume(s.a.w.w ) kama vile kauli za Imam Ali(a.s ) toka kwa Mtume(s.a.w.w ) na maelezo ya Zahra(a.s ) ndani ya hotuba yake mashuhuri aliyoitoa baada ya kifo cha Mtume(s.a.w.w ) yameelezea vizuri hali ya waarabu kabla ya Uislamu. Na pia imeunganisha kati ya yaliyopita na yaliyopo ambayo aliyatimiza Mtume(s.a.w.w ) , na majukumu makubwa yaliyofuatia yaliyopo juu ya wais- lamu ambao walitolewa na Uislamu toka kwenye shimo la ujinga mpaka kwenye nuru ya mwanga wa Uislamu.

Nne : Hakika anayemaliza kusoma kitabu hiki inampasa azalishe mafunzo ambayo yatampa njia ya kufikia malengo yanayokusudiwa katika kusoma historia ndani ya hatua zote mbili, na wala asitosheke na haya yaliyopo kwenye masomo ya hatua ya utangulizi.

Hatutaki kurudia mafunzo mara juu juu au mara nyingine kwa upana na undani zaidi, kwa ajili hiyo tunategemea waheshimiwa walimu wetu watazingatia malengo ya masomo kabla ya kuhoji silabasi ya kitabu. Na watatilia maanani silabasi ya kitabu kabla ya kuzama ndani ya vipengele vidogo vidogo vya historia ambavyo tumeviteua kwa ajili ya hatua hii. Pia watazingatia kikomo cha wakati na dharura ya kupangilia mafunzo kulingana na ubora ambao ni lazima kuzingatiwa katika silabasi ya mafunzo. Na kwa kuwa hiki si kitabu cha ziada bali kimeandaliwa kama kitabu cha kiada basi walimu watafundisha kulingana na silabasi ya mafunzo iliyopangwa.

Hatuna budi kusema kuwa kitabu hiki kilichapishwa mwanzo kwa jina la: ‘Dondoo za sera za viongozi wema’. Lakini baada ya kupi- tia upya mafunzo ya kitabu, kilibadilishwa jina na kuitwa:

‘Masomo ya utangulizi katika historia na sera ya viongozi wema’.

Mwisho tunatoa shukurani za dhati kwa ndugu zetu kamati ya elimu katika taasisi ya kimataifa inayosimamia vituo vya elimu na shule za kiislamu kwa msaada na juhudi walizozitoa.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu ampe uongofu na nguvu, hakika Yeye ndiye kiongozi bora na Mwenye kunusuru. Pia tunatoa shukuranu za dhati kwa mwandishi wa kitabu hiki Ustadh Sayyid Mundhir Al-Hakim (heshima yake idumu).

Jopo la kamati ya waandishi wa vitabu vya kiada.

1425 A.H.

SOMO LA KWANZA

HATUA YA MWANZO KUELEKEA KWENYE MASOMO YA SERA NA HISTORIA YA UISLAMU

KWANZA: SERA NA LENGO LA KUISOMA

1- Sera Kiistilahi

Sera ya mwanadamu ni njia yake na mwenendo wake katika maisha, hivyo sera ya Mtume na kizazi chake ni njia na mwenendo wao katika maisha. Sera hii inaonekana katika kauli zao, matendo yao na misimamo yao dhidi ya matukio na mambo mbalimbali ambayo yalitokea katika zama zao na wakaishi nayo kipindi cha karne tatu na miongo minne.

Yaani tangu uanze utume wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w ) mpaka mwisho wa ghaiba ndogo ya Imam wa kumi na mbili Muhammad bin Hasan Al-Askariy, Al-Mahdi hoja mwenye kungojewa.

2- Jinsi Qur’ani Ilivyotilia Umuhimu Sera

Hakika Qur’ani imetilia umuhimu sera kwa kubainisha sera ya man- abii na watu wema. Ikataka tufuate sera yao na kujifunza kupitia sera ya wale waliopita huku tukiwaidhika na sera yao. Pia imetuhimiza kujali sera ya hitimisho la manabii na bwana wa mitume, Muhammad bin Abdullah(s.a.w.w ) ikataka tumuige[3] baada ya kumwambia: “Na kwa hakika wewe unaongoza kwenye njia iliyonyooka.”[4]

Kisha akawaamrisha waislamu wote kukazania yote yanayotoka kwa yule asiyetamka la matamanio yake akasema: “Na anachokupeni Mtume basi kipokeeni, na anachokukatazeni basi jiepusheni .”[5]

Kisha akatuelekeza kwa kizazi cha Mtume, ambao Mwenyezi Mungu kawaondolea uchafu na kuwatakasa kabisa[6] . Akahimiza kushikamana na wakweli na kufuata mwenendo wao, hivyo Mwenyezi Mungu akasema: “Enyi mlioamini, mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wakweli .”[7]

3 - Lengo La Kusoma Sera

Hakika kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu na kizazi chake kitakasifu ni kufuata njia iliyonyooka inayofikisha kwenye wema na ushindi kwa sababu ni njia inayokuepusha na upotovu na ghadhabu za Mwenyezi Mungu. Na ndio njia ya manabii ambao Mwenyezi Mungu aliwaneemesha kwa neema ya uongofu wake unaowapeleka kwenye haki[8] . Ndiyo maana akaamrisha kuwafuata, Mwenyezi Mungu akasema: “Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata mwongozo wao .”[9]

Pia kwa ajili hiyo ndiyo maana sera ya yule hitimisho la manabii na sera ya mawasii wake watakasifu imekuwa ni chanzo kati ya vyanzo vya sheria ya kiislamu, na ni chemchemu ya maarifa na elimu ya kiis- lamu na ni sawa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu cha milele, kama ilivyoelezea kuhusu hilo Hadithi ya vizito viwili iliyo mutawatir[10] .

