HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU 0%

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU Mwandishi:
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi: Tarehe

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi: Jopo La Waandishi Wa Vitabu Vya Kiada
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi:

Matembeleo: 8721
Pakua: 2828

Maelezo zaidi:

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 8721 / Pakua: 2828
Kiwango Kiwango Kiwango
 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi:
Swahili

SOMO LA NNE: MAISHA YA NABII WA MWISHO

Hakika Mwenyezi Mungu alipenda asimamie malezi ya Muhammad(s.a.w.w ) amtoe mikononi mwa familia yake ili awe chini ya ulinzi wake ikiwa ni maandalizi ya kupata familia kubwa ambayo kiongozi wake atakuwa ni Muhammad.

Familia ambayo haitopendelea taifa wala lugha au rangi bali mbora wao ndani ya familia hiyo ni yule tu mwenye uchamungu. Hivyo Qur’ani imeelekeza maana hii kwa kusema: “Je hakukukuta ni yatima akakuhifadhi?” (Dhuha: 6). Mtume akaelezea kwa kusema: “Hakika Mola wangu alinilea akaboresha maadili yangu .”[34]

Hakika busara za Mwenyezi Mungu zilimnyima Muhammad(s.a.w.w ) mapenzi na huruma ya muda mfupi huku Mwenyezi Mungu akimpangia huruma na mapenzi ya muda mrefu usio na kikomo, kwani alimuhifadhi kwa babu yake kisha kwa ami yake, hivyo hao wawili wakawa wakimpendelea zaidi ya nafsi zao na zaidi ya watoto wao wa kuzaa.

Katika njia hiyo ya malezi wakatoa kila aina ya mapenzi na huruma kwa kiwango ambacho wazazi hawawezi kujitolea kwa watoto wao wa kuzaa.

Hilo ni miongoni mwa fadhila za Mwenyezi Mungu kwa Mtume(s.a.w.w ) bali hakika alimfanyia umuhimu maalumu pindi alipojitolea mwenyewe kumlinda na kumuhami kwa huruma yake, na hakika hakuna neema kubwa kama hii ambayo kaielezea Mwenyezi Mungu kwa kusema: “Na hakika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako ni kubwa .”[35]

KUZALIWA KWAKE: ZAMA, SEHEMU NA NAMNA

Alizaliwa(s.a.w.w) katika mji wa Makka ndani ya mwaka wa ndovu (tembo) mwezi wa mfungo sita.

Kwa Shia Imamiya ni mashuhuri kuwa alizaliwa alfajiri ya siku ya ijumaa ya terehe kumi na saba. Kwa wengine mashuhuri ni kuwa alizaliwa siku ya jumatatu terehe kumi na mbili wakati wa kuchomoza alfajiri au jua au wakati wa kukengeuka jua.

Lililo mashuhuri toka kwa Amina binti Wahabi kama alivyoelezea Ibnu Is’haqa ni kuwa: “Wakati Amina alipokuwa akielezea siku za mimba ya Mtume(s.a.w.w) alisema: Hakika Amina aliona nuru ikitoka mpaka akaona makasiri ya Basra kutokea ardhi ya Sham. Akaambiwa hakika wewe umembeba bwana wa umma huu, hivyo atakapotua aridhini sema: Namkinga kwa Mwenyezi Mungu mmoja dhidi ya shari ya kila hasidi, kisha mwite Muhammad.”[36]

Halima binti Dhuaybu As-Saadiyyah ameongeza kuwa: “Amina alisema: ‘Kisha naapa kwa Mwenyezi Mungu hakuna mimba niliyoona ni nyepesi kwangu na rahisi kama yake .”[37]

Al-Yaaqubiy amesema: “Alipozaliwa Muhammad(s.a.w.w) mashetani yalilaaniwa na nyota ziliporomoka, watu wakasema: Hakika hii ni alama ya Kiyama, watu wakapatwa na tetemeko la ardhi ambalo lilienea dunia nzima mpaka makanisa na mahekalu yakabomoka, na kikatoka sehemu yake kila kilichokuwa kikiabudiwa kinyume na Mwenyezi Mumgu.

Mambo ya kichawi yakaharibika na mashetani wao wakafungwa, kasri la Kisra likatetemeka hivyo yakaporomoka masharafu kumi na tatu na moto wa Farsi ukazimika.

Kabla ya hapo ulikuwa na muda wa miaka elfu bila kuzimika….Mtu kati ya Ahlul-kitabi alikwenda kwa maquraishi akiwemo Hisham bin Al-Mughirah, Al-Walid bin Al-Mughirah na Al-Utba bin Rabia akasema: “Usiku huu kazaliwa mtoto kwa ajili yenu[38] ……..ndani ya usiku huu kazaliwa nabii wa umma huu naye ni Ahmad wa mwisho……Kisha akatoa alama zinazomtambulisha.”[39]

KUNYONYA KWAKE

Maziwa ya mwanzo aliyonyonya baada ya maziwa ya mama yake mzazi yalikuwa ni ya Thuwaybah mjakazi wa Abu Lahabi bin Abdul Muttalib. Hiyo ilikuwa ni kabla hajanyonyeshwa na Halima binti Abu Dhuaybu As-Saadiyyah,[40] kwani watu wa Makka walikuwa wakiwanyonyesha watoto wao kwa wanawake wa vijijini kwa lengo la kutaka ufasaha.

Ushahidi juu ya hilo ni kauli yake mwenyewe(s.a.w.w) : “Mimi ndiye mfasaha kuliko wote wanaotamka kiarabu, zaidi ya hapo mimi ni mkurayshi na nimenyonyeshwa na watoto wa Saad .”