Zaidi ya hapo ni kuwa sera yao - Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote kwa ujumlaina faida kubwa katika kufahamu makusudio ya Kitabu kitakatifu na tafsiri ya Aya zake tukufu.

Pia sera yao hutubainishia jinsi ya kutekeleza mafunzo ya juu ya kiislamu katika maisha ya mwanadamu anayeishi katika maisha haya. Kwa hiyo tunafahamu kuwa kusoma sera yao kwa namna sahihi kutatupa silabasi muhimu katika malezi ya kiislamu na njia sahihi ya kujifunza mwenendo sahihi katika maisha.

PILI: MAHUSIANO KATI YA HISTORIA YA UISLAMU NA SERA

HISTORIA

Historia ni mkusanyiko wa matukio na uzoefu wa wanadamu waliopita ukilinganisha na zama tunazoishi hivi sasa.

HISTORIA YA UISLAMU

Hakika historia ya Uislamu ni historia ya dini ya milele ya kiislamu, tangu ulipodhihiri, kuenea kwake na harakati zake katika maisha. Pia inakusanya historia ya walioibeba dini na kuihami ambao walikesha wakihudumia na kulinda dini dhidi ya vitimbi vya maadui wake.

Hivyo hakika sera ya bwana wa mitume na sera ya kizazi chake kitakasifu ambacho kilipewa jukumu la kufikisha dini, kutekeleza na kuilinda, inakuwa ni sehemu isiyogawika ndani ya historia yenyewe ya Uislamu (yaani ndio historia yenyewe ya Uislamu).

Kwa sababu wao walizama ndani ya Uislamu na wakaihami sheria, wakatoa nafsi zao na maisha yao kwa ajili ya Uislamu. Hivyo misimamo yao ya kidini ndio Uislamu wenyewe na harakati zao ndio harakati za Uislamu wenyewe. Wao hudhihirisha kimatendo mafunzo halisi ya Uislamu na huyaelezea maelezo halisi. Hivyo historia yao ndio historia ya Uislamu katika hatua zake zote na mambo yake yote, wala siyo historia ya mtu fulani kati ya waislamu.

VYAVZO VYA HISTORIA YA UISLAMU NA SERA YA MTUME (S.A.W.W)

Hakika chanzo muhimu cha historia ya Uislamu na historia na sera ya manabii hasa historia na sera ya nabii wa mwisho(s.a.w.w) ni Kitabu cha milele cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani yake ya muujiza ambayo: “Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye hekima, Mwenye kuhimidiwa.”[11]

Ama vitabu vya sera, historia, tafsiri na Hadithi ambavyo viliandikwa baada ya kupita karne moja au zaidi tangu kufariki kwa Mtume(s.a.w.w) vyenyewe ni vyanzo vya daraja la pili.

Hakika vyanzo hivi vilivyokuja nyuma vimejumuisha ukweli huku pembeni yake vikiwa vimejaza visa vya uongo, Hadithi na habari za uzushi zilizowekwa kupitia ndimi za maswahaba au wanafunzi wa maswahaba.

Kwa ajili hiyo vyanzo hivi vinahitajia kipimo makini ili kupembua habari sahihi na kuzitenganisha na habari zilizochomekwa. Pia inatakiwa kuzipima na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna sahihi ya Mtume na akili salama ili ziwe ni mwongozo kwa watafuta ukweli.

ZAMA ZA HISTORIA YA UISLAMU

Historia ya Uislamu inaanzia pale alipopewa utume Mtukufu Mtume, tarehe ishirini na saba mfungo kumi (Rajabu) miaka kumi na tatu kabla ya hijra ya Mtume(s.a.w.w) , muda ambao maisha ya Uislamu wa kudumu yalianza na yakaendelea kuchanja mbuga ndani ya jamii ya kiarabu na mwanadamu chini ya mkono wa Mtukufu Mtume Muhammad bin Abdullah.

Uislamu ulikuwa ni mapinduzi ya Mwenyezi Mungu yenye mabadi- liko katika kila kitu, hivyo yalianzia Makka tukufu na kuishia kwenye kuasisi dola ya kiislamu iliyobarikiwa huko Madina na Bara la Arabu. Baada ya jihadi kubwa chini ya uongozi wa Mwenyezi Mungu Mwenye busara matunda yake yalionekana ndani ya muda mfupi, kinyume na historia nyingi za wito wa mabadiliko.

Zama hizi ambazo Mtume Muhammad(s.a.w.w) alianzisha mapinduzi haya yaliyobarikiwa tunaweza kuziita ni zama za Mtume Muhammad(s.a.w.w) , nazo ni zama za kufikisha Uislamu.

Ama zama zilizofuatia zenyewe ni zama za mawasii waliousiwa mapinduzi na dola ya Mtume. Hizi tunaweza kuziita zama za Maimam maasumina au zama za Maimam viongozi wema. Zama zote mbili zinagawanyika katika vipindi na nyakati mbili.

A) ZAMA ZA MTUME (S.A.W.W)

Zama za Nabii zina vipindi viwili tofauti navyo ni: Kipindi cha Makka na kipindi cha Madina. Kipindi cha kwanza kinaanzia pale ali- poruhusiwa kutangaza utume huko Makka na kinakomea pale alipohama toka Makka kuelekea Madina (Yathirib) katika usiku wa mwanzo wa mfunguo sita mwaka wa kumi na tatu tangu kupewa utume.

Kipindi cha pili kinaanzia pale alipofika Madina tarehe kumi na mbili ya mfungo sita ndani ya mwaka huo huo, na kinakomea pale alipofariki Mtume(s.a.w.w) tarehe ishirini na nane mfunguo tano mwaka wa kumi na moja tangu kuhamia Madina.

Katika kipindi cha Makka Mtume alitengeneza nguvu kali, alijenga Uislamu kiimani na kisheria kwa ajili ya maisha, hivyo ni kipindi cha kutengeneza umma wa kiislamu na kuanzisha kundi la waumini wenye kuamini Uislamu.

Ama kipindi cha Madina kinajitofautisha kwa kuasisiwa dola ya kiislamu, nayo ndiyo jengo la kwanza la kisiasa lenye sura ya dola ya kiislamu iliyojengeka katika kutekeleza sheria ya kiislamu ndani ya maisha. Katika vipindi vyote viwili wahyi wa Mwenyezi Mungu ndiyo uliokuwa ukimuelekeza yeye Mtume kama kiongozi wa umma wa kiislamu kupitia Aya za Qur’ani ambayo iliteremka ndani ya muda wa miaka ishirina na tatu.

Qur’ani imetuhifadhia matukio ya vipindi vyote viwili kupitia Aya zake. Hivyo tunaweza kuijua historia ya zama hizi iwapo tu tutajua kwa usahihi utaratibu wa kushuka Aya za Qur’ani tukufu. Hivyo tunaweza kugawa kipindi cha Makka katika vipindi viwili vifuatavyo:

Kipindi cha kuwalingania watu mahsusi na kuandaa mbegu za mwanzo za kundi la waumini. Muda wa kipindi hiki unakadiriwa ni miaka mitatu mpaka mitano.

Kipindi cha kuwalingania watu wote au kipindi cha kutangaza na kuanza mapambano dhidi ya shirki na ukafiri. Muda wa kipindi hiki unakadiriwa ni miaka mitatu mpaka minne.

Kipindi cha uhamishoni, nacho ni kipindi cha kuendeleza mkondo wa Uislamu. Kipindi hiki kimekusanya hijra tatu zenye kufuatana nazo ni: Kuhama kuelekea Uhabeshi (Ethiopia ya sasa), kisha kuelekea Taif na kisha kuelekea Madina.

Pia tunaweza kugawa kipindi cha Madina katika vipindi viwili tofauti navyo ni: Kipindi cha kuasisiwa dola ya kiislamu na kuihami ndani ya nusu ya kwanza ya kipindi cha Madina kuanzia hijra na kumalizikia vita vya Handaki au Ahzab.

Kipindi cha ufunguzi na kuendeleza mapinduzi ya kiislamu na kupan- ua wigo wa dola ya kiislamu. Hii ni kuanzia suluhu ya Hudaybiya mpaka mwaka wa Hijja ya mwisho ya kuaga, nayo ni nusu ya pili ya kipindi cha Madina.

B) ZAMA ZA MAIMAM WEMA

Hakika harakati za mageuzi ziliienea jamii ya kijahiliya hivyo kutokana na zilivyokuwa fikra, mafunzo, mila, na desturi za kijahiliya ni kuwa mapinduzi ya kiislamu na dola mpya ya Mtume(s.a.w.w) vilikuwa vinahitajia usia wa kiitikadi. Hiyo ni kwa sababu njia mbele ya harakati ilikuwa bado ndefu huku ikiendela kipindi chote cha vita nzito vya kiroho kati ya Uislamu na ujahiliya.

Kipindi kilichochukuliwa na mapinduzi, kisha dola ya Mtume hakikuwa kinatosha kung’oa mizizi yote ya ujahiliya na athari zake. Na hilo ni kama ilivyothibitisha historia ya matukio ambayo yalitokea baada tu ya kifo cha Mtume(s.a.w.w) .

Kwani baada ya Mtume(s.a.w.w) utawala wa kiislamu ulibakia ni mpira unaochezewa na watoto wa kizazi cha Umayya ambao kabla ya hapo walikuwa wamesimama kidete dhidi ya Uislamu kuanzia mwanzo mpaka sekunde ya mwisho[12] .