Alibakia(s.a.w.w) mikononi mwa Halima muda wa miaka miwili mpaka alipoacha kunyonya, ndipo Halima akamkabidhi kwa mama yake na kumpa habari za baraka zote alizoziona, hapo Amina akam- rudisha kwa Halima kisha baadae Halima akamrudisha kwa mama yake huku Mtume(s.a.w.w) akiwa na umri wa miaka mitano.[41]

MAJINA YAKE NA MAJINA YAKE YA HESHIMA

Muhammad bin Jubayri bin Mut’im amepokea toka kwa baba yake kuwa alimsikia Mtume(s.a.w.w) akisema: “Hakika mimi nina majina kadhaa: Mimi ni Muhammad, Ahmad na mfutaji, Mwenyezi Mungu atafuta ukafiri kupitia mimi. Na mimi ni mkusanyaji, Mwenyezi Mungu atakusanya watu chini ya nyayo zangu. Na mimi ndiye niliyefuata baadae hakuna mwingine yeyote baada yangu .”[42]

Jina lake la heshima lililo maarufu ni: Abu Qaasim. Imepokewa kutoka kwake kuwa alisema: “Jiiteni kwa jina langu lakini msijipe heshima kwa jina langu la heshima.”10 Pia inasemekana kuwa jina lake la heshima ndani ya Taurati ni: Baba wa wajane, na jina lake ni: Swahibul-Malhama.[43]

Al-Halbiy amesema: “Ni wazi kuwa majina yake yote yametokana na sifa za vitendo alivyotenda ambavyo vinalazimu sifa na ukamilifu, hivyo ndani ya kila sifa ana jina.”[44]

VIPINDI VYA MAISHA YAKE

Maisha ya Mtume(s.a.w.w) mwanzo yamegawanyika katika vipindi viwili tofauti:

Kipindi cha kwanza: Ni kuanzia alipozaliwa mpaka alipokabidhiwa unabii, nacho ni kipindi cha miaka arubaini.

Kipindi cha pili: Ni kuanzia alipokabidhiwa unabii mpaka alipofariki, nao ni muda wa miaka ishirini na tatu.

Katika vipindi vyote vya maisha yake, Muhammad bin Abdullah(s.a.w.w) alijulikana kwa maadili mema, kujitenga na vitendo vya shirki, kujitenga na unywaji pombe, kutokuhudhuria vikao vya upuuzi, kamari na zaidi ya hayo ambayo vijana wa zama hizo walikuwa wakivutiwa nayo. Kutokana na maadili yake mema alijulikana kwa jina la mwaminifu, hivyo maquraishi walipozozana kuhusu mtu atakayeweka jiwe jeusi waliangukia kwenye uamuzi wa Muhammad(s.a.w.w) huku wakikiri kuwa yeye ni mwaminifu asiyeyumba.

Wanahistoria wote wamekiri kuwa Muhammad(s.a.w.w) hakuwahi kuabudu sanamu na alikuwa akichukizwa na masanamu hayo. Alikuwa akihamia pango la Hira kila mwaka muda wa mwezi mzima……Pia alikuwa mbali na sifa za kijahiliya ambazo walikuwa nazo vijana wa kiarabu wa zama hizo. Bali alikuwa akikataza ibada ya masanamu pale anapopata fursa ya kufanya hivyo.

Kila kipindi kati ya vipindi vya maisha yake kimegawanyika sehemu nyingi, hivyo kipindi cha kwanza unaweza kukigawa sehemu tatu:

Sehemu ya kwanza: Ni kuanzia alipozaliwa mpaka aliposafiri safari yake ya kwanza ya Sham akiwa na ami yake Abu Talib. Kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.

Sehemu ya pili: Ni kuanzia pale aliporudi kutoka Sham mpaka alipomuoa Khadija. Kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano.

Sehemu ya tatu: Ni kuanzia alipooa mpaka alipokabidhiwa unabii akiwa na umri wa miaka arubaini.

Kipindi cha pili kimegawanyika zama mbili tofauti:

Zama za kwanza : Nazo ni zama za Makka ambazo zilichukua muda wa miaka kumi na tatu.

Zama za pili : Nazo ni zama za Madina[45] ambazo zilichukua muda wa miaka kumi.

MUHTSARI

Ni maarufu kuwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) alizaliwa yatima. Na mama yake Amina binti Wahabi aliona baadhi ya alama zilizojulisha kuwa mwanae atakuwa na jambo kubwa na cheo cha juu.

Hakukuwa na kalenda maarufu ya kuhifadhi kumbukumbu za matukio, hivyo historia ya kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) imehifadhiwa na tukio la kuhujumiwa kwa Kaaba, tukio ambalo hujulikana kwa jina la tukio la tembo. Qur’ani imeashiria tukio hili la kihistoria ndani ya Sura Al-Fiylu.

Ukoo wa Abdul Muttalib ulimjali sana Muhammad bin Abdullah(s.a.w.w) . Hilo lilidhihirika pale walipompeleka kunyonya kwa Bani Saad kwani baada ya maziwa ya mama yake walimpeleka kijijini ili akanyonye katika mazingira ya afya na ufasaha wa lugha.

Mtume ana majina mazuri, sifa nzuri na majina mazuri ya heshima. Maisha ya Mtume(s.a.w.w) yalichukua miaka sitini na tatu huku yakigawanyika vipindi viwili vikuu: Cha kwanza: Kuanzia alipozaliwa mpaka alipokabidhiwa unabii. Muda wake ni miaka arubaini. Cha pili: Kuanzia alipokabidhiwa unabii mpaka alipofariki. Muda wake ni miaka ishirini na tatu.

SOMO LA TANO: TABIA NA MWONEKANO WA HITIMISHO LA MANABII (S.A.W.W)

NDANI YA QUR’ANI TUKUFU

Hakika Muhammad bin Abdullah alisifika kwa sifa nzuri na maadili bora ambayo yalimtofautisha na kila aliyeishi katika zama zake au kabla yake au aliyekuja baada yake, hivyo ndio maana akawa ni mbora wa manabii. Hakika ukamilifu wake umeelezwa wazi na Qur’ani kupitia maelezo yake matukufu. Qur’ani imeelea ukamilifu wa akili yake na ubora wa maadili yake kwa kusema: “Kwa neema ya Mola wako wewe si mwenda wazimu.* Na kwa hakika una malipo yasiyokatika.*Na bila shaka una tabia njema tukufu .”[46]

Utumwa wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu umeonyeshwa na kauli ya Mwenyezi Mungu: “Utukufu ni wake ambaye alimpeleka mja wake usiku kutoka msikiti mtukufu mpaka msikiti wa mbali .”[47]