Kuanzia hapo Mtume kiongozi aliainisha Maimam kumi na wawili maasumina kwa amri toka kwa Mwenyezi Mungu. Ambao ni mawasii wenye uwezo watakaoshika nafasi yake ili kulinda mapinduzi yake, ujumbe wake, umma wake, na dola yake baada yake. Hivyo baada yake walisimamia jukumu la kutetea sheria ya Mwenyezi Mungu na dola ya bwana wa mitume na umma wa hitimisho la manabii.

Zama zao zimegawanyika katika vipindi viwili tofauti navyo ni: Kipindi cha kuonekana na kipindi cha ghaibu. Kipindi cha kuonekana kinaanzia pale alipofariki Mtume(s.a.w.w) na kinakomea mwaka 260 A.H. Pale alipofariki Imam wa kumi na moja kati yao naye ni Hasan Al-Askariy.

Ama kipindi cha ghaibu ni kipindi cha kutoonekana Imam wa kumi na mbili kati yao naye ni maasumu wa kumi na wane. Hujja bin Al- Hasan Al-Mahdi(a.s) mwenye kungojewa. Ambaye uimamu wake umefungana na ghaibu yake.

KIPINDI CHA GHAIBU NACHO KINA VIPINDI VIWILI:

Cha kwanza : Kipindi cha ghaibu fupi ambacho kilifikia muda wa miongo saba. Yaani kuanzia mwaka 260 mpaka 329 A.H.

Cha pili : Kipindi cha ghaibu ndefu ambacho kilifuata baada ya fupi ikiwa ni mwishoni mwa muongo wa tatu karne ya nne baada ya kufariki balozi wake wa nne mwaka 329 A.H. Nacho kinaendelea mpaka leo.

MUHTASARI

Sera ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na sera ya kizazi chake kitakasifu ni chanzo muhimu kati ya vyanzo vya maarifa na sheria ya kiislamu. Huzingatiwa pia kuwa ni nyenzo kati ya nyenzo za kufikia wema na mafanikio, kwa sababu kuwafuata wao ni mfano halisi wa kufuata njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka.

Historia ya kiislamu ndio historia ya Uislamu na ndio historia ya watetezi ambao walizama ndani na kujitoa muhanga kila dakika ya maisha yao katika njia ya Uislamu. Nao ni Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na kizazi chake kitakasifu kilichotakasika dhidi ya kila aina ya uchafu na kila aina ya dosari.

Qur’ani ndio chanzo muhimu cha historia na sera ya Mtume(s.a.w.w) na historia ya kiislamu. Kwa ajili hiyo vyanzo vyote vingine vya sera na historia vinapimwa kwa Qur’ani, kwa sababu vyanzo vingine vimekosa sifa ya “kumdiriki Mtume(s.a.w.w) ”, “kudiriki yote, umakini, na kutoegemea” kwenye maslahi ya makundi na madhehebu ambayo yalizuka baada ya zama za Mtume(s.a.w.w) .

Zama za Mtume wa mwisho(s.a.w.w) huchukuliwa kama mwanzo wa zama za historia ya kiislamu kisha hufuatiwa na zama za Maimam wema(a.s) .

SOMO LA PILI: MUHAMMAD BIN ABDULLAH (S.A.W.W) NI UTABIRI WA MANABII (A.S)

MWENENDO WA UTABIRI

Ni mwenendo wa Mwenyezi Mungu na ni rehema na amani kutoka Kwake kuwapa habari waja Wake za kuja kwa Mtume atakayemtuma kwao muda ujao. Hivyo manabii waliotangulia walikuwa wakim- bashiri Nabii atakayekuja baada yao.

Qur’ani imeashiria jinsi Yahya alivyobashiri unabii wa Isa (Al Imran: 39). Pia imeashiria jinsi Isa alivyobashiri unabii wa Muhammad (As-Swaf: 6). Hivyo manabii wote msitari wao ni mmoja kwani aliyetangulia humbashiri atakayemfuata, na huyu aliyefuata humwamini aliyetangulia. Mwenendo huu wa kubashiri umetamkwa na Qur’ani katika Sura ya tatu Aya ya themanini na moja. Zaidi ya hapo ni ushahidi na mifano halisi utakayoiona hapa mbele:

1. Qur’ani imeelezea utabiri wa Ibrahim kipenzi juu ya utume wa Nabii wa mwisho kwa ulimi wa dua akisema:

رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ { 129 }.

“Ewe Mola wetu, wapelekee mtume katika wao awasomee Aya zako na kuwafunza kitabu na hekima na kuwatakasa. Hakika wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.” (Al-Baqarah: 129).

Qur’ani imeeleza wazi kuwa utabiri wa Nabii Muhammad ulikuwemo ndani ya vitabu viwili: Taurati na Injili, na laiti kama utabiri huo usingekuwemo ndani ya vitabu hivyo basi watu wa vitabu hivyo wangeupinga waziwazi, Mwenyezi Mungu anasema:

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِنْدَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ يَأْمُرُهُمْ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنْكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ {157}.

“Ambao wanamfuata mtume, nabii aliyeko Makka ambaye wanamuona ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya, na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia maovu, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.” (Al-A’araf: 157).