Ama ukunjufu wa kifua chake umeashiriwa na Aya: “Je hatukuku- panulia kifua chako?”[48] Ama kumfuata kwake Mwenyezi Mungu katika kila kitu huku akimwogopa na kumnyenyekea yeye tu kumeelezwa na Aya: “Sifuati ila ninayofunuliwa kwa wahyi. Hakika mimi naogopa nikimwasi Mola wangu adhabu ya siku iliyo kuu .”[49] Ushahidi mwingine ni Aya: “Wale wanaofikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kumwogopa yeye wala hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhesabu .”[50]

Ama huruma yake na upole wake kwa walimwengu huku akiwahangaikia watu ili kuwaongoza waelekee kwa Mwenyezi Mungu kumeelezwa na Aya: “Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu.[51] Na akasema: “Bila shaka amekufikieni Mtume kutoka miongoni mwenu, yanamhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, kwa waumini ni mpole, mwenye kuwaonea huruma.”[52] Na Aya isemayo: “Enyi watu wa kitabu, hakika amek- wisha kufikieni mtume wetu, anayekubainishieni mengi mliyokuwa mkiyaficha katika kitabu, na kusamehe mengi”[53] inaonyesha msamaha wake.

Ama Aya isemayo: “Sema: Hii ndiyo njia yangu ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa ujuzi, mimi na wanaonifuata, na Mwenyezi Mungu ametakasika na kila upungufu wala mimi simo miongoni mwa washirikina[54] inaonyesha ufahamu wake na kudumu kwake katika njia ya uongofu wa Mola wake.

Pia hali hiyo inathibitishwa na Aya isemayo: “Sema: Na uite kwa Mola wako, bila shaka wewe uko juu ya mwongozo ulio sawa ”.[55] Na ile isemayo: “Basi tegemea kwa Mwenyezi Mungu hakika wewe uko juu ya haki iliyo wazi.”[56] Pia ile isemayo: “Yeye ndiye aliyemtuma mtume wake kwa mwongozo na kwa dini ya haki ili ishinde dini zote, ingawa washirikina wat- achukia.”[57] Zote hizo zinathibitisha hali hiyo.

Aya ifuatayo: “Ambao wanamfuata mtume, nabii aliyoko Makka, ambaye wanamwona ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia maovu, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.”[58] inathibitisha kutojifunza kwake toka kwa mtu yeyote huku akimkomboa mwanadamu dhidi ya kila aina minyororo.

Ama uadilifu na usawa wake katika maadili na mwenendo wake umeashiriwa na Aya isemayo: “Na hivyo tumekufanyeni umati bora ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe shahidi juu yenu.”[59]

Aya ifuatayo: “Bila shaka mnao mfano mwema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana.”[60]

Imethibitisha kuwa yeye ndiye mfano wa kuigwa katika ukamilifu wa mwanadamu. Ama utawala wake juu ya viumbe na cheo chake juu yao umethibitishwa na Aya isemayo: “Hakika kiongozi wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake.”[61]

Aya ifuatayo: “Muhammad mtume wa mwenyezi Mungu na walio pamoja naye ni imara mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao[62] inathibitisha jinsi alivyo mkali dhidi ya wapinzani na makafiri.

Ama Aya ifuatayo: “Ewe Nabii, kwa hakika sisi tumekutuma shahidi na mtoaji wa habari nzuri na muonyaji. Na muhitaji kwa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake na taa itoayo nuru.”[63] inathibitisha ufasaha wake, kuhusika kwake katika kila jukumu na kuwaongoza watu.

NDANI YA MAELEZO YA BWANA WA MAWASII (A.S)

Imam Ali(a.s ) amesema: “ ……Mpaka Mwenyezi Mungu alipomtuma Muhammad shahidi, mtoaji wa habari njema, mwonyaji, mbora wa viumbe kati ya watoto wote, na mbora wa viumbe watakasifu kati ya wakongwe wote, mtakasifu wa maadili kati ya watakasifu wote, na mbora wa ukarimu kati ya wakarimu wote .”[64]

“Akamteua kutokana na mti wa manabii, shubaku yenye mwanga, nywele za utosi wa watukufu…… na chemchemu ya hekima, tabibu maarufu kwa tiba yake, yuko tayari kwa dawa yake huku akifuatilia kwa hiyo dawa yake kila sehemu yenye mghafiliko na sehemu za shaka.”[65]

“Nakiri kuwa Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake aliyemteua kati ya viumbe Wake, aliyeteuliwa kwa ajili ya kubainisha ukweli halisi, aliyeteuliwa mahsusi kwa ajili ya miujiza mitukufu na ujumbe mtakatifu, mwenye kubainisha alama za uongofu kupitia ujumbe huo, hivyo mwenye kujitenga naye yumo katika upotevu mkubwa.”[66]

“Hakika Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad huku ndani ya waarabu hakuna anayejua kusoma kitabu wala anayedai unabii, hivyo akawapeleka watu mpaka akawafikisha sehemu yao, huku akiwafikisha eneo la uokovu wao, hivyo njia yao ikanyooka na sifa zao zikatulia.”[67]

Hivyo akavuka kiwango katika kutoa nasaha, akafuata njia sahihi na kulingania hekima na mawaidha mazuri .”[68]

“Mwenye kutangaza haki kupitia haki, mwenye kuondoa mchemko wa batili, na mwenye kuangamiza ukali wa upotovu. Kama alivyobebeshwa ndivyo alivyoinuka huku akisimama kwa nguvu zote kupitia amri yake. Mwenye kuharakisha katika kupata ridhaa Zako huku akiwa haogopi kwenda vitani wala si dhaifu katika nia. Mwenye kuhifadhi ufunuo Wako, mwenye kulinda ahadi Yako huku akiendelea kutekeleza maamrisho Yako……..Hivyo yeye ni mwaminifu mwenye kuaminika na muhazini wa elimu Yako ya siri.”[69]

“Imam wa atakayemcha Mwenyezi Mungu na jicho la atakayeongoka.”[70]

“Hivyo akapambana katika njia ya Mwenyezi Mungu dhidi ya wale waliyomkimbia na dhidi ya wale waliyojitenga Naye……..[71] kwa ajili ya kutetea dini Yake, huku haumzuwii kufanya hivyo mkusanyiko wa wote wenye kumpinga na ule wa wenye kutaka kuzima nuru yake.”[72]

“Ilikuwa tukizidiwa na ukali wa vita tunajikinga kwa mtume, hivyo hakuna yeyote kati yetu aliyekuwa karibu na adui zaidi yake.”[73]