Aya ya sita ya Surat Swaffu imeelezea waziwazi kuwa Isa(a.s ) alisadikisha Taurati na akambashiri Mtume atakayekuja baada yake jina lake Ahmad. Kama inavyoashiria kauli ya Mwenyezi Mungu:

وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِنْ بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ فَلَمَّا جَاءَهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ قَالُوا هَٰذَا سِحْرٌ مُبِينٌ {6}.

“Na aliposema Isa bin Mariam: Enyi wana wa Israeli, hakika mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu. Nimethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ni mwenye kutoa habari njema ya mtume atakayekuja baada yangu, jina lake ni Ahmad, lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhahiri” (As-Swaff: 6).

AHLUL-KITAB WAMNGOJEA NABII WA MWISHO

Manabii waliyotangulia hawakuishia tu kutoa sifa kuu za nabii aliyetabiriwa, bali zaidi ya hapo walitaja baadhi ya alama ambazo wale wanaopewa utabiri wanaweza kumjua vizuri.

Alama hizo ni kama vile sehemu atakayozaliwa, atakayohamia na sifa mahsusi za wakati atakaopewa utume. Pia alama za kipekee alizonazo mwilini, tabia na sheria zake za kipekee. Bali Qur’ani imeeleza kuwa walikuwa wanamjua kama wanavyowajua watoto zao (Al-An’am: 20).

Kutokana na utabiri huo wakafuatilia kivitendo na mwisho wakagun- dua sehemu atakayohamia na kusimamisha dola yake. Hapo wakafanya makazi yao na kuanza kuiombea nusra dini yake dhidi ya makafiri (Al-Baqarah: 89), na kuomba ushindi kupitia Mtume wa Mwenyezi Mungu dhidi ya Ausi na Khazraji.

Hivyo habari hizi zikaenea kwa wengine kupitia mapadri na wasomi wao, zikazagaa Madina zikafika hadi Makka. Wakampa habari Abdul Muttalib[13] na Abu Talib[14] huku wakiwahadharisha na vitimbi vya mayahudi.

Hivyo baada ya Mtume kutangaza utume wake, ujumbe wa makuraishi ulikwenda kwa mayahudi wa Madina kwa lengo la kuthibitisha ukweli wa madai ya unabii waliousikia toka kwa Muhammad, wakachukua baadhi ya mambo waliyomtahini nayo Mtume,[15] na hatimaye ukabainika ukweli wa madai yake.

Baadhi ya Ahlul-Kitabi na wengineo walimwamini Nabii Muhammad kwa kufuata alama hizi ambazo walizifahamu hata bila ya kumuom- ba muujiza wowote mahsusi (Al-Maidah: 83). Mpaka leo baadhi ya nakala za Taurati na Injili zimehifadhi baadhi ya utabiri huo.[16]

Na hivyo ndivyo ulivyofuatana utabiri wa unabii wa nabii wa mwisho Muhammad kabla ya kuzaliwa kwake. Kisha ukanukuliwa wakati wa uhai wake kabla ya kukabidhiwa unabii. Ulienea utabiri aliouelezea padri Buhayra kisha ushahidi wa Waraqa bin Nawfal juu ya utume wa Muhammad, ushahidi uliotokana na utabiri.[17]

Imam Ali(a.s ) ameelezea hali hiyo kwa kusema: “Mwenyezi Mungu hajawaacha viumbe wake bila ya nabii aliyetumwa au kitabu kilichoteremshwa, au hoja ya lazima, au njia ya wazi iliyonyooka. Mitume ambao uchache wa idadi yao au wingi wa wapingaji havikumzuwia aliyetangulia kumtaja atakayekuja baada yake, au aliyepita kutambulishwa na aliye kabla yake. Kwa mwenendo huo karne zikapita…Mpaka Mwenyezi Mungu alipomleta Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu ili kutekeleza utaratibu Wake na kutimiza unabii wake, huku ahadi yake ikiwa imechukuliwa kwa manabii waliyotangulia na alama zake zikiwa ni mashuhuri……..[18]

SIFA ZA NABII MUHAMMAD (S.A.W.W)

Ibnu Saad amepokea toka kwa Sahlu mtumwa wa Utayba ambaye alikuwa mkiristo wa Mar’yasi na alikuwa ni yatima aliyelelewa na mama yake mzazi na ami yake, pia alikuwa msomaji wa Injili, alisema kuwa: “Nikachukua kitabu cha ami yangu nikawa nakisoma mpaka iliponipita karatasi, hivyo nikataka kujua ni kipi kilichoandikwa katika karatasi iliyonipita. Nikaigusa kwa mkono wangu na pindi nilipoangalia nikakuta vitini vya karatasi vimeshikana hapo nikaviachanisha nikakuta ndani yake sifa za Muhammad:

Yeye si mfupi, si mrefu, mweupe, kati ya mabega yake kuna muhuri, mara nyingi hukaa mkao wa ihtibau, hapokei sadaka, anapanda punda na ngamia, anakamua mbuzi, anavaa kanzu chakavu, na atakayefanya hivyo basi kajiepusha na kiburi na yeye hufanya hivyo, na yeye anatokana na kizazi cha Ismail na jina lake ni Ahmad .”