“Hivyo muige Mtume wako mbora wa watakasifu. Hakika katika kumuiga kuna kigezo chema kwa atakayeiga. Aliidokoa dunia na wala hakuitamani kabisa, hivyo yeye ndiye aliyeiacha dunia bila kuijali, na ndiye aliyeliacha tumbo tupu bila dunia…… Alipewa dunia yote akakataa kuipokea………..Alikuwa akila huku kakaa aridhini, alikaa mkao wa mtumwa huku akishona viatu vyake kwa mkono wake……..Alitoka duniani bila kustarehe na nayo, na alifika akhera akiwa salama, hivyo hakulimbikiza kitu mpaka alipofariki.”[74]

Imepokewa kutoka kwa Hasan bin Ali(a.s ) kuwa Hindu bin Abi Halati alitoa wasifu wa Mtume(s.a.w.w ) kwa kusema: “Huanza kumtolea salamu yule aliyekutana naye……..Daima alikuwa na huzuni, mwingi wa tafakuri muda wote, mwimgi wa ukimya, hazungumzi pasipo na haja ya kuzungumza, huzungumza yenye kutosheleza, hazungumzi yasiyo na maana wala yaliyo pungufu, si mwenye kun- yanyapaa wala si mwenye kudharau.”

Hivyo neema ndogo kwake ilikuwa kubwa, haikashifu neema yoyote. Wala dunia na kichache alichokipata havimkasirishi. Anapopewa haki hakuna anayefahamu, wala hakutenda jambo kwa ghadhabu mpaka atakapoimiliki……..Anapoghadhibika huacha na kuondoka, na anapofurahi hubana sauti yake bali alama ya kucheka kwake ni tabasamu lake.

NDANI YA DONDOO ZA SERA YAKE KIJAMII

Husein bin Ali(a.s ) amepokea Hadithi kutoka kwa baba yake Imam Ali(a.s ) inayozungumzia sera ya Mtume(s.a.w.w ) kijamii:

“Anapokuwa nyumbani kwake hugawa muda wake mafungu matatu: Fungu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Fungu kwa ajili ya wakeze na fungu kwa ajili ya nafsi yake. Kisha fungu lake huligawa kwa ajili yake na kwa ajili ya kuhudumia jamii.

Mwenendo wake katika kuhudumia umma ulikuwa ni kuwatanguliza wale wenye ubora huku akigawa ubora wao kulingana na ubora wao katika dini.

Alikuwa akizuia ulimi wake isipokuwa katika yale yanayomuhusu huku akiwaunganisha pamoja bila kuwasambaratisha. Humheshimu mheshimiwa wa kila kundi huku akimtawalisha juu yao. Hujihadhari na kujilinda dhidi ya watu bila ya kupunguza bashasha yake wala tabia yake. Huwatafuta maswahaba zake wasipoonekana huku aki- ulizia matatizo ya watu.

Hulisifia jema na kulipa nguvu, na hulisifu kwa ubaya lile lililo baya huku akilishusha thamani. Jambo lake huwa wastani wala haghafiliki na kitu….Hapunguzi wala hazidishi huku aliye mbora mbele yake ni yule mwenye kuwanasihi sana waislam.

Na mwenye hadhi kubwa sana mbele yake ni yule mwenye kuwasaidia na kuwanusuru watu. Hakai wala hasimami ila akimtaja Mwenyezi Mungu. Humpa kila aliyekaa naye fungu lake, hivyo anapokaa na mtu humvumilia mpaka mtu yule aondoke mwenyewe.

Amwombaye haja yoyote humjibu kwa kumtekelezea haja yake na kwa kauli tamu. Kikao chake ni kikao cha heshima, ukweli na uaminifu. Muda wote alikuwa ni mwenye bashasha, mwenye tabia nyepesi, mpole, asiye mkali wala si mkavu wa tabia. Hakuwa mchekaji ovyo wala mtukanaji, hakuwa mwaibishaji au mwongeza chumvi katika kusifia.

Hujighafilisha na yale asiyoyapenda, hivyo alikuwa akinyamaza kwa sababu ya mambo manne: Kwa sababu ya busara, tahad- hari, ridhaa, na tafakari.”[75]

MUHTASARI

Mwenyezi Mungu katoa wasifu wa Mtume Wake Muhammad(s.a.w.w ) kwa kueleza sifa zake za ukamilifu wa kibinadamu, hivyo akamfanya mbora wa mitume, hitimisho lao, na kigezo chema amba- cho watakiiga wanadamu ili wanadamu hao wafikie kilele cha ukamilifu. Mwenyezi Mungu kawafafanulia waigaji sifa zake na maadili yake mazuri mema.

Kizazi chake ambacho ndio kijuacho zaidi yale yaliyomo nyumbani kimetoa wasifu wa mbora wao na mjumbe mwaminifu kupitia maneno yaliyo timilifu yaliyokusanya sifa zote. Huku maneno hayo yakitoa taswira ya ukamilifu na sifa ambazo zimemfanya awe ni kiigizo chema kwa wanaomfuata na bendera kwa wenye kuongoka.

Maelezo hayo yaliyonukuliwa kutoka kwa kizazi chake yametoa taswira ya adabu ya hali ya juu ya Mtume(s.a.w.w ) na sera yake binafsi na ya kijamii ya hali ya juu.

SOMO LA SITA: TABIA NA MWONEKANO WA HITIMISHO LA MANABII (S.A.W.W)

MSOMI ASIYEWAHI KUSOMA WALA KUANDIKA

Kati ya sifa za kipekee alizonazo Mtume wa mwisho(s.a.w .w ) ni kuwa yeye hakujifunza kusoma wala kuandika kutoka kwa mwalimu yeyote yule wa kibinadamu,[76] wala hakukulia katika mazingira ya kielimu bali alikuwa ndani ya jamii ya wajinga.

Hakuna yeyote aliyepinga ukweli huu uliyoelezwa na Qur’ani tukufu, bali alikuwa ndani ya jamii ambayo watu wake walikuwa ni wajinga sana kuliko watu wa jamii nyingine yoyote ile, lakini pamoja na hali hiyo alileta Kitabu kinacholingania elimu na maarifa, kikiamsha fikra na akili huku kikiwa kimekusanya aina zote za maarifa.