Sahlu akasema: “Nilipofika hapa katika kumtaja Muhammad ami yangu akaja na alipoiona karatasi alinipiga na kusema: “Kwa nini umefungua karatasi hii na kusoma?” Nikasema: Humu mna sifa za nabii Ahmad. Akasema: “Yeye bado hajakuja.”[19]

MUHTASARI

Matukio ya kihistoria yanaonyesha kuwa mwenendo wa manabii ni wa kiukamilifu wenye lengo moja na njia moja. Pia mwenendo wa Mwenyezi Mungu ni manabii waliyopo kuwabashiri watakaochukua nafasi zao katika unabii. Ikiwa ni huruma toka kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya mzigo walio nao wanadamu katika kuamini na kukubali na ni kumrahisishia nabii anayefuata kazi ya uhubiri na ulinganio.

Na kwa kuwa Uislamu na Mtume Muhammad vina umuhimu mkub- wa katika historia ya binadamu, na ukizingatia kuwa Uislamu ni dini inayohusu kila kitu na ndiyo dini ya mwisho huku Mtume(s.a.w.w ) akiwa ndiyo mtume wa mwisho, basi Uislamu huo ulibashiriwa tangu zamani na hilo limeelezwa na Qur’ani tukufu.

Kuna habari zilizoenea kabla ya Mtume kukabidhiwa utume ambazo zilikuwa zimebeba wasifu kamili wa Mtume Muhammadin(s.a.w.w ) na mazingira yake, zikiwataka watu wamwamini na wajiepushe na upotovu kwa kumfuata yeye.

Habari hizi zilisaidia baadhi ya Ahlul-Kitabu na wengineo kuamini dini ya Mtume Muhammad(s.a.w.w ) bila ya kuomba muujiza wowote mahsusi.

SOMO LA TATU: MAZINGIRA SAFI

Mazingira yana mchango mkubwa katika malezi ya mwanadamu, humfanya awe mwema au humharibu. Mazingira tunayokusudia hapa ni wale watu wanaomzunguka mwanadamu ambao mwanadamu huyu hupokea kutoka kwao misingi ya maarifa yake na lugha yake. Wanadamu ambao kupitia kwao hujifunza elimu na maarifa mbalimbali na huongoka kupitia kwao, kwani huathirika kulingana na wanadamu wanaomzunguka, hivyo yeye huwaathiri na wao humwathiri.

Familia ndio mazingira ya mwanzo ambayo wanadamu hukulia ndani yake wakiwemo manabii na walinganiaji wa tawhidi ambao walisi-mama kidete kupiga vita shirki, maadili machafu na mila potovu. Hakika Mwenyezi Mungu aliwaumba na kuwalea katika familia za tauhidi zenye kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu.

Baba wa manabii Adam(a.s ) ndiye aliyefundishwa majina yote na Mwenyezi Mungu kabla hajaletwa aridhini. Na yeye ndiye wa kwanza kumtakasa Mwenyezi Mungu na ndiye wa kwanza aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu katika tauhidi. Hivyo kwa mwenendo huo wakafuata manabii wote, manabii ambao wamehitimishwa na Muhammad(s.a.w.w ) .

MAZINGIRA YA MTUME (S.A.W.W) KWA MUJIBU WA MAELEZO YA AHLUL-BAYT

Imam Ali(a.s ) ameelezea mazingira ya tauhidi ambayo Mtume(s.a.w.w ) alitokana nayo akasema: “Akamteua kutokana na mti wa manabii, shubaka yenye mwanga, nywele za utosi wa watukufu na kitovu cha Makka”[20] “….Mahala pake alipoishi (Mfuko wa uzazi) ndiyo mahala bora, na chimbuko lake ndio chimbuko bora katika machimbuko ya madini ya utukufu na busati la amani .”[21]

“Hivyo akamleta toka ndani ya madini yenye chimbuko bora na asili tukufu, toka ndani ya mti ambao alikusudia kuwatoa ndani yake manabii na kuteua waaminifu wake kutoka humo.”[22]

“Kila Mwenyezi Mungu alipokiongeza kizazi kwa kugawa makundi mawili basi alikiweka kizazi chake katika kundi bora, kundi ambalo mzinifu hakuchangia chochote wala hakupata fungu lolote.”[23]

Pindi Qur’ani ilipotaja kuteuliwa kwa ajili ya ulimwengu wote Adam, Nuh, kizazi cha Ibrahim na kizazi cha Imran Mwenyezi Mungu aliendelea kwa kusema:

ذُرِّيَّةً بَعْضُهَا مِنْ بَعْضٍ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {34}.

“Kizazi cha wao kwa wao na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua” (Al Imrani: 34).

Akamtaja kipekee mtume wake wa mwisho kwa kusema:

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ. الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ {219}.

“Na umtegemee Mwenye nguvu, Mwenye rehema. Ambaye anakuona unaposimama. Na mageuko yako katika wale wanao- sujudu (Shu’araa: 217-219).”

Hivyo wote waliomtangulia Muhammad walikuwa wakisujudu na kunyenyekea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wala hawajamshirikisha na chochote hata sekunde moja.