Hakika Mtume(s.a.w.w ) alianza kuwafunza watu Kitabu na hekima[77] kwa silabasi nzuri sana mpaka akaibua ustaarabu wa kipekee ambao ulizamisha Magharibi na Mashariki kupitia elimu na maarifa yake, na bado mpaka leo nuru yake inang’aa, hivyo yeye Mtume(s.a.w.w ) ni mtu asiyewahi kusoma wala kuandika lakini alikuwa aking’oa ujinga, ujahili na ibada za masanamu huku akiwa amewaletea wanadamu dini ya hadhi ya juu na sheria ya kimataifa ambayo itawafaa wanadamu muda wote wa maisha yao.

Hivyo kupitia elimu, maarifa yake, maneno yake timilifu, ubora wa akili yake, mafunzo yake na silabasi yake ya malezi yeye mwenyewe huwa ni muujiza, kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu akasema:

“Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake nabii asiyewahi kuandika wala kusoma, ambaye anamwamini Mwenyezi Mungu na maneno yake, na mfuateni ili mpate kuongoka.”[78]

Hakika Mwenyezi Mungu alimfundisha yale aliyokuwa hayajui na akamfunza kitabu na hekima mpaka akawa nuru, taa yenye kuangaza, dalili, shahidi, mtume wa wazi, mshauri nasaha mwaminifu, mkum- bushaji, mwenye kutoa habari njema na mwenye kuonya.[79]

Yeye ndiye aliyemkunjua kifua kwa ajili yake, akamwandaa kupokea ufunuo na kutekeleza jukumu la kuongoza katika jamii ambayo ilikuwa imetawaliwa na ubaguzi, chuki na majivuno ya kijahiliya. Hivyo akawa ni kiongozi bora wa hali ya juu aliyetambuliwa na wanadamu katika uhubiri, malezi na mafunzo.

MWISLAMU WA KWANZA NA MBORA WA WANAIBADA

Hakika kilele cha mwanzo ambacho ni lazima kwa kila mwanadamu akifikie ili ajiandae kuteuliwa na kuchaguliwa na Mwenyezi Mungu ni unyenyekevu kamili kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Muumba wa ulimwengu. Pia kujisalimisha kiukamilifu mbele ya nguvu Zake tuku- fu na hekima zake kamilifu. Pia utumwa wa hiari uliotimia mbele ya Mwenyezi Mungu mmoja wa pekee aliye tegemeo.

Hakika Qur’ani tukufu imemtolea ushahidi nabii huyu aliyewapita manabii wote katika kila kitu, ikasema: “Na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha.”[80]

Hakika hicho ni kilele cha ukamilifu ambacho alikifikia mja huyu mkweli katika ibada zake, na akawa kawapita watu wote kwa ujumla. Hakika unyenyekevu wake wa kweli ulidhihirika katika matendo na kauli zake, hivyo akasema: “Kitulizo cha macho yangu ni Swala.”[81]

Hakika Swala ilipendezeshwa kwake kama yalivyopendezeshwa maji kwa mtu mwenye kiu, hivyo anywapo maji hukata kiu, lakini Mtume(s.a.w.w ) hakukatwa kiu na Swala, kwani daima aliusubiri kwa hamu muda wa Swala huku shauku ya kusimama mbele ya Mola wake ikiongezeka. Alikuwa akimwambia mwadhini wake: “Tupe raha ewe Bilal”[82] .

Imepokewa kuwa alikuwa akizungumza na familia yake na wao wakimzungumzisha lakini unapoingia wakati wa Swala huwa kama vile hawajui na hawamjui.[83] Kipindi anaposali kifua chake hutoa sauti ya kutetemeka kama sauti ya mchemko wa chungu huku akilia kutokana na kumwogopa Mwenyezi Mungu mtukufu hadi msala wake unalowana[84] .

Hivyo alikuwa akisali mpaka nyayo zake zinatoa harufu. Watu humwambia unafanya hivyo ilihali Mwenyezi Mungu ame- shakusamehe madhambi yako yaliyotangulia na yaliyofuatia. Hujibu: “Hivi haifai nikawa mja mwenye kushukuru?”[85]

Alikuwa akifunga mwezi wa Shabani na Ranadhani na siku tatu ndani ya kila mwezi,[86] huku akibadilika rangi uingiapo mwezi wa Ramadhani, Swala zake huongezeka huku akinyenyekea katika dua.[87]

Linapoingia kumi la mwisho la Ramadhani hujitenga na kuwahama wakeze huku akiupitisha usiku akiwa faragha kwa ajili ya ibada.[88]

Alikuwa akisema: “Dua ndiyo roho ya ibada, silaha ya muumini, nguzo ya dini na nuru ya mbingu na ardhi .”[89]

Daima alikuwa katika mawasiliano na Mwenyezi Mungu, akijifunga kwake kwa unyenyekevu na dua katika kazi yoyote ile kubwa au ndogo, bali alikuwa akimwomba Mwenyezi Mungu msamaha na kutubu kila siku mara sabini bila ya kuwa na dhambi yoyote.[90]

Hakuamka usingizini ila ni mnyenyekevu mwenye kusujudu.[91]

Alikuwa akimhimidi Mwenyezi Mungu kila siku mara mia tatu sitini akisema: “Kila sifa njema ni ya Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu wote, na ni nyingi katika kila hali.”

Daima alikuwa akisoma Qur’ani huku akiwa ni mwenye kushughulishwa sana na usomaji huo. Imani isiyo na mipaka kwa Mwenyezi Mungu:

Mwenyezi Mungu amemhimiza Mtume Wake(s.a.w.w) awe na imani isiyo na mipaka na Mola Wake kwa kusema: “Je, Mwenyezi Mungu hamtoshei mja wake?”[92]

Pia alisema: “Na umtegemee Mwenye nguvu, Mwenye rehema.* Ambaye anakuona unaposimama.* Na mageuko yako katika wale wanaosujudu.”[93]

Imepokewa kutoka kwa Jabir (r.a) kuwa: “Tulikuwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) tukafika kwenye mti wenye kivuli tukamwachia mti huo. Ghafla akatokea mtu kati ya mushrikina huku upanga wa Mtume(s.a.w.w ) ukiwa umetungikwa kwenye mti, ndipo mushrik yule alipouchukua upanga ule na kumwambia Mtume(s.a.w.w ) : “Je unaniogopa? “ Mtume akajibu: “Hapana.” Mushriku akasema: “Nani atakuzuwia dhidi yangu?” Mtume akajibu: “Mwenyezi Mungu.” Hapo upanga ukadondoka toka mikononi mwa mushriku.

Ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipouchukua na kusema: “Na wewe ni nani atakayekuzuwia dhidi yangu?” Akajibu: ‘Mbora wa wachukuaji.” Mtume akasema: “Je unakiri kuwa hapana mola wa haki isipokuwa Allah na kwamba hakika mimi ni Mtume wa Allah?” Mushriku akajibu: “Hapana, isipokuwa ninakuahidi kuwa sitokupiga vita, wala sitokuwa pamoja na watu wanaokupiga vita.

Hapo Mtume akamwachia, na mushriku akaenda kwa jamaa zake na kuwaambia: “Nimewajia toka kwa mbora wa watu.”[94]

USHUJAA WA HALI YA JUU

Mwenyezi Mungu ameeleza sifa za Mtume Wake(s.a.w.w ) kwa kusema: “Wale wanaofikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kumwogopa Yeye wala hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuh- esabu.”[95]

Imam Ali(a.s ) ambaye mashujaa wa kiarabu waliinamisha vichwa mbele yake ametupa wasifu makini kuhusu ushujaa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) akasema: “Pindi vita vinapokuwa vikali na kundi moja likalizidi kundi lingine basi tulikuwa tukijikinga kwa Mtume, hivyo hakuna yeyote anayekuwa karibu sana na maadui kuliko yeye.”[96]

Mikidad ameelezea msimamo wa Mtume(s.a.w.w ) siku ya Uhud baada ya watu kutawanyika huku wakimwacha Mtume(s.a.w.w ) peke yake, Mikidad amesema: “Naapa kwa yule aliyemtuma kwa haki, ukimwona Mtume(s.a.w.w ) kainua mguu wake shibri moja basi ujue yuko mbele ya adui huku kundi la jamaa wa adui likiwa limemvamia na muda huo huo likitawanyika kwa kumkimbia, utamwona kasimama akirusha upinde au akirusha jiwe mpaka mawe yawaenee.”[97]

UTAWA USIYOKUWA NA MFANO

Mwenyezi Mungu amesema kumwambia Mtume Wake(s.a.w.w ) kuwa: “Wala usivikodolee macho yako tulivyowastarehesha watu wengi miongoni mwao, ni mapambo ya maisha ya dunia, ili tuwajaribu kwa hayo, na riziki ya Mola Wako ni bora mno na iendeleayo.”[98]

Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa mkweli katika kuiacha dunia na mapambo yake. Aliiacha dunia mpaka ikapokewa toka kwa Abu Umamah toka kwa Mtume(s.a.w.w ) kuwa alisema: “Mola Wangu alinitunukia akataka aifanye Makka yote iwe dhahabu kwa ajili yangu, nikasema: Hapana Mola Wangu! lakini napenda niwe nashiba siku moja na kushinda na njaa siku nyingine……..Kwani nitakapokuwa na njaa nitakunyenyekea na kukukumbuka, na nitakaposhiba nitakushukuru na kukuhimidi”.[99]

Akalala juu ya changarawe na alipoamka zilikuwa zimeathiri ubavu wake. Akaambiwa: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu tungekuwekea kizuwizi.” Akajibu: “Mimi nina nini na hii dunia, kwani mimi si chochote ndani ya dunia hii isipokuwa ni kama msafiri aliyejipumzisha chini ya mti wa kivuli na baada ya mapumziko ataon- doka na kuuacha ule mti.”

Ibnu Abbas amesema: “Mtume(s.a.w.w ) alikuwa akilala njaa siku zenye kufuatana, huku familia yake ikiwa haipati chakula cha usiku. Mara nyingi mkate wao ulikuwa ni mkate wa shairi.”

Aisha amesema: “Familia ya Muhammad haikula milo miwili ndani ya siku moja isipokuwa mlo mmoja ulikuwa ni tende tu.”[100]

Akamwambia mtoto wa dada yake Urwah: “Hakika sisi tulikuwa tukiutazama mwezi mwandamo, kisha mwezi mwandamo mwingine hadi miezi miandamo mitatu katika miezi miwili huku ndani ya muda wote huo haujawashwa moto katika nyumba za Mtume(s.a.w.w ) .”

Urwah akamuuliza: “Ewe mama mdogo; alikuwa akiwalisha nini usiku?” Akajibu: “Vyeusi viwili: Tende na maji. Isipokuwa Mtume alikuwa na jirani yake wa kianswari aliyekuwa na mifugo, hivyo alikuwa akimpa Mtume wa Mwenyezi Mungu maziwa yake na Mtume anatupa sisi.”[101]

Pia amesema: “Mtume(s.a.w.w ) alifariki huku ngao yake ikiwa imewekwa rehani kwa yahudi kwa thamani ya vibaba thelathini vya shairi.”[102]

Imepokewa toka kwa Anas bin Malik kuwa: “Fatima(a .s) alimpelekea Mtume(s.a.w.w ) kipande cha mkate. Mtume akasema: “Ewe Fatima, kipande hiki cha nini? “Akajibu: “Ni kipande cha mkate kwani roho yangu haijaridhika mpaka nikuletee kipande hiki.” Mtume akasema: “Hakika hiki ni chakula cha kwanza kilichoingia ndani ya kinywa cha baba yako tangu siku tatu zilizopita.”[103]

Hii ni sura fupi na halisi ya utawa wa Mtume(s.a.w.w ) na jinsi alivyoipa mgongo dunia mpaka akafariki.

MUHTASARI

Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad bin Abdullah hakujifunza mikononi mwa mwanadamu yeyote, lakini alikuja na Kitabu cha kie- limu na kimaarifa cha kimataifa ambacho kimewataka wanadamu wote katika zama zote walete mfano wake.

Kupitia Kitabu hicho Mtume(s.a.w.w) aliweza kumtoa mwanadamu toka jamii ya kijinga mpaka jamii ya kielimu iliyokamilika yenye kustaarabika, huku akihimiza usiku na mchana juu ya utafutaji wa elimu na maarifa mbalimbali.