Imam Jafar As-Swadiq(a.s ) amefafanua geuko hili kwa kusema: “Ndani ya mifupa ya migongo ya manabii kulikuwa na nabii baada ya nabii mpaka akamleta toka mifupa ya mgongo wa baba yake kutokana na ndoa na wala si kwa uzinzi, hali hii ni tokea kwa Adam .”[24]

Nabii mwenyewe(s.a.w.w ) kaelezea hali hiyo waziwazi kwa kusema: “Nilihamishwa toka ndani ya mifupa ya migongo mitakasifu mpaka kwenye kizazi kitakasifu katika hali ya ndoa wala si hali ya uzinzi .”[25]

Pia akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu alimteua Ibrahim toka kizazi cha Adam akamfanya kipenzi. Akamteua Isma’il toka kizazi cha Ibrahim. Kisha akamteua Nazari toka kizazi cha Isma’il. Kisha akamteua Mudhira toka kizazi cha Nazari. Kisha akamteua Kinana toka kizazi cha Mudhar. Kisha akamteua Qurayshi toka kizazi cha Kinana. Kisha akateua kizazi cha Hashim toka kizazi cha Qurayshi. Kisha akateua kizazi cha Abdul Muttalib toka kizazi cha Hashim. Kisha akaniteua mimi toka kizazi cha Abdul Muttalib.”[26]

MAZINGIRA YA MTUME (S.A.W.W) KWA MUJIBU WA MAELEZO YA WANAHISTORIA

Wanahistoria wameeleza wazi kuwa Abdul Muttalib alikataa kuabudu masanamu. Akampwekesha Mwenyezi Mungu, akatekeleza nadhiri. Akaanzisha mienendo ambayo mingi kati ya hiyo imetajwa na Qur’ani huku ikiridhiwa na Mtume(s.a.w.w ) kupitia sunna yake.

Kati ya mienendo hiyo ni kutimiza nadhiri, fidia ya ngamia mia moja, kutooa maharimu na kutoyaendea majumba kwa nyuma. Pia kukata mkono wa mwizi, kukataza kuwauwa watoto wa kike, maapizano, kuharamisha pombe, kuharamisha zinaa na kutoa adhabu kwa mzinifu. Kuteua kwa bahati, kukataza kutufu uchi, kumkirimu mgeni, kutokutoa kitu wanapohiji isipokuwa toka kwenye mali waipendayo na kutukuza miezi mitukufu.

Walipokuja watu wa tembo maquraishi waliikimbia Haram, Abdul Muttalib akawaambia: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu sitoki haramu natafuta ushindi kupitia njia nyingine.”

Maquraishi wakawa wakisema: “Abdul Muttalib ni Ibrahim wa pili. Al-Masuudiy amesema: “Abdul Muttalib alikuwa akiwausia wanawe kuunga undugu, kulisha chakula na akiwatamanisha na kuwahofisha kufanya na kuaacha kitendo cha mtu anayetaraji siku ya Kiyama na ufufuo.”[27]

Al-Shahrastaniy amesema: “Alikuwa akiwaamrisha wanawe waache dhuluma na ujeuri. Akiwahimiza juu ya maadili mema. Akiwakataza mambo duni. Katika usia wake alikuwa akisema: Hakika dhalimu hatotoka ndani ya dunia hii isipokuwa baada ya malipo ya kisasi na kufikiwa na adhabu.”

Hivyo alipofariki mtu mmoja dhalimu ambaye hakufikiwa na adhabu, watu wakaanza kumuuliza Abdul Muttalib kuhusu hilo. Akafikiri na kusema: Naapa kwa Mwenyezi Mungu hakika nyuma ya nyumba hii kuna nyumba nyingine ambayo ndani ya nyumba hiyo mwema hulipwa wema wake na muovu ataadhibiwa kwa uovu wake.”[28]

MTOTO WA VICHINJWA VIWILI

Imam Ali Ridha(a.s ) aliulizwa kuhusu maana ya kauli ya Mtume: “Mimi ni mtoto wa vichinjwa viwili .” Akajibu: “Hakika Abdul Muttalib alijining’iniza katika mlango wa Kaaba akamuomba Mwenyezi Mungu amruzuku watoto kumi. Akaweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu kuwa atamchinja mmoja kati ya hao iwapo tu Mwenyezi Mungu atajibu dua yake.

Hivyo walipofika watoto kumi akasema: Hakika Mwenyezi Mungu kanitekelezea ombi langu, basi ni lazima nitekeleze nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Akawaingiza wanawe Kaaba na kuanza mchakato kati yao, na hatimaye mchakato huo ukaangukia kwa Abdullah baba wa Mtume(s.a.w.w ) na ndiye aliyekuwa kipenzi chake sana.