Hivyo kupitia Kitabu hicho aliasisi dola kubwa na kujenga ustaarabu wa pekee ambao mfano wake hau- jashuhudiwa na mwanadamu.

Mtume(s.a.w.w ) alibeba maana kamili ya ibada kwa Mwenyezi Mungu Muumba, hivyo alikuwa na mahusiano ya karibu sana na Mola Wake Mtukufu, mahusiano ambayo yalitokana na ujuzi, mapenzi, utashi, na moyo mkunjufu, hivyo akawa ni kiigizo chema katika swala yake, funga, dua na uombaji msamaha, kiigizo ambacho kinamchorea mwanadamu njia ya ukamilifu kuelekea kwa Muumba, Mjuzi.

Mtume(s.a.w.w ) alianza harakati akiwa amebeba jukumu kubwa huku akimtegemea Mwenyezi Mungu katika kila harakati na kila jambo, hivyo akawa ni shujaa, jasiri na mkakamavu katika kulingania njia ya Mwenyezi Mungu.

Mtume(s.a.w.w ) aliishi mbali na ladha za dunia na starehe zake, hivyo alikuwa ni sehemu ya mafakiri na masikini, akishirikiana nao katika taabu zao huku akitarajia rehema za Mola Wake, mnyenyekevu Kwake, mwenye kujitenga na kila ujeuri utokanao na starehe za dunia na furaha za mapambo yake.

SOMO LA SABA: TABIA NA MWONEKANO WA HITIMISHO LA MANABII (S.A.W.W)

UKARIMU

Ibnu Abbas amesema: “Mtume(s.a.w.w ) alikuwa mkarimu sana kati- ka mambo ya kheri, ukarimu wake ulikuwa ukiongezeka zaidi ndani ya mwezi wa Ramadhani……Alikuwa akikutana na Jibril ndani ya kila mwezi wa Ramadhani kila mwaka, hivyo akikutana na Jibril huwa mkarimu sana kuliko upepo uvumao.”[104]

Jaabir amesema: “Mtume(s.a.w.w ) hakuombwa chochote akajibu hapana.”[105]

Imepokewa kuwa Mtume(s.a.w.w ) alikwenda kwa muuza nguo aka- nunua kanzu kwa dirhamu nne akatoka huku kaivaa. Ghafla akatokea mtu kati ya answari na kusema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nivishe kanzu, hakika Mwenyezi Mungu atakuvisha nguo kati ya nguo za Peponi.”

Hapo Mtume(s.a.w.w ) akavua kanzu na kumvisha. Kisha Mtume(s.a.w.w ) akarudi dukani na kununua tena kanzu kwa dirhamu nne huku akibakiwa na dirhamu mbili. Ghafla akatokea kijakazi njiani huku akilia. Mtume akamuuliza: “Kitu gani kinakuliza?” Akjajibu: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mabwana zangu wamenipa dirhamu mbili nikanunulie unga lakini zimepotea.” Basi hapo Mtume(s.a.w.w ) akatoa dirhamu mbili na kumpa.

Kijakazi yule akasema: “Nahofia watanipiga.”

Mtume(s.a.w.w ) akaenda naye kwa mabwana zake, kisha Mtume(s.a.w.w ) akawatolea salamu. Wakaijua sauti yake, kisha akatoa mara ya pili, kisha mara ya tatu. Ndipo walipomjibu salamu yake. Mtume akasema: “Je mlisikia salamu yangu ya mwanzo?” Wakajibu: “Ndio, lakini tulipenda utusalimie zaidi, je ni jambo gani lililokusumbua?”

Mtume(s.a.w.w ) akajibu: “Nilimuonea huruma kijakazi huyu msije mkampiga.” Hapo bwana wake akasema: “Yeye yuko huru katika njia ya Mwenyezi Mungu, hivyo utaondoka naye.”

Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu akawabashiria heri na pepo kwa kusema: “Hakika Mwenyezi Mungu ametia baraka katika dirhamu kumi, kamvisha kanzu Mtume wake na mtu kati ya answari, na akam- pa uhuru mtumwa, ninamhimidi Mwenyezi Mungu, hakika Yeye ndiye aliyeturuzuku haya kwa uwezo Wake.”[106]

Alikuwa akiwaachia watumwa wote huru uingiapo mwezi wa Ramadhani huku akimpa kila mwombaji.[107]

UPOLE NA USAMEHEVU

Zaid bin Aslam amesema: “Tulipata habari kuwa Abdullah bin Salama alikuwa akisema: “Hakika sifa za Mtume wa Mwenyezi Mungu ndani ya Taurati ni: Ewe nabii hakika tumekutuma uwe shahidi, mbashiri, mwonyaji na kinga kwa wasiojua kusoma na kuandika. Wewe ni mja Wangu na Mtume Wangu, nimekuita jina la Al- Mutawakkil (Mwenye kunitegemea).

Si mkali wala si mshupavu wa moyo. Si mpiga kelele masokoni wala halipi ubaya kwa ubaya lakini husamehe. Sitomfisha mpaka ninyooshe dini iliyopinda na watu waseme: Hapana Mola wa haki isipokuwa Allah, hivyo kupitia yeye Mwenyezi Mungu afungue macho yasiyoona, masikio yasiyosikia na nyoyo zilizoziba.” Maneno hayo yalipomfikia Kaaby akasema: “Amesema kweli Abdullah bin Salama.”

Imepokewa toka kwa Aisha kuwa: “Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w ) hakulipiza kisasi dhidi ya jambo lolote alilotendewa binafsi isipokuwa linapovunja utukufu wa Mwenyezi Mungu. Hivyo hakukipiga kitu chochote kwa mkono wake isipokuwa akipige katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hakuna chochote alichoombwa akanyima isipokuwa aombwe jambo la dhambi. Hakika alikuwa mbali na jambo lolote la dhambi.”[108]

Ubaydu bin Umayr amesema: “Hakuna jambo lolote alilofanyiwa Mtume(s.a.w.w ) lisilolazimu adhabu kisheria isipokuwa alisamehe.”[109]

Anas amesema: “Nilimhudumia Mtume wa Mwenyezi Mungu muda wa miaka kumi, ndani ya muda wote huo hakuwahi kunifyonza na nilipofanya jambo lolote hakuniambia: Kwa nini umefanya hivi? Na nilipoacha jambo lolote hakuwahi kuniuliza: Kwa nini umeacha?”[110]

Alikuja bedui na kuvuta nguo ya Mtume(s.a.w.w ) kwa nguvu mpaka upinde wa nguo ukamuumiza Mtume shingoni, kisha bedui yule akasema: “Ewe Muhammad amrisha nipewe sehemu ya mali ya Mwenyezi Mungu iliyopo kwako.”

Mtume(s.a.w.w ) akamgeukia huku akitabasamu, kisha akaamrisha apewe.

Hakika Mtume alifahamika kwa usamehevu na upole muda wote wa maisha yake…….Hivyo alimsamehe Wahshiyu muuaji wa ami yake Hamza……Alimsamehe mwanamke wa kiyahudi aliyempa nyama ya mbuzi yenye sumu. Pia alimsamehe Abu Suf’yani huku akifanya kitendo cha kuingia nyumbani mwa Abu Suf’yani ni usalama dhidi ya kuuawa. Aliwasamehe maquraishi ambao walimpiga vita kwa kila aina ya nyenzo waliyokuwa nayo……huku akiwa katika kilele cha uwezo na nguvu lakini anawaombea heri kwa kusema: “Ewe Mola Wangu! waongoze jamaa zangu, hakika wao hawajui…….Nendeni hakika nyinyi ni watu mlioachiwa huru.”

Qur’ani imeweka bayana usamehevu wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w ) ikaelezea hilo kwa kusema:

Basi kwa sababu ya rehema ya Mwenyezi Mungu umekuwa mpole kwao na kama ungekuwa mkali mshupavu wa moyo wangekukimbia. Basi wasamehe na uwaombee msamaha na ushauriane nao katika mambo .”[111]

Na ikasema tena: “Bila shaka amekufikieni Mtume kutoka miongoni mwenu, yanamuhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, kwa waumini ni mpole, mwenye kurehemu .”[112]

Kwa usamehevu huu mkubwa Mtume(s.a.w.w) aliweza kukonga nyoyo ngumu kakamavu na kuzifanya zimzunguke na kuamini utume wake wa kudumu.

Haya: Imepokewa kutoka kwa Abu Saad Al-Khidriy kuwa: “Mtume(s.a.w.w) alikuwa na haya sana kuliko mtawa katika utawa wake, hivyo iwapo akichukizwa na jambo hufahamika kupitia uso wake.”[113]

Imepokewa kutoka kwa Ali(a.s) kuwa: “Iwapo Mtume(s.a.w.w) kaombwa kutenda jambo na akataka kulitenda basi husema: Ndio. Na iwapo hataki kulitenda hunyamaza kimya, wala hakuwa anasema hapana akataapo kutenda jambo.”[114]

UNYENYEKEVU

Imepokewa kutoka kwa Yahya bin Abi Kathiri kuwa Mtume(s.a.w.w) alisema: “Ninakula kama alavyo mtumwa, nakaa kama akaavyo mtumwa, hakika mimi ni mtumwa.”[115]

Siku moja Mtume(s.a.w.w) alimsemesha mtu, basi mtu huyo akatetemeka, hapo Mtume(s.a.w.w) akasema: “Tulia, hakika mimi si malaika isipokuwa mimi ni mtoto wa mwanamke wa kikurayshi ambaye alikuwa akila nyama kavu tu.”[116]

Imepokewa kutoka kwa Abu Amamah kuwa: “Mtume alitujia huku anatembelea fimbo basi tukasimama, hapo Mtume(s.a.w.w) akasema: Msisimame kama wanavyosimama waajemi kwani baadhi yao huwatukuza wengine.”14Alikuwa akiwatania maswahaba zake isipokuwa hatamki ila la kweli.[117]

Pia alikuwa akiwatolea watoto salamu.[118] Alishirikiana na swahaba zake katika kujenga msikiti.[119]

Akachimba handaki,[120] na mara nyingi alikuwa akiomba ushauri toka kwa maswahaba zake, japokuwa yeye ndiye aliyekuwa na akili bora kuliko watu wote.[121]

Mara nyingi alikuwa akisema: “Ewe Mola Wangu nipe uhai katika hali ya umaskini na unifishe nikiwa masikini. Hakika muovu wa kutupa ni yule anayekusanyikiwa na ufakiri wa dunia na adhabu ya Akhera.”[122]

Hii ni sura fupi sana kuhusu sifa za shakhsia ya Mtume(s.a.w.w) , na hizi ni baadhi tu ya tabia zake binafsi na za kijamii.

Pia kuna sura nyingi nzuri kuhusu mwenendo wake na sera yake kiutawala, kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kifamilia, mwenendo ambao unahitaji masomo ya ndani zaidi ili kufuata na kuuiga, hivyo masomo hayo tunayaacha kwa ajili ya muhula ujao.

Hivyo ndivyo zilivyotubainikia sifa za pekee za Mtume Muhammad(s.a.w.w) ambazo tunaweza kuzifupisha katika maneno yafuatayo:

Usafi wa familia, ulinzi wa Mwenyezi Mungu daima, tabia za hali ya juu, nafasi ya juu ya kijamii, maadili mema, ufasaha wa lugha, maisha mepesi, kujiepusha na kila aina ya shirki na kila aina ya mila potovu, kufikia kilele katika ibada ya Mwenyezi Mungu na unyenyekevu kwa ajili ya haki katika hali yoyote ile.

MUHTASARI

Hakika Mtume(s.a.w.w) alikuwa mkarimu sana, hivyo alikuwa akieneza upendo, ukarimu, wema na mali kwa watu wote, huku akitoa msamaha, huruma na ulaini kwao. Ili awaokoe toka kwenye ujinga wao na apate kuwaunganisha pamoja wawe kitu kimoja.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa anaishi na waislam kama mmoja wao huku haya zikimtukuza kwa kumpa haiba na heshima, huku unyenyekevu ukimzidishia heshima na utukufu. Hivyo alikuwa akiwahurumia wadogo na kuwaheshimu wakubwa. Alikuwa akisikia ushauri wa mnasihi ilihali yeye ni mwenye akili zitokazo mbinguni kwa njia ya ufunuo.