Akarudia mara ya pili mchakato huo ukaangukia tena kwa Abdullah. Akarudia kwa mara ya tatu mchakato ukaangukia kwa Abdullah. Ndipo alipomchukua na kuazimia kumchinja. Wakakusanyika maquraishi na kumkataza asifanye hivyo.”[29]

Imam Al-Baqir(a.s ) amesema: “Mchakato ukaangukia kwa Abdullah. Akazidisha majina kumi lakini bado mchakato ukamwan- gukia Abdullah. Akaendelea kuzidisha majina kumi kumi mpaka yakafika mia moja ndipo mchakato ulipoangukia kwa ngamia. Hapo Abdul-Muttalib akasema: ‘Sikumtendea haki Mola wangu,’ hivyo akarudia mara tatu na mara zote ukaangukia kwa ngamia. Akasema: ‘Sasa nimejua kuwa Mola Wangu kaniridhia.’ Ndipo alipochinja ngamia .”[30]

AMINA BINTI WAHAB

Baada ya miaka kumi tangu kuchimbwa Zamzamu na baada ya mwaka mmoja12 tangu Abdullah kufidiwa kwa ngamia Abdul Muttalib alitoka na mwanae Abdullah na kuenda nae katika nyumba ya Wahab bin Abdul Manafi bin Zahrat (wakati huo alikuwa ndio bwana wa kizazi cha Zahrah kinasaba na kisharaf). Hapo akamposa binti wa Wahabi, Amina kwa ajili ya Abdullah.

Amina alikuwa ndiye mwanamke bora kinasaba na kimaadili kwa maquraishi, hivyo Abdul Muttalib akamuozesha na kummilikisha Abdullah, Amina. Ndani ya nyumba ya Abdul Muttalib ndimo Abdullah alimomuingilia Amina na kupata ujauzito wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) .[31]

Imam Ali(a.s ) amesema: “Amina binti Wahabi aliona usingizini kuwa anaambiwa: Hakika aliyomo tumboni mwako ni bwana, hivyo ukimzaa mwite Muhammad.” Kisha Ali(a.s ) akasema: “Hivyo Mwenyezi Mungu alimpa jina kutoka ndani ya jina lake, kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mahmudu na huyu ni Muhammad.”[32]

Hakika Abdullah alipata umashuhuri mkubwa akawa ni mtu muhimu kwa watu, akawa ndiyo mazungumzo yao na kipenzi chao. Baada ya tukio la kisa cha fidia yake, kisa ambacho kilifanana na kisa cha babu yake Isma’il…… Mwenyezi Mungu akamjalia kukutana na binti bora kati ya mabinti wa kiquraishi……lakini hakumjalia kuishi nae muda mrefu. Kwani utafutaji ulimpeleka Sham akiwa na maquraishi kwa ajili ya biashara.

Alielekea Gaza huku akiwa amemuacha mke wake mja mzito, na alipokuwa akirudi alielekea Madina kwa lengo la kuwazuru wajomba zake na kuzidisha undugu, lakini mipango ya Mwenyezi Mungu haikumpa muda, hivyo akaugua huko na rafiki zake kulazimika kumwacha na kurudi huku wakiwa wamebeba habari za ugonjwa wake na kufikisha kwa baba yake Abdul Muttalib.

Abdul Muttalib akamtuma Al-Harithi ambaye ni mwanae mkubwa ili akamuuguze ndugu yake mpaka apone kisha arudi nae Makka. Isipokuwa mipango ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ikimuharakisha Abdullah, hivyo Al-Harithi hakufika Madina isipokuwa baada ya siku nyingi tangu kufariki kwa ndugu yake.[33]

Hivyo akarudi kwa baba yake akiwa na moyo wa huzuni, mwenye kutetemeka huku akibeba habari za kifo cha mtoto kipenzi kati ya watoto wa baba yake. Hakika ni habari nzito kwa Abdul Muttalib lakini hazikuteteresha subira yake wala hazikudhoofisha uvumilivu wake.

MUHTASARI

Hakika Mwenyezi Mungu aliweka umuhimu maalumu kwa manabii wake, hivyo akawezesha wazaliwe toka ndani ya familia takasifu ili wawe na uwezo wa kuwasafisha watu dhidi ya shirki. Hivyo ndivyo alivyomteua nabii Muhammad(s.a. w.w ) . Hakika alihama toka mifupa ya migongo mitakasifu yenye imani na toka mapaja ya utawa mpaka dunia ilipopata sharafu kwa kuzaliwa kwake.

Familia ya Mtume Muhammad(s.a.w.w ) ilikuwa ni familia na damu yenye kuheshimika, kwani yeye ametokana na nabii Ibrahim(a.s ) . Pia ilikuwa ikijihusisha na kulinda Haram ya Makka na kuitetea dhidi ya maadui.

Babu wa Mtume Abdul Muttalib aliishi zama ambazo ujumbe wa Mwenyezi Mungu ulikuwa umetoweka huku nguvu za shirki zikiwa zimedhihiri na ufisadi na dhuluma vikishamiri, lakini pamoja na hayo yote alikuwa ni mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu huku akilingania maadili mema, na njia hiyo ndiyo waliyopita watoto wake.

Abdul Muttalib alimjali sana mwanae Abdullah, hivyo akamwozesha mwanamke bora toka familia na damu yenye heshima. Lakini matak- wa ya Mwenyezi Mungu yalitaka Abdullah afariki kabla ya kuzaliwa mwanae Muhammad(s.a.w.w ) .